USIRUDI NYUMA KATIKA IMANI

USIRUDI NYUMA KATIKA IMANI

Tukiwa bado tupo mwanzo wa mwaka, ni wakati wa kushika sana vile tulivyo navyo na kuendelea mbele, wala si wakati wa kurudi nyuma kabisa.

Usiyarudie mambo ya kale uliyoyaacha, usiyatamani mambo ya kale uliyoyakimbia, usiirudie njia  ya kale uliyoikataa…

Ulikuwa upo mbali na anasa mwaka jana, basi huu si mwaka wa kuzirudia tena, usirudie ulevi uliouacha miaka ya nyuma, usirudie uzinzi ulioushinda miaka ya nyuma, usirudie kujichua ulikokuacha miaka ya nyuma,

Usirudie mavazi yasiyo na staha uliyoyaacha miaka ya nyuma, usirudie wala kuitamani mitindo ya kidunia uliyoiacha mwaka jana.

Usirudie starehe za kidunia, mwanzo huu wa mwaka ni wakati ambao shetani anafanya kazi kubwa sana kuwarudisha watu nyuma kiroho, na atashambulia mambo yafuatayo ili kuhakikisha mwamini anarudi nyuma kiroho.

    1. Afya.

Atajaribu kukuletea mashambulizi katika eneo la afya, kwa kuitikisa afya yako au ya watu wako wa karibu, ikiwemo pia afya ya uzazi.. Simama endelea mbele usirudi nyuma!.

     2. Uchumi.

Atajaribu kutikisa uchumi wako lakini, hawezi kuondoa baraka zako za mwaka, hivyo usitishwe na vimitikisiko vya uchumi vya ibilisi vya hapa na pale, ni vya muda tu wewe endelea mbele usirudie biashara haramu wala tamaa za mali ulizoziacha huko nyuma endelea mbele kwani Bwana anakujua.

     3. Ndoa.

Atakuletea vimitikisiko vya kifamilia vya hapa na pale, pia visikutishe kwani ni kawaida yake kutishia, lakini wewe endelea mbele na imani usirudie magomvi uliyoyaacha miaka ya nyuma, usirudie anasa za kupunguza mawazo ulizoziacha huko nyuma…yapo mambo mazuri mbele yako kwaajili ya huu mwaka.

Pia ondoa hofu ya kesho…kwamba itakuwaje kesho, itakuwaje disemba…ndio usijizuie kutafakari yajayo, lakini usiufanye moyo wako kuwa mzito kwaajili ya hayo, kwani huo pia ni mlango mwingine wa ibilisi kumrudisha mtu nyuma.

Ukiwa ndani ya Kristo fahamu kuwa mambo yote yatakuwa sawa, haijalishi itachukua muda gani au mambo yanaanzaje…kushinda ni lazima! na ni AMRI.

Usirudi nyuma Baba, usirudi nyuma Mama, usirudi nyuma kaka, usirudi nyuma dada, usirudi nyuma mtoto…kwani matokeo ya kurudi nyuma ni kumfadhaisha Bwana.

1 Samweli 15:11”Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia BWANA usiku kucha”.

Utakapofika mwisho wa mwaka tena uwe na sababu ya kumshukuru Bwana kama amekulinda hujarudi nyuma.

Ayubu 23:12 “Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu”.

Lakini kama ulikuwa umeshaanza kurudi nyuma, bado hujachelewa hebu kataa hiyo njia na leo mwombe Bwana rehema na kuziacha hizo njia utaona maajabu ya Bwana, kwani atakutia nguvu na utaendelea mbele kwa mbio kubwa, Bwana atakurehemu na utamfurahia.

Hosea 14:4 “Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao; nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo; kwa maana hasira yangu imemwacha”.

Isaya 50:5 “Bwana MUNGU amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma

Lakini usipojali na kuendelea katika njia hiyo ya kurudi nyuma, ipo hatari mbele yako..

Mithali 1:32  “Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua,

Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza”

USIRUDI NYUMA! USIRUDI NYUMA!…USIRUDI NYUMA!.

Ukiwa utahitaji msaada wa maombezi ili uzidi kusimama, basi piga namba hizi 0789001312.

Bwana anakupenda, na Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

USIRUDI NYUMA KWA KUITUMAINIA HAKI YAKO.

JINSI SODOMA NA GOMORA ILIVYOKUWA INAVUTIA SANA..

NI LAZIMA KUISHIKILIA IMANI MPAKA MWISHO.

SHIKA SANA ULICHO NACHO, ASIJE MTU AKAITWAA TAJI YAKO.

USIIGE TABIA YA NAAMANI

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments