Shalom,
Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima. Karibu tena tujifunze maneno ya uzima wa milele.
Yohana 1:35-39 inasema..
“Tena siku ya pili yake Yohana alikuwa amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi wake. 36 Akamtazama Yesu akitembea, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu!
37 Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu.
38 Yesu aligeuka, akawaona wakimfuata, akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi?
39 Akawaambia, Njoni, nanyi mtaona. Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. NAYO ILIKUWA YAPATA SAA KUMI”.
Unaweza ukajiuliza kulikuwa na umuhimu gani kwenye Habari hii kutoa muda ambao Yesu aligeuka na kuzungumza na wale wanafunzi wawili..?Ambao muda wenyewe ulikuwa ni saa kumi?..Ulishawahi kujiuliza umuhimu wa huo muda kuwekwa pale?. Wakati mwingi tunaweza kuona ni kawaida tu lakini, kila jambo lina sababu yake,.
Tukiitafakari tangu juu Habari hiyo utaona wanafunzi hao ambao mmojawapo alikuwa ni Andrea, walipoonyeshwa tu Yesu na Yohana mbatizaji , mara moja waliacha kumsikiliza Yohana na kuanza kumfuata Bwana kwa nyuma tena kimya kimya…
Hawakusubiri apotelee mbali kwasababu kumbuka wakati huo Yesu alikuwa anakatiza njiani, pengine alikuwa anatembea kwa mwendo wa kasi kidogo hatujui, lakini hawakumwacha apotee mbele ya macho yao.. waliendelea kumfuatilia hivyo hivyo mpaka wajue anapokaa, japo biblia haijaandika ni kwa muda gani waliutumia kumfuatilia , pengine jambo hilo lilianza majira ya asubuhi labda kwenye saa nne nne hivi , au saa 6, au saa 7 hatujui.. Lakini walimfuatilia kwa muda tu.
Hawakujua kuwa Bwana alishagundua kuwa kuna watu wawili wanamfuatailia kwa nyuma tangu mbali..wao hawakuligundua hilo, walidhani Bwana bado hajui chochote..
Ghafla tu majira fulani yalipofika kwenye saa kumi alasiri wakashangaa Bwana amewageukia, na kuwauliza.. ,
Mnatafuta nini? Pengine kwa hofu kidogo hawakuwa na cha kusema.. wakajibu Rabi unakaa wapi?.. Ndipo Bwana akawachukua na kwenda kuwaonyesha anapokaa, wakakaa naye siku ile yote..
Hiyo ilikuwa ni saa kumi alasiri Kabla jua halijazama walimpata Yesu.
Ndugu mpendwa,
Biblia inatuhimiza kuwa tutafute nasi tutaona kwasababu kila atafutaye ataona..
Leo hii unaweza ukawa unamtafuta Kristo, unaonyesha bidii kujifunza Neno lake, unafuata nyendo zake, nakwambia haijalishi itakugharimu muda mrefu kiasi gani kumtafuta, lakini ni uhakika kuwa kabla jua lako halijazama utamwona Kristo. Kristo hawezi kuruhusu mpaka giza liingie bado upo tu katika hali hiyo hiyo ya kumtafuta yeye. Hayupo hivyo..alisema kila atafutaye ni lazima apate.
Siku moja moja atajidhihirisha kwako, atajifunua kwako, kwa namna ambayo hakuifanya hapo mwanzo.
Watu wengi leo hii wamekata tamaa, kumtafuta Bwana, kisa miezi imepita, miaka kadhaa imepita, hawaoni Mungu akichua hatua yoyote maishani mwao? Hawajui kuwa, Bwana alishaona bidii yako ya kumtafuta Kristo tangu zamani, Lakini muda wako wa saa kumi ulikuwa haujafika..
Mtazame, Simeoni, yeye alikuwa ni mtu mwenye haki, lakini Mungu alimwambia kabla hujafa, utamwona Masihi.. Kati ya mabilioni ya watu waliokuwa duniani wakati ule, yeye ni mmoja kati ya watu wachache sana waliomtambua Kristo kuzaliwa kwake(Luka 2:25).
Hakuna mtu anayemtafuta Mungu, Mungu akamwacha, asijifunue kwake.
Lakini Saa kumi yako itafika tu, siku fulani, wakati fulani, majira fulani..Atakugeukia, na kujifunua kwako kwa namna isiyo ya kawaida, Na atakufahamisha mengi sana.
Usikate tamaa.
Luka 11:9 “Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; TAFUTENI, NANYI MTAONA; bisheni, nanyi mtafunguliwa.
10 Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.
11 Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?
12 Au akimwomba yai, atampa nge?
13 Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni HATAZIDI SANA KUWAPA ROHO MTAKATIFU HAO WAMWOMBAO?”
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
MKARIBIE BWANA ZAIDI ILI UFANYIKE NGUZO.
ALIYE MKUU KATIKA UFALME WA MBINGUNI.
KIFO CHA MTAKATIFU PERPETUA NA FELISTA.
MTANGO WA YONA.
Ni sahihi kumuita Mariamu mama wa Mungu?
KUWA WEWE.
About the author