Mungu anapompa mtu kazi ya kufanya, na mtu yule akawa na hofu na maadui wa Imani yake au akawa anakawia kawia basi nafasi yake anapewa mtu mwingine…Moja ya sababu kati ya nyingi inayompelekea mtu kupoteza nafasi yake ya utumishi ni HOFU.
Hofu ya kuwaogopa maadui wa Imani yako, hofu ya kuogopa endapo ukihubiri kinyume na mifumo ya adui shetani itakuwaje?..endapo ukiziharibu na kuzidhihirisha kazi za shetani itakuwaje?..Endapo nikizitukana kazi za adui, kama Daudi alivyozitukana itakuwaje?..Nikizidhalilisha kazi za kichawi itakuwaje?..hofu ya kwenda kuhubiri vijijini kuhofia wachawi wa kule, hofu ya kutamke jina la Yesu palipo na nguvu za giza n.k…Hofu ya namna hii ina madhara makubwa sana kiroho..
Katika biblia tunajifunza mtu mmoja aliyeitwa Eliya, ambaye alipewa jukumu la kuisafisha Israeli na kumwondoa mungu baali katikati ya Taifa la Mungu, lakini mwisho wa siku akaingiwa na hofu..na kulikimbia kusudi..
Kama ni mwanafunzi wa biblia, utakuwa unaielewa vyema Habari ya Nabii Eliya jinsi alivyowaua wale makuhani 450 wa Baali na 400 wa Ashera jumla yao 850 (1Wafalme 18:16-40)..Idadi hii ilikuwa ni kubwa sana Eliya aliyoiua ambayo ikasababisha upungufu mkubwa wa makuhani wa Baali katika nchi ya Israeli, hivyo kupelekea kiwango kikubwa cha Uovu kupunguzwa Israeli…Kwani makuhani hao waliajiriwa na mwanamke Yezebeli kutoka huko Lebanoni kuja kuingiza miungu migeni katika Taifa Takatifu la Mungu..
Kwani makuhani hao wa Baali walikuwa wanafanya uchawi na kuipotosha Israeli nzima…Hata wakati wanashindana na Nabii Eliya kushusha moto juu ya ile sadaka, sio kwamba hawakuwa na huo uwezo..huo uwezo wa kutengeneza moto wa kimiujiza ulikuwa ni uchawi mdogo sana kwao, ndio maana walikuwa na ujasiri wa kukubali changamoto ile na Eliya….lakini kwasababu hakuna uchawi wowote ambao unaweza kuwa na nguvu mbele ya Nguvu za Mungu aliye hai, ndio maana ghafla walijikuta wameshindwa kutengeneza moto wao wa kichawi juu ya ile sadaka siku ile…
jambo ambalo hapo kabla halikuwa jambo gumu kwao kulifanya.
Hivyo walikuwa ni wachawi ambao waliajiriwa na mwanamke Yezebeli ambaye ndiye aliyekuwa malkia wa Israeli wakati huo..(2Wafalme 9:22)… Lakini Eliya pamoja na kuipunguza idadi hiyo yote ya wachawi juu ya Israeli, bado hawakuisha wote…wapo wengine ambao walikuwa wapo mbali…na wengine walibaki Samaria …na Zaidi ya yote hata Yezebeli mwenyewe ambaye alikuwa amewaajiri, alikuwa bado yupo hai…
Hivyo Eliya japokuwa alipunguza machukizo juu ya Israeli kwa sehemu kubwa..lakini bado alikuwa hajautoa ule mzizi wote. Na Mungu alimkusudia yeye ndiye autoe mzizi wote na aisafishe Israeli yote lakini kwasababu ya vitisho vya Yezebeli kuutoa uhai wake alimwogopa na kumkimbia kunusuru uhai wake.…Eliya akakimbia mpaka Herobu kwa hofu ya Yezebeli na kumwomba Mungu autoe uhai wake….Hivyo kwa hofu alimwomba Mungu aikatishe hudama yake…Na Mungu aliitoa Huduma hiyo na kuwapa watu wengine watatu waimalizie ambao ni HAZAELI, ELISHA na YEHU.
1Wafalme 19:15 “Bwana akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu.
16 Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa AbelMehola mtie mafuta awe nabii mahali pako.
17 Na itakuwa atakayeokoka na upanga wa Hazaeli, Yehu atamwua; na atakayeokoka na upanga wa Yehu, Elisha atamwua”.
Sasa Neno la Mungu ni lazima litimie kwa mkono wa Hazaeli na Elisha na Yehu..kwamba uovu wa baali na makuhani wake na waanzilishi wake waondolewe Israeli kwa mikono ya hawa watatu…Sasa Habari za mambo aliyoyafanya Elisha na Hazaeli zipo katika maandiko…Lakini leo nataka tumtazame huyu mtu wa mwisho anayeitwa YEHU, jinsi gani alilimaliza kusudi la Mungu vizuri.
