JINSI MUNGU ANAVYOIPIGA NA KUIPONYA AFRIKA.

JINSI MUNGU ANAVYOIPIGA NA KUIPONYA AFRIKA.

Leo hii dunia nzima inaishangaa Afrika kwa mambo mawili makuu : La kwanza ni umaskini wake, na pili jinsi lilivyojikita katika mambo ya Imani . Bara pekee lenye idadi kubwa ya watu wanaoishi kwa kuamini  “mungu” kwasasa ni Afrika tu. Jambo ambalo huwezi kuliona katika bara lingine lolote duniani.

Leo hii tutaona sababu za kibiblia ni kwanini tupo hivi, ili na wewe ujue ni wapi unapopaswa usimame..katika nafasi yako Afrika.

Watu wasioamini Mungu, wala wasioisoma biblia wanatafsiri umaskini wa waafrika ni kutokana na uvivu wao, na ujinga wao, lakini ukweli ni kwamba zipo jamii zenye watu wavivu kuliko hata waafrika, lakini bado wanao maendeleo makubwa zaidi yetu,.

Vilevile licha ya biblia kutuonyesha kuwa maendeleo makubwa tangu zamani yalianzia katika bara la Afrika lakini historia pia inathibitisha hilo kwamfano yale mapiramidi yalio kule Misri, na Ethiopia hadi leo hii hakuna Uinjinia wowote umewahi kufikia ile teknolijia..Hiyo ni kuonyesha kuwa sio kwamba waafrika ni wajinga kama wanavyofikiriwa..

Lakini Biblia inatuambia kuwa ni yeye Mungu mwenyewe ndiye aliyeifanya Afrika kuwa duni kuliko mataifa yote ulimwenguni. Na hiyo yote ni kwasababu ya miungu yao na sanamu zao..Ukisoma Kitabu cha Isaya sura ya 19 chote na Ezekieli sura ya 29 vinaeleza unabii juu ya bara la Afrika. Hatuwezi kuandika aya zote hapa kwa nafasi yako unaweza ukazisoma..lakini tutaangalia baadhi ya aya..

  1. Awali ya yote biblia ilishatabiri kuwa waafrika watawaliwa.

Tusome

Isaya 19:4 “Nami nitawatoa hao Wamisri na kuwatia katika mikono ya bwana mgumu; na mfalme mkali atawatawala; asema Bwana, Bwana wa majeshi”.

Sasa kumbuka sehemu nyingine biblia inapoitaja Misri ujue inawakilisha bara zima la Afrika..

Ilishatabiri kuwa juu ya utawala wa wakoloni, wa kibepari..

  1. Vilevile ilishatabiri kuwa itachukuliwa utumwani, kama vile wana wa Israeli walivyochukuliwa utumwani:

Ezekieli 29:12 “Nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake, kati ya miji iliyoharibika, itakuwa maganjo muda wa miaka arobaini; nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, nami nitawatapanya kati ya nchi mbalimbali.

13 Maana Bwana MUNGU asema hivi; Mwisho wa miaka arobaini nitawakusanya Wamisri, na kuwatoa katika hizo kabila za watu, ambazo walitawanyika kati yao;

14 nami nitawarejeza Wamisri walio katika hali ya kufungwa, nami nitawarudisha hata nchi ya Pathrosi, hata nchi ya kuzaliwa kwao; NA HUKO WATAKUWA UFALME DUNI.

15 UTAKUWA DUNI KULIKO FALME ZOTE; wala hautajiinua tena juu ya mataifa; nami nitawapunguza, ili wasitawale tena juu ya mataifa”.

Unabii, huo ulitimia, Afrika ilianza kuangia utumwani na kutawaliwa kuanzia karne ya 16 na mpaka kufikia karne ya 19, utumwa ulikoma, hiyo ni miaka 400 kama vile wana wa Israeli walivyokaa Misri. Na Mungu alishasema itakuwa duni kuliko mataifa yote.

Lakini Kwanini Mungu aliruhusu hivyo? Je analipiza kisasi au anawachukia waafrika?

Jibu ni hapana sura hizo mbili zinatuonyesha Mungu alimua kufanya hivyo kwa watu wa Afrika kwasababu ya miungu yao, na sanamu zao, na uchawi wao, na uganga wao, na upigaji ramli wao (Isaya 19:3), ambavyo vimefaraka naye.. aliwadhoofisha kwa makusudi ili wajue kuwa hivyo vitu haviwezi kuwasaidia na kwamba wakati umefika sasa Mungu anawahitaji waafrika wamtumike yeye.

Kama tu leo hii, Mungu ameliadhibu bara hili lakini bado unaona waganga na uchawi bado ni mwingi, angaliacha katika mafanikio yake liwe kama mabara mengine yaliyofanikiwa duniani unadhani lingekuwaje? ndio lingekuwa chanzo cha machukizo yote ya ulimwengu mzima kotekote..rohoni na mwilini…Uchawi uliokuwepo kuanzia Misri(ambayo ipo ndani ya Bara la Afrika) ulikuwa ni wa viwango vya juu sana..walikuwa na uwezo wa kubadilisha fimbo kuwa nyoka. Mungu asingeukomesha saa hii ungekuwa umefikia viwango gani?

Hivyo Mungu ametupiga ili tumgeukie yeye hiyo ndio sababu kuu..Na jambo hilo ni kweli limezaa matunda, kwasababu leo hii Neema ya Mungu kweli ipo Afrika, idadi kubwa ya watu waliomaanisha kumtafuta MUNGU ipo Afrika, Hapo ndipo Mungu alipotuponyea..

Kitendo cha sisi kuchukuliwa utumwani, na kutawaliwa na mabepari, kulitufanya sisi tumtafute Mungu wa kweli.

Soma hapa biblia inavyosema..

Isaya 19:20 “Nayo itakuwa ishara na ushuhuda kwa Bwana wa majeshi katika nchi ya Misri; kwa maana watamlilia Bwana kwa sababu ya watu wawaoneao, naye atawapelekea mwokozi mwenye kuwatetea, naye atawaokoa.

21 Na Bwana atajulikana na Misri, na Wamisri watamjua Bwana katika siku hiyo; naam watamtumikia kwa dhabihu na matoleo, nao watamwekea Bwana nadhiri, na kuzitekeleza.

22 NAYE BWANA ATAPIGA MISRI, AKIPIGA NA KUPONYA; NAO WAKIRUDI KWA BWANA, ATAKUBALI MAOMBI YAO NA KUWAPONYA.

23 Katika siku hiyo itakuwako njia kuu itokayo Misri na kufika hata Ashuru; Mwashuri atafika Misri, na Mmisri atafika Ashuru, na Wamisri wataabudu pamoja na Waashuri.

24 Katika siku hiyo Israeli atakuwa wa tatu pamoja na Misri na Ashuru, watakuwa baraka kati ya dunia;

25 kwa kuwa Bwana wa majeshi amewabariki, akisema, WABARIKIWE WATU WANGU MISRI; na wewe Ashuru, kazi ya mikono yangu; na wewe Israeli, urithi wangu”.

Unaona, Mstari wa 21 unatuambia waafrika watajulikana na Bwana, watamtumikia kwa dhabihu na matoleo.. Lakini vilevile anasema atapiga na kuponya… na mstari wa 25 Mungu anasema, WABARIKIWE WATU WANGU MISRI.

Hivyo suala la umaskini wa Afrika, limeruhusiwa kabisa kwasababu hii, ili tumrudie yeye kwasababu anatupenda..

Umaskini wetu umesababishia utajiri wa Imani kwa Mungu..na ndio maana biblia inasema..

Yakobo 2:5 “…..Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao”?

Hivyo itakuwa ni jambo la kushangaza, Mungu amekuweka wewe na mimi katika nchi kama hizi, halafu bado huielewi sauti ya Mungu inataka nini kwako hutaki kuyasalimisha maisha yako kwa Bwana Yesu anayekupenda… Unaishi katika nchi ambazo utasikia injili kila kona ya barabara inahubiriwa,..lakini bado unapuuzia na kudhihaki, mataifa mengine wanaagiza wamishionari kutoka Afrika wawapelekee Neno la Mungu, lakini wewe unaichezea neema hii…Sasa hata hichi ukikikosa, ni nini basi utakuwa nacho ndugu?

Kumbuka hata hivyo neema hii nayo haitadumu huku milele, hivi karibuni Mungu atairejeza Israeli ilipoanzia, biblia inatabiri hivyo, na hapo ndipo mataifa yote ulimwenguni yataurudia upagani waliokuwa nayo mwanzoni na kwa pamoja sasa yatafanya kazi na mpinga-Kristo, ili baadaye yaje kuungana kuishambulia Israeli katika vita ile kuu ya mwisho ya Harmagedoni.. (Neema ni kama jua linachomoza upande huu na kuzama upande ule hivyo sio ya kudumu..ni kitu kinachohama..mataifa mengine Neema ya kuisikia injili haipo kabisa..yaani ile nguvu ya kuvutwa haipo…muda wao ni kama ulishapita..Na sisi muda wetu unakaribia kuisha, na neema hii itahamia Israeli..huku itakuwa kuamini injili ni ngumu kama ilivyo mataifa ya magharibi sasahivi)

Lakini sisi tulioipokea neema ya kumwamini YESU KRISTO na sio mtu mwingine yeyote, tutakuwa tumeshakwenda kwenye unyakuo kama haijahamia Israeli..Lakini wewe ambaye unaupenda ulimwengu huu, ambaye bado unaipenda miungu ya ukoo wenu, unakwenda kwa waganga, unapiga ramli, unadharau injili ya msalaba ambayo unapewa leo bure bila malipo yoyote..basi ujiandae tu na kupigwa na mkono wa Bwana kila siku, na baadaye kuishia katika ziwa la moto..

Hizi ni nyakati za hatari, na kila siku tunaona mabadiliko ya dunia..muda huu ni wa nyiongeza tu, Unyakuo ni wakati wowote, parapanda italia wafu watafufuka.. Je! Umejiweka tayari..Jibu lipo moyoni mwako.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Mitume wote waliopita walikuwa ni watu weupe hata manabii wote waliopita hadi Ma-papa ni ngozi nyeupe. ni kweli ngozi nyeusi ililaaniwa ?

WAKAMTUKANA MUNGU, WALA HAWAKUTUBU.

MJUMBE WA AGANO.

KIFO CHA MTAKATIFU POLIKAPI (Policarp).

UVUMILIVU WA MUNGU ULIPOKUWA UKINGOJA.

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOWAFUNULIA WATU MAANDIKO.

MAONO YA NABII AMOSI.

UNYAKUO.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest


2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

Mungu akubariki