Pamoja na mengi tunayoweza kujifunza kwa Mariamu mama yake Yesu..lakini pia yapo mengi ya kujifunza kwa Yusufu Babaye Yesu. Leo kwa Neema za Bwana tutajifunza tabia moja ya Yusufu ambayo katika hiyo itatusaidia nasi kujifunza kumpendeza Mungu.
Mathayo 1:19 “Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri.
20 Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
21 Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao”.
Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa Yusufu hakuwa baba wa damu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kama tunavyofahamu Mimba ya Bwana Yesu ilitungwa kimiujiza (kwa uweza wa Roho Mtakatifu)..hakukuhusisha Baba wa kimwili. Hivyo Bwana wetu Yesu Kristo hakuwa na baba wa kimwili.
Lakini pamoja na hayo tunajifunza tabia moja ya Yusufu ambaye alimkubali kama mwanawe wa kimwili. Na tabia hiyo sio nyingine Zaidi ya kuwa na HAKI..Mtu mwenye haki anakuwa anaonekana kuwa na haki mbele za Mungu, kadhalika anakuwa na haki mbele za Watu na pia anakuwa mwenye kutenda haki.
Hivyo kipindi fulani alimposa huyu mwanamke Mariamu..na akiwa katika hatua za kumwoa ghafla akamwona anaujauzito…Ni wazi kuwa Mariamu hakumwambia siku ile ya kwanza Malaika Gabrieli alipomtokea…aliificha siri ile, akiwaza pengine itakuwaje siku Yusufu akifahamu jambo hilo…Na mimba ikaendelea kukua mpaka ikafika kipindi ikaanza kuonekana kwa macho..na Yusufu akaiona.
Ilikuwa ni kipindi kigumu sana kwa Mariamu…akiwaza endapo Yusufu akimkataa itakuwaje!..jamii itamwelewaje?..Ni nani atakayeamini eti kwamba kapata mimba bila kukutana na mwanamume?..Ni wazi kuwa hakuna ambaye angemwelewa…Hivyo ni mawazo juu ya mawazo. (Ndugu kubeba kusudi la Mungu si jambo ambalo ni la kueleweka, wala si jambo la kupata heshima..lina gharama zake kubwa). Mariamu akiwa katika hali hiyo pengine alisema litakalo kuwa na liwe…Mimi nitamtegemea Bwana. (Hivyo ilihitaji Imani kubwa sana, kuitunza ile mimba isiyokuwa na Baba..haikuwa jambo jepesi). Leo tu hebu mwanamke apate mimba katika mazingira yasiyoeleweka eleweka ya uzinzi uone kama hatakwenda kuitoa…lakini haikuwa hivyo kwa Mariamu.
Baada ya Yusufu kugundua ile mimba…hata hakumuuliza Mariamu akaazimu kumwacha kwa siri…kwasababu alijua tayari kashakutana na mwanamume…Lakini katika ndoto Malaika akamwambia asimwache mkewe kwasababu mimba ile haikupatikana kwa uasherati bali kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Malaika yule katika ndoto akamtajia na jina la mtoto…Na alipokwenda kumuuliza pengine Mariamu na yeye akamuhadithia vile vile na jina la mtoto ni lile lile, hivyo hiyo ikawa ni uthibitisho wa kwamba mtoto yule ni wa kipekee katoka kwa Mungu..
Sasa hawa wawili Mariamu na Yusufu, mumewe wameshalitatua tatizo (wote wamekubali kuwa mimba ile ni ya kimiujiza)…Sasa Vipi kuhusu watu wa nje watawaelewaje?…Je! Yusufu atoke tu na kwenda kutangaza nje huko kuwa mke wangu kapata mimba kimiujiza?..si ataonekana mwendawazimu kwa watu wa kizazi alichopo?..nani atamuamini?….zaidi sana atamsababishia mke wake matatizo hata ya kupigwa kwa mawe kwa kosa la uzinzi…kwasababu watamhoji katolea wapi ile mimba?..Hivyo hapo inahitajika hekima nyingine ya ziada.
Na hekima hiyo si nyingine Zaidi ya kukubali tu kuchukua mashutumu…Yusufu ikambidi akubali kwamba yule ni mtoto wake kabisa….kwa namna nyingine tunaweza kusema “akakubali aonekane na watu kuwa alikutana na Mariamu kipindi kabla hawajaoana, na kwamba ile mimba ni ya kwake”..Alifanya hivyo kuzuia kumwaga lulu zake mbele za nguruwe…kama Bwana Yesu alivyokuja kusema huko mbeleni.
Mathayo 7: 6 “Msiwape mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua”.
Hivyo pengine kama Yusufu kutukanwa basi alitukanwa…kama kudharauliwa alidharauliwa, kama kuonekana ni mtu mwenye tamaa alionekana hivyo…Watu wote wakaona ni mtu tu mwenye tamaa kwanini asingesubiri wafunge ndoa ndipo amkaribie mkewe?..walionekana yeye na mkewe Mariamu wote ni waasherati, na huyo mtoto atakayezaliwa atakuwa kazaliwa katika zinaa… Na mambo mengine mengi…
Leo hii wengi wanapenda Bwana Yesu aje katika Maisha yao…lakini wanazikimbia gharama za kumpokea Yesu…(Yusufu na Mariamu hawakuzikimbia) badala yake walizikabili walisema liwalo na liwe…itakuja kujulikana baadaye ukweli ni upi…Acha leo tuonekane ni watu waovu na tusiofaa lakini siku moja tutang’aa na kutukuzwa.
Luka 6:22 “Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu.
23 Furahiwani siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni, maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo”
Ndugu kumpokea Yesu maana yake ni kukubali mashutumu, kukubali kuonekana mjinga..kukubali kudharauliwa, kukubali kuchukiwa, kukubali dhiki na wakati mwingine kudhihakiwa. Ukiona umempokea Yesu Kristo na unapendwa na watu wote katika hatua za awali basi bado hujampata.
Unapoona aibu leo kuacha kuvaa vimini, na suruali kwasababu unaogopa kuonekana mshamba..Usitegemee kamwe Mungu kutembea na wewe..Bado kusudi la Mungu halipo ndani yako..Unapokataa leo kuacha kuvaa mawigi na hereni na kupaka lipstick, wanja na kujipamba na mavipodozi…ukweli ni kwamba bado Kristo hajaingia ndani yako..upo katika njia ielekeayo upotevuni…pengine kanisani huambiwi haya, kwasababu wanahisi hivi au vile, labda utawakimbia lakini leo umeyasikia na umeyasoma…Utakwenda jehanamu ya moto usipoyaacha!!.
Usipotaka kuacha ulevi kisa tu unaogopa utaonekanaje na jamii ya walevi wenzako..fahamu kuwa Mungu hayupo na wewe kabisa, unapokataa kuacha wizi, uasherati, ufanyaji masturbation, utoaji mimba, ulaji rushwa, ulawiti, ufiraji, utukanaji, uuaji, n.k Mungu yupo mbali na wewe sana..kama ulisikia mahali wanakuambia kuwa ukiambiwa mambo hayo unahukumiwa…Leo hii isikie tena hukumu hiyo!..huko uendako unapotea!.
Mariamu na Yusufu walibaki wenyewe…wanarudi mjini kwao Bethlehemu pengine hata ndugu zao kule hawakuwa na habari nao, hata kuwatengea chumba na kuishia kwenda kupanga, na huko walikopanga hata pia hawakupata nafasi..Mfalme mkuu Yesu Kristo akazaliwa katika zizi la ng’ombe..na Huyo aliyezaliwa katika zizi la ng’ombe leo hii ndio sababu ya wokovu wetu sisi…Leo hii hata kuzaliwa kwake kwenye zizi la ng’ombe ni fahari kwetu. Haleluya!.
Je ungependa kumgeukia leo Kristo kwa moyo wako wote? Na kuacha dhambi na kukubali kubeba msalaba wako na kumfuata yeye na kuwa mwenye haki kama Yusufu?..Kumbuka tunaishi katika siku za mwisho na Kristo yupo mlangoni sana kurudi..Dakika hii tunapozungumza hayupo tena zizini..yupo mbingu za Mbingu, katika Nuru isiyoweza kukaribiwa biblia inasema hivyo katika..1Timotheo 6:14-16.
Kama upo tayari kufanya hivyo sasahivi.. basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.
EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, .
NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.
ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.
AMEN.
Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.
Fanya hayo na Bwana azidi kukubariki.
Tafadhali share na wengine, kadhalika kama utapenda kupata masomo haya kwa njia ya whatsapp,au inbox inaweza kututumia ujumbe mfupi inbox, pamoja na namba yako ya whatasapp..Vile vile tunakukaribisha kutembelea website yetu hii kwa mpangilio mzuri wa masomo haya na yaliyotangulia..
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii 0789001312
Mada Nyinginezo:
MARIAMU AKUTANA NA ELISABETI.
MARIAMU
URIMU NA THUMIMU NI NINI KATIKA BIBLIA?
JIHADHARI NA KUOSHWA MIGUU ISIVYOPASWA.
MIILI YA UTUKUFU ITAKUWAJE?
WAKAMCHA BWANA, NA KUITUMIKIA MIUNGU YAO WENYEWE.
WALE WAZEE ISHIRINI NA WANNE (24), WANA KAZI GANI?
MTU ASIYE PAMOJA NAMI YU KINYUME CHANGU.
About the author