Category Archive Home

MUNGU WANGU,MBONA UMENIACHA?.

Bwana wetu Yesu Kristo japo alikuwa ni Mungu mwenyewe katika mwili lakini hakuwa mnafiki kutokuonyesha hisia zote wanadamu wanazopitia wakiwa hapa duniani, Kama wengine walivyotazamia kuwa Mungu akiuvaa mwili, basi yeye atakuwa ni kama malaika duniani, Na ndio maana Waebrania 2:16-18 inasema:

16 Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu.

17 Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake.

18 Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.

Unaona? Bwana alilia palipopaswa kulia, sehemu nyingine aliomba Mungu amwepushe, na kikombe cha mateso ikiwa ni sawa sawa na mapenzi ya Baba yake, kwa namna ya kawaida tunaweza kusema hofu ya kibinadamu ya kuuawa ilimwingia.

Vile vile Japo siku zote alifahamu Baba yake yupo pamoja naye, hawezi kumwacha, na alishamweleza kitu kuhusu maisha yake, na mwisho wake utakavyokuwa, na yatakayotokea baada ya hapo, lakini kuna saa huzuni ilikuwa inamwingia….Halikadhalika Bwana akiwa pale msalabani alijua kabisa siku zisizodi tatu atakuwa utukufuni, akijua kabisa safari yake imeshakwisha kikamilifu, amebakisha dakika chache tu aondoke duniani lakini katika hatua ile ile ya mwisho, tunaona anamwambia baba yake maneno haya:

Mathayo 27:46 “Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

Fahamu kuwa alikuwa hazungumzi maneno haya ili kujifanya, ni kweli kabisa ndani ya moyo wake, hakuwa anaona uwepo wowote wa ki-Mungu, ndani yake hakukuwa na chochote, alikuwa hana tofauti na wale wezi aliosulibiwa nao, ni kama vile kaachwa Solemba, alikuwa kama mtu ambaye Mungu hajawahi kuzungumza naye kabisa, ndivyo alivyojiona ndani yake..

Tukitafsiri kwa lugha ya leo tunaweza kusema, Ee! Mungu mbona katika siku za raha ulikuwa pamoja nami, ulikuwa unatembea nami, wala hakukuwa na shida yoyote, iweje leo katika shida zangu, umejitenga mbali nami?. Mungu wangu, Mungu wangu, upo wapi mbona umeniacha?.

Hali kama hii hii ilimkuta Daudi wakati anakimbizwa na Sauli, wakati anapitia shida nyingi mapangoni, wakati yupo katika kukataliwa, na dhiki, akaona kama vile Mungu hajihusishi tena, kamwacha peke yake, tunasoma:

Zaburi 10:1 “Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali? Kwani kujificha nyakati za shida?”.

Zaburi 13: 1 Ee Bwana, hata lini utanisahau, hata milele? Hata lini utanificha uso wako?

2 Hata lini nifanye mashauri nafsini mwangu, Nikihuzunika moyoni mchana kutwa? Hata lini adui yangu atukuke juu yangu?

3 Ee Bwana, Mungu wangu, uangalie, uniitikie; Uyatie nuru macho yangu, Nisije nikalala usingizi wa mauti.

Nawe pia Wakati mwingine unaweza ukawa unapitia hali ngumu, magonjwa ya kutisha ambayo madaktari wamekuambia hakuna matumaini hapa, watu wanakutisha na kukupa shuhuda za waliokufa kwa magonjwa ya namna hiyo, unaumwa Kansa, unaumwa Ukimwi, Presha, Kisukari na magonjwa yote ya ajabu yaliyo duniani siku hizi. Umeombewa sana, ila hali bado ipo vilevile.

Na kweli ndani ya moyo wako unajua kabisa Mungu wako hawezi kukuacha, lakini bado unahisi kama vile hakuoni katika hali unayopitia sasa, unahisi kama vile, amekaa kimya, hachukui hatua yoyote kwa hilo tatizo ulilonalo kwa muda mrefu..

Nataka nikutie moyo, Biblia inasema Mungu hakuwahi kulidharau teso la mteswa. Na maneno hayo yafaraja tunayapata katika Kitabu cha Zaburi, kitabu kile kile ambacho Bwana YESU alikinukuu akiwa pale msalabani, ndicho hicho hicho Mungu alimpa majibu ya maneno yake…

Tusome:

ZABURI 22

1 Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu?

2 Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha.

3 Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli.

4 Baba zetu walikutumaini Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa.

5 Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini wasiaibike.

6 Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Laumu ya wanadamu na mzaha wa watu.

7 Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao;

8 Husema, Umtegemee Bwana; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye.

9 Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinitumainisha matitini mwa mama yangu.

10 Kwako nalitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu.

11 Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi.

12 Mafahali wengi wamenizunguka, Walio hodari wa Bashani wamenisonga;

13 Wananifumbulia vinywa vyao, Kama simba apapuraye na kunguruma.

14 Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya mtima wangu.

15 Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi wangu waambatana na taya zangu; Unaniweka katika mavumbi ya mauti

16 Kwa maana mbwa wamenizunguka; Kusanyiko la waovu wamenisonga; Wamenizua mikono na miguu.

17 Naweza kuihesabu mifupa yangu yote; Wao wananitazama na kunikodolea macho.

18 Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura.

19 Nawe, Bwana, usiwe mbali, Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia.

20 Uniponye nafsi yangu na upanga, Mpenzi wangu na nguvu za mbwa.

21 Kinywani mwa simba uniokoe; Naam, toka pembe za nyati umenijibu.

22 Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu, Katikati ya kusanyiko nitakusifu.

23 Ninyi mnaomcha Bwana, msifuni, Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni, Mcheni, enyi nyote mlio wazao wa Israeli.

24 MAANA HAKULIDHARAU TESO LA MTESWA, WALA HAKUCHUKIZWA NALO; WALA HAKUMFICHA USO WAKE, BALI ALIPOMLILIA AKAMSIKIA.

25 Kwako zinatoka sifa zangu Katika kusanyiko kubwa. Nitaziondoa nadhiri zangu Mbele yao wamchao.

26 Wapole watakula na kushiba, Wamtafutao Bwana watamsifu; Mioyo yenu na iishi milele.

27 Miisho yote ya dunia itakumbuka, Na watu watamrejea Bwana; Jamaa zote za mataifa watamsujudia.

28 Maana ufalme una Bwana, Naye ndiye awatawalaye mataifa.

29 Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu, Humwinamia wote washukao mavumbini; Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake,

30 Wazao wake watamtumikia. Zitasimuliwa habari za Bwana, Kwa kizazi kitakachokuja,

31 Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake, Ya kwamba ndiye aliyeyafanya.


Ukisoma ule mstari wa 24, anasema: 24 MAANA HAKULIDHARAU TESO LA MTESWA, WALA HAKUCHUKIZWA NALO; WALA HAKUMFICHA USO WAKE, BALI ALIPOMLILIA AKAMSIKIA.

Na wewe vile vile ambaye umeokoka, umepitia hali ya shida kwa muda mrefu, bila kuona dalili yoyote ya kuponywa au kutoka katika mahali ulipo, fahamu kuwa Mungu hajalidharau teso lako, wala hachukizwi nawe, wala hajauficha uso wake kwako, bali siku ile ya kwanza ulipomlilia alishakusikia, hivyo hutakufa. Kwahiyo kaa katika matumaini ya kuipokea muujiza wako, wakati aliokuandalia utaufurahia wema wake, ulio mwingi. Ilikuwa ni lazima Mungu aruhusu Bwana Yesu ayapitie yale ili alete faida kubwa zaidi katika ufalme wa mbinguni ndio maana Mungu alikaa kimya kwa wakati ule, lakini alipomaliza kazi yake, mateso yale yamekuwa sababu ya mimi na wewe kuupata wokovu. Vivyo hivyo na wewe usitishwe na kitu chochote, maadamu yupo pamoja na wewe sikuzote. Atakupigania.

Songa mbele na Bwana Yesu Kristo atakuonekania.

Ubarikiwe sana. Tafadhali “Share” Ujumbe huu na kwa wengine. Na Mungu atakubariki.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

BASI MUNGU AKAMUADHIMISHA SANA..

MNGOJEE BWANA

MAISHA ULIYOPITIA NYUMA NI USHUHUDA TOSHA WA WEWE KUMTUMIKIA MUNGU:

USIISHIE KUTAZAMA JUU, ENDELEA MBELE.


Rudi Nyumbani

 

Print this post

USIWE SABABU YA WATU KUMKUFURU MUNGU.

2 Samweli 12:9 “Kwa nini umelidharau neno la Bwana, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni.

10 Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako.

11 Bwana asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili.

12 Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na mbele ya jua.

13 Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa.

14 Lakini, KWA KUWA KWA TENDO HILI UMEWAPA ADUI ZA BWANA NAFASI KUBWA YA KUKUFURU, MTOTO ATAKAYEZALIWA KWAKO HAKIKA YAKE ATAKUFA”.

Shalom! Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe.

Leo tutajifunza, madhara ya kuruhusu dhambi katika maisha yetu!..Tukijifunza kwa Daudi, ambaye Mungu alimpaka mafuta awe Mfalme juu ya Israeli, kama wengi wetu tunavyojua, alikwenda katika njia za Mungu kwa ukamilifu wote isipokuwa katika habari za Mke wa Uria.

1 Wafalme 15:5 “kwa sababu Daudi alifanya yaliyo mema machoni pa Bwana, wala hakukosa katika yote aliyomwamuru, siku zote za maisha yake, isipokuwa katika habari ya Uria, Mhiti”.

Kosa la Daudi kumchukua mke wa Uria na kumwua Uria mwenyewe, ndio lililotia doa haki yake…Lilikuwa ni machukizo makubwa sana mbele za Mungu, mpaka Daudi alikuwa hatiani kufa…kwasababu alistahili kufa…Lakini kwasababu pia alikuwa ni mwepesi wa kujirudi na kukimbilia kutubu, Bwana alimhurumia na akaghairi kumwua, lakini hakumwacha bila adhabu.

Unajua wengi wetu tunadhani madhara ya dhambi ni kumwudhi Mungu tu basi..si zaidi ya hapo…lakini kiuhalisia madhara ya dhambi ni marefu sana, hayaishii tu kumwudhi Mungu bali yanakwenda mpaka kuathiri kazi ya Mungu.

Unaweza ukatenda sasahivi jambo, wewe ukaliona ni dogo tu! Lakini hilo jambo ulilolifanya likaenda kusababisha madhara mengine makubwa huko, ya jina la Mungu likatukanwa..kwahiyo ikawa umemletea mazao mengi shetani. Ndio maana kuna umuhimu mkubwa sana wa kujiepusha na dhambi za makusudi.

Tukirudi kwa Daudi tunaona alifanya nayeye dhambi kama hiyo ya makusudi, yeye alifanya kwa siri, akijua ni dhambi ndogo, lakini mbele ya jicho la Mungu ilikuwa ni dhambi yenye kuleta madhara makubwa katika Israeli..Kwa maana kwa kitendo kile Daudi alichokifanya, watu wote ambao walikuwa wanamsifia Daudi kuwa ni Mtumishi wa Mungu mkamilifu, waliposikia kamwua mtu asiye na hatia na kumwibia mke wake, walimdharau Mungu wake,…Hayo ndiyo madhara ambayo Mungu yanamchukiza zaidi.

Ndio maana Bwana alimwambia katika ule mstari wa 14 maneno yafuatayo.. “14 Lakini, KWA KUWA KWA TENDO HILI UMEWAPA ADUI ZA BWANA NAFASI KUBWA YA KUKUFURU, MTOTO ATAKAYEZALIWA KWAKO HAKIKA YAKE ATAKUFA”.

Mtoto Yule Mungu alimwua sio kwasababu ya makosa ya huyo mtoto, ni kwasababu ya Daudi, na aliadhibiwa hivyo kwasababu ALIWAPA ADUI ZA BWANA NAFASI YA KUKUFURU.

Hivyo na sisi tunajifunza hapo, tusipime kimo cha dhambi kwa jicho la juu juu tu! Kwamba nitatenda dhambi na kutubu! Tambua kuwa dhambi za makusudi zina madhara makubwa sana, sio kwako tu bali pia katika kuidhoofisha kazi ya ufalme wa mbinguni. Kwasababu zinasababisha jina la Mungu linatukanwa.

Warumi 2:21 “basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe?

22 Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu? 

23 Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati?.

24 KWA MAANA JINA LA MUNGU LATUKANWA KATIKA MATAIFA KWA AJILI YENU, kama ilivyoandikwa”.

Hatupaswi kufanya watu wamkufuru Mungu wetu kwa tabia zetu za ubishi, mashindano, wizi, kwa uasherati, uzinzi, wizi na utukanaji na mambo mengine yote machafu, Ni heri useme wewe sio mkristo kuliko useme ni mkristo halafu mtu asiyeamini akukute unafanya hayo mambo, utakuwa umemfanya aamini kuwa Ukristo ni unafki na uongo, jambo ambalo si kweli. Utakuwa unamsulibisha Kristo mara ya pili.

Daudi alimsababishia Yule mke wa Uria uchungu mwingi, kwa kumwulia mumewe na pamoja na huyo mtoto aliyemzaa Bwana alimwua… lakini Bwana alimfariji baadaye, Mama yake Sulemani alikuwa ni huyu mke wa Uria, ingawa Daudi alikuwa na wake wengi wenye watoto wengi lakini wana wao hawakuketi mahali pa Daudi isipokuwa mwana wa huyu mke wa Uria ambaye alikuwa ni Sulemani, mfalme mkuu.

Kwahiyo tunaonywa tujichunguze mienendo yetu, na tuyajue madhara ya dhambi kuwa hayaishii tu kutuletea sisi madhara, bali pia yanaathiri kazi za Mungu za kuwavuta watu kwake.

Ubarikiwe.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali, au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

MSHAHARA WA DHAMBI:

DHAMBI ZINAZOTANGULIA NA ZINAZOFUATA.

SWALI: JE! KUNA DHAMBI KUBWA NA NDOGO, NA KAMA HAKUNA JE! MTU ALIYEUA NA ALIYETUKANA JE WATAPATA ADHABU SAWA?


Rudi Nyumbani

Print this post

LAANA YA YERIKO.

Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze maneno ya uzima. Wana wa Israeli walipokuwa wanavuka Yordani kuingia Kaanani kama tunavyosoma habari walikutana na kizuizi kikubwa sana, nacho si kingine zaidi ya Mji wa Yeriko pamoja na watu wake ambao walikuwa hodari sana, majitu makubwa yenye nguvu, hayo ndiyo yaliyowasababishia mpaka Mungu achukizwe nao, kwa vile walivyojiona mbele zao kama mapanzi na hivyo Mungu akakasirishwa nao na kuwafanya wazunguke jangwani kwa muda wa miaka 40.

Hivyo mji huu wenye kuta kubwa, ulikuwa ni kama kikwazo kikubwa cha wana wa Israeli kumiliki nchi yao tangu zamani, hata hakukuwa na mji uliokuwa mkubwa zaidi ya ule, mfano Yeriko usingekuwepo, wana wa Israeli tangu zamani wangeshakuwa wamewasili katika nchi yao ya Kaanani Mungu aliyowaahidia.

Sasa ndio baadaye tunaona Yoshua baada ya kupewa maagizo ya kuushambulia ule mji, kwa kuuzunguka mara 7, kisha waingie ndani waue kila kitu, na walipomaliza vita, na kuuchoma mji tunaona Yoshua anasimama na kuzungumza maneno haya ya Laana:

Yoshua 6:26 “Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za Bwana mtu yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo.

27 Basi Bwana alikuwa pamoja na Yoshua; sifa zake zikaenea katika nchi ile yote”.

Tunaona Laana hii Yoshua aliitamka tu kwa mji huu, wa Yeriko hakutamka maneno kama hayo kwenye miji mingine ya Kaanani waliyoishambulia, ni kwasababu gani? Ni kwasababu Yeriko ndio mji pekee uliowatesa, na ndio uliowagharimu muda mwingi kuuweka chini. Yoshua ndio anayejua vizuri shida waliyoipata wakati ule walipokuwa na wale wapepelezi wenzake miaka 40 iliyopita jinsi mji huo ulivyokuwa kikwazo kikubwa kwao mbele za Mungu, Mpaka Yoshua akaona kujengwa tena mji huo ni sawa na kukumbushwa machungu yote ya kule jangwani..Ndio maana akazungumza Laana ile.

Hivyo wale watu waliokuwa na Yoshua, waliyashika maneno yale, hata wakati wamemaliza kuiteka miji yote na kuanza kujenga na kupanda, kama Bwana alivyowaagiza kuwa watakapoingia nchi ya ahadi wajenge na kupanda maana atawabikia kwa vingi…lakini ule mji wa Yeriko ulibakia vile vile bila kuguswa kama makumbusho ya Taifa, hakuna aliyedhubutu kwenda kuuendeleza kwa namna yoyote ile, na hiyo iliendelea kwa miaka mingi mbeleni.

Lakini baada ya miaka kama 530 hivi kupita, wakati wa utawala wa mfalme Ahabu, alitokea mtu mmoja, aliyeitwa Hieli mbetheli, yeye kwa kutokujua, au kwa kupuuzia, au kwa uzembe wake wa kutofuatilia msingi ipoje, na torati inasema nini juu ya mji huo, hakujiuliza ni kwanini mji huo umeachwa ukiwa muda mwingi angali mingine inaendelezwa yeye akanyanyuka na kwenda kuanza kuujenga Yeriko,..Na Laana ile ikampata sawasawa na maneno ya Yoshua.

1Wafalme16:34 “Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.”

Hii inatufundisha nini?, …kutokujua sheria hakukufanyi wewe usihukumiwe kwa sheria..Mungu akitamka laana zake halikadhalika na Baraka zake haijalishi unafahamu au haufahamu zitakupata tu. Hapa tunaona jambo hili lilitimia miaka 530 baadaye, nataka nikuambie hata na Leo eneo la Israeli ambalo mji wa Yeriko ulikuwepo, mtu aliyehusika au atakayehusika kuliendeleza eneo hilo jambo hili lilimpata au litampata haijalishi anafahamu au afahamu.

Sasa hiyo ni laana inayowahusu waisraeli, na agano la Kale, lakini vilevile katika agano jipya ipo laana ya namna hiyo hiyo imetolewa na Mtume Paulo..Tena hii ndio mbaya zaidi kwasababu inahusisha na mambo ya rohoni moja kwa moja.

Wakati ule, Mitume walipokuwa wanateseka, kuuhubiri injili ya ufalme wa mbinguni unaopatikana kwa Imani ya YESU KRISTO tu, wakiwa wanazunguka huku na huko, wakipitia hatari nyingi za kupigwa, na kufungwa na kuuawa, Na mwisho wa siku wanafanikiwa kuifikisha injili duniani kote..Mataifa yanaokoka, watu wanamtazama Yesu Kristo, wanaufurahia wokovu wake, wamestarehe.

Lakini huku nyuma kukaanza kutokea jopo lingine la wayahudi wa uongo, mitume wa uongo, waalimu wa uongo na manabii wa uongo, wakaanza kuwafundisha wale watu ambao walishamwamini Kristo injili ya namna nyingine ambayo mitume hawakuipeleka kwao. Jambo hili liliwahuzunisha sana mitume mpaka ikafikia hatua mtume Paulo anatoa laana hii kwa uweza wa Roho:

Wagalatia1:6 “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia INJILI YA NAMNA NYINGINE.

7 Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo.

8 Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, NA ALAANIWE.

9 Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, NA ALAANIWE.

10 Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo.”

Umeona, laana hii ilitoka karibia miaka 2000 iliyopita, na inayo nguvu ile ile hadi sasa, kama kipindi kile kulikuwa kumeshaanza kuonekana mitume wa uongo, sasahivi tusemeje.Hakuna mtu asiyejua hilo, Kila mahali tunasikia injili ambazo ukizilinganisha na injili za mitume hazina uhalisia wowote.. Na hatujui kuwa laana hii inaendelea kufanya kazi hadi sasa. Tusijidanganye na kusema hatujui, ni vizuri kabla ya kutaka kuwa waalimu, au wahubiri wa Neno la Mungu, tufahamu biblia inatufundisha nini au inataka nini. Vinginevyo tunaweza kujikuta tunadondokea katika laana mbaya ya Mungu pasipo hata sisi kujua.

Bwana Yesu alifunga vitabu vya agano jipya kwa maneno haya:

Ufunuo 22:17 “Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure.

18 Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.

19 Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.”

Tufundishe Injili ya mitume ili tuwe katika Upande salama. Bwana atusaidie katika hilo.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

MADHARA YA KUTAFUTA ISHARA.

MWAMUZI WA KWELI

TUMEPEWA, SI KUMWAMINI TU KRISTO, ILA NA KUTESWA KWA AJILI YAKE;

NJIA YA MSALABA


Rudi Nyumbani

Print this post

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 4

Shalom! Karibu tujifunze Biblia, bado tupo katika mwendelezo wa kujifunza vitabu vya Biblia, tukiwa tayari tumeshavitazama vitabu tisa vya kwanza, na leo tutaendelea na kitabu kimoja kinachofuata kijulikanacho kama Samweli wa Pili,

Kumbuka huu ni uchambuzi tu! Ambao umechukua tu baadhi ya sehemu, sio ukamilifu wote, na biblia haina tafsiri moja maalumu, hapana! Mstari mmoja unaweza kuwa na mafunuo au mafunzo zaidi hata ya milioni moja, kwa jinsi tu Roho atakavyopenda kumfunulia mtu na mtu.

Kwahiyo ikiwa wewe ni mkristo mwenye Roho Mtakatifu ndani yako ni vizuri pia kuutumia muda wako binafsi kuisoma biblia yako, ukiwa peke yako, kwani Roho anaweza kukufunulia jambo ambalo haujawahi kulisikia likihubiriwa kwa mtu yoyote au mtumishi yoyote. Kwasababu Roho ya Mungu sio ya mwanadamu. Yeye hagawanywi kwa vipimo, hivyo mtu yoyote akiwa na NIA ya kujua, Roho Mtakatifu atamfunulia yote kama alivyoahidi katika neno lake.(Yohana 16:13)

Katika kitabu kilichopita cha Samweli wa kwanza (1Samweli), tulishaona kuwa kitabu hichi kiliandikwa na Nabii Samweli mwenyewe, isipokuwa katika sehemu za mwishoni mwa kitabu hicho, ambazo ziliandikwa na Nabii Nathani na Nabii Gadi, kwasababu Samweli asingeweza kuandika habari za kufa kwake mwenyewe katika kitabu hicho, hivyo ni wazi kuwa kuna wengine ndio waliondika sehemu hizo za mwisho..kama hujapitia bado hichi kitabu basi ni vizuri ukapitia kwanza uchambuzi wa vitabu vya mwanzo ili tuende pamoja huku mbeleni. BOFYA HAPA⏩ Vitabu vya biblia:Sehemu ya 3

Kitabu cha Samweli wa Pili, kiliandikwa na Nabii Nathani na sehemu baadhi kiliandikwa na Nabii Gadi..Nabii Nathani alikuwa ni Nabii wa Mungu, Wafalme hawakuwa manabii, ilikuwa ni ngumu wao kusikia Neno la moja kwa moja kutoka kwa Mungu, hivyo walihitaji watu maalumu waliopewa hiyo karama (ambao ndio manabii) kwahiyo kila mfalme alikuwa na manabii kadhaa ambao ndio walikuwa washauri wake wa karibu na ndio waliokuwa wanawaambia mambo yote Mungu aliyozungumza kuwahusu wao na ufalme wao. Kwahiyo Nathani alikuwa ni Nabii wa Mfalme Daudi, chochote Bwana alichokuwa anataka kuzungumza alikuwa anamwambia Nathani na kisha Nathani anakwenda kumwambia Daudi..kwahiyo Nathani kwasababu muda wote ndio alikuwa anakaa na Daudi yeye ndiye aliyekuwa anarekodi matukio yote ya utawala wake kwa kuongozwa na Mungu.

Sasa kitabu hichi kinaelezea maisha ya Daudi katika Ufalme wake, Kumbuka baada ya kufa mfalme wa Kwanza wa Israeli (yaani Sauli), Daudi ndio aliuchukua utawala mahali pake, kwasababu aliahidiwa na Mungu kuwa atatawala juu ya Israeli. Kwahiyo kitabu hichi kinamhusu Daudi mwanzo mwisho.

Unaweza kuipata historia ya Daudi kwa kusoma mwenyewe kitabu cha Samweli wa kwanza, lakini kwa ufupi ni kwamba Daudi hakuupata ufalme kama Sauli alivyoupata..Ukielewa vizuri jambo hili litakusaidia kujua kuwa wakati mwingine njia za Mungu si kama za mwanadamu,…utajifunza pia kutokujilinganisha na mtu mwingine na kumshukuru Mungu kwa kila kitu, katika mahali ulipowekwa… kwasababu njia hazifanani…Umewahi kusikia watu ambao Mungu kawabariki kwa mali za urithi na wale ambao Mungu kawabariki kwa kuhangaika kwao wenyewe?…Makundi yote haya mawili yanaweza yakawa yamepewa thawabu hiyo moja na Mungu mwenyewe isipokuwa katika njia mbili tofauti, mmoja kwa kurithi pasipo kuhangaika na mwingine kwa kuhangaika..Lakini kila moja ina faida zake na hasara zake.

Na kwa Daudi ilikuwa ni hivyo hivyo, Mfalme wa Kwanza Sauli, aliupata ufalme pasipo hata kuhangaika, baada ya kutiwa tu mafuta na Samweli, Bwana akamtengenezea njia akawa mfalme ndani ya usiku mmoja pasipo hata kuhangaika, lakini ilipofika zamu ya Daudi kuwa mfalme juu ya Israeli, shughuli ilikuwa ni nzito kidogo…hakuupata kama Sauli alivyoupata…Na hiyo ni kwasababu ilimpendeza Mungu iwe hivyo, ndio maana unaona Daudi alimpendeza Mungu zaidi ya Sauli.

Daudi baada ya kupakwa mafuta na nabii Samweli alidhani itakuwa ni rahisi tu kuingia kwenye ile enzi kama ilivyokuwa kwa Sauli, alijua utafika wakati tu, Israeli wote watautii unabii wa Samweli juu ya yeye kuwa mfalme na hivyo watakusanyika na kwenda kumwomba awe mfalme kwasababu amechaguliwa na Mungu, kama ilivyokuwa kwa Sauli hakutakuwa na upinzani wowote…lakini ukisoma biblia ndio utajua mambo Daudi aliyoyapitia mpaka alipokuja kuwa mfalme…Aliteseka nyikani kutwa kuchwa kuwindwa kama ndege kwa muda wa si chini ya miaka 15, baada tu ya kupakwa mafuta, aliongeza idadi ya maadui kwa kasi kubwa, mpaka mfalme alikuwa adui yake…Jaribu kujenga picha sasahivi unakuwa adui wa Raisi?..utakimbia wapi asijue? Maana anao wapelelezi wake kila kona, hata kitongoji wa kijiji atakuwa adui yako kwasababu akikuona ni kama kapata deal la fedha, au “kick” kwa mfalme…Inahitaji mkono wa Mungu tu! Kuepukana naye…ndio Daudi naye alikuwa hivyo hivyo, ilihitajika mkono wa Mungu tu kuepuka na mkono wa Mfalme Sauli aliyekuwa anamwinda usiku kucha.

Ilifika kipindi akawa hakai mjini tena, anakaa maporini na kwenye mapango kwa miaka ya kutosha, kwasababu akitokeza mjini tu, waandishi wa habari wapo wa kumpelekea mfalme taarifa, chakula kilikuwa ni cha kwenda kuomba! Omba! Unakula leo hujui kesho itakuwaje!..kuna wakati alikuwa anapungukiwa kabisa anapitia njaa kali pamoja na wale watu wachache aliokuwa nao…na mbaya zaidi alipata maadui ambao walikuwa wanamchochea kwa mfalme mambo ya uongo…

Ilifika kipindi wale mafilisti ambao alikuwa anawaita wamelaaniwa na wasiotahiriwa, wale ambao aliwaulia jemedari wao Goliathi, alikimbilia nchini kwao kuomba msaada (kuungana nao) [1Samweli 27:1], joto lilikuwa kali Israeli mpaka akaona akiendelea kukaa Israeli ana muda mchache sana wa kuishi…maana alikuwa anatafutwa kila kona, alikuwa na kesi za kutengenezewa si haba!.kiasi kwamba alikuwa anajua akishikwa tu na mfalme ni anakwenda kuchunwa ngozi mzima mzima. Ilifika kipindi hofu ya Mfalme ilikuwa kubwa hata kwa Israeli kiasi kwamba ukimwona Daudi halafu hujatoa taarifa na ikajulikana ulimwona hujatoa taarifa, ilikuwa ni KIFO!.

Sijui kama ulishawahi kupitia hali kama hivyo? Daudi hakuna chochote alichokuwa anafanya cha kujiendeleza kwa miaka zaidi ya 15.Wala alikuwa haishi maisha ya raha, Ni pori na yeye yeye na pori, Sio wewe unapitia kusemwa kidogo unasema una maadui!! Unapitia kutukanwa kidogo unasema unamaadui!..unatengwa kidogo unalalamika na kunung’unika unasema una maadui na bado unakula vizuri na unakunywa, na kesho unao uhakika wa kuishi… Daudi mpaka alihamia nchi jirani, kwenda kwa watu wasiotahiriwa ambao aliwatukana hapo kabla, angalau apate unafuu, kwa makubaliano kuwa hata ikitokea vita dhidi ya ndugu zake yupo tayari kuungana na wafilisti kwenda kinyume nao…

Taifa zima lilimgeuka, hata kama kulikuwa na wachache waliomkubali lakini itasaidia nini, kama Serikali nzima iko kinyume chako?..Wewe sasahivi Raisi atoe agizo la kukutafuta ili uuawe, ukizingatia kwenu ni wakulima na wafugaji, huna chochote…si utasema ni heri usingezaliwa…tena afadhali siku hizi mfumo wetu ni wa Uraisi ,zamani ilikuwa ni Ufalme, Mfalme alikuwa yupo juu ya sheria, tofauti na sasahivi ambapo Raisi hayupo juu ya sheria, na Mfalme alikuwa anatawala mpaka afe sio sasahivi baada ya miaka 10 tu amebadilika ameingia mwingine..

Kwahiyo hayo ndio mambo Daudi aliyokuwa anayapitia …Wengi wetu hatujui Kitabu cha Zaburi kiliandikwaje andikwaje! Sehemu kubwa ya kitabu cha Zaburi Daudi alikiandika akiwa nyikani, alipokuwa anawindwa…wakati anapitia shida! Ndipo akawa anasema….

Zaburi 13:1 “Ee Bwana, hata lini utanisahau, hata milele? Hata lini utanificha uso wako?

2 Hata lini nifanye mashauri nafsini mwangu, Nikihuzunika moyoni mchana kutwa? Hata lini adui yangu atukuke juu yangu?

3 Ee Bwana, Mungu wangu, uangalie, uniitikie; Uyatie nuru macho yangu, Nisije nikalala usingizi wa mauti.

4 Adui yangu asije akasema, Nimemshinda; Watesi wangu wasifurahi ninapoondoshwa.

5 Nami nimezitumainia fadhili zako; Moyo wangu na uufurahie wokovu wako.

6 Naam, nimwimbie Bwana, Kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu”.

Huo ni mfano wa Maombi ya Daudi akiwa katika tabu ya kuwindwa na majeshi ya Mfalme Sauli..na hakuomba leo yakajibiwa leo leo…yalichukua miaka ya kutosha…Kwahiyo hizo Zaburi hazikuandikwa na mtu aliyekuwa hajui nini anazungumza, hakumwandikia mtu hizo, alijiandikia yeye…kila maombi aliyokuwa anaomba alikuwa anayaandika…ndio sisi tunayasoma leo kama ZABURI.

Kila hatua aliyokuwa anapitia alipokuwa anatafutwa, alikuwa anamwomba Mungu na kumshukuru na kumwimbia..na kila nyimbo kila sala na kila shukrani alikuwa anaiiandika, siku baada ya siku..Kuna wakati Daudi alikuwa hatiani kufa kwa kushikwa na Sauli, alikuwa ameshazingirwa pande zote, lakini Bwana akamwokoa na mkono wa Sauli, hivyo akamwimbia Mungu nyimbo za kumshukuru na akaziandika zote…

Sehemu chache sana za Zaburi Daudi aliziandika akiwa tayari kashakuwa mfalme…na nyingi ya hizo aliziandika kwa lengo la kumshukuru Mungu jinsi alivyomwokoa na maadui zake alipokuwa taabuni…Sasa utauliza ni wapi penye uthibitisho kuwa Zaburi iliandikwa na Daudi wakati yupo matesoni au wakati yupo kwenye ufalme?…Ukisoma kitabu cha Zaburi 18:1-7 biblia inasema “

1 Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;

2 Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.

3 Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa, Hivyo nitaokoka na adui zangu.

4 Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.

5 Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili.

6 Katika shida yangu nalimwita Bwana, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake.

7 Ndipo nchi iliyotikisika na kutetemeka, Misingi ya milima ikasuka-suka; Ikatikisika kwa sababu alikuwa na ghadhabu……”

Ukisoma mistari hiyo ya mlango wa 18 wa Zaburi, unaweza usielewe mwandishi kwanini aliandika hivyo au ni nini kilichomsukuma mpaka akaandika hivyo…alikuwa katika mazingira gani?…sasa jibu la swali hilo tunalipata katika kitabu cha 2 Samweli 22…

2 Samweli 22:1 BASI DAUDI AKAMWAMBIA BWANA MANENO YA WIMBO HUU, SIKU ILE BWANA ALIPOMWOKOA MIKONONI MWA ADUI ZAKE ZOTE, NA MKONONI MWA SAULI;

2 akasema, Bwana ndiye jabali langu, na ngome yangu, na mwokozi wangu, naam, wangu;

3 Mungu wa mwamba wangu, nitamwamini yeye; Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, mnara wangu, na makimbilio yangu; Mwokozi wangu, waniokoa na jeuri.

4 Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa; Hivyo nitaokoka na adui zangu.

5 Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.

6 Kamba za kuzimu zilinizunguka; Mitego ya mauti ikanikabili.

7 Katika shida yangu nalimwita Bwana, Naam, nikamlalamikia Mungu wangu;

8 Ndipo nchi ilipotikisika na kutetemeka, Misingi ya mbinguni ikasuka-suka Na kutikisika, kwa sababu alikuwa na ghadhabu…”.

Umeona sababu za Daudi kuandika Zaburi?… Hivyo kitabu cha Samweli wa pili kinatufundisha jinsi Mungu anavyotenda kazi juu ya mtu na mtu…njia atakayotumia kukupa wewe, sio sawa na atakavyotumia kumpa mwingine, ni vizuri zaidi kupenda kupitishwa njia ngumu kwasababu hizo ndio zinazotufanya mara nyingi tuwe wakamilifu kuliko zile njia rahisi. Njia rahisi za kupata kitu zinatufanya tusikithamini kile kitu chenyewe,…kama Mfalme Sauli alipata ufalme kwa njia rahisi ndio maana hakuuthamini ufalme wake, akawa anafanya mambo ambayo Mungu hakumuagiza,…

lakini Daudi kwa miaka zaidi ya 15 alijaribiwa kwa mateso na hatari za vifo na kwa kurudia rudia kuomba pasipo majibu ya papo kwa hapo…..ndipo tunaona alipokuja kuupata ufalme aliuthamini sana, na aliishi kulingana na mapenzi ya Mungu..siku zote za ufalme wake, mpaka Mungu akamwahidia uzao wake utamtoa MASIHI (BWANA YESU KRISTO) ambaye sasa ndiye mkombozi wetu MWANA WA DAUDI. Katika ufalme wake alijifunza kunyenyekea na kuwathamini na kuwafariji pia walioko kwenye tabu..maana na yeye alishayapitia hayo..alikuwa hawaonei watu maana anajua uchungu wa kuonewa na kukimbizwa..

Pia kitabu hichi kinatufundisha njia kamili ya Mungu ni kutupa kidogo kidogo, mpaka kinakuwa kingi (Mithali 13:11)…usipende njia za haraka haraka, nyingi ya hizo sio mpango wa Mungu, utaona pamoja na Daudi kupitia taabu zote hizo hata ufalme hakupewa wote ndani ya siku moja…ukisoma biblia utakuja kuona kuwa alipewa na Mungu kwanza utawala juu ya Kabila moja kwa miaka 7, na baadaye ndipo akapewa utawala wa Israeli yote kwa miaka 33..Na aliishi kwa kumpendeza Mungu maisha yake yote, isipokuwa kwa kasoro ndogo ndogo alizokuwa nazo, lakini kwa ujumla alimpendeza Mungu sana..hiyo ni kutokana na kunolewa vyema kabla ya kuipokea ahadi aliyopewa na Mungu.

Na pia tunajifunza katika kitabu hichi kutokukata tamaa…Daudi alipitia tabu, mpaka dakika ya mwisho aliyokuwa amekata tamaa ndio kipindi hicho hicho Mungu alimpa ufalme, kipindi ambacho yupo nchi nyingine..kipindi ambacho asingetarajia, wala kulikuwa hakuna dalili yoyote ya yeye kumiliki ufalme ndio kipindi alichopokea ufalme tofauti na mategemeo yake, pengine alidhani wakati anamuua mfilisti wakati Israeli wote wanamshangalia ndio angeupata ufalme lakini badala yake, mahali ambapo yupo katika shida nchi ya ugenini ndipo Mungu anamnyanyua..kadhalika, njia za Mungu hazichunguziki, kipindi ambacho mtu anaweza kusema hapa haiwezekani tena, afadhali ingekuwa jana au juzi au mwaka juzi, lakini hajui kuwa kumbe huo ndio wakati uliofaa wa Mungu, kwahiyo ni kujifunza kuishi maisha ya kutokukata tamaa na kutokunung’unika siku zote na kumwamini Mungu.

Na mwisho maisha ya Daudi yamebeba siri ya Maisha ya Yesu Kristo, jinsi alivyopitia na kuishi ni Ufunuo wa Yesu Kristo jinsi alivyoishi hapa duniani..Naye pia alikuwa ni mfalme aliyekataliwa kama Daudi, na hata zaidi ya Daudi..tangu kuzaliwa kwake. Biblia inatuambia hivyo katika..

Isaya 53:1 Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?

2 Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.

3 Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.

4 Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.

Tunaona Herode alitamani kumwua, hata Israeli hawakumwamini ingawa yeye ndiye aliyeteuliwa na kupakwa mafuta na Mungu kuwa mfalme juu ya Israeli..lakini alipofika miaka 30 kama Daudi ndipo ulimwengu kidogo kidogo ukaanza kumsikia, ile ahadi ya ufalme ikaanza kutimia…akaanza kuutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa…Na alipokufa na kufufuka ikatimia, sasahivi hatumtambui tu kama mfalme bali ni MFALME MKUU,MUNGU MWENYE NGUVU..Tutakuja kuulewa vizuri ufalme wake wakati wa Utawala wa miaka 1000 hapa duniani, sasahivi bado.

Hivyo kama hujayakabidhi maisha yako kwake ni vyema ukafanya hivyo leo usikawie kawie kwasababu haya maisha hatujapewa guarantee ya kufika kesho, na hakuna mwingine utakayeweza kupata tumaini kwake kama sio KRISTO…Yeye ndiye mpakwa mafuta pekee wa Mungu, tubu leo kwa kudhamiria kabisa kuacha dhambi, kama hujafanya hivyo…ukabatizwe katika ubatizo sahihi kwa jina lake upate ondoleo la dhambi zako, na kisha upokee kipawa cha Roho wake Mtakatifu, kabla mlango wa Neema haujafungwa.

Bwana akubariki sana

Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Kwa mwendelezo >>>VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 5


Mada Nyinginezo:

ALIYE MKUU KATIKA UFALME WA MBINGUNI.

TABIA YAKO NI YA MNYAMA GANI?

MANABII WALISEMA “NENO LA MUNGU LIKANIJIA” ..MAANA YA HILI NENO NI NINI?.

MSTARI HUU UNA MAANA GANI? “TUPA CHAKULA CHAKO USONI PA MAJI; MAANA UTAKIONA BAADA YA SIKU NYINGI”. (MHUBIRI 11:1)

JE! VITABU VYA BIBLIA VILIWEZAJE KUKUSANYWA PAMOJA?


Rudi Nyumbani:

Print this post

PEPETO LA MUNGU.

Siku moja nilipokuwa nakula wali na choroko, nilikutana na zile choroko ngumu ambazo tunajua hata ukizipika vipi huwa haziivi, nilishazoea kukutana nazo mara kwa mara, lakini sikuhiyo nilikutana nazo nyingi kiasi cha kushindwa kula chakula, hapo ndipo nilipotamani kujua hasaa huwa zinaondolewaje kwenye choroko nzuri, kwasababu wakati zinachambuliwa huwa hazionekana, ni rahisi kweli kutoa uchafu wote, na makapi yote lakini zile haziondoki zina sura ile ile kama choroko nyingine..

Ndipo nikafuatilia na kuuliza, nikagundua kuwa kumbe choroko hazichambuliwi kama maharage, maharage utatoa uchafu unaouna na kwenda kuosha na kubandika kazi imeisha, lakini choroko huwa inaenda hatua nyingine ya ziada,..Na ndio maana ukila chakula kwenye hoteli nzuri inayothamini huduma zake, chakula kama hichi huwezi kukutana na hizo choroko-mawe mdomoni, niziite hivyo, je! wanafanya nini?.

Wao wakishamaliza kutoa ule uchafu unaoonekana katika hatua ya awali, na kuziosha vizuri choroko zao, hatua inayofuata huwa wanachukua maji ya moto, kisha wanaziweka choroko ndani yake, na kuziacha hapo kwa muda wa kama dakika 5 hivi, kisha warudi kuyamwaga yale maji yote, halafu wanazimwaga kwenye sinia au ungo, wanaanza kuchambua tena, Sasa zile choroko-mawe ambazo hata uzipike na makaa ya mawe haziivi, zinajionyesha zenyewe.Kwasababu katika hatua ya awali zile nyingine zinapoanza kubadilika rangi na kuwa kama jani lililokauka hivi, zenyewe huwa zinabakia na ukijani wake hivyo hivyo kama vile vimetolewa jana shambani,..Hivyo ni rahisi kuziona na kuzitoa moja moja na kuzitupa..baadaye zile zilizobakia nzuri, wanazirudisha jikoni, na kuzipika mpaka mwisho ziive, Na hapo hata ule sufuria nzima la choroko huwezi kukutana na choroko-mawe hata moja mdomoni..

Ndivyo ilivyo hata katika kanisa la Kristo, Mungu naye huwa anachambua watu wake, katika hatua za awali, anawaita wengi sana kwake, na wengi wanamwamini na kusema mimi ni mkristo, nimeokoka, kiasi kwamba ni ngumu kutofautisha mkristo wa kweli ni yupi na Yule feki ni yupi, wote wamebatizwa, wote ni waaminio, wote ni washirika, ni sawa tu na zile choroko zinazooshwa katika maji, haijalishi ndani yao kuna nini..Lakini sasa ili lile andiko litimie linalosema “walioitwa ni wengi, lakini wateule ni wachache”, kutenganisha magugu, na ngano ni lazima kutokee..

Hapo ndipo maji ya moyo ambayo ndio (Neno la Mungu kama upanga linapopita juu ya watu)..kuangalia ni wapi watatii, na ni wapi watakuwa sugu..Hiyo ndio hatua ambayo Kristo anatupima kwa kile tulichokisikia na kufundishwa kutoka katika Neno lake na jinsi tunavyokitendea kazi,..Ikiwa wewe unajiita mkristo halafu umehubiriwa Neno miaka mingi, na ndani yako hakuonekani mabadiliko yoyote, bado ni mzinzi, mtukanaji, mvaaji vibaya, mtazamaji pornography, msengenyaji, mwendaji Disco n.k..na huku nyuma umebatizwa, ni mshirika mzuri wa Kanisani, mwimbaji kwaya,..wewe ni zile choroko-mawe ambazo hazisikii joto la maji, na siku si nyingi utaingia katika pepeteo la pili na la mwisho. Ambalo hilo ni pepeto la milele, hakuna kurudiwa tena. Hili andiko ndipo linapotimia.

1Yohana 2:19 “Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu.

Wakati wengine Mungu anawavukisha madarasa mengine ya kiroho, wanapikwa vizuri, kwa ajili ya kuurithi ufalme wa mbinguni, wewe kumbe siku nyingi ulishatupwa nje, unakuwa msindikizaji tu pasipo hata wewe kujijua, na dalili mojawapo itakayokuonyesha kuwa siku nyingi Mungu alishakuacha ni wewe kuzidi kuwa vuguvugu wa ajabu, na wenzako maisha yao ya rohoni kuimarika.

Mungu huwa anasema na watu katika viwango tofauti, ikiwa katika hatua awali, mafundisho ya msingi hayakurekebishi, mafundisho gani mengine utafundishwa yakugeuze. Choroko-mawe hata zikiachwa mpaka hatua ya mwisho bado zitabakia vile vile tu.

Ndugu tunaishi katika kanisa la 7 na la mwisho linalojulikana kama LAODIKIA, naamini utakuwa unalifahamu hilo, ni kanisa ambalo linasifika kwa tabia ya kuwa vuguvugu kuliko makanisa yote yaliyotangulia huko nyuma. (soma Ufu3:14). Na kumbuka pia SIRI ya Mungu ipo kwa bibi-arusi wa Kristo tu, na sio pamoja na Masuria..Masuria ndio wale wanawali wapumbavu ambao tunasoma walikuwa wanamngojea Bwana wao, aje lakini hawakuwa na mafuta ya ziada katika TAA ZAO (Mathayo 25)..Mbaya sana na Huo ndio uvuguvugu unaozungumziwa, nusu kwa Bwana, nusu, kwa shetani..nusu choroko, nusu uchafu…na hivyo unakuwa umekidhi vigezo vyote vya kuwa CHOROKO-MAWE. Na kustahili kutapikwa.

Wakati unao sasa wa kutengeneza mambo yako sawa, kabla mlango wa rehema hujafungwa, Mungu ni mwaminifu ukitubu atakupokea na kukuhifadhi kwake..

2Petro 1:10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe.

11 Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo”.

Ubarikiwe. Tafadhali “Share” Ujumbe huu na wengine. Na Bwana atakubariki.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

WALIOITWA NI WENGI, ILA WATEULE NI WACHACHE.

TABIA YA KIPEKEE USIYOIJUA KUHUSU NENO LA MUNGU.

HATUA ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUTUONGOZA.

TUKAZE MWENDO KWA TULIYOANDALIWA.


Rudi Nyumbani

Print this post

USIPIGE MATEKE MCHOKOO!


Karibu tujifunze Biblia, leo tutajifunza juu ya kukaa katika kusudi la Mungu.

Tukizidi kujifunza juu ya wito wa Mtume Paulo, tunaweza kupata mambo mengi sana ambayo yataweza kutusaidia sisi katika kuongeza maarifa yetu ya kumjua Mungu. Tukisoma kitabu cha Matendo ya mitume mlango wa 26, biblia inasema…

Matendo 26:14 “Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? NI VIGUMU KWAKO KUUPIGA MATEKE MCHOKOO. 15 Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi”.

Tunaona Mtume Paulo, alipokuwa anaelekea Dameski kuwakamata na kuwafunga wakristo ndipo akatokewa na Bwana njiani! Na Neno la kwanza kuambiwa ni “ Sauli Sauli mbona waniudhi?”… Hilo ni swali lisilokuwa na jibu..Ni kama vile Bwana alishawahi kumwonya mara nyingi lakini akawa hasikii…Maana ni ngumu mtu usiyemjua kuja kwako ghafla tu na kukwambia mbona unaniudhi?…Ni wazi kuwa huyo mtu mtakuwa mnajuana kwa namna moja au nyingine.

Kadhalika Paulo sio kwamba alikuwa hamjui kabisa Bwana Yesu, alikuwa anamjua na alishawahi kumsikia kipindi Bwana anaishi duniani, na alishaisikia injili ya kumvuta kwa Kristo hapo kabla…Kwasababu asingeweza kuanza kuwashika wakristo kama hakusikia kitu walichokuwa wanakihubiri, hivyo Roho Mtakatifu alikuwa anamvuta tangu zamani ndani ya moyo wake na kumshuhudia kabisa kuwa Kristo ndiye njia ya kweli lakini alikuwa anashupaza shingo, anaikataa ile sauti ndani yake, anashindana na agizo la Mungu. Ndio maana utaona hata wakati wa kifo cha Stefano alikuwepo pale akisikiliza Stefano alivyokuwa anahubiri…

Matendo 7:53 “ninyi mlioipokea torati kwa agizo la malaika msiishike.

54 Basi WALIPOSIKIA MANENO HAYA, WAKACHOMWA MIOYO, wakamsagia meno.

55 Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu.

56 Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu.

57 Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja,

58 wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli.

59 Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu.

60 Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. NA SAULI ALIKUWA AKIONA VEMA KWA KUUAWA KWAKE”.

Biblia inasema hapo waliposikia yale mahubiri ya Stefano “wakachomwa mioyo yao”…Maana ya kuchomwa mioyo hapo… “ni kufahamu kuwa kinachozungumziwa ni ukweli”…hakuna mtu anaweza kuchomwa moyo kama kitu kinachozungumzwa ni cha uongo hakuna! Ukweli ndio unaochoma watu mioyo….hivyo kwa wivu wakataka kumwua Stefano na Sauli naye (ambaye ndiye Paulo) naye alikuwepo pale pale akichomwa moyo akijua kabisa stefano anachozungumza ni kweli. Na kinachochoma watu mioyo ni Neno la Mungu ambalo ndilo KWELI yenyewe.

Kuna wengine ambao wakisikia Neno la Mungu wanachomwa mioyo na kukusudia kutubu au kuacha njia zao mbaya kama ilivyokuwa wakati wa Pentekoste kama tunavyosoma katika:

Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? 

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”..

Na kuna wengine wanaposikia Neno la Mungu linawachoma ndani wanaifanya mioyo yao kuwa migumu zaidi na kuipinga na kukusudia kumzimisha Roho ndio kama hawa wakina Sauli, walichomwa mioyo yao, lakini hawakutaka kutubu badala yake walimwua Stefano.

Kwahiyo Paulo alikuwa anajua kabisa kuwa Kristo ni mwana wa Daudi, na ni kweli alikufa na akafufuka.. moyoni alikuwa anashuhudiwa kabisa kuwa huo ndio kweli, na si yeye peke yake bali hata na baadhi ya makuhani na mafarisayo na wakuu, walikuwa wanajua kabisa Yesu ndiye Kristo lakini kwa kuwa wana wivu…wakawa wanampinga (Matendo 5:17, Marko 12:14).

Yohana 12:42 “Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi.

 43 Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu”.

Lakini kwasababu Sauli alikuwa anaipenda DINI kuliko kuyafuata mapenzi ya Mungu, akawa anashindana na agizo la Mungu, na kwa kuendelea kuwaua watumishi wa Kristo na hiyo ndio ikawa sababu ya Bwana kumtokea na kumwambia mbona waniudhi?…Na alipotokewa na Bwana jambo la kwanza kumwuliza ni nani wewe? Bwana?…anauliza swali na hapo hapo analo jibu!…alijua kabisa ni Bwana Yesu.

Sasa utaona baada ya Bwana kumwambia tu Sauli mbona waniudhi, kuna sentensi nyingine inayofuata hapo mbele yake…alisema “NI VIGUMU KWAKO KUUPIGA MATEKE MCHOKOO”

Sasa swali la kujiuliza mchokoo ni Nini?

Mchokoo ni fimbo Fulani yenye ncha ya chuma kwa mbele iliyokuwa inatengenezwa kwa mfano wa mkuki Fulani hivi, ambao wakulima wa zamani walikuwa wanaitumia kuwaongozea ng’ombe wakati wa kulima…Wakati wa kulima kulikuwa kuna ng’ombe baadhi waliokuwa na kiburi, hawataki kutembea mbele, wanaweza kuanza vizuri lakini wakifika katikati ya safari, ukijaribu kuwalazimisha tu kwenda mbele wanarusha mateke hivyo kazi inakuwa haiendi…..hivyo fimbo ya kawaida ilikuwa haiwezi kuwaongoza kwahiyo zamani ndio walikuwa wanatengeneza hiyo fimbo maalumu yenye ncha kwa mbele na kuiweka nyuma ya ng’ombe wakati wa kulima…endapo ng’ombe akikataa kusonga mbele na kurusha mateke anakutana na hiyo fimbo yenye ncha! Na inamchoma na kumwumiza, hivyo anajikuta anafanya kazi bila shuruti!..

Sasa ndio hapa Bwana anamwambia Paulo “Ni vigumu kwako kupiga mateke mchokoo”…Au kwa lugha nyepesi ni sawa na kusema “ni vigumu kwako kushindana na agizo la Mungu utakuwa unajiumiza mwenyewe”….

Bwana Yesu alimwona Paulo alikuwa anashindana na kusudi lake, na hivyo akamwambia atakuwa anajiumiza mwenyewe kwa wivu wake na hasira zake na chuki zake na kiburi chake juu ya kazi ya Mungu…Wakati anafikiria kuwaua watakatifu ndio kuwakomoa hakujua kuwa ndio anajitafutia mabaya mwenyewe, ndivyo anavyozidi kujiangamiza mwenyewe kama vile kujichomaa kwa mchokoo…….Na kama sio Bwana kumtokea njiani pengine huko alikokuwa anakwenda ndio kungekuwa mwisho wake asingerudi tena.…Kama tu Balaamu, wakati anafikiria kwenda kuwalaani Israeli wakati Bwana ameshamwonya kwa nguvu asiende, yeye akazidi kushindana na agizo la Mungu na kukusudia kwenda…kumbe njiani wakati anakwenda Bwana alikuwa ameshamkusudia mauti! Bwana alikuwa amemwandaa tayari malaika wake kumwangamiza…kama sio Punda kuzungumza naye, habari ya Balaamu leo isingekuwepo kwenye biblia.

Na hata leo, kuna watu pia wanashindana na kusudi la Mungu, Bwana anasema hivi? Wao wanasema hivi na kuwafundisha watu upotofu na hali wanajua kabisa wanachokifanya sio sahihi….huko ni kushindana na agizo la Mungu, ni kupiga mateke mchokoo hivyo utajiumiza mwenyewe? Usijaribu kushindana na kusudi la Mungu kwa namna yoyote ile, ni kujihatarishia Maisha..Unaona mahali injili inahubiriwa unakwenda kusumbua au kuvuruga, au kuweka kikwazo chochote isiendelee mbele, kwasababu tu ya hasira zako binafsi, au chuki zako au wivu wako…usifanye hivyo tena…

Unapojaribu kudhoofisha kazi ya Mungu kwa namna yoyote ile ni kupiga mateke mchokoo..ni kujitafutia shari badala ya heri..kwajinsi unavyoiharibu, ule uharibifu ni kama mkuki kwako, unapenya kwenye maisha yako kwa nguvu ile ile utakayoitumia kuharibu kazi ya Mungu…kama vile mchokoo unavyopenya kwenye nyama ya ng’ombe… Paulo na Balaamu walipata Neema tu! Ya kuonyeshwa hatari waliyokuwa wanaiendea mbeleni lakini inaweza isiwe hivyo kwetu (mimi na wewe)… Usiingilie kabisa kazi za Mungu kwa ubaya kwa namna yoyote ile..utakuwa unashindana na Mungu mwenyewe na si mwanadamu..KAA CHONJO!

Ubarikiwe sana.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Print this post

ROHO YA ELIYA KATIKA AGANO JIPYA INATENDAJE KAZI?.

Jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima. Leo tutajifunza juu ya utendaji kazi wa roho ya Eliya ulivyokuwa katika agano la kale na jinsi unavyotenda kazi sasa katika agano jipya. Watu wengi wanachanganyikiwa sana hapa hususani katika hichi kipindi tunachoishi sasa ambacho jopo kubwa la manabii wengi wa ukweli na wa uongo limenyanyuka, na wengi wao wakijiitaa majina kama haya Eliya, wengine Musa, wengine Manabii wakuu n.k..Hivyo ni vizuri pia tukagusia jambo hili ili tujue ni wapi tunapaswa tusimamie.

Sasa tukirudi kwenye maandiko, ili tujifunze kidogo huduma ya Eliya ilikuwaje itatusaidia kupata picha halisi ya sasa inavyopaswa iwe,.Kumbuka Eliya alinyanyuka wakati maovu yapo katika kilele chake ndani ya Taifa la Israeli kipindi cha utawala wa mwabudu-sanamu mfalme Ahabu aliyechochewa na mke wake mchawi aliyeitwa Yezebeli, Ilifikia hatua mbaya sana kiasi kwamba ndani ya Taifa la Yahweh(Israeli), kulikuwa hakuna nabii wa Mungu aliyetembea hadharani, ilikuwa akikutwa, jambo ni moja tu, Kifo!. Hivyo wengi wao walijificha mapangoni, jambo ambalo lilimchukiza Mungu sana, na bila shaka kama Mungu asingemnyanyua mtu kama Eliya basi Taifa ile lingeangamizwa lote.

Lakini Mungu kwasababu anayo makusudi na Israeli akamteua mtu huyu, akamtia mafuta, ili aende kutimiza kusudi lake juu ya wana wa Israeli, na kusudi lenyewe lilikuwa NI “KUWAGEUZA MIOYO YAO IMRUDIE MUNGU” Ndipo tunaona Mungu akamjalia Eliya uweza mwingi sana uambatane na huduma yake, ili watu waamini, kama vile tunavyosoma wakati ule alipoposhusha moto alisema maneno haya:

1Wafalme 18:37 “Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, NA YA KUWA WEWE UMEWAGEUZA MOYO WAKURUDIE.

38 Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji.”

Unaona, Eliya hakushusha moto ili kuufurahisha umma au kuwakomoa manabii wa baali hapana! Bali alifanya vile ili wana wa Israeli ambao hawakuwahi kuona Mungu akifanya miujiza mubashara kama alivyofanya Misri waone na pale pale waamini kuwa kweli Mungu anaishi, hivyo wageuke!…Ndio maana baada ya tukio hilo unaona Israeli wote wanaanguka na Kusema “ 1 Wafalme 18:39.. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.” Hapo Tayari mioyo yao imeshageuzwa!

lakini Sasa Eliya alipoondoka alikuja Elisha, ambaye tunaona alioomba kwa Eliya sehemu ya mara dufu ya roho yake ije juu yake. Hapa hakusema naomba uje mara mbili juu yangu..Hapana..anasema:

2Wafalme 2:9 “……..Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu.”

Ikimaanisha kuwa aliomba yale mafuta Eliya aliyotiwa na Mungu, yashuke juu yake mara mbili zaidi..na sio Eliya aingie ndani yake mara mbili hapana! Bali yale mafuta yaliyo juu ya Eliya yawe juu yake mara mbili Zaidi….Ili atimize kusudi lile lile la kuwapatanisha wana wa Israeli, wamrudie Mungu wao Yehova. Elisha naye alipomaliza huduma yake ya kuwapatanisha wana wa Israeli, tunaona ikapita miaka mingi kidogo

Mpaka kufikia kipindi cha Nabii Malaki, ambaye alikuwa ni nabii wa mwisho aliyeandika agano la kale, Yehova akawapa tena ahadi ya Eliya kuja kabla ya kuja ile siku ya Bwana, na iliyo kuu na kuogofya.

Malaki 4:5 “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya.

6 Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.”

Sasa kama tulivyosema anaposema nitawapelekea Eliya nabii hamaanishi, Eliya atakuja tena kwa mara nyingine duniani na kufanya kazi kama alizokuwa anafanya zamani, hapana, Mungu mara nyingi anatumia majina ya watu au vitu, ili kuwasilisha dhima ya ujumbe wake ipasavyo, ili ieleweke, kwamfano biblia inaposema “wanao Musa na manabii”(Luka 16:29) haimaanishi kuwa Ni Musa kweli yupo hapo, hapana bali inamaanisha “wanayo torati ya Musa, na Maneno ya manabii”..Vivyo hivyo hapa inaposema nitawapelekea Eliya nabii, haimaanishi Eliya atashuka aje duniani, hapana! Bali anamanisha Roho, au huduma ya Eliya nabii atairejesha tena duniani kabla ya huo wakati aliousema kufika.

Ndipo sasa, tunapoingia katika agano jipya, tabia na muundo wa Roho ile inabadilika,na Agano lenyewe lilivyo. Ndiposa tunamwona Eliya wa kwanza aliyeletwa na Mungu kwetu alikuwa ni Yohana mbatizaji, yeye alikuwa anafanyakazi ya kuieguza mioyo ya watu imwelekee mwokozi, yaani wayahudi wamwangilie Huyo anayekuja yaani YESU KRISTO MFALME wa ULIMWENGU.

Yohana hakuwa na huduma nyingine zaidi ya hiyo, mpaka siku anakufa mafundisho yake yalikuwa ni kumshuhudia YESU tu, alikuwa hana habari ya kutaka kujijua yeye ni nani, wala watu wanasema nini kuhusu yeye.. Ile Roho iliyokuja juu yake ilikuwa na kazi moja tu ya kuwahimiza watu wamwangilie mwokozi wa ulimwengu kwasababu yeye ndiye kila kitu kwasasa. Na ndio mwisho wa yote…Baada yake hakuna Nabii wala mtume, wala mwalimu, atakayekuja kuwaokoa watu, na yeye ndio mfalme wa milele…

Sasa Yohana alikuwa anafungua au tunaweza kusema alikuwa anatoa mwongozo, au alikuwa anatoa taswira ya jinsi Roho hii ya Eliya itakavyokuwa inatenda kazi kwa kipindi chote cha agano jipya…Na hivyo haikuishia kwake.

Bali iliendelea na kuendelea na kuendelea kwa kila nyakati ya kanisa. Ilitoka kwa Yohana mbatizaji, ikaingia kwa mitume wa YESU KRISTO, ikatoka kwa mitume wa Yesu ikaingia kwa Mtume Paulo ndio maana wote hawa hawakuwa na habari ya kujisifia au kujieleza wao ni akina nani, au vyeo vyao, bali habari yao ilikuwa ni moja tu, kumshuhudia YESU KRISTO ambaye ndio mwanzo na mwisho wa kila kitu(Alfa na Omega).…Kuigeuza mioyo ya watu wasiomjua Yesu, imrudie yeye (Matendo 26:16-18)..Kwamba yeye ndio aliyekuwa anangojewa kumaliza kila kitu, hakuna mwingine wala hatakaa awepo mwingine, yeye ndio mwokozi, na ni Mungu, na ni tegemeo pekee la watu wote duniani, yeyote atakayemfuata huyo hatapotea..

Hivyo na watu wote waliofuata ambao walikuwa waaminifu kumshuhudia Kristo na sio kitu kingine chochote katika siku zao zote za huduma yao, ile Roho ya Eliya ilikuwa juu yao, hiyo ni aidha wajue au wasijue, aidha Mungu awaambie au asiwaambie, Roho ile ya Eliya ilikuwa inatenda kazi juu yao. Na hata sasa inatenda kazi.

Hivyo nataka nikuambie usitishwe na mtu yeyote kujiita jina lolote analolijua yeye, ajiite Eliya, ajiite Musa, ajiite Paulo, ajiite kuhani, n.k. hayo yote yasikusumbue ni majina tu, lakini tazama je! Ushuhuda anaoubeba ni ushuhuda wa namna gani?..Je! ni kuigeuza mioyo ya watu imwelekee KRISTO au iwaelekee wao wenyewe?, kama ni Kristo basi huyo ni ana roho ya Eliya kweli, lakini cha kusikitisha ni kuwa wengi wa hawa watu wanaojiita majina haya (japo si wote) malengo yao ni kuwavuta watu wawatazame wao, au kama si hivyo, ni ili watu wawaone kuwa wanaupako wa manabii, na hivyo wanafanyika kuwa ni manabii wa uongo kwasababu ushuhuda wanaoubeba ni ushuhuda wa uongo. Kwasababu biblia inasema “Ushuhuda wa Yesu ndio Roho ya Unabii soma Ufunuo 19:10” hivyo mtu yeyote asiyemshuhudia Yesu badala yake anajishuhudia yeye au anamshuhudia mtu mwingine, ni Dhahiri kuwa yeye huyo ni Nabii wa uongo kulingana na maandiko.

1 Yohana 5:9 “….Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa Mungu ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe”.

Kama maneno mawili unamtaja Kristo, halafu maneno kumi yanakuelekea wewe utaachaje kuwa Nabii wa uongo…Katika Biblia yote huwezi kuona mahali popote Nabii Eliya kajizungumzia yeye hata kidogo, au kajisifia, kwanza hata miaka yake haijarekodiwa pale, wala familia yake, wala ndugu zake, wala mali zake, yeye alikuwa na kazi moja tu! Kumhubiri Mungu wa Israeli na Kuigeuza mioyo ya wana wa Israeli imgeukie wao basi!.

Kwa kumalizia tu, ni kwamba HATUNA NABII mwingine zaidi ya BWANA YESU KRISTO, wala HATUNA MWALIMU mwingine zadi ya YESU KRISTO, Wala hatuna MCHUNGAJI mwingine Zaidi ya YESU KRISTO, wengine wote tunaojiita ni manabii, au waalimu, au wachungaji, ni tunamhakisi tu yeye! Huyo ndio Mungu aliyemtia mafuta, Nabii wa kwanza na wa mwisho, mwalimu wa kwanza na wa mwisho, mchungaji wa kwanza na wa mwisho, kwahiyo wote tunapaswa tuelekeze “vidole vya mahubiri yetu kwake”, mtu yeyote anayedai kafunuliwa, au ni mtume au mchungaji, au anayo roho ya unabii, halafu anahubiri injili isiyomshuhudia Yesu Kristo, huyo ni NABII WA UONGO! Hivyo tu!

Yesu Kristo ndiye Mkuu wa Uzima, hivyo kama hujamkabidhi Maisha yako, ni vizuri ukafanya hivyo leo, maadamu mlango wa Neema upo, itafika kipindi utafungwa na utatamani kuingia usiweze, hivyo tubu leo, ukabatizwe katika jina lake, kwa ajili ya ondoleo la dhambi zake naye atakufanya kuwa kiumbe kipya.

Ubarikiwe sana.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


NABII ELIYA NI NANI?

YEZEBELI NI NANI?

NINI MAANA YA HILI ANDIKO “USHUHUDA WA YESU NDIO ROHO YA UNABII” (UFUNUO 19:10)?

TABIA YA WAZI INAYOWATOFAUTISHA MANABII WA UONGO NA WALE WA UKWELI.


Rudi Nyumbani

Print this post

AGIZO LA UTUME.

Utukufu na heshima una Bwana wetu Yesu Kristo, milele na milele…

Karibu tutafakari pamoja Neno la Mungu, naamini kuna kitu cha kipekee Bwana alichotuandalia mezani pake siku ya leo.

Kwa ufupi sana leo tutajifunza juu ya “Agizo la Utume, Paulo alilopewa na Bwana Yesu Kristo mwenyewe”.

Kama wengi wetu tunavyojua kuwa sehemu ya kwanza ambayo inamwelezea Paulo jinsi alivyotokewa na Bwana njiani haikueleza kwa mapana na marefu ni maneno gani aliyoambiwa na Bwana Yesu, inaishia kusema tu! Simama uingie mjini utaambiwa yakupasayo kufanya…tusome.

Matendo 9:3 “Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni.

4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi?

5 Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.

6 Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.

7 Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu.

8 Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski.

9 Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi”.

Kama tunavyosoma haielezei kwa mapana, Bwana alimwambia nini Paulo kuhusu kusudi la kumtokea…lakini tukizidi kukisoma kitabu hichi cha Matendo ya mitume, karibia na sura za mwisho mwisho tunaweza kuona ujumbe Bwana aliompa Paulo siku ile alipomtokea njiani…

Matendo 26:13 “….ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote.

14 Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo.

15 Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi.

16 Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako;

17 nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao;

18 uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi”.

Unaona katika habari hiyo Mungu alimwambia Paulo mambo makuu manne.

1) Uwafumbue watu macho yao.

2) Awageuze waiache giza na kuielekea nuru.

3) Waziache na nguvu za shetani na kumwelekea Mungu.

4) Kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.

Hakuna sehemu hapo Bwana anamwagiza Paulo, akawafanye watu wawe washirika wa kanisa lake..au akawafanye watu wawe wa kuombewa tu! Au awahubirie Utajiri na mafanikio..bali unaona anaambiwa akawafumbue watu macho…Kufumbuliwa macho maana yake kuonyeshwa ni kitu gani kipo mbele yako huko unakokwenda usichokijua! Na kitu gani kilikuwepo huko unakotoka usichokijua, Na ni kitu gani kipo hapo ulipo usichokijua….Ndio maana alizungumza maneno haya katika moja ya nyaraka zake.

Pili aliambiwa awafundishe watu waiache giza waigeukie Nuru, kuacha giza maana yake ni kuacha matendo yote ya giza, kama uasherati, ulevi, wizi, uongo, uchawi, n.k. Alisema maneno haya mahali Fulani…

Waefeso 5:6 “Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi.

7 Basi msishirikiane nao.

8 Kwa maana zamani ninyi MLIKUWA GIZA, BALI SASA MMEKUWA NURU KATIKA BWANA; enendeni kama watoto wa nuru,

9 kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli;

10 mkihakiki ni nini impendezayo Bwana.

11 Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee;”

Tatu aliagizwa awageuze watu waziache nguvu za shetani na kumgeukia Mungu: zingatia hilo Neno ‘waziache’ sio wakaombewe! Wengi sasahivi wanatafuta kwenda kuombewa waache uasherati, au uchawi, au wizi, utasikia mtu anakuambia niombee niacha uasherati!…Ndugu hivyo vitu haviwezi kuondoka kwa kuombewa peke yake kama wewe mwenyewe kutoka moyoni mwako hujakusudia kuviacha…hata uombeweje haviwezi kuondoka kama hujakata shauri..Maana ya kutubu ni kuacha kile ulichokuwa unakifanya hapo kabla…sio tu kuomba msamaha peke yake! Hapana msamaha lazima uambatane na vitendo. Unapotubia uasherati maana yake unaachana na huyo mtu unayetembea naye sasa ambaye si mke wako au mume wako, unaachana na utazamaji wa pornography, na ufanyaji wa masturbation, unakwenda kuchoma nguo zote zi kiasherati, na mambo yote yanayohusiana na uasherati, kadhalika na uchawi ni hivyo hivyo unachoma nyenzo zote za kichawi na unaacha kabisa na hayo mambo…hiyo ndio maana ya kutubu!

Mithali 28:13 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye NA KUZIACHA atapata rehema”.

Na mwisho anaambiwa kisha wapate msamaha wa dhambi na kuwa urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa Imani iliyo kwake yeye Yesu Kristo..Msamaha wa dhambi ni matokea ya mambo yote hayo hapo juu, kufumbuliwa macho, kutubu na kuachana na dhambi pamoja na nguvu za giza.

Katika Nyaraka zote Mtume Paulo alizoandika utaona zote zimetimiza hivyo vipengele muhimu hapo juu…Ndio maana Bwana akazitukuza nyaraka za Mtume Paulo Zaidi ya za wengi, na kuzifanya kuwa msingi kwa vizazi vyote, kwasababu zimehubiri lile lile kusudi Bwana alilolitaka lifike kwa watu wake, na ndio maana zinatufaa mpaka sisi sasahivi.

Hivyo ndugu…Kristo anataka kuyaona hayo hayo mambo yakijidhihirisha katika Maisha yetu..kwamba macho yetu yafumbuke, tuone tuliko toka, tulipo sasa na tunakokwenda…2) tuigeukie Nuru 3) Tuziache nguvu za shetani tumgeukie yeye na 4) Tupate msamaha wa dhambi na kuwa miongoni mwa waliotakaswa kwa Imani. Hayo mambo ndiyo anayohitaji kutaka kwetu!.

Swali ni Je! Umeyapata hayo ndani yako? Je umeigeukia nuru? Je! Umeziacha nguvu za shetani? Je! Umepata msamaha wa dhambi zako kwa kutubu na kubatizwa ubatizo sahihi?. Kama sivyo, wakati ndio huu wa kurekebisha kile ambacho hakijakaa sawa ndani yako, katika wakati huu mchache uliobaki kabla ya unyakuo.

Bwana akubariki.

Pia kwa Maswali, Ushauri, Maombezi au Ratiba za Ibada Wasiliana kwa namba hizi

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

UMEFUNGWA KATIKA GIZA NA UVULI WA MAUTI?

IKO NJIA IONEKANAYO KUWA SAWA MACHONI PA MTU.

 DHAMBI ZINAZOTANGULIA NA ZINAZOFUATA.


Rudi Nyumbani

Print this post

JE! UKRISTO UNAMPA MTU DHAMANA YA KUWA TAJIRI?

Jina la mwokozi wetu Yesu Kristo litukuzwe daima, Natumaini Mungu amekupa neema ya kuiona siku ya leo, hata mimi pia, hivyo ni vizuri wote tukashiriki neema hizi pia tukamshukuru kwa kujifunza Neno lake.

Watu wengi sana hususani kwa wakati huu tunaoishi wanafahamu au wanafundishwa kuwa Ukija kwa Kristo ni lazima uwe tajiri, Ibrahimu alibarikiwa, Isaka alibarikiwa, Yakobo alibarikiwa, Daudi alibarikiwa Sulemani alibarikiwa kwanini na wewe usibarikiwe ikiwa ni mzao wa Ibrahimu kweli kweli. Hivyo hiyo imekuwa chachu ya kuwavuta watu wengi sana waujaribu ukristo,, lakini kwa bahati mbaya pengine kinapopita kipindi Fulani kirefu, na hawaona mabadaliko waliyokuwa wanayatazamia kwa Mungu pengine baada ya kuombewa sana, na kufarijiwa sana, wanaanza kurudi nyuma au wengine wanaishia kuuacha wokovu moja kwa moja..Wengine wanaanza kumnung’unikia Mungu, mbona hivi, mbona vile, mbona hujibu maombi yangu?,

Wengine wanaanza kuwanyooshea watu vidole Yule kachukua nyota yangu, Yule kaniloga, Yule ananiendea kila siku kwa waganga n.k..Utagundua pia maombi ya mtu wa namna hiyo sikuzote yanakuwa ni ya vita kupigana na watu asiowajua, wokovu wake unakua ni mgumu sana, kila siku anaangalia chanzo cha tatizo ni wapi, leo hii atasema pengine ni huu mti niliopanda hapa nyumbani kwangu ndio unaozuia Baraka zangu, ataenda kuukata na asipoona mabadiliko kesho yake atasema labda ni hili jina nililopewa na mababu zangu ndio chanzo cha matatizo yangu yote, ataenda kufanyiwa maombi ya deliverance, akiona tatizo bado lipo, kesho kutwa atasikia mahali Fulani wanasema watu waliozaliwa usiku huwa wanavita kubwa sana ya rohoni, akiangalia yeye alizaliwa saa 7 usiku, hivyo ataenda kujaribu na huko aombewe, akiona bado tatizo linaendelea, atasikia tena mahali pengine wanasema hupati pesa kwasababu huinenei sadaka yako, ataanza kuzinenea sadaka zake zote, atakaa muda Fulani aone kama kuna mabadiliko akiona hakuna chochote atakimbilia pengine ataambiwa toa sadaka ya ukombozi, ni kwasababu hujakomboa kiwanja chako na biashara yako na ndio maana hupati wateja wengi, atafanya hivyo tena, huko kote haoni matokeo yoyote..ataaenda pengine ataambiwa weka chumvi hii na maji haya ya upako kwenye biashara yako…na kadhalika na kadhalika, maisha yake ya ukristo yanakuwa ndio hayo kila siku, ukihesabu nguvu na fedha aliyoitaabikia kutafuta msaada wa mafanikio yake hailingani na kile alichokipata.

Kaka/dada tumekuwa tukiuona ukristo kuwa ni mgumu namna hii kwasababu wakati tunauingia hatukujua ukristo hasaa msingi wake umejengwa wapi na unamuhitaji mtu awe ni wa namna gani..Tumejikuta tunauingia tu ili tukatimiziwe matakwa yetu, na ndio huko tunakutana na ugumu mwingi ambao huo umekuja kwa kukosa kwetu maarifa. Tukumbuke kuwa Agano la kale ni tofauti na Agano jipya, agano lile lilikuwa ni kivuli cha mambo yatakayoendelea rohoni katika agano jipya, Mungu alimwahidia Ibrahimu na uzao wake Urithi huu wa hapa duniani, atambarikia hapa, Agano la Ibrahimu na Mungu lilikuwa ni la hapa hapa duniani, hivyo hatushangai kuona Mungu akiwabariki Waisraeli kwa vitu vyote vya kidunia, lakini sisi tulio wakristo, hatujapewa nchi ya kurithi hapa duniani, Urithi wetu na wenyeji wetu upo mbinguni(Wafilipi 3:20), hivyo Baraka zetu hasaa ni Baraka za kimbinguni, kwasababu huko ndio utajiri wetu wote ulipo na ndio mahali ambapo hata Bwana Yesu mwenyewe alituambia tujiwekee hazina huko mahali ambapo wezi hawawezi kufika wala kuharibiwa na kutu.(Luka 12:33-34).

Hiyo yote ni kuonyesha kuwa ukristo unaoletwa na Bwana wetu YESU KRISTO, hautoi kipaumbele cha utajiri wa ulimwengu huu.. (sisemi kuwa anataka tuwe maskini hapana), lakini hiyo ni kuonyesha kuwa kiwango chako cha utajiri au umaskini hakihusiani kwa vyovyote na ufalme wa mbinguni. Na hivyo kila mtu aliye mkristo anapaswa ajifunze kuridhika katika hali ile aliyopo maadamu maisha yake kila siku yanaimarika kwa Kristo, Biblia imesema hivyo. Tukiwa na Chakula na nguo, tu basi hiyo inatutosha kusonga mbele na ukristo wetu, na kusitawi kabisa mbele za Kristo Yesu.

(1Timotheo 6:8 ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo.).

Lakini watu wakristo wanaomfuata Kristo kwa namna moja au nyingine kwa lengo la kutajirika au kupata mali tazama wengi wao wanaishia katika upotevu, na hawadumu katika wokovu kwanza wanakuwa hawapendi kusikia habari za ufalme wa mbinguni, hata watu wanaohubiri hizo habari huwa wanawachukia, na saa nyingine kuwabeza, kwasababu hazina zao tayari walishaziweka katika mambo ya ulimwengu huu. Na bado wanajiita wakristo, wanajifunza kukipenda kiganja cha Bwana Zaidi ya kumpenda Bwana mwenyewe.

Hata wakimwona mkristo Fulani ni maskini wanaujarisi kabisa kusema Yule hana Mungu, wanasahau kuwa kulikuwa na kanisa lenye wakristo maskini sana kupindukia, wala Mungu hakulipa utajiri wowote zaidi Mungu aliwaambia wawe waaminifu hata kufa nao watapewa taji la uzima. Lakini pamoja na umaskini wao mbele za Mungu walionekana matajiri, (Soma Ufunuo 2:8-11 “ Na kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika; Haya ndiyo aneneyo yeye aliye wa kwanza na wa mwisho, aliyekuwa amekufa, kisha akawa hai. 9 Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani.”) .

Vile vile kulikuwa na kanisa lililojiona kuwa ni tajiri sana halihitaji kitu chochote lakini mbele za Mungu lilionekana kuwa ni maskini kupindukia, tena ule umaskini wa kuwa uchi, na unyonge na upofu na kanisa hilo ndio hili tunaloishi mimi na wewe linaloitwa Laodikia(Soma Ufunuo 3:14-22 “… Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi….”).

Biblia inaweka wazi pia ni ngumu kwa tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni..

Marko 10:23 “Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!

24 Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu! 

25 Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.

Hivyo ikiwa wewe ni mkristo Mungu kakubariki kwa vingi au kwa vichache, jambo la msingi ni kujifunza kuridhika ukifahamu kuwa wenyeji wako upo mbinguni na kwamba utumie muda wako mwingi zaidi kujiwekea hazina kule mbinguni, kuliko hapa, Tukijizoesha hivyo hatutajikwaa mahali popote na huo ndio Ukristo wa kweli. Kiasi kwamba ifikie kipindi tuseme Bwana akitupa vingi ni sawa na asipotupa vingi pia ni sawa! Maadamu kasema hatatupungukia kabisa hiyo inatosha!

Waebrania 13:5 “ Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa”

Ubarikiwe sana.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

NJIA YA ‘UTAJIRI MKUU’ KWA KIJANA.

JE! UMEFUNDISHWA?

AYUBU 28 : HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?


Rudi Nyumbani

 

 

Print this post

MPENDEZE MUNGU ZAIDI.


Biblia inasema katikaWaefeso 5:9 “kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; 10 MKIHAKIKI NI NINI IMPENDEZAYO BWANA”. Mstari wa 10 unatuambia, mkihakiki ni nini impendezayo Bwana…Kwahiyo ni wajibu wetu, kuchunguza na kuhakiki ni mambo gani yanayompendeza Bwana zaidi.. Na leo tutajifunza moja ya jambo linalompendeza Bwana zaidi.

Katika habari ifuatayo tunaweza kujifunza jambo hilo kwa undani…tusome:

Luka 8:22 “Ikawa siku zile mojawapo alipanda chomboni yeye na wanafunzi wake, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo ya ziwa. Wakatweka matanga.

23 Nao walipokuwa wakienda, alilala usingizi. Ikashuka tufani juu ya ziwa, chombo kikaanza kujaa maji, wakawa katika hatari.

24 Wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana mkubwa, Bwana mkubwa, tunaangamia. Akaamka, akaukemea upepo na msukosuko wa maji, vikakoma; kukawa shwari.

25 Akawaambia, Imani yenu iko wapi? Wakaogopa, wakamaka, wakisema wao kwa wao, Ni nani huyu basi hata anaamuru upepo na maji, navyo vyamtii?”

Hapa tunaona, Bwana Yesu alikuwa anavuka kwenda ng’ambo ya pili, akiwa na wanafunzi wake, lakini njiani, alilala na hali ikabadilika..shetani akawatikisa kidogo..

Katika haya Maisha pia, tupo safarini, na safari ni safari tu inaweza kuwa ya nchi kavu, majini au angani…ilimradi inakutoa sehemu moja hadi nyingine, na katikati ya safari ni kawaida kukutana na vikwazo mbali mbali na changamoto mbali mbali…Na Maisha tunayoishi ndio hivyo, Safari ya mtu aliyemkabidhi Kristo Maisha yake, ni tofauti na ya mtu ambaye hajampa Kristo maisha yake. Safari ya aliyeokoka anakuwa anasafiri na Bwana Yesu, na atatafutwa na Adui kila kona, lakini yule ambaye hajampa Kristo Maisha yake anakuwa anasafiri peke yake na roho za mashetani.

Lakini katika safari hii, tunaona Bwana Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wanasafiri kihuduma, kwenda kuvua roho za watu upande wa pili..jambo ambalo shetani haliwezi kumpendeza hata kidogo…kwani muda mfupi tu baadaye, mtu mwenye mapepo mengi kama jeshi atakwenda kufunguliwa na kwa kupitia kufunguliwa kwake maelfu ya watu watatubu na kumgeukia Mungu, hivyo jambo hilo lisingemfurahisha shetani hata kidogo, kwahiyo suluhisho la haraka ni kuwaletea kikwazo safarini, ni kikwazo pekee baharini ni kuleta tufani.

Lakini tunaona wanafunzi walipoona ile tufani jinsi ilivyo kubwa, waliogopa mpaka kufikia hatua ya kukata tamaa, mpaka chombo kikaanza kujaa maji..na Bwana Yesu akiwa ndani humo humo…Walipoona hali imezidi kuwa mbaya ndipo wakaenda kumwamsha Bwana kuomba msaada na Bwana akawasaidia, kwa kuukemea ule upepo, na muda ule ule ukatulia.

Lakini tunajifunza Bwana hakufurahishwa sana na kile kitendo cha wao kukosa Imani, kwa ufupi wangepaswa tu kuamini kuwa wasingezama kwa namna yoyote ile na hivyo dhoruma itaisha kwa namna yoyote ile…lakini mpaka kufikia hatua ya kusema tunaangamia! Hiyo ni hatua ya mwisho ya kukata tamaa na kuliruhusu lile jambo litokee…kulikuwa hakuna haja ya kumwamsha Bwana walipaswa tu waamini kuwa hata iweje hawawezi kufa, kwani BWANA MKUBWA yupo nao ndani hata kama wasingeukemea ule upepo kitendo cha wao kuamini tu kuwa hawawezi kufa hiyo ilikuwa ni Imani tosha! Ya kuikatisha ile dhoruba!

Na sisi katika safari yetu kuna wakati Kristo analala, sio kwamba hayupo na sisi au katuacha hapana! Bali anakuwa amelala…shetani anapoleta misuko suko ya huku na kule, sio wakati wakuogopa na kupaniki ni wakati wa kuamini kuwa mambo yote yatakuwa shwari kwakuwa tunaye YESU moyoni mwetu…hata kama hanijibu kwa sasa, lakini chombo changu hakiwezi kuzama…Chombo cha wakina Petro kingewezaje kuzama na Kristo akiwa ndani?…unaweza kutengeneza picha Bwana Yesu anakufa maji?…au anajiokoa yeye peke yake na kuacha wanafunzi wake wafe maji?..unaona jambo hilo haliwezekani…Ni kitendo cha kuamini tu kuwa maadamu Yesu yupo ndani, awe macho au amelalala mambo yote sawasawa….tunaye Yesu moyoni mwetu hivyo ni shwari kuu…hata kama nje tunaona dhoruba, ni inapita tu!…

Lakini kwasababu Bwana Yesu ni msaada kwetu kwa hali zote, hata katika udhaifu wetu anatusaidia mwisho wa siku, ndio maana unaona japokuwa wanafunzi walikuwa wamepoteza tumaini la Maisha lakini Yesu aliwasaidia pia, akaukemea upepo kwa niaba yao lakini sio kwamba alipendezwa nao sana kwa kitendo hicho.…Kadhalika watu wengi leo Kristo anawasaidia kwa njia hiyo hiyo, inatokea mtu anapitia tatizo kidogo tu! Utaanza kuona anavyolalamika? Nakufa! Nakufa Mungu wangu! Nimekwisha mimi… Mungu hunisikii?..Ni kweli kwa kelele hizo utapata msaada! Lakini utakuwa hujampendeza Mungu…utakufaje na yeye yupo na wewe chomboni? Mapenzi ya Mungu ni haya kwamba ukiwa naye hakuna lolote litakalokutokea kwa madhara maadamu unaye Mungu..Maadamu unauhakika upo naye sawa…

Na maana ya kuwa na Kristo chomboni ni “kuwa na Kristo moyoni mwako kwa kuzishika amri zake na kuishi Maisha ya utakatifu”..hapo tufani inapokuja hauhitaji kumwamsha itaisha yenyewe…na utakuwa umempendeza Zaidi. Hutakuwa tatizo kidogo tu likitokea unapaniki, au unakata tamaa, au unatoa hitimisho kuwa utakufa!..Bwana atakuuliza Imani yako iko wapi?.

Bwana Yupo na wewe, wewe uliyeamua kumfuata hivyo usiogope mabaya yatakapokuja!..Bwana yupo na wewe, wewe uliyeamua kuyakabidhi Maisha yako kwake, hawezi kukuacha uangamie, ingawa dhoruba zitakuja hata ukiwa naye…lakini usiogope! Hakuna lolote litakalokutokea..Unapokwenda kuhubiri kama Bwana alivyokwenda na wanafunzi wake dhoruba inapokuja usiogope Bwana yu pamoja nawe, usianze kufikia hitimisho kwamba umekufa! Au umekwisha! Usianze kabisa kufikiria hayo mambo, ukianza kufikiria hivyo shetani atakupepeta kweli kweli…yeye mwenyewe alisema kuwa atakuwa pamoja nasi mpaka Ukamilifu wa Dahari. Sasa hawezi kutudanganya, maneno yake siku zote ni ya ukweli.

Wana wa Israeli Bwana alipowatoa Misri na kuwapeleka kwenye lile jangwa, lisilo na maji wala chakula, walipopitia njaa kidogo tu! Siku mbili tatu wakaanza kunung’unika..kwamba wapo katikati ya jangwa watatolea wapi chakula na maji?..Sasa unaweza kuwaza Mungu atakutoaje mahali penye chakula na akupeleka jangwani halafu asijue namna ya kukulisha kule jangwani?..kwahiyo walipoona kumekuwa kimya kidogo Mungu hazungumzi, wakaanza kupiga kelele tunaangamia! Tunaangamia! Ni kweli kwa kelele zile walipata nyama muda mfupi sana baadaye, pamoja na mana, wakala wakashiba lakini Mungu hakupendezwa nao…Walipaswa kujua tu! Maadamu wanaye Mungu, mambo yote yatakuwa sawasawa, Mungu hawezi kuwaacha wafe na njaa au wafe kwa kukosa maji!..Ni kitendo cha kutulia tu, muda mchache mbele wangekwenda kula mana na nyama za kutosha, na wangesahau kuwa walipitia njaa.

Bwana atusaidie, tuzidi kumpendeza yeye Zaidi na zaidi..na tuzidi kuyahikiki mambo gani yanayompendeza siku zote.

Ubarikiwe sana.

Pia kwa Maombezi/Ushauri/Maswali/Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba 

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


 

Mada Zinazoendana:

JIPE MOYO.

BWANA YESU ALIKUWA ANAONYESHA KUWA MUNGU NI MUNGU MWENYE AKILI TIMAMU.

UPONYAJI WA YESU.


Rudi Nyumbani

Print this post