Shalom mpendwa, Karibu katika kuyatafakari maneno ya uzima..
Tunaijua Habari ya Gideoni na wanajeshi wake 300, lakini ni vizuri tukajikumbusha tena, naamini lipo jambo jipya tutajifunza leo ndani yake..Tusome..
Waamuzi 7:4 “Bwana akamwambia Gideoni; Hata sasa watu hawa ni wengi mno; uwalete chini majini, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako; kisha itakuwa ya kwamba yule nitakayekuambia, Huyu atakwenda pamoja nawe, ndiye atakayekwenda pamoja nawe; na mtu yule nitakayekuambia, Huyu hatakwenda pamoja nawe, basi mtu huyo hatakwenda.
5 Basi akawaleta watu chini majini. Bwana akamwambia Gideoni, Kila mtu atakayeyaramba maji kwa ulimi wake, kama vile arambavyo mbwa, huyo utamweka kando; kadhalika kila mtu apigaye magoti kunywa.
6 Na hesabu ya hao waliokunywa kwa kuramba-ramba, wakipeleka mkono kinywani, ilikuwa watu mia tatu; bali watu wengine wote walipiga magoti kunywa maji.
7 Bwana akamwambia Gideoni, Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba maji nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako; lakini watu hawa wote wengine na waende zao, kila mtu mahali pake”.
Amen.
Ukitazama hapo, utaona lile kundi la kwanza walipofika tu majini jambo la kwanza walipiga magoti, jambo ambalo wale wengine hawakulifanya…
Pili walikutanisha midomo yao na yale maji ya mto moja kwa moja.Kwasababu walikuwa na kiu sana, hivyo njia pekee walioina kuwa itaondoa kiu yao kwa haraka ni kwa kupelekea midomo moja kwa moja majini, ili wanywe kwa haraka haraka bila bugdha yoyote.
Tofauti na wale wenzao, ambao walikuwa kwanza wanayakusanya maji kwenye mikono yao, kisha wanayalamba kidogo kidogo, kisha tena wanachota na kulamba hivyo hivyo, kidogo kidogo hadi walipokata kiu yao..
Walikuwa wanahakikisha kwanza kile wanachokinywa kabla ya kukinywa, bila kujali kuwa yatakuwa yanakaa kidogo tu kwenye mikono yao, na kuvuja vuja..Bila kujali kujitesa kuchota chota kila mara.
Pia walikataa kupiga magoti kuelekea maji, bali waliinama tu, au walichuchumaa, na hiyo ikawapa wigo mzuri wa kuona hatari iliyo mbele yao, kiasi kwamba hata adui angetokea mbele yao wangeweza kuacha wanachokifanya na kupigana nao, tofauti na wale wengine..
Vivyo hivyo, hata sisi, ni kweli tupo ulimwenguni, na wakati mwingine itatupasa tuchume vya ulimwenguni kidogo, lakini tukijisahau kuwa tupo mapambanoni na adui yetu shetani yupo mbele yetu, tukayapigia magoti mambo ya ulimwengu huu.. yaani kufanya mambo ya ulimwengu huu kuwa ndio kila kitu kwetu.Tujue kuwa hatufai kwa ufalme wa mbinguni.
Sio kila kinachokuja mbele yetu, ni cha kukipaparikia kwa moyo wote, sio kila fursa ni kutoka kwa Mungu vingine ni mitego ya adui,..Unapaswa uchague kazi, unapaswa uchague marafiki, unapaswa uchague mazingira ya kuishi..Sio kila kazi ilimradi tu inakupa pesa ni ya kuifanya..Unapaswa uipitishe kwanza kwenye mikono yako ya rohoni, uangalie je! Hii kazi ni salama, haitaniletea athari yoyote katika wokovu wangu huko mbeleni? Je hii kazi ni kulingana na Neno?..
Sasa ukishaiona haiikinzani na Neno la Mungu na haina madhara kiimani, ndipo unairamba tena kidogo kidogo, na sio kuikurupukia.. Kila tenda inayokuja inaipitisha kwenye maandiko kwanza, je ina sumu ya adui?..kama askari hawa walivyoipitisha maji mikononi kwanza kabla ya kuyanywa…Unaitazama je! Ina rushwa ndani yake?, je ina utapeli ndani yake n.k
Lakini kama hutajiuliza chochote wewe, kila fursa inayokuja mbele yetu, tunaipaparikia hutufai kuwa askari wa Mungu..haijalishi ni nzuri vipi, kwasababu huwezi jua baadaye itakufanya hata ule wakati wako uliokuwa unautumia kuomba unamezwa na shughuli hizo, au jumapili yako ulikuwa unakwenda ibadani sasa, inaingiliwa na kazi hizo, au mavazi yako uliyokuwa unavaa ya staha yanageuzwa na kuwa ya kikahaba.
