Category Archive Wanandoa

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 1: Upande wa wanaume)

Katika siku hizi za mwisho, migogoro ya kindoa imekuwa ni mingi sana, kiasi kwamba ndoa kudumu hata mwaka mmoja, ni jambo la kushukuru sana. Kila kukicha mikwaruzano, hakuna amani, kila mmoja amemchoka mwenzake. Mpaka wengine kudhani huyo mwenzi aliyemuoa au aliyeolewa naye halikuwa chaguo sahihi kutoka kwa Mungu, hivyo  suluhisho pekee ni kuachana.

Nataka nikuambie, kabla hujafikiria kuachana na huyo mwenzi wako, Tafuta kwanza kama kuna watu walishapitia tatizo kama hilo la kwako, na uone walilitatuaje tatuaje, au mwisho wao ulikuwaje..

Kumbuka kuvunjika kwa ndoa, ni kushindwa kwa pande zote mbili (au moja), kujua wajibu wake katika ndoa kama Neno la Mungu linavyoagiza..

Ndoa inafananishwa na safari ya Maisha/ ya wokovu, si wakati wote, itakuwa ni “HONEY MOON”, si wakati wote mtakuwa ni vijana, si wakati wote mtakuwa Pamoja, na si wakati wote mambo yataenda sawa.. Haijalishi ndoa hiyo, atakuwa ameifungishwa Mungu mwenyewe Kanisani au la.  Kushuka na kupanda kutakuwa ni sehemu ya Maisha yenu.

Leo hii tutajifunza, mfano wa ndoa moja maarufu katika biblia, na jinsi ilivyokumbana  na migogoro mikubwa sana, ambayo naamini ni Zaidi ya migogoro ya ndoa zote zilizowahi kutokea ulimwenguni, lakini Pamoja na hayo  bado iliendelea kudumu hadi dakika ya mwisho, naamini kwa kupitia hiyo itakuponya na wewe pia ambaye kwenye ndoa yako zimeshaanza kuonekana dalili za nyufa.

Na ndoa hiyo si nyingine Zaidi  ya ile ya ADAMU.

Adamu alichaguliwa mke na Mungu mwenyewe, tena aliyeumbwa kutoka katika ubavu wake kabisa,kuonyesha kuwa ni wake kweli kweli,. Lakini waliishi kwa kipindi Fulani kirefu kwa raha na furaha bila taabu wala shida yoyote,  hadi siku mambo yalipoanza kubadilika,

Na yalibadilika, kwa kukengeuka kwa mwanamke kwanza, pale ambapo aliacha kusikiliza maagizo ya mume wake(aliyopewa na Mungu), ya kutokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, lakini yeye akayala kwa tamaa ya kutaka kuwa kama Mungu, ya kutaka kuwa kichwa (yaani kumzidi hata mume wake),ya kutaka kumiliki,  akayala bila kumshirikisha mume wake, lakini kinyume chake ni kuwa tamaa hiyo Mungu aliipindua na kuihamishia kwa mume wake badala yake, na ndio maana utaona leo hii  kwanini wanaume wanauchu wa kutawala, kuwa vichwa, hiyo tamaa mwanzoni haikuwepo kwao bali ilikuwa kwa mwanamke, baada ya kuasi Mungu ndio akamuadhibu mwanamke kwa kosa hilo la kumuhamishia mwanaume.

Mwanzo 3:16 “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala”.

Sasa na baadaye Adamu alipoona, mke wake kaharibu, ameasi, akakubali na yeye, kuingia katika matatizo ya mke wake kwa hiari yake yeye mwenyewe (kwasababu yeye hakudanganywa), na baada ya hapo, Mungu akamlaani naye pia.

Tangu huo wakati, Maisha yakawa magumu kweli, kwasababu dhambi imeshaingia, kulima kwa shida kukanza, magonjwa yakazuka, vifo vikaingia, kila aina ya shida ikazuka tangu huo wakati na kuendelea, kila kukicha hali ndio ilizidi kuwa mbaya, hadi kwa Watoto waliowazaa, hakuna amani katikati yao, wakawa wanauana.. Embu tengeneza picha ingekuwa wewe ni Adamu ungemfanyaje huyo mwanamke baada ya hapo?

Ni wazi kuwa ungempa talaka siku ile ile ya kwanza alipofanya kosa lile si ndio?. Tena baada ya hapo ungekuwa ni wa kulaumu Maisha yako yote, kwamba Mungu amekupa mkosi na balaa, ni heri ungebakia tu peke yako bila kuoa, lakini tangu ulipompata huyo mwanamke, mambo yako ndio yameenda kombo kabisa kabisa…

Lile kampuni amelifilisi, mali zote zimepukutika umerudia umaskini ambao ulikuwa umeshauaga zamani, amekuletea gonjwa la ukimwi kwa kutanga tanga kwake, amekufanya utengane sio tu na ndugu zako, bali hata na Mungu wako. Mwanzoni ulikuwa  ukifanya ibada vizuri, lakini tangu umuoe yule mwanamke, muda kusali haupo! Kila kitu unakipata kwa shida, tofauti na ulivyokuwa ‘Single’.

Lawama kama hizo Adamu angestahili kuwa nazo kwa mke wake, Lakini hatuoni mahali popote Adamu alimwacha mke wake, na kutamani kuishi na wanyama kama hapo mwanzo, bali alimkumbatia, akakubaliana na hali, akamsamehe, akayapanga tena upya. Akijua kuwa ule tayari ni ubavu wake. Na Mungu hakukosea kumpa, lilikuwa ni chaguo sahihi.

Mwanaume,

Kumbuka kuwa, mpaka umefikia hatua ya kumwoa huyo binti/ mwanamke, ujue kuwa ndio UBAVU wako huo Mungu aliokupa, usidhani kumtambua mke mwema ni mpaka uishi naye bila migogoro, sikuzote za Maisha yako, si kweli. Huyo ambaye upo naye katika migogoro, ni wako, na atabakia kuwa wako mpaka kifo kitakapowatenganisha.

Unachopaswa kufanya ni wewe kusimama katika nafasi yako kama ADAMU.

Suluhisho sio kumwacha, kumbuka ukimwacha huyo maana yake, unataka kurudia kuishi na Wanyama, Mpende mke wako, kwasababu hakuna kitu kinachojenga Zaidi ya upendo, mkumbatie, msamehe, mjenge upya, mvumilie, pale anapokosa, hata kama alikuletea balaa kubwa namna gani, mkumbuke Adamu, alivyoweza kuwa mvumilivu, kwa kunyang’anywa kila kitu na Mungu lakini hakumwacha Hawa. Kwani biblia inasema aliishi miaka 930, na unajua mara nyingi wanawake huwa wanakuwa na umri mrefu kuliko wanaume, kwahiyo si ajabu kuona Adamu aliishi na mke wake kwa Zaidi ya miaka hata 800, lakini sisi miaka 3 tu tumeshachokana.

Biblia inasema..

Waefeso 5:25 “Enyi waume, WAPENDENI WAKE ZENU, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;

26 ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno;

27 apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.

28 Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.

29 Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa.

30 Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake.

31 Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja”.

UPENDO KWA MKE wako, ni agizo kutoka kwa Mungu, na sio ihari yako tu mwenyewe. Ukiwa mwanaume wa namna hii, nataka nikuambie utaiponya ndoa yako, na itadumu sana. Wanawake kukengeuka haraka, ni jambo la kawaida, lakini wakisharudi, wanakuwa ni lulu nzuri kwako. Jifunze kusamehe, na vilevile kumpenda.

Lakini hayo yote huwezi kuyafikia kama upo nje ya Kristo. Hivyo Okoka, mkaribishe Yesu katika Maisha yako, tubu dhambi zako, kwa kumaanisha kabisa, kisha ubatizwe, upokee Roho Mtakatifu, na Kristo atakupa uwezo huo, wa kumpenda mkeo kama alivyokuwa Adamu.

Bwana akubariki.

Usikose, sehemu ya pili ya Makala hii.. Ambayo inamlenga mwanamke, kama chanzo cha migogoro ndani ya ndoa, na afanye nini ili aweze kuiponya ndoa yake.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Je! “Mke wa ujana wako” ni yupi kibiblia?

Ndoa ya serikali ni halali?

NDOA NA HARUSI TAKATIFU.

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.

Rudi nyumbani

Print this post

MAFUNDISHO YA NDOA.

Mafundisho ya ndoa, na mahusiano.


Ikiwa wewe ndio kwanza unataka kuingia katika mahusiano Yapo mambo kadha wa kadha unahitaji kufahamu.

Jambo la kwanza:

ni lazima ujue njia sahihi ya kumpata mwenza wako, vilevile ujue wakati sahihi wa kumchagua huyo mwenza unayemtaka..

Hapa ndipo watu wengi wanapokosea, wakidhani ni yule tu anayevutia machoni huyo ndiye anayefaa, au ni ule wakati tu wanapojisikia kuoa au kuolewa ndio wanapopaswa waingie katika mahusiano. Ukitumia kanuni hiyo upo hatarini sana  kujutia huko mbeleni..Ni sharti kwanza utulize akili yako bila kuruhusu hisia zako kukuongoza..

Ili kufahamu kwa urefu njia sahihi ya kumpata Mwenza wa Maisha Bofya hapa >>NJIA SAHIHI YA KUMPATA MWENZA WA MAISHA KIBIBLIA.

Jambo la Pili:

Unahitaji kufahamu Mambo ya kuepukana nayo wakati mpo katika mahusiano ya uchumba. Watu wengi wanadhani ukishamchumbia binti, basi tayari mpo huru kufanya naye tendo la ndoa wakati wowote..Usijaribu kufanya hivyo kwasababu yapo madhara mengi na makubwa ya ndani na ya nje,.Kwanza Licha ya kuwa unafanya uasherati, ambao hata ukifa utakwenda jehanum, Lakini pia unapoteza baraka zote ambazo Mungu alikuwa ameshakuandalia kwa ajili ya ndoa yako inayokuja.. yapo madhara mengine pia,

Ili kufahamu zaidi madhara hayo na jinsi ya kujiepusha nayo bofya hapa >>JE NI DHAMBI KUWA NA MAHUSIANO KABLA YA NDOA?

Jambo la Tatu:

Ili ndoa yako iwe ni ya heri na mafanikio, na yenye kupokea baraka kamili kutoka kwa Mungu, Ni lazima ndoa hiyo  iwe imefungishwa na Mungu mwenyewe..Nikisema Mungu namaanisha KANISANI.

Wapo watu wanaosema, mimi nimefunga ndoa yangu kimila, wengine wanasema tumefunga kiserikalini, N.k., Haijalishi hizo zote utaziita ni ndoa, Lakini hizo sio ndoa za kikristo zinazostahili baraka zote za Kristo.

Ili kufahamu faida na madhara ya kutokufungika ndoa kanisani bofya hapa >> NDOA NA HARUSI TAKATIFU.


Sasa ikiwa wewe tayari umeshaingia kwenye ndoa, na umekidhi hivyo vigezo vyote hapo juu.

Basi yapo pia mambo kadhaa unahitaji kujua. Nimekutana na watu wengi wenye matatizo katika ndoa zao. Husasani wanawake, wengine wameachwa na waume zao, wengine wametelekezwa, wengine wao ndio wanamatatizo n.k.k

lakini zipo siri ambazo bado hawajazijua za mafaniko ya ndoa zao ambazo biblia imeziweka wazi..

Kwamfano Ukimtazama Ruthu, yule hakuwa mwanamke wa Kiyahudi kama wengine tuonaowasoma kwenye biblia, lakini jiulize ni kwanini hadi leo hii unamsoma katika maandiko matakatifu,vilevile ni kwanini uzao wake ulibarikiwa kuliko hata uzao wa wanawake wengine waliokuwa wazao wa kiyahudi,? kiasi kwamba mpaka mfalme Daudi, alipitishwa  katika uzao wake,na sio tu wa Daudi bali pia wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa kupitia Yusufu?..

Kama hujafahamu bado siri ni nini , leo nataka nikupe, siri ipo kwa MKWEWE, NAOMI..Hivyo Ili na wewe mwanamke ubarikiwe uzao wako, na uwe na jina kubwa basi siri yako ipo kwa wakwe zako, hilo haliepukiki..

Ili kufahamu Zaidi habari hizo bofya hapa..>>EWE MKE! HESHIMA YAKO IPO KWA WAKWE ZAKO.

Vilevile unahitaji kumfahamu mwanamke mwengine anayejulikana  kama ESTA.. Cha ajabu Esta na Ruthu ni wanawake wawili pekee ambao wanavitabu vyao maalumu vinavyojitegemea katika biblia nzima..Lakini cha kushangaza Zaidi ni kuwa wanawake wengi hawajua siri zilizo ndani ya wanawake hawa. Wanakimbilia kusoma habari za  wanaume, kama wakina Daudi, na Eliya, na Samweli, lakini wanaacha mafundisho ya msingi yanayowahusu kutoka habari za wanawake wenzao kama hawa..

Kama ulikuwa hujui Esta, mpaka amekuwa malkia ni kwasababu kulikuwa na mwanamke mwingine ambaye alikosa heshima kwa mume wake ambaye ni Mfalme, na hiyo yote ni kutokana na uzuri aliokuwa nao,..

Hivyo Baada ya mfalme kukiona kiburi chake ndipo akamtoa katika nafasi ya umalkia, na baadaye Esta akapata kibali cha kuchukua nafasi yake, ukisoma pale utaona Esta naye kilichomfanya awe malkia hakikuwa kigezo cha uzuri wake kama wengi wanavyodhani, au elimu yake, au umaarufu wake, hapana, bali kutoka kwa Hegai msimamizi wa mfalme…ambapo kuna  siri kubwa sana hapo unapaswa uifahamu pia wewe kama mwanamke..

kwa maelezo marefu bofya hapa>> ESTA: Mlango wa 1 & 2

Vivyo hivyo na wewe mwanamke, kudhani kuwa uzuri wako, au elimu yako, au fedha zako, ndio zinaweza kukufanya usimuheshimu mume wako, ukweli ni kwamba ndoa yako haitadumu, na atakayeilaani sio mume wako. Bali ni Mungu mwenyewe kwasababu umekosa kufuata kanuni za kimaandiko Mungu alizoziweka juu ya ndoa ya kikristo.

Waefeso 5:24  “Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo”

Vilevile, kama mwanamke unapaswa ujue nafasi yako katika familia, na katika kanisa la Kristo ni ipi…

Tumezoea kuona nyaraka nyingi zilizoandikwa na mitume zikielekezwa kwa makanisa au wanaume kama vile Timotheo, au Tito, au Filemoni, lakini Upo waraka mmoja mtume Yohana aliuandika kwa mama mmoja mteule..Ambao hata wewe mwanamke ukiujua ufunuo wake  utajifunza nafasi yako katika kanisa la Mungu na  uleaji wako wa Watoto.

Bofya hapa ili kufahamu zaidi >> MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

Vilevile na wewe  kama MWANAUME (Baba), ni lazima ufahamu nafasi yako pia katika Familia..

Jambo moja kwako ni hili  Bwana Yesu alisema..

Waefeso 5:25  “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;

26  ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno;

27  apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.

28  Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.

29  Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa.

30  Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake.

31  Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.

32  Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa.

33  Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe”

Ukimpenda mke wako, utamuhudumia, kwa chakula, kwa malazi, na makazi, ukimpenda mke wako utamtunza kwa mavazi, ukimpenda mke wako utawapenda na ndugu zake..Ukimpenda mke wako, utawapenda na Watoto wake, na hivyo utawatimizia majukumu yote ya nyumbani..

Lakini ukikosa akili kama Nabali alivyokuwa, Unakuwa mlevi, hujali wageni, huwi mkarimu, humchi Mungu, wala hutimizii familia yako mahitaji yake, wewe ni pombe tu, Ujue kuwa Mungu atakuuwa mwenyewe kabla ya wakati wako kama alivyomuua Nabali, na Mke wako mwenye akili ataenda kuolewa na mtu mwingine mwenye akili zaidi yako wee na atakayemjali kuliko wewe..kama ilivyokuwa kwa Abigaili mke wa Nabali.. (Soma 1Samweli 25 )

Sasa kwanini hayo yote yakukute?

Hivyo wote wawili mkizingatia kanuni hizo kila mmoja katika nafasi yake, basi muwe na uhakika kuwa Bwana ataifanya ndoa yenu kuwa ya amani siku zote, yenye mafanikio, na yenye matunda kwa Mungu.

Lakini Mwisho kabisa..

Kila mmoja analojukumu lake binafsi la kumtafuta Bwana, na kumpenda Bwana kuliko kitu kingine chochote. Kwasababu Biblia inasema, wakati tuliobakiwa nao ni mfupi..

1Wakorintho 7:29  “Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana”

Hizi ni nyakati za mwisho ambazo, biblia inatushauri tujikite Zaidi katika kuutafuta ufalme wa Mbinguni, kwasababu unyakuo upo karibu. Hivyo japokuwa utakuwa katika ndoa lakini usijiingize sana, au kwa namna nyingine usizamishwe sana katika mambo ya kifamilia mpaka ukasahau kuwa kuna wokovu na Unyakuo..Kwasababu hata huyo uliye naye, Akifa leo anaweza kuwa wa mwingine..Na Zaidi ya yote kule juu mbinguni tuendapo hakutakuwa na kuoa au kuolewa, Hivyo masuala ya ndoa si masuala ya kuyapa kipaumbele sana ziadi ya yale ya ufalme wa mbinguni..Lakini yape kipaumbele Zaidi ya mambo mengine ya kidunia.

Bwana akubariki sana.


Mada Nyinginezo:

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

KWANINI WENGINE WANYAKULIWE,NA WENGINE WAACHWE?

KIFO CHA MTAKATIFU PERPETUA NA FELISTA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

EWE MKE! HESHIMA YAKO IPO KWA WAKWE ZAKO.

Heshima na Baraka za mwanamke uliyeolewa zipo kwa wakwe zako (hususani mama mkwe wako).

Vitabu viwili vikuu vilivyoitwa kwa majina ya wanawake ni Esta, na Ruthu. Vimeitwa hivyo sio kwasababu tu Mungu anataka kupitisha ujumbe wake wa wokovu kwa kanisa, lakini pia upo ujumbe mahususi unaowahusu wanawake.

Leo tutamtazama Ruthu kwa maneno machache sana. Wanawake wengi wanapitia mikwaruzo katika ndoa zao, na kikubwa ni saikolojia wanayojijengea kabla na baada ya kuolewa kwao, kuhusu wakwe zao, hususani mama-mkwe..Na hapo ndipo panapokuwa chanzo cha matatizo yote…Wanawake wengi wanaoniuliza juu ya matatizo ya ndoa zao, nimegundua kuwa asilimia kubwa hawana mahusiano mazuri na wakwe zao.

Nataka nikuambie ulipokuwa hujaolewa Baraka zako zilikuwa kwa wazazi wako waliokuzaa, lakini unapoolewa ujue kuwa Baraka za ndoa na za uzao wako zinahamia kwa wakwe zako haijalishi ni wabaya kiasi gani..

Kama tunavyofahamu habari ya Ruthu, na Orpa, wote hawa wawili waliolewa na watoto wa Naomi mkwe wao, lakini kwa bahati mbaya, Naomi akafiwa na mume wake na watoto wake wote wawili akabakia kuwa mjane, hivyo akawa hana mume wala mtoto wala mjukuu,..Lakini Naomi kwa ukarimu wake akawatangazia uhuru wakwe zake, warudi makwao kila mmoja akaolewe tena kwasababu bado walikuwa ni vijana na pia bado hawajazaa..Orpa akakubali kuondoa kurudi kwao, lakini Ruthu hakukubali kwasababu alijua Baraka zake zipo wapi…

Hivyo akaamua kurudi na mkwe wake nchi ya Israeli, akajitoa tu kama wakfu kuwa kama mjakazi wake, walipofika wakaishi pamoja,Na Ruthu akawa anamtumika mkwe wake kama mtoto wake kwa amani tu..Ruthu aliipoteza nafsi yake, ili tu amrudhishe mama mkwe wake, lakini alijua ndani yake haitakuwa bure kuwa vile.

Lakini kama tunavyojua, ni nini kilifuata baadaye..Licha tu ya Ruthu kuolewa na Yule tajiri Boazi ndugu yake Naomi, lakini watu wote walimwona kuwa anastahili kuliko watoto 7 wa Naomi..

Ruthu 4: 13 “Basi Boazi akamtwaa Ruthu, naye akawa mke wake; naye akaingia kwake, na Bwana akamjalia kuchukua mimba, naye akazaa mtoto wa kiume.

14 Nao wale wanawake wakamwambia Naomi, Na ahimidiwe Bwana, asiyekuacha leo hali huna wa jamaa aliye karibu; jina lake huyu na liwe kuu katika Israeli.

15 Naye atakurejezea uhai wako, na kukuangalia katika uzee wako; kwa maana mkweo, ambaye akupenda, NAYE ANAKUFAA KULIKO WATOTO SABA, ndiye aliyemzaa.

16 Basi Naomi akamtwaa yule mtoto, akamweka kifuani pake, akawa mlezi wake”.

Embu jiulize wewe mwanamke uliyeolewa, Je, mkwe wako alishawahi kukuona unastahili kuliko watoto wake wote alionao?.. Alishawahi kujivunia kwako kwa namna hiyo? Kama hakuna chochote alichowahi kujivunia kwako, lipo tatizo.

Na kama hiyo haitoshi, Ruthu ambaye alikuwa ni mwanamke wa kimataifa, akahesabiwa katika uzao wa Kiyahudi kama vile Rahabu alivyohesabiwa kwa tendo lake tu hilo , na huko huko baadaye ndipo alipokuja kutokea Mfalme Daudi.. Uzao wa kifalme na uzao wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Jaribu kufikiria tena jinsi uzao wake ulivyobarikiwa zaidi hata ya wanawake wengi wa kiebrania waliozaliwa na Ibrahimu…Na hiyo yote siri ilikuwa kwa MAMA MKWE WAKE na si penginepo. Ni yeye tu na Esta ndio waliopata nafasi ya vitabu vyao kuandikwa majina yao.

Hata wewe mwanamke uliyeolewa au unayekwenda kuolewa.. Timiza jukumu lako la kuwapenda wakwe zako kwasababu huko ndipo uzao wako utakapobarikiwa na ndipo ndoa yako itakapokuwa na amani..

Wewe kama siku zote huna habari na wakwe zako, unawasengenya, huwahudumii, huwaheshimu, unagombana nao, unawapenda kinafki tu, unafanya ili kutimiza wajibu tu, lakini hujitoi kwao, unaifikiria familia yako tu na ndugu zako…usitazamie kuwa Utabarikiwa uzao wako.

Biblia inakupa fundisho, litii ulifuate , watu wengi wenye matatizo ya ndoa huwa chimbuko ni hapo, pasipo hata wao kujua. Ikiwa humpendi mama wa mume wako, na usimpende na mume wako pia, lakini kama unampenda mume wako basi mpende na mama yake na ndugu zake ndipo utakapoishi kwa rah ana amani katika familia yako. Unaweza ukasema mimi ninaishi kwa raha, hao wakwe wananihusu nini..ni kweli utaishi leo kwa raha, lakini uzao wako unaweza usiishi kwa raha huko mbeleni..Na vile vile Maisha yako pia yanaweza yasiwe ya baraka.

Hiyo ni sheria ya Mungu ambayo ipo katika maandiko, ikiwa utataka kuwazaa akina YESE na Mfalme Daudi basi ambata na wakwe zako bega kwa bega, na kanuni hiyo itakulipa..Epuka mafundisho na injili za kwenda kupiga maadui zako, na kuwalenga wakwe zako..hapo utakuwa unazipiga baraka zako mwenyewe, utakuwa unajimaliza mwenyewe, ukidhani unajihami kumbe unajimaliza…Ukiona kuna kasoro Fulani ipeleke kwenye sala ukimwomba Mungu azidi kukupatanisha na wakwe zako sana, maana milango ya baraka zako ndio ipo huko.. siku zote zingatia hilo

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Rudi Nyumbani:

Print this post