Neno la Mungu linasema katika …
Warumi 14:10 “……. Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu.
11 Kwa kuwa imeandikwa, Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri Mungu.
12 Basi ni hivyo, KILA MTU MIONGONI MWETU ATATOA HABARI ZAKE MWENYEWE MBELE ZA MUNGU”.
Siku ya hukumu inakuja..Ambapo kila mtu atatoa habari zake mwenyewe atasimama mbele ya kiti cha hukumu na kuhukumiwa iwe ni mtakatifu, iwe ni mwenye dhambi…Mhubiri 3:17 “Nikasema moyoni mwangu, Mungu atawahukumu wenye haki na wasio haki..”
Hukumu ya watakatifu itakuwa tofauti na hukumu ya wenye dhambi..Watakatifu hawatahukumiwa kwa lengo la kuadhibiwa, bali ajili ya thawabu. Aliyekuwa mwaminifu Zaidi atapewa thawabu nyingi Zaidi na aliyekuwa mwaminifu kidogo atalipwa kidogo. Lakini ambaye hakuwa mwaminifu kabisa huyo atahukumiwa adhabu ya kutupwa katika ziwa la moto pamoja na wenye dhambi.
Na wale walio waovu sana watahukumiwa Zaidi kuliko hao wengine.
Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.
48 Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi”.
Na miongoni mwa watakaohukumiwa kutupwa katika ziwa la moto, kila mmoja atahukumiwa kulingana na matendo yake..Ufunuo 20:13 “Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake”
Ufunuo 2:23 “Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake.
Siku hiyo kama vile mwezi unavyoangaza watu wote wakiuona juu..ndivyo itakavyokuwa siku hiyo Maisha ya kila mtu yataangazwa tangu anazaliwa mpaka anakufa, siku moja baada ya nyingine, lisaa limoja baada ya lingine, dakika moja hadi dakika nyingine..mambo yote aliyoyafanya na kuyawaza kwa wazi na kwa siri yatawekwa hadharani. Na kila Neno na tendo litapimwa…Na kutakuwa na kuulizwa maswali kwanini ulifanya hivi au kwanini ulifanya vile, ulikuwa na lengo gani la kufanya vile. Na kila tendo na Neno litapimwa na kuangaliwa lilileta hasara kiasi gani katika ufalme wa Mbinguni..Na kila mtu atatoa habari zake mwenyewe, atatoa hesabu na sio maelezo..Kuna tofauti ya kutoa hesabu na kutoa maelezo..Biblia inasema hivyo..
Mathayo 12: 36 “Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu.
37 Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa”.
Siku hiyo hakutakuwa na mtu mwingine pembeni kukusaidia kuzungumza…utazungumza wewe mwenyewe…sababu ya wewe kunena yale maneno ya matusi ni ipi, sababu ya wewe kuwa mwizi ni ipi, sababu ya wewe kuzungumza yale maneno ya makufuru ni ipi. Utatoa hesabu ya neno moja baada ya lingine, halitarukwa hata moja..Hata yale mambo ya siri ambayo unadhani hakuna mtu angeweza kuyajua..yatawekwa wazi siku ile.
Luka 12:2“ Lakini hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa, wala lililofichwa ambalo halitajulikana
3 Basi, yo yote mliyosema gizani yatasikiwa mwangani; na mliyonena sikioni mwa mtu katika vyumba vya ndani, yatahubiriwa juu ya dari”.
Ndugu Kama hujamkabidhi Yesu Kristo Maisha yako..Ni vyema ukafanya hivyo sasahivi..Mkabidhi yeye Maisha yako..si tu kwasababu hutaki kwenda hukumuni bali pia kwasababu unahitaji wokovu..Wokovu ni wa lazima kwa kila mtu, kama unapenda kweli Maisha basi utatamani kuishi milele..Na umilele huo haupo kwa mwingine zaidi ya Yesu kristo. Lakini usipomkubali Yesu Kristo leo, na kufuata mapenzi ya wazazi wako, au ndugu zako, au marafiki zako, au jamii yako..Nataka nikukumbushe tena na tena siku ile utasimama wewe peke yako.
Ukisoma Amri zote za Mungu, na kila mahali anapotoa maagizo yake, pote ni kama anazungumza na mtu mmoja mmoja…pote utaona anasema usiibe, usizini, usiabudu miungu mingine(Kutoka 20)…na hasemi msiibe, msizini au msiue..hutaona hicho kitu sehemu nyingi kwenye biblia..kasome kumbu 28 …..Hiyo yote ni kuonyesha kuwa maagizo ya Mungu anatoa kwa mtu mmoja..haijalishi hapo anapotoa hayo maagizo wapo watu wengi kiasi gani….anakupa maagizo wewe kama wewe na mimi kama mimi (anashughulika na mtu mmoja mmoja)…Sio mimi na mjomba wangu au na dada yangu…hapana mimi kama mimi..kwasababu siku ile nitakuwa peke yangu…Nitatoa habari zangu mwenyewe mbele ya kiti cha hukumu…
Biblia inazidi kusema katika..
Wagalatia 6:5 “Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe”.
Hivyo leo hii kata shauri na kusema nimeamua kumfuata Yesu kwa gharama zozote zile mimi kama mimi peke yangu..Jitwike msalaba wako na jikane nafsi, kama ulikuwa unavaa vimini, na suruali kazichome moto sasahivi usitazame Rafiki zangu watanionaje, ndugu zangu waliozoea kuniona navaa hivyo vitu wananionaje usitazame kushoto wala kulia wala usitafute ushauri kwa mtu yoyote…
Kumbuka siku ile utakuwa peke yako..ulikuwa unaweka make-up katupe sasahivi vipodozi vyote, ulikuwa mlevi kamwage hizo pombe kwenye friji yako kama zipo, ulikuwa mvutaji wa sigara unaacha kwa vitendo, ulikuwa mwasherati unaacha, simu yako ilikuwa umeijaza nyimbo na video za kidunia zifute zote sasahivi na mambo mengine yote maovu unayavua leo. Na kisha piga magoti mwambie Bwana nimetubu! kwa vitendo kuanzia leo hayo mambo nimeacha..Na atakusamehe kwasababu yeye ni mwingi wa huruma na Rehema…na kuna amani ya ajabu itaingia ndani yako saa hiyo hiyo baada ya kuacha hayo mambo..Hiyo Amani itakayoingia ni uthibitisho wa msamaha wako.
Hivyo usimzimishe Roho, haraka sana tafuta kanisa la kweli la Kristo lililo karibu na wewe au mtu yoyote wa Mungu ambaye yupo karibu na wewe atakusaidia.. Na jifunze kusoma Neno la Mungu mwenyewe na kutafuta ubatizo sahihi, na Roho Mtakatifu atakusaidia kukuongoza na kukutia katika kweli yote ya kimaandiko..wala hatakuacha mguu wako upotee njia hata siku moja, atakuwa pamoja na wewe hata ukamilifu wa dahari kama alivyosema katika Neno lake.
Bwana akubariki.
Tafadhali share na wengine.
Mada Nyinginezo:
Kuna hukumu za aina ngapi?
Jehanamu ni nini?
MBINGUNI NI WAPI?
BONDE LA KUKATA MANENO.
USIPOKUWA MWAMINIFU, NAFASI YAKO ITACHUKULIWA.
MAUTI YA PILI NI NINI?
JIHADHARI NA KUOSHWA MIGUU ISIVYOPASWA.
About the author