Nguvu za Mungu ni nini?, Nguvu ya Imani ni nini? Na jinsi gani ya kupokea nguvu za Mungu..
Karibu tujifunze maswali haya machache..
NGUVU ZA MUNGU NI NINI?
Kabla ya kuelewa nguvu za Mungu ni nini, ni vizuri tukajua maana ya nguvu.. “Nguvu maana yake ni uwezo wa kufanya kitu au jambo”..Kwahiyo nguvu za Mungu ni uwezo wa Mungu kufanya mambo…Nguvu hizo zinapomwingia mtu, Mtu huyo anakuwa na uwezo wa kufanya jambo kama Mungu.
Sasa tukitazama ulimwengu tunaweza kuona vitu vilivyoumbwa..ikiwa na maana kuwa ilitumika nguvu fulani kuviumba vitu hivyo..Na hiyo ni dhahiri kuwa sio nguvu inayotokana na chakula..kwasababu hakuna mtu mwenye misuli mikubwa anayetegemea misuli iliyotengenezwa na chakula anachokula mwenye uwezo wa kulining’iniza jua kule juu kabisa, au kuujaza mlima kwa mawe na udongo kwa kiwango kile…Hiyo inamaanisha kuwa ni lazima kuna nguvu nyingine imetumika kufanya hayo..isiyotokana na chakula. Sasa kuivumbua nguvu hiyo iliyoyafanya hayo yote ndio tunarudi kwenye kitabu kinachoitwa biblia kupata jibu lake.
Waebrania 11:3 “Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri”.
Kwa kupitia mstari huo tunaweza sasa kupata majibu yetu kwamba vitu vyote Mungu aliviumbwa kwa Imani. Hivyo Imani ndio Nguvu ya Mungu…Na imani ya KiMungu inaposhuka ndani yetu nasi pia tunakuwa na nguvu za kufanya makubwa kama aliyoyafanya Mungu wetu.
Na tafsiri ya Imani tunaipata katika biblia hiyo hiyo..
Waebrania 11:1 “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.”.
NGUVU YA IMANI
Imani ina uwezo wa kufanya mambo makubwa ambayo kwa namna ya kawaida yanaweza kuonekana kama hayawezekaniki…Biblia inasema kwa Imani mtu anaweza kuhamisha milima.(1Wakorintho 13:2)
Luka 17:6 “Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii”.
Mathayo 17:20 “amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.
NAMNA YA KUPOKEA NGUVU ZA MUNGU.
Kama tulivyotangulia kusoma kwamba nguvu za Mungu ni IMANI, Hivyo kupokea nguvu hizo ni sawa na kusema kupokea Imani kama ile ya Mungu.
Sasa namna ya kuipata hiyo Imani ambayo ndiyo nguvu zenyewe za Mungu tunaisoma kwenye Biblia kama ifuatavyo.
Warumi 10:17 “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo”.
Unapolisikia Neno la Kristo na kulitafakari na kulielewa..kiwango fulani cha Imani kinajengeka ndani yako..na ujasiri unaongezeka pia..na mtu anavyozidi kulielewa zaidi na zaidi ndivyo imani yake inavyozidi kukua zaidi na zaidi…mpaka anapofikia kiwango cha kufanya makubwa.
Hivyo Neno la Mungu ndio Biblia takatifu, na ndio Neno la Kristo…Popote panapozungumziwa Neno la Mungu ndio hilo hilo neno la Kristo, na ndio hiyo hiyo Biblia takatifu…maneno hayo matatu yasikuchanganye.
Ukiwa na nguvu hizi za Mungu za kutosha hakuna chochote kitakachoweza kukushinda kama vile kwa Mungu hakuna chochote kinachoweza kumshinda sasa…kwasababu ana nguvu nyingi.
Je unataka leo uanze kupokea Nguvu hizi za Mungu?..anza kwa kulisoma Neno hili la Kristo na kulitii…
Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;
30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.
Ukilisoma Neno hili na kulielewa na kukata shauri la kutubu na kumfuata Yesu kwa moyo wako wote..utakuwa ndio mwanza wa kupokea Nguvu za Mungu.
Bwana akubariki sana.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mafundisho mengine:
Mada Nyinginezo:
About the author