Category Archive Home

JINSI YA KUSHINDA VISULISULI(Mithali 10:25)

SWALI: Nini maana ya hii Mithali 10:25

Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena; Bali mwenye haki ni msingi wa milele.


JIBU: Mstari huo unajifafanua vizuri kwenye ule mfano Bwana Yesu aliutoa kuhusiana na watu wanaoyasikia maneno yake, halafu hawayatendi. Tusome.

Mathayo 7:24  Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba;

25  mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba.

26  Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga;

27  mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.

Hivyo tukirejea katika vifungu vile vya kwenye mithali. Unaweza kuelewa mtu asiye haki hasaa ni nani?

Ni Yule ambaye anaisikia injili, halafu hatii.  Mtu Yule anayesema ameokoka, lakini zao la wokovu halionekana ndani yake. Rohoni anaonekana hana tofauti na yule ambaye hajamjua Mungu kabisa. Wote hao huitwa wasio haki. Bado wapo dhambini, hawajakombolewa na damu ya Yesu Kristo.

Hawa wataonekana kwa nje kama vile ni watakatifu. Lakini kinapokuja tu kisulisuli  aidha  cha majaribu, shida, dhiki, udhia,au mapigo kwa ajili ya Kristo, mara ghafla wanarudi nyuma, wanakuwa kama watu ambao hawajawahi kumjua Mungu kabisa, kwasababu hakujikita katika mwamba. Wengine sio majaribu ya shida, bali yale ya mafanikio makubwa, ndio hapo anasa zinawazidi wanamsahau Mungu, wanaiaga imani, kwani walimfuata Yesu kwasababu ya shida tu. Wengine ndoa, elimu, vyeo wakishavipata, huwaoni tena kwa Yesu.

Lakini mtu anayeyasikia maneno ya Kristo na kuyatii, ni kinyume chake, huitwa msingi wa milele. Huyo hatikiswi na wimbi, kisulisuli au dhoruba yoyote. Kwasababu yupo juu ya mwamba.

Okoka, upokee msamaha wa dhambi, kisha ishi kufuata na toba yako, ili uhakika wa kusimama uwe nao wakati wote.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MWAMBA WETU.

Mtu asiye na akili ni nani kibiblia?

TUNAHESABIWA HAKI BURE KWA NJIA YA IMANI.

TUNAHESABIWA HAKI BURE KWA NJIA YA IMANI.

Rudi Nyumbani

Print this post

Maelezo ya Mithali 28:28 Wasio haki wainukapo, wanadamu hujificha; Bali waangamiapo, wenye haki huongezeka.

SWALI: Nini maana ya  Mithali 28:28 Wasio haki wainukapo, wanadamu hujificha; Bali waangamiapo, wenye haki huongezeka.


JIBU: Mithali hii hulenga hasaa watawala, iwe ni serikalini, kwenye mataasisi, makanisa n.k. endapo waongozao ni waovu, basi hufanya hata watu (hususani wale wema) kujificha, Au kutoonekana kabisa.

Ndio kama ilivyokuwa katika kipindi cha mfalme Ahabu, alipoiharibu nchi yote ya Israeli kwa kuweka miungu migeni, akichochewa na mkewe Yezebeli. Wakati huo Manabii wengi wa Mungu waliuliwa, na wale waliosalia walijificha wasionekane kabisa, wakabakia tu makuhani wa baali na wenye dhambi. Kiasi kwamba Eliya akadhani ni yeye tu peke yake nabii aliyebakia Israeli. Kuonyesha ni jinsi gani wenye haki, walivyokuwa adimu wakati huo. Lakini Mungu alimwambia Eliya, nimejisazia watu elfu saba wasiopigia goti baali.

Warumi 11:3  Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu.

4  Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali.

5  Basi ni vivi hivi wakati huu wa sasa, yako mabaki waliochaguliwa kwa neema.

Ni kama leo tu ulimwenguni, tunavyoona kiwango cha watenda maasi na  maasi kinavyozidi kuongezeka, ndivyo inavyokuwa ngumu kukutana na watakatifu halisi, na hiyo inaweza pelekea pengine ukajidhani mpo wachache, au hakuna kabisa kama wewe.

Ukiwa katika mazingira kama haya usipumbazike, ukafanana na ulimwengu. Bali fahamu kuwa wapo, isipokuwa Mungu amewaficha tu. Siku watakapoondolewa waovu duniani ndipo utajua kuwa Mungu anao watakatifu wake, wengi.

Ndio maana ya hilo neno Bali “waangamiapo wasio haki, wenye haki huongezeka”.

Binti ambaye unatembea kwa kujisitiri barabarani, na huwenda huoni aliye kama wewe mtaa mzima, usife moyo, ni kwasababu wasio haki ni wengi. Kijana uliyeamua kuishi maisha ya mbali na uzinzi na anasa usijidhani upo peke yako, songa mbele tambua, ni  Mungu amewaficha tu watu wake. 

Kwasababu ni Neno la kweli kabisa wasio haki wastawipo, wenye haki hujificha, (sio kwamba wamekufa, bali wapo). Wakati utafika waovu wataondolewa, na sisi tutamiliki na kuangaza. Usiwe mfauta wimbi, nyakati hizi ni za hatari. Ni sawa na kichuguu tu, waweza kudhani hakina kumbikumbi ndani, kina huoni chochote kinachotoka humo,  lakini wakati wa mvua, unastaajabia wingi wao umetoka wapi. Vivyo hivyo na wewe endelea kutembea kwa ujasiri katika wokovu wako. Unyakuo umekaribia. Tambua Bwana analo jeshi lake.

Mithali 28:28 Wasio haki wainukapo, wanadamu hujificha; Bali waangamiapo, wenye haki huongezeka.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Miungu wasio na kikao pamoja na wenye mwili.

Nawiwa na Wayunani na wasio Wayunani.

Semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; (Luka 17:10) 

Rudi Nyumbani

Print this post

Tafsiri ya Mithali 27:15 Kutona-tona daima siku ya mvua nyingi, Na mwanamke mgomvi ni sawasawa;

SWALI: Nini maana ya Mithali 27:15 Kutona-tona daima siku ya mvua nyingi, Na mwanamke mgomvi ni sawasawa;


JIBU: Neno Kutona-tona kama lilivyotumika hapo, ni “maji yanayovuja darini”.

Hivyo anaposema Kutona-tona daima siku ya mvua nyingi. Anamaanisha kitendo cha kuvuja sana kwa dari siku ya mvua nyingi, na kitendo cha kukaa na mwanamke mgomvi ndani ni sawasawa.

Kwa namna gani?

Tunajua ukikaa kwenye nyumba ambayo dari lake halikujengwa vizuri, mvua kubwa inaponyesha maji mengi huchuruzika na kuingia ndani. Wakati umelala utashangaa maji yanakudondekea kitandani mwako, yanachuruzikia kwenye makochi, yanakwenda mpaka kwenye makapeti, jambo ambalo litakufanya usitulie hata kidogo humo ndani utakuwa tu bize, kusogoza vitu ovyo ovyo visilowe, na mbaya ni pale mvua inapokuwa kubwa, na maji kuongezeka ndani, mwisho huwa ni kutoka kabisa nje na kuiacha nyumba.

Ikiwa umeshawahi kupitia changamoto kama hiyo ya kuvujiwa nyumba, unaelewa ni kero kiasi gani.

Ndivyo anavyofananisha kutendo hicho na kuishi na mwanamke mgomvi. Ikilenga hasaa wanandoa. Kumbuka aliyeandika mithali hizi ni Sulemani, alikuwa anatambua anachokisema, kwasababu aliishi na wanawake elfu moja(1000) kama wake zake, na alijua masumbufu yao. Alikutana na changamoto za baadhi yao.

Mwanamke mgomvi, kibiblia ni Yule asimheshimu mumewe, ni Yule anayemwendesha mumewe, anayemkaripia, asiyekuwa msikivu, kila jambo analolifanya mumewe ni kulikosoa tu, mwenye kiburi na mwenye maneno mengi, asiye na staha.

Wanawake wa namna hii, huwataabisha waume zao sana, na hatimaye wengine huwafanya wahame kabisa nyumba, kukaa mbali na familia zao. Ni dari linalovuja utawezaje kukaa kwenye nyumba hiyo?

Andiko hilo limerudiwa pia katika;

Mithali 19:13 Mwana mpumbavu ni msiba kwa babaye; Na ugomvi wa mke kama kutona-tona daima.

Uonapo familia zenye migogoro ya namna hii ni kuziombea sana Bwana aziponye.

Maandiko hayo yamewekwa sio kuonyesha mabaya kwa jinsia ya kike, hapana, bali imetoa tahadhari ili yasitokee kwa wanawake wa kikristo.

Biblia imetoa mwenendo wa mwanamke halisi wa kikristo, inasema  awe ni wa kumtii mume wake. Awe ni mwenye kiasi, na MPOLE, na adabu. Akifanya hivyo atasimama vema kwenye nyumba yake, badala ya kuiharibu kinyume chake ataijenga.

1Timotheo 2:9  Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;

10  bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.

11  Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna.

Soma pia.

1Petro 3:1  Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno;

2  wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu. 3  Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;

4  bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, ROHO YA UPOLE NA UTULIVU, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.

5  Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao.

6  Kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yo yote.

Hivyo wewe kama mwanamke ukitembea katika hayo, utakuwa katika upande salama wa Mungu.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Wokovu wa milele/ Ulinzi wa daima (eternal security) Je! ni neno la kimaandiko?

HUIJUI KAZI YA MUNGU, AFANYAYE MAMBO YOTE.

ALIJARIBIWA SAWASAWA NA SISI KATIKA MAMBO YOTE.

Rudi Nyumbani

Print this post

JE UNAZAA MATUNDA NA KUWAPONYA MATAIFA?

Sisi tuliookolewa pamoja na Bwana wetu Yesu Kristo, tunafananishwa na mti mmoja alioupanda Mungu mwenyewe ulimwengu. Na wote tunayo sehemu katika mti huo, na tumewekewa wajibu wa kufanya.

Bwana wetu Yesu Kristo anafananishwa na shina la mti, halafu sisi tunafananishwa na matawi.

Shina ni kuanzia kwenye mizizi, hadi mahali matawi yanapotokea. Hivyo Bwana wetu Yesu, ndiye anayechukua uhai wetu moja kwa kutoka kwa Mungu na kutuletea sisi. Lakini sisi ni kuanzia kwenye matawi mpaka kwenye matunda.

Yohana 15:1-2,5

[1]Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. 

[2]Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa….

[5]Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. 

Sasa wengi wetu tunachoona katika mashina ni matunda tu peke yake. lakini leo ni vema tuone jambo hili kwa ndani. Kwa kawaida tawi huundwa na vitu viwili, cha kwanza ni majani, na cha pili ni matunda.

na vyote viwili vinapaswa vionekane katika shina. 

Hivyo mimi na wewe kama watakatifu, ni lazima tujiulize je majani yapo? na je matunda  yake pia yapo? 

Matunda ni nini?

Tafsiri ya awali ya matunda kama ilivyozungumziwa kwenye mfano ya mti, sio kuwavua watu kwa Kristo, kama inavyodhaniwa, hapana bali ni Kutoa tunda la wokovu wako. Yaani tunda la toba.

Yohana mbatizaji kwa uvuvio wa Roho alilifafanua vema..Tusome.

Mathayo 3:7-10

[7]Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? 

[8]Basi zaeni matunda yapasayo toba; 

[9]wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto. 

[10]Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. 

Aliwaona mafarisayo ambao walikiri kwa ujasiri wao ni wajumbe wa Yehova, uzao wa Ibrahimu, lakini mioyoni mwao, maovu na machafu ya kila namna yamewajaa. Hivyo wakaonekana ni miti isiyo na matunda.

Matunda ndio yale yanayojulikana kama tunda la Roho, ambayo kila mwamini anapaswa afanye bidii kuyatoa moyoni mwake katika maisha yake yote ya wokovu, awapo hapa duniani. Ambayo ni; 

Wagalatia 5:22

[22]Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu

[23]upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. 

Mtu yeyote anayefanya bidii kuonyesha wokovu wake kimatendo, mtu huyo humzalia Mungu matunda, ambayo ndio chakula cha Roho wa Mungu. Na hivyo hufurahishwa sana na sisi..

Majani ni nini?

Lakini kama tulivyosema shina huundwa na majani pamoja na matunda. Sasa majani, ni utumishi ambao kila mmoja wetu amepewa wa kuwavuta wengine kwa Kristo, kwa karama aliyopewa ndani yake. 

Tuliagizwa na Bwana tuenende ulimwenguni kote, tukahubiri injili na kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi wake (Mathayo 28:19),

Unapowashuhudia wengine, ni kwamba majani yako yanawaponya mataifa, na hivyo unawaokoa. Kumbuka majani kimsingi hayana ladha, mara nyingi hutumika kama tiba. Ndicho Bwana anachokifanya kwa wenye dhambi kupitia sisi, tunapowashuhudia.

Ufunuo wa Yohana 22:1-2

[1]Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo, 

[2]katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na MAJANI YA MTI HUO NI YA KUWAPONYA MATAIFA. 

Umeona? Kumbe majani yake, ni lengo la kuwaponya mataifa, watu wasiomjua Mungu. Tujiulize je na sisi tunayaponya mataifa kwa kuhubiri injili?

Wewe kama mkristo uliyemshirika wa mti wa uzima huna budi kuwa mhubiri wa injili usikae tu, hivi hivi ukasema tayari nimeokolewa inatosha, fanya jambo kwa Bwana. Waeleze wengine habari za Yesu, waponywe. Usijidharau ukasema siwezi, kumbuka aitendaye kazi hiyo ni Kristo ndani yako, wewe ni tawi tu. washuhudie wengine.

Lakini si kuhubiri tu, halafu maisha yako yapo kinyume na Kristo, hapana hilo nalo ni hatari, ukiwa na majani tu, halafu huna matunda ya wokovu moyoni mwako..Utalaaniwa.

Marko 11:13

[13]Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini.

[14]Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia. 

Umeona hawa ni watu, wanaodhani kumtumikia Mungu tu yatosha hakuna haja ya kuishi maisha matakatifu. wanakutwa na majani tu peke yake.

Tuhakikishe tuna majani, lakini vilevile tuna matunda kwasababu sisi ni shina, ndani ya mti wa uzima. Na neema ya Mungu itatusaidia.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Tafsiri ya Mithali 27:18 Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake;

KWANINI MTINI KATIKATI YA MIZABIBU?

UMEIZALIA MATUNDA MIAKA 4 YA NEEMA ULIYOPEWA?

Rudi Nyumbani


 

Print this post

Je kazi ya udalali ni dhambi?

Swali: Je kazi ya udalali ni dhambi, na Mkristo anaruhusiwa kuifanya?


Jibu: Dalali ni yule mtu anayeuza kitu kwa niaba ya mwingine na kisha kuchukia asilimia fulani ya faida ya kile kilichouzwa.

Au pia dalali anaweza kuwa mtu mwenye kutafuta soko la bidhaa ya mtu mwingine na kisha kuchukua asilimia ya faida inayopatikana.

Kama hiyo ndio maana au tafsiri ya udalali, basi mtu akiifanya “SI DHAMBI”, Kwani hata ununuaji wa bidhaa kiwandani na uuzaji masokoni kwa namna moja au nyingine ni “Udalali”, kwani utanunua kwa gharama ndogo na kuuza kwa gharama kubwa na kisha kuichukua ile faida….Hapo tayari umeshakuwa dalali wa wenye kuitengeneza ile bidhaa..

Kwahiyo udalali si dhambi ikiwa tu haujahusisha mambo yafuatayo.

   1. UONGO.

Labda umepewa kazi ya kutafuta mteja wa bidhaa husika, halafu ukampata na kumwekea kiwango cha juu sana nje na mapatano na yule aliyekupa bidhaa (lengo la kufanya hivyo ni ili wewe upate faida kubwa na ya haraka)…

Au mteja amehitaji bidhaa au nyumba na wewe ukamlaghai kwa uongo na kumpa kitu ambacho kiko chini ya viwango na huku ukijua kabisa kuwa kitu hiko hakistahili hiyo gharama, Huo wote ni Uongo na udalali huo ni haramu.

   2.Dhuluma.(Utapeli).

Unapomdhulumu mtu fedha au bidhaa yake, aidha kwa kumlipa kisasi au kwasababu nyigine yoyote udalali huo ni haramu.

3. Haifanyiki ndani ya nyumba ya Mungu..

Udalali unaofanyika ndani ya Nyumba ya MUNGU ni haramu..

Utaona Bwana YESU aliwafukuza wale madalali wote waliokuwa wanabadili fedha ndani ya nyumba ya MUNGU.

Yohana 2:15 “Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao;”

Vivyo hivyo kanisani si sehemu ya minada, na udalali, ni sehemu ya Ibada takatifu ya roho na kweli.

Swali lingine je?…Fedha ya udalali inaweza kutolewa sadaka ikiwemo Zaka?.

Jibu ni Ndio!.. kama  udalali huo haujahusisha mambo hayo hapo juu, basi inaweza kutolewa sadaka ikiwemo Zaka(yaani fungu la Kumi), na ikakubalika mbele za Mungu.

Na je mkristo anaweza kufanya kazi ya udalali??..

Jibu ni Ndio! Anaweza kufanya, ikiwa hatatumia Uongo, au dhuluma, au rushwa, au kufanya ndani ya kanisa la Mungu.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

KAMA MHUBIRI USIWE MFANO WA DIOTREFE.

UNAWAFAHAMU MANABII WA UONGO?

TUZIJARIBU HIZI ROHO.

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

WALA HAKUSIMAMA MTU PAMOJA NAYE, YUSUFU ALIPOJITAMBULISHA KWA NDUGUZE

Rudi Nyumbani

Print this post

JE UMEJIFUNZA ULE WIMBO MPYA?

Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo, Tukijua kuwa ule mwisho unakaribia, hatuna budi siku baada ya siku tujichunguze je! Tumekamilika vema? ili siku ile tusionekane na mawaa mbele zake. Tulipokee taji timilifu tuliloandaliwa mbinguni na mwokozi wetu Yesu Kristo kwa neema zake.

Leo, napenda tufahamu juu ya wimbo mpya. Kama wewe ni msomaji mzuri wa kitabu cha Ufunuo. Utagundua zimetajwa nyimbo kuu tatu.

  1. Wimbo wa Musa
  2. Wimbo wa Mwanakondoo
  3. Wimbo mpya

Swali ni je! Hizi nyimbo ni zipi na zinatimiaje?

Wimbo wa Musa na wa mwanakondoo tunazisoma, katika Ufunuo 15:2-3

Ufunuo 15:2  Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, na wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kando-kando ya hiyo bahari ya kioo, wenye vinubi vya Mungu.

3  Nao WAUIMBA WIMBO WA MUSA, MTUMWA WA MUNGU, NA WIMBO WA MWANA-KONDOO, wakisema, Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa

Wimbo wa Musa, ni injili ya Musa, ambayo iliwafanya watu wa kale, kutembea katika hiyo ili wamkaribie Mungu, ndiyo ile torati, ambayo wale waliokuwa katika agano la Ibrahimu kwa uzao, walirithi neema hiyo. Hivyo wana wa Israeli wote walikuwa wanauimba wimbo wa Musa. Yoyote ambaye hakuwa hana wimbo huo, basi wokovu au kumkaribia Mungu hakukuwezekana kwake.

Lakini wimbo wa Musa haukuwa na ukamilifu wote kwasababu ulikuwa ni wa mwilini, na wa kutarajia ahadi ya mwokozi mbeleni. Hivyo Mungu akaleta wimbo mwingine mpya kwa wanadamu wote. Ndio huo wimbo wa mwana-kondoo.

Ambayo ni injili ya neema iliyoletwa na Bwana wetu Yesu Kristo na kuhubiriwa na mitume wake. Kwa ufupi sisi wote tuliomwamini Yesu Kristo katika agano hili jipya, kwa pamoja tunauimba wimbo wa mwana-kondoo. Ndio maana kiini cha imani, na wokovu wetu ni Yesu Kristo. Mtu yeyote ambaye hajaoshwa dhambi zake kwa damu ya Yesu, hawezi kumwona Mungu, wala kamwe hataweza kumwelewa, haijalishi ataonyesha bidii zake nyingi kiasi gani. Kwasababu ndio utimilifu wote.

Lakini upo wimbo mwingine wa Tatu ndio huo wimbo mpya.

Wimbo huu, si wote watakaoweza kuuimba, lakini watakaoweza kuuimba watakuwa karibu sana na mwana-kondoo (Yesu Kristo), baada ya maisha haya. Ndio wale washindao, Ndio wale Yesu aliosema atawakiri mbele ya Baba na malaika zake, ndio wale watakaoketi pamoja naye katika viti vya enzi, ndio wale watakaotoka mashariki, magharibi, kaskazini na kusini, kula mkate naye mezani pake. Na vigezo amevianisha pale. Anasema..

Ufunuo 14:1  Kisha nikaona, na tazama, huyo Mwana-Kondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu mia na arobaini na nne elfu pamoja naye, wenye jina lake na jina la Baba yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao.

2  Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni, kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu. Na hiyo sauti niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi, wakivipiga vinubi vyao;

3  na KUIMBA WIMBO MPYA mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele ya wale wenye uhai wanne, na wale wazee; WALA HAPANA MTU ALIYEWEZA KUJIFUNZA WIMBO ULE, ila wale mia na arobaini na nne elfu, WALIONUNULIWA KATIKA NCHI.

4  HAWA NDIO WASIOTIWA UNAJISI PAMOJA NA WANAWAKE, KWA MAANA NI BIKIRA. Hawa ndio wamfuatao Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo.

