Mwanamke wa Kikristo unapaswa ujue nini?
Karibu tujifunze Biblia, ambayo ndiyo mwanga wa njia zetu na Taa iongozayo miguu yetu.
Ujumbe huu unakuhusu wewe binti wa Mungu ambaye pengine una bidii ya kumtafuta Mungu, karibu leo tujifunze baadhi ya mambo ambayo yatakusaidia katika safari yako ya imani, na yatakayokuongezea maarifa ya kutosha ya namna ya kutembea na Mungu kwa jinsi anavyotaka wewe utembee naye.
Jambo la kwanza la kuzingatia binti wa Mungu usomapo biblia…usikimbilie kusoma habari za wanaume kama wakina Musa, Daudi, Ezekieli, Yohana au Paulo…Ni vizuri kusoma hayo yote!..lakini nataka nikuambie kwamba ukikimbilia kusoma habari za hao bila kusoma kwanza habari za wanawake wenzako kama wewe katika maandiko hakika nakuambia utakuwa umeukwepa msingi mkubwa sana na wa muhimu katika maisha yako.
Kabla ya kutaka kujifunza habari za Daudi na Ushujaa wake…Hebu ingia ndani kwanza kajifunze habari za bibi yake Daudi aliyeitwa RUTHU, ni jinsi gani alimpendeza Mungu..kayasome maisha yake na kajifunze habari zake kwa mapana na marefu jinsi alivyoishi na wakwe zake na jinsi alivyompendeza mumewe Boazi..Ikiwezekana kamata kalamu na karatasi zinakili zile points zote, zishike hizo na kuziishi ndizo zitakazokusaidia sana kuwa mwanamke unayeishi kwa kumpendeza Mungu kuliko kujifunza habari za ushujaa wa Daudi. Ushujaa wa Daudi kwako wewe mwanamke hauna manufaa sana kwako zaidi ya ushujaa wa Ruthu bibi yake Daudi, au ushujaa wa Abigaeli mkewe Daudi.
Kabla ya kujifunza kwa kina habari za Daudi jinsi alivyomwangusha Goliathi..hebu kajifunze kwanza habari za Abigaili mke wa Daudi jinsi alivyomzuia Daudi kwenda kumwaga damu, kajifunze kwanza jinsi Abigaili alivyomnyenyekea Daudi…ziige hizo tabia kwanza za mke wa Daudi, kabla ya kwenda kuziiga za Daudi.(1Samweli 25:2)
Hali kadhalika kabla ya kwenda kujifunza juu ya Imani ya Ibrahimu..Hebu kwanza jikite kumsoma kwa undani SARA!..Zitafute siri za mafanikio za Sara kabla ya kutamani kuzitafuta za Ibrahimu..za Ibrahimu hazitakusaidia sana wewe mwanamke zaidi ya za Sara..Ibrahimu aliambiwa akatahiriwe na asingefanya hivyo alikuwa anakwenda kinyume na maagizo ya Mungu sasa wewe Tohara inakusaidia nini, hayo maagizo yanakufundisha nini wewe?…Lakini ukijiingia ndani kujifunza Jinsi gani Sara alimpendeza Mungu..ukazijua siri zote za maisha ya Sara hakika hutabaki kama ulivyo, na shetani hatakaa akuweze kamwe kama alivyowashindwa wakina Sara.
Sara alifikia hatua ya kumweshimu mumewe mpaka akafikia hatua ya kumuita mumewe “Bwana” (kasome 1Petro 3:6)..Hebu na wewe iga kwanza hayo mazuri ya Sara kabla ya kukimbilia kutamani mazuri ya Ibrahimu.
Vivyo hivyo kabla ya kukimbilia kujifunza juu ya Petro, Yohana au Mathayo wanafunzi wa Bwana Yesu..hebu tenga muda kwanza kujifunza juu la kundi lingine la waliomfuata Yesu kwa bidii mfano wakina (Mariamu Magdalene, Susana, wakina Martha na Miriamu)…Ingia ndani kujifunza maisha ya hawa wanawake watakatifu ni jinsi gani walivyompendeza Mungu…usikimbilie kujifunza juu ya Mitume jinsi walivyokuwa hodari wa kwenda vijiji na vijiji kuhubiri…hayo hayatakusaidia sana zaidi ya kujifunza juu ya wanawake wakina Susana walivyomhudumia Bwana kwa mali zao..Hawakuwa miongoni mwa waliotumwa na Bwana kuzunguka huko na huko…. lakini sehemu kubwa ya Huduma ya Bwana michango ilitoka kwa hawa wanawake watakatifu.. Hilo ndio Jeshi kubwa linalomtumika Bwana!!
Luka 8:1 “Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye,
2 na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba,
3 na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, NA WENGINE WENGI, WALIOKUWA WAKIMHUDUMIA KWA MALI ZAO”.
Kabla ya kujifunza mazuri ya Tajiri Zakayo jinsi alivyomkaribisha Bwana nyumbani kwake na kutoa zaidi ya Nusu ya mali zake na kuwapa masikini(Luka 19:1-8)…Hebu kajifunze kwanza juu ya Martha jinsi alivyomkaribisha Bwana nyumbani kwake na akatoa Marhamu ya Nardo safi yenye thamani nyingi akampaka Yesu miguuni..na wala hakwenda kuiuza na kuwapa maskini kama ambavyo angefanya Zakayo…Na hiyo ikamsababisha kumpendeza Yesu zaidi ya alivyofanya Zakayo.(Yohana 12:1-7). Kajifunze ni kwanini alifanya vile Martha na wewe ukafanye vilevile…
Usitangulie kujifunza juu ya mazingira Bwana Yesu aliyowatokea Mitume wake 12..shughulika sana kujifunza juu ya mazingira aliyowatokea wale wanawake walio mashujaa wa Imani..Hata hivyo Pamoja na Utume waliokuwa nao wakina Petro lakini hawakuwa wa kwanza kujua kwamba Bwana amefufuka..badala yake ni wale wanawake watakatifu ndio walioifunua siri hiyo wa kwanza ya kufufuka kwa Bwana.. Mariamu ni mwanamke wa kikristo aliyekaa katika nafasi yake na ndiye aliyekuwa wa kwanza kujua kwamba mwokozi anazaliwa ulimwenguni na Zaidi ya yote yeye ndiye aliyempokea..ni wanawake hao hao ndio waliokuwa wa kwanza kujua Mwokozi hayupo kaburini yu hai!….Huoni kama kuna siri kubwa sana hapo?…hata kuja kwa pili kwa Kristo si ajabu baadhi ya wanawake watakatifu ndio watakaokuwa wakwaza kujua…sasa kwanini leo unaikimbia nafasi yako wewe mwanamke wa kikristo??…Unataka kuwa PETRO?
Na wanawake wengine wote katika biblia ambao walikuwa ni mashujaa wa Imani.. kajifunze kwao kabla ya kwenda kujifunza juu ya mashujaa wa Imani wa kiume..kajifunze jinsi walivyovaa, kajifunze jinsi walivyojisitiri…kajifunze juu ya akina Debora jinsi alivyokuwa mnyenyekevu kwa Baraka na Israeli yote, kajifunze juu ya akina Hana, Rahabu, Dorkasi, Esta na wengineo wengi.
Nenda pia kasome, Waraka ule wa pili wa Yohana ambao uliandikwa kwa mama yule mteule jinsi alivyowalea Watoto wake na kuwatunza, mpaka wakakaa katika hiyo kweli, na sifa zake zikavuma katikati ya mitume wa Kristo, na kuaswa kuwa asiyaache matendo yake, bali aipokee thawabu tilimlifu..
Halidhalika, kasome maandiko yanayowazungumzia wanawake wengi, tabia zao mbaya ujiepushe nazo..Na moja ya tabia ambayo imendikwa ni ile ya Udadisi (Au kwa lugha ya kisasa umbea/usengenyaji) soma 1Timotheo 5:13. Itakufaa Zaidi kuliko mambo mengi unayoyasoma katika biblia..
Vivyo hivyo katika makosa usikimbilie kujifunza makosa ya wanaume wa kwenye biblia…kwamfano kosa la Daudi kulala na mke wa Uria sehemu yako ipo wewe kama mwanamke?..au linakufundisha nini?…zaidi somo lile linawafaa wanaume…Wewe kajifunze jinsi wanawake kama YEZEBELI walivyomchukiza Mungu..kajifunze ni tabia gani alizokuwa nazo mwanamke Yezebeli zilizomfanya Mungu amchukue…Yezebeli alikuwa ni mchawi, muuaji na mwanamke anayejipamba uso….Ni mwanamke pekee aliyekuwa anapaka uwanja machoni ndani ya Biblia nzima hakuna aliyekuwa kama yeye..(kasome 2Wafalme 9:30), vivyo hivyo kajifunze kwa wanawake waliofanya makosa kama Mke wa Luthu, makosa yale na wewe usiyafanye, Mke wa Ayubu…kajifunze wanawake wengine waliofanya makosa kama Yule mke wa Ahasuero aliyeitwa Vashti, ambaye alikuwa na kiburi hamweshimu mume wake, kisa tu yeye ni mzuri mpaka kusababisha nafasi yake kuchukuliwa na mwanamke mwenye adabu kama Esta. Jifunze juu ya viburi vya hao vilipowafikisha kabla ya kujifunza juu ya kiburi cha mwanamume Kora aliyemdharau Musa mtumishi wa Mungu.
Bwana akubariki sana…Naamini kwa hayo machache pamoja na mengine mengi Bwana atakayokufunulia utapiga hatua moja katika kuyatenda mapenzi ya Mungu, Ewe mwanamke wa kikristo.
Maran atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA
MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.
EWE MKE! HESHIMA YAKO IPO KWA WAKWE ZAKO.
RABONI!
MARIAMU AKUTANA NA ELISABETI.
TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI:
Je! Mungu anaupendeleo kwa wanaume zaidi ya wanawake?
CHAPA YA MNYAMA
About the author