Vile vile na marafiki pia, sio kila mtu unayekutana naye ni lazima awe Rafiki yako tu, unapaswa umpitishe kwanza kwenye mikono yako ya rohoni, kisha ukimwona anaendana na Imani yako, ndipo uanze kuunga naye urafiki, tena kidogo kidogo, mpaka utakapomthitisha kamili baada ya muda mrefu..Wengi leo wanawachunguza marafiki kama ni washirikina tu!..hicho ndicho wanachoweza kuchuguza..lakini hawawez kuchunguza huyu rafiki kama ni mlevi, au kama ni mtu wa rushwa, au mtu wa kutomjali Mungu..wengi hayo macho hawana, wana macho tu ya kuchunguza ushirikina.
Vilevile na mazingira, sio kila mazingira yanayokujia mbele yako ni ya kuishi au kukubaliana nayo..chunguza kwanza..Chunguza chochote kile kabla hujakifanya ukikilinganisha na wokovu wako, Je, ni salama?..kwasababu wokovu ni kitu cha kulinda na kukipigania kuliko kitu kingine chochote. Biblia inasema Imani tumekabidhiwa mara moja tu!
Kwasababu mitego ya adui ipo kila kona. Mungu aliona mbele ndio maana hakuwaruhusu wale wengine waende vitani, kwasababu alijua huko mbeleni, askari wataishiwa nguvu sana, watakuwa na kiu na njaa, lakini bado mapambano hayajaisha, Je watakuwa tayari kutotazama mambo ya mwilini wakaendelea na mapambano? (Soma Waamuzi 8:4). Ndio maana akawatenga wale 300 tu..waliovumilia kunywa maji kwa uangalifu na taratibu taratibu.
Na sisi pia tukitaka tuwe askari kamili wa Kristo, Bwana atusaidie tuyazingatie hayo….
Mungu akubariki sana.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
NINI NI KILICHOMFANYA IBRAHIMU AKUBALI KUMTOA MWANAWE SADAKA?
Mungu anapompa mtu kazi ya kufanya, na mtu yule akawa na hofu na maadui wa Imani yake au akawa anakawia kawia basi nafasi yake anapewa mtu mwingine…Moja ya sababu kati ya nyingi inayompelekea mtu kupoteza nafasi yake ya utumishi ni HOFU.
Hofu ya kuwaogopa maadui wa Imani yako, hofu ya kuogopa endapo ukihubiri kinyume na mifumo ya adui shetani itakuwaje?..endapo ukiziharibu na kuzidhihirisha kazi za shetani itakuwaje?..Endapo nikizitukana kazi za adui, kama Daudi alivyozitukana itakuwaje?..Nikizidhalilisha kazi za kichawi itakuwaje?..hofu ya kwenda kuhubiri vijijini kuhofia wachawi wa kule, hofu ya kutamke jina la Yesu palipo na nguvu za giza n.k…Hofu ya namna hii ina madhara makubwa sana kiroho..
Katika biblia tunajifunza mtu mmoja aliyeitwa Eliya, ambaye alipewa jukumu la kuisafisha Israeli na kumwondoa mungu baali katikati ya Taifa la Mungu, lakini mwisho wa siku akaingiwa na hofu..na kulikimbia kusudi..
Kama ni mwanafunzi wa biblia, utakuwa unaielewa vyema Habari ya Nabii Eliya jinsi alivyowaua wale makuhani 450 wa Baali na 400 wa Ashera jumla yao 850 (1Wafalme 18:16-40)..Idadi hii ilikuwa ni kubwa sana Eliya aliyoiua ambayo ikasababisha upungufu mkubwa wa makuhani wa Baali katika nchi ya Israeli, hivyo kupelekea kiwango kikubwa cha Uovu kupunguzwa Israeli…Kwani makuhani hao waliajiriwa na mwanamke Yezebeli kutoka huko Lebanoni kuja kuingiza miungu migeni katika Taifa Takatifu la Mungu..
Kwani makuhani hao wa Baali walikuwa wanafanya uchawi na kuipotosha Israeli nzima…Hata wakati wanashindana na Nabii Eliya kushusha moto juu ya ile sadaka, sio kwamba hawakuwa na huo uwezo..huo uwezo wa kutengeneza moto wa kimiujiza ulikuwa ni uchawi mdogo sana kwao, ndio maana walikuwa na ujasiri wa kukubali changamoto ile na Eliya….lakini kwasababu hakuna uchawi wowote ambao unaweza kuwa na nguvu mbele ya Nguvu za Mungu aliye hai, ndio maana ghafla walijikuta wameshindwa kutengeneza moto wao wa kichawi juu ya ile sadaka siku ile…
jambo ambalo hapo kabla halikuwa jambo gumu kwao kulifanya.
Hivyo walikuwa ni wachawi ambao waliajiriwa na mwanamke Yezebeli ambaye ndiye aliyekuwa malkia wa Israeli wakati huo..(2Wafalme 9:22)… Lakini Eliya pamoja na kuipunguza idadi hiyo yote ya wachawi juu ya Israeli, bado hawakuisha wote…wapo wengine ambao walikuwa wapo mbali…na wengine walibaki Samaria …na Zaidi ya yote hata Yezebeli mwenyewe ambaye alikuwa amewaajiri, alikuwa bado yupo hai…
Hivyo Eliya japokuwa alipunguza machukizo juu ya Israeli kwa sehemu kubwa..lakini bado alikuwa hajautoa ule mzizi wote. Na Mungu alimkusudia yeye ndiye autoe mzizi wote na aisafishe Israeli yote lakini kwasababu ya vitisho vya Yezebeli kuutoa uhai wake alimwogopa na kumkimbia kunusuru uhai wake.…Eliya akakimbia mpaka Herobu kwa hofu ya Yezebeli na kumwomba Mungu autoe uhai wake….Hivyo kwa hofu alimwomba Mungu aikatishe hudama yake…Na Mungu aliitoa Huduma hiyo na kuwapa watu wengine watatu waimalizie ambao ni HAZAELI, ELISHA na YEHU.
1Wafalme 19:15 “Bwana akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu.
16 Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa AbelMehola mtie mafuta awe nabii mahali pako.
17 Na itakuwa atakayeokoka na upanga wa Hazaeli, Yehu atamwua; na atakayeokoka na upanga wa Yehu, Elisha atamwua”.
Sasa Neno la Mungu ni lazima litimie kwa mkono wa Hazaeli na Elisha na Yehu..kwamba uovu wa baali na makuhani wake na waanzilishi wake waondolewe Israeli kwa mikono ya hawa watatu…Sasa Habari za mambo aliyoyafanya Elisha na Hazaeli zipo katika maandiko…Lakini leo nataka tumtazame huyu mtu wa mwisho anayeitwa YEHU, jinsi gani alilimaliza kusudi la Mungu vizuri.
Yehu, alitiwa Mafuta na Eliya mwenyewe awe mfalme juu ya Israeli…ingawa hakuwa mkamilifu sana, lakini Mungu alimpa ujasiri mkuu kuliko wa Eliya…pale ambapo Eliya alimwogopa Yezebeli na kumkimbia huyu Yehu alimfuata Yezebeli kwenye jumba lake la kifalme na kumtoa kwenye umalkia ili auawe…na sio hilo tu!…bali aliwaua manabii wote wa Baali ambao walikuwa wamesalia kwa siku moja Zaidi hata ya ile idadi ya Eliya aliyoiua kule Karmeli. Na akamtoa mungu anayeitwa baali katika Taifa la Israeli, na baada ya hapo, wana wa Israeli hawakuabudu tena baali..
2Wafalme 10:18 “Yehu akawakusanya watu wote, akawaambia, Ahabu alimtumikia Baali kidogo; bali Yehu atamtumikia sana.
19 Basi niitieni manabii wote wa Baali, wote wamwabuduo, na makuhani wake wote; mtu asikose kuwapo hata mmoja. Maana ninayo dhabihu kubwa ya kumtolea Baali; ye yote atakayekosa kuwapo hataishi. Lakini Yehu alifanya hayo kwa hila, ili awaharibu waliomwabudu Baali.
20 Yehu akasema, Takaseni kusanyiko la dini kwa Baali. Wakalitangaza.
21 Yehu akatuma wajumbe katika Israeli yote, nao wote waliomwabudu Baali wakaja, wala hakusalia mtu ye yote asiyekuja. Wakaingia nyumbani mwa Baali; ikajaa nyumba ya Baali tangu mlango hata mlango.
22 Akamwambia yule aliyekuwa juu ya hazina ya mavazi, Uwatolee mavazi wote wanaomwabudu Baali. Akawatolea mavazi.
23 Akaingia Yehu na Yehonadabu mwana wa Rekabu nyumbani mwa Baali, akawaambia waliomwabudu Baali, Tafuteni mkaangalie, asiwepo hapa pamoja nanyi mtu amtumikiaye Bwana, ila wamwabuduo Baali peke yao.
