1Wakorintho 1:26 “Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa;”
Kwanini Mtume Paulo, alisisitiza kwamba tuangalie sana mwito wetu? Ni Kwasababu kwenye mwito ndipo watu wengi, tunapokosa shabaha, tukidhani Mungu anahitaji kwanza ujuzi fulani, au ukubwa fulani ndipo atuite tumtumikie, au tunadhani wale wenye vyeo vikubwa ndio hao Mungu anawatumia sana katika kazi yake.
Wito wa Mungu, ni tofauti na wito wa kibinadamu, Mungu akikuita, jambo la kwanza analolifanya kwako ni kukufagia kwanza, ikiwa wewe ni mtu mwenye ujuzi, au cheo fulani, au elimu fulani kubwa, ni anaondoa kwanza huo ujuzi wako kwake, anakufanya kuwa si kitu chochote, ndipo sasa akutumie, vinginevyo ukienda na cheo chako kwake, ukadhani hicho ndicho kitakachomshawishi yeye atembee na wewe, ujue kuwa umepotea.
Tumtazame, Musa, yeye alikuwa mrithi wa Farao, alikuwa anayo elimu kubwa ambayo hakuna asiyejua hilo , Biblia inatuambia Musa alifundishwa hekima yote ya ki-Misri na alikuwa pia ni mjuzi wa kipekee sana katika kuongea.
Warumi 7:22 “Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo”.
Na kumbuka kwa wakati ule taifa kama Misri ni sawa na Marekani ya leo, ni taifa lililokuwa linashikilia uchumi wa ulimwengu mzima.
Lakini tunaona Mungu alipoanza kumvuta kwake, alikimbilia kule jangwani, na huko akawa anachunga mifugo ya mkwe wake Yethro, kwa muda mrefu sana wa miaka 40, wakati wote huo, Mungu hakujionyesha kwake, wala kujidhihirisha, unaweza ukajiuliza ni kwanini ichukue muda wote huo? hiyo yote ni Mungu alikuwa anamwondolea kwanza ule utashi wake aliokuwa anajiona anao, ule ujuzi wake, ambao hapo mwanzo alidhani pengine ndio angeutumia huo kuwaokoa wana wa Israeli, lakini ikawa ni kinyume na matazamio yake, aliendelea kukaa katika hali hiyo hiyo kwa muda wa miaka 40 mizima.
Na wakati ambapo hata ule ujuzi wake wa kuzungumza umekufa, hapo ndipo Mungu alipomwita, na ndio maana utaona alipoitwa na Mungu jambo la kwanza alimwambia kuwa yeye sio Mnenaji, yaani hana uwezo tena kwa kuzungumza siasa majukwaani, kama alivyokuwa nao kule mwanzoni,
Kutoka 4:10 “Musa akamwambia Bwana Ee Bwana, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito.
11 Bwana akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, Bwana”?
Unaona? Musa huyu huyu, biblia inatuambia alikuja kuwa MPOLE kuliko watu wote waliokuwa duniani wakati ule. Kutoka kuwa muuaji, mpaka kuwa mtu mpole sana zaidi ya watu wote, si jambo jepesi inahitaji kujishusha kwa Mungu kweli kweli.
Hesabu 12:3 “Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi.”
Mtu kama huyo ndio Mungu alitembea naye. Na kanuni za Mungu huwa hazibadiliki, akisema hivi, ndivyo ilivyo, hata sasa, Mungu hatembei na watu wanaojiona kuwa ni bora kuliko wengine, hawatumii watu wanaojiona wana elimu kubwa au washupavu kuliko wenzao, hawatumii kamwe watu wanaojiona ni vigogo kuliko wenzao, Na kama akitaka kukutumia basi jiandae kufanywa kama Musa,. Jiandae kushushwa kwanza. Vinginevyo sahau kutumiwa na Mungu.
Na ndio maana ukiendelea pale utaona anasema..
1Wakorintho 1:26 “Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa;
27 bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu;
28 tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko;
29 mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu”.
Ndivyo ilivyo watu wasiokuwa na utashi wowote ni rahisi sana wao kutumiwa na Mungu kuliko watu wenye vyeo au wenye elimu kubwa za kidunia, kwasababu hao hawana cha kujisifia mbele za Mungu. Na watu wa namna hii ndio Mungu anaowafunulia siri zake nyingi.
Luka 10:21 “Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza”.
Halikadhalika, watu wasio na elimu kubwa za theolojia ndio wanaokuwa katika nafasi kubwa ya kutumiwa na Mungu kuliko hao wengine, kwasababu hawa hawana cha kutegemea isipokuwa uongozo wa Roho Mtakatifu, lakini hao wengine watategemea elimu zao za dini ndio ziwasapoti, au ziwalinde, au ziwape heshima.
Vivyo hivyo na sisi pia tunapaswa tuutafakari sana mwito wetu, tujiulize je Mungu tumempa nafasi ya ngapi katika maisha yetu, Je! Ni kweli tumeshusha viburi vyetu na kuvua ujuzi wetu, ili kumruhusu yeye atutumie? Au tumejikweza kwake na kujiona sisi ni wa kipekee sana kisa tuna elimu, au tuna vyeo, au tuna heshima kuliko wengine.
Tuutafakari mwito wetu, ili tujue ni wapi Mungu anataka tutembee naye, na tuanze kujishusha kuanzia sasa.. Kwasababu kiburi ni adui mkubwa wa utumishi wa Mungu. Tukitaka tutumiwe na Mungu tushushe kwanza viburi vyeo, na kujiona sisi ni sawa na watu wengine wote.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mafundisho mengine:
Mada Nyinginezo:
About the author