Kwanini wajane vijana hawakupaswa kuandikwa?

Kwanini wajane vijana hawakupaswa kuandikwa?

SWALI: Kwanini Mtume Paulo, alimkataza Timotheo asiwaandike wajane vijana? Je wajane vijana hawapaswi kusaidiwa au?


Jibu: Kabla ya kwenda kwenye jibu la swali letu, kuna mambo muhimu ya kufahamu kwanza ya utangulizi.

Katika kanisa la kwanza kulikuwa na utaratibu wa kuwasaidia wazee, hususani wale wenye umri mkubwa sana. Ambao hawawezi kufanya kazi wala hawana mtu wa kuwasaidia, kama Watoto au wajukuu.

Sasa haikuwa kila mzee tu, anayejiunga na kanisa alikuwa anasaidiwa la! Haikuwa hivyo, Kulikuwa na vigezo au sifa za wazee waliokuwa wanastahili kusaidiwa. Na sifa hizo tunazisoma katika kitabu cha Timotheo..

1Timotheo 5:9  “Mjane asiandikwe isipokuwa umri wake amepata miaka sitini; naye amekuwa mke wa mume mmoja;

10  naye ameshuhudiwa kwa matendo mema; ikiwa amelea watoto, ikiwa amekaribisha wageni, ikiwa amewaosha watakatifu miguu, ikiwa amewasaidia wateswao, ikiwa amefuata kwa bidii kila tendo jema”.

  1. Sifa ya kwanza ni lazima awe mjane:

       Maana yake ni kwamba kama sio mjane, anaye mume..basi huyo tayari anaweza kuhudumiwa na Mume wake, kwa mahitaji yake, hivyo asiandikwe kwenye orodha ya wanaostahili kusaidiwa na kanisa ili kanisa lisije likalemewa.

  1. Sifa ya pili, hata akiwa Mjane, ni lazima umri wake uwe ni miaka 60 na Zaidi:

 Maana yake ni kwamba akiwa chini ya umri huo, bado anayo nguvu za kufanya kazi za kujipatia kipato, hivyo anaweza kuendelea kufanya kazi zake za mikono huku akiendelea na kazi ya kuhudumu katika kanisa..Ili kanisa lisije likalemewa.

  1. Ni ya tatu ni lazima awe Mke wa Mume mmoja:

Maana yake ni kwamba kabla ya mume wake kufa, awe na rekodi ya kuwa na huyo huyo mume  mmoja, na sio awe na rekodi ya kuwa na wanaume wengi. Mwanamke yeyote mwenye hiyo rekodi ya kuwa na wanaume wengi, hana sifa ya kuandikwa kwenye orodha ya wanaohitaji kusaidiwa.

  1. Na sifa ya nne na ya mwisho, ni lazima awe na rekodi ya matendo mema.

Maana yake ni kwamba sio tu mtu, kazeeka hivyo anaona sehemu ya kwenda kumalizia pensheni ya uzeeni ni kanisani, hivyo anakwenda kujiunga ili tu awe ana hudumiwa. Biblia imesema watu wa namna hiyo wasiandikwe..Watu wanaopaswa kuandikwa ni lazima wawe na rekodi ya kuifanya kazi ya Mungu katika kanisa Pamoja na matendo mema, na utakatifu.

  • Kama ni mwanamke ni lazima awe na rekodi ya kuwaosha watakatifu miguu, kwa miaka kadhaa ndani ya kanisa
  • Ni lazima awe na rekodi ya matendo mema, maana yake ni kwamba tangu aamini, mpaka anafikia uzee hana picha yoyote mbaya aliyoiacha..kwamfano hajarekodiwa kuwa mzinzi, hajawahi kukutwa akiwa mtukanaji, au mlevi, au mshirikina n.k
  • Amerekodiwa kuwa mkaribishaji, maana yake mwenye upendo kwa watu wote, na si mchoyo.

Sasa hapo biblia imeruhusu watu wenye sifa hizo kusaidiwa, lakini haikusema kila mwanamke anayefikia umri wa miaka 60 au Zaidi na ni mjane, ni lazima aandikwe kwenye orodha ya watakaosaidiwa. Hapana!!.. Kama mjane ana miaka Zaidi ya 60, na una uwezo mzuri wa kiuchumi, hapaswi kuandikwa, vile vile kama anao Watoto, au ndugu ambao wanaweza kumtunza vizuri, ni mume tu ndio hana, vile vile hapaswi kuandikwa. Wanaondikwa ni wale wajane kweli kweli ambao hawana mtu yeyote waliyebakiwa naye wa kuwasaidia, wamebaki wenyewe. Na tumaini lao lote lipo kwa Bwana, hao ndio wanaopaswa kuwekwa kwenye orodha ili kanisa lisilemewe.

1Timotheo 5:3  “Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli.

4  Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu.

5  Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku”

1Timotheo 5: 16  “Mwanamke aaminiye, akiwa ana wajane, na awasaidie mwenyewe, Kanisa lisilemewe; ili liwasaidie wale walio wajane kweli kweli”.

Sasa tukirudi kwenye swali, ni kwanini wajane vijana hawapaswi kuandikwa?.

Sababu ya kwanza tumeshaiona hapo juu, ni ili kanisa lisilemewe, kwasababu wanao nguvu na uwezo wa kufanya kazi, hivyo fungu hilo la posho, ni heri likawasaidie wale ambao hawana uwezo kabisa wa kufanya kazi, wenye umri mkubwa, ambao hawana tumaini kabisa.

Sababu ya pili ndiyo hiyo tunayoisoma katika 1Timotheo 5:11-15.

Tusome..

1Timotheo 5:11  “Bali wajane walio vijana ukatae kuwaandika hao, maana, wakizidiwa na tamaa kinyume cha Kristo, wataka kuolewa;

12  nao wana hukumu kwa kuwa wameiacha imani yao ya kwanza.

13  Tena, pamoja na hayo, hujifunza kuwa wavivu, wakizunguka-zunguka nyumba kwa nyumba; wala si wavivu tu, lakini ni wachongezi na wadadisi, wakinena maneno yasiyowapasa.

14  Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu.

15  Kwa maana wengine wamekwisha kugeuka na kumfuata Shetani”

Ni ukweli usiopingika kuwa asilimia kubwa ya wanawake ni “watu wa kupenda udadi, au umbea, kutafuta tafuta kujua mambo ya watu wengine”.. Na wengi wa hao ni wale ambao hawana shughuli maalumu za kufanya, na wenye umri kati ya miaka 20-45 na wengine hadi 50. Mwanamke wa rika hili, akishakosa shughuli ya kufanya, na Zaidi akiwa hajaolewa, ni rahisi sana kuchukuliwa na hiyo roho ya udadisi dadisi. Na wivu wivu, tofauti na mwanamke ambaye ameolewa au mwenye shughuli maalumu ya kufanya. Kwasababu mwanamke aliyeolewa atakuwa akili yake yote ipo katika kuiendesha familia yake na kuitunza na kuangalia Watoto wake.

Sasa katika kanisa pia wapo wanawake, ambao ni wa rika hilo, Ambao baada ya waume zao kufa wamekuwa wajane, hivyo na wenyewe wanajiweka kwenye kundi hilo la wanawake wajane ambao kazi yao ni kudumu katika sala na maombi na kuhudumu kanisani siku zote (tumaini lao lote lipo kwa Bwana 1Timotheo. 5:5)… Hivyo na wao wanajiweka katika kundi la watu wanaohitaji kusaidiwa na kanisa.

Lakini tatizo lilionekana kwamba wengi wa wanawake hawa ambao ni vijana, wanakuja kugeuka tabia siku za mbeleni na kuanza kujiingiza kwenye mahusiano yasiyo rasmi, na tabia hizo za udadisi. Na hivyo hivyo wanakuwa wameiacha Imani ambayo walikuwa nayo hapo kwanza. Na hivyo kujiingia kwenye hukumu, kwasababu wameiacha Imani.

Kuacha Imani ya kwanza, maana yake kuacha njia ya haki waliyokuwa wanaiendea hapo kwanza.

Kwahiyo wanawake hawa, biblia imesema wasiandikwe, badala yake ni vizuri wakaolewa tena, ili wazae Watoto, wawe na majukumu, kwasababu watakapokuwa na majukumu na watakapokuwa na Watoto, watakuwa busy na familia zao, hivyo si rahisi kushawishika kuwaka tamaa na kuwa wadadisi, tofauti na wakitanga tanga bila kuwa na majukumu, ni rahisi kuchukuliwa na tamaa za kila namna.

Lakini pia kumbuka si wanawake wote ambao ni wajane na ni vijana, wana tabia hizo…Hapana!..Hapo biblia imemaanisha ni wengi wao, lakini si wote. Wapo ambao ni  wajane vijana, au hawajaolewa lakini wanaishikilia Imani, Ingawa wapo wachache sana. Katika biblia alikuwepo mwanamke aliyeitwa Ana, ambaye aliishikilia Imani bila kuiacha tangu mume wake alipokufa angali akiwa bado binti mdogo, na mpaka akiwa na miaka 80, hakuiacha Imani. Na Mungu akampa neema ya kumjua mtoto Yesu kuwa ndiye Masihi katika uchanga ule. Wakati wengine hata Yesu alipokuwa mtu mzima bado hawakumwamini.

Luka 2:36  “Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake.

37  Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba.

38  Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake”.

Bwana atubariki

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Wanaowachukua wanawake wajinga mateka ni akina nani?

Je! Mungu anaupendeleo kwa wanaume zaidi ya wanawake?

TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI:

Kwanini wanawake wengi huwa wanalipuka mapepo?

CHUKI ULIZO NAZO KWA MAADUI ZAKO, SIZO ALIZONAZO MUNGU JUU YAO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments