Sisi tuliookolewa pamoja na Bwana wetu Yesu Kristo, tunafananishwa na mti mmoja alioupanda Mungu mwenyewe ulimwengu. Na wote tunayo sehemu katika mti huo, na tumewekewa wajibu wa kufanya.
Bwana wetu Yesu Kristo anafananishwa na shina la mti, halafu sisi tunafananishwa na matawi.
Shina ni kuanzia kwenye mizizi, hadi mahali matawi yanapotokea. Hivyo Bwana wetu Yesu, ndiye anayechukua uhai wetu moja kwa kutoka kwa Mungu na kutuletea sisi. Lakini sisi ni kuanzia kwenye matawi mpaka kwenye matunda.
Yohana 15:1-2,5
[1]Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima.
[2]Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa….
[5]Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.
Sasa wengi wetu tunachoona katika mashina ni matunda tu peke yake. lakini leo ni vema tuone jambo hili kwa ndani. Kwa kawaida tawi huundwa na vitu viwili, cha kwanza ni majani, na cha pili ni matunda.
na vyote viwili vinapaswa vionekane katika shina.
Hivyo mimi na wewe kama watakatifu, ni lazima tujiulize je majani yapo? na je matunda yake pia yapo?
Matunda ni nini?
Tafsiri ya awali ya matunda kama ilivyozungumziwa kwenye mfano ya mti, sio kuwavua watu kwa Kristo, kama inavyodhaniwa, hapana bali ni Kutoa tunda la wokovu wako. Yaani tunda la toba.
Yohana mbatizaji kwa uvuvio wa Roho alilifafanua vema..Tusome.
Mathayo 3:7-10
[7]Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?
[8]Basi zaeni matunda yapasayo toba;
[9]wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto.
[10]Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.
Aliwaona mafarisayo ambao walikiri kwa ujasiri wao ni wajumbe wa Yehova, uzao wa Ibrahimu, lakini mioyoni mwao, maovu na machafu ya kila namna yamewajaa. Hivyo wakaonekana ni miti isiyo na matunda.
Matunda ndio yale yanayojulikana kama tunda la Roho, ambayo kila mwamini anapaswa afanye bidii kuyatoa moyoni mwake katika maisha yake yote ya wokovu, awapo hapa duniani. Ambayo ni;
Wagalatia 5:22
[22]Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu
[23]upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.
Mtu yeyote anayefanya bidii kuonyesha wokovu wake kimatendo, mtu huyo humzalia Mungu matunda, ambayo ndio chakula cha Roho wa Mungu. Na hivyo hufurahishwa sana na sisi..
Lakini kama tulivyosema shina huundwa na majani pamoja na matunda. Sasa majani, ni utumishi ambao kila mmoja wetu amepewa wa kuwavuta wengine kwa Kristo, kwa karama aliyopewa ndani yake.
Tuliagizwa na Bwana tuenende ulimwenguni kote, tukahubiri injili na kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi wake (Mathayo 28:19),
Unapowashuhudia wengine, ni kwamba majani yako yanawaponya mataifa, na hivyo unawaokoa. Kumbuka majani kimsingi hayana ladha, mara nyingi hutumika kama tiba. Ndicho Bwana anachokifanya kwa wenye dhambi kupitia sisi, tunapowashuhudia.
Ufunuo wa Yohana 22:1-2
[1]Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo,
[2]katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na MAJANI YA MTI HUO NI YA KUWAPONYA MATAIFA.
Umeona? Kumbe majani yake, ni lengo la kuwaponya mataifa, watu wasiomjua Mungu. Tujiulize je na sisi tunayaponya mataifa kwa kuhubiri injili?
Wewe kama mkristo uliyemshirika wa mti wa uzima huna budi kuwa mhubiri wa injili usikae tu, hivi hivi ukasema tayari nimeokolewa inatosha, fanya jambo kwa Bwana. Waeleze wengine habari za Yesu, waponywe. Usijidharau ukasema siwezi, kumbuka aitendaye kazi hiyo ni Kristo ndani yako, wewe ni tawi tu. washuhudie wengine.
Lakini si kuhubiri tu, halafu maisha yako yapo kinyume na Kristo, hapana hilo nalo ni hatari, ukiwa na majani tu, halafu huna matunda ya wokovu moyoni mwako..Utalaaniwa.
Marko 11:13
[13]Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini.
[14]Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia.
Umeona hawa ni watu, wanaodhani kumtumikia Mungu tu yatosha hakuna haja ya kuishi maisha matakatifu. wanakutwa na majani tu peke yake.
Tuhakikishe tuna majani, lakini vilevile tuna matunda kwasababu sisi ni shina, ndani ya mti wa uzima. Na neema ya Mungu itatusaidia.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Tafsiri ya Mithali 27:18 Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake;
KWANINI MTINI KATIKATI YA MIZABIBU?
UMEIZALIA MATUNDA MIAKA 4 YA NEEMA ULIYOPEWA?
Rudi Nyumbani
Kama mwamini hizi si nyakati za kuishi kilegevu, unapoona, watu wanakufa katika dhambi na kwenda jehanamu bila kumjua Kristo, unajisikiaje, unapoona kazi za shetani zinasitawi, na kuwaharibu watu unawezaje kutujulia moyoni mwako?
Ni Funzo gani unalipata nyuma ya hasira ya Samsoni? Alipoona mke wake ameuzwa kwa wageni na baba-mkwe wake, je alitulia, na kusema basi tu hii siyo bahati yangu? Kinyume chake Alinyanyuka kwa hasira akasema ninakwenda kulipiza kisasi, kwa hawa wafilisti.
Alikwenda kuwachukua mbweha mia tatu (300), Akawafunga wawili wawili mikia yao, kisha, akawafungia mienge ya moto, na kuwaachia waingie kwenye mashamba ya ngano ya wafilisti. Baada ya hapo ni jambo gani akawa analifanya? Ni kuwaangalia tu wale mbweha walivyokuwa wanayateketeza mashamba ya ngano hekari kwa mahekari. Jambo lililowafanya wafilisti waamke wote kwenye majumba yao wamtafute huyu Samsoni ni nani?
Waamuzi 15:3 “Samsoni akasema, Safari hii nitakuwa sina hatia katika habari za hawa Wafilisti, hapo nitakapowadhuru. 4 Samsoni akaenda akakamata mbweha mia tatu; kisha akatwaa vienge vya moto akawafunga mbweha mkia kwa mkia, akatia kienge kati ya kila mikia miwili. 5 Alipokwisha kuviwasha moto vile vienge, akawaachia mbweha kati ya ngano ya Wafilisti, akayateketeza matita, na ngano, hata na mashamba ya mizeituni”
Ni Yesu Kristo,
Bwana alipoona kazi za adui zinapaswa ziharibiwe pale Israeli. Alichofanya ni kuwachukua wanafunzi wake pia, akawatuma wawili-wawili akawaambia waende mahali alipotaka yeye kwenda, akawapa amri ya kutoa pepo, kupooza magonjwa na kuhubiri habari njema. Na unajua ni nini kilitokea baada ya pale, ndani ya kipindi kifupi, waliporudi?
Yesu alikuwa akiwaangalia “MBWEHA WAKE” katika roho wakiziharibu kazi za shetani, akasema, nalimwona shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme.. Ha! ha! ha! ha! Mbweha wamfanya kazi.
Luka 10:17 “Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. 18 Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. 19 Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru”.
Na sisi (yaani mimi na wewe), tuliookoka, Ikiwa umeshajazwa “Roho Mtakatifu” wewe tayari ni mbweha, Sijui unasubiri nini kwenda kuziharibu kazi za shetani, kwa kumuhubiri Kristo, na wokovu wake? Unasubiri nini mpendwa?
Angalia Yesu alichokisema..
Luka 12:49 “Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi?
Moto umekwisha kuwekwa kwenye mkia wako, angalia usije ukazima kabla haujafanya kazi yake. Ndio huo moto wa Roho Mtakatifu unaochoma ndani yako, kukuagiza uhihubiri neema ya Kristo kwa ndugu zako na watu wengine ili waokoke.
Kwa pamoja tunaweza upindua ulimwengu. Tumuhubiri Kristo, hilo ndilo agizo kuu kwa wanadamu wote. Kila mmoja wetu ni mbweha wa Kristo. Simama sasa, pokea ujasiri, kamuhubiri Kristo, watu waokoke.
Bwana akubariki
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
KWANINI KILA MWAMINI ANAPASWA AWE MHUBIRI WA INJILI