5  NA KATIKA VINYWA VYAO HAUKUONEKANA UONGO. MAANA HAWANA MAWAA

Kama tunavyoweza kuona hapo tabia za wale walioweza kuuimba wimbo huo ni mbili;

  1. Hawakutiwa unajisi na wanawake.

Hapo hamaanishi kuwa hawakuwa wazinzi, hapana, (ni kweli uzinzi sio jambo lao) bali anamaanisha hasaa uzinzi wa rohoni, yaani Kumwabudu Mungu pamoja na sanamu. Na sanamu kwa wakati wetu si tu vile vinyago vya kuchonga tu, bali pia ni kitu chochote kinachochukua nafasi ya Mungu wako moyoni. Wengine mali, wengine tv,  wengine mipira, wengine elimu, wengine ma-magemu, wengine ushirikina, wengine udhehebu. Hizo ni sanamu, unapozidhibiti wewe kama mkristo hiyo ni hatua mojawapo ya kuweza kuuimba wimbo huo mpya.

Lakini anasema..

  1. Katika vinywa vyao haukuonekana uongo, maana hawana mawaa.

Ni watu walionena kweli yote ya  Mungu (injili ya Kristo), wala hawakuibatilisha kwa ajili ya fedha, au maslahi, au cheo, au unafki au wafuasi. Bali waliitetea kweli yote ya Mungu na kuiishi pia, . Maana yake mimi na wewe tukiinena kweli ya Kristo na kuiishi, basi vinywani mwetu tunakuwa hatuna uongo.

Na matokeo ya mtu wa jinsi hii, ni kwamba anakuwa nafasi maalumu sana mbinguni(Ufunuo 5:8-9), Ni sawa na leo unajisikiaje unapoitwa uishi ikulu na raisi wako? Unajisikiaje kila mahali aendapo na msafara wake wewe upo pamoja naye. Anapopokea heshimu, na wewe unapokea naye.

Hivyo bidii ina malipo. Nyakati tulizonazo sio kusema nimeokoka hiyo inatosha!.. Ni nyakati za kujifunza wimbo huu mpya kwa bidii. Kutijahidi kumpendeza Bwana. Na yeye mwenyewe ameahidi neema yake itatusaidia.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

KARAMU YA MWANA-KONDOO.

JE! NI DHAMBI KUIMBA WIMBO WA TAIFA?

Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule(Kutoka 12:4)

Rudi Nyumbani

Print this post

MWONGOZO WA MAOMBI YA FAMILIA

 

Huu ni mwongozo wa maombi maalumu kwa ajili ya familia yako. Kama watakatifu, ni wajibu wetu kuziombea familia, Lakini sio kuziombea tu, bali kufahamu maeneo muhimu ya kugusia kwenye maombi hayo. Huu ni mwongozo maalumu wa maombi ya familia. Bofya juu ufungue chapisho hilo (pdf)

Pia Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MWONGOZO WA MAOMBI YA ASUBUHI.

TEMBEA NDANI YA SUKOTHI YAKO.-Maafundisho maalumu kwa watumishi

Print this post

VUA SAMAKI, NA SAMAKI WASIKUVUE WEWE.

(Masomo maalumu kwaajili ya watumishi).

Kama Mhubiri au Mtumishi wa Mungu, usiupende ulimwengu wala usiikimbia sauti ya Mungu.

Bwana YESU alimwambia Petro maneno haya…

Luka 5:10 “na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, TANGU SASA UTAKUWA UKIVUA WATU”.

Hapa tunaona Bwana YESU anawafananisha “watu” na “samaki”…na “dunia” anaifananisha na  “bahari”…

Tena anazidi kulithibitisha hili katika Mathayo 13:47- 49..

Mathayo 13:47 “Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna;

48  hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa

49  Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki,”

Kama samaki wanawakilisha watu waliopo duniani, basi Injili ya BWANA YESU ndio NYAVU na Bwana amekusudia tuwavue watu (samaki) kutoka katika dunia, na si samaki watuvue sisi na kutushusha baharini. Maana yake samaki wanatakiwa watolewe kwenye maji, na si samaki watuvute sisi majini.

Utauliza je! MHUBIRI anaweza kuvuliwa na samaki?.. jibu ni NDIO!

Utakumbuka kisa cha YONA? Alipoikimbia sauti ya BWANA, ni nini kilitokea?, biblia inasema ALIMEZWA na samaki na akakaa tumboni mwa samaki siku tatu.

