USIHUSISHE HISIA KATIKA KUMTOLEA MUNGU.

USIHUSISHE HISIA KATIKA KUMTOLEA MUNGU.

Sadaka kubwa na ya kwanza ambayo ina thamani kubwa sana mbele za Mungu ni MAISHA YETU. Tunapoyatoa Maisha yetu kwake kwa kumwamini Mwanawe Yesu Kristo, na kuuacha ulimwengu, na kumuishia yeye kwa kuzishika amri zake na kuifanya kazi yake…hiyo ni sadaka kubwa na ya kwanza inayompendeza Mungu na sio mali zetu. Sadaka ya Maisha yetu ina majibu makubwa na thawabu kubwa sana…na thawabu yake kuu ni Uzima wa milele.. Yaani kuishi Maisha yasiyo na mwisho baada ya Maisha haya…Unayatoa Maisha yako sadaka ya miaka hii 80 au 90 au 100 tunayoishi…na unapata thawabu ya kuishi miaka milioni mara milioni…isiyo na uzee, shida, dhiki wala mateso.

Hivyo ni muhimu sana kuyatoa Maisha kuwa sadaka kwa Mungu wetu..Kwasababu hata yeye sadaka kubwa aliyoitoa kwa ajili yetu ni Maisha ya mwanawe mpendwa…Hivyo na sisi sadaka kubwa tunayoweza kumrudishia ni kuyatoa Maisha yetu kwake.

Lakini Pamoja na hayo, sadaka nyingine ya muhimu ni ya mali zetu. Tunapotoa mali zetu kwaajili ya Mungu wetu tunajitengenezea daraja kubwa la kubarikiwa hapa duniani. Wengi wanajiuliza je ni kiasi gani ninachopaswa kumtolea Mungu?…Kiasi mtu anachopaswa kumtolea Mungu ni kiwango chochote ambacho si kilema…Kilema maana yake ni kitu chenye kasoro/mapungufu.. Hicho hatupaswi kumpelekea Mungu wetu kwasababu tukifanya hivyo ni kumdharau na kumvunjia heshima..Mungu aliyeziumba nyota na mbingu hastahili makombo yetu..anastahili vilivyo bora.

Mfano wa sadaka kilema ni hii…Umepata laki mbili halafu unampa Mungu aliyekupa pumzi sh efu 1 tu au mia 5 na hiyo nyingine unaifanyia mambo yako ya kimaendeleo…Hiyo ni sadaka kilema..Hali kadhalika sadaka isiyo kilema ni ile umepata ya sh. Elfu 5 unamtolea Mungu elfu 2 au 3 au 4 au hata elfu 5 yote. Hivyo unaweza ukatoa kiwango sawa na mtu mwingine lakini sadaka yako ikawa ni kilema kutokana na mapato unayoyapata ukilinganishwa na mwenzako.

Sasa kuna jambo moja la muhimu la kujifunza. Wengi wanapenda kujionea huruma, au kuonea huruma wengine….Nataka nikuambie ndugu mpendwa…katika suala la kumtolea Mungu hakuna kuoneana huruma wala kumwonea mtu huruma…Umepata elfu 5, na umepanga kumtolea Mungu yote…basi fanya hivyo usianze kujionea huruma utabakiwa na nini, utakula nini, itakuwaje baada ya hapo!…Kama una moyo wa kujihurumia basi usitoe kabisa…lakini katika kumtolea Mungu hakunaga HISIA. Ni aidha unamtolea Mungu au humtolei..basi!.

Ibrahimu alipotaka kumtolea Mungu mwanawe..aliweka kando hisia. Ingawa alikuwa na chaguzi aidha kukubali au kukataa…lakini yeye alikubali kwa kuishinda hisia.

Eliya naye alipofika kwa yule mjane..alimwambia niandalie kwanza mimi na kisha ujifanyie wewe na mwanao, hakuanza kwa kuanza kumhurumia oo ampikie kwanza mwanawe ndipo na yeye apikiwe, hakikuwepo hicho kitu,.….Hivyo yule mwanamke naye alikuwa na chaguzi mbili mbele yake, kujihurumia kwanza yeye na mwana au kumsikiliza yule nabii mzee anayekuja kutaka kula chakula cha mwanae…alikuwa na chaguzi hakulazimishwa…Hivyo aliamua kuikataa huruma yake na mwanawe na kumtolea Mungu…Na kama tunavyoijua ile Habari…baada ya pale, lile pipa halikupunguka.

Utasema hiyo ni Agano la kale… watu walikuwa wagumu na sheria zilikuwa ni kali, vipi kuhusu agano jipya?

Katika Marko 12:41 tunasoma Habari, ifuatayo “Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. 42 Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa.

43 Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina;

44 maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia”.

Huyo ni Bwana alikuwa ameketi karibu na chombo cha Sadaka anatazama….mbele yake anaona matajiri wanakuja na kutia noti zao humo…ghafla anatokea bibi maskini na mjane, huyo anamwona anakwenda kutia mule ndani ya hazina senti mbili, kiasi cha nusu pesa (maana yake hata haijakamilika kuitwa fedha kamili)..hicho alichokitoa huyo mama mjane biblia inasema ilikuwa ndiyo riziki yake yote..maana yake hana kitu baada ya pale hata chakula….na mbaya Zaidi alikuwa ni maskini na hana mume, na pengine ni kikongwe tayari.

Sasa tukio hilo Bwana alikuwa analitazama…Lakini tunasoma Bwana hakwenda kumzuia na kumwambia ooh! bibi maskini, ndio hicho tu ulichobakiwa nacho, usikitoe, nenda katumie kununua angalau unga ujipikie chakula chako ule…badala yake alimwacha akitoe hata hicho kidogo alichobakiwa nacho. Kwanini? kwasababu kutoa hakuhusiani na HISIA hata kidogo, hakuangalii hali mtu uliyo nayo au utakayokuwepo nayo baada ya hapo.

Hata Mungu wetu alipotaka kutuletea ukombozi kupitia mwanawe, mpendwa Yesu Kristo hakuangalia HISIA kwamba mwanawe anakwenda kuchapwa mijeledi na kusulubiwa uchi na kuuawa, tena mwanawe asiye na hatia…lakini alimtoa hivyo hivyo, kwasababu utoaji hauhusiani na hisia.

Na vivyo hivyo hata sasa, unapotaka kumtolea Mungu, usianze kujihurumia, kama una moyo wa kujihurumia basi ni heri usitoe kabisa!, hicho ulichopanga kumtolea Mungu kakifanyie shughuli nyingine, lakini kama umepanga kumtolea Mungu usianze kujiangalia hali yako, kwamba mimi niko hivi au vile, halafu bado nikitoe hichi, yaani mimi sina nyumba, sina chakula, sina hiki wala kile halafu bado nimtolee Mungu…ukidhani hizo hisia zako zinamgusa sana yeye!…Kama hazikumgusa kwa yule bibi kizee, aliyetoa senti mbili, ambaye alikuwa hana mume na ni maskini na bado ni mzee, sijui labda wewe matatizo yako ni makubwa zaidi kuliko yale, ambayo yanaweza kuugusa moyo wake akakuhurumia..

Hivyo usianze kutazama hali yako ni kujidanganya mwenyewe na kujizuilia baraka zako..shetani asikufumbe macho kukuletea orodha ya shida zako ili usimtolee Mungu, hayo mawazo yakija yakatae kwa Jina la Yesu. Ni mawazo ya shetani, hata mtu akikuletea hayo mawazo yakatae kwasababu mtu huyo pengine anatumika na shetani pasipo kujijua.

Lakini Pamoja na hayo yote, tunajua mwisho wa Bwana siku zote ni mzuri, Badala ya Isaka kufa badala yake alibarikiwa siku ile, vivyo hivyo badala ya yule mwanamke kufa njaa yeye na mwanae kipindi cha Eliya, alishiba na kusaza kipindi cha njaa na ukame…hali kadhalika hata huyu mjane ambaye alitoa senti mbili zake kwa siri, lakini Bwana alimwona na kumtangaza hadharani, bila shaka alipotoka pale alipewa vitu vingi na wale waliokuwa wanamheshimu Bwana, ingawa biblia haijasema..lakini ni wazi kuwa baraka zake zilianza palepale baada ya Bwana kumtangaza kiwango alichokitoa…Hivyo faida za kumtolea Mungu bila kuhusisha hisia ndio hizo mwisho wake…Lakini tukimsikiliza shetani na kuziheshimu hisia hatutaambulia chochote…Tutaishia kuona kwamba Mungu yeye anafilisi tu watu na hana huruma.

Bwana akubariki sana.

Mwisho kabisa, Kama bado hujaokoka, unasubiri nini?.. unasubiri kufa ghafla katika dhambi na kushuka kuzimu? Au unasubiri kuachwa kwenye unyakuo? Au unangoja dhiki kuu ambayo ipo karibuni kuanza?. Nakushauri uokoke kwasababu hizi ni siku za mwisho, sio wakati wa kujivuni dini wala dhehebu..Mifumo ya Dini na madhehebu, ndiyo itakayohusika kwa sehemu kubwa kuiunda ile chapa ya mnyama, ambapo itafika wakati mtu asipokuwa nayo hataweza kuuza wala kununua.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Je! ni vema kwa mkristo kwenda hospitali au kutumia miti shamba anapougua?

Je! kuchora tattoo ni dhambi?

Ni sahihi kumuita Mariamu mama wa Mungu?

WINGU KUBWA LA MASHAHIDI.

KWANINI MUNGU ALIMTUMIA MUSA KWA VIWANGO VILE?

UJIO WA BWANA YESU.

NAO WAKADHANI YA KUWA YUMO KATIKA MSAFARA;

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments