Title July 2018

JE! UMEYABATILISHA MAMBO YA KITOTO?

1Wakoritho 13: 11 “Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto”.
 
Katika maisha ya kawaida, mwanadamu ni lazima apitie katika hatua hizi mbili; UTOTO na UTU UZIMA. Na kila hatua ni lazima iwe na uongozi juu yake, Kwamfano mtoto mdogo hawezi kujiongoza mwenyewe kwasababu akili yake haijakomaa kuweza kutambua jema na baya au kupambanua kanuni za maisha hivyo ni lazima aandaliwe na mzazi wake au mlezi wake kanuni fulani za kufuata aidha apende au asipende kwake huyo zinakuwa ni sheria na amri, na ndio maana tunaweza kuona mtoto anapofikisha umri fulani labda miaka 6/7, anapelekewa shule sio kwa mapenzi yake, hapana, pia analazimishwa kuamshwa asubuhi kila siku ili aende shule na tunafahamu hakuna mtoto anayependa kuamshwa asubuhi apige mswaki na kwenda shule, yeye atatamani tu acheze cheze na kurukaruka,
 
Kadhalika akirudi baadaye nyumbani, atalazamishwa alale mchana, atalazimishwa aoge, atalazimishwa afanye homework,atachaguliwa nguo za kuvaa, na wakati mwingine atachaguliwa mpaka na marafiki wa kucheza naye, n.k. Hivi vyote atafanya tu hata kama hataki, na wakati mwingine akikosea mojawapo ya hizo kanuni alizowekewa itamgharimu adhabu. Hivyo ukichunguza kwa undani utaona kuwa sio kwamba Yule mtoto anatimiza zile sheria kwa kupenda la! Bali anafanya vile kwa kutimiza tu matakwa ya baba / mama yake basi, laiti angepewa uhuru kidogo tu! Asingedhubutu kufanya mojawapo ya hayo, angeenda kufanya mambo yake mengi kuzurura zurura tu.
 
TABIA YA MTU MZIMA.
 
Lakini Yule mtoto atakapokuwa mtu mzima kidogo kidogo mabadiliko yataanza kutokea ndani yake, ataanza kuona umuhimu wa yeye kuamka asubuhi na mapema na kupiga mswaki mwenyewe, na umuhimu wa kwenda shule , ataona umuhimu wa kuoga, ataona umuhimu wa kuwa na marafiki wazuri, n.k. Lakini ni kwasababu gani anafanya hivyo?. Ni kwasababu ameshakuwa mtu mzima na anajua kufanya hivyo ni kwa faida yake mwenyewe na sio kwa faida ya mzazi. Na hiyo ndiyo dalili kubwa ya kuonyesha kuwa mtu huyo amekuwa. Kwasababu ile sheria na maagizo aliyopewa na wazazi wake sasa anayatimiza mwenyewe ndani ya moyo wake pasipo kushurutishwa. Na ndipo mzazi anapoona sababu ya kumwamini na kumwacha huru kabisa kabisa ayaongoze maisha yake mwenyewe.
 
Mfano mwingine tunaweza tukajifunza kwa mwanafunzi: alipokuwa shule ya msingi ni tofauti na atakapokuwa chuo kikuu, kule nyuma alikuwa analazimishwa kuwepo shule kila siku alfajiri, ahudhurie kila kipindi cha darasani, alilazimshwa avae sare, alichapwa alipokosea, alikaguliwa notes alizoandika n.k.. Lakini alipofika chuo hakuna tena sheria ya kumwambia aamke alfajiri kila siku aende chuo, ni kwasababu gani? Ni kwasababu chuo kinatambua kwamba Yule mtu anajielewa, hivyo hata asipohudhuria leo atakuwa na sababu za msingi za kutokufanya hivyo tofauti na alipokuwa shule ya msingi, mfano angepewa uhuru tu! Angeutumia katika michezo na utoro, kadhalika pia akiwa chuo hapewi sare, hashikiwi kiboko kulazimishwa kusoma, hakaguliwi notes n.k. lakini japokuwa hakuna sheria zote hizo, mwisho wa siku utakuta Yule mwanafunzi anafaulu. Unaona hapo? hayo yote haimaanishi kuwa chuo hakikuwa na sheria hapana, kilikuwa nayo sana tu, bali kimemweka huru mbali na ile sheria kwasababu kilitambua aliyefika chuo ameshajitambua vya kutosha na anajua jukumu lake kama mwanafunzi.
 
Kadhalika na katika KANISA LA MUNGU nalo pia limepitia katika hatua zote mbili: UTOTO na UTU UZIMA. Hatua ya utoto ni pale Mungu alipolizaa kanisa kwa mara ya kwanza kule jangwani, hivyo kama lilikuwa ni changa ni dhahiri kuwa lingehitaji kupewa sheria ya kuliongoza kwasababu halijaweza bado kupambanua mema na mabaya. Na ndio tunaona sheria/ Torati ilikuja na zile amri zote kutolewa kwa mkono wa Musa na kupewa watu, kwamba waishi katika hizo. Na kama tunavyojua sheria kwa mtoto inakuwa ni AMRI na sio OMBI, kadhalika na hawa nao (kanisa-jangwani waisraeli) ilikuwa ni AMRI kuzitimiza sheria za Mungu zilizotolewa, ndio maana ilikuwa ni amri mtu asiibe, asizini, asiue, aishike sabato, asiabudu sanamu n.k.na kwa yeyote asiyefanya aliadhibiwa vikali. Na kwasababu walikuwa ni watoto walifanya vile kwaajili ya kumridhisha tu baba yao (MUNGU), Walitimiza zile sheria sio kwasababu wanapenda hapana, ni kwasababu baba yao hapendi dhambi, laiti wangeachiwa uhuru kidogo wasingezishika.
 
Lakini ulipofika wakati wa KANISA LA MUNGU KUKUA, Ilipasa zile sheria ziingizwe ndani ya moyo wa kanisa ili zitimizwe kwa mapenzi ya mtu mwenyewe na sio mapenzi ya Mungu na bila shuruti. Kama biblia ilivyotabiri zamani za manabii tukisoma.
 
Yeremia 31: 31 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.
32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.
33 Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; NITATIA SHERIA YANGU NDANI YAO, NA KATIKA MIOYO YAO NITAIANDIKA; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
34 Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena”.
 
Jambo hili lilikuja kutimia siku ya PENTEKOSTE, pale ROHO wa Mungu alipomiminwa juu ya mioyo ya watu kwa mara ya kwanza na kuwafanya wavuke daraja la utoto na kuingia katika daraja la UTU UZIMA. Sasa kuanzia huo wakati Roho alipomshukia mtu, kitu cha kwanza alichokuwa anafanya ni kuiingiza ile sheria ndani ya moyo wake, kiasi kwamba Yule mtu ile sheria anakuwa anaitimiza kwa mapenzi yake mwenyewe na sio kwa mapenzi ya Mungu. Kama vile mwanafunzi aliyeko chuo anasoma kwa mapenzi yake na sio kwa mapenzi ya Baba yake au mama yake tofauti na alivyokuwa akifanya shule ya msingi. Hicho ndicho alichokifanya Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste. Na ndio anachoendelea kukifanya mpaka sasa hivi.
 
Sasa kuanzia ule wakati wote walioshukiwa na Roho wa Mungu, wakawa hawazini, sio kwasababu Mungu kawakataza bali ni kwasababu waliona ni kwa faida yao wenyewe, wakawa hawaabudu sanamu sio kwasababu Mungu kawakataza hapana bali ni kwasababu wanajua Mungu pekee ndiye anayestahili kuabudiwa, wakawa wanaomba sio kwasababu Mungu kawaagiza lakini kwasababu waliona umuhimu wa kuomba kama Mkristo ili kuepukana na majaribu, hawakuishika sabato kama amri, kwamba tumwabudu Mungu tu katika siku fulani, hapana bali sabato yao ilikuwa kila siku, kwasababu walijua Mungu haabudiwi katika siku Fulani bali katika Roho na Kweli.Kadhalika na zile sheria zote walizopewa walipokuwa wachanga walikuwa wanazitimiza pasipo AMRI bali kwa moyo na kwa uelewa. Kwasababu hiyo basi Mungu akawacha huru kabisa mbali na SHERIA na TORATI. Na ndio maana biblia inasema:
 
Wagalitia 5: 18 “Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria”. Na pia inasema…
Warumi 8: 2 “Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti”.
Warumi 8: 4 “ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho”.
 
Kwahiyo unaona hapo? Umuhimu wa kuwa na Roho Mtakatifu?..Ni kukufanya wewe utoke katika hali ya utoto wa kiroho(utumwa) na uingie katika hali ya utu uzima(Uhuru) na hiyo ndiyo neema. Ukiona mtu pale unapomuuliza ni kwanini huzini, au huibi? Na anakwambia ni kwasababu Mungu kanikataza, moja kwa moja unajua huyo bado ni mtoto yupo chini ya Sheria hata kama atajifanya yupo chini ya neema. Ukiona mtu anakwambia mimi nashikilia siku moja ya kuabudia sabato, unajua huyo naye yupo chini ya sheria ya utoto, au mtu akikuambia mimi sivai vimini, sinywi pombe, sivuti sigara kwasababu Mungu kakataza, ujue huyo pia ni mtoto bado hajawekwa huru na sheria ya dhambi, Ukiona mtu anasema mimi siabudu sanamu kwasababu amri ya 2 inasema hivyo, unajua kabisa huyo bado ni mtoto Roho wa Mungu bado hajamfanya kuwa huru nk….
 
Lakini wale wote waliowekwa huru na ROHO, hawataona mzigo wowote kuishi maisha ya utakatifu wataona kutokuzini, kutokuvaa vimini, kutokuweka make-up, kutokuvaa suruali, kutokusengenya, kutoiba, kutokwenda disco, n.k. wataona kuwa hayo ni majukumu yao na ni kwa faida ya Roho zao na sio kwa faida ya Mungu, au sio kwasababu Mungu kawaambia. Watafanya yote yawapasayo kufanya iwe ni Mungu kawaagiza, au hajawaagiza.. Na hiyo ndio DALILI ya mtu kuwa amepokea kweli kweli Roho Mtakatifu…Utakatifu anautimizwa kwa kupenda na sio kwa maagizo Fulani.
 
Warumi 8: 9 “Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake”.
 

Hivyo ndugu, na wewe upo katika uchanga au utu uzima?. Umejazwa Roho Mtakatifu au bado unaongozwa na dini?. Tafuta Roho Mtakatifu kumbuka Roho Mtakatifu ndio muhuri wa Mungu (Waefeso 4:30) pasipo huyo hakuna UNYAKUO.

Ubarikiwe sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

JIRANI YAKO NI NANI?

UMUHIMU WA KUISHI MAISHA YAMPENDEZAYO MUNGU SASA.

JIHADHARI NA ROHO ZIDANGANYAZO

JE! SISI NI WAFALME NA MAKUHANI KWA NAMNA GANI?

PETRO ALIAMBIWA NA BWANA YESU UKIONGOKA WAIMARISHE NA NDUGU ZAKO. JE! KUONGOKA MAANA YAKE NINI?


Rudi Nyumbani

Print this post

Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga

Licha ya kuwa na INJILI YA MSALABA,ambayo ndio kiini cha kila mwanadamu ipo injili nyingine pia ijulikanayo kama INJILI YA MILELE, hii ni tofauti na injili ya msalaba. Injili ya msalaba yenyewe inatangaza wokovu kwa mwanadamu tu, kwa kupitia mmoja naye ni YESU KRISTO BWANA wetu. Kwahiyo injili nyingine yeyote inayodai kumkomboa mwanadamu na haimweki Bwana Yesu kama kiini cha injili yenyewe, basi injili hiyo ni batili, kwasababu yeye pekee ndiye Njia, kweli na uzima, hakuna mtu yeyote atakayemwona Mungu, pasipo kupitia kwake yeye biblia inasema hivyo(Yohana 14:6).. Kwahiyo zipo injili nyingi zinazodai zinaweza kumkomboa mwanadamu lakini kati ya hizo ni moja tu itakayoweza kumkomboa mwananadau! Nayo ni Kwa kupitia Yesu Kristo, na ndio maana Mtume Paulo alisema|:
 
2Wakoritho 11: 4 “Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au INJILI NYINGINE msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye!”
 
Unaona hapo? Biblia inasema kuna Yesu mwingine, roho mwingine na injili nyingine tofauti na ile iliyohubiriwa na mitume. Kwahiyo injili yoyote inayohusishwa na ukombozi wa mwanadamu inapaswa imlenge YESU KRISTO ALIYESULIBIWA,akafa na kufufuka kama kiini cha Ukombozi wenyewe, kwa asilimia mia yeye peke yake na sio pamoja mtu mwingine.
 
Lakini leo kwa ufupi tutaitazama INJILI YA MILELE ambayo ipo na imezungumziwa katika biblia..kama tunavyosoma katika;
Ufunuo 14: 6 “Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, mwenye INJILI YA MILELE, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa,
7 akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji”.
 
Sasa hii injili ya milele ni ipi?
 
Kama jina lake lilivyo “Milele” inamaana kuwa ni injili ambayo Ipo milele yote, ilikuwepo kabla ya mwanadamu kuumbwa, ipo sasa, na itaendelea kuwepo milele na milele, Kumbuka INJILI YA MSALABA ilikuwa na mwanzo, na itakuwa na mwisho, mwanzo wake ilikuwa ni Kalvari, na mwisho wake itakuwa katika Unyakuo. Baada ya hapo hakutakuwa na nafasi tena ya ukombozi, kwasababu mlango wa neema utakuwa umefungwa. Kitakachokuwa kimebaki ni ile ile injili ambayo ilikuwepo milele na milele.
 
Na ndio maana ukisoma mstari huo hapo juu utaona kuwa yule malaika(mjumbe) anapita kuitangaza hiyo injili ambapo kwa wakati huo unyakuo wa kanisa utakuwa umeshapita na mlango wa neema ya kuokolewa utakuwa umefungwa kwa watu wa mataifa.
 
Kwahiyo injili hii ni tofauti na ya msalaba tuliyonayo sasa, hii ya msalaba tunaifahamu kwa “kuhubiriwa”. Hatuwezi kuifahamu pasipo kuhubiriwa ndio maana biblia inasema katika;
 
Warumi 10: 13 “kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana{YESU KRISTO} ataokoka.
14 Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? TENA WAMSIKIEJE PASIPO MHUBIRI?
15 Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!{INJILI YA MSALABA}”
 
Kwahiyo unaona hapo, ni lazima awepo mtu wa kuihubiri ndipo watu waokolewe.
 
Tofauti na ilivyo INJILI YA MILELE. Injili hii haisambazwi kwa kuhubiriwa na mtu yeyote, Ni Mungu mwenyewe anaiweka ndani ya mtu, katika eneo maalumu la moyo wa mwanadamu linaloitwa “DHAMIRA”..ambayo kila mtu anazaliwa nayo. Na inafanya kazi ya kuhukumu njia zote mbaya zinazokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu ndani ya mtu..Na Injili hii haipo tu kwa wanadamu, ilikuwepo hata kwa malaika, kwasababu ni ya milele, ilikuwepo huko enzi na enzi, ipo na itakuwepo.
 
Kwahiyo sasa kitendo tu cha mtu kuwa mwanadamu, tayari moja kwa moja kuna kitu ndani yake kitakuwa kinamshuhudia mambo yanayofaa na yasiyofaa, bila hata kuhubiriwa au na mtu yeyote, au kukumbushwa na mtu yeyote, kwamfano, kila mtu anafahamu kuwa uuaji sio sawa, iwe anayo hofu ya Mungu au hana hofu ya Mungu, kila mtu anafahamu kuwa dhuluma ni mbaya, hata kama sheria isingesema hivyo, ndani ya moyo wake dhamira inamuhubiria kuwa kitendo hicho ni kibaya, Kadhalika haihitaji kuifahamu biblia kujua kuwa uonevu ni makosa, wizi ni makosa, utukanaji, ubakaji, rushwa ni makosa hayo yote hata kama mtu hajawahi kumsikia Mungu, au chochote kinachoitwa Mungu anajua kabisa hayo mambo hayafai kufanya, pia haihitaji kwenda katika vyuo vya biblia kutambua kuwa kulala na ndugu yako wa damu ni makosa, kadhalika na ushoga au usagaji ni makosa, utajikuta tu wewe mwenyewe unachukia kufanya hivyo au unalipinga hilo wazo ndani yako pale linapokuja kwasababu unajua kabisa kuwa hayo ni makosa. Sasa hiyo ndio inayoitwa INJILI YA MILELE, Mungu anayoihubiri ndani ya moyo wa mtu. Na ndiyo hiyo siku za mwisho itakuja kukumbushwa kwa watu, wamche Mungu.wakati huo unyakuo utakuwa umeshapita.
 
Kwahiyo usidhani kuwa wale watu ambao hajasikia habari za YESU(Injili ya msalaba) mahali popote, hawatahukumiwa. Hapana Watahukumiwa tu kama wale wengine kwa injili hiyo. Watu wa kipindi cha Nuhu hawakuwa na sheria waliyopewa na Mungu kama watu wa Musa na kuendelea,Na ndio maana Mtume Paulo alieleza habari za watu hawa kama tunavyosoma katika…
 
Warumi 1: 17 Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.
18 Kwa maana GADHABU YA MUNGU imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu.
19 Kwa kuwa MAMBO YA MUNGU YANAYOJULIKANA YAMEKUWA DHAHIRI NDANI YAO, KWA MAANA MUNGU.
20 Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; YAANI, UWEZA WAKE WA MILELE NA UUNGU WAKE; hata wasiwe na UDHURU;
21 kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.
22 Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika;
23 wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo.
24 Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao.
25 Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.
26 Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili;
27 wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.
28 Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.
29 Wamejawa na UDHALIMU, UOVU na TAMAA na UBAYA; wamejawa na HUSUDA, na UUAJI, na FITINA, na HADAA; watu wa NIA MBAYA, wenye KUSENGENYA,
30 wenye KUSINGIZIA, wenye KUMCHUKIA MUNGU, wenye JEURI, wenye KUTAKABARI, wenye MAJIVUNO, wenye KUTUNGA MABAYA, WASIOTII WAZAZI WAO,
31 wasio na UFAHAMU, wenye KUVUNJA MAAGANO, WASIOPENDA JAMAA ZAO, WASIO NA REHEMA;
32 ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao.
 
Umeona hapo ndugu, biblia inasema wakijua kabisa watendao mambo kama hayo wamestahili mauti lakini bado wanayatenda. Dhamira zao zikiwashuhudia ndani kuwa wanayoyafanya sio sahihi lakini wanaendelea kuyafanya, Na wewe je! Ambaye upo kwenye dhambi utahitaji mhubiri siku moja aje kukuthibitishia kwenye biblia kwamba, uvutaji sigara ni dhambi, au uasherati ni dhambi?? Angali ndani ya moyo wako dhamira inakushuhudia kabisa unachofanya ni makosa?..hakika unaweza usilione lakini fahamu kuwa hukumu inakungojea.!
 
Wewe unayevaa vimini, na kutembea nusu uchi barabarani unasema Mungu haangalii mavazi lakini moyo wako unakuambia kabisa hayo ni makosa unayoyafanya na bado unaweka moyo mgumu, wewe unayevaa suruali,unayepaka wanja, na kupaka lipstick, na kuvaa wig na hereni, Hukumu ipo mbeleni dada!, wewe unayesengenya, wewe ambaye ni shoga, wewe unayejisaga, wewe unayetoa mimba, wewe uliye mwasherati, wewe uliye mlevi, wewe unayetazama pornography, wewe unayefanya masturbation, wewe unayeabudu sanamu za watakatifu waliokufa zamani angalia biblia inavyokuambia hapo juu < wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu(sanamu), na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo >..Unaona unajua kabisa Mungu hawezi kufananishwa na mfano wowote wa kinyago cha kuchonga lakini wewe bado unakwenda kuvipiga magoti na kuviabudu..
 
2Wakorintho 6: 16 inasema “Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu?”..
 
Lakini biblia inaendelea kusema kwa jinsi utakavyozidi kuweka moyo wako mgumu, kuna kipindi kitafika Mungu anakuacha uendelee hivyo hivyo kwasababu umekataa kuitii hiyo sauti inayosema ndani yako, mpaka ile siku ya hukumu ije na utaingia kuzimu!! Alisema “”28 Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa”.
Kwahiyo dada/kaka hukumu ya Mungu haikwepeki hata uwe nje ya kanisa, njia pekee ni kujisalimisha maisha yako kwa BWANA YESU ambaye yeye ndiye aliyetoa uhai wake ili akuokoe, Tubu geuka, ukapewe uwezo wa kushinda dhambi. Muda umekwenda kuliko unavyodhani, na Injili ya msalaba sio ya milele utafika wakati utatamani uingie utakosa, muda ndio huu, mpe Bwana maisha yako tangu sasa.
 
Ubarikiwe.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
 
Tafadhali “Share” kwa wengine na Mungu atakubariki
https://wingulamashahidi.org/2019/10/17/nilimwona-shetani-akianguku-kutoka-mbinguni/
https://wingulamashahidi.org/2019/08/12/usitafute-faida-yako-mwenyewe-bali-ya-wengine/

Print this post

Je! ni kweli dunia iliumbwa takribani miaka 6000 iliyopita? na je! shetani alikuwepo duniani wakati dunia inaumbwa?

JIBU: Kulingana na hesabu ya vizazi na miaka yao waliyoishi katika biblia, inakadiriwa tangu Edeni mpaka wakati wa Gharika, ni miaka elfu 2, na tangu wakati wa gharika mpaka kuzaliwa kwa Bwana Yesu ilipita miaka elfu 2 hivi, na tangu kipindi cha Bwana wetu Yesu hata leo nacho pia ni kipindi cha miaka elfu 2 kimepita. Kwahiyo jumla yake tangu Edeni mpaka sasa ni miaka kama elfu 6 hivi, au imezidi kidogo au imepungua kidogo..Sasa kumbuka huo ulikuwa ni mwanzo wa Edeni, lakini haukuwa mwanzo wa Dunia..dunia ilikuwepo kabla ya Edeni..Tunasoma.
 
Mwanzo 1:1 “hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi”
 
…hapa hajasema huo mwanzo ulikuwa ni wa miaka mingapi iliyopita inaweza ikawa ni miaka elfu kumi, milioni kumi au vinginevyo…
 
lakini mstari wa pili unasema nayo nchi ilikuwa ukiwa na utupu inamaanisha kuwa kuna jambo lilitokea likaifanya hiyo nchi kuwa ukiwa baada ya Mungu kuziumba mbingu na nchi na hapa si mwingine zaidi ya shetani ndiye aliyeiharibu na kuifanya ukiwa (kama anavyoendelea kuiharibu sasa hivi) maana Mungu hakuiumba ukiwa yaani dunia iwe ukiwa bali ikaliwe na watu,
 
Isaya 48:18 inasema
 
18 Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine. “.
 
Lakini baada ya dunia kuharibiwa kwa viwango vya hali ya juu, ikapoteza umbo lake ikawa kama moja ya sayari nyingine, na ndio tunaona Mungu akaanza kufanya uumbaji upya baada ya nchi kukaa muda mrefu katika hali ya ukiwa, hapo mbingu na nchi zilikuwa tayari zimeshaumbwa muda mrefu nyuma.
 
Kwahiyo mwanadamu na viumbe vyote inakadiriwa viliumbwa takribani miaka  6000 iliyopita lakini dunia iliumbwa kabla ya hapo na shetani alikuwepo duniani kabla ya mwanadamu kuumbwa, kwasababu tunamuona alionekana katika bustani ya Edeni na biblia inamwita shetani kama yule nyoka wa zamani
 
Ufunuo 20:2 Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu;,
 
kwahiyo inamaanisha alikuwepo toka zamani kabla hata ya mwanadamu kuumbwa, ambapo tunaona alitupwa huku duniani baada ya kuasi mbinguni pamoja na malaika zake.
 
Ubarikiwe sana.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada zinazoendana:

JUMA LA 70 LA DANIELI

Kati ya Unyakuo wa kanisa, Dhiki kuu, Vita vya har-magedoni, Utawala wa miaka 1000, Vita ya Gogu na Magogu, hukumu ya kiti cha enzi cheupe. Je, ni kipi kinaanza na kingine kufuata?

SIKU YA BWANA INAYOTISHA YAJA!

AMIN! NAWAAMBIA KIZAZI HIKI HAKITAPITA!


Rudi Nyumbani:

Print this post

Nini maana ya kusali kwa kupayuka payuka?

Swali linaendelea…..Na Je, nisali kwa namna gani ili maombi yangu yasionekane kuwa ni ya kupayuka payuka mbele za Mungu?
 
JIBU: Mungu akubariki ndugu, Mathayo 6:7 Inasema:
 
Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi.
 