Yona 1:17 “Bwana akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku”

Vile vile, na mtumishi/mhubiri anayeikimbia sauti ya Mungu, kitakachofuata ni KUMEZWA NA WATU WA ULIMWENGU, (Mtu huyu anawekwa mikononi mwa watu wakuu wa ulimwengu) ambao hawana huruma, wenye nguvu kuliko yeye.

Tumbo la samaki ni vifungo vyote vya mateso vya watu wa kidunia,

Je wewe ni Mhubiri??…Isikie sauti ya Mungu, simama hubiri Neno la Mungu, usiende njia ya bahari (ya ulimwengu)…Ukienda njia ya ulimwengu ya bahari) iwe kwa lengo la kuhubiri sio kwa kufuata mambo yako, kwani bahari ina hatari nyingi.

Usiwe kama Nabii Yona ambaye aliikimbia sauti ya Mungu na kwenda njia ya bahari, na akapata ajali ile.

Bwana atusaidie sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

UNAMCHUKULIA YESU KWAKO KAMA NANI?

Makasia ni nini? (Yona 1:13).

MADHARA YA KUTAFUTA ISHARA.

TWEKA MPAKA VILINDINI.

NI MAJIRA YAPI YA NEEMA WEWE UPO?

Rudi Nyumbani

Print this post

Je gharika ya Nuhu iliangamiza hadi samaki wa baharini na nyangumi?.

Jibu:  Jibu la swali hili tutalipata katika ule mstari wa 22, sura ya 7 ya kitabu cha Mwanzo…

Mwanzo 7:22 “kila kitu chenye pumzi ya roho ya uhai puani mwake kikafa, kila kilichokuwako katika nchi kavu”.

Hapo yanatajwa mambo mawili, 

 1. Kila chenye roho ya uhai puani kikafa.

Kufuatia andiko hili, ni wazi kuwa samaki hawapumui kupitia pua kwasababu wao wapo chini ya maji..

2. Pia Kila kilichokuwako katika nchi kavu.

Kupitia maneno haya ni wazi kuwa gharika haikuwahusu viumbe wa majini  au baharini, kwasababu hao hawaishi nchi kavu.

Vile vile hatusomi popote kuwa Nuhu aliingiza nyangumi, au kambale ndani ya safina, badala yake tunaona ni wanyama tu peke yao, na tena walimfuata Nuhu mwenyewe na wala Nuhu hakwenda kuwatafuta, sasa kwa mantiki hiyo nyangumi wangemfuataje Nuhu safinani?.

Kwahiyo ni wazi kuwa gharika ile ilihusu viumbe waliooishi nchi kavu, ambao ni wanadamu ndege, wanyama na wadudu.

Mwanzo 7:20 “Maji yakapata nguvu, hata ikafunikwa milima kiasi cha mikono kumi na mitano. 

21 Wakafa wote wenye mwili waendao juu ya nchi, na ndege, na wanyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu, na kila kitambaacho chenye kutambaa juu ya nchi, na kila mwanadamu”

Sasa kama ni hivyo, basi samaki walihifadhiwa wapi wakati wa gharika?

Jibu ni kwamba samaki waliendelea kubaki majini wakati wa gharika.

Lakini pamoja na hayo biblia inatabiri ujio wa gharika nyingine ambayo si ya maji tena bali ya moto, ambapo viumbe vyote vitafumuliwa na hakuna kitakachosalia..

2 Petro 3:6 “kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia. 

7 Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu. 

8 Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. 

9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba. 

10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. 

11 Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa”.

Bwana atusaidie tukae katika mwenendo wa UTAKATIFU na UTAUWA.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

NAYE AKASIMAMA JUU YA MCHANGA WA BAHARI.

NUHU WA SASA.

UNAMCHUKULIA YESU KWAKO KAMA NANI?

KWANINI NI NUHU, AYUBU NA DANIELI?

Makasia ni nini? (Yona 1:13).

Rudi Nyumbani

Print this post

Bwana alimaanisha nini kusema “Yeye aapaye kwa hekalu, huapa kwa hilo”? (Mathayo 23:20)

Jibu: Ili tuweze kuelewa vizuri, turejee mistari hiyo (kuanzia ule mstari wa 16 -22).

Mathayo 23:16  “Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga.

17  Wapumbavu ninyi na vipofu; maana ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au lile hekalu liitakasalo dhahabu?

18  Tena, Mtu atakayeapa kwa madhabahu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa sadaka iliyo juu yake, amejifunga.

19  Vipofu ninyi; maana ni ipi iliyo kubwa, ile sadaka, au ile madhabahu iitakasayo sadaka?

20  Basi yeye aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hiyo, na kwa vitu vyote vilivyo juu yake.

21  Naye aapaye kwa hekalu, huapa kwa hilo, na kwa yeye akaaye ndani yake.

22  Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa yeye aketiye juu yake”.

Shabaha kubwa ya Bwana YESU hapo si kuhalalisha VIAPO, Kwamba ni halali Mtu kuapa kwa Hekalu au kwa maadhahabu!.. La! Hiyo haikuwa shabaha yake kwani tayari alishaonya kuhusu viapo katika Mathayo 5:33-37.

Mathayo 5:33 “Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo, ila mtimizie Bwana nyapo zako;

34  lakini mimi nawaambia, USIAPE KABISA; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;

35  wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu.

36  Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. 37  Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu”.

Na Pia Mtume Yakobo akaliandika jambo hilo hilo katika Yakobo 5:12.

Kwahiyo lengo la Bwana YESU halikuwa kuhalalisha viapo, bali ni kuonyesha UOVU na UNAFIKI wa viongozi hao wa kiyahudi (Mafarisayo na Masadukayo na waandishi) kupitia viapo vyao!. Kwamba wanavipa nguvu viapo vya sadaka Zaidi ya viapo vya Hekalu ambalo ndani yake lina Mungu na sadaka pia…Lakini wenyewe wanatazama sadaka tu!.

Maana yake ni kwamba kama Mtu ameapa kutoa sadaka (dhahabu au kitu kingine chochote) basi amejifunga (maana yake ni lazima atimize kiapo chake hicho, na asipotimiza ni dhambi kubwa)..lakini kama ameapa tu kwa kwa hekalu (labda kuabudu siku hiyo hekaluni, na asiabudu), basi sio kosa kubwa sana!!..

Ila kwa upande wa dhahabu (sadaka), ni kosa kubwa! Pasipo kuona kuwa Hekalu/Madhabahu ni kuu kuliko sadaka! Kwamba aliyeapa kwa Hekalu kaapa jambo kubwa sana kuliko yule aliyeapa kwa sadaka (dhahabu) peke yake itolewayo Hekaluni… kwasababu ndani ya Hekalu ndiko kwenye taratibu zote za matoleo, na si ndani ya matoleo ndio kwenye Hekalu…Ila Mafarisayo walikuwa hawalioni hilo, na ndio maana Bwana YESU anawaita vipofu.

Na kwanini walikuwa wamevipa hadhi kubwa viapo vya sadaka kuliko vya Hekalu??… Hakuna sababu nyingine Zaidi ya kwamba walikuwa wanapenda fedha!!!, walijua ya kwamba wakiwabana watu katika matoleo basi watanufaika Zaidi, hivyo walijali matoleo kuliko Hekalu la Mungu pamoja na madhabahu yake..

Na jambo hilo hilo utaona Bwana YESU alilirudia juu ya “vile vipasavyo kuwasaidia wazazi”..ambapo Mafarisayo walisema endapo mtu akipata chochote na kile anaweza kukifanya chote wakfu (yaani Korbani) na wala asiwape chochote wazazi, na isiwe dhambi!… jambo ambalo ni baya sana! (soma Marko 7:11).. na kwa maelezo marefu juu ya habari hiyo ya Korbani fungua hapa >>>>Neno Korbani linamaanisha nini? (Marko 7:11)

Mfano kamili wa baadhi ya viongozi wa kiimani wa leo??…. Utaona wanathamini Matoleo Zaidi ya Hekalu la Mungu na taratibu zake. Utaona mtu akiahidi kuja kanisani na asije, haiwi shida….lakini hebu mtu aahidi kutoa halafu asitoe!, inakuwa ni vita vikali na ni laana kubwa!…pasipo kujua kuwa nyumba ya Mungu ni kuu kuliko sadaka, kwasababu ndani ya nyumba ya Mungu kuna matoleo!.. (Na mtu akiiheshimu nyumba ya Mungu ataheshimu pia matoleo).

Bwana atusaidie sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Ipi tofauti kati ya matoleo na sadaka?

WEWE NI HEKALU LA MUNGU.

JE! UNA MASIKIO YANAYOSIKIA?

UJIO WA BWANA YESU.

CHACHU YA MAFARISAYO NA CHACHU YA HERODE.

Rudi Nyumbani

Print this post