Zekaria 10:1 “Mwombeni Bwana mvua wakati wa masika, naam, Bwana afanyaye umeme, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi kondeni”.
Umewahi kujiuliza kwanini hapo maandiko yanasema “Mwombeni Bwana mvua WAKATI WA MASIKA” na si wakati mwingine wowote kama kiangazi?..
Ni kwasababu msimu wa masika ni msimu wa mvua, hivyo inapotokea hakuna mvua si jambo la kawaida, kwahiyo tukiomba mvua msimu huo ni hoja yenye nguvu, lakini tunapoomba mvua msimu wa kiangazi zinakuwa si hoja zenye nguvu!.. Ndicho maandiko yanachokimaanisha hapo.
Maombi ya kuomba kwa wakati ni mazuri na yana majibu ya haraka kuliko yale ya kuomba nje ya msimu/majira.
Unaomba mume/mke na bado ni mwanafunzi, unaomba mali na bado unasoma, unaomba umtimikie MUNGU na bado hujaokoka!, maombi ya namna hiyo ni nadra sana kujibiwa!.. ni wachache sana wanaojibiwa hayo maombi!!.. sio kwamba ni maombi mabaya au vinavyoombwa ni vitu vibaya!. La! Ni vizuri lakini vinaombwa nje ya majira yake.
Hapo maandiko yanasema “Mwombeni Bwana Mvua wakati wa Masika”.. Maana yake ni lazima ujue uhusiano wa kile unachomwomba MUNGU na majira uliyopo. Kama kitu bado majira yake usitumie nguvu kubwa kuomba, shughulika na vile ambavyo sasa ndio majira yake.
Kama wewe ni mwanafunzi usiombe MUNGU akupe hela kwa sasa….badala yake mwombe akufanikishe katika masomo ufaulu, uwe kichwa, hayo mengine bado msimu wake!..
Kama wewe ni binti/kijana na bado upo chini ya wazazi unawategemea, usiombe MUNGU akuonyeshe mume wako/mke wako, badala yake mwombe ulinzi juu ya tabia yako mpaka utakapofika wakati wa wewe kujitegemea na kufikiri kuingia katika ndoa.
Lakini kama umeshaingia katika msimu basi ni haki yako kumwomba BWANA!, Na unapomwomba Bwana jambo sahihi katika msimu sahihi, MUNGU ni mwenye huruma atakupa unachokihitaji haraka sana, na hata kikichelewa atakupa sababu kwanini kinachelewa, na sababu za BWANA zote ni Bora na wala si za kumwumiza Mtu, kwasababu yeye kamwe hawezi kuruhusu tujaribiwe kupita tuwezavyo.
Vumilia tu ukiona umeshaingia kwenye msimu na bado matokeo hujayaona!, yatakuja tu!..usikate tama a wala kuishiwa nguvu, mwamini MUNGU na mngojee, naye atakupa nguvu mpya kila siku.
Jambo la mwisho la kujua ni kwamba wokovu pia unao msimu wake, na msimu wa Wokovu ndio sasa..
Huu ndio wakati wa MUNGU kutupa wokovu na kutusikia maombi yetu, kwani utafika wakati ambapo hakutakuwa tena na wokovu wala maombi kusikiwa, ndivyo maandiko yanavyosema..
2Wakorintho 6:1 “Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure.
2 (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa)”
Sasa kama siku ya Wokovu ndio sasa, unasubiri nini usimpokee YESU?.. je unadhani itakuwa hivi siku zote?.. utafika wakati mlango wa Neema utafungwa, na hakutakuwa tena na msamaha wa dhambi wala ondoleo la dhambi, mti ulipoangukia huko huko utalala (Mhubiri 11:3).
Sasa unayadharau mahubiri na mafundisho ya uzima, unayoyapokea kila mahali yanayokuonya kuhusu dhambi, je unadhani hali itakuwa hivyo kila siku?…Majira yatabadilika ndugu, utafika wakati kutakuwa hakuna kuponywa tena mwili na roho!.
2Nyakati 36:15 “Naye Bwana, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake;
16 lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, HATA ILIPOZIDI GHADHABU YA BWANA JUU YA WATU WAKE, HATA KUSIWE NA KUPONYA”.
Bwana atusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Nzige, Parare, madumadu na tunutu ni wadudu gani? (Yoeli 2:25)?
MAASI KUONGEZEKA NI ISHARA YA NINI?.
JIFUNZE JAMBO KWENYE UKOO WA YESU, UWE NA AMANI
Kwanini madhabahu zilitengenezwa kwa mawe yasiyochongwa?
Kwanini Mungu auweke Mti wa Mema na Mabaya katikati ya bustani?
About the author