Title March 2021

Neno Maganjo linamaanisha nini katika biblia?

Maganjo ni kitu kilichoharibiwa, kwa mfano jengo likiharibiwa labda tuseme kwa  kombora, lile gofu linalobakia ndio maganjo. Au mji unapochomwa moto, yale masalia salia ya mji, ndio maganjo.

Mungu amekuwa akitumia Neno hili kuonyesha jinsi adhabu yake itakavyokuwa kwa wasiomcha yeye.

Hivi ni baadhi ya vifungu ambavyo utaweza kukutana na Neno hilo;

Walawi 26:30 “Nami nitapaharibu mahali penu palipoinuka, na kuziangusha sanamu zenu za jua, nami nitaitupa mizoga yenu juu ya mizoga ya sanamu zenu; na roho yangu itawachukia.

31 NAMI NITAIFANYA MIJI YENU IWE MAGANJO, na mahali penu patakatifu nitapatia ukiwa; wala sitasikia harufu ya manukato yenu yapendezayo.

32 Nami nitaitia hiyo nchi ukiwa; na adui zenu watakaokaa huko wataistaajabia”.

Ezekieli 6:14 “Nami nitanyosha mkono wangu juu yao, na kuifanya nchi kuwa MAGANJO, tena ukiwa mbaya kuliko jangwa upande wa Dibla, katika makao yao yote; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana”.

Yeremia 51:42 “Bahari imefika juu ya Babeli, Umefunikwa kwa wingi wa mawimbi yake.

43 Miji yake imekuwa MAGANJO; Nchi ya ukame, na jangwa; Nchi asimokaa mtu ye yote, Wala hapiti mwanadamu huko”.

Yeremia 4:7 “Simba ametoka katika kichaka chake, ndiye aangamizaye mataifa; ameanza kushika njia, ametoka katika mahali pake; ili aifanye nchi yako kuwa ukiwa, miji yako ifanywe MAGANJO, asibaki mwenyeji ndani yake. 8 Kwa sababu hiyo jifungeni nguo za magunia; ombolezeni na kulia kwa uchungu; kwa maana hasira kali ya Bwana haikugeuka na kutuacha”.

Som pia Ezekieli 12:20, 29:12, Amosi 9:14

Hata sasa, huu ulimwengu, utakwenda kufanywa maganjo kipindi si kirefu, haijalishi umejengwa vizuri kiasi gani, haijalishi umeshafikia hatua ya kuwa ustaarabu mzuri namna gani,..Bwana Yesu alisema kuwa hakuna jiwe litakalosalia juu ya jiwe. Kila kitu unachokiona leo hii kitateketezwa, siku ile ya Bwana itakapofika. Kila kitu kitafumuliwa, moto utaisafisha kweli kweli hii dunia, kama vile gharika ilivyoisafisha dunia ya kwanza wakati ule wa Nuhu.

Soma.

2Petro 3:10 “Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.

11 Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa,

12 mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka”?

Swali ni je! Mimi na wewe tumeekeza wapi maisha yetu?  Je ni duniani au mbinguni?..Kumbuka duniani ni tunapita, yapo maisha ya milele huko mbeleni yanatungojea.. Ni wajibu wetu kutambua lililo la muhimu kwanza, ambalo ni wokovu wetu, Lengo la Mungu kuifanya hii dunia kuwa maganjo si kwamba ni mbaya hapana, bali sisi ndio tumeifanya kuwa mbaya kwa dhambi zetu, na hivyo ni lazima iteketezwe tu.

Hivyo sisi sote tusiwe washirika wa hiyo ghadhabu ya Mungu. Kumbuka Unyakuo upo mlangoni. Na haya mambo hatutashangaa kuyaona yakitimia hata kwenye kizazi chetu.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Pomboo ni nini katika biblia?(Kutoka 25:5, Ezekieli 16:10)

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 2

KWA WALE WALIO NJE “YOTE” HUFANYWA KWA MIFANO.

UFUNUO: Mlango wa 14

Sodoma ipo nchi gani?

Rudi nyumbani

Print this post

KWA WALE WALIO NJE “YOTE” HUFANYWA KWA MIFANO.

Nakusalimu katika jina la Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo, ambaye yeye peke yake ndiye Mungu, aliyeshuka katika mwili wa kibinadamu kutukomboa sisi.

Yapo mambo ambayo hatuwezi kudhania kama Bwana Yesu angeyafanya alipokuwa hapa duniani.. Japo alikuja kweli kutuokoa, lakini hakuufanya wokovu kuwa mrahisi kiivyo kama wengi tunavyodhani.

Yesu havutiwi na wingi wa watu  wanaokuja  kumsikiliza, au wanaosema wanamfuata, hilo halimshawishi hata kidogo kutoa siri zake zote za wokovu. Wakati ule kulikuwa na umati mkubwa wa watu, ambao walikuwa wakimfuata kila mahali,  wengine mpaka wanakanyagana, sasa unaweza kudhani Bwana angetumia fursa ile, kuwapa siri za Mungu wazi wazi.. Lakini biblia inatuambia hilo hakulifanya, badala yake alizungumza nao kwa mifano (yaani mafumbo). Na kama unavyojua mafumbo huwa hayampi tu majibu ya moja kwa moja, ikiwa na maana kuwa mtu anaweza akatoka hapo asipate jibu la wazo lako kama hatofikiria sana, au kutaka kuambiwa maana yake.. Unaweza kujiuliza kwanini afanye vile?

Bwana Yesu hataki kuwaokoa watu wasiomaanisha kweli kuutaka wokovu ndani ya mioyo yao. Haokoi wasikilizaji tu, bali watu wanaotaka kuelewa nini maana ya wokovu na wokovu huo unapatikanaje ndani ya mioyo yao. Na ndio maana alizungumza nao kwanza kwa mafumbo, na baadaye akawaambia wanafunzi wake kauli hii .”kwa wale walio nje, YOTE hufanywa kwa mifano”..Unaona? Hakusema “machache” hapana, bali YOTE.. Ikiwa na maana hakuna kufananuliwa chochote, ikiwa upo mbali na Kristo. Habari za Kristo zitakuwa mafumbo tu kwako, haijalishi wewe unamfuata kwenye mikutano yake, au unahudhuria semina zake nyingi kiasi gani.

Watu wengi waliomfuata Kristo walikuwa ni watembeleaji tu, wengine walimtafuta kwa ajili miujiza, wengine kama wapelelezi, wengine wasikilizaji tu wa kupoteza muda ili uende, wengine ni kuutazama mwonekano wake upoje, anavaaje,n.k…Hayo tu, hawana cha ziada..Wachache sana ndio waliokuwa wanatafuta kumjua yeye kwa kile alichokileta duniani, na ndio hao ambao baada ya mafundisho kuisha, walijiona nafsini mwao hakuna chochote walichokipata, zaidi ya stori stori tu, hakuna lolote lililowajengwa rohoni, ndipo wakamfuata akiwa peke yake, katika utulivu wakamwomba awafunulie siri za mifano ile… Hao ndio Yesu alikuwa amewakusudia wokovu.

Marko 4:10 “Naye alipokuwa peke yake, wale watu waliomzunguka, na wale Thenashara, walimwuliza habari za ile mifano.

11 Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, BALI KWA WALE WALIO NJE YOTE HUFANYWA KWA MIFANO,

12 ili wakitazama watazame, wasione; Na wakisikia wasikie, wasielewe; Wasije wakaongoka, na kusamehewa”

Leo hii, upo umati mkubwa sana katika kanisa, upo umati mkubwa sana wanaosema wanamtafuta Mungu kila mahali,.Wakidhani Yesu anavutiwa na kumtembelea kwao.

Hilo halipo, ikiwa mtu mwenyewe binafsi hataki kumtafuta Kristo akiwa peke yake, amsaidie, hataki kuonyesha bidii yake kwa Kristo kujifunza na kumtafakari, kukitendea kazi kile alichokisikia, asahau kuupokea wokovu wake halisi wa  kweli kweli.

Na ndio maana leo hii, utaona wokovu hauna nguvu yoyote ndani ya mioyo ya baadhi ya watu, mtu atasema ameokoka, lakini uzinzi unamshinda, ulevi unamshinda. Amekaa miaka mingi katika kanisa lakini hajui hata kama kuna jambo linaloitwa Unyakuo, hajui kama hili kanisa tunaloishi ndio kanisa la mwisho, lijulikanalo kama LAODIKIA kulingana na maandiko (Ufunuo 3), na kwamba hakutakuwa na kanisa lingine zaidi ya hili, hajui mpango wa Mungu kwa kanisa lake kwa wakati huu tunaoishi ni nini? Lakini atasema anamjua Kristo, na amemwona. Hajui kuwa hata watu wa kipindi kile walimwona Yesu, wakala naye, wakasikia sauti yake, wakaona miujiza yake mingi, lakini aliowafunulia siri za ufalme wa mbinguni ni wachache sana. Wale waliokwenda kutendea kazi kile walichokisikia.

Ndugu Bwana Yesu anawaokoa watu waliomaanisha kweli kweli, sio wasikilizaji tu, wasio na bidii yoyote, miaka nenda rudi, ni wasikilizaji tu wa mahubiri, makanisani,  mitandaoni, n.k.,  huwajishughulishi  kwa lolote kumtafuta Yesu binafsi, wakidhani kuwa Yesu amewafunulia tayari siri zake.

Huu wakati sio wa  kuwa vuguvugu, ni wakati wa kujitwika msalaba wako na kumfuata YESU. Kumbuka alisema..

Mathayo 16:24 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.

25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.

26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake”?

Vinginevyo, tukiwa watu wasiomaanisha, kama wale makutano, tujue kuwa YOTE, ya Yesu, tutayasikia tu kama mifano.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

UFUNUO: Mlango wa 3 part 3

UFUNUO: Mlango wa 14

NI NINI TUNAJIFUNZA KWA DEMA NA MARKO?

Biblia ina maana gani inaposema akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko?

Rudi nyumbani

Print this post