Kutoka 22:31 “Nanyi mtakuwa watu watakatifu kwangu mimi; kwa hiyo msiile nyama yo yote iliyoraruliwa huko kondeni na mnyama wa mwitu; mtawatupia mbwa nyama hiyo”.
Shalom,
Katika agano la kale Mungu aliwapa wana wa Israeli agizo la kutokula nyama yoyote ambayo hawakuiwinda wao. Hiyo yote ni kwasababu ya usalama wa miili yao. Na alifanya hivyo pia kulifundisha kanisa lake rohoni, jinsi linavyopaswa lienende katika maisha ya utakatifu.
Kwa namna ya kawaida ukikutana na swala aliyekufa porini, huwezi kumla kwasababu hujui kilichompelekea kuuliwa ni nini, pengine aliumwa na nyoka, halafu wewe unakwenda kumla, bila shaka utajikuta unaingia katika matatizo yasiyokuwa ya lazima. Au pengine aliuliwa kweli na simba, lakini baada ya muda mfupi wakatokea fisi, wakaanza kuila ila ile nyama, na wewe baadaye ukaikuta ukaichukua, hujui pengine waliacha bakteria gani wenye madhara, wewe unakula tu.
Na ndio maana Mungu aliwakataza sio tu kula mnyama aliyeraruliwa bali pia wasile kibudu cha aina yoyote.
Walawi 22:8 “Nyamafu au mnyama aliyeraruliwa na wanyama asile, asijitie unajisi kwa hiyo nyama; mimi ndimi Bwana”.
Ni sawa tu na sasahivi, ukienda dukani halafu ukauziwa soda iliyofunguliwa, ni wazi kuwa huwezi kuinywa..Kwasababu hujui aliyeifungua alikuwa na lengo gani, pengine alitia sumu ndani yake, au kama sio sumu, ni dhahiri kubwa hata ubora wake utakuwa umepungua, na imesha expire.. hivyo utakapokunywa utakuwa umejihatarisha wewe mwenyewe.
Na ndivyo ilivyo leo hii rohoni, Mungu anataka kila mkristo ajue wajibu wake.. Asiwe ni mtu wa kulishwa lishwa tu kila fundisho ambalo linaletwa mbele yake, bila ya yeye mwenyewe kulihakiki kwanza katika maandiko yake matakatifu ubora wake. Mungu anataka tuwe wenye tabia hii kuhakiki.
Ni lazima ulipime kwa Neno la Mungu, na ndio maana kuna umuhimu sana, wa wewe kama mkristo kusoma biblia kila siku, huku ukimwomba Roho Mtakatifu akusaidie kuyaelewa. Vinginevyo utalishwa hata yasiyokupasa. Hata ukiambiwa mti Fulani uliopandwa hapo uwani kwako ni ishara ya mauti, utaamini, na kwenda kuukata kwasababu hujui maandiko, ukiambiwa mjusi sebuleni ni roho ya mkosi, utakwenda kushindana na mijusi yote duniani, kwasababu hujui maandiko yanazungumzia nini kuhusiana na hayo mambo.
Neno la Bwana linatuambia..
1 Yohana 4:1 “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani”.
Swali ni Je! wewe umekuwa ni wa kula kila unachokutana nacho njiani?..Je, ulishawahi kujishughulisha mwenyewe kutafuta mawindo yako? Au kuhakiki kuwa hicho unacholishwa ni salama, kimefungashwa vizuri na kwamba unajua chanzo chake ni nini?
Kama sivyo, anza sasa kufanya hivyo, kwasababu katika siku hizi za mwisho biblia inasema manabii wengi wa uongo watawadanganya wengi, hata yamkini wale walio wateule. Kwahiyo thibitisha ubora wa chakula chako kila siku. Mungu ametoa ruhusa kabisa kwa sisi kufanya hivyo. Usiseme tu AMEN! AMEN! Kwa kila fundisho unalolisikia au unalolisoma mitandaoni, lithibitishe kwanza ndipo ulipokee. Kama bado huelewi chanzo chake ni wapi, liache lipite kwa hao wengine, ambao biblia imewataja kama mbwa, kwasababu sikuzote mbwa hawachagui, wala hawajui kama hichi kimechacha, au kimeoza, au kina sumu, maadamu tu kinamwonekano wa kuliwa kwao ni chakula.
Lakini sisi sio mbwa, wa kupokea kila ufunuo au fundisho. Tuyahakiki yote. Tujitaabishe kuwinda mawindo yetu wenyewe. Watu wengi wamedanganywa na hawajui kuwa wamedanganywa kwa njia hii…Na ndio maana wengi wao wanashikilia udhehebu na udini, hata kama wataambiwa hakuna ziwa la moto, kwasababu kasisi wao kalithibitisha hilo wataamini.
Kutoka 22:31 “Nanyi mtakuwa watu watakatifu kwangu mimi; kwa hiyo msiile nyama yo yote iliyoraruliwa huko kondeni na mnyama wa mwitu; mtawatupia mbwa nyama hiyo”.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya “saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada?”
About the author