Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze biblia leo tena.
Vipo vipindi tofauti tofauti ambavyo kila mkristo atavipitia…maana biblia inasema katika..
Mhubiri 3:1 “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.2 Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa; ….
4 Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza”.
Hata uwe unampendeza Mungu kiasi gani/ hata uwe mkamilifu mbele za Mungu kiasi gani..ni lazima utapitia vipindi vya kulia tu katika Maisha yako!..ni kweli asilimia kubwa ya Maisha yako itatawaliwa na furaha na amani..lakini ni lazima utapitia tu vipindi tofauti tofauti vya kulia na vya huzuni.
Sasa katika Imani pia vipo vipindi ambavyo utamwona Mungu sanaaa..na vipindi ambavyo hutamwona (utaona kuna ukimya Fulani maishani mwako)!…Sio kwamba atakuwa amekuacha kabisa! Au hakufuatilii wala kukusaidia…Hapana atakuwa yupo anakuona na kukujua lakini atakuwa kama amejiepusha na wewe”. Bwana Yesu kuna kipindi alisema “Mungu wangu, Mungu wangu mbona umeniacha”…hivyo huo wakati wa kuachwa upo!…Wengi hawalijui hili, ndio maana wanapopitia kipindi Fulani cha Maisha wanarudi nyuma na kuuacha wokovu…
Sasa leo tutajifunza hicho kipindi ni kipi lakini kabla ya kuendelea mbele zaidi hebu usome mfano huu taratibu sana, kisha tutaendelea…
Luka 15:3 “Akawaambia mfano huu, akisema,
4 Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda NYIKANI, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?
5 Naye akiisha kumwona, HUMWEKA MABEGANI PAKE AKIFURAHI.
6 Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea.
7 Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu”.
Mfano huo unaonyesha ni jinsi gani..Bwana anaweza akawaacha kondoo 99 nyikani na kwenda kumtafuta kondoo mmoja aliyepotea. Umewahi kujiuliza kwanini awaache wale kondoo 99, na kwanini asiende nao?..na kwanini awaache NYIKANI na si kwenye zizi, mahali palipo salama?…
Maana yake ni kwamba anawaacha peke yao sehemu ya wazi isiyo na uzio, ambayo inaonekana ni sehemu hatari, lakini ni salama….Sehemu ambayo Wanyama wakali wanapita, sehemu ambayo inaogopesha!…na mbaya zaidi wanaachwa peke yao…Na lengo la Bwana kuwaacha ni ili akatafute kondoo wengine..
Sasa hao kondoo walioachwa nyikani pengine ni wewe unayepitia ukame sasa, humwoni Bwana kama ulivyomwona wakati umeokoka. Sasa ufanye nini katika hiyo nyika yenye utata?
Kumbuka hapo ni nyikani, mahali pasipo na uzio.. hivyo sio wakati wa kuzunguka zunguka huko na kule…kaa hapo hapo ulipo ndio mahali salama!…hapo hapo mahali Bwana alipokuacha!..(maana yake ni kwamba anaelewa kabisa mahali alipokuacha utakuwa salama mpaka atakaporudi) tulia hapo hapo hata kama ukitazama kushoto humwoni Bwana, ukitazama kulia umwoni Bwana kama ilivyokuwa hapo kwanza…wewe tambua kuwa hapo ulipo upo sehemu salama..lishike Neno lake lile lile na Imani!…
Haupo ndani ya uzio, ikiwa na maana kuwa vishawishi vya kukuvuta utoke kwenye mstari wa wokovu, utaviona, usianze kuzurula…wala kuhama hama…tulia hapo hapo….Hali kadhalika pembeni unaweza kuona dalili ya kudhurika na wanyama wanaopita kule, na unaweza kuona kama vile hakuna ulinzi, usiogope! Kaa hapo hapo ndio sehemu salama (aliyekuacha hapo sio mjinga)….Hivyo tumia muda wako kujifunza Neno na kuwaimarisha wengine na kuwalinda wasitoke kwenye hifadhi ya Mungu..kwa kuwafundisha wokovu na kuwafariji mpaka wakati wa Bwana kurudi.
Kumbuka tena kuna wakati Fulani Kristo alikuweka mabegani alipokupata…lakini si wakati wote utakuwa mabegani mwake…wakati ukiwa mabegani mwake ulikuwa unamwona kwenye ndoto kila siku, ulikuwa unauhisi uwepo wake kila mahali, ulipomwomba kitu ulikipata papo kwa hapo…(wakati huo ulikuwa mabegani mwake, mbingu ilifurahia kukupata) lakini hautakuwa hivyo siku zote…utafika wakati utashushwa mabegani na wewe utakwenda kuungana na wenzako nyikani na Bwana atakwenda kutafuta kondoo wengine waliopotea.
Kama ni leo umempa Kristo Maisha yako, basi uwe tayari kwa hicho kipindi kuja mbele yako. Jifunze kumwelewa sana Bwana wakati huu wa sasa, ambao unamwona sana… kwasababu wakati wa ukame utafika!..kama hutamwelewa sana wakati huu, wakati wa kuachwa nyikani utaikimbia na kuiacha nyika.
Na hapo ndipo watu wengi walipopotelea. Imani ni ya kuilinda sana.
Bwana atubariki
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
MAJARIBU MATATU YA YESU KRISTO
MASHAHIDI 40 WALIOUAWA MJINI SEBASTE, NI UJUMBE KWETU.
IKIMBIE DHAMBI KWA GHARAMA ZOZOTE ZILE!
MKUMBUKE MKE WA LUTU.
UNYAKUO.
JUMA LA 70 LA DANIELI
MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.
About the author