KUNENA KWA LUGHA.
Kuna aina nyingi za lugha, zipo lugha za wanadamu na lugha za malaika, lugha za wanadamu ndio kama hizi tunazozifahamu na kuzizungumza; Kiswahili, kingereza, kiarabu, kizulu n.k..Na lugha za malaika nazo zipo nyingi, hatuwezi tukazielewa kwa upeo wetu wa kibinadamu.
1Wakoritho 13: 1 “Nijaposema kwa LUGHA ZA WANADAMU na ZA MALAIKA, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao”.
Sasa moja ya ishara kubwa kati ya nyingi ambayo Bwana aliichagua siku ile ya Pentekoste ijidhihirishe kama ushahidi kuwa Roho Mtakatifu amemwagwa juu ya watu wake ni ISHARA YA LUGHA. Kumbuka: angependa kutumia ishara nyingine pia angeweza, kama watu kutabiri, watu kung’aa nyuso zao kama Musa, n.k lakini yeye alipenda kutumia ishara ya lugha, kama tu alivyotumia ishara ya lugha kuwatapanya watu waliokuwa wanaujenga mnara wa Babeli. Sasa kilichotokea siku ile ya Pentekoste baada ya Roho Mtakatifu kushuka juu ya watu, watu kujikuta wanapata msukumo wa ajabu(au uwezo wa ajabu) kuzungumza lugha wasizozijua.
Na lugha hizo hazikuwa lugha za MALAIKA hapana! Bali zilikuwa ni lugha za WANADAMU. Ili tuelewe vizuri tujifunze kwa mfano ufuatao. Petro mwanafunzi wa Yesu alikuwa anaongea ki-galilaya lakini hawezi kuongea kiyunani, Roho aliposhuka juu yake siku ile ya Pentekoste, alisikia uwezo na msukumo wa ajabu ndani yake, na kujikuta anamtukuza Mungu kwa lugha nyingine pasipo kujua ile lugha anayoizungumza ni ya kiyunani. Na kadhalika Mathayo naye lugha yake ya asili ni ki-galilaya lakini nguvu ilipomjia akajikuta anamtukuza Mungu kwa lugha ya kiarabu, pasipo kujua kwamba anaongea kiarabu..na vivyo hivyo kwa wanafunzi wengine wote na wale wote waliokuwepo siku ile ya Pentekoste.
Sasa wao pasipo kujua kwamba zile lugha wanazoziongea ni lugha halisi, wale watu wa nje ndio waliowasikia wanazungumza kwa lugha zao, labda tuseme kuliwepo na wayunani pale ghafla wanamsikia mtu akimtukuza Mungu huko ghorofani kwa lugha ya kiyunani, na hali anajua kabisa pale mjini wayunani wenzake ni wa kubahatisha, na Kadhalika kama palikuwepo na muarabu kafika pale mjini Yerusalemu kwa biashara yake, ghafla anamsikia mtu huko ghorofani anapaza sauti akimshukuru Mungu kwa lugha yake ya kiarabu, tena kiarabu kile cha ndani kabisa na hali anajua kabisa katika huo mji hakuna waarabu wenzake wengi, na cha ajabu akimtazama mtu anayenena hana hata dalili ya kufahamu tamaduni za kiarabu,ni wazi kabisa ataishia kuduwaa tu!. Sasa ndicho kilichotokea siku ya Pentekoste.
Ni mfano leo usafiri na kwenda Kijiji kimoja huko China, na wakati umefika huko, unamsikia mchina mmoja huko anaongea kichaga kile cha ndani kabisa, wakati unajiuliza hilo ni nini, unasikia mchina mwingine huko anamsifu Mungu kwa kimakonde! Bila shaka utashangaa na kujiuliza hawa wote si ni wachina! Imekuwaje basi mimi kuwasikia wakizungumza kwa lugha zetu za asili za kiafrika?. Sasa hiyo ishara ya lugha Bwana Yesu aliiachia siku ile ya Pentekoste ili watu wote wajue kwamba kuna kitu kipya kimemwagwa duniani (nacho si kingine Zaidi ya Roho Mtakatifu). Lakini Roho Mtakatifu mwenyewe sio lugha, kama tulivyosema hiyo ni ishara Roho Mtakatifu aliyoichagua tu kujidhihirisha yeye, anaweza akatumia ishara nyingine tofauti na hiyo, mtu akishindwa kuelewa hilo, atadhani kuwa asiponena kwa lugha basi hana Roho Mtakatifu ndani yake, Na ndio hapo inapelekea kulazimisha kufanya hivyo na asiponena mwisho wake anaishia kunena kwa akili zake tu, na sio kwa jinsi Roho anavyowajalia.
Kunena kwa lugha ni karama Roho wa Mungu anayoitoa kama yeye apendavyo na sio kila mtu anaweza kuwa nayo. Sasa nini kinatokea Roho Mtakatifu anapoingia ndani ya Mtu?Roho Mtakatifu anapoingia ndani ya mtu, hali atakayoisikia mtu yule kwa mara ya kwanza sio kunena kwa lugha, kwasababu lugha kazi yake ni ishara kwa watu wa nje wasioamini, kuwaonyesha kwamba kuna jambo jipya limeshuka juu ya huyo mtu, lakini kama Roho ameshuka juu ya mtu na yule mtu yupo peke yake, hakuna lugha hapo!.
Jambo la kwanza atakalolisikia yule mtu ndani yake baada ya Roho Mtakatifu kushuka ni badiliko kubwa ndani ya moyo wake, atajisikia anaichukia dhambi, na maisha yake ya zamani, atajikuta anatamani na anakuwa na kiu ya KUWA MTAKATIFU, na huo ndio uthibitisho wa kwanza na sio kutamani kunena kwa lugha, au kuona maono, au kutabiri.Uthibitisho wa ROHO YA UASHERATI ndani ya mtu ni UASHERATI sio kuzungumza kingereza, vivyo hivyo uthibitisho wa ROHO YA MAUAJI ndani ya mtu ni MAUAJI anayoyafanya na sio elimu yake, huwezi kusema elimu ya mtu ndio uthibitisho wa Roho ya mauaji iliyopo ndani ya huyo mtu, Vivyo hivyo na ROHO MTAKATIFU kama jina lake lilivyo “MTAKATIFU” uthibitisho kwamba mtu yule anaye Roho Mtakatifu ndani yake ni UTAKATIFU ANAOUISHI, na sio lugha anazoziongea, Kwahiyo hizi lugha, ni ISHARA TU na Bwana anachagua nani wa kumpa hii na nani wa kumpa ile.
Hivyo jambo la kwanza mtu akipokea Roho Mtakatifu ni kuanza kuona ile kiu ya kupenda dhambi inakufa, anaanza kupenda kuwa MTAKATIFU na kuishi maisha ya kumcha Mungu, Sasa vya ziada ndio hizo ishara nyingine zinafuatana naye, labda anaona MAONO, lakini haneni kwa lugha, sasa mtu kama huyo anaweza akadhani hajapokea Roho Mtakatifu kwasababu tu hajanena kwa lugha, hajui kwamba Roho Mtakatifu yupo ndani yake, na amemchagulia ishara ya Maono iambatane naye badala ya ishara ya lugha.
Mwingine katubu dhambi na ghafla anaona kiu ya kupenda dhambi inakufa anatamani na anaanza kuishi maisha ya UTAKATIFU, lakini anajigundua kila anapolala anaota ndoto na zile ndoto zinakuja kutokea kama zilivyo, lakini hajanena kwa lugha, naye huyo Roho kapenda kumpa kipawa cha NDOTO badala ya lugha, Vivyo hivyo na wengine watapewa, karama za uponyaji badala ya LUGHA, wengine watapewa karama za unabii badala ya lugha, wengine watapewa karama neno la faraja, wengine karama za neno la maarifa, wengine watapewa uinjilisti badala ya lugha, wengine watapewa lugha badala ya uinjilisti, na maono, wengine waalimu, wengine wachungaji, N.k na wengine watapewa karama mbili mbili, wengine tatu tatu, wengine moja tu n.k Lakini wote hawatenena kwa lugha wala wote hawatakuwa manabii n.k na ndio maana Mtume Paulo ililisema hilo katika..
1Wakoritho 12: 28 “ Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha.29 Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza?30 Wote wana karama za kuponya wagonjwa? WOTE WANENA KWA LUGHA? Wote wafasiri?”
Umeona hapo? Sio wote watanena kwa lugha. Hivyo usikazane kutafuta kunena kwa lugha, kama hiyo karama haipo ndani yako,[sisemi kama ukimwomba Mungu hatakupa,] lakini ikiwa haipo ndani yako zidi kujaa Roho Mtakatifu, na baki katika nafasi uliyoitiwa.
Ubarikiwe.
Ikiwa utahitaji msaada zaidi ya mafundisho ya kila siku/maombezi/ubatizo/ushauri basi wasiliana nasi kwa namba zetu hizi +255693036618/+2557890001312
Au jiunge na makundi yetu ya mafundisho ya kila siku kwa kwa njia ya Whatsapp kwa kubofya hapa >>>> WHATSAPP GROUP
Print this post
Asante mtumishi Mungu akubariki na azidi kukutenda mema
asante sana mtumishi.
Amen
Barikiwa sana mwalimu.
Mbariwe