Nimempa Shetani watu hao, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.

Nimempa Shetani watu hao, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.

SWALI: Naomba kufahamu maudhui ya mstari huu,

1Timotheo 1:20 “Katika hao wamo Himenayo na Iskanda, ambao nimempa Shetani watu hao, ili wafundishwe wasimtukane Mungu”.


JIBU: Awali ya yote, kabla ya kufahamu ni kwanini Mtume Paulo anatoa hukumu kali kama hiyo tuangalie mistari ya juu yake ambayo inaeleza sifa, za hao watu.

Ukisoma mstari wa 19, Paulo anamuasa Timotheo, awe ni mtu mwenye Imani, lakini sio Imani tu, bali pia “dhamiri njema”.. Ni vitu vinavyokwenda sambamba.

1Timotheo 1:19 “uwe mwenye imani na dhamiri njema, ambayo wengine wameisukumia mbali, wakaangamia kwa habari ya Imani.

20 Katika hao wamo Himenayo na Iskanda, ambao nimempa Shetani watu hao, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.”

Dhamiri ni kile kitu cha ndani kinachomshuhudia mtu kwamba anachokifanya ni sahihi au sio sahihi. Hivyo pale mtu anapokuwa na dhamiri njema, maana yake ni kuwa, anaitii nafsi yake, inapofanya kosa, pale inaposuta, anakuwa tayari kugeuka. Hivyo mtu kama huyu huwa anaishi kwa kujichunga, na kuwahurumia na kwa kuogopa hukumu pale anapojaribu kuwapotosha watu.. Kwasababu dhamiri yake njema inamshitaki.

Lakini mtu ambaye hana dhamiri njema, ni kwamba, hata anapoona jambo Fulani alifanyalo ni baya, anastahili hukumu, yeye hajali, bali anafanya atakalo, kwa maslahi yake. Atakuwa tayari kuwafundisha watu mafundisho potofu kwa makusudi kabisa akijua kabisa alifanyalo ni upotevu, lakini yeye ataendelea kufanya, kwa furaha kabisa..

Sasa ndio hapo mtume Paulo, anawatolea mfano watu hao, waliokosa dhamiri njema. Ambao ni Himenayo, na Iskanda. Watu hawa walikuwa ni wabaya, kwasababu walikuwa wanapindua Imani za watu kwa makusudi, wala sio kwa bahati mbaya wakiwafundisha kinyume na mafundisho ya mitume,.

Kwamfano huyu Himenayo, tunasoma tena, Paulo akieleza mafundisho yake potofu, ya kuwaambia watu Ufufuo wa wafu tayari umeshatokea.. Hivyo watu wengi wakaiacha Imani na kumgeukia yeye.

2Timotheo 2:16 “Jiepushe na maneno yasiyo na maana, ambayo si ya dini; kwa kuwa wataendelea zaidi katika maovu,

17 na neno lao litaenea kama donda-ndugu. Miongoni mwa hao wamo Himenayo na Fileto,

18 walioikosa ile kweli, wakisema ya kwamba kiyama imekwisha kuwapo, hata kuipindua imani ya watu kadha wa kadha”.

Na mwezake Iskanda, ambaye wengi wanaamini ndio huyu aliyezungumziwa katika vifungu hivi; Ambaye alimpinga sana Paulo katika kazi zake za kihuduma.

2Timotheo 4:14 “Iskanda, mfua shaba, alionyesha ubaya mwingi kwangu; Bwana atamlipa sawasawa na matendo yake.

15 Nawe ujihadhari na huyo, kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu”.

Hivyo, makundi haya, Mtume Paulo hakushughulika nayo kabisa, bali kwa mamlaka aliyopewa, aliwaacha mikoni mwa shetani, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.  Maana yake ni kuwa, ulinzi wa Mungu uliondolewa juu yao, ili shetani apate nafasi ya kuwashughulikia, ili yamkini watubu.

Aidha walikumbwa na magonjwa, au mapigo, au hata vifo hatujui.. Lakini kuwekwa mikoni mwa shetani, adhabu kali kama hizo utakumbana nazo.(Tunaona kwa ayubu pale  alivyoondolewa wigo wa ulinzi na Mungu, jinsi majangwa makali yalivyompata)..Ndivyo ilivyokuwa kwa hawa wakina Himenayo na mwenzake.

Hii ni kutufundisha  nini?

Yapo mamlaka ambayo Watakatifu wamepewa, kwa watu ambao wanauchezea ukristo, Ikiwa unafanya dhambi kwa makusudi, angali unaujua ukweli, na upo ndani ya mwili wa Kristo, kuwa makini sana, kwasababu hukumu yoyote itakayotolewa juu yako na wao lazima ikupate.. Na kama utakuwa unafanya kwa siri, kanisa halitajua, lakini Mungu atajua.. Na yeye mwenyewe atakuweka mikononi mwa ibilisi, upigwe. Ukishafikia hatua hii, waweza hata poteza Maisha yako.

Soma;

1Wakorintho 5:1 “Yakini habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye.

2 Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo.

3 Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi mwenyewe nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo.

4 Katika jina la Bwana wetu Yesu, ninyi mkiwa mmekusanyika pamoja na roho yangu, pamoja na uweza wa Bwana wetu Yesu;

5 kumtolea Shetani mtu huyo, ili mwili uadhibiwe, ili na roho iokolewe katika siku ya Bwana Yesu”.

Bwana atupe Imani ya kweli na dhamiri safi.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

DHAMBI YA MAUTI

Dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu ni ipi?

MFANO WA MAMBO HAYO NI UBATIZO.

MAZUNGUMZO MABAYA HUHARIBU TABIA NJEMA.

NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?

KAMA UNAPENDA MAISHA, NA KUTAKA SIKU YAKO IWE NJEMA.

Gumegume ni nini? (Isaya 50:7)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments