Unapomwona maskini na kumhurumia na kuamua kumsaidia kwa kile alichopungukiwa, na kuifanya huzuni yake iondoke, hapo ni sawa na umeichukua huzuni yake, unapokutana na mtu ambaye hana chakula kabisa na ukaamuhurumia na kuamua kumpa kile chakula kidogo ulichokuwa nacho wewe ambacho ungepaswa ukile wewe, hapo ni sawa umeichukua njaa yake na kujitwika juu yako,Unapomwona mtu anakwenda kufa na wewe ukajitoa kufa kwa niaba yake, hapo ni sawa na umeichukua mauti yake.
Na kwetu sisi wanadamu ndio hivyo hivyo, kwa dhambi zetu tulistahili kufa, tulistahili kupotea kabisa lakini alitokea mmoja aliyetuhurumia ambaye hakustahili kufa, hakustahili kupotea, hakustahili kuadhibiwa akachukua hayo matatizo yetu yote na kujitwika juu yetu ili sisi tuwe huru..
Ndio hapo ili kwamba sisi tusife hana budi yeye kufa kwa niaba yetu, ili kwamba sisi tusiadhibiwe hana budi yeye kuadhibiwa kwa niaba yetu na hiyo yote ni kutokana tu na huruma yake kwetu sisi..
2 Wakorintho 8:9 “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake”.
Ili kwamba upande mmoja uwe na vingi na lazima upande mwingine upungukiwe, ili kwamba sisi tupone ni lazima mmoja aangamie, hiyo ndiyo sababu Bwana Yesu Kristo alikufa kwa ajili yetu ili kwamba sisi tupate uzima wa milele…kulikuwa hakuna njia nyingine ya mkato ya sisi kuokolewa bila ya njia hiyo ya mmoja kuchukua matatizo ya mwingine…hata mahakamani pasipopatikana mdhamini hakuna kuachiwa huru..Ndio maana Biblia inasema..
Yohana 1:29 “Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!”.
Na kama alichukua matatizo yetu na kujitwika juu yake ni dhahiri kuwa kwa hali ya kawaida asingepaswa kufufuka tena, kwasababu makosa yetu sisi yalistahili adhabu ya milele…Lakini SIRI iliyopo kubwa hapo ni kwamba, Kristo alifufuka tena, kwa ukamilifu wake alisimama na kushinda hoja! Hivyo mauti ikashindwa juu yake, kuzimu ikashindwa juu yake, na hivyo akavishinda vyote na kufufuka bila dhambi yoyote..Hatia yote aliishinda.
Waebrania 9:28 “Kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu”.
Ni sawa na wewe ukutwe na makosa fulani yanayostahili kufungwa kifungo cha maisha, halafu atokee mtu na kuichukua kesi yako wewe na ashtakiwe kwa kupandishwa kizimbani kabisa na ahukumiwe na kufungwa, na kisha baada ya siku chache unamwona mtaani yupo huru, anakwambia kesi imekwisha! Wote tupo huru wala usiwe na wasiwasi… Lazima utajiuliza ni nini kimetokea?..aidha katoroka gerezani au labda kesi yake imerudiwa kusikilizwa tena na ikatokea kashinda hoja? Yatakuwepo maswali mengi yasiyo na majibu!..Na zaidi ya yote huyo kukuondolea wasiwasi anakwambia nimekabidhiwa UJAJI MKUU wa Taifa lote, hukumu zote zipo chini yake na wafungwa wote wapo chini yake.
Na ndicho kilichotokea kwa Bwana Wetu Yesu Kristo, alijitwika kesi yetu na kuhukumiwa kufa, ambapo sisi ndio tungestahili kufa lakini baada ya siku chache, alifufuka na kutoka kaburini na kuwaambia wanafunzi wake…Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani”.
Bwana Yesu kwasasa ndiye aliye mhukumu wa watu wote walio hai na waliokufa..
Matendo 10:40 “Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika,
41 si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndio sisi, tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu.
42 Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na wafu”.
Lakini Neema hiyo Kristo aliyoibeba sio kwa watu wote!..Ni kwanini sio kwa watu wote? Ni kwasababu sio watu wote watapenda au watataka wokovu, wengine hawatataka kuokolewa, hivyo haiwezekani kuwalazimisha..Kila mtu Mungu kampa uhuru wa kuchagua apendalo, UZIMA au MAUTI.
Kumbukumbu 30: 15 “Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya;”
Yesu ndio Nuru ya ulimwengu, chagua Nuru leo ambao ndio UZIMA, na si giza..Kwasababu wengi katika siku hizi za mwisho watachagua giza na wala si Nuru kwa hiari yao wenyewe..kama maandiko yanavyosema.
Yohana 3: 18 “Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.
19 Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.
20 Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa”.
Kama hujasalimisha maisha yako kwake ni vyema ukafanya hivyo leo kwa kutubu dhambi zako zote kwa kudhamiria kutokurudia kuzifanya tena, na kutafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Bwana Yesu Kristo, kwaajili ya ondoleo la dhambi zako(sawasawa na Matendo 2:38 inavyosema).na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi.
Kwa kufanya hivyo utakuwa umeutua mzigo wako wa dhambi na Bwana Yesu atakuwa amekuingiza miongoni mwa wale waliochukuliwa dhambi zao na hivyo utakuwa umenusurika na hukumu ya Mungu itakayoijilia ulimwengu wote kipindi sio kirefu kijacho..
Bwana akubariki sana.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
TOFAUTI KATIKA YA ZAKA NA SADAKA NI IPI?
Madhabahu zote wana wa Israeli walizomjengea Mungu ilikuwa ni lazima wazijenge katika mahali pa juu, hivyo ndivyo walivyoagizwa na Mungu, mahali ambapo pameinuka, au waiinue madhabahu yenyewe juu,..kwasababu maana ya neno lenyewe madhabahu ni ‘”palipo inuka”, hakukuwa na nama yoyote madhabahu ikajengwa bondeni, au shimoni na Mungu alifanya hivyo makusudi kufunua mambo makubwa kiroho, jambo hilo hilo hata wapagani baadaye walikuja kuliiga, nao pia madhabahu zao wakawa wanazijenga sehemu za juu, au wanazinyanyua juu, na ndio maana utasoma kwenye biblia sehemu nyingi wakati wa enzi za wafalme, Bwana anawakemea wayahudi kwa makosa yao ya kutokuziondoa sehemu za juu,..akiwa na maana ya madhabahu zao za sanamu walizozijijengea kwa uchawi wao, Shetani siku zote ni mwigaji, hakuna jambo jipya alilowahi kulibuni yeye mwenyewe, alipomuona Mungu anawaagiza wana wa Israeli watoe kafara za wanyama kwa ajili ya upatanisho wa dhambi zao, yeye naye akaiga mambo hayo hayo, na ndivyo ilivyokuwa hata katika madhabahu zake.
Sasa wakati madhabahu ilipojengwa na kunyanyuliwa juu, mtu yeyote atakayeiendea ambaye ni kuhani alipewa masharti ya kuiendea na mavazi rasmi ya kuvaa. Kuhani mkuu au kuhani yoyote ilikuwa ni lazima avae mavazi ya kumsitiri mwili wake wote, hivyo ziliandaliwa kanzu nzuri za kitani, ndefu, ambazo mtu akivaa hizo zilimsitiri mwili wake wote, lakini hiyo peke yake haikutosha kumsitiri mtu maeneo yote, kwani wakati wa kuiendea madhabahu ambayo imenyanyuliwa ni lazima utapandisha ngazi ili kuifikia juu, na hivyo kanzu kwa upande wa chini huwa haisitiri, kunakuwa wazi, na ilikuwa mfano uchi wao ukionekana tu madhabahuni pa Mungu ilikuwa ni mauti, Mungu mwenyewe anakuua.
Kutoka 20:26 “Tena hutapanda kwenda madhabahuni kwangu kwa daraja, uchi wako usidhihirike juu yake.”
Hivyo kutatua tatizo hilo, Bwana akawapa makuhani wake wote amri kuwa watengenezewe suruali ambazo watazivaa kwa ndani ili kusudi kwamba watakapopanda kwenda madhabahuni, uchi wao usionekane kwa chini, wawe salama.
Kutoka 28:39 “Na hiyo kanzu utaifuma ya kitani nzuri ya kazi ya urembo, ufanye na kilemba cha nguo ya kitani nzuri, nawe utafanya mshipi wa kazi ya mwenye kutia taraza.40 Kisha utafanya kanzu kwa ajili ya wana wa Haruni, nawe wafanyie mishipi, wafanyie na kofia kwa utukufu na uzuri.
41 Nawe mvike huyo nduguyo Haruni na wanawe nao mavazi hayo; nawe watie mafuta, na kuwaweka kwa kazi takatifu, na kuwatakasa, ili wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani.
42 Nawe wafanyie suruali za nguo ya kitani, ili kufunika tupu ya miili yao; suruali hizo zitafika tangu kiunoni hata mapajani;43 na Haruni na wanawe watazivaa, hapo watakapoingia katika hema ya kukutania, au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike katika mahali patakatifu; wasije wakachukua uovu, wakafa; hii itakuwa ni amri ya milele kwake yeye, na kwa wazao wake.”
Lakini tunapaswa tujiulize mambo haya yanafunua nini katika agano jipya?. Jambo la kwanza ni kwamba Madhabahu ya Mungu tunayomwabudia katika Roho imenyanyuka sana tena imenyanyuka juu kuliko hata ya akina Haruni nayo ipo mbinguni na sadaka yake juu yake, ambayo ni Bwana wetu Yesu Kristo, Vyote hivi vipo mbinguni.
Hivyo tunapokwenda mbele ya madhabahu hii, kupeleka mahitaji yetu, au kumfanyia Mungu ibada, tunapaswa tuwe makini sana, kwanza tunapaswa tuwe tumesitiriwa sio tu kwa mavazi ya nje, bali pia na kwa yale ya ndani vinginevyo tunaweza tukajiona tupo sawa lakini kumbe tunajitafutia kifo, badala ya uzima.
