SWALI: Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?”
JIBU: Ili tupate picha kamili tuisome habari yake kuanzia juu kidogo, kwasababu Bwana alichokisema kinategemea hiyo habari iliyokuwa juu yake…
Luka 18 :1-8
“1 Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.
2 Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu.
3 Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu.
4 Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu,
5 lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.
6 Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu.
7 Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?
8 Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani”?
Kama tunavyosoma hapo alipomaliza tu kueleza hiyo habari ya huyo mjane ndipo akaongezea na hicho kipenge mwishoni.. “walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani”? Kumaanisha kuwa siku ya kuja kwake anatazamia kuona imani yenye mfano wa huyo mwanamke, kama kigezo cha mtu kunyakuliwa.
Huyo mwanamke, hakuvunjwa moyo, pale alipoona hakuna dalili yoyote ya kutendewa haki na Yule kadhi dhalimu, lakini aliendelea hivyo hivyo tu kila siku kama kipofu, akiamini siku moja atapatiwa haki yake, na mwisho wa siku akaipata, jaribu kujiweka wewe katika mazingira kama hayo, ni wazi utakata tamaa mapema pale unapoona mtu hata haoneshi dalili ya kukusikiliza, unaweza kusema anadharau, lakini kumbe hujui moyoni mwake unamtesa sana.
Vivyo hivyo, katika nyakati hizi za mwisho, nyakati za masumbufu ya maisha, nyakati ambazo watu wengi wamekata tamaa ya kumngojea Yesu, wengine wamerudi kwenye dunia, wengine wanadhihaki wanasema huyo Yesu mnayemsubiria yupo wapi? Kama biblia inavyosema katika..
2Petro 3:3 “Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe,
4 na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa”.
Wengine watasema mnamwomba yeye ambaye hawajali..unaona?
Lakini siku atakapokuja Yesu, jambo la kwanza kama alivyosema ni kuwa ataangalia IMANI kwanza, ataaangalia wale waliokuwa na Imani kwake, ambao hawakukatishwa tamaa kuomba ufalme wake uje, (Mathayo 6:9), japokuwa alionekana kama amechelewa, watu ambao hawakuruhusu kurudi nyuma..hao ndio atakaowaangalia..Na hao ndio kitendo cha kufumba na kufumbua watatoweka duniani siku ile.
Wengine wote watabaki hapa duniani, na wale ambao walikuwa wameshakufa tayari, Jicho la Yesu nalo litatazama mpaka kule makaburini, kama mtu alikufa bila imani hiyo, atabakia pale pale makaburini, watakaofufuliwa ni wale tu ambao mpaka dakika ya mwisho ya maisha yao waliishi kama vile Yesu anarudi muda wao, hao ndio watakaosikia sauti yake mwana wa Adam una wataungana na wale walio hai kwa pamoja kwenda kwenye karama ya mwana-kondoo mbinguni.
Lakini swali ni Je! imani hiyo ipo ndani yetu au imeshakufa siku nyingi?..Jibu unalo. Tunachopaswa kufanya sasa, ni kutungeneza mahusiano yetu na Mungu vizuri katika hichi kipindi kifupi cha maisha tulichobakiwa nacho hapa duniani, tujue kalenda ya Mungu duniani sasa ni ipi?…Pale ulimwengu unapozidi kwenda mbali na Imani na kudhihaki sisi ndio tuzidi kuomba na kumlilia Mungu zaidi kama huyu mjane..
Na siku moja isiyokuwa na jina, kitendo cha kufumba na kufumbua, tutajiona pale mawingu na majeshi ya malaika wengi yamekuja kutulaki, na parapanda ya Mungu. Itakuwa ni raha isiyo na kifani, maneno ya kibinadamu hayawezi kuelezea. Hivyo tuishi kwa Imani Bwana atakapokuja aione ndani yetu.
Jina la Bwana libarikiwe Milele.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Mlima sinai upo nchi gani? Na Je unaijua Sinai yako ya rohoni?
About the author