Udhihirisho wa Bwana Yesu kabla ya kufufuka, ulikuwa ni tofauti na baada ya kufufuka..Kabla ya kusulibiwa Bwana Yesu alikuwa anaonekana kila mahali na sehemu nyingi, hata watu waliotaka kumwona na kumfahamu, walikuwa wakimtafuta kwa bidii wanampata mahali popote..Alifanya huduma yake kwa wazi sana..Lakini haikuwa hivyo tena baada ya kufufuka kwake. Baada ya kufufuka kutoka katika wafu, hakuwa anajidhihirisha kwa kila mtu, isipokuwa kwa watu wachache sana, tena,sana sana wale wanafunzi wake…Wengine wote waliosalia ambao walikuwa hawafuatani naye wala hawajishughulishi na mambo yake, walibakia kuamini uongo kwamba Bwana hajafufuka ameibiwa na wanafunzi wake usiku, na kuzusha kwamba amefufuka.
Kwahiyo waliokuwa wana uhakika kwamba Bwana Yesu kafufuka kweli kweli ni wale wanafunzi wake tu, na ndugu zake Bwana pamoja na kikundi cha watu wachache sana waliokuwa wanafuatana naye, mamilioni ya watu waliokuwa pale Yerusalemu hawakujua chochote..Na siku ya unyakuo itakuwa hivyo hivyo watakaomwona Kristo mawinguni watakuwa wachache sana kati ya mabilioni ya watu wanaoishi duniani.
Wakati hata ule mti ambao ulimsulibishia Bwana haujaoza, Tayari Bwana alikuwa anazungumza na wanafunzi wake katika vyumba vya ndani vya siri. Wakati ambao bado watu walikuwa wanamwombolezea tayari yeye ameshawatokea wengi na kuzungumza nao.
Wakati Pilato, Herode,mafarisayo, masadukayo pamoja na wayahudi wamestarehe wakisheherekea na kudhani Bwana sasa ni marehemu, kumbe maili kadhaa tu hapo,si mbali na wao Bwana anawaaga wanafunzi wake na kuchukuliwa juu mbinguni..
Matendo 1: 4 “Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu;
5 ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache.
6 Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme?
7 Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.
8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.
9 Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao.
10 Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe,
11 wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.
12 Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato”.
Kwahiyo tunaweza tukaona kujidhihirisha kwa Bwana baada ya kufufuka kulikuwa ni kwa siri sana, sio wote waliokuwa wanajua kinachoendelea wakati ule.
Lakini jambo la kipekee tunaloweza kujifunza ni kwamba, Wakati Bwana anachukuliwa juu katika wingu..wale wanafunzi walikuwa wanamtazama kwa macho yao jinsi alivyokuwa anaondoka hatua kwa hatua..jinsi wingu lilivyomchukua mpaka kupotelea mawinguni…Lakini tunaona baada ya kudumu kwa muda mrefu wakiangalia mawinguni malaika wawili waliwatokea katikati yao na kuwahamisha akili zao wasibaki kuangalia mbinguni, kwa maana Kwa jinsi hiyo hiyo aliyoondokea ndio atakayorudia..hivyo waache kuangalia juu, wakaendelee na mambo mengine yanayohusiana na kuutangaza ufalme wa mbinguni..Mpaka wakati wa Bwana kurudi, wakawe mashahidi wa Yesu Kristo, wakiutangaza ufalme wa mbinguni kwa watu wengine.
Kwa wakati huo ulikuwa ndio ule wakati Bwana Yesu aliowaambia mafarisayo kwamba utafika wakati Bwana arusi ataondolewa na ndipo wanafunzi wake watafunga na kuomboleza.
Mathayo 9: 14 “Wakati ule wanafunzi wake Yohana wakamwendea, wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi?
15 Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga”.
Siku zote upo wakati ambao Bwana atatembea na Mtu, kama mtu na rafiki yake au mpenzi wake, na upo wakati ambao Bwana atatembea na mtu kama mtu na mtumwa wake..wakati huo Bwana ataondoka juu, na kukutuma kama mfanya kazi katika shamba lake.
Utakuwa ni wakati wa Bwana kugeuza hisia zako, na kukusukuma kwenda kuzaa matunda zaidi badala ya kukaa mwenyewe mwenyewe tu!..
Nakumbuka kipindi cha kwanza kwanza nampa Bwana maisha yangu, nilikuwa sitamani kitu kingine chochote zaidi ya kuondoka kwenye hii dunia na kwenda kwa Baba..Nilikuwa natamani leo Kristo arudi niondoke..(sio kwamba hata sasa bado sikitamani,nakitamani hicho kitu sana) na nilikuwa namwona Bwana akinifariji kwa namna ya kipekee kwa njia hiyo, nilikuwa naona maono, na ishara baadhi kuthibitisha njia hiyo..Lakini ilifika wakati mambo yalibadilika ndani…
Nilianza kuhisi kuna majukumu Fulani nayakwepa, Nilianza kusikia msukumo mwingine tofauti na ule wa kwanza, badala ya kukaa peke yangu na kujifunza tu Neno, na kusikiliza tu mahubiri na kusoma vitabu..huku nikitamani siku yoyote parapanda ilie niondoke…Nilianza kuhisi kuna umuhimu wa kwenda kusambaza habari za Yesu Kristo kwa watu wengine..Jambo hilo lilikuja ndani kwa nguvu sana kwa muda mrefu kidogo..mpaka ikafika wakati siku ikipita pasipo kufanya chochote katika kuisambaza kazi ya Mungu, nakosa amani, hata nguvu za mwili naona zinapungua kabisa..Kwahiyo nikahama kutoka kutazama tu mbinguni na kuanza kazi nyingine ya kuhubiri, ndio angalau unafuu ndani ya nafsi ukarudi.
Kwahiyo ikawa nikiona tu ndani amani imetoweka najua sehemu ya kwenda kuirudisha.. “ni kwenda kuwahubiria wengine habari njema”..amani inarudi kama kawaida na siku yangu inaenda vizuri, tofauti na hapo kwanza ambapo hata nisipofanya hivyo..nikisoma tu Neno na kusikiliza mahubiri na kusali basi Napata amani.
Nimetoa ushuhuda huu mfupi tu wa mimi binafsi kuonyesha kwamba kuna nyakati na majira, kuna wakati wa kukaa na Bwana arusi (Yesu Kristo) na kuna wakati wa Bwana arusi kuondolewa.. Waliooa au walioolewa wanafahamu kuwa kuna wakati wa mume na mke kukaa pamoja kwa raha na furaha, wakiwa wawili tu..na kuna wakati wa majukumu, wakati ambao watoto wamezaliwa wanahitajika kutunzwa, wakati huo upendo lazima ugawanyike kidogo, sehemu Fulani lazima uelekee katika kuwatunza watoto. Upendo unahamia kwa watoto.
Na katika Ukristo nako ni hivyo hivyo, upo wakati wa kufurahi na Bwana, kipindi cha mwanzo cha wokovu lakini pia upo wakati wa kwenda kuzaa matunda, kipindi ambacho Bwana arusi ataondolewa..wakati ambao unalazimika kujihusisha na watoto wa kiroho zaidi, kuliko kitu kingine zaidi…Kama ilivyokuwa kwa wanafunzi, walikaa na Bwana miaka mitatu na nusu kwa raha…na siku Bwana anaondoka walidhani wataendelea kutembea naye na kula naye kama hapo kwanza..walimwuliza Bwana huu ndio wakati wa kurejeshewa ufalme (Yaani wakati wa kutawala na Bwana wao kwa raha na furaha pasipo usumbufu)..Lakini Bwana aliwaambia huo ni wakati wa kupokea nguvu kuwa mashuhuda wake, na kupeleka injili duniani kote na kuleta mazao mengi katika ufalme wa mbinguni…huo sio wakati wa kustarehe tena, ni wakati wa kufunga,na kuombeleza, ni wakati wa kupambana vita.
Kwa kupitia ujumbe huu mfupi, naamini utakuwa umeongeza kitu katika vile Bwana alivyokujalia kuvijua, ni maombi yangu kuwa Bwana atakusaidia Katika hilo, utapofikia katika hiyo hatua au kama upo katika hiyo hatua Bwana akufanikishe sana na azidi kukutia nguvu katika kuifanya kazi yake.
Kama hujampa Bwana maisha yako, nakushauri ufanye hivyo leo, kabla mlango wa Neema haujafungwa, kwa Kristo atakuja na wala hatudanganyi..Yeye anatupenda ndio maana amejitoa maisha yake kwa ajili yako na yangu.Hivyo mgeukie leo ukatubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na yeye atakupokea kama alivyoahidi, na pia haraka tafuta mahali ukabatizwe ikiwa haukubatizwa ipasavyo, ili upate ondoleo la dhambi zako, na utakuwa na uhakika wa Uzima wa milele na kuiona Mbingu.
Bwana akubariki, Tafadhali “share” Ujumbe huu kwa wengine,
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
MUNGU KUSEMA NA WEWE PEKEE, HAITOSHI KUKUPA USHINDI.
NINI MAANA YA KUHUBIRI INJILI KWA KILA KIUMBE?
Siku hiyo itakuwa ni siku ya namna gani?, Siku hiyo ya watakatifu wote kunyakuliwa, siku hiyo ambayo itakuwa ni mwisho wa taabu zote kwa wana wa Mungu..Siku ambayo tutakutana na YESU uso kwa uso, siku ambayo Bwana atakapokwenda kuweka wazi mambo yake yote aliyokuwa ametuandalia tangu zamani , makao yetu ya milele, Biblia inasema ni mambo ambayo hata malaika watakatifu wanatamani kuyachulingulia wayaone yakoje..
Ni kama tu vile na sisi tulivyo na shauku ya kuona walau kwa uchache jinsi mbingu ilivyo, kwani tumekuwa tukiisikia uzuri wake usio wa kawaida tangu zamani jinsi ulivyo lakini tusiuone, Na kwa namna hiyo hiyo malaika nao sasa huko juu mbinguni, wanatamani kwa shauku kubwa walau waonjeshwe mambo walioandaliwa wateule wa Mungu na YESU KRISTO mwenyewe siku ile itakavyokuwa. Huko walipo Malaika watakatifu wanasikia tu! kuwa kuna utukufu mkubwa Bwana amewaandalia watakatifu wake, wanafahamu kuwa ni utukufu ulio mkuu sana usioneneka. lakini bado hawajauona ni wa namna gani, wanajua kuwa siku ya ukombozi wa watoto wa Mungu ni siku KUU sana, mambo yasiyoneneka wala kutamkika yatafunuliwa katika siku hizo, hivyo hiyo inawafanya wao nao waitamani siku hiyo ije kwa haraka wao nao wayashuhudie mambo hayo ya ajabu.
1Wakorintho 2:9 “Lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao”.
Na Sio malaika tu peke yao, hata viumbe vingine vyote vinaitamani hiyo siku ifike, Mtume Paulo anasema ..
Warumi 8:18 “Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama UTUKUFU ULE UTAKAOFUNULIWA KWETU.
19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia KWA SHAUKU NYINGI kufunuliwa kwa wana wa Mungu.
20 Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye atiyevitiisha katika tumaini;
21 kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu”.
Kwasasa hatuwezi kusema mengi kwasababu bado hatujafunuliwa mambo yenyewe lakini tunafahamu sifa moja ya Mungu KUWA YEYE HUWA HASEMI UONGO, na kama alivyosema “ kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu”..Alimaanisha kuwa tunaweza kuchukulia hivyo vitu kwa upeo wetu wa kibinadamu kiwepesi wepesi lakini siku tutakapokuja kuyaona hayo mambo ndipo tutakapojua kweli mawazo yake yalikuwa mbali sana na sisi tulivyokuwa kufikiri.
Siku hiyo sisi tutakapoondoka hapa duniani, haitakuwa heri kwetu tu sisi na viumbe vyote, bali itakuwa heri pia kwa Malaika wote walioko mbinguni. Kutakuwa na shangwe na furaha isiyoneneka.
Hivyo ndugu tukikaa na kuyatafakari hayo kwa utulivu, basi hatutajali ni mambo mangapi yatapita mbele yetu mabaya, sisi siku zote tutaelekeza macho yetu mbinguni, hatutajali ulimwengu unasemaje, sisi tutamtazama mwokozi wetu YESU KRISTO daima, huku tukingojea kwa saburi yale Mungu aliyoutandalia, tutaishi kama wapitaji na wasafiri tu hapa duniani.
1Petro 1:9-16
“9 KATIKA KUUPOKEA MWISHO WA IMANI YENU, YAANI, WOKOVU WA ROHO ZENU.
10 Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi.
11 Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, NA UTUKUFU UTAKAOKUWAKO BAADA YA HAYO.
12 Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. MAMBO HAYO MALAIKA WANATAMANI KUYACHUNGULIA.
13 Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo.
14 Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu;
15 bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;
16 kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”
Tukaze mwendo, ikiwa maisha yako sasa yapo mbali na Kristo, huu ni wakati wa kumrudia yeye maadamu mlango wa neema bado upo wazi, kumbuka siku ile ukijikuta umeachwa majuto hayatakuwa kwasababu unakwenda Jehanum, hapana majuto makubwa yatakujia kwasababu umekosa mambo mazuri ya umilele Mungu aliokuwa amewaandalia watoto wake tangu zamani.
Hivyo tubu kabisa kwa kudhamiria kuanza maisha mapya katika Bwana, na haraka bila kukawia nenda ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwenye maji tele, na kwa Jina la YESU KRISTO..Ili upate ondoleo la dhambi zao kulingana na Matendo 2:38., kisha Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu kama alivyoahidi, na kuanzia hapo nawe utakuwa umeingizwa na kuwa mmojawapo wa waliostahili kuuona huo utukufu ambao utakuja kufunuliwa siku za hivi karibuni. Tunaishi katika siku za mwisho Zidi kudumu katika utakatifu, na ushirika na kusali daima.
Bwana akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Tafadhali “share” Ujumbe huu kwa wengine.
Mada Zinazoendana:
VIUNO VYENU VIWE VIMEFUNGWA NA TAA ZENU ZIWE ZINAWAKA
Ufunuo 16:15 “ (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.)”
Umewahi kujiuliza kwanini Bwana Yesu sehemu nyingi ujio wake anaufananisha na mwizi. Kwanini Bwana anajifananisha na wezi na sio watu watakatifu.. Tunafahamu wizi sio kitu kizuri, na moja ya Amri za Mungu ni “USIIBE”. Lakini hapa tunaona Bwana anajifananisha na mwizi. Kwanini anafanya hivyo?.
Ni wazi kuwa kuna hekima tunaweza kuiona hata katika waovu..Ndio maana Bwana alisema mahali pengine tuwe na “Busara kama nyoka”..Nyoka sio kiumbe chenye ishara nzuri, kuanzia Edeni mpaka sasa, shetani alikitumia kupenyeza dhambi ulimwenguni.. Lakini Bwana alituambia tuwe na Busara kama nyoka…Na zaidi ya yote yeye mwenyewe Bwana anajifananisha na Yule nyoka wa shaba Musa aliomnyanyua kule jangwani.
Yohana 3: 14 “Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa;
15 ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye”.
Na sehemu nyingine tena Bwana anajifananisha na yule Kadhi dhalimu:
Luka 18: 1 “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.
2 Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu.
3 Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu.
4 Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu,
5 lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.
6 Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu.
7 Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?
8 Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?”
Tena Sehemu nyingine Bwana anatufundisha kupitia mfano wa WAKILI DHALIMU aliyekuwa mwizi wa mali za Bwana wake na mwisho akatenda kwa Busara, Bwana akasema nasi pia tujifanyie rafiki kwa mali ya udhalimu ili itakapokosekana watukaribishe kwenye makao ya milele.
Luka 16: 1 “Tena, aliwaambia wanafunzi wake, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake.
2 Akamwita, akamwambia, Ni habari gani hii ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena.
3 Yule wakili akasema moyoni mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya.
4 Najua nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao.
5 Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu?
6 Akasema, Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini.
7 Kisha akamwambia mwingine, Na wewe wawiwani? Akasema, Makanda mia ya ngano. Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini.
8 Yule bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru.
9 Nami nawaambia, Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele”.
Sehemu zote hizo Bwana hatumii watu wazuri au watakatifu kutufundisha Bali anatumia watu waovu, sio kwamba anataka tujifunze uovu wao, au tuige tabia zao hapana bali anataka tujifunze hekima yao. Kwasababu wana wa ulimwengu huu (wasiomjua Mungu biblia inasema wana hekima katika mambo yao).
Sasa tukirudi kwenye ule mfano wa Mwivi Bwana alioutuoa na kusema “Tazama naja kama mwivi”…Tunajua mwivi sio mtu mzuri, anakuja kwa lengo la kuiba…Lakini busara ya mwivi siku zote hapendi kusumbuliwa wala hapendi kumsumbua Yule anayemwibia..atafanya mambo yake kimya na taratibu na akishaiba anakwenda zake..Kwasababu hiyo basi anasubiria watu wakati wamelala na wamechoka usiku wa manane ndio anakuja na kuingia ndani na kuiba kisha kuondoka…Anakuja wakati ambao mali anayoitafuta na mwenye mali wamejitenga vizuri kabisa, anakuja wakati ambao nafasi ya matengano ni kati ya mali na mwenye mali ni kubwa sana..Hiyo ni hekima ya hali ya juu.
