Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima, Ni siku nyingine tena Bwana ametupa neema ya kuiona, hivyo nakukaribisha tuzidi kuyatafakari maneno ya uzima maadamu siku ya ukombozi wetu inazidi kukaribia.
Mungu anapotupa Neno la ahadi, huwa haiishii hapo tu, bali kuna majira yanafika, hizo ahadi zinatujaribu, Utamwona Yusufu pindi alipopewa maono ya kuwa utafika wakati baba yake na mama zake na ndugu zake watamwinamia, (yaani kwa ufupi atakuwa mkuu), tendo lile alidhani lingetokea tu papo kwa papo, Lakini kama tunavyojua habari mambo ndio yalikuwa kinyume na matarajio yako, kwanza aliuzwa na ndugu zake, akaenda kuwa mtumwa Misri.
Na alipofika kwenye ile nyumba ya Potifa kama mtumwa walau akaanza kuona unafuu pale alipofanywa kuwa msimamizi wa mali na kazi za bosi wake, pengine akadhani Mungu kashaanza kumkumbuka, lakini mambo yakabadilika tena baada ya kukutana na mke wa Potifa na kumsababishia apelekwe gerezani, akafungwa huko muda mrefu, tena lile gereza la wafungwa wa wafalme ambao hao hawana mdhamana, wanasubiria siku yoyote tu kuuawa.
Sasa mambo hayo yote Yusufu aliyoyapitia, hayakuletwa na shetani, bali ni Mungu aliyeruhusu ayapitie, zilikuwa ni ahadi za Bwana zikimjaribu kwa wakati ule. Aone kama Je! bado atashikamana na utimilifu wake kabla ya kuzipokea zile ahadi zenyewe?
Zaburi 105:17 “Alimpeleka mtu mbele yao, Yusufu aliuzwa utumwani.
18 Walimwumiza miguu yake kwa pingu, Akatiwa katika minyororo ya chuma.
19 Hata wakati wa kuwadia neno lake, AHADI YA BWANA ILIMJARIBU”.
Jambo kama hilo, tunaliona kwa Ibrahimu pia, Mungu alimuahidia kuwa atamfanya kuwa baba wa mataifa mengi, na uzao wake utakuwa mwingi kama nyota za mbinguni, lakini jambo hilo hakulipata siku hiyo hiyo, hakulipata mwezi huo huo, hakulipata mwaka huo huo..Bali ilipita miaka mingi, zaidi ya 25,akiwa mzee wa miaka karibu 100, ndipo dalili zinaanza kuonekana onekana kwa kumpata Isaka.
Lakini ghafla naye tena dalili hizo zinaenda kuzimwa, pale Mungu anapomwambia, amchukue Isaka akamtoe kafara mbele zake, kwa namna ya kawaida ni rahisi kusema huyu sio Mungu, lakini Ibrahimu alitii kwasababu alijua ni wakati wa Ahadi za Bwana kumjaribu. Akapanda na Isaka kule mlimani, akijua kabisa tayari hana mtoto, wazo la kuwa Mungu ataghahiri halikupita katika akili yake hata kidogo.
Mwanzo 22:1 “Ikawa baada ya mambo hayo MUNGU ALIMJARIBU IBRAHIMU, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa.
2 Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.
3 Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu.”
Umeona, agano la kale ni kivuli cha agano jipya.
Na sisi kama kanisa, Mungu ametupa ahadi zilizo kubwa zaidi ya akina Ibrahimu na Yusufu, tumepewa maono makubwa sana, na maono yenyewe ni kuurithi ufalme wa mbinguni, ahadi za kuketi pamoja na Yesu katika kiti chake cha enzi kule mbinguni, ahadi za kufanywa nguzo, ahadi za kuwa wafalme wa makuhani wa Bwana katika ile Yerusalemu mpya itakayoshuka kutoka mbinguni kwa Baba ambayo njia zake ni za dhahabu,
Unategemea vipi ahadi hizi zisitujaribu?
Zitatujaribu tu wakati mwingine, Mungu anafanya hivyo ili aone je! ni kweli tumemaanisha kwenda mbinguni au la? .Hivyo wewe na mimi tukipitia mazingira ya upingamizi, usifikiri kuwa ahadi ya Mungu ya kuwa mfalme na kuhani imebatilika kwetu…La! Haijabatilika hata kidogo..ipo pale pale.
Kupitia vikwazo vya namna mbalimbali kwa ajili ya imani yako, usitetereke hata kidogo, wala usikufuru, macho yako yasiache kuzitazama ahadi Mungu alizokuwekea mbele kama Ibrahimu na Yusufu. Hata kama hakuna dalili inayoonekana leo, fikiri juu ya uzuri wa mbinguni, Kwasababu moja ya hizi siku, parapanda italia, wafu watafufuliwa, kisha kwa pamoja tutaicha hii dunia kwa mara ya kwanza, tutakwenda mbinguni katika karamu tuliyoandaliwa na Bwana Yesu, tutaisheherekea hiyo kwa kipindi cha kirefu, tutazuru mitaa yote ya mbinguni, tutaona mambo ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia, hapo tukiwa na miili ya utukufu, isiyoumwa, isiyozeeka, isiyougua, kisha tutarudi hapa duniani kutawala na Bwana Yesu kwa kipindi cha miaka 1000 kama wafalme, na baada ya hapo tutaingia katika ile Yerusalemu mpya, ambapo Makao ya Mungu yatakuwa pamoja na sisi wanadamu milele.
Mambo tuliyoandaliwa huko, hayajawahi kuingia katika moyo wa mwanadamu yoyote, biblia inatuambia hivyo. Kwahiyo tusichoke kumngojea Mungu, tusichoke kuzingojea ahadi za Bwana za milele. Utaona pamoja na kwamba Ibrahimu na Yusufu na Ayubu walipitia katika mapito yote yale, lakini mwisho wao ulikuwa ni mzuri, wa kufundisha na wa kuokoa na sio wa kukomoa, Yusufu kuuzwa utumwani ni kwasababu njaa ilikuwa mbele, hivyo alihitajika kwenda Misri kuwaandalia ndugu zake makao, na chakula, Ibrahimu kumtoa kafara mwanawe, ilikuwa ni ujumbe kwa kanisa juu ya dhabihu ya Yesu Kristo. N.k.
Vivyo hivyo na sisi tuliookoka, tusipozimia mioyo ahadi zetu zitatufikia.
Isaya 40:29 “Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo.
30 Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka;
31 bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia”.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Ibada ni nini,Na je ili ikamilike inapaswa iwe na nini na nini?
About the author