Jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima. Leo tutajifunza juu ya utendaji kazi wa roho ya Eliya ulivyokuwa katika agano la kale na jinsi unavyotenda kazi sasa katika agano jipya. Watu wengi wanachanganyikiwa sana hapa hususani katika hichi kipindi tunachoishi sasa ambacho jopo kubwa la manabii wengi wa ukweli na wa uongo limenyanyuka, na wengi wao wakijiitaa majina kama haya Eliya, wengine Musa, wengine Manabii wakuu n.k..Hivyo ni vizuri pia tukagusia jambo hili ili tujue ni wapi tunapaswa tusimamie.
Sasa tukirudi kwenye maandiko, ili tujifunze kidogo huduma ya Eliya ilikuwaje itatusaidia kupata picha halisi ya sasa inavyopaswa iwe,.Kumbuka Eliya alinyanyuka wakati maovu yapo katika kilele chake ndani ya Taifa la Israeli kipindi cha utawala wa mwabudu-sanamu mfalme Ahabu aliyechochewa na mke wake mchawi aliyeitwa Yezebeli, Ilifikia hatua mbaya sana kiasi kwamba ndani ya Taifa la Yahweh(Israeli), kulikuwa hakuna nabii wa Mungu aliyetembea hadharani, ilikuwa akikutwa, jambo ni moja tu, Kifo!. Hivyo wengi wao walijificha mapangoni, jambo ambalo lilimchukiza Mungu sana, na bila shaka kama Mungu asingemnyanyua mtu kama Eliya basi Taifa ile lingeangamizwa lote.
Lakini Mungu kwasababu anayo makusudi na Israeli akamteua mtu huyu, akamtia mafuta, ili aende kutimiza kusudi lake juu ya wana wa Israeli, na kusudi lenyewe lilikuwa NI “KUWAGEUZA MIOYO YAO IMRUDIE MUNGU” Ndipo tunaona Mungu akamjalia Eliya uweza mwingi sana uambatane na huduma yake, ili watu waamini, kama vile tunavyosoma wakati ule alipoposhusha moto alisema maneno haya:
1Wafalme 18:37 “Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, NA YA KUWA WEWE UMEWAGEUZA MOYO WAKURUDIE. 38 Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji.”
1Wafalme 18:37 “Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, NA YA KUWA WEWE UMEWAGEUZA MOYO WAKURUDIE.
38 Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji.”
Unaona, Eliya hakushusha moto ili kuufurahisha umma au kuwakomoa manabii wa baali hapana! Bali alifanya vile ili wana wa Israeli ambao hawakuwahi kuona Mungu akifanya miujiza mubashara kama alivyofanya Misri waone na pale pale waamini kuwa kweli Mungu anaishi, hivyo wageuke!…Ndio maana baada ya tukio hilo unaona Israeli wote wanaanguka na Kusema “ 1 Wafalme 18:39.. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.” Hapo Tayari mioyo yao imeshageuzwa!
lakini Sasa Eliya alipoondoka alikuja Elisha, ambaye tunaona alioomba kwa Eliya sehemu ya mara dufu ya roho yake ije juu yake. Hapa hakusema naomba uje mara mbili juu yangu..Hapana..anasema:
2Wafalme 2:9 “……..Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu.”
Ikimaanisha kuwa aliomba yale mafuta Eliya aliyotiwa na Mungu, yashuke juu yake mara mbili zaidi..na sio Eliya aingie ndani yake mara mbili hapana! Bali yale mafuta yaliyo juu ya Eliya yawe juu yake mara mbili Zaidi….Ili atimize kusudi lile lile la kuwapatanisha wana wa Israeli, wamrudie Mungu wao Yehova. Elisha naye alipomaliza huduma yake ya kuwapatanisha wana wa Israeli, tunaona ikapita miaka mingi kidogo
Mpaka kufikia kipindi cha Nabii Malaki, ambaye alikuwa ni nabii wa mwisho aliyeandika agano la kale, Yehova akawapa tena ahadi ya Eliya kuja kabla ya kuja ile siku ya Bwana, na iliyo kuu na kuogofya.
Malaki 4:5 “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya. 6 Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.”
Malaki 4:5 “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya.
6 Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.”
Sasa kama tulivyosema anaposema nitawapelekea Eliya nabii hamaanishi, Eliya atakuja tena kwa mara nyingine duniani na kufanya kazi kama alizokuwa anafanya zamani, hapana, Mungu mara nyingi anatumia majina ya watu au vitu, ili kuwasilisha dhima ya ujumbe wake ipasavyo, ili ieleweke, kwamfano biblia inaposema “wanao Musa na manabii”(Luka 16:29) haimaanishi kuwa Ni Musa kweli yupo hapo, hapana bali inamaanisha “wanayo torati ya Musa, na Maneno ya manabii”..Vivyo hivyo hapa inaposema nitawapelekea Eliya nabii, haimaanishi Eliya atashuka aje duniani, hapana! Bali anamanisha Roho, au huduma ya Eliya nabii atairejesha tena duniani kabla ya huo wakati aliousema kufika.
Ndipo sasa, tunapoingia katika agano jipya, tabia na muundo wa Roho ile inabadilika,na Agano lenyewe lilivyo. Ndiposa tunamwona Eliya wa kwanza aliyeletwa na Mungu kwetu alikuwa ni Yohana mbatizaji, yeye alikuwa anafanyakazi ya kuieguza mioyo ya watu imwelekee mwokozi, yaani wayahudi wamwangilie Huyo anayekuja yaani YESU KRISTO MFALME wa ULIMWENGU.
Yohana hakuwa na huduma nyingine zaidi ya hiyo, mpaka siku anakufa mafundisho yake yalikuwa ni kumshuhudia YESU tu, alikuwa hana habari ya kutaka kujijua yeye ni nani, wala watu wanasema nini kuhusu yeye.. Ile Roho iliyokuja juu yake ilikuwa na kazi moja tu ya kuwahimiza watu wamwangilie mwokozi wa ulimwengu kwasababu yeye ndiye kila kitu kwasasa. Na ndio mwisho wa yote…Baada yake hakuna Nabii wala mtume, wala mwalimu, atakayekuja kuwaokoa watu, na yeye ndio mfalme wa milele…
Sasa Yohana alikuwa anafungua au tunaweza kusema alikuwa anatoa mwongozo, au alikuwa anatoa taswira ya jinsi Roho hii ya Eliya itakavyokuwa inatenda kazi kwa kipindi chote cha agano jipya…Na hivyo haikuishia kwake.
Bali iliendelea na kuendelea na kuendelea kwa kila nyakati ya kanisa. Ilitoka kwa Yohana mbatizaji, ikaingia kwa mitume wa YESU KRISTO, ikatoka kwa mitume wa Yesu ikaingia kwa Mtume Paulo ndio maana wote hawa hawakuwa na habari ya kujisifia au kujieleza wao ni akina nani, au vyeo vyao, bali habari yao ilikuwa ni moja tu, kumshuhudia YESU KRISTO ambaye ndio mwanzo na mwisho wa kila kitu(Alfa na Omega).…Kuigeuza mioyo ya watu wasiomjua Yesu, imrudie yeye (Matendo 26:16-18)..Kwamba yeye ndio aliyekuwa anangojewa kumaliza kila kitu, hakuna mwingine wala hatakaa awepo mwingine, yeye ndio mwokozi, na ni Mungu, na ni tegemeo pekee la watu wote duniani, yeyote atakayemfuata huyo hatapotea..
Hivyo na watu wote waliofuata ambao walikuwa waaminifu kumshuhudia Kristo na sio kitu kingine chochote katika siku zao zote za huduma yao, ile Roho ya Eliya ilikuwa juu yao, hiyo ni aidha wajue au wasijue, aidha Mungu awaambie au asiwaambie, Roho ile ya Eliya ilikuwa inatenda kazi juu yao. Na hata sasa inatenda kazi.
Hivyo nataka nikuambie usitishwe na mtu yeyote kujiita jina lolote analolijua yeye, ajiite Eliya, ajiite Musa, ajiite Paulo, ajiite kuhani, n.k. hayo yote yasikusumbue ni majina tu, lakini tazama je! Ushuhuda anaoubeba ni ushuhuda wa namna gani?..Je! ni kuigeuza mioyo ya watu imwelekee KRISTO au iwaelekee wao wenyewe?, kama ni Kristo basi huyo ni ana roho ya Eliya kweli, lakini cha kusikitisha ni kuwa wengi wa hawa watu wanaojiita majina haya (japo si wote) malengo yao ni kuwavuta watu wawatazame wao, au kama si hivyo, ni ili watu wawaone kuwa wanaupako wa manabii, na hivyo wanafanyika kuwa ni manabii wa uongo kwasababu ushuhuda wanaoubeba ni ushuhuda wa uongo. Kwasababu biblia inasema “Ushuhuda wa Yesu ndio Roho ya Unabii soma Ufunuo 19:10” hivyo mtu yeyote asiyemshuhudia Yesu badala yake anajishuhudia yeye au anamshuhudia mtu mwingine, ni Dhahiri kuwa yeye huyo ni Nabii wa uongo kulingana na maandiko.
1 Yohana 5:9 “….Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa Mungu ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe”.
Kama maneno mawili unamtaja Kristo, halafu maneno kumi yanakuelekea wewe utaachaje kuwa Nabii wa uongo…Katika Biblia yote huwezi kuona mahali popote Nabii Eliya kajizungumzia yeye hata kidogo, au kajisifia, kwanza hata miaka yake haijarekodiwa pale, wala familia yake, wala ndugu zake, wala mali zake, yeye alikuwa na kazi moja tu! Kumhubiri Mungu wa Israeli na Kuigeuza mioyo ya wana wa Israeli imgeukie wao basi!.
Kwa kumalizia tu, ni kwamba HATUNA NABII mwingine zaidi ya BWANA YESU KRISTO, wala HATUNA MWALIMU mwingine zadi ya YESU KRISTO, Wala hatuna MCHUNGAJI mwingine Zaidi ya YESU KRISTO, wengine wote tunaojiita ni manabii, au waalimu, au wachungaji, ni tunamhakisi tu yeye! Huyo ndio Mungu aliyemtia mafuta, Nabii wa kwanza na wa mwisho, mwalimu wa kwanza na wa mwisho, mchungaji wa kwanza na wa mwisho, kwahiyo wote tunapaswa tuelekeze “vidole vya mahubiri yetu kwake”, mtu yeyote anayedai kafunuliwa, au ni mtume au mchungaji, au anayo roho ya unabii, halafu anahubiri injili isiyomshuhudia Yesu Kristo, huyo ni NABII WA UONGO! Hivyo tu!
Yesu Kristo ndiye Mkuu wa Uzima, hivyo kama hujamkabidhi Maisha yako, ni vizuri ukafanya hivyo leo, maadamu mlango wa Neema upo, itafika kipindi utafungwa na utatamani kuingia usiweze, hivyo tubu leo, ukabatizwe katika jina lake, kwa ajili ya ondoleo la dhambi zake naye atakufanya kuwa kiumbe kipya.
Ubarikiwe sana.
Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba
+225693036618/ +225789001312
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
NABII ELIYA NI NANI?
YEZEBELI NI NANI?
NINI MAANA YA HILI ANDIKO “USHUHUDA WA YESU NDIO ROHO YA UNABII” (UFUNUO 19:10)?
TABIA YA WAZI INAYOWATOFAUTISHA MANABII WA UONGO NA WALE WA UKWELI.
Rudi Nyumbani
Print this post
Amina
Karibu…