SOMO no. 01 (HAWA)

SOMO no. 01 (HAWA)

HAWA

Karibu katika mfululizo wa masomo yawahusuyo wanawake wa kwenye biblia, katika mfululizo huu, tutajifunza mengi yahusuyo majukumu ya wanawake kibiblia.

Katika biblia kulikuwepo na wanawake waliokuwa mfano mzuri wa kuigwa, na ambao hawakuwa mfano mzuri wa kuigwa, vile vile walikuwepo wanawake waliokuwa ni manabii wa kweli, na vile vile walikuwepo manabii wa uongo.

Kama mwanamke ni vizuri kujifunza kwa wote hawa, kabla ya kuanza kujifunza kwa Manabii na watumishi wa Mungu wa kiume katika maandiko.

Kwasababu mbio za wanaume ni tofauti na za wanawake. Katika tuzo na thawabu mbinguni hawatalingalishwa wanaume na wanawake.. bali wanaume kwa wanaume, na wanawake kwa wanawake..

Hata katika mbio za kidunia, wanawake wanapewa tuzo kulingana na mbio zao wao, na wanaume vivyo hivyo.. huwa hawachanganywi katika mbio, vinginevyo tuzo zote zingeenda kwa wanaume tu!, kwasababu ni ngumu wanawake kuwazidi mbio wanaume..

Hivyo ili kulitatua hilo, ndipo wanawatenga wanaume na wanawake.. Na Yule anayeibuka kidedea kwa wanawake anapewa tuzo sawa na yule aliyeibuka kidedea kwa wanaume..

1Wakorintho 9:24“ Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate.

25  Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika.

26  Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa; ”

Hivyo leo tutaanza kwa kujifunza kutoka kwa mwanamke wa kwanza, aliyeitwa Hawa. Kwa Hawa yapo mazuri ya kujifunza lakini pia yapo mabaya tusiyopaswa kujifunza kwayo..

Hawa ndiye mwanamke wa kwanza kuumbwa, na biblia inasema aliumbwa kama Msaidizi kwa Adamu (Mwanzo 2:20). Amsaidie katika majukumu yote ambayo Mungu alimpa Adamu. Hivyo HUDUMA ya kwanza ya Hawa aliyopewa na Mungu ilikuwa ni USAIDIZI!.. Na si “mke” Au “Mama”  Mungu hakumuumbia Adamu mke!, suala la mke lilikuja baadaye!.. Hakumuona Adamu na kumwona Yupo mwenyewe hivyo anahitaji mke wa kumliwaza!, au anahitaji mama wa kumlelea watoto wake!, ..Hapana!.. bali aliona anahitaji msaidizi wa kumsaidia shughuli alizompa..Hilo! ndilo la kwanza.. hayo mengine yalikuja baadaye.

Mwanzo 2:20 “Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; LAKINI HAKUONEKANA WA KUMSAIDIA ADAMU ALIYEFANANA NAYE”

Na usaidizi huo Hawa aliopewa si wa kutumia nguvu, ndio maana hakuumbwa na misuli, zaidi ya yote aliumbwa mwororo na mwenye umbo la wastani. Mungu angetaka awe msaidizi wa kutumia nguvu bila shaka angemuumba mwenye nguvu na mkubwa kuliko Adamu, lakini tunaona hakuwa hivyo.

Ikimaanisha kuwa usaidizi wake sio wa kutumia manguvu, bali hekima na akili. Wanyama kama ng’ombe, punda, farasi hao ndio waliumbwa kama wasaidizi wa Adamu kwa kutumia nguvu ndio maana waliumbwa wenye nguvu kuliko Adamu, ili ngamia amsaidie Adamu safari yake, hana budi awe mkubwa na mwenye nguvu kuliko Adamu. Lakini si Hawa!, usaidizi wa Hawa ulikuwa ni wa tofauti..

Hivyo USAIDIZI ndio huduma ya kwanza HAWA aliyopewa, Na hiyo hiyo huduma ya usaidizi Mungu alianza kuiweka kwa mwanamke wa kwanza anayeitwa Hawa, na wazao wote wa kike wanaofuata baada yake, wanayo hii HUDUMA ndani yao..Ndio maana wanaendelea kuzaliwa wakiwa kama Hawa, kimwonekano, wasio na misuli kama Hawa wa kwanza.

Hivyo hilo ni jambo la kwanza ambalo kila mwanamke anapaswa alijue, na shetani asilopenda walijue. Mungu anapomwangalia mwanamke yeyote duniani, anamwangalia kwanza kama MSAIDIZI kabla ya kumwangalia kama mke au Mama!. Hivyo kitu cha kwanza mwanamke anachopaswa kukifikiri na kukitafuta si Mume ili kumpendeza Mungu..bali Ile huduma ya usaidizi iliyopo ndani yake!, namna atakavyoivumbua na kuitumia ipasavyo.

Mwanzo 2:18 “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye”

Hivyo kama mwanamke ni lazima ujue!.. Usaidizi wako ni nini katika mahali ulipo!…Kibali ulichopewa unakitumiaje!.. ukienda mahali unapoona ni rahisi mwanamke kuaminika, na kukubalika kuliko mwanaume ni lazima ujiulize ..Ni kwanini iwe hivyo?..Ni lazima ujue kuwa kuna jambo la kusaidia pale, ambalo haliwezi kufanywa na wanaume!.. na jambo hilo si la kutumia nguvu bali akili, na hekima..Hivyo ni vyema uwe mshapu wa kulivumbua na kulitekeleza..

Labda tuchukue mfano pale katika Edeni.

Pengine wakati Adamu anawapa majina wale wanyama.. Hawa alipokuja akaweka mfumo bora wa kuwakumbuka, kwa kuwagawanya katika makundi au kwa kazi zao wanazozifanya!..ambao pengine kwa Adamu peke yake ingekuwa ni ngumu au asingeweka utaratibu mzuri..(Huo ni mfano tu).. Maana yake ni kwamba Hawa alipewa akili ya ziada, ambapo ikichanganyikana na ile ya Adamu, basi kazi ingefanyika vizuri zaidi!..

Vile vile katika kanisa, yapo mambo mengi hayapo sawa, ambayo yanahitaji usaidizi!.. Hayo yamefichwa kwenye macho ya wanaume, lakini yamewekwa wazi kwa wanawake werevu.

Katika kanisa ipo mifumo mingi ambayo kweli ni ya kiMungu, lakini endapo ikiendelea kwa namna hiyo hiyo, inaweza kuchukua muda mrefu zaidi kutekelezeka, au hata kama ikitekelezeka basi isitekelezeke kwa ufasaha.. Ni wajibu wako wewe kama mwanamke wa kikristo kutafuta namna ya kulitatua hilo.

Umeona kuna jambo Fulani linakwenda kupotea, haraka sana unaingia kwenye maombi, au unakusanya wenzako wachache na kuingia kwenye maombi kuliombea,  au kuna jambo umeona halijafanyika vizuri chukua nafasi hiyo wewe kulifanya lifanyike vizuri zaidi ili mambo yasiharibike,  usisubiri mwingine afanye!, kila jambo unaloona ni tatizo au linaelekea kuwa gumu unatafuta namna ya kulitatua haraka sana, …Na hulitatui kwa kumuagiza mtu mwingine akalifanye! Bali kwa wewe mwenyewe kulifanya!… vinginevyo wewe hutakuwa tena msaidizi, bali ndiye unayesaidiwa kutekelezewa majukumu yako.

Kumbuka Sifa moja ya msaidizi sio yeye kusaidiwa!, bali ni yeye kusaidia. Kwahiyo kila kitu mwanamke anachokiona kinahitaji marekebisho na msaada, hana budi kukifanya yeye kabla ya kumwambia mwingine, ili akidhi vigezo vya kuwa msaidizi..

Na hekima ya kuona mambo ambayo yanahitaji msaada katika kanisa au katika maisha inatoka kwenye Neno la Mungu. Huwezi kukaa hulijui Neno la Mungu, halafu uwe na jicho la kuona marekebisho!.. Itakuwa ni ngumu sana, zaidi utaishia kudanganywa na Yule mwovu na kufanya uharibifu mkubwa kwasababu wewe ni lango!

Hawa alianza vizuri kazi ya usaidizi, lakini alipoanza kutoka nje ya mpango wa Mungu, na kwenda kutafuta maarifa kinyume na maagizo ya Mungu, akajikuta badala ya kumsaidia Adamu kuujenga ufalme, akajikuta anamsaidia kuubomoa!.. Na anguko lake likawa kubwa ambapo madhara yake mpaka leo hii yapo!!.

Vile vile mwanamke yeyote asipolijua Neno la Mungu na kudumu katika hilo, basi kazi yake au macho yake yatakuwa hayaoni kujenga bali kubomoa (Na hatajua kama amepofushwa macho). Na mwanamke ndiye shabaha ya kwanza ya adui kutafuta kupitishia uharibifu wake kabla hata ya mwanaume.

Hivyo kama mwanamke hauna budi kutafuta kujifunza Neno kwa bidii..usiku na mchana, ili hekima iingie ndani yako, ili macho yako yaone madhaifu sahihi, na uweze kuyarekebisha. Hilo ndio jukumu lako la kwanza ulilopewa, hayo mengine ya kuwa Mama, au mke hayana umuhimu sana zaidi ya hilo la USAIDIZI!.

Ukifanyika kuwa msaada mkubwa katika kazi ya Mungu na kuifanya ikue na kustawi, basi fahamu kuwa Mungu anakuheshimu sana na una thawabu kubwa sana mbinguni, kwasababu ndiyo huduma ya kwanza Mungu aliyompa mwanamke. (Unakuwa umetii agizo la Msingi na la awali)

Hata Bwana Mungu wetu, alipoona kutakuwa na kasoro nyingi baada ya Bwana wetu Yesu kuondoka duniani, alituachia msaidizi, ambaye ndiye Roho Mtakatifu. Kazi ya Roho Mtakatifu sio sisi kumsaidia yeye, bali ni yeye kutusaidia sisi..

Warumi 8:26  “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.

27  Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu”

Je na wewe unachunguza mambo?, na kuchukua udhaifu wa wengine, na hata wa kazi ya Mungu, na kuwa msaidizi bora?..kama bado!.. anza leo kwa bidii, na utaona jinsi Mungu atakavyotembea na wewe kwa viwango vingine!

Bwana akubariki.

Huu ni msingi wa kwanza tuliouweka,kuhusu huduma ya kwanza ya Mwanamke!..Tutazidi kusonga mbele kutazama, wanawake wengine, na mambo ya kujifunza kuhusu wao, hivyo usikose mwendelezo.

Bwana akubariki.

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

Majina mbalimbali ya Mungu na maana zake.

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

KIKWAZO CHA EUODIA NA SINTIKE.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments