Category Archive Mafundisho

Uchimbueni udongo wa mashamba yenu.

Hosea 10:12

[12]Jipandieni katika haki, vuneni kwa fadhili; uchimbueni udongo wa mashamba yenu, kwa maana wakati umewadia wa kumtafuta BWANA, hata atakapokuja na kuwanyeshea haki.

Tunaishi katika majira ambayo kumtafuta Mungu hakupaswi kuwe kwa juu juu tu… kumbuka Neno la Mungu linatufananisha sisi na wakulima wapandao na wenye malengo ya kuvuna kwa vile tuvipandavyo…

Na sikuzote mkulima yoyote labda tuseme yule wa nafaka hatupi mbegu zake tu juu ya ardhi akitarajia ziote, bali utamkuta Na jembe, tena lile imara analikita chini ardhini kwa nguvu, huku jasho likimtoka.

Kimsingi kupiga jembe chini ndio kazi aliyonayo mkulima, haijalishi ardhi itakuwa ngumu kiasi gani hana budi kuichimba kwa nguvu, ili mbegu izame aone matokeo… vinginevyo hatavuna chochote.

Bwana anasema…

Uchimbueni udongo wa mashamba yenu, kwa maana wakati umewadia wa kumtafuta BWANA,

Kumtafuta BWANA…ni kuchimba chini…

Yaani kama ni maombi basi ni Maombi ya masafa marefu sio yale mfano wa kuombea chai ya asubuhi, kama ni kusoma na kujifunza Neno, basi ni kufanya hivyo vya kutosha kila siku sio kuamka na mstari mmoja, au kusubiri Tu kuhubiriwa YouTube halafu basi..

Kama ni ibada, kujifunza Kudumu uweponi mwa Mungu kwa nyakati ndefu…huko ndiko kuchimba chini ambako Bwana anakutaka…

Tusipende mambo ya juu juu, yatatugharimu vibaya sana, na tutajikuta tunapata hasara ya mbegu zetu kuliwa na ndege..

Fahamu kuwa Yesu amekaribia kurudi.. Je umezama Kweli ndani yake? Je unamtafuta kwa bidii, je umejiweka tayari kumpokea? Kama ni hapana basi anza sasa..

Kwasababu mbinguni hakitaingia kinyonge.

Chimba ardhi yako.

Neema ya Bwana akufunike.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Print this post

Mwandishi wa kitabu cha wimbo uliobora.

Aliyekiandika kitabu hiki ni Sulemani, mwana wa Daudi. Kufuatana na utambulisho wake mwanzoni kabisa mwa kitabu hichi.

Wimbo 1:1 Wimbo ulio bora, wa Sulemani

Mfalme Sulemani alijaliwa hekima na Mungu kuandika nyimbo nyingi sana Pamoja na Mifano mingi. Kama 1Wafalme 4:32 inavyosema aliandika Nyimbo elfu moja, na tano.

Sasa miongoni mwa hizo nyimbo, basi huu ulikuwa mmojawapo. Na ndio uliokuwa bora kuliko zote. Ndio maana umeitwa wimbo ulio bora.

Ni sawa na kusema Mfalme wa Wafalme, au Patakatifu pa Patakatifu. Ikiwa na maana kuna pazuri  kweli, lakini papo pazuri Zaidi ya kote, au kuna wafalme kweli lakini yupo aliyezidi wote. Ndivyo ilivyo katika vitabu vya Sulemani.

Hichi ndio kitabu ambacho, kimebeba hekima ya juu kuliko zote Sulemani alizojaliwa na Mungu kuziandika. Ni kitabu chenye maudhui ya kimahusiano kati ya mtu na mpenzi wake, ikifunua mahusiano yaliyopo kati yetu sisi na Kristo rohoni.

Kwa Maelezo mapana juu ya uchambuzi wa kitabu hichi bofya hapa >>> VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 11 (Mithali, Wimbo ulio bora, Mhubiri)

Lakini pia kwa mafunzo mbalimbali yaliyomo ndani ya kitabu hichi, bofya masomo yafuatayo.>>

Nini maana ya Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, (Wimbo 2:7)

USIKAWIE- KAWIE KUUFUNGUA MOYO WAKO

NYAKATI TOFAUTI- TOFAUTI ZA UPENDO.

MAAJABU YA AGANO LA UPENDO WA KRISTO.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Print this post

KISIMA BADO KINA MAJI, KIFUKUE TENA.

Isaka, alipofika mahali panaitwa Gerari alivikumbuka visima vilivyochimbwa na baba yake Ibrahimu zamani, lakini alipotazama na kuvikuta vimeharibiwa, alianza kazi ya kuvichimba tena, Alipokifukua cha kwanza na kutoa maji maandiko yanatuambia wachungaji wa mahali pale wakakigombania..

Akakiita Eseki, akasogea mbele kodogo akakichimbika Kingine tena nacho kikagombaniwa akikiita Sitna, akasogea tena Mbele akachimba kingine cha tatu..

Hicho hawakukigombania akakiita..Rehobothi

Kisha akasema..Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.

Mwanzo 26:18-22

[18]Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye.

[19]Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika.

[20]Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye.

[21]Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna.

[22]Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.

Sauti ya Mungu nyuma ya habari hii ni nini?

Fahamu ukishaokoka, kuna kisima cha maji ya uzima kinapandwa ndani yako na Yesu Kristo mwenyewe. Kisima hiki licha ya kukupa uzima wa milele..lakini kina kazi ya kukupa raha, kukustawisha na kukufanikisha, maisha yako hapa duniani na mbinguni.

Yohana 7:38

[38]Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.

Anasema tena..

Yohana 4:14

[14]walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.

Lakini ni kazi ya adui kukifukia kisima hicho, na hatimaye uwe mkavu kabisa usione raha ya wokovu au matunda yoyote ya imani yako ndani ya Kristo.

Hapo mwanzo ulikuwa ni moto rohoni, ulikuwa unaweza kuomba, kusoma Neno, Bwana alijifunua kwako kwa viwango vya juu..Ukitembea uliuhisi uwepo wa Roho Mtakatifu karibu na wewe…lakini sasa huhisi chochote,huwezi tena kuomba, kushuhudia n.k ukiona hivyo fahamu kuwa kisima kimefukiwa…lakini tumaini ni kuwa maji yapo chini waweza kuanza tena kuchimba na kurudia viwango vyako vya juu hata na zaidi..

Ulirudi nyuma, mpaka ukafikia hatua ya kuyatenda yale machafu ya dunia uliyoyaacha, Ukahisi kama Mungu hawezi kukusamehe tena…ukweli ni kwamba tumaini lipo, anza tu kukichimba kisima chako, maji utayaona.

Ulikuwa na maono mazuri, Na shauku ya kufikia hatma yako, ulikuwa unaona mwendelezo mzuri wa kile ulichokuwa unakifanya hata katika magumu hukutukisika lakini yale maono yamekufa, huelewi ni nini kimetokea, ujue kisima kimefukiwa…anza Upya tena.

Ila ni lazima ukubali kuchukua hatua bila kukata tamaa..Ilimgharimu Isaka visima vitatu lakini hakukata tamaa, hata alipofukua cha kwanza alisumbuliwa, akaendelea tena na tena…alipofikia cha tatu..ambacho ni Rehobothi..basi ikawa ni pumziko lake la daima.

Sisi kama watoto wa Mungu ni Lazima tujue adui ana wivu na hapendi kuona chemchemi za uzima na mafanikio zinabubujika ndani yetu…atafanya juu chini kuhakikisha vinafukiwa na hatimaye kutoona matokeo yoyote ya wokovu kwenye maisha yetu, na wakati huo sio mpango wa Mungu ..ataleta majaribu, misuko-suko, tufani n.k. Lakini ukistahimili Mpaka mwisho utashinda..na hatimaye utakaa mahali pa kudumu pa raha yako kama Isaka..

Ufanye nini?

Anza sasa kujizoesha kwa nguvu kusoma Neno, hata kama mwili hautaki, omba, hudhuria Mikesha acha uvivu, jitenge na dhambi zote. Na hatimaye utaona mwanzo mpya tena wenye nguvu rohoni mpaka mwilini.

Chimba kisima chako

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Print this post

UJUE UZIMA WA MILELE.

Mtu akikuuliza “Kufanikiwa nini?”..bila shaka unaweza kumjibu ni kuwa na “kazi nzuri yenye kipato kizuri na kuwa na afya njema”. (Hii ni tafsiri nyepesi na rahisi tu).

Sasa tukirudi katika roho, Uzima wa milele ni nini?..biblia imetupa majibu mafupi na marahisi..

Yohana 17:3 “Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma”

Ukimjua MUNGU na YESU KRISTO unao uzima wa milele..

Sasa si kwamba MUNGU na YESU ni vitu viwili tofauti.. La! ni MUNGU mmoja katika madhihirisho mawili tofauti..

Mfano mtu anaweza kukuona wewe mubashara (live)…au akakuona kupitia picha yako. Sasa wewe kwenye picha na wewe wa mubashara sio watu wawili tofauti ni mtu mmoja katika madhihirisho mawili tofauti.

Wakati mwingine badala ya kuonekana wewe mubashara unaweza kutuma picha yako au kuibandika katika nyaraka zako muhimu kama vyeti, au vitambulisho au barua na ikawa ni wewe yule yule.

Na YESU ni picha kamili ya Mungu, aliyemwona YESU amemwona MUNGU BABA, kwahiyo hatuwezi tena kutafuta kujua Baba yupoje, tukimwona Yesu tumemwona Baba, ndivyo maandiko yasemavyo..

Yohana 14:8 “Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha.

9 Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?”

Yohana 14:7 “Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona”

Sasa turudi kwenye “UZIMA WA MILELE”...anasema…“Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma”.

Maana yake ukisema unamjua MUNGU halafu unamkataa YESU maana yake huna UZIMA WA MILELE, Kwasababu YESU ni ufunuo kamili wa Mungu katika mwili.

Utaona watu wanasema, mimi namwamini Mungu lakini simwamini YESU, sasa utaikanaje picha ya mtu na kumkiri mtu?..

Nimekuletea picha yangu, halafu unaikana, na bado unakiri kunijua?.. kama ukiikana picha yangu maana yake unanifanya mimi kuwa mwongo.

Vile vile ukimkana YESU na kukiri kumjua MUNGU unamfanya MUNGU kuwa mwongo. (Soma 1Yohana 5:10).

Kama humwamini YESU ni moja kwa moja umwamini MUNGU pia, hiyo haina kutafakari mara mbili..kama humjui Yesu ni moja kwa moja humjui Mungu Baba hiyo haina kutafakari mara mbili pia.

Yohana 8:19 “Basi wakamwambia, Yuko wapi Baba yako? Yesu akajibu, Mimi hamnijui, wala Baba yangu hammjui; kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba yangu”.

Kwahiyo wakati huu Uzima wa milele unapatikana kwa YESU tu pekee yake, zingatia hilo: YESU TU PEKE YAKE!!.…usijaribu kumtafuta Mungu nje ya YESU, ni kupoteza muda.

Usijaribu kumtumikia Mungu nje ya Yesu, ni kupoteza muda, usitafute uzima wa milele nje ya Yesu, ni kupoteza muda na uzima wako wa milele, akitokea mtu, awe nabii, mtume au mchungaji amshuhudii Yesu kama ndie njia pekee ya kufika mbinguni, mkimbie!

Akitokea kuhani na kukufundisha kuna mwingine au wengine wanaoweza kufanya kazi kama ya YESU, mkimbie!.. Kristo YESU hana pacha, wala msaidizi kwamba pia kupitia mtakatifu fulani aliye hai au aliyekufa tunaweza kumwona Mungu, kwamba tukimwamini huyo tunaweza kumwona MUNGU, kimbia!

YESU si mtu wa pembeni aliyeletwa kutuokoa, ni Mungu mwenyewe aliyevaa mwili… yaani Mungu aliyetengeneza mwili na kuweka tabia zake zote ndani ya huo mwili, akaja ili atuonyeshe njia na kutukomboa, hivyo hana msaidizi, kajitosheleza kwasababu yeye ni MUNGU. (1Timotheo 3:16).

Kwahiyo tusipomwamini Yesu kwa namna hiyo hatuna uzima wa milele, haijalishi tutajitahidi kufanya mema kiasi gani, kama tumeshamsikia na hatutaki kumwamini, hatuna uzima wa milele.

Swali ni je?.. Unao uzima wa milele?..je umemwamini YESU na kuyafanya anayoyasema?.

Luka 6:46 “Na kwa nini mnaniita, Bwana, Bwana, walakini hamyatendi nisemayo?

47 Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake.

48 Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri.

49 Lakini yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaishukia kwa nguvu, ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba ile yakawa makubwa”.

Mwamini YESU na tenda ayasemayo.

Maran atha!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

TENDA AGIZO LA YESU, HILO NDIO LITAKALOKULINDA.

UJIO WA BWANA YESU.

MAASI KUONGEZEKA NI ISHARA YA NINI?.

Na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa?. Ni mwamba gani huo?(Mathayo 16:18)

Print this post

WALAKINI MIMI SI PEKE YANGU.

Jina la Mwokozi YESU libarikiwe, karibu tujifunze Biblia.

Ni muhimu kupambana sana mpaka kufikia hatua ya Mungu kuwa kila kitu kwetu, maana yake hata watu wote wakikuacha, au kukutenga, au kukusahau, bado MUNGU ni faraja tosha kwako zaidi ya watu elfu, au ndugu elfu.

Tukifikia hii hatua tutakuwa watu wa furaha siku zote, na watu wa kuishi bila kutegemea sana hamasa kutoka kwa watu au vitu.

Tukiweza kufikia kiwango kwamba faraha kutoka kwa watu haziwi sababu kuu za msukumo wetu kue delea mbele, tutakuwa watu wakuu sana mbele za Mungu.

Pia tukiweza kufikia kiwango kwamba maneno mabaya au dhihaka au kukatishwa tamaa na watu haziwi sababu ya kukata tamaa na kuumia, pia tutakuwa watu wa kuu sana mbele za watu.

Wakristo wengi tunahamasika sana pale tunapohamaishwa na watu, tunapata nguvu zaidi pale tunapotiwa nguvu na watu, na pia tunavunjika moyo sana pale tunapovunjwa moyo na watu, lakini haikuwa hivyo kwa Bwana wetu YESU KRISTO, yeye faraja yake na huzuni yake ilikuwa kwa Baba..

Kiasi kwamba hata watu elfu wangemtukuza na kumtia moyo kama kutiwa huko moyo hakujatoka mwa Baba yake, hakukuweza kumhamasisha kitu.

Hali kadhalika hata watu wote wakitoa maneno ya kuvunja moyo au watu wote wakimwacha na akabaki peke yake, maadamu anaye Baba yake haikumvunja moyo wala kumkatisha tamaa, ndivyo maandiko yasemavyo..

Yohana 16:32 “Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami”.

Hapo Bwana YESU aliona saa inakuja kwamba kila mtu atamkimbia na atabaki peke yake na kweli huo wakati ulitimia pale askari wa Herode walipokuja kumkamata Bwana Yesu pale bustanini, maandiko yanatuonyesha walikimbia wote, na hata mwengine walikimbia uchi (Marko 14:51-52).

Lakini hatuoni Bwana Yesu akivunjika moyo kwa hilo tendo, kwasababu anajua na ana uhakika kwamba Baba yupo naye..

Anajua watu wote wakimwacha haimaanisha Baba yake kamwacha…

Lakini ulipofika wakati wa Baba kumwacha kwa kitambo kwasababu ya dhambi za ulimwengu, ndipo tunaona Kristo anajali na kuhuzunika..

Mathayo 27:46 “Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

Na sisi hatuna budi kufika hii hatua, Mungu wetu, na Baba yetu abaki yeye kuwa faraja yetu ya mwisho, kiasi kwamba hata dunia nzima ikiondoka, Baba yetu atabaki kuwa hamasa yetu, faraja yetu, yaani awe mwanzo na mwisho kwetu.

Na hata dunia nzima ikutusifia na kutupa maneno ya hamasa, bado hamasa ya Baba yetu ndio itakayokamilisha furaha yetu.

Bwana Yesu atusaidie sana.

Zaburi 9:10 “Nao wakujuao jina lako wakutumaini Wewe, Maana Wewe, BWANA hukuwaacha wakutafutao”

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

UTENDAJI KAZI MWINGINE WA ROHO MTAKATIFU USIOUFAHAMU.

FUNGUO ZA UZIMA, MAUTI NA KUZIMU.

Je, kama hauna ubatizo sahihi hauwezi kuwa na Roho Mtakatifu?

WALIKUWA WAKINUNUA NA KUUZA, WAKIOA NA KUOLEWA KAMA ISHARA YA KANISA !

MFALME ANAKUJA.

Print this post

KATAZO LA MUNGU, NI MAFANIKIO.

Ukikatazwa na Mungu, haimaanishi kuwa umenyimwa unachoomba, kinyume chake amepewa kwa uzuri wa juu zaidi.

Kuna kipindi Daudi aliingiwa na Nia ya kutaka kumjengea Mungu nyumba ..Hivyo akaanda Mali zake nyingi ili aanze ujenzi…lakini alipolileta Hilo wazo kwa Mungu, ilikuwa ni tofauti na alivyotarajia..

Mungu hakumruhusu bali kinyume chake akamwambia wewe hutanijengea mimi nyumba…kwasababu umemwaga damu ya watu wengi, lakini mwanao ndiye atakayenijengea…

1 Mambo ya Nyakati 22:7-8

[7]Daudi akamwambia Sulemani mwanawe, Kwangu mimi nia yangu ilikuwa kujenga nyumba kwa ajili ya jina la BWANA, Mungu wangu.

[8]Lakini neno la BWANA likanijia, kusema, Wewe umemwaga damu nyingi, na vita vikubwa umevifanya; wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu;

Jiweke katika hiyo hali unatamani ufanye kitu fulani chema, lakini Mungu anakuambia (aidha kwa maneno au vitendo) hapana wewe hustahili kufanya au kuchukua nafasi hiyo, kwasababu hii na hii na hii, bali ataichukua kijakazi wako, mtumwa wako, rafiki yako, mpendwa mwenzako…Sasa Kibinadamu hilo linaweza likaleta ukakasi lisikuvutie Masikioni mwako…kwasababu unajua litampa cheo mwezako.

Pengine ndivyo angeweza kufikiri Daudi… Lakini alijifunza kunyenyekea, na kumtii Mungu na kuachilia kijiti kwa mwingine…

matokeo yake ikiwa ujenzi ule ukadumishwa na jina lililodumishwa halikuwa lingine bali la Daudi kwa vizazi vyote vijavyo..aliyejenga alikuwa ni Sulemani, lakini utukufu ulikuja kwa jina la Daudi mpaka leo linatajwa.

Hii ni kutufundishia kukubali kunyenyekea Katika mapenzi yote ya Mungu..Zipo nyakati hutafanya wewe, hata kama umeomba na kuitamani hiyo nafasi yakupasa ukubali wengine wafanye, upo wakati hutatukuzwa wewe kubali wengine watukuzwe kupitia wewe, hutaheshimiwa wewe lakini fanya bidii wengine waheshimiwe kupitia wewe…kwasababu hiyo ndio ngazi ya kuinuliwa na Mungu, na matokeo yake utayaona..

Makatazo ya Mungu ni fursa ya mafanikio, unaweza ukawa hujapewa uzao, lakini ukamlea mtoto wa mwingine, Mungu akaja kumfanya raisi wa nchi, ukaitwa mama wa Taifa. Hivyo maadamu unatembea katika njia za Bwana na umeomba, amini kuwa Mungu amekupa zaidi ya kile ukiwazacho.

Kamwe Using’ang’anie jambo, bali jifunze kuachilia neema ya Mungu yenyewe kuamua, kwasababu hutapoteza chochote..

Waefeso 3:20

[20]Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;

Bwana awe nawe…

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Print this post

MWILI NI KWA BWANA na BWANA NI KWA MWILI.

Je Mungu anaangalia mwili na kuihitaji?.. jibu ni Ndio!.. maandiko yanathibitisha hilo wazi kabisa..

1Wakorintho 6:13 “Vyakula ni kwa tumbo, na tumbo ni kwa vyakula; lakini Mungu atavitowesha vyote viwili, tumbo na vyakula. LAKINI MWILI SI kwa zinaa, BALI NI KWA BWANA, NAYE BWANA NI KWA MWILI”.

Nataka uone hayo maneno ya mwisho yanayosema “…mwili si kwa zinaa, BALI NI KWA BWANA, NAYE BWANA NI KWA MWILI” Kumbe “miili yetu” ipo mahususi kwaajili ya “Bwana” na Bwana yupo mahususi kwaajili ya “miili yetu”.. Si ajabu tunapomwomba mahitaji ya mwilini anatujibu haraka sana kama tu vile ya rohoni.

Si ajabu tunapoteseka katika mwili hapendi, kwasababu miili yetu ni ya thamani sana kwake, kwaufupi ili tuwe wanadamu ni lazima tuwe na miili..

Sasa je! huu usemi ya kwamba Mungu haangalii mwili unatoka wapi?.. bila shaka ni kwa ibilisi!.

Maandiko yanazidi kusema kuwa  “sisi si mali yetu wenyewe”

1Wakorintho 6:19 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe”.

Tuzidi kusogea mbele katika andiko hilo… tujifunze ni kwa namna gani MWILI ni Kwa BWANA na BWANA ni kwa MWILI.

Muunganiko wa Miili yetu na Kristo ni mpana sana kiasi kwamba Biblia inatafsiri “viungo vyetu vya mwili ni viungo vya Kristo pia”.. maana yake huo mkono unaouona kama ni wako, kibiblia ni mkono wa Kristo, hayo macho si yako bali ni ya Kristo, kwahiyo kama umemwamini Yesu halafu ukaenda kufanya zinaa, maana yake umechukua kiungo cha Kristo na kukifanyisha zinaa..ndivyo Biblia inavyosema..

1Wakorintho 6:15 “Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha!”

Huo mguu unaoona ni wako kiuhalisia kama umeokoka si wako tena bali ni wa Kristo… ndio maana Bwana Yesu alisema mahali watakapowakaribisha basi wamemkaribisha yeye Kristo..na wakiwakataa wamemkataa yeye Kristo… kwanini?.. ni kwasababu miili yetu si mali yetu wenyewe baada ya kuokoka!, bali viungo vyetu vyote vinakuwa ni vya Kristo na vina mhubiri Kristo.

Luka 10:16 “Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma”.

Umeona??.. maana yake mtu aliyeokoka ni “Kristo anayetembea”.. ukiendelea kujifunza zaidi katika habari ile ya hukumu ya kondoo na mbuzi katika Mathayo 25:31-46… utaona wale watu waliuliza “ni lini Bwana tulipokuona  una njaa, upo uchi tukakulisha na kukuvisha” ndipo Yesu atawaambia “kwa kadri mlivyowatendea wadogo wale basi walimtendea yeye”… wadogo wanaozungumziwa pale ni “watu wa Mungu wanaohubiri habari njema”.

Kwahiyo kumbe matumbo yenye njaa ya watu wa kweli wa Mungu ni matumbo ya Kristo, kumbe miguu yenye vumbi ya watu wa Mungu wa kweli ni miguu ya Kristo.. kwaujumla kumbe miili ya watu wa Mungu ni miili ya YESU mwenyewe!… si ajabu pale alisema “…nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha!”

Sasa kama ni hivyo kwanini unauvika mwili wako mavazi ya jinsia nyingine…je ni Kristo yupi unayemhubiri kwa uvaaji wako?..kwanini unafanya zinaa?, kwanini unachora mwili wako?, kwanini unauvutisha sigara na kuunywesha pombe?

Yachukulie haya kwa uzito mtu wa Mungu, wala si usipuuzie!, na kusema Mungu haangalii mwili?.. jihadharia na mafundisho ya uongo! Yanayokuambia kuutunza mwisho ni mafundisho ya sheria na vifungo!.. Tunapookoka hatujapewa uhuru wa kufanya dhambi!, La! Hatujafunguliwa kufanya dhambi!.

Siku ya mwisho hatutafufuliwa roho bali miili ndio itakayofufuliwa, na Kristo hakutoa roho yake kwa ukombozi wetu, bali mwili wake wenye damu, mifupa, mishipa, nyama, moyo, miguu, mikono, ngozi !.. vyote Kristo alivitoa kwaajili ya ukombozi wetu..

Waebrania 10:5 “Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari”.

Biblia inazidi kutufundisha kuitoa miili yetu kwa Bwana..

Warumi 12:1 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana”..

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MAAJABU YA AGANO LA UPENDO WA KRISTO.

Tofauti kati ya makuhani na walawi ni ipi?

Je Bwana YESU alimjibu Pilato au hakumjibu? Je biblia inajichanganya?

KILA MMOJA WENU AJUE KUUWEZA MWILI WAKE.

MTUMAINIE YESU ASIYEISHA MATUKIO.

Print this post

NAKUJUA JINA LAKO!

Kutoka 33:17 “Bwana akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, NAMI NAKUJUA JINA LAKO

Jina la Mtu limebeba siri kubwa sana,  lakini kabla ya kutazama jina la MUNGU.

Kitu pekee kilichomtambulisha na kinachomtambulisha MUNGU kwetu sasahivi ni JINA LAKE!.. Kamwe hajawahi kutuonyesha Sura yake, wala kuitangaza mahali popote pale!, bali jina lake.. bali jina lake amelitangaza na kulitukuza sana..

Sasa si kwamba anapenda kujificha kwetu!.. La bali ametuchagulia kilicho bora kwake tukijue!.. Kwahiyo kulicho bora kwake kwetu ni jina lake zaidi ya sura yake.

Na kilicho bora kwa MUNGU kwetu kukijua ni MAJINA YETU zaidi ya SURA ZETU… Utauliza kivipi?..

Kitu pekee kinachoko sasa mbinguni kinachotutambulisha sisi sio SURA ZETU bali ni MAJINA YETU.. Mbinguni hakuna picha zetu!, bali majina!..

Ufunuo 13:8 “Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye JINA LAKE HALIKUANDIKWA katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia”.

Soma pia Ufunuo 17:8,  Ufunuo 3:5,  Wafilipi 4:3 utaona hakuna sura kule za watu kule mbinguni… hivyo uzuri wako wa sura, weupe wako, weusi wako, urefu wako, ufupi wako, unene wako, ubounsa wako na wangu unaishia hapa!!!..

Hiyo pia ndio sababu ya Bwana YESU kuwaambia wanafunzi wake wasifurahia pepo wanavyowatii bali wafurahie majina yao yameandikwa mbinguni…

Luka 10:20 “Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni”.

Na unajua, Mungu anatujua kwa majina zaidi ya Sura na rangi?…ndivyo alivyomwambia hata nabii Musa.

Kutoka 33:17 “Bwana akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, NAMI NAKUJUA JINA LAKO”.

Umeona hapo?.. Mungu anamwambia Musa anamjua jina lake, sio sura yake…. Kwahiyo ni muhimu sana kuaangalia MAJINA YETU na kuyatengeneza…. Maandiko yanasema ni heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi..

Mithali 22:1 “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi…”

Sasa tunachaguaje majina??.. je tubadilishe majina tuliyonayo?.. jibu ni La!.. tutaendelea kuwa na majina yetu haya haya ikiwa kama yana maana njema.. Lakini majina yetu haya haya yanaweza kubadilika na kuwa BORA..

Kwa jinsi jina lako linavyozidi kuwa Bora mbele za Mungu, ndivyo nafasi yako mbinguni inavyozidi kuwa kubwa, na kwa kadiri linavyozidi kufifia mbele za Mungu ndivyo mbinguni linavyofutika kumbukumbu lako..

Sasa tunafanyaje majina yetu kuwa Bora?.. Si kwa kwenda kuyatolea sadaka ya ukombozi, au kuyaombea kwenye mkesha.. La!.. unaweza kutoa sadaka za aina zote duniani na jina lako lisiwe mbinguni, lakini bado likaendelea kuwa kubwa mbele za watu, na unaweza kuwa na jina la heshima kwa mbele za watu lakini mbele za Mungu ukawa huna jina.

Ifuatayo ni njia pekee ya kulitakasa jina lako, na hivyo heshima yako, na hadhi yako.. na njia hiyo si nyingine zaidi ya KUMCHA MUNGU, na KUJITENGA NA DHAMBI.. Utauliza kivipi, tusome maandiko yafuatayo?.

Kutoka 32:31 “Musa akarejea kwa Bwana akasema, Aa! Watu hawa wametenda dhambi kuu wamejifanyia miungu ya dhahabu.

32 Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao — na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika.

33 Bwana akamwambia Musa, MTU YE YOTE ALIYENITENDA DHAMBI NDIYE NITAKAYEMFUTA KATIKA KITABU CHANGU”.

Umeona kitu kinachochafua jina la Mtu?… ni DHAMBI, Hiko ndicho kinachomwondoa mtu kwenye kumbukumbu za MUNGU, na si tu mbinguni na hata duniani pia..

Kumbukumbu 29:20 “Bwana hatamsamehe mtu huyo, lakini wakati huo hasira ya Bwana na wivu wake vitafuka moshi juu ya mtu yule, na laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki itamkalia juu yake, na BWANA ATALIFUTA JINA LAKE CHINI YA MBINGU”.

Huenda dhambi imechafua jina lako!.. suluhisho ni moja tu, kutubu na kuacha dhambi!.. jina lako hilo litasomeka kwenye kitabu cha mwanakondoo mbinguni.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MSINGI WA NYUMBA YA MUNGU, NI JINA LA MUNGU.

KWANINI TUNAOMBA KWA JINA LA YESU?

HAPO NDIPO WATU WALIPOANZA KULIITIA JINA LA BWANA.

FAIDA NYINGINE YA MAOMBI YA KUSHUKURU.

FUNDISHA KILE UNACHOKITENDA NA KUKIISHI

Print this post

Je umewaonea utungu watoto wako?

Ulishawahi kuona mwanamke anajifungua mtoto bila kusikia utungu wowote? Hilo jambo bila shaka Litakuwa ni la ajabu… kwasababu haliendani kabisa na kanuni za asili …

hata maandiko yanasema hivyo..

Isaya 66:7-8

[7]Kabla hajaona utungu alizaa; Kabla maumivu yake hayajampata, Alizaa mtoto mwanamume.

[8]Ni nani aliyesikia neno kama hili? Ni nani aliyeona mambo kama haya? Je! Nchi yaweza kuzaliwa siku moja? Taifa laweza kuzaliwa mara?..

Ni kanuni ya asili ili kiumbe kipya kizaliwe, mzaaji ni lazima apate utungu tu kama malipo ya kile akizaacho ..kila mwanadamu unayemwona chini ya jua, kuna mtu alipata maumivu kwa ajili yake..

Kanuni hii ipo rohoni pia…Kila mtakatifu unayemwona (aliyesimama), haikuwa bure bure…au kirahisi rahisi tu kama unavyodhani, kuna Waliopitia utungu juu yao…

Utauliza hili lipo wapi Kwenye maandiko?.

Paulo kwa Wagalatia,aliandika maneno haya;

Wagalatia 4:19

[19]Vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu;

Paulo anawalilia wagalatia, kwa jinsi walivyoiacha neema ya Kristo, na kurudia mafundisho ya kiyahudi..anasema nawaonea utungu tena….tafsiri yake ni kuwa hapo nyuma alishawahi kuwaonea utungu…akawazaa…lakini sasa ni kama vile wanahitaji kuzaliwa tena….

Hivyo watu wote waliozaliwa mara ya pili wapo Waliowanea utungu.

Siku za Utungu mwanamke hupitia mambo haya:

1). Hulia na kuugua: 

Maana yake hiki ni kipindi cha machozi na kuomba juu ya wale wote unaotamani wampokee Kristo..ndiyo tabia waliokuwa nayo mitume.

Matendo ya Mitume 20:31

[31]Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi.

Watu wengi wanatamani kuona geuko la dhati kwa jamii zao, rafiki zao, waume zao, watoto wao lakini hawana muda wa kuwaombea kwa kuzama sana kwa kipindi kirefu na wakati mwingine kufunga huku wakiwahubiria…wanaikwepa Kanuni hii ya kiumbe kipya kuzaliwa.

2) Mwanamke hupitia hatari mbalimbali zinazohatarisha maisha; 

Hichi kipindi wanawake wengi huchungulia kifo, kwa sababu ya maumivu, au shinikizo au kutokwa na damu nyingi sana.

Ndivyo ilivyo pale unapojaribu, Kumvuta mwenye dhambi aifikie toba ya kweli, adui huanza kuinua vita, dhidi yako wewe na huyo unayemzaa.. lile joka litataka kufanya vita na wewe.

Ufunuo wa Yohana 12:1-4

[1]Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili.

[2]Naye alikuwa ana mimba, akilia, hali ana utungu na kuumwa katika kuzaa.

[3]Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba.

[4]Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake.

Ukijikuta katika wakati huu fahamu ni kung’ang’ana kumfuatilia kondoo huyo bila kujali hali au vipingamizi…unaweza kuona visababu sababu visivyoeleweka, mara hataki tena kukusikiliza, mara anaumwa, mara ndugu zake wanampinga, mara anakuwa mzito.hapa hupaswi kukata tamaa..endelea kumfuatilia kwasababu hizo ni hila za adui kumzuia asikate shauri kwa Bwana Yesu..

Fahamu tu kazi yako si bure upo wakati ataamini na kugeuka kabisa kabisa kwasababu Nguvu uliyonayo na kuu kuliko ya ibilisi..na furaha yako itakuwa ni pamoja na malaika mbinguni. (Luka 15:10).

Pia Biblia inasema…

Yohana 16:21

[21]Mwanamke azaapo, yuna huzuni kwa kuwa saa yake imefika; lakini akiisha kuzaa mwana, haikumbuki tena ile dhiki, kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtu ulimwenguni.

Upo wakati utayafurahia matunda yako. Siku utakapoona kupitia hao makumi, mamia, maelfu ya watu wanaokoka..na siku ile Bwana anakupa thawabu kwa tunda hilo ulilomzalia.

Swali ni je utungu wako upo wapi?.. ni wapi unaweza kusema yule ni mwana wangu nimemzaa mimi katika Kristo?..

Kwenda tu kusema Yesu anakupenda okoka, halafu ukamwongoza Sala ya toba na kumwacha…hili halimaanishi huyo ni mtoto wako. Ndio maana wapo watu wengi wanaosema leo wamemkiri Yesu, lakini ukiwaangalia sio viumbe vipya..kwasababu hawakuzaliwa, bali waliaminishwa tu.

Tukubali kuzaa kwa kuwafundisha, kuwaombea sana, na kuwafuatilia mpaka watakapokata shauri la kweli kumpokea Yesu.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

DALILI ZIPI ZITAMTAMBULISHA MTU KUWA AMEFANYIKA KIUMBE KIPYA?

MAFUNDISHO MAALUMU KWA WAONGOFU WAPYA.

MAUMIVU  NYUMA-YA-HUDUMA.

Print this post

NYAKATI TOFAUTI- TOFAUTI ZA UPENDO.

Wimbo Ulio Bora 2:10-13

[10]Mpendwa wangu alinena, akaniambia,  Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako,

[11]Maana tazama, kaskazi imepita,  Masika imekwisha, imekwenda zake;

[12]Maua yatokea katika nchi,  Wakati wa kupelea umefika, Na sauti ya mwigo husikiwa kwetu.

[13]Mtini wapevusha tini zake, Na mizabibu inachanua, Inatoa harufu yake nzuri; Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako.

Mahusiano yoyote yale hukumbwa na vipindi tofauti tofauti.ni sawa na dunia na misimu yake, kuna vipindi Vya kiangazi, vipindi vya masika, vipindi vya joto, na vipindi vya baridi…

Vivyo hivyo pia mahusiano yoyote hukumbwa na nyakati kama Hizi..

Watu wa agano la kale walikuwa katika nyakati ngumu za upendo na Mungu, nyakati zao zilijawa na misuko-suko, ukame na kutaabika, nyakati za jasho na damu…Kwasababu shetani alikuwa na nafasi kubwa katika maisha ya wanadamu, lakini walikuwa hawajamjua bado Mungu vizuri.

Lakini mwokozi alipokuja, alituliza dhoruba zote, mawimbi yote, jua lote, mizigo yote, na taabu zote ..alilitimiza hilo kwa kujitoa kwake pale msalabani. Ndio maana akasema yeye ni Bwana wa sabato, ( pumziko). Kwasababu Alikuja kuleta pumziko haswaa la pendo lake, ili mtu asikae katika masumbufu ya aina yoyote rohoni.

Hivyo leo hii anasema nasi kama mtu amwambiaye mpenzi wake habari za faraja..

10]Mpendwa wangu alinena, akaniambia,  Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako,

[11]Maana tazama, kaskazi imepita, Masika imekwisha, imekwenda zake; [12]Maua yatokea katika nchi, Wakati wa kupelea umefika,

Huu ni wakati wa kuitikia wito wake mkuu wa upendo usio na usumbufu.. mpokee sasa ukuburudishe maishani. Akupe uzima wa milele, akupe faraja na tumaini uone maana ya maisha. Nyakati hizi ni za hatari, ulimwengu hauwezi kukupeleka popote, kinyume chake utaishia jehanamu tu ukiufuata, lakini ukimgeukia mwokozi na kumfuata utapata uzima wa milele.

SHALOM.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MAAJABU YA AGANO LA UPENDO WA KRISTO.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 11 (Mithali, Wimbo ulio bora, Mhubiri)

JAWA NA UPENDO UNAOTAFUTA.

Print this post