Na ndio Bwana Yesu naye ataitumia hekima hiyo hiyo wakati wa kuja kulichukua kanisa lake..atakachofanya kwanza ni kuja wakati ambao magugu na ngano vimeshajitenga..wakati ambao ulimwengu umelala usingizi na kumsahau Mungu, wakati ambao watakatifu wametengwa na ulimwengu wote, wakati ambao watakatifu wanaonekana ni watu wasiokuwa na maana, ulimwengu umewachoka, ulimwengu umeacha kuthamini mambo ya muhimu yahusuyo roho zao, Huo ndio wakati Bwana Yesu anakuja kuwaiba watu wake kutoka ulimwenguni.
Kama vile mwizi anapokuja, huwa anakuja wakati ambao watu hawaangalii tena tv zao ndani wamezichoka, wakati ambao watu hawatumii tena magari yao ya thamani wameyaacha yapumzike..wakati ambao simu zao za mikononi wamechoka kuzitumia n.k Huo ndio wakati mwizi anakuja kuzichukua.
Mteule wa Mungu hizi nyakati ni za hatari, nyakati ambazo ulimwengu haumtaki tena Kristo..Wakati ambao Watakatifu wanaonekana hawana thamani tena ulimwenguni, wakati ambao watakatifu wamechokwa na watu wa ulimwengu huu, ujue ni wakati wa matenganisho..vitu vya thamani vimechokwa kutumiwa, huo ndio wakati mwivi anakuja..wakati ambao usingizi wa anasa, na uasherati na ulevi umewavaa wengi huo ndio wakati Kristo anapoivamia nyumba.
Na siku ya kuwanyakuwa watu wake hakuna mtu atakayejua siku hiyo..baada ya kipindi Fulani kupita ndipo hapo watakapojua kuwa kuna baadhi ya watu hawapo? Watu wetu wa muhimu na wa thamani waliokuwa wanatuhubiria habari njema za maisha ya umilele na utakatifu wametoweka.
Na kama vile mtu anavyopata uchungu wa kuibiwa mali yake ya thamani..ndivyo watu wengi siku hiyo watakavyopata uchungu wa kuachwa ulimwenguni na wapendwa wao wa thamani..watazidi kupata uchungu mwingi watakapoanza kupitia dhiki ya mpinga kristo na siku ya BWANA inayotisha. Watalia na kujuta na kuomboleza.. Kumbuka kitakachowaumiza sana sio mapigo yale bali ni “kwanini hawakukesha”..hicho ndicho kitakachowaumiza sana.. Ni kwanini wenzao wameondoka na wao wamebaki?? Na kwamba wenzao wapo utukufuni mbinguni milele na wao wataenda kwenye lile ziwa la moto, watasikia wivu uliochanganyikana na hasira mbaya sana.. Uchungu huo unafananishwa na uchungu wa mtu KUIBIWA MALI YAKE USIKU, na siku hiyo watu wote walioachwa watamchukia Bwana Yesu kuliko hapo kwanza. Watamchukia kwa ukomo wa chuki, Kama vile watu wanavyowachukia wezi baada ya kuibiwa. Watamkufuru na kumtukana, na dhiki watakazopitia zitaongeza hasira yao.
Ufunuo 16: 8 “Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto.
9 Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa, NAO WAKALITUKANA JINA LA MUNGU ALIYE NA MAMLAKA JUU YA MAPIGO HAYO; WALA HAWAKUTUBU WALA KUMPA UTUKUFU.
10 Na huyo wa tano akakimimina kitasa chake juu ya kiti cha enzi cha yule mnyama; ufalme wake ukatiwa giza; wakatafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu,
11 WAKAMTUKANA MUNGU WA MBINGU KWA SABABU YA MAUMIVU YAO, NA KWA SABABU YA MAJIPU YAO; WALA HAWAKUYATUBIA MATENDO YAO”.
Watu wengi wanasema kutakuwa na nafasi ya kutubu wakati huo?? Ndugu yangu, ndugu yangu nataka nikuambie huo ni uongo wa shetani, siku hiyo hakutakuwa na nafasi ya kutubu. Utakuwa ni wakati wa maombolezo na vilio na hasira na uchungu..Wanadamu wote walioachwa watataka kufanya vita na mwanakondoo, watamchukia Yesu Kristo..
Kama ulishawahi kuibiwa unaweza ukaulewa uchungu wa kuibiwa..ni mbaya sana, wengi wasiomjua Mungu wanaishia kuwachukia wezi maisha yao yote… Ndio maana Bwana naye anatuonya kwasababu anauona UCHUNGU utakaokuja huko mbeleni kwa wanadamu wote watakaoachwa..anatuonya na kutuambia “KESHENI” naja upesi.