Yehu, alitiwa Mafuta na Eliya mwenyewe awe mfalme juu ya Israeli…ingawa hakuwa mkamilifu sana, lakini Mungu alimpa ujasiri mkuu kuliko wa Eliya…pale ambapo Eliya alimwogopa Yezebeli na kumkimbia huyu Yehu alimfuata Yezebeli kwenye jumba lake la kifalme na kumtoa kwenye umalkia ili auawe…na sio hilo tu!…bali aliwaua manabii wote wa Baali ambao walikuwa wamesalia kwa siku moja Zaidi hata ya ile idadi ya Eliya aliyoiua kule Karmeli. Na akamtoa mungu anayeitwa baali katika Taifa la Israeli, na baada ya hapo, wana wa Israeli hawakuabudu tena baali..
2Wafalme 10:18 “Yehu akawakusanya watu wote, akawaambia, Ahabu alimtumikia Baali kidogo; bali Yehu atamtumikia sana.
19 Basi niitieni manabii wote wa Baali, wote wamwabuduo, na makuhani wake wote; mtu asikose kuwapo hata mmoja. Maana ninayo dhabihu kubwa ya kumtolea Baali; ye yote atakayekosa kuwapo hataishi. Lakini Yehu alifanya hayo kwa hila, ili awaharibu waliomwabudu Baali.
20 Yehu akasema, Takaseni kusanyiko la dini kwa Baali. Wakalitangaza.
21 Yehu akatuma wajumbe katika Israeli yote, nao wote waliomwabudu Baali wakaja, wala hakusalia mtu ye yote asiyekuja. Wakaingia nyumbani mwa Baali; ikajaa nyumba ya Baali tangu mlango hata mlango.
22 Akamwambia yule aliyekuwa juu ya hazina ya mavazi, Uwatolee mavazi wote wanaomwabudu Baali. Akawatolea mavazi.
23 Akaingia Yehu na Yehonadabu mwana wa Rekabu nyumbani mwa Baali, akawaambia waliomwabudu Baali, Tafuteni mkaangalie, asiwepo hapa pamoja nanyi mtu amtumikiaye Bwana, ila wamwabuduo Baali peke yao.
24 Wakaingia ili watoe dhabihu na sadaka za kuteketezwa. Basi Yehu alikuwa amejiwekea nje watu themanini, akasema, Mtu mmoja akiokoka wa watu niliowatia mikononi mwenu, amwachaye huyo, roho yake itakuwa badala ya roho yake.
25 Ikawa mara alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa, Yehu akawaambia walinzi na maakida, Ingieni mwapige; mtu awaye yote asitoke. Basi wakawapiga kwa makali ya upanga; walinzi na maakida wakawatupa nje, wakaenda mpaka mji wa nyumba ya Baali.
26 Wakazitoa nguzo zilizokuwamo nyumbani mwa Baali, wakaziteketeza.
27 Wakaibomoa nguzo ya Baali, na kuiangusha nyumba ya Baali, wakaifanya choo hata leo.
28 NDIVYO YEHU ALIVYOMHARIBU BAALI KATIKA ISRAELI”
Sasa katika Habari hiyo tunajifunza ni kwamba..kama sio Nabii Eliya kumwogopa Yezebeli, Mungu angelimaliza kusudi lote mkononi mwake,…kwasababu huyo Yezebeli ambaye alikuwa anamwogopa Yehu alikuja kumuua kirahisi sana, wala hata hakutumia upanga wala silaha kumuua…aliwaambia tu watu wamkamate wamtupe dirishani..hivyo tu!..(2wafalme 9:30-35).
Na sisi hatupaswi kumwogopa Adui shetani na vitisho vyake, katika kulitimiza kusudi la Mungu..Maadui wa Imani yetu ni wengi, na wana vitisho vikali…lakini hatupaswi kusikiliza vitisho vyao…
Haihitaji mapanga na marungu kumwangusha Yezebeli…ni amri tu! Kama Yehu alivyofanya…Na sisi haihitaji majeshi wala michanganyiko mingi kumwondoa Adui shetani mbele yetu..bali inahitajika amri tu!..Unatamka na Yezebeli anakwenda chini..
Hivyo usiogope mganga mtaani kwako, usiogope wachawi vijijini kwako, usiogope mwanasiasa mbele yako, usiogope chochote kijiitacho kikuu mbele yako ambacho kinakutishia Imani yako au huduma yako..wewe litazame kusudi la Mungu tu kulitimiza na kulimaliza.
Zekaria 4:6 “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi”..
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
NENO LA MUNGU NI DAWA ILIYO TOFAUTI NA DAWA NYINGINE.
NENO LA MUNGU NI TAA
NITAFUNGUAJE MILANGO ILIYOFUNGWA MBELE YANGU?
MAPAMBANO DHIDI YA SHETANI.
NAO WAKADHANI YA KUWA YUMO KATIKA MSAFARA;
UCHAWI WA BALAAMU.
KIFO CHA MTAKATIFU PERPETUA NA FELISTA.
About the author