Vitabu vilivyothibitika vya historia vinavyoeleza maisha na vifo vya watakaifu wengi wa kwanza vinaeleza kuwa Antipa alikuwa ni kasisi aliyeteuliwa na mtume Yohana, kuwa mwangalizi wa kanisa lililokuwa Pergamo. Kama vile Timotheo alivyowekwa na Mtume Paulo kuwa mwangalizi wa makanisa yote baada yake.
Ikumbukwe kuwa kipindi hicho ndio wakati ambao kanisa la kwanza la Kristo lilikuwa katika kilele cha dhiki ambacho kiliasisiwa na mtawala katili wa kirumi aliyeitwa Nero (54 W.W -68 W.W)..
Nero ndiye aliyehusika kwa kumwagika kwa damu ya mashahidi wengi wa Kristo katika kanisa la kwanza. Na hiyo ilisababishwa na tukio la moto usiojulikana chanzo chake ni nini kuzuka huko Rumi mjini, na kusingiziwa wakristo ndio waliousababisha moto huo..Hivyo marufuku ikapigwa kwa mtu yeyote kujihusisha na imani ya kikristo.
Kipindi hicho mtu yeyote ambaye alionekana anaishikilia imani ya kikristo adhabu yake ilikuwa ni kifo na kama hutakufa basi utafungwa na kupelekwa uamishoni. Mtume Yohana baada ya kukwepa majaribio mengi ya kifo kimiujiza walimshika na kwenda kumfunga katika kisiwa cha Patmo. Huko ndipo Mungu alipompa ufunuo wa kitabu cha Ufunuo.
Na katika moja ya barua alizopewa azirudishe kwa yale makanisa 7, ndani yake Kristo alimkumbusha juu ya mtu aliyemfahamu anayeitwa Antipa..
Tusome:
Ufunuo 2:12 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na huo upanga mkali, wenye makali kuwili.
13 Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani”.
Unaona Antipa alikuwa ni mtu aliyethibitika katika imani, japo alikuwa katikati ya vita vikali vya imani kama vile vya kuuawa na kuteswa, lakini hakuacha kuihubiri injili kwa nguvu. Katika utumishi wake alifanikiwa kuwageuza watu wengi wa mji ule kuacha kutoa sadaka kwa miungu , na masanamu. Lakini makuhani wa kipagani wa Rumi, walipomwona anawavuna watu wao wengi, na kuiacha Imani yao. walimfuata na kumkataza asiwafundishe watu imani za miungu migeni katika jamii yao. Na asiingilie miungu yao. Kama tu ilivyokuwa kwa Mtume Paulo alipofika kule Efeso, na kuwahubiria watu habari ya Kristo, wale wachonga vinyago walipoona biashara yao inakaribia kufa, walizusha vurugu katika mji.(Matendo 19:24)
Lakini Antipa hakusita kuwaambia bila kuogopa.. Alisikika akiwaambia
…“mimi siyatumikii mapepo ambayo yanaweza kunikimbia, yasiyo na maisha ya milele, mimi ninamwabudu Mungu muweza yote, Na nitaendelea kumwabudu Mungu muumba wa vyote, katika Kristo Yesu na Roho Mtakatifu siku zote za maisha yangu”.
Wale makuhani wakamjibu, na kumwambia mungu wetu sisi alikuwepo tangu zamani, lakini nyie mnamuabudu Yesu ambaye aliuliwa na Pontio Pilato kama uhalifu.
Lakini Antipa naye hakuacha kuwajibu..
“miungu yenu ya kipagani ni kazi ya mikono ya watu ambayo ndani yake kinachozaliwa si kingine zaidi ya maovu na machafuko”.
Antipa aliendelea kwa ushujaa huo huo kuikiri imani yake katika YESU KRISTO bila woga mbele zao daima. Wale makuhani wa kipagani walipoona mtu huyu hana dalili ya kuacha kumuhubiri Kristo, na kuwafundisha watu wasiabudu sanamu, uzalendo ukawashinda wakamkamata na kumpeleka mbele Ya hekalu la mungu wao Artemi. Wakamtupa ndani ya tanuru la moto jekundu la shaba ambalo walikuwa wameliandaa kwa ajili ya kutengeneza ng’ombe wao kwa shaba ile.wakamtupa ndani mule.
Wakati akiwa ndani ya moto ule mkali alisikika akiomba, akisema Mungu ipokee roho yangu. Na pia ziimarishe imani za wakristo wote. Kisha akalala katika usingizi wa amani kama ule wa Stefano.
Usiku ulipofika, ndugu zake wa imani wakaja kumchukua na kwenda kumzika pembezoni mwa mji huo wa Pergamo.
Siku zikapita siku zinakaenda, pengine akasahaulika na wengi lakini siku moja baada ya miaka kadhaa mbele, Mtume Yohana akiwa katika kisiwa cha Patmo.. alimsikia Yesu Kristo akimtaja kwa maneno haya:..
“Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu”..
Hadi sisi leo hii tunazisoma na kuziandika habari zake.
Mtume Paulo aliandika hivi juu ya watu hawa:
Waebrania 11:36 “wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;
37 walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya;
38 (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.
39 Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi;
40 kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi”.
Kisha akamalizia na kusema..
Waebrania 12:1 “Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na WINGU KUBWA LA MASHAHIDI namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu”.
Tunapokuwa wakristo halafu bado tunashikilia mizigo ya vimini, mizigo ya makeup, mizigo ya nguo za kikahaba, mizigo ya uchawi, ushirikina, uzinzi na hasira… tutawezaje kupiga mbio kwa spidi kama hawa watu waliojikana nafsi siku ile?. Ikiwa leo hii mizigo ya uzinzi bado tunaishikilia, mizigo ya mustabation, mizigo ya betting, mizigo ya usengenyaji, mizigo ya rushwa, mizigo ya shughuli za ulimwengu huu zisizotupa hata nafasi ya kumfanyia Mungu ibada..Tutaweza siku ile kufananishwa na kundi hili la watu?.
Bwana hana upendeleo, kile apandacho mtu ndicho atakachovuna.. Mungu atusaidie sana tupande kilichochema, ili siku ile tuvune kilichochema. Tuitumie mizigo yetu. Tumtazame Kristo.
Ikiwa hujampa Kristo Maisha yako!..Nataka nikuambie haijalishi utakufa kifo cha heshima kiasi gani na kuzikwa na watu wengi kiasi gani…Kumbukumbu lako litakuwa limeishia hapo hapo hakuna mtu atakukumbuka wala Mbingu haitakukumbuka…lakini Ukitubu na kumwishia Kristo leo, ukasema kuanzia leo mimi ni anasa basii,..mimi na ulevi basii mimi na uasherati basii..ukaonyesha kwa vitendo kabisa kwamba umeachana na hivyo vitu…
Basi Yesu Kristo atakusamehe kama alivyosema katika Neno lake..na hata ukifa leo hii kumbukumbu lako halitasahauliwa kama Antipa..na Bwana atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi ulizokuwa unashindwa kuzishinda..na atakuongoza na kuijua kweli yote ya maandiko..Ikiwa upo tayari kufanya hivyo..hapo ulipo tubu na Bwana atakusamehe.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Ubarikiwe sana..
Mada Nyinginezo:
VIFO VYA MITUME WA YESU/ JINSI MITUME WALIVYOKUFA.
TUMEPEWA, SI KUMWAMINI TU KRISTO, ILA NA KUTESWA KWA AJILI YAKE;
ALIYE MKUU KATIKA UFALME WA MBINGUNI.
SIKU ILE NA SAA ILE.
WAMNGOJEAO BWANA WATAPATA NGUVU MPYA.
About the author