Jibu: Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa makosa yote yanastahili msamaha. Hata kama tumetendewa makosa makubwa kiasi gani, mwisho wa siku ni lazima tusamehe, hiyo ndio sheria ya Imani. Hakuna ukristo bila msamaha, kwasababu kila mwanadamu katenda dhambi, na wote tunapata msamaha wa dhambi bure kupitia damu ya Yesu, tunapomwamini. Hivyo na sisi hatuna budi kusamehe kama Bwana alivyotusamehe sisi.
Lakini kuna jambo moja ambalo Bwana Yesu alilizungumza ambalo tukijifunza hilo vizuri tutapata kuelewa vizuri muktakabadhi wa msahama
Tusome..
Luka 12:58 “Maana, unapofuatana na mshitaki wako kwenda kwa mwamuzi, hapo njiani fanya bidii kupatanishwa naye, asije akakuburuta mpaka mbele ya kadhi; yule kadhi akakutia mikononi mwake mwenye kulipiza, na yule mwenye kulipiza akakutupa gerezani.
59 Nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho”
Hayo maneno yalizungumzwa na Bwana Yesu mwenyewe. Na kama ukiyatafakari kwa makini utagundua kuwa Bwana anaonyesha hatua za mtu ambaye ni Mdhulumuji, na hataki kukiri dhuluma zake, na kuzidi kujihesabia haki (au kwa lugha nyepesi yule mtu ambaye hataki kuacha njia zake mbaya), kama ni mwizi au tapeli, anatapeli leo na kesho anarudia inakuwa kama ni tabia yake, yeye kazi yake ni kusababisha wengine walie tu na kuhuzunika kila siku.
Sasa Bwana Yesu anasema mtu wa namna hiyo akiri makosa yake mapema, aachane na hiyo kazi ya utapeli aiache(maana yake apatane na jamii yake, mapema) kabla hajashikwa na kupandishwa mahakamani na kuhukumiwa… Hapo Bwana Yesu anamalizia kwa kusema “NAKUAMBİA, HUTOKİ HUMO KAMWE HATA UİSHE KULİPA SENTİ YA MWİSHO” Ukisoma Mathayo 5:26 inasema … “ Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.”…. Neno Amin amini, maana yake ni Hakika!!… hakika!!
Sasa unaweza kujiuliza kwanini Bwana aseme maneno hayo?..Hakika hakika!! Hutoki huko.
Ni kwasababu anataka kuonyesha kuwa Mahakama na Vyombo vya dola vimepewa mamlaka makubwa ya kutawala kutoka mbinguni.. Ukitiwa mikononi mwa polisi kwa kosa lolote ambalo ni halali umelitenda ni sawa kabisa na umetiwa mikononi mwa Mungu mwenyewe kwaajili ya adhabu..
Hivyo kwa lugha rahisi kabisa tunaweza kusema polisi ni kiboko cha Mungu..
Warumi 13: 1 “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.
2 Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu.
3 Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake;
4 kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu.
5 Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri”
Kwahiyo basi kama umemwona mtu ni tapeli na anatapeli watu, na kuwafanya waumie..mwitie Polisi, hufanyi dhambi, atakwenda polisi na hatatoka huko!! Mpaka ameiva vizuri!!..Lakini kama akikiri njia yake mapema na kuiacha, hapo amepatana na wewe na jamii yote, hivyo umwache usifanye lolote, wala usimpeleke polisi. Na pia kama ni kibaka kakuibia, hapo hapo na ukamshika na akatubu mbele yako kwa kuomba radhi kabisa msamehe, usimripoti..
Lakini kama mtu ni muuaji, au jambazi.. mripoti polisi (hufanyi dhambi)...Lakini kama alikuwa ni muuaji miaka ya zamani na sasa kashabadilika ni mtu mwema na hata pengine kashaokoka, huna haja ya kuchimbua makosa yake ya zamani na kuyapeleka polisi.
Vivyo hivyo kama ni mbakaji, au ni mtu wa dhuluma, au ni mtu asiyefaa kitabia katika jamii, anayefanya mambo maovu kwa makusudi na huku anajua kabisa anayoyafanya sio sawa na anandelea kuyafanya, pamoja na kuonywa mara nyingi..Mtu huyo mripoti polisi utakuwa hujafanya dhambi na zaidi ya yote utakuwa umefanya jambo jema.
Vivyo hivyo kama umedhulumiwa mali zako na yule mdhulumuji unaona ni mtu aliyejizoeza kuyafanya hayo, na ameshawafanyia wengi, na anazidi kuwafanyia wengine..maana yake huyo kashaonywa mara nyingi lakini kashupaza shingo, mtu wa namna hiyo mpeleke mahakamani, utakuwa umesaidia asiendelee kufanya hivyo kwa watu wengine, na kusababisha huzuni na majonzi kwa watu wengine. Utakuwa hujafanya dhambi. Lakini kumbuka hatuzungumzii suala la kujichukulia sheria mkononi, kwamba ameiba sasa unampiga, au ameua sasa na wewe unatafuta kumuua.. Hapana! Ukifanya hivyo utakuwa unatenda dhambi…Kwasababu biblia hapo juu inasema Mamlaka ndio zimepewa ruhusa za kutoa hukumu, na Mungu mwenyewe, na si wewe wala mimi.
Na mambo mengine yoyote ambayo unaona kuna mtu au watu wanayafanya ambayo yanaleta au yataleta madhara makubwa sana katika jamii, na kuifanya jamii iharibike, au watu kupoteza maisha..Ripoti polisi, kwasababu vyombo hivyo pia vinatimiza kusudi la Mungu duniani.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
About the author