Wakati ule Bwana Yesu anafufuka, utaona, lipo kundi la watu alilitokea akiwa kule kule Yerusalemu, lakini lipo kundi lingine alilipa masharti ni wapi atakapokutana nalo.
Kwa mfano Yesu wale watu wawili waliokuwa wanakwenda kwenye Kijiji kimoja kilichoitwa Emau, karibu na Yerusalemu, Kristo aliwatokea huko huko (Luka 24:13-33). utaona pia aliwatokea wale wanawake waliokwenda Kaburini siku ile ya kwanza ya juma alipofufuka, akazungumza nao, kisha akaondoka.
Lakini hakuwatokea mitume wake 11 hata mmoja akiwa huko Yerusalemu, badala yake, aliwaagiza wale wanawake, kuwa wakawaambie, Bwana amesema atawatangulia kwenda Galilaya ndipo watakapomuona.
Mathayo 28:9 “Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Wakakaribia wakamshika miguu, wakamsujudia.
10 Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie NDUGU ZANGU waende Galilaya, ndiko watakakoniona”.
Unaweza kujiuliza ni kwanini awape masharti ya mahali pa kukutana nao, Kumbuka pia hata kabla ya Yesu kufa, aliwaambia pia wanafunzi wake maneno hayo hayo, utasoma hilo katika
Marko 14:27 “Yesu akawaambia, Mtakunguwazwa ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika.
28 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya”.
Kwahiyo hilo halikuwa agizo la kila mtu bali lilikuwa mahususi kwa baadhi ya watu wale ambao aliwaita “NDUGU ZAKE”,tofauti na wale wengine, Na ukisoma pale vizuri utagundua kuwa haikuwa mahali popote tu kule Galilaya, hapana bali Bwana Yesu aliwapa na eneo husika kabisa watakalomwonea, nalo lilikuwa katika ule mlima aliowaelekeza.
Ndipo ukisoma pale utaona baada ya Bwana Yesu kufufuka wakafunga safari kweli, kutoka Yerusalemu, mpaka Galilaya, umbali wa kama KM 120, hivi, , wakaenda moja kwa moja mpaka kwenye huo mlima aliowaagiza, ndipo wakakutana naye uso kwa uso na kuwapa maagizo;
Mathayo 28:16 “Na wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda Galilaya mpaka mlima ule aliowaagiza Yesu.
17 Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao waliona shaka.
18 Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.
19 Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;
20 na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari”.
Sasa unaweza ukajiuliza ni kwanini, ajidhihirishe kwao akiwa Galilaya na sio kule Yerusalemu ,kama alivyofanya kwa wale wengine? Kulikuwa na sababu gani ya yeye kuwachosha wasafiri umbali wote ule mrefu mpaka Galilaya wakati angeweza tu kuwatokea palepale Yerusalemu na kuwapa maagizo?
Jibu ni kuwa Bwana alikuwa anataka mawazo yao kwa wakati ule yaelekee kule.
Utakumbuka kuwa Galilaya ndio mji Yesu alikolelewa, mpaka anaanza huduma, yaani kwa ufupi ni kuwa sehemu kubwa ya Huduma yake aliifanya akiwa Galilaya, hata mitume wake wote aliwaitia huko, ishara nyingi na miujiza yake mingi aliifanya Galilaya, ni sehemu ndogo sana ya huduma yake aliifanya akiwa Yerusalemu.
Hivyo Kristo kuwaambia mitume wake ninawatangulia Galilaya ni kuwaonyesha kuwa Moyo wake, baada ya kufufuka kwake haukuwa tena Yerusalemu kwa mitume wake.. Hakutaka wamwone kwa jicho ya Yerusalemu, kama wale wengine bali kwa jicho la Galilaya, kule alipotumikia muda wake wote akiifanya kazi ya Mungu.
Huko ndipo alipowaambia enendeni ulimwenguni kote mkawafanya mataifa kuwa wanafunzi, kama mimi nilivyokuwa ninawafanya huku Galilaya, nami nitakuwa pamoja nanyi mpaka ukamilifu wa dahari.
Nini Kristo alitaka tufahamu katika habari hiyo.?
Ni kuwa hata sasa, ikiwa wewe ni mwanafunzi wa Yesu, au unataka uwe mwanafunzi wa Yesu kweli, basi fahamu kuwa hutamwona Kristo Yerusalemu, aliposulibiwa, hutamwona Kristo katika mafundisho ya msalaba tu kila siku, mafundisho ya kuamini, au ya vitubio, yaani kama wewe miaka nenda rudi, hujui kingine Yesu anachokitaka kwetu zaidi ya kutubu na kuokoka, basi, wewe bado upo Yerusalemu.
Kristo anataka uitazame na kazi yake pia, anataka uone alivyofanya yeye akiwa duniani na wewe ukafanye vivyo hivyo, anataka uone kuwa kuna watu wanahitaji kuhubiriwa Injili, kuna watu wanahitaji kupata wokovu, kufunguliwa, kuwekwa huru kutoka katika dhambi na vifungo mbalimbali, hicho ndicho Kristo anataka uone kwa wakati wa sasa. Hiyo ndio Galilaya yako unapopaswa uende ukakutane na Yesu.
Lakini kama wewe ni wa kusikia tu injili, na kusema AMEN, au kusema mimi nimeokoka, basi, huna cha Ziada, ujue kuwa wewe si “NDUGU” yake Kristo, Wewe si “MWANAFUNZI WAKE”. Huwezi kumfurahisisha kwa lolote.
Nyakati hizi tunazoishi ni nyakati ambazo, zilitabiriwa kuwa kutakuwa na njaa mbaya sana, sio ile njaa ya kukosa chakula, bali ni ile ya kukosa kuyasikia maneno ya Mungu, Nabii Amosi alionyeshwa hilo
Amosi 8:11 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana”.
Jiulize kwa upande wako, tangu Kristo amefufuka ndani yako, ni kazi gani ya ziada umeifanya kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Bado upo Yerusalemu tu, Galilaya hutaki kwenda..Upo buzy na kazi zako, upo buzy na shughuli za kidunia, upo buzy na familia yako, Galilaya kwako ni mbali sana, kule hakuna pesa, hakuna kujulikana, utaonekana mshamba, utadharauliwa, utachekwa,
Ndugu jitathmini ukristo wako ikiwa hata unaona ugumu kuichangia kazi ya injili, unategemea vipi utaweza kuwahubiria wengine habari za ufalme wa mbinguni, hata hicho kitakushinda tu, Na taji lako litakuwa hafifu, au usipokee kabisa taji huko unapokwenda!
Tuamke sote, tuanze kuwagawia na wengine kile Bwana alichotugawia sisi, katika kipindi hiki cha njaa cha siku za mwisho.
Maran atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
RABI, UNAKAA WAPI?
NI SAA KUMI NA MBILI (12) TU, ZA KRISTO KWAKO.
KURUDI ISRAELI KWASASA NI KUGUMU, SIO KAMA KULE MWANZONI.
Bahari mbalimbali zilizoorodheshwa kwenye biblia.
OLE WAKO KORAZINI NA BETHSAIDA.
About the author