MAUAJI YA HALAIKI NDANI YA KANISA.

MAUAJI YA HALAIKI NDANI YA KANISA.

Mwaka 1994 kulizuka vita mbaya ya kikabila huko nchini Rwanda, Vita hivyo vilidumu kwa miezi mitatu tu, lakini maafa yaliyotokea, yalizidi hata vita zilizopiganwa kwa miaka mingi katika mataifa mengine. Ni heri vifo vingekuwa vya kupigwa bunduki tu basi, lakini watu walikuwa wakiuliwa kinyama wakichinjana na wengine kuchomwa moto makanisani, mpaka leo dunia haiwezi kusahau yaliyotokea Rwanda wakati ule.

Ilikuwa ni vita vya makabila mawili tu, lakini mapambano yake yalitisha sana, kwani ndani ya muda huo mfupi watu zaidi ya laki nane waliuliwa. Hiyo inatukumbusha mauaji mengine kama haya, katika biblia,. Na yenyewe yalikuwa ni kati ya pande mbili, watu wa taifa moja. Na hao si wengine zaidi ya Yuda na Israeli.

Ilifika wakati Hawakuwezi kukaa tena pamoja, na hiyo ni kwasababu  hawakujua chanzo cha tatizo lao ni nini, mpaka wakaanza kupigana, hatujui vita hiyo ilichukua siku ngapi, pengine moja, au mbili tu, lakini watu waliouawa siku hiyo walikuwa ni laki 5 (500,000). Jaribu kutengeneza picha taifa dogo kama mji wa Daresalaam, wanaanguka watu laki tano, si jambo la kawaida kabisa, hayo ni zaidi ya mauaji ya halaiki. Katika biblia nzima hakujawahi kutokea Israeli kuwaua hata maadui zao kwa idadi kubwa kama hiyo waliouana wao kwa wao. Walikuwa na maadui wakubwa kama vile wafilisti, lakini hawakuwahi kuwaua kwa idadi kubwa namna hiyo.

2Nyakati 13:15 “Ndipo wakapiga kelele watu wa Yuda; ikawa, watu na Yuda walipopiga kelele, Mungu akampiga Yeroboamu na Israeli wote mbele ya Abiya na Yuda.

16 Wana wa Israeli wakakimbia mbele ya Yuda; naye Mungu akawaua mikononi mwao.

17 Abiya na watu wake wakawapiga mapigo makuu; hata wakaanguka wameuawa wa Israeli mia tano elfu, watu wateule.

18 Ndivyo walivyotiishwa wana wa Israeli wakati ule, wakashinda wana wa Yuda, kwa kuwa walimtegemea Bwana, Mungu wa baba zao.

19 Abiya akamfuata Yeroboamu,”

Hiyo ni kuonyesha kuwa vita vya ndani huwa ni vibaya zaidi kuliko vita vingine vyote. Na haviwi rahisi kuvizima, vinapoa tu muda lakini baadaye tena vitanyanyuka, kama ilivyokuwa kwa Israeli huo ni mfano wa vita moja tu, vilipita vita nyingine nyingi na zote zilileta maafa mengi, utadhani lile sio taifa la Mungu.

Tunaweza kudhani vita hivi havipo sasa..

Kumbuka Israeli ni kivuli cha kanisa la rohoni linaloendelea sasa hivi. Leo hii duniani kuna madhehebu zaidi ya 30,000 na yote yanadai kuwa ni ya Ki-kristo.  Hivyo ni sawa na kusema wote ni Taifa la Israeli, isipokuwa makabila tofauti tofuati. Lakini hatujui kuwa hiyo ni dalili mbaya sana. Hadi sasa tulipofikia vita za kidhehebu zimerindima, mauaji ya kiroho yanayoendelea katikati ya watu wanaomwamini Kristo, siku baada ya siku tena yanaongeza kwa idadi kubwa sana. Huyu anapigana na huyu, na yule anapigana na huyu..Mwisho wake ni nini,?

Lazima tujue Israeli iligawanyika kwasababu gani..Iligawanyika kwa sababu moja tu ya Sulemani, kuacha kuenenda katika njia za Mungu na kuenda kuitolea miungu mingine sadaka, lakini wakati huo huo, ndani yake kulikuwa na ahadi za Mungu ambazo alimuahidi baba yake, hivyo ili Mungu kutimiza haki yote ya ahadi na adhabu, ndipo akaugawanya ufalme wake na kumpa mtu mwingine, na wakati huo huo akamwachia ufalme kidogo kwa ajili ya Daudi baba yake. (1Wafalme 11:9-14) Huo ndio ulikuwa mwanzo wa Israeli kugawanyika. Lakini kama waisraeli baada ya pale wangetaka kumrudia Mungu wao, ni wazi kuwa Mungu angeurejesha ufalme kwa uzao mmoja wa Daudi na Israeli yote ingekuwa kitu kimoja.

Vivyo hivyo leo hii ni kwanini Kanisa la Kristo limegawanyika? Ni kwasababu tunaye Kristo ndani yetu, na wakati huo huo tunaabudu mambo mengine, Mungu ametuadhibu kwa kutugawanya kama ilivyo leo hii. Na matokeo ya kugawanyika ni vita. Vita hizi zitaendelea kama hatutarudi kwenye misingi ya Neno, kama hatutajua kosa letu ni nini, tutauana sana,  biblia inasema hivyo..

Bwana alisema..

Yohana 16:2 “Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada”.

Imefikia hatua badala mtu akuelekeze kwa Kristo anakuelekeza kwenye dini yake, ili ujenge chuki na wale wengine wasio wa dhehebu lao, ukristo umehama sasa kutoka katika kuelekeza mapambano dhidi ya adui wa nje (shetani) hadi kujikita katika mapambano ya sisi kwa sisi. Kilichojaa ndani yetu ni udhehebu na udini, tukidhani hivyo ndivyo vinavyompendeza Mungu.

Bwana anasema, tutokea huko, tumrudie yeye.

Ufunuo 18:4 “Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake”.

Ondoka kwenye kamba hizi kamba za kidhehebu, ndugu yangu. Shikamana na Kristo kwa wakati huu uliobakiwa nao hapa duniani, hakikisha huyo ndiye anayekaa katika moyo wako kuliko jambo lingine lolote.

Bwana akabariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Chuo cha vita vya Bwana ni kipi?(Hesabu 21:14)

NAYE AKASIMAMA JUU YA MCHANGA WA BAHARI.

Nini maana ya Dirii, Chepeo na Utayari?

NAMNA YA KUITAMBUA SAUTI YA MUNGU INAPOZUNGUMZA NA WEWE

SI MAPEPO YOTE NI YA KULIPUKA.

THAWABU YA UAMINIFU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments