Shalom. Karibu tujifunze Biblia…
Wana wa Israeli walipomwacha Mungu kwa muda mrefu na kuitumikia miungu mingine migeni.. Mungu aliwatoa katika nchi yao na kuwapeleka katika mataifa ya mbali..Israeli akaipeleka Babeli na baadaye Yuda nayo akaipeleka Ashuru nchi ikabakia tupu…Lakini mfalme wa Ashuru kuona nchi imebaki haina watu, akaamua kukusanya baadhi ya watu kutoka katika baadhi ya nchi za jirani na za mbali na kuwapa nchi hiyo ya Israeli waishi ndani yake..ili pasibaki patupu…Lakini hao watu wakaishi mule bila kujua kuwa ile ni nchi takatifu, na haipaswi kutiwa unajisi..Mungu akawaletea Wanyama wakali kama simba..mpaka walipojifunza kuishi kulingana na kawaida ya hiyo nchi…
Tusome..
2Wafalme 17:23 “hata Bwana akawaondoa Waisraeli wasiwe mbele zake, kama vile alivyosema kwa kinywa cha watumishi wake wote, manabii. Basi Waisraeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe, waende nchi ya Ashuru, hata leo.
24 Naye mfalme wa Ashuru akaleta watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli; wakaumiliki Samaria, wakakaa katika miji yake.
25 Basi ikawa, wakati ule walipoanza kukaa huko, hawakumcha Bwana; kwa hiyo Bwana akapeleka simba kati yao, nao wakawaua baadhi yao.
26 Kwa hiyo wakamwambia mfalme wa Ashuru, wakasema, Wale wa mataifa uliowahamisha, na kuwaweka katika miji ya Samaria, hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi; kwa hiyo amepeleka simba kati yao, na tazama, wanawaua, kwa sababu hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi.
27 Ndipo mfalme wa Ashuru akatoa amri, akasema, Mpelekeni mmojawapo wa makuhani, mliowachukua kutoka huko; aende akakae huko, akawafundishe kawaida ya Mungu wa nchi.
28 Basi mmoja wa makuhani waliochukuliwa kutoka Samaria akaenda akakaa katika Betheli, akawafundisha jinsi ilivyowapasa kumcha Bwana.
29 Lakini pamoja na hayo watu wa kila taifa wakajifanyia miungu yao wenyewe, wakaiweka katika nyumba za mahali pa juu, walipopafanya Wasamaria, kila taifa katika miji yao walimokaa.
30 Watu wa Babeli wakafanya Sukoth-benothi kuwa mungu wao, watu wa Kutha wakafanya Nergali, watu wa Hamathi wakafanya Ashima,
31 Waavi wakafanya Nibhazi na Tartaki; nao Wasefarvi wakawaunguza wana wao katika moto kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu.
32 Basi hivyo wakamcha Bwana, nao wakijifanyia wengine wao kuwa makuhani wa mahali pa juu, ambao waliwafanyia dhabihu katika nyumba za mahali pa juu.
33 WAKAMCHA BWANA, NA KUITUMIKIA MIUNGU YAO WENYEWE, sawasawa na kawaida za mataifa ambao wao walihamishwa kutoka kwao”.
Nataka tuone huo mstari wa 33 wa mwisho unaosema “WAKAMCHA BWANA, NA KUITUMIKIA MIUNGU YAO WENYEWE”…Sentensi hiyo maana yake walifanya vitu viwili kwa wakati mmoja…yaani walimcha Mungu na hapo hapo waliitumikia miungu yao.
Kwanini walimcha Bwana?..Ni ili tu wasiendelee kuuawa na simba…na kwanini waliendelea pia kuitumikia miungu yao waliyotoka nayo huko?…Ni kwasababu wanaipenda na hawawezi kuacha asili yao.
Kwahiyo ili kuendelea kuishi vizuri katika hiyo nchi, wasiendelee kuliwa na simba.. wakaona njia pekee ni kuchanganya mambo…Nusu Mungu,nusu sanamu…Nusu kutoa zaka nusu kufanya anasa, na kwenda kwa waganga…Nusu kufanya mema nusu kutenda mambo maovu…Nusu kutumikia Mungu wa kweli wa Israeli nusu kuitumikia miungu ya makabila yao waliyotoka nayo huko kwenye mataifa. Jambo hilo likawasababishia wakae chini ya laana muda mrefu badala ya baraka.
Huoni ni jambo linaloendelea hata leo..UVUGUVUGU. Nusu moto nusu baridi… Utakuta mtu ni mkristo anamtumikia Mungu wa kweli kanisani anakwenda na kuhudumu vizuri tu, analipa na zaka lakini akirudi kijijini kwao anaitumikia miungu ya mababu zake?.. atatoa kafara kidogo..atatambika kidogo, atatoa n.k…Mungu kwake ni kama kinga tu!..anamcha Mungu ili tu wachawi wasimpate, ili tu mambo yake yaende vizuri ili tu apate mke au mume wa kikristo, ili tu aeleweke kwenye jamii yake n.k lakini ndani kabisa wa moyo wake anaipenda na kuithamini miungu ya kwao. Tena ataisifia sana na kuiheshimu na kuiogopa kuliko hata Mungu wa kweli. Hatakosa matambiko yote ya kila msimu yanayofanyika kule. Ataendelea kuishikilia Imani yake na dhehebu lake ili tu asionekane kama ni mpagani wala mwabudu miungu… lakini ndani ya moyo wake anaiheshimu Zaidi miungu ya kwao…ndani ya moyo wake anazithamini Zaidi zile chale alizochanjwa na wale wazee waliomtambikia kuliko Mungu wa mbingu na nchi anayemfuata kila siku kanisani…Ataogopa Zaidi vitisho vya wazee wa mila lakini amri za Mungu hazitamwogopesha hata kidogo.n.k
Hivyo ndugu mpendwa…Bwana wetu Yesu Kristo alituonya sana kuhusu kuwa vuguvugu alisema…
Ufunuo 3:15 “Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi”
Na tena inasema katika ..
2Wakorintho 6:14 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?
15 Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?
16 Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
17 Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.
18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike”.
Mkristo Kufanya matambiko ya kimila ni dhambi, Mkristo kufanya matambiko ya marehemu ni dhambi, kuchanja chale ni machukizo mbele za Mungu…mtu wa Mungu hupaswi kufanya hivyo..kwenda kijijini kwenu kutafuta suluhisho la matatizo kwa mizimu ni machukizo makubwa mbele za Mungu…kwenda kusafisha nyota kwenu kwa mila za ulikotokea ni machukizo makubwa mbele za Mungu…Mkristo kwenda kufanya kafara yoyote na kujihusisha na kafara za kimila ni machukizo mbele za Bwana.
Sasa swali ni je! Tusiishi na ndugu wa ukoo wanaofanya hayo?..Jibu ni la! Tutaishi nao..lakini si kuchangamana nao kiimani..Unapookoka jambo la kwanza unalotakiwa kufanya ni kuhakikisha Imani yako na msimamo wako unatambulika na watu wote..hususani na familia yako na ukoo wako…Wote wanapaswa wajue kuwa wewe umegeuka na kuwa Mkristo, na siku ya kwanza wakikuambia ufanye hayo na kuwaeleza msimamo wako utawaudhi na dhiki lazima ije kidogo!..hivyo hilo weka akilini? Utapitia dhiki kwa kipindi Fulani na hata ikiwezekana kutengwa…lakini utafika wakati watakubaliana tu na wewe ulivyo!..Na mtaendelea kuishi kwa namna hiyo…
Usiogope laana watakazokulaani wala usiogope kwamba watakuloga…hakuna Uchawi juu ya Yakobo wala uganga juu ya Israeli likumbuke hilo siku zote (Hesabu 23:23). Wala huhitaji kuingia kwenye maombi ya vita kushindana wasikuloge..kitendo tu cha wewe kukana vile tayari kuna nguvu ya Mungu inakulinda kwa namna isiyokuwa ya kawaida..kwahiyo hakuna lolote litakalokupata.
Kadhalika kama nyumba yako umezindikwa kayaondoe hayo mazindiko yote sasahivi…kadhalika na vitu vingine vyote visivyo vya kikristo, usivichangaye na Ukristo wako….Unafahamu kabisa kwenye biblia hakuna sehemu yoyote Mungu alihusianishwa na sanamu, la mtakatifu yeyote, hakuna mahali popote sanamu la bikira Maria linaabudiwa, lakini wewe kwa kulijua hilo unasema nimeokoka, na bado unakwenda kuisujudia sanamu hiyo ili tu kuwaridhisha wazazi wako, nataka nikuambie hayo ni machukizo makubwa sana mbele za Mungu “Usimche Mungu na kuitumikia miungu yako”..Usijaribu kufanya hayo mambo mawili kwa wakati mmoja. Ni machukizo makubwa na yenye madhara mara mbili, kwasababu biblia ndio inayataja hayo kama uasherati wa kiroho.
Bwana akubariki sana.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii 0789001312
Mada Nyinginezo:
AGENDA KUBWA YA SHETANI KWA KANISA HILI LA LAODIKIA.
HISIA YA MUNGU ILIYO MBAYA KULIKO ZOTE.
Bwana aliposema kuwa yeye ni “Mungu wa miungu” alikuwa na maana gani?..je! yeye ni Mungu wa sanamu?
NI NINI KINAKUPATA UNAPOIPUUZIA INJILI?
MAANA YA RANGI KIBIBLIA.
MIILI YA UTUKUFU ITAKUWAJE?
TAZAMA, MWISRAELI KWELI KWELI, HAMNA HILA NDANI YAKE!
JE! MUNGU NI NANI?
About the author