SWALI: Ukisoma Yohana 1:19-26 inaelezea habari za Yohana mbatizaji akijitambulisha yeye ni nani! Napata shida katika mstari wa 21, alipoulizwa ” wewe u nabii yule” akajibu la!.
Huyu nabii yule, ambaye wayahudi walimtegemea kuja, ni nani?
Maana Yohana alishaulizwa kama yeye ni KRISTO, au ELIYA mwanzoni na akakanusha kuwa yeye si hao…Sasa huyu nabii yule ni nani?
JIBU: Tusome..
Yohana 1:19 “Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani?
20 Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo.
21 Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La.
22 Basi wakamwambia, U nani? Tuwape majibu wale waliotupeleka. Wanenaje juu ya nafsi yako”?
Mstari huu umetafsiriwa vibaya hususani kwa watu wasio wakristo wanaosema huo ni unabii unaomzungumzia mtume Mohamedi, kuwa atakuja baada ya Kristo kuwarejeza watu kwa Mungu
Lakini biblia haitabiri jambo lolote kuhusu kuja kwa mtu mwingine baada ya Kristo, yeye ndiye Alpha na Omega, hakuna nabii au mtume mwingine yoyote ambaye atatumwa baada ya Kristo, kuwaongoza watu katika njia ya kweli..Kama mtu atajiita mtume au Nabii basi ajue huduma yake italenga katika kuwaelekeza watu kwa huyu nabii mkuu Yesu Kristo,..Lakini sio kupokea maagizo yake tofauti yanayodai kuwa yanawaongoza watu kwa Mungu.
Sasa swali ni nani aliyekuwa anazungumziwa pale?
Kabla ya kufahamu ni nani aliyekuwa anazungumziwa pale, ni vizuri kufahamu Unabii Musa aliutoa huko nyuma kuhusu nabii mwingine ambaye Mungu atamnyanyua kama yeye, (Kumbukumbu 18:15-22)..Sasa biblia inaweka wazi kabisa nabii huyo aliyezungumziwa ni Yesu Kristo na hilo tunalithibitisha katika (Matendo 3:22-23) ukipata nafasi unaweza kuvisoma kwa muda wako vifungu hivyo…
Sasa Je hawa wayahudi walimaanisha nabii gani tena huyu? Ambaye walimuulizia Yohana..?
Jibu ni kwamba enzi zile wayahudi walikuwa na mitazamo mingi ambayo mengine haikuwa sahihi, na hiyo ni kutokana na kuwa na ukimya wa miaka mingi bila kuzukiwa na nabii yoyote Israeli, tangu nabii wa mwisho ambaye aliyejulikana kama Malaki..Hiyo ikawafanya wengi wao waamini kuwa wapo manabii wa kale kama Yeremia watafufuka au watashushwa kwa ajili ya kuwatolea unabii na maneno ya Mungu..
Na ndio maana utaona pale Bwana Yesu alipowauliza mitume wake, kuwa yeye ni nani walimjibu hivi..
Mathayo 16:13 “ Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? 14 Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.
Soma tena..
Luka 9:7 “Na Herode mfalme akasikia habari za yote yaliyotendeka, akafadhaika kwa sababu watu wengine walisema ya kwamba Yohana amefufuka katika wafu,
8 na wengine ya kwamba Eliya ametokea, na wengine ya kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka”.
Soma pia Luka 9:19..utaona jambo hilo hilo…
Mistari hii yote inathibitisha kuwa, wayahudi walikuwa wanatazamia kuwa mmojawapo wa manabii wa kale atanyanyuka kabla ya kuwasili masihi (Kristo) duniani, ambaye labda ni Yeremia, au Danieli, au Isaya… mtazamo ambao haukuwa sahihi.
Na ndio maana hata pale utaona sasa kwanini Yohana aliulizwa je “wewe u nabii yule” wakirejea mmojawapo wa manabii wa kale amekuja kuwahubiria maneno ya Mungu…Lakini yeye akajibu La!.
Hivyo kwa hitimisho hakuna Nabii mwingine aliyetokea wala tunayemngojea sasa, atakayekuwa mkuu Zaidi ya Masihi YESU KRISTO. Huyo ndiye chapa na nafsi ya Mungu, na mkuu wa wa wafalme wa Dunia, na Bwana wa Mabwana.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
About the author