Kifo cha mtakatifu perpetua na felista kimebeba ujumbe gani kwetu?
Perpetua alizaliwa huko Tunis (Mji mkuu wa Tunisia) Afrika ya Kaskazini mwaka unaokadiriwa kuwa wa 182, alizaliwa katika familia ya kitajiri, yenye kuheshimika sana, baba yake alikuwa ni mpagani, lakini Perpetua aliupokea Ukristo na kuwa mfuasi kamili wa Kristo, japo historia haionyeshi ni kipindi gani aligeuzwa kuwa mkristo..Lakini ilifika wakati mfalme wa Kirumi aliyeitwa Septimius Severus…Alipiga marufuku ukristo katika majimbo ya Afrika kaskazini, kwamba mtu yoyote asijihusishe na imani yoyote ya kikristo au ya kiyahudi..Wakati huo Perpetua alikuwa anaishi na mume wake, pamoja na kijakazi wake aliyeitwa Felista, na katoto chake kachanga alichokuwa bado anakinyonyesha wakati huo ..
Sasa wakati agizo hilo linatolewa Perpetua alikuwa katika mafundisho ya kuelekea kubatizwa, lakini alibatizwa kabla ya kupelekwa gerezani..Ndipo baadaye yeye pamoja na wenzake wanne, wote walikamatwa na kupelekwa gerezani.
Baba yake kusikia vile, alikwenda moja kwa moja mpaka gerezani kumtazama binti yake ili kutafuta njia ya kumtoa, ndipo akamshauri Perpetua aukane ukristo, atoke gerezani aendelee na maisha yake ya kawaida..
Lakini Perpetua alimwambia Baba yake maneno haya.. “Baba unakiona hichi chungu hapa?”
Akasema ndio,
Je kinaweza kuitwa jina lingine tofauti na vile kilivyo?
Akasema, hapana!
Basi hata mimi siwezi kuitwa jina lingine tofuati na mimi nilivyo..Mkristo.
Ilipofika Siku ya pili Perpetua, alihamishwa gereza alilokuwepo na kupelekwa gereza lingine zuri zaidi ili aweze kumnyonyesha mtoto wake…Lakini baba yake hakukata tamaa alimfuata tena siku nyingine, lakini safari hii alikuja kwa kumbembeleza sana.
Akimwambia…Nihurumie mwanangu!, nihurumie mwanangu!, ikiwa ninastahili kweli kuitwa baba yako, ikiwa nimekupenda zaidi hata ya kaka zako, ikiwa nimekulea mpaka umefikia hatua hii ya heshima..basi nihurumie mimi baba yako..kubali kukataa tu wewe sio mkristo.
Akamdondokea, mpaka magotini akambusu mikono yake..akamwambia, mwanangu usiniache nikapata aibu kama hii katikati ya watu. Fikiri juu ya kaka zako, fikiri juu ya mama yako, fikiri juu ya shangazi zako, fikiri hata juu ya huyu mtoto wako mchanga ambaye hataweza kuishi pindi utakapokufa..Ghairi hayo maamuzi yako magumu!, uendelee na maisha yako ya kawaida.
Perpetua alizidi kuwa imara na msimamo yake akamtia moyo baba yake..Akaendelea kukaa kule kule gerezani.
Na Siku ya kuhojiwa ilipofika Perpetua na wenzake walipandishwa kizimbani mbele ya gavana, Na wenzake walipoulizwa kwanza juu ya msimamo wao walikiri kuwa wao ni wakristo, na wote wakakataa ibada za mfalme. Swali likageuzwa kwa Perpetua, naye akaulizwa na Gavana kuhusu msimamo wake.
Wakati huo baba yake alikuwa hapo karibu, amembeba mtoto wake yule, akamwambia, kubali ibada za mfalme, achana na hiyo imani yako, mwonee huruma mtoto wako.
Lakini Perpetua akasema mbele ya wote..Siwezi kufanya hivyo!!
Gavana akamuuliza, kwahiyo wewe ni mkristo.
Ndio! Perpetua alijibu..
Baba yake akaingilia kati akimlazimisha Pepertua aikane imani, lakini Hawakuwa na muda tena, wakamchukua yeye na wenzake wakawapeleka katika viwanja vya michezo (Arena) ili wauawe. Kufika kule kuliwa na wanyama wakali ambao tayari wameshaandaliwa, ambapo wanyama kama chui, dubu walikuwa wanaachiliwa kwa wanaume, na nyati kwa wanawake..wakamtupa Perpetua na yeye pamoja na wenzake, na kijakazi wake Felista ambaye kwa wakati huo alikuwa ni mjamzito naye..
Akaachiliwa nyati, akamchota Perpetua juu, wakati akiwa chini akaende kumsaidia kijakazi wake Felista, huku wote wamelowa damu..Wakaona haitaoshi wakawaleta kwa wauaji wa kirumi katika ma-arena hayo ili wauliwe kwa upanga..
Perpetua alikufa mwaka wa 203 akiwa bado mama mdogo mwenye umri wa miaka 22, hakuona ujana wake kuwa ni kitu kuliko Kristo, hakuona heshima yake ya kitajiri kuwa ni kitu kuliko Kristo, wala hakuhesabu kuikana imani kisa baba, au mama au mtoto wake.. Bali aliisimamia imani hadi dakika ya mwisho..
Biblia inatuambia..
Waebrania 11:35 “…..Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora;
36 wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;
37 walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga;
Swali la kujiuliza kwetu sisi hususani kwako wewe mwanamke kutokana na mada hii:
Je unauthamini wokovu wako vipi?..Unasema umeokoka lakini kuacha kuvaa vimini na masuruali na manguo ya utupu, unaona ni vigumu, unajiona wewe ni kijana, Perpetua pengine alikuwa ni kijana Zaidi yako, tena aliyezaliwa katika nyumba ya kitukufu ya kitajiri pengine kuliko wewe, lakini hakuudosha utakatifu wake.
Kila tusomapo habari kama hizi tusiishie tu kuzisoma kama hadithi bali tufahamu kuwa..tunahimizwa na sisi pia tupige mbio kama hao, na kutupa kila mzigo wa dhambi unaotulemea na kutuzungika kwa upesi, kwasababu hawa ndio watakaotuhuku siku ile mbele za Bwana..kuwa walikuwa wazuri kushinda sisi lakini hawakuikana imani, walikuwa katika hatari kubwa kuliko sisi lakini hawakuupuuzia wokovu, walikuwa ni matajiri kuliko sisi lakini hawakusema utajiri wangu ni kizuizi nisikane nafsi..Walikuwa ni wajawazito, na wenye watoto wachanga, lakini hawakuthamini hicho zaidi ya wokovu wao..wewe na mimi tutajibu nini mbele za Bwana siku ile? Au tunafikiri watu hao walikuwa hawasikii maumivu, au walikuwa wana roho sana..hapana, ni walikana tu!..Biblia inasema hata Eliya hakuwa mtu wa ajabu sana, alikuwa ni mtu mwenye tabia sawa na sisi, lakini walijikana kwa gharama zote.
Waebrania 12:1 “Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu”
Ubarikiwe.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
About the author