24 Wakaingia ili watoe dhabihu na sadaka za kuteketezwa. Basi Yehu alikuwa amejiwekea nje watu themanini, akasema, Mtu mmoja akiokoka wa watu niliowatia mikononi mwenu, amwachaye huyo, roho yake itakuwa badala ya roho yake.
25 Ikawa mara alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa, Yehu akawaambia walinzi na maakida, Ingieni mwapige; mtu awaye yote asitoke. Basi wakawapiga kwa makali ya upanga; walinzi na maakida wakawatupa nje, wakaenda mpaka mji wa nyumba ya Baali.
26 Wakazitoa nguzo zilizokuwamo nyumbani mwa Baali, wakaziteketeza.
27 Wakaibomoa nguzo ya Baali, na kuiangusha nyumba ya Baali, wakaifanya choo hata leo.
28 NDIVYO YEHU ALIVYOMHARIBU BAALI KATIKA ISRAELI”
Sasa katika Habari hiyo tunajifunza ni kwamba..kama sio Nabii Eliya kumwogopa Yezebeli, Mungu angelimaliza kusudi lote mkononi mwake,…kwasababu huyo Yezebeli ambaye alikuwa anamwogopa Yehu alikuja kumuua kirahisi sana, wala hata hakutumia upanga wala silaha kumuua…aliwaambia tu watu wamkamate wamtupe dirishani..hivyo tu!..(2wafalme 9:30-35).
Na sisi hatupaswi kumwogopa Adui shetani na vitisho vyake, katika kulitimiza kusudi la Mungu..Maadui wa Imani yetu ni wengi, na wana vitisho vikali…lakini hatupaswi kusikiliza vitisho vyao…
Haihitaji mapanga na marungu kumwangusha Yezebeli…ni amri tu! Kama Yehu alivyofanya…Na sisi haihitaji majeshi wala michanganyiko mingi kumwondoa Adui shetani mbele yetu..bali inahitajika amri tu!..Unatamka na Yezebeli anakwenda chini..
Hivyo usiogope mganga mtaani kwako, usiogope wachawi vijijini kwako, usiogope mwanasiasa mbele yako, usiogope chochote kijiitacho kikuu mbele yako ambacho kinakutishia Imani yako au huduma yako..wewe litazame kusudi la Mungu tu kulitimiza na kulimaliza.
Zekaria 4:6 “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi”..
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
NENO LA MUNGU NI DAWA ILIYO TOFAUTI NA DAWA NYINGINE.
NENO LA MUNGU NI TAA
NITAFUNGUAJE MILANGO ILIYOFUNGWA MBELE YANGU?
MAPAMBANO DHIDI YA SHETANI.
NAO WAKADHANI YA KUWA YUMO KATIKA MSAFARA;
UCHAWI WA BALAAMU.
KIFO CHA MTAKATIFU PERPETUA NA FELISTA.
Waefeso 5:15 “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima;
16 mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu.
17 Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.
18 Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; BALI MJAZWE ROHO”;
Mwishoni mwa mstari huo wa 18 biblia inatuambia ‘”bali mjazwe Roho”.. Hili Ni neno endelevu, Sasa kumbuka Mtume Paulo alipokuwa anazungumza na kanisa hili la Efeso Alijua kabisa walishapokea Roho Mtakatifu tangu zamani walipoamini, na ndio maana likawa kanisa kubwa lilolitwa Efeso, Lakini hiyo haikumfanya mtume Paulo aone wamefika, bali aliwaasa siku baada ya siku wajazwe Roho, kwasababu alijua kuwa Roho anaweza kuzimishwa ndani ya mtu, hali kadhalika pia anaweza kujaa na kupungua kwa jinsi mtu atakavyokuwa makini au mzembe katika wokovu wake.
Hata sisi wakristo wa zama hizi ambazo uovu wetu ni mkubwa kuliko ule wa kanisa la Efeso, kusema tu, tumeokoka, au tumepokea Roho Mtakatifu, na huku bado uhusiano wetu na Mungu haueleweki haitoshi kutufikisha mbinguni, bali tunapaswa tujazwe Roho Mtakatifu siku baada ya siku mpaka siku ile ya Unyakuo itakapotukuta..
Kwasababu tukipuuzia jambo hilo, tutafananishwa na wale wanawali wapumbavu tunaowasoma katika Mathayo 25 ambao walikuwa wanamngojea Bwana wao lakini hawakuwa na mafuta ya kutosha ya kuwafikisha hadi ule wakati wa kumlaki Bwana wao.. matokeo yake saa ile ilipofika ya Bwana wao kutokea, ndio wakajishtukia kuwa taa zao zinakwenda kuzima…Sasa wakati wanakwenda kununua huku nyuma tayari Bwana arusi ameshawasili na kuwachukua wale aliowakuta wapo tayari na kuingia nao karamuni..Na wale wengine waliokwenda kuchukua mafuta waliporudi wakajikuta wameshachelewa.. Hasara ikawa ni kwao na taabu yao yote ya kumngojea Bwana ikiwa ni bure.. Japokuwa nao pia walikuwa ni wanawali (mabikira) yaani wameokoka, ambao wanamngojea tu Bwana wao kwa saburi kama wale wengine.. Lakini kwasababu ya kupuuzia jambo la msingi la mafuta katika chupa zao ikawafanya wakose karamu..
Siku zote mafuta yanafananishwa na Roho Mtakatifu..Tunapompokea Roho Mtakatifu siku zile za kwanza tulipookoka, tulipokea mafuta ya kuwasha tu vyombo vyetu vya usafari..Lakini tukiridhika na yale tu, hatutafika mbali. Ndugu ili kukivuka hichi kipindi cha Uovu uliokirithiri duniani sasa..Tunapaswa tuendelee kujazwa Roho..
Pengine utauliza nifanye nini ili nijazwe Roho Mtakatifu?
Roho Mtakatifu anaweza kuendelea kujaa ndani yetu, kwa walau mambo makuu manne.
Biblia inasema, Luka 13:13 “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”
Ukiwa mtu wa kuomba, na kukataa uvivu kwa kutokusali walau saa moja kwa siku, ndivyo utavyojiongezea mafuta yako ya rohoni na hivyo Roho Mtakatifu atapata wigo mpana wa kuyatawala maisha yako siku baada ya siku.
2. Kwa kujifunza kwa bidii Neno la Mungu..; Neno ndio chakula cha uzima wa mtu. Usipojibidiisha kujifunza Neno la Mungu, kutafuta habari za uzima, usidhani kuwa Roho Mtakatifu atapata nafasi ya kukufundisha kitu chochote ndani yako. Kwasababu Mungu yupo katika Neno lake(Sauti ya Mungu ni Neno lake). Ukiwa umeokoka, halafu unaona uvivu kujifunza Biblia basi ujue Roho wa Mungu ameshazimika ndani yako kitambo..Na hivyo hata wakati wa unyakuo utakapofika utafananishwa na wale wanawali wapumbavu.
3. Kaa mbali na uovu; Siku zote dhambi inavutia, lakini mwisho wake ni mbaya..Tunapoivumilia dhambi katika maisha yetu ndivyo Mungu anavyouficha uso wake. Na matokeo yake Roho Mtakatifu anazimika, au anaondoka kabisa ndani yetu.(Isaya 59:2)
4. Tangaza habari njema: Ukiwafundisha wengine, na wewe hapo hapo Roho wa Mungu anakufundisha, ukiwafungulia wengine hazina ya maneno ya uzima, Roho Mtakatifu anapata nafasi ya kukufunulia wewe Zaidi na kukutumia, ili kuwaokoa watu wake..Na hivyo ni sharti atakaujaza tu Roho wake, kwasababu siku zote unafanya kazi yake..Na hapo utakuwa na nafasi nyingine ya kuwa karibu na yeye.
Hivyo tusiridhike tu, na hali za kiroho tulizopo, tukajificha nyuma ya kivuli cha Neno nimeokoka..Tunapaswa tujiulize Je! Mafuta tuliyonayo yanatutosha mpaka wakati wa kuja kwa Bwana? Kama sivyo basi huu ndio wakati wa kuzitengeneza upya taa zetu..kwa kuhakikisha kuwa kila siku Roho Mtakatifu anapata nafasi maishani mwetu..Ili ile siku ambayo hatujui ni lini itakapotujilia kwa ghafla basi tuwe na uhakika kuwa UNYAKUO hautatupita.
Ubarikiwe.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOWAFUNULIA WATU MAANDIKO.
Je! hizi roho saba za Mungu ni zipi? na je zinatofautiana na Roho Mtakatifu?
RABI, UNAKAA WAPI?
NA MTU MMOJA AKAVUTA UPINDE KWA KUBAHATISHA, AKAMPIGA MFALME
KUTUBU SIO KUOMBA REHEMA.
MATUNDA 9 YA ROHO MTAKATIFU