Mavazi ya nje ni yapi?. Ni mwonekano wako wote wa nje kwa ujumla,.Ikiwa leo hii unaweza kutembea barabarani na vimini wewe kama mwanamke na suruali na nguo zinazochora maungo yako..na kibaya Zaidi huoni hata aibu kuingia nazo katika nyumba ya ibada, madhabahuni pa Mungu na mavazi hayo ni dalili kubwa ya kujichumilia mauti. Vile vile unakuwa mlevi, na bado unakwenda mbele za Mungu, huko ni kujitafutia kifo ndugu, kama umeamua kuwa baridi ni heri ukawa baridi kwelikweli, kuliko kuwa vuguvugu.
Mtume Petro wakati anavua akiwa nusu uchi, Bwana alipotokea alijitupa kwenye maji kuficha uchi wake, kwasababu ya kumheshimu Bwana, na yeye alikuwa ni mwanamume…
itakuwaje kwako wewe mwanamke! Mbele ya Bwana? Unafikiri unapaswa ujisitiri kiasi gani?
Vilevile mavazi ya ndani, ni mambo yaliyo moyoni mwako, mambo ambayo kwa nje hayawezi kuonekana lakini kwa ndani hayaelezeki kwa jinsi yalivyo mabaya, mfano wa wale mafarisayo na waandishi Bwana Yesu aliowazungumzia..
Mathayo 23:28 “Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi”.
Ndani unayo chuki na watu, unao wivu, ndani umewawekea wengine vinyongo na vikwazo, ndani umeweka kisasi halafu bado unapanda madhabahuni pa Mungu kwenda kumwomba, au kumfanyia ibada, hapo ni sawa na kuhani aliyevaa kitani nzuri ndefu ambayo kwa nje unaonekana kweli wewe ni mwema lakini mbele za Mungu upo uchi..
Hiyo ni mbaya sana, unatazama pornography kwa siri, unazini kwa siri kwasababu wanakwaya wenzako hawajakuona unadhani pia Mungu hakuoni, unakwenda disco kisirisiri, lakini huku nyuma unakwenda kumwimbia Mungu na kumwabudu..Nataka nikuambie ni heri usifanye kabisa au utubu uamue kumwishia Mungu.
Fahamu kuwa kanisa hili tunaloishi ndilo kanisa la saba lijulikanalo kama kanisa la Laodikia, na ndio la mwisho, na kama huufahamu ujumbe wa kanisa hilo unaweza kusoma katika Ufunuo 3:14-21 uone kama tabia zinazozungumziwa pale haziendani na ukristo uliopo sasa?. Hili ni kanisa vuguvugu, ambalo linajiona kuwa Tajiri lakini ni uchi, maskini na dhaifu..
Ufunuo 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.
19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.
22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”
Unaona hapo? Bwana anatupa shauri tununue kwake mavazi meupe aibu ya uchi wetu isipate kuonekana, “kumbuka huo ni ushauri sio lazima”..na mavazi hayo anayoyazungumzia ni yale ya nje na ya ndani. Ndugu usipumbazwe na mambo mengi maovu unayoyaona sasahivi ulimwenguni. Yalitabiriwa yatakuwa hivyo na kuzidi kuongozeka katika siku za mwisho,. Lakini pia Bwana alituahidia sisi wa kanisa la Mwisho la Laodikia thawabu kubwa kuliko makanisa mengine yote yaliyotutangulia ikiwa tutashinda.
Tafakari aliposema tutaketi pamoja naye Mfalme wa wafalme, Bwana wa Mabwana Yesu Kristo katika Enzi yake, hilo sio jambo dogo. Hivyo kwa mtu yoyote mwenye akili timamu atayahesabia Maisha haya ya kitambo tu kuwa si kitu cha kulinganisha na thawabu hizo zinazokuja.
Hivyo ndugu, ikiwa bado upo nje ya Kristo, Usiipuzie hii neema iliyopo sasa. Tubu kwa kumaanisha kabisa kuacha dhambi, kisha uende ukabatizwe kulingana na maandiko kwa kuzamishwa katika maji mengi kwa jina la BWANA YESU ukapate ondoleo la dhambi zako, na Bwana atakupa kipawa cha Roho mtakatifu (Matendo 2:38).
Bwana yupo mlangoni kurudi, naye mwenyewe anasema anakuja upesi! Na wala hatakawia.
Ubarikiwe sana.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
MAVAZI YAPASAY KUVALIWA NA WANAWAKE NI YAPI?
JE! NI DHAMBI KWA KIJANA ALIYEOKOKA KUVAA SURUALI ZA KUBANA (MODEL), KUNYOA MITINDO?
Unaweza ukawa ni mchungaji mzuri,au mwalimu mzuri wa Neno la Mungu, unaweza ukawa una mafunuo mengi na kufahamu mambo mengi, lakini je! Katika huduma yako au utumishi wako unalitumia kwa halali Neno la kweli?. Mtume Paulo alimwambia Timotheo Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali.(2Timotheo 2:5). Unaona? tuchukulie mfano wanariadha, ikiwa mtu atatumia dawa za kusisimua misuli ili awe na pumzi zaidi ya wengine pale atakapokimbia, ni kweli anaweza akawa mshindi lakini hatapewa taji pale atakapobainika kafanya hila katika huo mchezo, kwasababu hajashiriki kwa halali katika michezo, au ikiwa mtu ataanza kukikimbia kabla ya kipenga kupigwa, huyo naye atatolewa katika mashindano kwasababu hajashiriki kihalali katika michezo, vilevile ikiwa waliagizwa wazunguke uwanja mara 10, lakini akatokea mmojawapo kakaidi amri na kukatisha katikati ya uwanja..Tunajua ni kitu gani kitakachofuata, bila shaka atapigwa Penalti na atatolewa katika mashindano hata kama ilikuwa imebaki mzunguko mmoja amalizie na ushindi, hiyo yote ni kwasababu hajashiriki kihalali.…
Vivyo hivyo katika mienendo yetu tunapolipeleka Neno la Mungu tusipojifunza Kulitumia kihalali, tunaweza tukajikuta katika hasara na tabu yetu mwisho wa siku inakuwa ni bure.
Na ndio maana mbeleni kidogo Paulo aliendelea kumsisitiza Timotheo maneno haya:
2Timotheo 2:15 “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, UKITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI”
Unaona, anamsihi ajionyeshe kuwa amekubaliwa na Mungu, ajionyeshe kuwa amekomaa katika mashindano ya wokovu, sio mtu atakayeleta aibu mbeleni kwa kushindwa kumaliza ungwe yake vizuri, na ndio tafsiri ya hilo Neno “mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari,” …kutahayari maana yake ni ‘kuabisha’
DALILI IPI ZITAKUTAMBULISHA KUWA HAUTUMII KWA HALALI NENO LA KWELI?
Sababu kuu Paulo ambayo aliitoa pale ni “Mashindano ya Maneno”.
2 Timotheo 2:14 “Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao.
15 Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, UKITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI.
16 Jiepushe na maneno yasiyo na maana, ambayo si ya dini; kwa kuwa wataendelea zaidi katika maovu,
17 na neno lao litaenea kama donda-ndugu. Miongoni mwa hao wamo Himenayo na Fileto,
18 walioikosa ile kweli, wakisema ya kwamba kiyama imekwisha kuwapo, hata kuipindua imani ya watu kadha wa kadha”.
Unaona?, sio hapo tu, sehemu nyingi sana Mtume Paulo alikuwa anamwonya Timotheo ajiepusha na mashindano ya maneno, ambayo madhara yake ni kama donda-ndugu. Donda-ndugu ni kidonda sugu kisichopona, kinakwenda miezi na miezi, miaka na miaka, hata kitibiweje hakitibiki, njia pekee ya kukiondoa ni kukata kile kiungo au lile Eneo. Sasa hiyo imefananishwa na mashindano ya maneno kwa watu wa Mungu, kwa jinsi mtu anavyojizoesha katika hali hiyo ndivyo anavyojiharibu nafsi yake kidogo kidogo, mpaka mwisho wa siku anajikuta anagota katika itikadi Fulani ya kidini ambayo hawezi tena kubadilika hata kama ni ya uongo, anabakia kuwa ni mtu wa mijibizano tu na mashindano ya itikadi zake siku zote, na ndio watu kama hao mwisho wa siku wanazama katika mafundisho potofu ambapo kuwatoa huko haiwezekani tena….
Mungu hakai katika mashindano, ikiwa mtu kakusudiwa kuamini ataamini, kama haamini, hawezi kuamini, pengine sio wakati wake huo. Ndugu ikiwa umepewa neema ya kuwa mhubiri wa injili basi usitumie karama yako kuwa mtu wa mashindano, hayo hayawezi kumjenga mtu zaidi yanamuharibu tu Yule asikiaye, ‘tutumie kwa halali Neno la kweli’,..Tudumu katika mfundisho ya Neno la Mungu..
Leo utaona kuna mijadala baina ya wa-kristo na waislamu, tazama kwa makini uone kama kuna mtu yeyote anajegwa au anavutwa kwa Kristo kwa malumbano yale..kinyume chake unazaliwa ugomvi, matusi na mizaha, hata wale ambao walikuwa wanaonyesha dalili za kuja kwa Kristo, wakiona machafuko yale ndio wana-kwenda mbali zaidi, hiyo yote ni kwasababu hatulitumii kwa halali Neno la Kweli, na hivyo mbele za Mungu tunatapanya badala ya kukusanya.
Na ndio maana Mtume Paulo bado alikuwa anaendelea kumsihi Timotheo, tusome:
2Timotheo 2:23 “Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi.
24 Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu;
25 akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli;
26 wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.”
Hivyo Sisi ndio Timotheo wa sasa tukubali maonyo haya ya mitume, tukapokee taji bora lililowekwa mbele yetu.
Bwana akubariki sana.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
TUZO UTAPEWA KULINGANA NA NAFASI YAKO
TUNAPOSEMA TUISHI KWA NENO, INAMAANISHA TUISHI MAISHA YA NAMNA GANI?
MANENO YA MUNGU YANAPINDULIWAJE?
Matendo 2:1 “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.
2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.
3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.
4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.
5 Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu.
6 Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.
7 Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya?
8 Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?
9 Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia”,
10 Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu,
11 Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.
12 Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?
13 Wengine walidhihaki, wakisema, wamelewa kwa mvinyo mpya”.
Hata ilipotimia siku ya Pentekoste!!…Sentensi hiyo inaonyesha ni kama vile siku hiyo tayari ilikuwa imepangwa…na hivyo ni kama vile ilikuwa inangojewa ifike…ni sawa na mtu aseme… “hata ilipotimia siku ya kufikishwa kizimbani” au “hata ilipotimia siku ya kufanya kufanya mtihani”…sentensi hizo zinaonesha kuwa kuna tarehe Fulani zilizokuwa zimepangwa kwa tukio Fulani…Biblia inazidi kusema kuwa “walikuwako wote mahali pamoja”..kuashiria kuwa walishaambiwa wasisambaratike bali wakae pamoja mpaka hiyo siku ifike.
Mstari wa pili unasema 2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi”.
Uvumi uliotokea hapo sio uvumi wa upepo huu wa asili tunaoujua, ambapo ukitokea miti inapepesuka, mapazi yanapeperuka n.k bali ni uvumi wa upepo wa roho, ambao ili kuulezea vizuri biblia imefananisha na kama uvumi wa upepo wa kawaida wa asili…ndio maana hapo biblia inasema UVUMI KAMA, Zingatia hilo neno ‘kama’ ikiwa na maana sio upepo wa kawaida bali ni mwingine wa Roho
Sasa huu ni upepo wa Roho ambao hauwezi kuonekana kwa macho, kazi yake ni kumpeleka mtu mahali ambapo hajataka kwenda kwa nguvu zake mwenyewe, au hajataka kufanya kwa nguvu zake mwenyewe au kutamka kwa akili zake mwenyewe…Huu ndio Bwana Yesu aliosema mahali Fulani kuwa mtu aliyezaliwa mara ya pili anakuwa nao..
Yohana 3:8 “Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho”.
Unaona kila mtu aliyezaliwa kwa Roho Mtakatifu kuna upepo Fulani wa Roho unaompeleka mahali asipopachagua yeye…Kwa urefu juu ya somo hili la upepo wa Roho, unaweza kulisoma mwisho kabisa mwa somo hili.
Sasa uvumi huu wa Upepo wa Roho ulipowashukia hawa watu siku ile ya Pentekoste ni nini kiliwatokea?..Tusome
Mstari unaofuata unasema….. “3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.
4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka”.
Ni wazi kuwa upepo ule ungewasukuma kuzungumza kitu ambacho hawajataka kuzungumza kwa akili zao, kingewafanya waende mahali ambapo hawajataka kwenda kwa akili zao, kama tu vile upepo wa kawaida unapovuma mahali unaweza hata kuezua mabati na kuwahamisha watu kuwatupa mahali ambapo hawajataka kwenda..
Na ndicho kilichotokea hapa, wote wakajikuta wanaanza kuzungumza lugha ambazo kwa akili zao hawajataka kuzizingumza bali wamesukumwa kuzizungumza.
Na biblia inasema kukawatokea “ndimi”…ndimi ni wingi wa neno “ULIMI”..Na ulimi tafsiri yake iliyotumika hapo sio ulimi tunaotumia kula, bali “LUGHA”…Kwahiyo hapo ziliwashukia ‘lugha’…Sasa swali ni je! Ni lugha moja? Au ngapi?…Jibu lipo hapo hapo..’ ‘zikawatokea ndimi zilizogawanyikana’….yaani ziliwatokea lugha zilizogawanyikana…sio lugha moja…bali nyingi, na kila mtu iliyomshukia ilikuwa na tofauti na ya mwenzake…Ni kama tu kilichotokea pale Babeli, kila mtu alijikuta anaongea lugha yake…
Na biblia inasema wote wakaanza kuzungumza kwa lugha mpya, kila mmoja ya kwake tofauti na mwingine, kwa jinsi Roho alivyowajalia..ikiwa na maana kuwa si kwa jinsi ya akili zao bali kwa jinsi Roho alivyowajalia.
Na pia kumbuka Ndimi zilizowatokea zilikuwa ni ndimi za Moto, yaani lugha za moto!..Lugha za moto ni tofauti na lugha za kawaida.
Lugha za moto au ndimi za moto ni lugha ambazo mtu aliyejawa na Roho Mtakatifu anazizungumza ambazo zimejaa Neno la Mungu linalochoma nafsi ya Mtu anayesikia na kumfanya atubu au aache uovu anaoufanya…Na lugha hizi za moto/ndimi za moto hazipo tu kwa wahubiri wanaozungumza kwa njia ya maneno, bali hata kwa waimbaji wanaoimba nyimbo zinazowabadilisha watu wanaosikia na zinazomtukuza Mungu, hizo ndio lugha za moto au ndimi za Moto ambazo pia ziliwatokea hawa watu siku ya Pentekoste.
Kama walikuwa watu 120, pale walipokusanyika, upepo wa Roho uliposhuka, lugha 120 zilitokea pale pale, labda ingekuwa ni nyakati hizi, zingesikika lugha 120 tofauti tofauti watu wale wakizizungumza, kama ni kiingereza, kichina, kimasai, Kiswahili, kimakonde, kifaransa n.k
Na maneno waliyokuwa wanazungumza yalikuwa ni maneno ya kumtukuza Mungu katika hizo lugha walizokuwa wanazungumza, labda mmoja alikuwa anasema…’ ‘wewe Bwana unaweza kwa lugha ya kichina’…mwingine ‘tubuni ufalme wa Mungu umekaribia kwa lugha ya kifaransa’…labda mwingine tena akasikika akisema ‘utukufu una wewe ee Mungu wa miungu kwa lugha ya kiswahili’ n.k
Sasa Yerusalemu kipindi hicho kulikuwa na watu kutoka duniani kote waliokuwa wanakuja kuabudu, kila mmoja akasikia watu wanazungumza kwa lugha ya walikotokea, wakashangaa sana…Ni sawa leo uende kijiji cha china huko katikati kabisa halafu usikie mtu mchina anamsifu Mungu kwa lugha ya kwenu ya kihaya? Lazima utashangaa huyo mtu kajuaje hiyo lugha na hali yeye ni mchina na hajawahi kufika Tanzania na wala hawajui watanzania…Ndicho kilichotokea pale siku ya Pentekoste…watu kutoka kila kona walisikia lugha zao zikizungumzwa Yerusalemu na watu waliojazwa Roho….Na watu kuona hiyo ishara ikawaogopesha sana! Wakawaendea na kuwauliza maana ya mambo hayo ni nini? Ndipo wale waliojazwa na Roho na kusukumwa na upepo wa Roho na kuanza kusema kwa ndimi za moto wakawaambia…
Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.
40 Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi’’.
Unaona maana ya kunena kwa lugha mpya?..sio haya machafuko ambayo tunayaona sasahivi, watu wanazungumza maneno yasiyojulikana na hakuna mtu wa kutafsiri, Roho Mtakatifu hayupo hivyo! Mmoja anaponena lazima wawepo wafasiri anayesikia kile kilichonenwa,kama hapa siku ya pentekoste watu waliokuwa nje walisikia lugha zao za asili hao tayari walikuwa ni wafasiri…sasa endapo wangesikia watu wanazungumza lugha zisizoeleweka na kisha hakuna mtu wa kuwafasiria wangevutwaje kwa Kristo?
Ndugu, ndimi hizi za moto..bado zinapita sasa..Unaposikia injili na unaona unakuchoma ndani ya moyo wako na kukuvuta utubu! Fahamu kuwa ni Roho Mtakatifu anakuvuta kwake…anataka ugeuke uache dhambi na anasa, na mabaya yako yote, akuoshe kwa damu yake.
Biblia inasema hao watu baada ya kuchomwa mioyo yao? Wakawauliza mitume wafanyaje?!…Pengine na wewe una swali hilo hilo leo?…Nifanyaje?..Jibu lipo hapo hapo kwenye biblia mstari unaofuata..
“Tubu ukabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo, upate ondoleo la dhambi”..
Hivyo hapo ulipo tenga dakika chache peke yako, tubia dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha kabisa…unakusudia kuacha uasherati kama ulikuwa unaufanya, rushwa, utukanaji, ukahaba, wizi, ulevi, anasa, ushoga, ulawiti, uuaji, usagaji, utazamaji pornograph, ufanyaji masturbation, n.k na kisha katafute ubatizo sahihi, wa kimaandiko kama ulivyoyasoma hapo juu, ubatizo sahihi ni wa kuzama mwili wote kwenye maji na kwa jina la BWANA YESU huo utakufanya umpe Roho Mtakatifu kibali cha kufanya kazi ndani yako..kwa kufanya hivyo utakuwa umetimiza matakwa yote ya Mungu anayotaka juu ya maisha yako..na kujiweka katika mstari mzuri wa kwenda mbinguni.
Bwana akubariki sana.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
JE! KUNENA KWA LUGHA MPYA KUKOJE?
JE! NI LAZIMA WATU WOTE WANENE KWA LUGHA?
KUWA MAKINI NA MITANDAO, NI SHIMO REFU.
Kama vile wema na fadhili zake hazikomi kutufuata siku zote za maisha yetu basi na Jina la Bwana wetu Yesu Kristo lizidi kubarikiwa daima, Milele na milele.Amina. Karibu tujifunze maneno ya uzima.
Kama wanavyosema ni heri mtu ufe kwa kupigwa rasasi kichwani ambapo ndani ya sekunde chache tu unajua utakuwa umeshaondoka kuliko kufa kwa njaa, kufa kwa kukosa maji au chakula, kwani kifo cha namna hiyo huwa ni cha taratibu na cha mateso ya muda mrefu,.
Biblia yenyewe inakubaliana na hayo maneno tukisoma katika
Maombolezo 4:9 “Heri wale waliouawa kwa upanga Kuliko wao waliouawa kwa njaa; Maana hao husinyaa, wakichomwa Kwa kukosa matunda ya mashamba.’’
Unaona na hiyo sio katika mwili tu, bali pia ipo katika Roho ni heri wale watu ambao Mungu alishawauwa kiroho siku nyingi, kuliko wale watu ambao bado wapo hai, wana hangaika huku na huko kutafuta chakula cha rohoni lakini hawakipati, watu wa namna hiyo kifo chao cha kiroho kinakuwa ni kibaya sana na cha mateso mengi..
Mwanzoni mwa mwaka wa 2007 nikiwa mimi pamoja na ndugu wengine 5,Mungu alituambia waziwazi kwa unabii kuwa kuna kipindi cha ukame kinapita duniani kote, Kwa wakati huo sikujua ni kwa namna gani njaa itakuja nilidhani Neno la Mungu litakuwa halihubiriwi kabisa, Kumbe sivyo.
Sikuzote ili kujipima kama upo katika njaa au haupo, ni uwezo wa kutambua ubora wa chakula unachokula, jaribu kufanya uchunguzi kaa siku moja bila kula kuanzia asubuhi mpaka jioni halafu uletewe maharage ya juzi uambiwe ule, nakuambia utauona ni mtamu kweli, lakini subiri njaa ile iwe imeshapoa halafu uletewe maharage yale yale ule, moja kwa moja utaanza kuona kasoro nyingi zilizopo katika yale maharage ambazo hapo mwanzo hukuziona, pengine utasema maharage gani haya hayana ladha, hajaungwa vizuri kwanza yamechacha, na yamezidi chumvi hayafai kuliwa yataniletea kiungulia..
Husemi hivyo kwasababu ya dharau ya shibe hapana lakini unazungumza ukweli wake kuwa sio bora, Sasa hapo ni kwasababu ile Njaa mwanzoni ilikudanganya hata kwa vitu visivyokuwa na manufaa kwa mwili wako kuviona vinafaa. Biblia inasema:
Mithali 27:7 “Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali; Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu.”
Ndivyo ilivyo katika hizi siku ambazo kila mtu anajua kuwa ni za mwisho, Mungu alisema ataleta njaa duniani kote, si njaa ya kukosa chakula cha kimwili, bali njaa ya watu kukosa kuyasikia maneno yake..
Amosi 8:11 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana.
12 Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione.
13 Siku hiyo wanawali wazuri na wavulana watazimia kwa kiu.
14 Na hao waapao kwa dhambi ya Samaria, na kusema, Kama aishivyo Mungu wako, Ee Dani, na, Kama iishivyo njia ya Beer-sheba, hao nao wataanguka, wasiinuke tena.”
Sababu hiyo basi njaa hiyo inawatafuna watu leo hii kiasi cha kufikia hatua ya kuoana hata yale mafundisho manyonge kuwa ni yenye nguvu..yale mafundisho ya uongo kuwa ni ya kweli.
Kila ufunuo, kila unabii unaokuja hata kama haumjengi mtu, basi utapokelewa tu kwa moyo wote,na watu wanashukuru Mungu kwa huo, hiyo yote ni kwasababu ya njaa. Hata mtu akisema mimi ni YESU au Mungu, huku akitoa maandiko yake machache yanayothibitisha anachokisimamia bado watu wataona ni Neno la Mungu lililo hai …Kusingekuwa na njaa, manabii wa uongo na waalimu wa uongo wasingepata sehemu ya kupelekea mafundisho yao manyonge, lakini kwasababu uhitaji upo mkubwa hata vile feki navyo vinapata soko..kama tu vile simu za kichina.
Ndugu, janga hili la rohoni, linanihusu mimi na wewe, tusipotaka kumwendea na kukaa chini ya Yusufu wetu wa sasa ambaye ni YESU KRISTO, atupaye chakula sahihi cha roho kwa wakati husika..Hakika tutakufa kwa kiu na kwa njaa. Tutazunguka huko na huko, tutakwenda Nigeria, china mpaka ulaya, tukidhani kule ndipo chakula kipo, lakini mwisho wake baada ya mahangaiko hayo na mateso hayo yote tunakufa kwa njaa na kwenda kuzimu. Embu jiulize taabu zako zote, unaishia kwenda kukutana na mlevi kuzimu ambaye hajawahi hata kuwa na shughuli na Mungu.
Ashukuriwe Mungu, Ni Bwana Yesu pekee aliyeahidi atatupa msaidizi ambaye atatufundisha na kuturejesha katika kweli yote..Na msaidizi huyu ni Roho Mtakatifu, mtu yoyote atakayempokea huyu hakika hata potea, wala hatakufa kwa njaa kwani kama alivyoahidi atahakikisha anakaa mahali ambapo chakula halisi cha kweli kipo kwa maana palipo mzoga ndipo watakapokusanyika TAI (Mathayo 24:28)
Unachopaswa kufanya ni kumtii Kristo kwa kumkaribisha aje ndani ya maisha yako akubadilishe uwe kiumbe kipya. Na hiyo inakuja kwa kutubu kwa kudhamiria kabisa kuacha dhambi, na kwenda kubatizwa katika ubatizo wa maji mengi kwa jina lake, kama ishara ya ondoleo la dhambi zako. Kisha ukishafanya hivyo yeye mwenyewe atakuwa na jukumu la kukupa Roho wake Mtakatifu akuongoze na kukutia katika kweli yote(Yohana 16:13). Huyo ndiye atakayekupa wewe nguvu ya kuendelea mbele, wakati wa kipindi hichi kikali cha njaa..
Usijaribu kujitafutia mwenyewe chakula kwa kanuni zako, utakufa kwa njaa..Ndio utafananishwa na hao biblia inayosema “watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione (Amosi 8:12)”…Ni kwasababu gani? Ni kwasababu hawakutaka kufuata uongozi wa Roho Mtakatifu,
Ndugu Roho Mtakatifu ndio salama yetu katika haya majira ya siku za mwisho za njaa tunazoishi. Bila Roho Mtakatifu, Hakuna mbingu wala hakuna kumjua Mungu, bali ni kukisubiria kifo..Mtafute yeye angali yupo, kwa maana ahadi hiyo ni ya kila mtu amwombaye Baba..
“…je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”(Luka 11:13)
Ubarikiwe sana.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO
Yeremia 17:5 “ Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana.6 Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.”
Jina la Bwana libarikiwe, Biblia inasema amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemwacha Bwana.
Matokeo ya kumwacha Mungu moyoni ni kumtegemea mwanadamu, unapoamini kuwa mtu fulani ndio kashikilia hatma ya Maisha yako, huko ni kumtegemea mwanadamu…
Unapoziamini methali za wanadamu na kuliacha Neno la Mungu huko ni kumtegemea mwanadamu, Unapoamka asubuhi na jambo la kwanza ni kumfikiria boss wako na hata humshukuru Mungu kwa kukuamsha salama, huko ni kumtegemea mwanadamu,
Unapotii maagizo ya watu fulani waliokuzunguka na kuyadharau maagizo ya Mungu, kwa kisingizio usipotii utakosa kazi, utakosa fursa, utakosa heshima, utakosa hadhi. Huko ni kumtegemea mwanadamu na hivyo ni kujikuta unaishi katika laana.
Biblia inasema pia amelaaniwa mtu yule amfanyaye mwanadamu kuwa KINGA YAKE. Unapomtegemea mtu fulani asilimia mia kama mlinzi wako, au kama tumaini lako, ni kuishi chini ya laana…Unapomtegemea mlinzi wako wa getini na kujitumainisha na walinzi wanaokuzunguka ni kujiweka chini ya laana, ndio! Utakuwa na walinzi sio dhambi…lakini kuweka tumaini lako la kwanza juu yao..na kusema wao, wasipokuwepo wewe umekwisha..Ni kuishi chini ya laana, Biblia inasema..
Zaburi 127 :1 “Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure. 2 Kazi yenu ni bure, mnaoamka mapema, Na kukawia kwenda kulala, Na kula chakula cha taabu; Yeye humpa mpenzi wake usingizi”.
Unapowaamini madaktari asilimia mia kwamba uzima wako upo juu ya elimu yao, na utaalamu wao, na huku moyoni mwako Imani na Mungu imepotea kabisa, huko ni kumtegemea mwanadamu hivyo ni kujiweka chini ya laana…Elimu ya udaktari yote haiwezi kutibu kifo, lakini yupo mmoja awezaye kuwafufua waliokufa, huyo ndio wa kumtegemea hivyo kujitumainisha kwa madawa, au kwa mahospitali na huku moyoni mwako Mungu hana nafasi..ni kuishi chini ya laana, mwisho wa siku daktari akitoa ripoti hii kuwa una siku kadhaa za kuishi, au wiki kadhaa, unapaniki sana, hiyo ni hatari sana…… madaktari wanapaswa wawe tu ni vyombo ambavyo Mungu anavitumia kutuhudumia, lakini sio waponyaji wako, wala watu wanaostahili kuchukua heshima ya Mungu, kwasababu Mungu anaweza kutumia njia nyingine kukuponya bila kutumia hao..hivyo tumaini letu lote ni kutoka kwa Bwana.
Lakini pia Biblia inasema..
Yeremia 17:7 “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake.
8 Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.”
Ukimfanya Bwana ndio jawabu lako la mwisho, na kumwamini yeye kuwa ndio kila kitu…Neno linasema utakuwa kama mti uliopandwa kando kando ya maji..hautaona hofu wakati wa hari (jua/kiangazi)..wala hautahangaika wakati wa uchache wa mvua, wala hautaacha kuzaa matunda…
Dalili ya kwanza ya kujipima kama unamtegemea mwanadamu au la ni hofu ya Maisha!! Ukishaanza kuona una hofu fulani ya Maisha kuogopa unaweza kupatwa na jambo fulani baya kutoka kwa watu, usipofanya kitu fulani…labda usipotoa rushwa, au usipokubali kushirikiana nao kwenye jambo fulani na watu fulani, au usipojaribu kufuata njia zao au kuishi kama wao, au kuishi kama wanavyotaka,au kuvaa kama wao, unaanza kuwa na hofu ya kufa, au hofu ya Kesho itakuaje, nitavaaje, nitakulaje, nitaishije!…hizo ni moja ya dalili za kumtegemea mwanadamu…lakini wote wanaomtegemea Bwana biblia inasema hawatakuwa na hofu, hawatakuwa na wasiwasi kuwa Kesho,au Kesho kutwa watakosa riziki, wanajua kabisa katika shughuli zao Mungu atakuwa pamoja nao tu hata kama leo wanajiona hawana kitu, wanajua Kesho Mungu atafungua njia itapatikana tu! Hivyo hawapepeswi na maneno wala upepo wa hofu za Maisha haya…
Wakitishiwa kuwa watafukuzwa kazi wasipofanya jambo fulani, hilo haliwababishi, wakitishiwa kuwa watahatarisha kazi zao wasipomtii boss wao kwenda kumkusanyia rushwa hawaweweseki, kama Danieli alivyozingirwa na maadui waliompangia mabaya kwa mwenendo wake wa kukataa kula rushwa..
Biblia inasema pia mtu yule amtegemeaye mwanadamu hataacha kuzaa matunda, kwanini? kwasababu anakuwa kama amepandwa kando kando ya mto…Na kuzaa matunda kuko kwa namna Mbili..kuzaa matunda ya mwili kama kufanikiwa katika mambo yote ya mwilini…shughuli na kazi zinakuwa zinafanikiwa, na pia uzao wa tumbo unabarikiwa, na namna ya pili ni kuzaa matunda ya roho, ambayo ni upendo, upole, kiasi, uvumilivu, Fadhili, furaha, amani, n.k (Wagalatia 5:22) pamoja na kuwaleta watu kwa Kristo, ambayo thawabu yake ni juu mbinguni.
Bwana akubariki sana.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
NI JAMBO LINALOMTAMANISHA SANA BWANA TUMWOMBE BILA KUKATA TAMAA?
Tukisoma kitabu cha Waamuzi ile sura ya 19, tunaona habari ya mtu mmoja Mlawi ambaye alikuwa na suria wake mzinifu, Hiyo pekee haikutosha yule suria aliondoka na kurudi nyumbani kwa baba yake, Lakini kwa jinsi Yule mtu alivyokuwa anampenda Suria wake miezi minne ilipoisha alifunga safari kutoka mjini kwake na kwenda kumfuata nyumbani kwa baba yake ili kumsihi arudi nyumbani.
Lakini alipokuwa njiani kurudi nyumbani na giza limeshaingia alikutana na mzee mmoja aliyetoka shamba ambaye alimwona amesimama barabarani hana pa kulala, hivyo alimkaribisha nyumbani kwake alale usiku ule ili kesho yake aendelee na safari yake, lakini kumbe huku nyuma wenyeji wa ule mji walikuwa wanawafuatilia, na usiku ule ule wakamfuata Yule mzee nyumbani wakigonga mlango wake kwake wakisema tutolee huyo mtu tulale naye, mambo yale yale yaliyotendekea sodoma yanajirudia tena Israeli, lakini Yule mzee alikuwa mkarimu sana, akawasihi awape binti yake ambaye ni bikira wamfanyie ouvu wao, wamuache Yule mgeni aliyeingia nyumbani kwake akae katika hali ya usalama, lakini walikataa, nusu wamuue Yule mzee, ndipo Yule mtu akaamua kutoka akawapa suria wake wamfanye wanachotaka kumfanya..
Kwa ukatili mkubwa sana wale watu walimbaka Yule mwanamke usiku kucha, tengeneza picha pengine wanaume zaidi ya 100 walikuwa pale nje, mpaka kunapambazuka bado wanaendelea kumfanyia uovu ule, hadi walipoona mwanga unakaribia kutoka ndipo wakamwacha wakaondoka, Yule mwanamke kufika tu mlangoni mwa ile nyumba hali ikawa mbaya zaidi akafa pale pale, Asubuhi mume wake anafungua mlango amwambie amka tuondoke zetu, anakutana na maiti mlangoni..
Kama tunavyosoma habari akamchukua Yule mwanamke akaenda kujifungia nyumbani mwake mwenyewe, akamkata kiungo baada ya kiungo akavigawa mafungu 12. Kisha akavichukua na kwenda kuviweka katika mipaka yote ya Israeli kwa idadi ya makabila yao, ndipo watu kuona kitendo kile walishtuka sana. Wakijiuliza jambo hili maana yake ni nini?. Kwani halijawahi kutokea katika Israeli tangu walipotoka Misri, Ndipo Yule mtu akaanza kuwaelezea jinsi tukio lilivyokuwa.
Watu wote wakasema haiwezekani ni lazima hao watu ambao wamefanya hivi huko Benyamini watolewe wauawe ili kuondoa ouvu Israeli. Lakini Benyamini walipoambiwa wawatoe watu hao waligoma..Kwao halikuwa kama jambo la kushtusha sana, kuonesha ni jinsi gani walivyokuwa wameoza kwa uovu kama wa Sodoma na Gomora..Ndipo makabila yote 11 ya Israeli yaliyosalia yakaapa hawatakaa wawape binti zao, na zaidi ya yote wakakusanyika kwenda kuisambaratisha Benyamini juu ya uso wa Israeli.
Siku ile ile watu mashujaa wakahesabiwa. Ndipo wakamuuliza Mungu juu ya kabila lipi lianze kwenda kupigana nao, ndipo Mungu akawajibu na kuwaambia lianze kwenda kabila la Yuda. Lakini walipokwenda mambo yalikuwa tofauti na walivyotazamia, badala ya kuwaangamiza Benyamini wale waovu wao ndio walioangamizwa, walipigwa kwa mapigo makuu, watu 22,000 wa Israeli waliuliwa siku ile.
Waamuzi 20:22 “Lakini watu hao, watu wa Israeli, walijitia nguvu, wakaviandaa vile vita mara ya pili mahali pale walipojiandaa siku ya kwanza.
23 Wana wa Israeli WAKAKWEA JUU NA KULIA MBELE ZA BWANA HATA JIONI; wakamwuliza Bwana, wakisema, Je! Niende nikaribie tena kupiga vita juu ya wana wa Benyamini ndugu yangu? Bwana akasema, Haya, kweeni, mwende kupigana naye.
24 Basi wana wa Israeli wakakaribia juu ya wana wa Benyamini siku ya pili.
25 Benyamini alitoka kupigana nao kutoka Gibea siku ya pili, wakaangamiza hata nchi watu kumi na nane elfu tena katika watu wa Israeli; hao wote walikuwa wenye kutumia upanga.
Tunaona hapo japo Mungu aliwaambia wakwee kupigana nao lakini bado hawakufua dafu, watu wengine 18,000 wa Israeli waliuliwa vibaya na jeshi dogo la Wabenyamini.
Ni rahisi kusema, mbona Mungu si mwaminifu kwetu, mbona tumelia mbele zake siku nzima na ametupa majibu kabisa tukwee lakini matokeo yanakuja tofauti?. Mbona tuna lengo zuri la kumwondolea uovu Israeli, lakini waovu ndio wanazidi kufanikiwa na kututukana.
Lakini tunasoma, mara ya Tatu walipokwenda mbele za Bwana, hawakwenda na vilio na kufunga tu peke yake, lakini pia wanamtolea Bwana Sadaka za Amani na za kuteketezwa.Tusome..
Waamuzi 20:26 “Ndipo wana Israeli wote, na hao watu wote, wakakwea, wakaenda Betheli, na kulia, wakaketi hapo mbele za Bwana, wakafunga siku hiyo hata jioni; NAO WAKASONGEZA SADAKA ZA KUTEKETEZWA NA SADAKA ZA AMANI MBELE ZA BWANA.
27 Kisha wana wa Israeli wakauliza kwa Bwana (kwa sababu sanduku la agano la Mungu lilikuwako huko siku hizo,
28 na Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, alikuwa anasimama mbele ya hilo sanduku siku hizo), wakasema, Je! Nitoke tena niende kupigana na wana wa Benyamini ndugu yangu, au niache? Bwana akawaambia, Haya, kweeni; kwa kuwa kesho nitamtoa na kumtia mkononi mwako.
29 Basi Israeli akaweka watu wavizie kinyume cha Gibea kuuzunguka pande zote.”
Tunasoma safari hii Mungu hakuwaambia wakwee tu, bali aliongezea na kuwaambia “Kesho nitawatoa na kuwatia mikononi mwenu”. Na baada ya hapo ukiendelea kusoma utaona jinsi Benyamini ilivyoshambuliwa na kuangamizwa vibaya mno, kwa nafasi yako pekee soma habari yote ilivyoishia utaona jinsi maangamizi yale yalivyokuwa makubwa…Ilikuwa bado kidogo tu lile kabila lingefutika lote, watu wa Benyamini walibakia wachache kama faru tulionao mbugani. Na kama sio Israeli kughairi mashambulizi yao na kuwaruhusu wale waliosalia wakaibe wake huko leo hii tungekuwa tunayafahamu na kuyaosoma makabila 11 tu ya Israeli.
Haijalishi unachokwenda kuomba mbele za Mungu ni chema kiasi gani, haijalishi unalia mbele za Mungu kiasi gani, haijalishi unafunga wiki, miezi au miaka kiasi gana, kuna mambo mengine hayawezi kutoka hivi hivi bila ya kuhusisha SADAKA. Kama vile hao walivyotoa sadaka za aina mbili za kuteketezwa na za amani, vivyo hivyo na sisi katika agano jipya tunazo sadaka za aina mbili, Ya kwanza ni ya kuteketezwa ambayo ni Yesu Kristo, aliyeteketezwa kwa ajili yetu,alichinjwa kwa ajili yetu.
Hivyo Kama upo nje ya Yesu Kristo ndugu halafu unamwendea Mungu na kumwomba akupiganie katika vita vyako, nataka nikuambie utaishia pabaya na kuvunjika moyo, na kuona kama Mungu hayupo. Vile vile na wewe uliye ndani ya Kristo, unamwomba Bwana akupiganie katika majaribu yako, halafu unakwenda mbele zake mikono mitupu, kuna uwezekano mkubwa wa tatizo lako kutokuondoka…
Kwasababu wapo wakristo ambao ni Hodari wa kuomba kweli kweli na kulia na kufunga mfano wa hawa wana wa Israeli. Lakini kwenye suala la kumtolea Mungu, wanadharau, wanaona kama Mungu hatazami hilo, wanasema yeye sikuzote huwa anatazama moyo. Nataka nikuambie, Mungu anapendezwa na moyo wa shukrani, pale unapomtolea Mungu mfuko wako anaona huyu mtu ananithamini, sio kwamba anayo haja ya fedha yako, lakini ni utaratibu wake, anapendezwa zaidi ya wenye moyo wa utoaji. unapomwendea Mungu na kumwomba akufanikishe katika jambo lako zito au jepesi jifunze kuambatanisha na sadaka ipeleke madhabahuni pake ndugu.
Unaweza kusema ooh! Mungu ameniambia yupo pamoja na mimi, Mungu kanionyesha maono, Mungu kanipa unabii, lakini utashangaa kwanini bado unashindwa pamoja na maono yako yote, Ni kwasababu unakuwa kama hawa Waisraeli.
Mungu kila wakati alikuwa anawaambia Kweeni, ni yeye kabisa alikuwa anawasapoti katika walichokuwa wanakifanya lakini tunaona japo walikuwa na jeshi la watu LAKI NNE, walipigwa na jeshi dogo la watu ELFU 26 tu la Wabenyamini. Na wewe vilevile usishangae kushindwa na mambo madogo, ukilinganisha na nguvu iliyoiwekeza katika hilo mbele za Mungu, Tatizo linaweza kuwepo hapo.
Anza kujifunza kumtolewa Bwana, naye atazifanya njia zako kuwa nyepesi.
Bwana akabariki. Tafadhali “Share ” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
TOFAUTI KATIKA YA ZAKA NA SADAKA NI IPI?
Luka 14:12 “Akamwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo.
13 Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu,
14 nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki”.
Katika habari hii, tunaona Bwana Yesu alialikwa na mtu mmoja mkuu sana miongoni mwa Mafarisayo ale chakula cha mchana nyumbani kwake, na bila shaka mtu huyu alikuwa ni tajiri, na katika karamu yake alialika watu wakuu, watu wa maana, na si watu wa kawaida kawaida tu, Lakini kuna kitu ambacho Bwana Yesu alikiona kimepunguka katika ukarimu wake mwema wa kuwaalika watu na wageni katika shughuli zake, kwani si wote wenye moyo kama huo.Wengine wanaweza wakawa ni matajiri na wakuu, lakini wakala vitu vyao peke yao, lakini huyu alikuwa watofauti kidogo.
Lakini pamoja na hayo, Bwana Yesu aligundua watu aliowaalika walikuwa ni matajiri tu, watu wenye uwezo kama yeye, Hivyo Bwana Yesu kwa kuliona hilo ili kumsidia kuifanya taabu yake isiwe bure, ndipo akamwambia kwa kumshauri wakati mwingine, kuwa atakapofanya sherehe awaalike watu wasiokuwa na uwezo wa kumlipa mfano wa hicho alichokifanya..Kwasababu akiwaalika watu wenye uwezo, wale watu nao watarudisha mapigo siku moja, watamwalika na yeye kwenye karamu zao na thawabu yake itakuwa imeshalipwa na wao, lakini mbinguni hatakuwa na kitu, hivyo ili taabu yake na wema wake uwe na nguvu idumuyo, siku nyingine akifanya karamu kubwa kama hiyo, asiiachie thawabu yake ilipizwe na wanadamu bali ije ilipizwe na Mungu katika siku ya ufufuo wa wenye haki, hivyo awaalike watu wasiokuwa na uwezo wa kumfanyia kama kile alichowafanyia.
Hata leo hii, yapo mambo mengi tunayafanya tukidhani tutalipwa tutakapofika mbinguni kwa ukarimu tunaoufanya..Kwa mfano leo hii labda kutokee mchango wa sherehe fulani ni rahisi kuchangia harusi ya boss wako, au mfanyakazi mwenzako kwasababu unajua kuna siku moja na wewe utahitaji wakuchangie kwenye sherehe yako, au ya ndugu yako. Lakini ukisikia yupo jirani yako ambaye ni maskini hana mbele wala nyuma kipato chake ni kidogo hata hakimtoshelezi yeye mwenyewe, halafu mwanawe anataka kuoa, hivyo anahitaji sapoti yako kidogo, Ukweli ni kwamba wengi wetu tutakuwa tayari kuingia mitini, ni kwasababu gani?, Ni kwasababu tunaona mbeleni huyu anaweza asiwe na msaada kwangu siku shughuli yangu, hivyo hata nisipomsaidia hainiathiri chochote.
Kiuhalisia Mungu hatakulaumu ulipochangia sherehe ya Yule boss wako na kuiacha hii ya huyu maskini, zaidi Mungu atakulipa, na kukulipa kwake kutakuwa ni kwa kupitia wao, na habari thawabu yako itakuwa imeishaipata hapa hapa duniani, juu mbinguni utakuwa huna kitu chochote. Ukinunua zawadi si zote uzipeleke kwa marafiki na ndugu, nyingine tenga wapelekee wasio na uwezo wa kukulipa,watu wasio na faida yoyote kwako. Unapokopesha usikopeshe wale tu ambao watakupa na Riba juu yake..Kopesha hata na Yule ambaye hawezi kukulipa na Riba juu yake mwenye uwezo wa kukurudishia kiwango kile kile ulichompa.
Luka 6:35 “Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, NA THAWABU YENU ITAKUWA NYINGI; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu”.
Na ndio sababu ambayo Bwana alimshauri huyu mtu aliyemwalika, nasi tupokee ushauri huo, tutafute thawabu zinazodumu milele. Ni kweli wakati mwingine unaweza kuona ni mzigo kuwa msaada kwa wasiokunufaisha Lakini thawabu yake, utaiona siku ile utakapofika mbinguni. Maana kiwango cha hazina yako ndicho kitakachofunua utajiri utakaokuwa nao mbinguni.
“Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. (Wagalatia 6:9)”
Bwana akubariki.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
KATIKA BIBLIA KUNA UFUFUO WA AINA NGAPI?
TUZO UTAPEWA KULINGANA NA NAFASI YAKO.
Maombi yamegawanyika katika sehemu kuu tatu 1) kushukuru 2) kuwasilisha mahitaji kwa mungu 3) Kutangaza.
1) MAOMBI YA SHUKRANI; Maombi haya ya shukrani ni Dhahiri na yanajulika na Wengi, kwamfano maombi ya kushukuru ni muhimu sana, na ni wajibu wa kila mtu, kuyafanya…Na haya yanahusisha kumshukuru Mungu kwa Uzima anaotupa, kumshukuru Mungu kwa afya anayotupa, ukizingatia wakati unapumua kuna wengine wapo ICU, wengine Mochwari n.k, pia maombi haya yanahusisha kumshukuru Mungu kwa mambo yote mabaya aliyokukingia katika wiki yote iliyoisha, mwezi wote uliopita na miaka yote iliyopita nyuma yako, njiani umepishana na mapepo mengi, shetani alikuwa amepanga mauti na ajali nyingi juu yako lakini Mungu kakuepusha nazo zote pasipo hata kukuambia, uthibitisho ni wewe kuimaliza wiki salama, na pia yanahusisha kumshukuru Mungu kwa riziki zote za kiduni anazotupatia, katika shughuli zetu na mapato yetu yote,..Kwahiyo maombi haya kwa ujumla yanahusisha kumshukuru Mungu kwa mambo yote anayoyafanya tunayoyaona na tusiyoyaona. Ni maombi yanayoonesha unyenyekevu wetu mbele za Mungu na kumwonesha Mungu wetu kuwa tunathamini na kuutambua na kuujali ulinzi wake na Fadhili zake juu yetu. Kwahiyo ni sehemu ya maombi ambayo ni muhimu sana.
2) Sehemu ya pili ya maombi ni ile ya KUWASILISHA MAHITAJI YETU MBELE ZA MUNGU. Hii inahusisha kumwendea Mungu kwa unyenyekevu kumwomba atufanyie au atupatie jambo Fulani katika Maisha yetu, Tunamwendea tukiamini kuwa yeye ndiye mpaji wetu (YEHOVA-YIRE). Tunamwomba azidi kutupa riziki zetu, azidi kuzifanikisha kazi zetu za mikono, azidi kutupa afya, azidi kutuepusha na yule mwovu na mipango yake yote, azidi kutupa Neema ya kumjua yeye Zaidi popote tuendapo atukutanishe na injili yake na kuitii, azidi kutupa mioyo ya nyama na si ya jiwe katika kutenda mapenzi yake, azidi kutupa hekima, tunamwomba Bwana azidi kutupa furaha, amani, upendo pamoja na kibali kila tuendapo, na kutufanikisha katika mambo yote katika masaa ya siku yaliyobakia, wiki na katika mwezi huu na unaokuja. Hapa tunamwomba Mungu atuepushe na kila jaribu lililopangwa na shetani kinyume chetu mbele yetu..Kama Bwana alivyosema mahali Fulani “Ombeni kwamba msiingie majaribuni. (Luka 22:40)”.
Ikiwa na maana kuwa usipoomba ni lazima utaingia majaribuni tu!..Wakina Petro usiku ule Bwana aliwaambia waamke kusali ili wasiingie majaribuni wakapuuza, wakalemewa na usingizi wakalala, masaa machache baadaye Petro alipojaribiwa na Ibilisi amkiri Yesu, alishindwa mwisho wake akamkana mara 3 lakini endapo angeomba usiku ule kama Bwana alivyomwambia na kuifunika siku yake wakati Ibilisi anamjaribu angeshinda lile jaribu, saa ile nguvu fulani ya ujasiri ingemshukia pale pale na angemkiri Bwana badala ya kumkana, au Mungu angemuepusha kabisa na jaribu hilo. Lakini kutokana na kwamba alikuwa hana hazina ya maombi ya kutosha, nguvu za roho zilikuwa chin alishindwa. Na aina zote za majaribu zinaweza kuzuiwa au kuepukwa kwa maombi… unapopita mahali na watu kukuudhi mpaka kukasirika na kugombana mpaka kutoa maneno machafu hilo ni majaribu ambalo ungeweza kulizuia kwa kuomba usiku mmoja kabla hujalala, au asubuhi kabla ya kuanza shughuli zako.
Kadhalika unapojikuta unafanya kitu kisichofaa ambacho hukutarajia au hukupanga kukifanya hilo nalo ni jaribu ambalo lingeweza kuzuiliwa kwa kuomba kabla ya kuianza siku..Na dhambi nyingine zote za bahati mbaya zinasababishwa na upungufu wa maombi. Inapotokea safari ya ghafla ambayo ni ya hasara na si ya faida hilo nalo ni jaribu ambalo endapo ungeomba lisingekukuta.nk n.K.
3) Sehemu ya tatu na ya mwisho ya maombi ni maombi ya KUTANGAZA. Hii ni sehemu ya mwisho na ya muhimu sana kwa kila Mkristo kuifanya. Na faida yake kuu ya haya maombi ni ile ile ya KUTUEPUSHA NA MAJARIBU, Maombi haya ni maombi ya kimamlaka…Maombi haya na yale ya KUPELEKA MAHITAJI yanakazi moja tu nayo ni KUTUEPUSHA NA MAJARIBU.
Sasa kabla ya kuingia kujifunza juu ya jambo hili hebu kwanza tujifunze ulinzi wa kiMungu juu ya mtu aliyezaliwa mara ya pili.
Mtu anapozaliwa mara ya pili, na kuishi Maisha yanayompendeza Mungu asilimia zote, kunakuwa kuna ulinzi Fulani wa kiujumla ambao Mungu anauachilia juu yake, kiasi kwamba huyo mtu hata iweje hawezi kupotea, shetani hawezi kumtoa mkononi mwa Mungu, labda tu huyo mtu kwa hiyari yake mwenyewe aamue kujiuza kwa shetani, lakini kwa namna nyingine yoyote hawezi kutoka mikononi mwa Mungu, anakuwa analindwa kuanzia unywele wake mpaka unyayo wako, na anakuwa amevuka kutoka mautini kuingia uzimani, …Lakini pamoja na huo ulinzi wa kiujumla kuna sehemu ndogo sana ambayo Mungu kamwachia shetani aimiliki..na hiyo ni kutokana na kwamba bado tupo katika miili hii ya dhambi, sehemu yote ya ulinzi wa kiMungu tutakuja kuipata baada ya ukombozi wa miili yetu pale tutakapovaa miili mipya ya utukufu.
Ndio maana unaona sasa japokuwa umeokoka na unaishi Maisha ya kumpendeza Mungu kwa asilimia zote lakini bado utapitia wakati mwingine wa viudhaifu vya hapa na pale, utaumwa kichwa, utajisikia kichefuchefu, mafua yatakusumbua, wakati mwingine itakubidi umeze Panadol kupunguza maumivu au uende hospitali n.k. Sasa hiyo yote ni kuonesha kuwa Mungu hajaipa miili yetu hii asilimia 100 ulinzi…ingawa hivi viudhaifu haviwezi kutuathiri kiasi cha kututoa kwenye Imani, kwasababu Mungu hawezi kuruhusu tujaribiwe kupita tuwezavyo, alisema hivyo katika Neno lake.
1Wakoritho 10: 13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili”.
Kwahiyo haya majaribu madogo madogo ni lazima yaje! Na ni wazi kuwa yanaletwa na shetani kututesa tu! Na kutuhangaisha…Kwahiyo shetani anachokifanya ni kutumia hii nafasi aliyopewa ya sehemu ndogo ambayo Mungu kaiacha, kutujaribu…Na kwasababu anajua hawezi kumjaribu mwamini kwa asilimia zote, atahakikisha kuwa hiyo sehemu ndogo aliyopewa anaitumia ipasavyo.
Sasa swali? Anaitumiaje?
Anaitumia kwa KUTANGAZA, Anawatumia watu kutamka maneno Fulani Fulani juu yako, ambayo hayo yanaweza kutokea kama walivyozungumza, kwasababu Mungu alivyomuumba mwanadamu akizungumza kitu kwa Imani ni lazima kitokee hata kama mtu huyo sio mchawi. Ndio maana wazazi hata kama ni waabudu sanamu wanao uwezo wa kumbariki mtoto au kumlaani, na hizo baraka au laana zikampata huyo mtoto hivyo hivyo kama alivyozisema. Kwasababu hiyo basi shetani anaweza kutumia watu au wachawi au mapepo yake KUTANGAZA mambo Fulani mabaya juu ya mtu.
Kumbuka tena kwa msisitizo..kama umezaliwa mara ya pili na kuishi Maisha yampendezayo, haijalishi ni mambo gani makubwa watayatangaza juu yako, hayatatimia yote kwasababu kuna asilimia kubwa ya ulinzi wa kiMungu kwenye Maisha yako, lakini pia yapo baadhi madogo madogo yanayoweza kutimia na hiyo ni kwasababu hatujapewa dhamana wa ulinzi wa miili hii asilimia zote kama tulivyotangulia kusema..(huu ni msingi mkubwa ambao unahitaji kuelewa) Na sio kwamba Mungu kashindwa kutufunika asilimia zote, hapana ni kwasababu tu ndivyo imempendeza iwe hivyo…kwamba tujue kwamba bado tupo duniani?, tujue kuwa sisi bado ni wadhaifu mbele zake, na tujifunze kumtegemea yeye na kumwomba ulinzi…na pia tujue kuwa vita bado vinaendelea…mpaka siku tutakapovaa ile ya utukufu, ndipo vita vitaisha.
2Wakorintho 1:8 “Maana ndugu, hatupendi, msijue habari ya dhiki ile iliyotupata katika Asia, ya kwamba tulilemewa mno kuliko nguvu zetu, hata tukakata tamaa ya kuishi.
9 Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu, bali tumtumaini Mungu, awafufuaye wafu,
10 aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna ile; tena atatuokoa; ambaye tumemtumaini kwamba atazidi kutuokoa;”
Sasa ili kupunguza nguvu za shetani kwa majaribu yake anayoyatumia kwa NJIA YA KUTANGAZA…Na sisi tulioamini tuna wajibu huo huo, wa kuingia kwenye maombi ya kuzipunguza hizo nguvu ndogo ndogo za shetani zinazofanya kazi kwenye Maisha yetu…Na maombi hayo hatuyafanyi kwa kupeleka mahitaji mbele za Mungu, bali kwa KUTANGAZA kama yeye anavyotangaza..Ndio hapo sasa Kila siku kabla ya kuianza siku unatamka baraka katika siku hiyo, unalaani na kufuta kila kazi zote za Adui zilizopangwa katika siku hiyo kwa jina la YESU, Unalaani vidhiki na vijaribu vidogo vidogo vilivyopangwa na shetani…Na unatamka kwa maneno yanayosikika kabisa, kwasababu maneno yanaumba, kwa Mungu aliiumba dunia kwa Neno, Unatamka kwa kutangaza kuziharibu nguvu zote na kufuta maneno yote yaliyozungumzwa na watu, wachawi, au mapepo katika siku nzima…unalaani nguvu zote za giza zilizoachiwa siku hiyo zitakazokufanya uikane Imani, au upate hasara ya jambo Fulani, au zitakazokufanya ulumbane au ugombane na watu, unalaani kwa kinywa chako kila nguvu zote za giza zilizoachiwa na yule adui kukufanya usipate muda wa kusoma Neno,na kila ratiba isiyoeleweka iliyopangwa kuzimu kinyume chako na ndugu zako…Unahikikisha unagusa kila kipengele katika Maisha yako, afya yako,familia yako, kazi yako na Imani yako. Usiache kitu!, kwasababu na yule adui anajua anaomlango mdogo juu ya Maisha yako hivyo anakaza kuutumia vizuri.
Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.”
Kwa kufanya hivyo utakuwa umeharibu mipango yote midogo midogo ambayo shetani alikuwa amepanga kukusumbua katika siku hiyo na wiki hiyo. Na hivyo utakuwa umejiongezea Ulinzi wa kiMungu kwa asilimia nyingine kadhaa mbele. Kama alikuwa akuletee viugomvi, viugonjwa, unashangaa siku inaisha bila hivyo vitu, kama alikuwa amekusudia kukuletea vitabu vya hapa na pale visivyoeleweka vinatoweka.
Nakumbuka mwanzoni mwanzoni nampa Bwana Maisha, nilikuwa napitia changamoto nyingi sana na nilikuwa sijui chanzo chake ni nini?..lakini baada ya kujifunza somo la maombi, niliona mabadiliko makubwa sana…
Kwa hiyo ni maombi ya Muhimu sana na kila Mwamini anatakiwa aombe. Na ni moja ya silaha 6 tulizopewa katika biblia..
Waefeso 6: 11 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,
15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;
16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;
18 KWA SALA ZOTE NA MAOMBI MKISALI KILA WAKATI KATIKA ROHO, MKIKESHA KWA JAMBO HILO NA KUDUMU KATIKA KUWAOMBEA WATAKATIFU WOTE;
19 pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili;
20 ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo;
hata nipate ujasiri katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena.”
Kwa kumalizia kumbuka kuwa muda wa chini Bwana Yesu aliotuamuru tusali kwa siku ni LISAA LIMOJA.
Mathayo 26: 40 “Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? 41 Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”
Umeona hapo, roho zetu zipo tayari kuomba lakini miili ndio inayokataa, hivyo mambo mengine ni unalazimisha, kama Bwana asiyekuwa na dhambi aliomba Zaidi ya lisaa limoja, unafikiri inatupasaje sisi wenye dhambi?..unakataa usingizi na uvivu wa kuomba, unalazimisha mambo, utashangaa dakika za kwanza unapata shinda lakini baaada ya dakika 10-15 mbeleni unashangaa kuna nguvu Fulani inakuvaa unajikuta unazama kwenye maombi…Na kwa vipengele hivyo vitatu ukianza na kushukuru, kisha kupeleka maombi na kutangaza baraka..huwezi kuacha kumaliza lisaa na Zaidi..
Na pia kumbuka kuwaombea na wengine, katika vipengele vyote hivyo vitatu, hata hichi unachokisoma hakijapewa guarantee ya ulinzi asilimia 100, kinahitaji maombi kiweze kuendelea kuwepo, kwahiyo uombapo ukumbuke kugusia kila eneo, pamoja na sisi tunaoandika hizi habari, Ili injili ya Mungu izidi kwenda mbele, kwa Neema za Mungu.
Bwana akubariki sana.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
NI JAMBO LINALOMTAMANISHA SANA BWANA TUMWOMBE BILA KUKATA TAMAA?
RUDIA, TENA NA TENA KUMWOMBA MUNGU USIKATE TAMAA.
NI KWA NAMNA GANI TUTASHINDA MAJARIBU?
ROHO I RADHI, LAKINI MWILI NI DHAIFU.
Shalom! Mtu wa Mungu, maandiko yanatuagiza tusiache kuonyana kila siku, maadamu iitwapo leo (Waebrani 3:13). Hivyo nakukaribisha tujifunze leo jambo moja lihusulo BIBLIA.
Nilipokuwa ninatafakari hili Neno linalosema “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.” Nikajiuliza hii njia ionekanayo kuwa sawa ni ipi?..Mtu akiwa mtukanaji, mtu akiwa muuaji, mtu akiwa ni fisadi n.k, njia yake haiwezi kuonekana ni sawa machoni pake, ni wazi kuwa anafahamu anapoeleka ni pabaya..Lakini njia inayoweza kuonekana ni sawa machoni pa mtu ni ipi?, ni ile inayotoka katika maandiko (BIBLIA), pale maandiko yanapomthibitishia mtu kuwa kitu hichi au kile anachokifanya kimeandikwa, basi hilo linampa amani ya kufahamu kuwa yupo katika njia sahihi.
Nataka nikuambie, biblia ni kitabu kitakatifu sana, kimekamilika na kujitosheleza kwa namna zote, hakiwezi kuongezwa wala hakiwezi kupungumzwa, lakini nataka nikuambie pia Biblia hii si ya watakatifu peke yao: Biblia si mti wenye tunda la aina moja, bali ni mti wenye matunda ya aina nyingi tofauti tofauti,. na kila mtu anachuma kinachomfaa na kuondoka kulingana na matakwa yake mwenyewe.
Na hiyo yote ni kwasababu biblia ni Neno la Mungu, na Neno la Mungu tunajua ndio lililoumba kila kitu (Yohana 1:1), halikuumba vyema tu bali hata na viovu pia, hivyo pumzi ya kila kitu inategemea hilo Neno. kwahiyo kila mtu na kila mmoja na inaweza kumnufaisha kulingana na matakwa yake mwenyewe. Shetani inamnufaisha katika lengo lake la kupoteza watu, na amefanikiwa kweli kupoteza mamilioni ya watu kwa kupitia biblia unayoisoma, hata alijaribu kuitumia hiyo hiyo kumwangusha Bwana akashindwa..
Madaktari wanaitumia hii kuwasaidia kubuni aina mbalimbali za matibabu, hata ukiangalia nembo yao kubwa maarufu inayotumiwa na Shirika la Afya ulimwenguni (WHO), utaona ni Yule nyoka wa shaba ambaye Musa aliwaagiza wana wa Israeli wamtazame ili wapone kutokana na sumu ya nyoka. Utamaduni huo ambao baadaye uligeuka kuwa wa kipagani, ulirithiwa na mataifa mengine ya kipagani kama Ugiriki wakahusisha na tiba za kienyeji na mambo hayo, na ndio huko huko mpaka ikawa maarufu katika masuala yote ya tiba duniani leo hii.
Biblia hii hii inayoisoma inatumiwa na majeshi, kubuni mbinu mpya za kupigani: Na wanafanikiwa vizuri sana. Wakati wewe unafurahia kusoma zile habari za vita vya Yoshua na waamuzi, wengine huko wanaiga mbinu za kivita. Biblia hii hii inatumiwa na wanasiasa kutengeza sera zao za kampeni na wanafanikiwa katika hilo, Msome mtu kama kwame Nkrumah raisi wa kwanza wa Ghana,si jinsi alivyoupindua utawala wa kikoloni kwa maandishi ya maandiko.
Biblia hii hii inatumiwa na wachawi na wanajimu, kuwasaidia kufanya uchawi wao: Wasingefahamu kitu kinachoitwa kafara na nguvu iliyokatika damu kama wasingesoma katika biblia..Katika Agano la kale kafara za Wanyama zilikuwa zinafanyika kwaajili ya upatanisho…Asili ya kuvaa hirizi si kutoka kwa wachawi…Wana wa Israeli waliagizwa na Mungu wazivae kwenye vipaji vya nyuso zao, ili kuwakumbusha sheria za Mungu, (vilikuwa ni viboksi vidogo vilivyokuwa vimebeba baadhi ya maneno ya kwenye Torati) lakini Baadaye shetani akaja kuiba huo utamaduni na kutengeneza za kwake kwa lengo la kulogea watu.
Wafanya-biashara na matajiri: Kanuni za kufanikiwa zote wanazitolea katika maandiko,kupanda na kuvuna. Kufanya kazi kwa bidii,n.k. zipo huko, wanazitumia na zinawaletea mafanikio makubwa sana.
Vile vile biblia hii hii inatumiwa na manabii wa Uongo, kutimiza matakwa yao: Wanasoma na kufahamu kuwa ndani ya jina la YESU, kuna uweza wa kipekee, kila kitu kinatii, hivyo hata mtu ambaye alishamkufuru Mungu siku nyingi, anaouwezo wa kulitumia hili jina ili kuamirisha chochote na kikamtii, hata kuamisha milima…hivyo anaweza kutumia fursa hiyo kujipatia mali, au kuwapoteza, kwa kisingizio cha miujiza, na anafanikiwa kabisa, na ndio maana Bwana Yesu alisema wengi watakuja siku ile wakisema Bwana Bwana…, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu. (Mathayo 7:21).
Lakini pia biblia hii hii inatumiwa na watu wengine, na inawapa UZIMA WA MILELE.
Unaweza ukaona hapo, jinsi Biblia inavyofungua milango ya mambo mengi, hata yale maovu, lakini sio milango yote mtu akiingia kwa kupitia biblia inamletea mwisho mwema. Na ndio maana ukisoma maneno ya kwanza kabisa Bwana Yesu aliyoyahubiri ni haya, TUBUNI, KWA MAANA UFALME WA MBINGUNI UMEKARIBIA(Mathayo 4:17)..Na habari zake zote zilikuwa zinalenga ufalme wa mbinguni, kama ukitafuta mahali Bwana Yesu anakufundisha utajiri na mafanikio ya kidunia nataka nikuambie unaweza ukavunjika moyo, zaidi ya yote watu waliojaribu kumfauta kujaribu kumuuliza kuhusu mambo kama hayo aliishia kuwaambia “Uzima wa mtu haupo katika mwingi wa vitu alivyonavyo”(Luka 12:15).
Alikuwepo kwa lengo moja tu la msingi, nalo ni kumpa mtu uzima wa milele. Na wote waliomfuata waliupokea bali waliomkataa hawakaupata bali walipata sehemu ya vipengele vingine katika maandiko.,Leo hii usifurahie na kusema biblia inahimiza hichi ninachokifanya..ukadhani kuwa upo sahihi wakati wote katika hiyo njia…Unapaswa ujiulize je! matokea ya hichi ninachokifanya mwisho wake ni nini?,..Ni uzima wa milele au Mauti, au huna-uhakika?. Ikiwa ni mauti au huna-uhakika, hata kama kuna vifungu vinakusapoti, achana nacho, tafuta kilicho cha msingi kwanza, na biblia imeshaturahisishia kufahamu kilicho cha msingi, nacho ni YESU KRISTO..
Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”
Ni heri ukakifanya hicho, lakini huku nyuma jambo la msingi la wokovu wako na uzima wa milele lipo pamoja na wewe, hiyo haina shida kabisa,lakini unaacha mambo ya wokovu na habari za kwenda mbinguni, unasema biblia inaniambia hivi au vile …Kumbuka Yesu anasema “hapa yupo aliye mkuu zaidi ya Sulemani”.
Hivyo kwa kumalizia ni vizuri tukajua jinsi ya kuyavunja vunja maandiko na kuchagua vile vilivyo vya muhimu kwanza, ambavyo ni vya UFALME WA MBINGUNI NA HAKI YAKE NA HIVYO VINGINE VILIVYOSALIA TUTAZIDISHIWA tu Bwana ameahidi hilo, yeye si mwongo. Tunajua hizi ni nyakati za kumalizia, Kristo yupo karibuni kurudi kushinda hata sisi tunavyoweza kufikiria..Ikiwa utasikia unyakuo umepita leo na wewe umebaki utakuwa katika hali gani?. Kumbuka atakayeona uchungu zaidi sio mlevi, au jambazi, atakayeona uchungu ni Yule mkristo aliye vuguvugu ambaye aliitupilia injili za wokovu na kwenda mbinguni akageukia injili za namna nyingine za faraji, ambazo thawabu zake zinaishia hapa hapa duniani…siku hiyo huyo ndio atakayeomboleza..Kwasababu alidhani kuwa ndio njia aindeayo uzimani..Lakini mwisho wake umekupeleka kuingia katika dhiki kuu.
Utasema siku ile, Hatukupata mali kwa jina lako Bwana?, hatukufunguliwa matumbo yetu yaliyokuwa tasa kwa jina lako?, hatukufungua biashara nzuri kwa unabii wako?.nk Ni kweli mambo hayo yote uliyafanya kwa jina la Yesu lipitalo majina yote na lifungualo vifungo vyote, lakini siku ile Bwana atasema ondokeni kwangu! Kwanini? kwasababu jina hilo ulipaswa ulitumie pia kukuletea wokovu wako wa milele, si tu vitu vya ulim:wengu huu vinavyopita, jina hilo ulipaswa pia ubatiziwe kwalo, kulingana na Matendo 2:38, Matendo 8:16, Matendo 19:5 na Matendo 10:48. ili upate ondoleo la dhambi zako na upokee kipawa cha Roho Mtakatifu..Umepata fahari zote na ulimwengu mzima kwa jina hilo lakini umekosa uzima kwa jina hilo, itakufaidia nini?.
Jihadhari na njia zinazoonekana ni nzuri, zinazopendwa na kufuatwa na wengi kwa kivuli cha biblia, nyingi zinaelekea upotevuni. kumbuka njia ni nyembamba ielekeayo uzimani
Ubarikiwe sana.Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
IKO NJIA IONEKANAYO KUWA SAWA MACHONI PA MTU.
NJIA KUU YA KUINGIA KATIKA ULE MJI.
NJIA MUNGU ALIYOIWEKA KWA KILA JAMBO
NJIA YA BWANA INATENGENEZWA WAPI?