Mwanadamu kaumbwa kwa vitu viwili: MWILI na ROHO, Na kila upande una namna yake ya kutunzwa, na namna yake ya kuangamizwa, kila kimoja kina namna yake ya kupata uzima, na namna yake kupata mauti. Kwamfano mwili unatunzwa kwa vyakula vya kimwilini, na maji ya kimwilini, vivyo hivyo unaharibiwa kwa vitu vya kimwili, mwili ukikosa chakula au maji unakufa, kadhalika ukiunguzwa na moto unakufa.
Na roho pia ipo vivyo hivyo, ili iiishi inahitaji vyakula vya aina yake ya rohoni, na maji yake ya rohoni, hivyo ikikosa hivyo vitu, basi hiyo roho nayo itakufa, na pia roho ikiunguzwa na moto wa rohoni itakufa vile vile, lakini moto wa mwilini hauwezi ukaiunguza roho, kwasababu Mungu alivyoyaumba maumbile ya mwili ni tofauti na yale ya roho.
Tukirudi katika maandiko, Kristo alikuja kuvikomboa vyote viwili (yaani miili yetu na roho zetu), ili vipate uzima wa milele, hivyo kwasababu alikuja kuzikomboa roho zetu, hawezi kutumia zana za mwilini kuzipa roho zetu uzima wa milele, ni sharti azizalishie roho zetu chakula cha rohoni, na maji ya rohoni ili zipate uzima huo. Na ndio maana alisema wazi Katika..
Yohana 6:35 “Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe”.
Unaona chakula na maji yanayozungumziwa hapo sio vya mwilini bali vya rohoni.
Sasa watu ambao watakufa leo hii, ambao hawajaokolewa, moja kwa moja roho zao zinashuka mahali panapoitwa kuzimu au Jehanum. Kule ni mahali ambapo mtu anawekwa kwa muda akisubiria hukumu ya mwisho ya mwanakondoo..
Tunaweza kusema kwa lugha ya sasa ni mahabusu au lockup ambapo mtu anakaa kule akingoja apandishwe kizimbani asomewe mashtaka yake kisha akatumikie kifungo chake aidha cha miaka 10 au 20 au cha maisha. Na ndivyo ilivyo kwa Jehanum hiyo ni tofauti na ziwa la moto. Ziwa la moto lenyewe linakuja mara baada ya hukumu ya mwanakondoo ambapo wakati huo kila mwenye dhambi atatumikia adhabu yake kwa kipimo cha uasi wake alioufanya duniani.
Tazamia pia…
Kumbuka Bwana alipokuwa amesimama katikati ya makutano ya watu wengi akipaza sauti yake kwa nguvu nyingi sana na kwa bidii kuwaambia watu waende kwake wanywe MAJI YA UZIMA yanayotoka kwake hakuwa anatania au anasema mambo ambayo hayana maana sana katika maisha ya mtu, hapana ndugu yangu, Alijua kabisa upo wakati roho za watu zitalia na kuugua kusikoweza kunenwa zikitafuta walau hata tone moja tu ya hayo maji wasilipate…Embu sikiliza Bwana Yesu alivyopaza sauti yake kwa bidii kuwasii watu katikati ya makutano siku ile kwenye sikukuu..
Yohana 7:37 “Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, MTU AKIONA KIU, NA AJE KWANGU ANYWE.
38 Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, MITO YA MAJI YALIYO HAI ITATOKA NDANI YAKE.”
Sasa kumbuka haya maji faida yake sio kukupa uzima wa roho yako hapa duniani tu, hapana bali hii inaendelea hata baada ya kufa, lakini watu ambao hawajataka kuyanywa haya Maji sasa hivi, wakati yanapatikana kwa wingi na bure, utafika wakati karibia na kufa au baada ya kufa watatambua umuhimu wa haya maji, na pale watakapoyatafuta watayakosa..wakizitazama roho zao zinaenda kufa kwa kukosa maji, watahangaika kwa namna isiyoelezeka wakiyatafuta hayo maji ya uzima wasiyapate…Ndio tunarudi kwenye ule mfano wa Lazaro Bwana Yesu alioutoa katika..
Luka 16:19 “Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa.
20 Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi,
21 naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake.
22 Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa.
23 Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake.
24 Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro ACHOVYE NCHA YA KIDOLE CHAKE MAJINI, AUBURUDISHE ULIMI WANGU; kwa sababu ninateswa katika moto huu.
25 Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa.
26 Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.
27 Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu,
28 kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso.
29 Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao.
30 Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu.
31 Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu”.
Tukisoma habari hiyo, tunaona kabisa wakati unaozungumziwa hapo ni wakati ambao watu wanaishi duniani na wengine wapo katika upande wa pili; aidha kuzimu au mahali pa starehe, Ni wazi kuwa mtu anapokufa bado anaendelea kuishi, mwili wake unabaki hapa hapa duniani lakini roho yake inaendelea kuishi mahali Fulani.
Kumbuka hapo mwili umeshabaki makaburini, kinachoendelea kuishi ni roho, na kama tulivyoona roho haiunguzwi kwa moto wa kawaida kama huu, hapana moto wa roho ni mwingine ambao hata sasa mtu anaweza akauhisi, jaribu kufikiri leo hii umehukumiwa kwenda kunyongwa, ukijua kuwa una dakika chache tu za kuishi, ni dhahiri kuwa ndani yako kutawaka moto ambao huo huwezi kuuelezea kwasababu unajua ni adhabu inayogharimu maisha yako hapa duniani,
Sasa huo unaousikia ndio moto wa roho isipokuwa katika kiwango kidogo sana, unaichoma roho yako, upo moto hasaa usioelezeka ambao utakuja baada ya kifo, pale utakapogundua hakuna mageuzi milele, una kipindi kifupi tu kisha ukatupwe kwenye lile ziwa la moto katika maangamizi ya milele, Utajisikiaje siku hiyo? Hiyo roho yako itakuwa ikihangaika kiasi gani ndugu?.Huo ndio moto yule tajiri uliokuwa unamuunguza kule kuzimu katika vifungo vya giza alivyokuwepo.
Jambo lingine tunaona liliokuwa linamtesa yule tajiri kule kuzimu ni KIU.. Hakuwa na kiu ya maji haya ya kisimani, kwasababu kule kuzimu mwili haupo alishauacha makaburini..Bali alikuwa na KIU YA MAJI YA UZIMA YAUPAO ROHO YAKE UZIMA. Alitamani apate walau tone moja la yale maji, apate uzima kidogo wa roho yake utakaomfanya angalau aishi kidogo, lakini hakupata,.. Alitamani apate nafasi ya pili ya kutubu dhambi zake, ili apate uzima lakini alikuwa ameshachelewa, alitamani abatizwe akitumaini hata siku ile atakayohukumiwa apate neema lakini alishachelewa, alitamani hata afanye ushirika na wakristo lakini muda ulishapita, alitamani akawashuhudie wengine habari njema lakini mlango ulikuwa umefungwa n.k.
Alipokuwa duniani aliikata ile KIU ya kutafuta UZIMA kwa mambo mengine, kwasababu ya utajiri wake akaikata kwa mali akiamini kuwa mali zinaweza kumpa uzima badala ya YESU KRISTO, hatuoni hata watu leo hii wakisema ukipata pesa umepata kila kitu,? Hawajui ya kwamba pesa haimpi mtu uzima, isipokuwa yale maji yanayotoka kwa Bwana YESU mwenyewe. Utajiri wa AFYA ulimdanganya akidhani kuwa afya yake itadumu, kwa lishe bora aliyokuwa akiizingatia na kwa wingi wa matabibu aliokuwa nao hakuna haja ya kumtafuta mwingine wa kumpa uzima, hao wanatosha kukata kiu yake..
Kwa wingi wa ANASA alizozitumainia, akaona zinatosha kumpa amani na furaha na raha, hivyo akapuuzia Amani idumuyo inayotoka kwa Bwana. Utajiri wake wa mambo yote, marafiki, ndugu, jamii, mali, afya, n.k. hakuna hata moja baada ya kufa vilifanikiwa kukatisha KIU iliyokuwa ndani yake..Jambo hilo alikuja kulingundua baada ya kufa.Na ndio maana hapo analia akitaka TONE moja tu la MAJI YA UZIMA.? Ndugu HAYO MAJI yalivyo na thamani kubwa baada ya kufa…Utatamani tone moja tu utakosa.
Leo hii unaweza kuona mtu baada ya kupatwa na mabaya, aidha kaambiwa na madaktari ugonjwa alionao anao mwezi mmoja tu wa kuishi, utaona mtu huyo kama alikuwa sio mkristo anaanza kuhangaika kumtafuta Mungu, lakini hapo kwanza wakati ni mzima alikuwa anaudhihaki wokovu,..Sasa hiyo ndio dalili ya ile KIU HALISI inaanza kuja ndani yake, hapo ndio unaanza kuona mtu anamtafuta mchungaji, anapigia watumishi simu wamuombee, au wamuhubiri n.k.. Sasa akishakufa katika dhambi zake, huko anakokwenda hiyo KIU inajizidisha mara nyingi sana zisizoweza kuelezeka ndipo majuto yasiyokuwa ya kawaida yatamjia.
Huko Jehanum Bwana Yesu alieleza pia kuna FUNZA ambaye hafi kama tunavyosoma katika
Marko 9:43” Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika;
44 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.
45 Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum;
46 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.
47 Na jicho lako likikukosesha, ling’oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum;
48 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki”
Ukichunguza hapo utaona huyo FUNZA ni mmoja, ikiashiria kuwa wote watakaokuwa kule wataumizwa na huyo huyo mmoja, dhiki na shida watakazopitia watu wote watakaokuwepo huko zitafanana. Sasa huyu FUNZA ni nani?.
Tunajua siku zote funza huwa hawaji isipokuwa tu pale penye mzoga..Na kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanautafuna ule mzoga mpaka unakwisha.. Sasa huyu FUNZA sio wa mwilini, kwasababu huko hakuna mwili, kazi ya mwili itakuja kuonekana katika ziwa la moto ambalo tutaliona mbeleni kidogo.
Huyu FUNZA ni KUMBUKUMBU ZENYE MAJUTO. Hizi kumbukumbu kila mmoja atakayekuwepo kuzimu, zitamla, kila mmoja atakuwa anajutia maisha yake aliyoishi duniani, atakumbuka kuanzia siku ile alipokuwa mdogo anahubiriwa injili na kuipuuzia, atakumbuka siku aliyokuwa anadhihaki kazi ya Mungu, atakumbuka siku alizokuwa anafanya uasherati huku Roho wa Mungu akimwonya kwamba hicho kitu anachokifanya ni dhambi lakini hakutaka kusikia, atakumbuka siku aliyokuwa anasoma mahubirini na kuyapuuzia,
Atakumbuka muda aliokuwa anakawia kutubu mpaka kifo kilipomkuta kwa ghafla, atasema imekuwaje kuwaje nimefika hapa muda ambao bado?, yale majivuno yangu yananisaidia nini hapa?, ule uzuri wangu uko wapi tena?, zile pesa zangu mbona haziji kunitetea huku,.wale rafiki zangu niliokuwa nafanya nao anasa kumbe walinidanganya,..Ni majuto yasiyoelezeka utakapogundua kuwa wewe ni UZAO wa NYOKA, na ulidanganywa na shetani roho yako inakwenda kuteketezwa. UTALIWA NA HAYO MAWAZO kama vile FUNZA atafunavyo mzoga.
Sasa hayo majuto yatafikia kiwango ambacho hutatamani hata yule adui yako uliyekuwa unamchukia kuliko wote afike mahali ulipo, asifanye makosa uliyoyafanya wewe. Na ndio maana yule tajiri aliomba ndugu zake wakahubiriwe lakini akaambiwa wapo Musa na Manabii wawasikilize wao..Kuna watu leo hii wapo kuzimu wanakuombea wewe usifike kule. Ndugu kule sio mahali pa kufika kabisa.
Sasa baada ya huyo funza kuwala kwa muda mrefu utafika wakati sasa, wafu wote watafufuliwa katika miili yao waliyokuwa nayo hapa duniani, kisha kusimama mbele ya kile kiti cheupe cha Hukumu cha mwanakondoo (YESU KRISTO). (Ufunuo 20:11-15) Bwana Yesu alisema..
Yohana 5:28 “Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake.
29 Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu”.
Sasa hawa wote waliokuwa kuzimu watafufuliwa, na kuvaa miili yao ya duniani waliyokuwepo nayo, ili wahukumiwe na kupewa sababu ya wao kwanini wanastahili adhabu inayofuata. Hivyo kila mmoja atahukumiwa kulingana na matendo yake na wingi wake wa dhambi alizozifanya. Kila mmoja wapo biblia inasema atakuwa na SEHEMU YAKE huko katika ziwa la moto..kwasababu ni ziwa litakuwa na nafasi kubwa, kila mmoja atakuwa na eneo lake peke yake akiungua.
Huko ndiko mwili na roho vyote kwa pamoja vitaangamizwa kwenye moto mkali sana utakaounguza mwili na roho kushinda hata ule uliokuwepo Jehanum. Hivyo ndugu tukiyajua hayo biblia ilishaweka wazi kabisa Katika
Ufunuo 21:8 “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”
Kumbuka ndugu usifanye makosa kujiona ni TAJIRI na kuyadharau MAJI YA UZIMA kwasababu afya yako ni nzuri, au una mali ya kukutosha, au familia nzuri, au una ulinzi, n.k. hayo yote ipo siku yataondoka lakini KIU itabaki pale pale isipoikata leo hii, hautaweza kuikata kule..Usipumbazike na mambo ya ulimwengu huu yanayopita yakakupa kiburi kwamba Kristo hana faida yoyote katika maisha yako..
Na haya ndiyo Maneno aliyomalizia Bwana YESU katika kitabu cha biblia:
Ufunuo 22:16 “Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi.
17 Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! NAYE MWENYE KIU NA AJE; NA YEYE ATAKAYE, NA AYATWAE MAJI YA UZIMA BURE.”
Tubu ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji tele na kwa jina la Yesu Kristo, na uuishie utakatifu angali muda upo.
Ubarikiwe.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Tafadhali “Share” kwa wengine ujumbe huu na Bwana atakubariki.
About the author