SWALI: Kwanini Mungu alimwambia Musa hakuna mtu awazaye kuuona uso wake akaishi,(Kutoka 33:20) Je! Kwa Mungu kuna mauti, tunapaswa tujihadhari naye?
JIBU: Tunajua biblia inatuambia kuwa kwa Mungu ndipo chemchemi za maji ya uzima zinapotoka, na ndipo chanzo cha uhai kwa kila kiumbe hai kinapozaliwa..
Zaburi 104:29 “Wewe wauficha uso wako, Wao wanafadhaika; Waiondoa pumzi yao, wanakufa, Na kuyarudia mavumbi yao,
30 Waipeleka roho yako, wanaumbwa, Nawe waufanya upya uso wa nchi.
Hivyo kusema kwa Mungu kuna mauti, jibu ni La, badala yake ndio kuna uzima..
Lakini swali linakuja ni kwanini basi Mungu alimwambia Musa maneno yale, kuwa hakuna mtu atakayeuona uso wake na akaishi?? Je! Kila atakayemwona Mungu ni lazima afe?..Na ndio maana Mungu akamwonyesha tu Musa sehemu ya nyuma ya utukufu wake ili asife au?
Kauli hiyo ukiitafakari kwa haraka unaweza kudhani Mungu alimaanisha kifo, lakini si kweli, kwasababu Mungu sio Kifo, tukimwona Mungu katika utimilifu wote ndivyo tutakavyozidi kuishi, isipokuwa sasa hatutaishi tena katika hali hii ya Maisha ya kawaida tuliyonayo siku zote..
Yaani itatulizimu kuvuka viwango hivi, na kwenda viwango vingine kiasi kwamba hata haya Maisha ya hapa duniani yatakuwa hayana maana tena kwetu, kuyaishi hatutaweza kuendelea kuishi tena hapa duniani..tutahamishwa na kuingia katika Maisha ya ufalme wa Mungu wetu..
Chukulia mfano, mtoto mdogo labda wa miaka 5, halafu akiwa bado ni mdogo vilevile umwondolee akili yake ya kitoto, kisha umwekee ubongo wa mtu mzima wa miaka 40 ndani yake..halafu umpe toy, za kitoto au umnunulie midoli aichezee.. Wewe unadhani ataifurahia tena, au atacheza nayo tena?…Kinyume chake utamwona ananyanyuka, na kwenda kusikiliza BBC, akitoka hapo utaona anaanza kuzungumzia Habari za uwekezaji, na kupanga mipango ya kimaendeleo.., kamwe huwezi kumkuta anachezea tena matope, au anaruka ruka barabarani kama Watoto wengine..
Ni kwasababu gani? Ni kwasababu akili yake imevukishwa mipaka yake ya utoto, hivyo hawezi kuishi tena Maisha ya utoto aliyopaswa ayaishi kwa umri wake..
Vivyo hivyo tukimwona Mungu kwa utimilifu wote, Maisha ya hapa duniani ndivyo yatakavyokuwa hayana maana tena kwetu.kinachobakia ni Kuondoka tu..
Bwana wetu YESU KRISTO yeye peke yake ndiye aliyemwona Mungu katika utimilifu wote..
Yohana 1:18 “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua”.
Na ndio maana aliondoka na kupaa na mpaka sasa, hajawahi kutokea mtu kama yeye, wakati huu wa sasa yupo kifuani mwa Mungu, hata makerubi na maserafi hajafikia bado hatua hiyo. Maisha yake hapa duniani yalikuwa ni ya kimiujiza tu, mpaka wengine wanadhani biblia iliongeza chumvi pale iliposema, mambo yote aliyoyafanya Yesu kama yangeandikwa moja moja sijui kama vitabu vyote duniani vingetosha..(Yohana 21:25)
Yesu alikuwa na uwezo wa kuuondoa uhai wake, na kuurudisha akiwa bado hapa hapa duniani,(Yohana 10:18), lakini hakutaka kufanya hivyo ili tu kutimiza kusudi la kutuokoa sisi, Je! Mtu huyo ni wa kawaida?
Na sisi pia tuzidi kumwomba Mungu azidi kujifunua kwetu, Zaidi na Zaidi, ili nasi tukifikie hatua ya kumjua yeye, mpaka kuifikia hatua ya kuondolewa duniani kwa tukio lile kuu la (UNYAKUO) alilotuahidia. Kama Bwana wetu alivyochukuliwa juu.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
About the author