KUMCHA MUNGU NI NINI? NA MTU ANAMCHAJE MUNGU?

KUMCHA MUNGU NI NINI? NA MTU ANAMCHAJE MUNGU?

Kumcha Mungu ni kukoje?


Kumcha Mungu ni Neno la jumla, linalomaanisha kujishughulisha na mambo yote yanayompendeza Mungu ikiwemo; kumpenda, kumtii, kumwogopa, kuchukia uovu, kumtumikia yeye, kufanya mapenzi yake, kumwabudu, kumfanyia ibada n.k. hiyo ndio maana ya kumcha Mungu..Ni tendo la jumla linalomaanisha kufanya mambo yote anayotaka wewe uyafanye.

Na ni  jukumu la kila mwanadamu chini ya jua kumcha Mungu. Na biblia imetoa faida nyingi za kufanya hivyo.

Tutaziorodhesha faida chache hapa, naamini kwa kuzijua hizo itakusaidia na wewe ambaye bado hujajua faida za kumtii Mungu, kukupa hamasa na wewe uanze kufanya.

  1. Faida ya kwanza kabisa ni kuwa unapata uzima wa milele.

Mithali 14:27 “Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti”.

Unaona unapokusudia kusema leo, naanza kumtafuta Mungu, basi hapo hapo tayari unafungua mlango wa chemchemi za uzima wa milele kububujika ndani yako.

    2. Kumcha Mungu unafungua mlango wa maarifa:

Mithali 1:7 “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu”.

Leo hii ukachagua kumtafuta Mungu katika maisha yako, ukajinyima kufuatana na njia za ulimwengu, basi Mungu anakupa zawadi nzuri sana ijulikanayo kama  maarifa..Maarifa hayo mtu mwingine yoyote hawezi kupewa, Ukiwa unaendelea tu kuishi maisha ya kumpendezesha Mungu, kuna kipindi kitafika utaanza kuona mabadiliko  fulani ndani yako ambayo yatakutofautisha ki-uelewa wewe na Mtu mwingine.

Mfano tunamwona Danieli na Wenzake watatu (Shedraki, Meshaki, na Abednego), wao walipoitwa na mfalme walichagua fungu la kumcha Mungu kuliko kujifurahisha na vyakula najisi vya kifalme..Na hiyo ikawapelekea baadaye mwishoni walipokuja ku-dahiliwa na mfalme, wakaonekana wao ni bora mara 10 zaidi ya wale wenzao waliokuwa wanajifurahisha katika vyakula vya kifalme.

Danieli 1:17 “Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danieli naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto.

18 Hata mwisho wa siku zile alizoziagiza mfalme za kuwaingiza, mkuu wa matowashi akawaingiza mbele ya mfalme Nebukadreza.

19 Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria; kwa hiyo wakasimama mbele ya mfalme.

20 Na katika kila jambo la hekima na ufahamu alilowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake”.

Hivyo na wewe ukiamua leo kumcha Mungu, yaani kutafuta kuyatenda mapenzi yake yapo maarifa mengine yatokayo mbinguni yataingia ndani yako kukutofautisha na ulimwengu wote.

      3.Kumcha Mungu, unapata hekima;

Zaburi 111:10 “Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima, Wote wafanyao hayo wana akili njema, Sifa zake zakaa milele”.

Sulemani alichagua kwanza kumcha Mungu, ndipo akapata hekima ambayo  iliwazidi watu wote ulimwengu..Hekima inakusaidia kupambanua mambo, inakusaidia kuelewa hata maandiko..Leo hii unaweza kusoma biblia usiielewe, lakini ukiwa ni mtu wa kutafuta kumjua Mungu na kuzidi kutaka kujifunza kutenda mapenzi yake, hekima hiyo Mungu anaileta ndani yako, na kujikuta unapata ufahamu wa kuyaelewa maandiko, na kupambanua mambo.

4.Kumcha Mungu kunaongeza siku za kuishi.

Mithali 10:27 “Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa”.

Kama ulidhani ni kuwaheshimu tu wazazi ndio kunaongeza siku za kuishi..Basi leo ujue kuwa ukiishi kwa kumpendeza Mungu nako pia kunazidisha siku zako za kuishi duniani. Mwangalie Ibrahimu, mwangalie Ayubu, mwangalie Yakobo n.k. hawa wote walikuwa ni wacha Mungu, na Mungu akawapa maisha marefu.

  5.Kumcha Mungu ni ulinzi kwa watoto wako.

Mithali 14:26 “Kumcha Bwana ni tumaini imara; Watoto wake watakuwa na kimbilio”.

Ukijibidiisha wewe kumtumikia Mungu, faida zake haziishi tu kwako, bali mpaka wa watoto wako,utakapokuwa haupo duniani,  ndivyo ilivyokuwa kwa watoto wa Ibrahimu, na watoto wa Yakobo na watoto wa Yusufu,

   6. Kumcha Bwana ni utajiri.

Mithali 22:4 “Thawabu ya unyenyekevu ambao ni kumcha Bwana Ni utajiri, na heshima, nayo ni uzima”.

Kama ukijibidiisha kuifanya kazi yake, Mungu anakupa na utajiri pia juu yake, wakati wake ukifika..

Bwana Yesu alisema..

Marko 10:29 “Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili,

30 ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele”.

Hizo zote ni faida zitokanazo na mtu Yule anayejishughulisha na mambo ya Mungu.

Lakini utawezaje kuishi maisha ya kumcha Mungu?

Ikiwa wewe umeokoka tayari, ni biblia pekee ndio itakayokuwa msaada wako wakati wote.Ukiwa msomaji wa Biblia itakayokusaidia kulifanya lile joto la kumcha Bwana liendelee kudumu ndani yako.. Lakini ukiwa sio msomaji wa biblia, yaani ni mivivu, ni rahisi kulipunguza kama sio kuacha kabisa kuyafanya mapenzi ya Mungu, biblia ni mwanga hiyo pekee ndio inatoa faraja, inatoa tumaini, inatia nguvu, inaonya, inakumbusha, inaongoza, inashauri..Hivyo ikiwa wewe ni msomaji mzuri wa biblia ni rahisi kwako kuishi maisha ya kumcha Mungu sikuzote..

Na ndio maana Mungu aliwapa wana wa Israeli, mpaka na wafalme maagizo haya kujifunza torati daima;

Kumbukumbu 17:18 “.. ajiandikie nakala ya torati hii katika chuo, kufuata hicho kilicho mbele ya makuhani Walawi;

19 na awe nayo, asome humo siku zote atakazoishi; ili apate kujifunza kumcha Bwana, Mungu wake, ayashike maneno yote ya torati hii na amri hizi, kwa kuyafanya;

Hivyo nawe pia jifunze biblia kwa muda mwingi uwezavyo. Na pia jitenge na mambo maovu

Mithali 8:13 “Kumcha Bwana ni kuchukia uovu; Kiburi na majivuno, na njia mbovu, Na kinywa cha ukaidi pia nakichukia’.

Kwa kufanya hivyo faida zote tulizo zihorodhesha hapo juu zitakuja juu ya maisha yako.

Lakini kama hujaokoka,  na unataka leo uanze safari yako na Mungu, basi uamuzi, huo ni mzuri, hapo ulipo Bwana anaweza kukusamehe na kukuokoa kabisa..Ikiwa tu utakuwa tayari kutubu kwa kumaanisha..Hivyo kama  upo tayari kufanya hivyo basi bofya hapa, kwa ajili ya kuongozwa sala ya toba >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe: +255 789001312

Mada Nyinginezo:

RABI, UNAKAA WAPI?

WEWE NI BWANA UNIPONYAYE.

Nifanye nini ili niwe na uhakika nikifa naenda mbinguni?

NINI KINATOKEA BAADA YA KIFO?

TABIA YA KIPEKEE USIYOIJUA KUHUSU NENO LA MUNGU.

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

YATAMBUE MAJIRA YA KUJILIWA KWAKO.

NAO WALIOKUWA WAMEKUSUDIWA UZIMA WA MILELE WAKAAMINI.

MANENO ALIYOWEZA KUTAMKA YESU TU PEKE YAKE.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

Ameen