Maandiko yanasema, Neno la Mungu ni kama Upanga unaokata kuwili, (yaani una makali pande mbili,mfano wa sime). Na lina uwezo wa kuzigawanya Nafsi na Roho.
Mtu aliyejikana Nafsi yake, na kuyakataa mapenzi yake kwajili ya Mungu, maana yake ni kwamba Neno la Mungu kama Upanga limeingia ndani yake na kuitenganisha Roho yake na Nafsi yake, ndio maana mtu huyo haishi tena kwa nafsi yake, bali kwa roho yake tu, ambayo hiyo ndio inayotenda mapenzi ya Mungu!
Waebrania 4:12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata KUZIGAWANYA NAFSI NA ROHO, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
13 Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu”.
Umeona?, hakuna kitu kingine chochote kinachoweza kumtenga mtu na nafsi yake, isipokuwa Neno la Mungu tu!.. Hakuna mtu anayeweza kusema ameukataa ulimwengu, amejikana nafsi yake na huku upanga haujapita moyoni mwake.
Upanga wa Mungu yaani Neno lake, ndio unaoweza kututenga sisi na mambo ambayo tumeshindwa sisi kutengana nayo kwa nguvu zetu, huwezi kujitenga na hasira kama huu upanga hujapita ndani yako,kukutenga wewe na hiyo hasira, huwezi kujitenga na vinyongo na visasi kama huu upanga hujaingia ndani yako, kuna vitu unaweza kujitenga navyo, lakini kuna vingine vinahitaji upanga wa Roho (Neno la Mungu), ili vikuachie.. kwasababu vimejishonanisha na roho yako, au nafsi yako.
Ni lazima uruhusu upanga uingie ndani yako ili uweze kuvitenganisha vitu hivyo.
Sasa utaruhusu vipi huu upanga uingie ndani yako?
Maandiko yanasema Bwana Yesu ndiye Neno la Mungu,
Ufunuo 19:13 “Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.
14 Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi”.
Unaweza kusoma pia Yohana 1:1, utaliona jambo hilo hilo,
Hivyo kama Kristo ndiye NENO LA MUNGU, maana yake yeye ndiye UPANGA, ambapo anapoingia moyoni anatenganisha roho yako na nafsi yako, hakuna chochote kilichopo ndani yako kilichojificha asikijue, atayasafisha mawazo yako yote na kutenganisha uovu na wema ndani yako. Na kukuweka katika hali salama ya kuyatenda mapenzi ya Baba tu.
Kumbuka tena maandiko yanasema..
Waebrania 4:12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata KUZIGAWANYA NAFSI NA ROHO, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
13 Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu”.
Hivyo kama tunataka kuwa wakamilifu, kama tunataka kuwa huru rohoni, kama tunataka kuyatenda mapenzi ya Mungu, BASI TUNAMHITAJI YESU SANA MIOYONI MWETU.
Wengi leo wanaye YESU katika biashara zao, wanaye Yesu katika watoto wao, wanaye Yesu katika viungo vyao, lakini hawana Yesu MIOYONI MWAO. Upanga umepita katika shughuli zao, upanga umepita katika biashara zao hata wameona shetani kawekwa mbali nao, kadhalikaupanga umepita katika miili yao hata wameona wametengwa mbali na magonjwa yaliyokuwa yanawasumbua lakini UPANGA BADO HAUJAINGIA MIOYONI MWAO.
Mariamu aliyekuwa mamaye Yesu, ijapokuwa alikuwa na Yesu katika tumbo lake, lakini wakati ule bado alikuwa hajampata Yesu moyoni..Ndio maana Simoni, Yule nabii mzee alimwambia maneno haya..
Luka 2:34 “Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.
35 NAWE MWENYEWE, UPANGA UTAINGIA MOYONI MWAKO, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi”.
Kuna tofauti kubwa ya Yesu kuwepo tumboni mwa Mariamu na Yesu kuwepo moyoni mwa Mariamu..Ulifika wakati Mariamu alikuwa hana budi kumwamini Yesu kama mwokozi wake na Bwana wake, na si kama “mtoto wake”. Nafasi ya Mariamu kama mama wa Yesu, iliwahi kuisha mapema sana, kabla hata ya Bwana Yesu kusulubishwa, Mariamu alishaacha kitambo sana kumwona Bwana kama mwanawe, ilifika wakati alianza kumjua kama Bwana na Mwokozi, na kuyaamini maneno yake na kwenda kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu. (Huo ni wakati ambapo upanga uliingia ndani yake na yeye pia).
Swali la kujiuliza ni je! Na wewe Upanga umeingia moyoni mwako?, au upo tu! Nje kwenye biashara yako?. Upanga ukiingia ndani yako kule kuupenda ulimwengu kunakufa, kule kujikana nafsi kunaingia ndani yako, kiasi kwamba hata ndugu wakuchukie, hata marafiki wajitenge nawe, hata ukose kila kitu lakini huwezi kuacha kuyafanya mapenzi ya Baba.
Dunia nzima inaweza kukuona umerukwa na akili, lakini wewe unajitambua unazo akili timamu katika Kristo. Mageuzi kama hayo katika maisha yako ndio uthibitisho kuwa Upanga umeingia ndani yako.
Mathayo 10:34 “Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; LA! SIKUJA KULETA AMANI, BALI UPANGA.
35 Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu;
36 na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.
37 Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.
38 Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili.
39 MWENYE KUIONA NAFSI YAKE ATAIPOTEZA; NAYE MWENYE KUIPOTEZA NAFSI YAKE KWA AJILI YANGU ATAIONA.
Kama bado hujampokea Yesu maishani mwako, basi mtafute mtumishi yoyote wa Mungu wa kweli, na mweleze kuwa unahitaji kumpokea Yesu, atakusaidia katika kukuongoza sala ya kumpokea Yesu, au wasiliana nasi kwa namba hizi hapa chini.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Kwanini Bwana Yesu aliwaagiza wanafunzi wake wakanunue upanga?
About the author