Bwana Yesu sehemu nyingi aliifananisha baadhi ya mifumo ya maisha yetu na ufalme wa mbinguni…Kwamfano utaona alisema ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua (Mathayo 13:45).
Maana yake ni kwamba injili au Neno la Mungu pia limeandikwa katikati ya maisha yetu…
Yupo mtu mmoja aliufananisha ufalme wa mbinguni na sayari iliyo mbali sana….ambayo kwa mbali inaonekana ndogo sana kama nyota…lakini isogelewapo na kukaribiwa zaidi ni kubwa mno yenye uwezo wa kubeba viumbe vyote vya ulimwengu….Au kama ndege iliyo mbali sana angali, ambapo tukiwa huku chini tunaweza kuiona ni ndogo sana kuliko kalamu…lakini ishukapo chini ni kubwa yenye uwezo wa kubeba watu wengi na mizigo yao..
Hali kadhalika ufalme wa mbinguni unaonekana ni mdogo sana ukiwa mbali na mtu au watu…lakini ushukapo chini au ukaribiwapo ni mkubwa san ana wenye uwezo wa kubeba watu wengi na mizigo yao.. Hiyo yote ni mifano ya maisha ambayo imebeba injili ya Mungu ndani yake.
Upo mfano mwingine wa kimaisha ambao tunaweza kuutafakari kwa pamoja….ambao huo utaweza kutusaidia kumjua Mungu zaidi na ulinzi wake kwetu…
Hebu tafakari zile hifadhi za taifa kule porini, ndani yake kuna wanyama wengi, wanaishi…lakini wote wanalindwa na mamlaka kuu ya serikali pasipo wao kujijua, ushwari wa wao kuishi bila kuuawa na majangili inatokana na kazi ngumu askari wanazozifanya usiku na mchana kuzizunguka hifadhi hizo…ipo mipaka ambayo wananchi hawaruhusiwi kuisogelea kabisa licha ya kuiingia.
Na watoto wa Mungu wanakuwa wapo kwenye hifadhi ya Mungu…wanalindwa na serikali ya mbinguni…Malaika wanahakikisha kwamba hakuna pepo lolote linaloingia ndani ya mipaka hiyo na kuwadhuru…tunaweza tusiwaone malaika kwa macho siku zote za maisha yetu, lakini wapo wanatulinda..
Lakini kama tunavyojua mnyama yoyote akitoka nje ya ile hifadhi, usalama wake unapotea kwasababu huko nje majangili wapo na maadui wengi…hali kadhalika wanyama wanaoishi katikati ya wanadamu kifo chao hakithaminiki…mbwa wa kawaida halindwi na akifa anaonekana kama uchafu tu…lakini mbwa mwitu mmoja akifa ni hasara kubwa kwa Taifa. Wana thamani kubwa sana kwa taifa..na hakuna nchi inaweka nembo yake ya taifa mnyama wa kufugwa, utaona mara nyingi ni wanyama waliopo kwenye hifadhi za Taifa.
Hivyo na sisi tukitaka tusiishi maisha ya mashaka, maisha ambayo hayana usumbufu, yaliyokusudiwa kuishi mwanadamu…maisha ya ulinzi, maisha ya kuthaminika na mamlaka ya mbinguni, hatuna budi kuingia ndani ya “hifadhi ya Mungu (yaani ya mbinguni)”…Malaika kazi yao ni kuwahudumia tu wateule wa Mungu kasome waebrania 1:14, hakuna askari wa hifadhi anashughulika na mbwa wa kufuga (sehemu yao ni ndogo sana)…lakini wanakesha kwa wanyama wa hifadhini…Na malaika wa Mungu ni hivyo hivyo, wanakesha kuwalinda na kuwahudumia watakatifu.
Hakuna malaika anayetumwa kwenda kumlinda mwasherati asife, hakuna malaika anayetumwa kwenda kumlinda muuaji asikamatwe, au mtukanaji asiwindwe na wachawi n.k
Kwahiyo tunapokaa chini ya hifadhi ya Kristo ndio tunajipandisha thamani..Na hifadhi ya Mungu inazungukwa na mipaka ya Neno la Mungu…unapomwamini Yesu Kristo na kutubu dhambi zote na kubatizwa tayari unakuwa chini ya mamlaka ya mbinguni…shetani hawezi kukusogelea tena….na unapozidi kutoikaribia na kutoivuka ile mipaka ndivyo unavyozidi kuwa salama…Neno la Mungu linasema usiibe, usizini, usiue, usile rushwa n.k. Hiyo ndiyo mipaka.
Kama hujamwamini Yesu unasubiri nini?..mlango wa neema upo wazi, lakini hautakuwa hivyo siku zote…Tubu leo mgeukie Yesu, hizi ni siku za mwisho, na Yesu anakaribia kurudi. Fanya bidii ili uingie katika hifadhi ya Mungu.
Maran atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
About the author