LEO WOKOVU UMEFIKA NYUMBANI HUMU

LEO WOKOVU UMEFIKA NYUMBANI HUMU

Je! Wokovu umekufikia?

Wengi wanasema wamepata wokovu lakini kiuhalisia wokovu bado haujawafikia.
Leo napenda tujifunze juu ya viashiria vinavyorhibitisha kuwa wokovu umetufikia, au umefika nyumbani kwetu.

Tusome habari za mtu mmoja aliyeitwa Zakayo, ambaye kupitia yeye tutajua kama wokovu na sisi umefika nyumbani kwetu au la!

Luka 19:1-10
“1 Naye alipoingia Yeriko alipita katikati yake.

2 Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri.

3 Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo.

4 Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile.

5 Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako.

6 Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha.

7 Hata watu walipoona, walinung’unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi.

8 Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.

9 Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.

10 Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea”.

Nataka tuuone huo mstari wa 8, ni kitu gani Zakayo alichokifanya kikamsababisha mpaka Mwokozi Yesu aseme.. “Leo Wokovu umefika nyumbani humu”

Na kitu chenyewe ndicho hicho tunachokisoma..huo mstari wa 8.

“8 Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.”

Umeona?..Zakayo alijiona yeye ni mwenye dhambi, na kutubu…lakini aliona toba ya midomo peke yake haitoshi, na ilihali mali nyingi alizonazo ni kutokana na kuwadhulumu watu..akaona aib mbele za Bwana na vile vile moyo wake ukamchoma.
Alichofanya alitoa nusu ya mali yake yote iliyo ya halali na kuwapa masikini, na zaidi ya yote, wale wote aliowadhulumu aliwarudishia mara 4,.

Maana yake ni kwamba kama kuna kiwanja alimdhulumu mtu, alimrudishia mara 4, maana yake viwanja 4..

Kama kuna fedha alimdhulumu mtu, alimrudishia mara 4..

Na huo moyo wa toba yenye matendo ndio Bwana aliokuwa anauhitaji.. Na Bwana ndio akamwambia maneno yale “Leo wokovu umefika nyumbani humu”

Hebu jiulize leo ndugu, tangu umempokea Yesu, vile vitu vya wizi ulivyoiba, umemrudishia mwenyewe?..au umetubu tu kwa mdomo na kuishia hapo, na kuendelea kuwa navyo?

Zile mali za dhuluma ulizozipata bado unafurahia kukaa nazo baada ya kuokoka?..Zakayo hakuona vyema kukaa nazo, aliona aibu mbele za Bwana na alipoziondoa na ndipo Wokovu ulipoingia nyumbani mwake.

Sisi tunaonaje raha kubakiwa na simu za wizi?, Kubakiwa na fedha za dhuluma, kubakiwa na heshima wa hila n.k
Bwana wetu hafurahiwi na toba za midomo tu!..bali na za matendo,

Tunapotubu ni lazima na maisha yetu yabadilike, hata watu wa nje waone kweli pale pana mtu aliyebadilika, watu wa nje hawashawishiki kwa maneno ya midomo tu, ndipo waamini kuwa tumebadilika..wanashawishika wanapoona umewarudishia vile ulivyowadhulumu.

Kadhalika hawatashawishika kusikia kuwa umetubu kwa mdomo huku mavazi yako na mwonekano wako ni bado ule ule wa kikahaba au kihuni.

Wakikuona bado unavaa nguo za kubana, bado unavaa vimini, bado unajipamba uso kama Yezebeli, haijalishi unahudhuria kanisani kila siku kiasi gani..bado watakuona wewe ni kahaba na muhuni tu.

Wakisikia umetubu lakini bado huyo mke uliye naye si wako ni wa mtu mwingine, huyo mume uliye naye si wako ni wa mtu mwingine, hawashawishiki hata kidogo..na zaidi ya yote Kristo hakujui.

Tunapotubu hatuna budi kuzaa matunda yanayotokana na toba zetu hizo..

Mathayo 3:8-10
“ 8 Basi zaeni matunda yapasayo toba;

9 wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto.

10 Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni”.

Je! Toba yako ina matunda?

Kama bado basi ni wakati wa kuanza upya, kama ni mwanamke baada ya kutubu weka mbali vipodozi vyote, kaa mbali na dhuluma na biashara haramu..na kama ni mwanamume ni hivyo hivyo, kuviondoa vyote ulivyovipata kwa dhuluma na kujitenga na udunia.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.

Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

KUONGOZWA SALA YA TOBA

MAOMBI YA TOBA.

Sala ya Toba na Rehema.

Ni lazima mtu aongozwe sala ya toba ili awe ameokoka?

NGUVU YA MSAMAHA

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

Amen Amen

Fried-rich@son ofJESUS%
Fried-rich@son ofJESUS%
3 years ago

Amina mtumishi kama 2nafanya uasherati, uongo, masturbation practice, kutaza x(porn graphic photo&video) n.k. Inatupasa tufumbue macho leo na tuachane nayo kabsa!
Ubarikiwe sana mtumwa wa BWANA!