 Sasa mstari huo ukiangalia kwenye tafsiri nyingine hilo neno “kupayuka-payuka” halimaanishi kama “kupaza sauti kwa nguvu,” kama watu wengi wanavyodhani, hapana bali linamaanisha “KURUDIA-RUDIA” maneno yale yale, Hilo la kupaza sauti kwa nguvu mstari wake ni ule wa juu yake kabla ya huu unaosema:
 
“Mathayo 6: 5 Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao.
 
6 Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
 
 
Unaona, aina hii ya watu ndio wanaopenda kupaza sauti zao kwa nguvu kwa lengo la kuonekana na watu ndio hao wanaoonekana wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia. Watu wa namna hiyo Bwana anasema Wamekwisha kupata thawabu yao, Lakini pia kumbuka hilo halimaanishi watu wasiombe kwa kupaza sauti zao, hapana, biblia inasisitiza sana tupaze sauti zetu tumliliapo Mungu…Lakini sio kwa lengo la kujionyesha sisi tunajua kusali, au sisi ni wa kiroho sana. Vinginevyo tutakuwa tumeshapata thawabu zetu.
 
Lakini sasa kwa wale wanao payuka payuka mstari wao ndio huo unaofuata…
 
 
7 Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi.
8 Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. “
 
Hivyo watu wanao rudia-rudia maneno, kwa mfano watu dini nyingine na watu wanaosali rozari na sala za bikira mariamu wanafahamu, huwa wanarudia rudia maneno yale yale kwa muda mrefu hata masaa na masaa wakidhani kuwa kwa kufanya vile Mungu atasikia dua zao. Hizo ni desturi za kipagani ndio maana tumeonywa tusifanane na hao. kwahiyo tunapoenda mbele za Mungu tuwe na malengo, tutoe hoja zetu zote, kisha zikishaisha, basi, tushukuru tuondoke Tukiamini kuwa Mungu kashatusikia na sio kuanza kurudia rudia tena kile tulichokiomba kana kwamba Mungu hasikii,. kwa ufupi usiweke mfumo fulani unaoonyesha mrudio rudio katika kusali, kuwa huru mbele za Mungu ndivyo Sala zako zitakavyokuwa na thamani mbele za Mungu.
 
Ubarikiwe sana.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada zinazoendana:

Biblia ituambia tusalimiane kwa busu takatifu. Hili busu ndio lipi?

JE! NI LAZIMA WATU WOTE WANENE KWA LUGHA?

Kunena kwa lugha kukoje?

“heri walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao” je hatuna ruhusa ya kuwa matajiri katika roho?


Rudi Nyumbani:

 

Print this post

Je! wayahudi wote wataokolewa kulingana na Warumi 11:26?

 SWALI: Je! Wayahudi wote wataokolewa? maana biblia inasema katika;

Warumi 11:25 “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili.
26 Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake”.

Hapo anaposema Israeli wote wataokoka, je hata kama ni watenda dhambi wataokolewa siku ya mwisho?


JIBU: Watu wengi wanadhani hivyo, lakini ukweli ni kwamba Hapana! sio waisraeli wote watakaookolewa bali wale tu walioishi maisha yanayolingana na torati yao ila wengine wasioishi kulingana na maagizo ya dini yao (torati) watahukumiwa kama tu watu wasioamini…

Warumi 9:6-7 ” Si kana kwamba neno la Mungu limetanguka. Maana hawawi wote Waisraeli walio wa uzao wa Israeli. Wala hawawi wote wana kwa kuwa wazao wa Ibrahimu, bali, Katika Isaka wazao wako wataitwa; ”

 Unaona hapo! ni kama tu vile si “wakristo” wote walio “wa-kristo” kwelikweli isipokuwa wale waliozaliwa mara ya pili, na kuishi maisha matakatifu. Wapo wengi leo wanaojiita wakristo, kwasababu tu wamezaliwa kwenye familia za kikristo lakini ukiangalia mienendo yao, na matendo yao hayaendani na ukristo, sasa hao wanakuwa ni wakristo-jina vivyo hivyo na kwa wayahudi. Wapo wayahudi wengi leo hii japo ni wayahudi kweli kweli lakini hawaamini hata kama kuna Mungu ni kama wapagani, na hata hawamtazamii Masihi wao, wanapinga kila imani!.

Sasa mtu wa namna hiyo hawezi kuokolewa isipokuwa labda atubu na kubadili mwenendo wake?.Hata katika biblia agano la kale wapo wengi ambao waliharibiwa na Mungu japo walikuwa ni wayahudi kweli kweli mfano tunao Kora na Dathani, na wale wana wawili wa Eli n.k. Wapo wengine pia biblia inarekodi ni wachawi, na wapinga-kristo mfano tunamwona yule aliyekutana na Paulo aliyeitwa Bar Yesu:

Matendo 13:6 “Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, MCHAWI, nabii wa uongo, MYAHUDI jina lake Bar-Yesu;

7 mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu.

8 Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani.

9 Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho,

10 akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? “

Unaona Bar Yesu alikuwa mchawi, Kwahiyo siyo wayahudi wote walio waisraeli, na sio wayahudi wote watakaookolewa bali ni wale watakaozishika amri za Mungu ambao majina yao yameandikwa kwenye kitabu cha uzima kabla misingi ya ulimwengu kuwekwa.

Lakini ijapokuwa kwasasa hivi wayahudi wengi hawamkubali Yesu kama masihi wao (Lakini wanamwamini YEHOVA), Hiyo Mungu karuhusu ni kwa makusudi kabisa ya Mungu kafanya hivyo ili sisi mataifa tupate neema ya kuokolewa, lakini utafika wakati nao umeshakaribia ambapo neema itaondoka kwetu na kurejea tena israeli, wakati huo wayahudi wengi (walio wayahudi hasaa wenye hofu ya Mungu) watampokea Kristo kama Masihi wao, na kubatilisha desturi zao za sheria na kuipokea neema ya BWANA YESU KRISTO.

Warumi 11:24 “Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa ukatolewa katika mzeituni, ulio mzeituni mwitu kwa asili yake, kisha ukapandikizwa, kinyume cha asili, katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana wale walio wa asili kuweza kupandikizwa katika mzeituni wao wenyewe?

25 Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili.

26 Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake.

Na baada ya hayo kutokea hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.(Mathayo 24:14), je! jiulize wakati sasa neema inakaribia kuondoka huku kwetu wewe umeipokea? kwasababu utafika wakati utatamani kuingia utashindwa pale mwenye nyumba (Bwana Yesu) atakaposimama na kufunga mlango Luka 13:25..biblia inasema mlango ni mwembamba na njia imesonga iendayo uzimani na wanaoiona ni wachache, je! na wewe umeiona njia? je! taa yako inawaka, maisha yako yanahakisi wokovu? muda umekwenda kushinda tunavyofikiri kama Mungu aliweza kuwakatilia mbali watu wake (wayahudi) ili sisi mataifa ambao tulikuwa makafiri tupate neema, unadhani atashindwa kutukatilia na sisi mbali ili awarejee watu wake wateule israeli?? Ambapo hivi karibuni atafanya hivyo?.

Waebrania 2:3″ sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia;”

Ubarikiwe sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

MAJONZI YA MTUME PAULO KWA NDUGU ZAKE.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita.

FANYA KAMA UONAVYO VEMA.

NINI KINATOKEA BAADA YA KIFO?

AINA SABA (7) ZA UNAFIKI, AMBAZO UNAPASWA UJIEPUSHE NAZO.

Rudi Nyumbani

Print this post

SWALI : Dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu ni ipi?

JIBU: Tukisoma;

Mathayo 12:25-32 ” Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo.

25 Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama.

26 Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje?

27 Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu.

28 Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.

29 Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake.

30 Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya.

31 Kwa sababu hiyo nawaambia, KILA DHAMBI, NA KILA NENO LA KUFURU, watasamehewa wanadamu, ILA KWA KUMKUFURU ROHO HAWATASAMEHEWA.

32 Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao. “

Tunavyosoma mistari hiyo tunaona kabisa wale Mafarisayo walikuwa wanajua Bwana Yesu ni kweli alikuwa anatoa pepo, na kutenda mambo yote kwa uweza wa Roho wa Mungu, lakini wao kwa ajili ya wivu, na kwa tamaa zao wenyewe, ili tu wawavutie watu kwao, wakakusudia kwa makusudi kabisa, wawageuze watu mioyo ili watu wasimuamini Bwana Yesu,wawaamini wao, na ndipo wakaanza kutoa maneno ya makufuru wanawaambia watu kuwa BWANA anatoa pepo kwa uwezo wa belzebuli mkuu wa Pepo angali ndani ya mioyo yao walikuwa wanajua kabisa anachofanya ni kwa uweza wa Roho wa Mungu.

Ukweli wa jambo hilo unajidhihirisha kwa Nikodemo ambaye naye alikuwa ni mmoja wa wale mafarisayo alipomwendea Yesu usiku na kumwambia

Yohana 3:1-2″Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi.

2 Huyo alimjia usiku, akamwambia, RABI, “TWAJUA” YA KUWA U MWALIMU, UMETOKA KWA MUNGU; KWA MAANA HAKUNA MTU AWEZAYE KUZIFANYA ISHARA HIZI UZIFANYAZO WEWE, ISIPOKUWA MUNGU YU PAMOJA NAYE. “

kwahiyo unaona walikuwa wanajua kabisa lakini kwa ajili ya wivu wakaanza kuzusha maneno ya uongo juu ya kazi ya Roho wa Mungu, sasa huko ndiko kumkufuru Roho Mtakatifu. hivyo basi Bwana Yesu alitoa angalizo tunapozitazama kazi za Mungu, pale mtu mwenye Roho wa Mungu anatenda kazi za Mungu kweli huku tunajua ni Mungu ndiye anayefanya kazi ndani yake, na kuanza kusema yule ni mchawi, au anatumia uchawi, au mshirikina, au tapeli, au mwizi, ili tu watu wasiziamini kazi za Mungu au vinginevyo, au unaanza kuzusha propaganda za uongo juu yake, pengine kwa kusudi la kumkomoa! hapo ndugu utakuwa unajimaliza mwenyewe. (Ni kweli si watumishi wote ni wa Mungu, hao ni sawa kuufunua uovu wao). Lakini Hapa tunamzungumzia yule unayemfahamu kabisa ni mtumishi wa BWANA,..wewe hujui umewakosesha wangapi, ambao kwa kupitia yeye, watu wengi wangeokolewa? kufanya hivyo ni hatari sana tuwe makini.

Hivyo hii dhambi inawahusu wale wanaozipinga kazi za Mungu kwa makusudi kabisa (Mfano wa mafarisayo). Hao kwao hakuna msamaha, hawawezi tena kutubu hata iweje wanachongojea ni ziwa la moto.

Lakini shetani naye anapenda kulitumia hili neno kuwafunga watu wajione kuwa wamemkufuru Roho Mtakatifu na kwamba dhambi zao hazisameheki hata wafanyeje,
Hii inakuja sana sana kwa watu waliowachanga ki-imani, kuna shuhuda nyingi za watu waliofungwa na shetani kwa namna hiyo wakidhani kuwa dhambi zao hazisameheki, kuna watu wamekata tamaa wanajiona kwa wingi wa dhambi zao, Mungu hawezi kuwasemehe tena, pengine wameua, wametoa mimba sana, n.k, Sasa jambo la namna hii likija katika mawazo yako likatae linatoka kwa yule mwovu kukufanya wewe ujione kuwa Mungu hawezi kukusamehe umemkufuru, hivyo usijisumbue kutubu kwasababu Mungu hatakusikiliza.

Kumbuka kama tulivyosema Dhambi hii inakaa kwa wale watu ambao ndani yao mioyo ya toba imekufa, au hofu ya Mungu haipo tena kwao, watu waliojikinai, wanaompinga Mungu katika fikra zao japo kuwa walimjua Mungu na uweza wake wote, wanazipotosha kazi za Mungu kwa makusudi kwa faida zao wenyewe, ili wawavute watu kwao, au wawe washirika wao na sio kwa Mungu. Hivyo basi kitendo tu cha wewe kuwa na hii hofu ya kumwogopa Mungu ujue Roho wa Mungu anatenda kazi ndani yako na hayo mawazo ya kwamba umemkufuru Roho Mtakatifu yapinge huyo ni adui ndio moja ya njia zake hizo ili usiufikie wokovu na anapenda kuwatesa watu wengi katika andiko hili.

Ubarikiwe sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada zinazoendana:

DHAMBI YA MAUTI

DHAMBI ILIYOMKOSESHA SHETANI.

DHAMBI ZINAZOTANGULIA NA ZINAZOFUATA.

DHAMBI ISIYO NA MSAMAHA.


Rudi Nyumbani:

Print this post

Je! dhambi zote ni sawa Kuna dhambi kubwa na ndogo?

 

SWALI: Naomba kufahamu Je! Kuna dhambi kubwa na ndogo, na kama hakuna je! Mtu aliyeua na aliyetukana je watapata adhabu sawa?


JIBU: Dhambi ni dhambi iwe kubwa au ndogo, zote ni kosa, biblia inasema.

Yakobo 2:10 “Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote.

11 Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sheria. “

Unaona hapo? Kwahiyo mtu akitenda dhambi iwe kubwa au ndogo ataadhibiwa. lakini adhabu zitatofautiana huko waendako kulingana na wingi wa makosa, kwasababu Bwana Yesu pia alisema aliyeua kwa upanga atauawa kwa upanga, apandacho mtu ndicho atakachovuna. adhabu ya shetani haiwezi ikawa sawa na adhabu ya mwanadamu. Biblia inaeleza..

Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, ATAPIGWA SANA.

48 Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, ATAPIGWA KIDOGO. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi. “

Kwahiyo mapigo yanatofautiana kulingana na matendo ya mtu aliyoyatenda akiwa hapa duniani, ni kama tu vile thawabu zitavyotofautiana kwa mtu na mtu mbinguni kwa jinsi alivyotaabika katika kumtumikia Bwana vivyo hivyo na jehanamu adhabu zitatofautiana kulingana na dhambi mtu alizotenda akiwa ulimwenguni. Na jinsi gani alivyoipuuzia neema ya wokovu.

Hivyo hatupaswi kuipima dhambi kwa namna yoyote, ni kukaa nayo mbali kwasababu iwe ni kubwa au ndogo mshahara wake ni MAUTI, Warumi 6:23.

Dhambi kubwa na ndogo zote zina adhabu ya mauti.

Je! Umempa Yesu maisha yako ndugu yangu? Unatambua kuwa hizi ni nyakati za mwisho?. Ukifa leo utakuwa mgeni wa nani, huko uendako?. Tubu sasa mgeukie yeye atakusamehe, na kukupa uzima wa milele.

Mungu akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada nyinginezo:

Dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu ni ipi?

“Yodi” ni nini ?

Nini maana ya “Kandake” (Matendo 8:27)

Wote wanaokumbwa na mauti sasa ni kutokana na dhambi zao?

Je wale waliomsulubisha Bwana, wataenda mbinguni, kwakuwa walisamehewa?

UNYAKUO.

Rudi Nyumbani 



Print this post