Katika maandiko tunasoma kwamba Mungu alimshuhudia Musa kuwa ndiye mtu mpole kuliko watu wote duniani, lakini tunaona huyo Musa mbeleni (katika Hesabu 31:15) anakuja kuonekana kama mkatili sana?, hapo sijaelewa!.
Tusome,
Hesabu 31:14 “Musa akawakasirikia majemadari wa jeshi, na hao maakida wa elfu elfu, na wakuu wa mia mia, hao waliorudi kutoka katika kupiga vita.
15 MUSA AKAWAULIZA, JE! MMEWAPONYA WANAWAKE WOTE HAI?
16 Tazama, hawa ndio waliowakosesha wana wa Israeli, kwa shauri la Balaamu, wamfanyie Bwana dhambi katika hilo jambo la Peori, na kwa hivyo pigo lilikuwa katika mkutano wa Bwana.
17 Basi KWA AJILI HIYO MWUENI KILA MUME KATIKA HAO WATOTO, na kila mwanamke aliyemjua mume kwa kulala pamoja naye”.
Tusome tena..
Hesabu 12:3 “Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi”.
Bwana Mungu hawezi kusema uongo, ni kweli Musa alikuwa mtu mpole kuliko watu wote duniani, lakini hakuzaliwa hivyo, maandiko yanatuambia pia Musa hapo kwanza alikuwa mtu Hodari wa maneno na matendo.(maana yake hakuwa mpole), ndio maana alikimbia Misri baada ya kugundulika kuwa kaua mtu.
Matendo 7:22 “Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo”.
Sasa unaweza kujiuliza upole alikuja kuutolewa wapi?
Baada ya Musa kumkimbia Farao, alikwenda nchi ya Midiani, akiwa huko Mungu alikishusha kiburi chake, akamnyenyekeza kutoka kuwa Mwana wa kifalme mpaka mchunga mbuzi na kondoo, alichunga mifugo ya Yethro mkwewe kwa miaka mingi sana (Takribani miaka 40), hivyo kile kiburi chake chote kikaisha, yale majivuno yake yote yakaisha, ule ujuzi wake wote wa kuzungumza ukaisha, akawa ni mtu mpole sana, asiyeweza kuongea sana. Na ndipo katika wakati huo Mungu akamtokea na kumwagiza ashuke Misri akawaokoe ndugu zake. (Kwahiyo ni Mungu ndiye aliyemfanya mpole).
Lakini swali ni je! Kama tayari Mungu kamfanya mpole kwanini mbeleni tunaona tena anatoa mashauri ya kuua watu?
Hesabu 31:17 “Basi KWA AJILI HIYO MWUENI KILA MUME KATIKA HAO WATOTO, na kila mwanamke aliyemjua mume kwa kulala pamoja naye”.
Jibu ni kwamba, Musa hakutoa amri ya kuua kwa matakwa yake yeye, au kwa agizo lake yeye, BALI KWA AGIZO LA MUNGU. Mungu ndiye aliyetoa maagizo ya kuua watu wote wa Midiani, bila kubakisha yeyote, kutokana na kosa la wamidiani kumtoa Balaamu, na kumtuma kwa Balaki mfalme wa Moabu, ili awalaani Israeli, hivyo Mungu akaikasirikia nchi ya Midiani na kumwagiza Musa akawaue watu wote.
Na Musa alipowatuma majemedari wa Israeli wakaue, kwa agizo hilo la Bwana, wale majemedari wakaua kweli wanaume na wafalme lakini wakawaacha hai wanawake!, jambo ambalo ni kinyume na maagizo Bwana aliyoyatoa.
Tusome tena,
Hesabu 31:7 “Nao wakapigana na Midiani kama Bwana alivyomwagiza Musa; nao wakamwua kila mume.
8 Nao wafalme wa Midiani wakawaua pamoja na watu wengine waliouawa; Evi, na Rekemu, na Suri, na Huri, na Reba, hao wafalme watano wa Midiani; Balaamu mwana wa Beori naye wakamwua kwa upanga.
9 Wana wa Israeli wakawachukua mateka wanawake wa Midiani na watoto wao; na ng’ombe zao wote, na kondoo zao wote, na mali zao zote, wakachukua nyara.
10 Na miji yao yote, kila mahali walipokuwa wakikaa, na marago yao yote wakayateketeza kwa moto.
11 Nao wakatwaa hizo nyara zote, na mateka yote, ya wanadamu na ya wanyama.
12 Nao wakawaleta mateka ya wanadamu, na mateka ya wanyama, na hizo nyara, na kuyaweka mbele ya Musa, na mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wa wana wa Israeli, hapo maragoni katika nchi tambarare za Moabu, zilizo karibu na Yordani hapo Yeriko.
13 Basi Musa, na Eleazari kuhani, na wakuu wote wa huo mkutano, wakatoka nje kwenda kuwalaki nje ya marago.
14 MUSA AKAWAKASIRIKIA MAJEMADARI WA JESHI, NA HAO MAAKIDA WA ELFU ELFU, NA WAKUU WA MIA MIA, HAO WALIORUDI KUTOKA KATIKA KUPIGA VITA.
15 MUSA AKAWAULIZA, JE! MMEWAPONYA WANAWAKE WOTE HAI?
16 Tazama, hawa ndio waliowakosesha wana wa Israeli, kwa shauri la Balaamu, wamfanyie Bwana dhambi katika hilo jambo la Peori, na kwa hivyo pigo lilikuwa katika mkutano wa Bwana.
17 Basi kwa ajili hiyo mwueni kila mume katika hao watoto, na kila mwanamke aliyemjua mume kwa kulala pamoja naye”.
Hivyo Musa aliendelea kuwa mpole vile vile, kuliko watu wote, lakini alikuwa anayashika maagizo ya BWANA bila kupindisha, kile Bwana atakachokisema anakitekeleza kama kilivyo ili ampendeze Mungu, na aliwaamuru watu kuyafanya maagizo ya Bwana bila kuyapindisha.
Tunachoweza kujifunza na sisi ni kwamba, hatuna budi kuyatekeleza maagizo ya Bwana kama yalivyo, bila kuyapindisha, haijalishi tutaonekanaje!
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 2: Upande wa wanawake)
About the author