Luka 21:34 “ Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo;
35 kwa kuwa ndivyo ITAKAVYOWAJILIA WATU WOTE WAKAAO JUU YA USO WA DUNIA NZIMA.
36 BASI, KESHENI NINYI KILA WAKATI, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu.”
Mathayo 24: 42 “Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.
43 Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.
44 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja”.
Kukesha hapo sio kukesha kwa mwili kutojizuia kulala, hapana bali ni kukesha katika roho,kwa kuishi maisha ya uangalifu, na utakatifu, kuishi kwa kuzisoma nyakati na kuyaelewa majira tunayoishi, kuishi kwa kuweka kando uasherati, ulevi, anasa, mavazi yasiyompendeza Mungu, matusi, rushwa, na mambo yote mabaya na kudumu katika kujifunza Neno la Mungu kila wakati. Hiyo ndio maana ya kukesha. Siku zinakuja hizi ni za hatari sana, tuwe macho wapendwa.
Maneno ya Mungu yaliyofunga kitabu cha biblia ni maneno ya Bwana Yesu na maneno hayo aliyoyasema ni haya..
Ufunuo 22:20 “Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu.
21 Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote. Amina.”
Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine, BWANA akubariki sana.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
LUKA 12:20 INASEMA “USIKU HUU WA LEO WANATAKA ROHO YAKO!” NI WAKINA NANI HAWA WANAOITAKA ROHO YAKE?
NINI MAANA YA KUISHI KWA KUUKOMBOA WAKATI?.
Tukisoma kitabu cha Mwanzo biblia inatuambia “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi”, pia tukirudi kusoma tena maandiko biblia inatuambie vile vile “Mungu ni Roho” (Yohana 4:24), Hivyo katika mstari huo ni sawa na kusema hapo mwanzo “Roho wa Mungu aliziumba mbingu na nchi, 2 Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.”..
Kwahiyo hapo tunaona Roho wa Mungu alifanya kazi mara mbili, katika utengenezaji wa ulimwengu. ya kwanza ni kuumba mbingu na nchi, na ya pili ni kuja kuitengeneza tena nchi ili kutimiza lengo Fulani ambalo amelikusudia, na lengo hilo si lingine zaidi ya kuifanya nchi IZAE, isibaki tena katika hali ya ukiwa. Ipo sababu kwa nini Mungu aliacha nafasi kati ya kuumbwa kwa dunia baada ya kukaa katika ukiwa wa muda mrefu na kuja kutengenezwa tena Ipo sababu.
Lakini Mungu kutujuza hayo kwa ufupi ni kutufundisha kanuni zake utendaji kazi. Na kanuni hiyo hiyo Mungu anaitumia kwa mtu yeyote anayempa Kristo maisha yake leo.
Jambo la kwanza pale mtu anadhamiria kwa dhati kabisa kutoka moyoni mwake kumpa Kristo maisha yake, kwa kutubu na kuacha dhambi zake zote, na kwenda kubatizwa katika ubatizo ulio sahihi wa kimaandiko, basi mtu huyo anakuwa ni sawa kaumbwa kwa mara ya kwanza, Roho wa Mungu anakuwa amefanya kazi yake ya kumuumba na kuwa kitu halisi kinachoonekana,. Mtu kama huyo anakuwa ameshatiwa muhuri na Roho Mtakatifu kuwa ni milki halali ya Mungu. Ni kazi ya Mungu iliyo tayari kwa matumizi yake. Lakini hawi kitu kilichokamilika mbele zake, anakuwa anafananishwa na nchi iliyokuwa imeumbwa na Roho Mtakatifu ambayo ipo katika hali ya ukiwa.
Sasa ile hatua ya pili ambayo Roho wa Mungu anatua mwenyewe juu ya nchi ya kuifanya kuwa nchi izaayo, ni jambo lingine ambalo hilo lilichukua muda kidogo tofauti na lile la kwanza la uumbaji. Hali hiyo hiyo inakuwa pia na kwa mtu aliyezaliwa mara ya pili leo.Kumbuka kama biblia inavyosema Roho Mtakatifu ni ahadi kwa wale wote watakaomjia na kumpokea:
Matendo 2:38 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
39 KWA KUWA AHADI HII NI KWA AJILI YENU, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.
Hii ikiwa na maana kuwa mtu yeyote yule pindi tu anapompokea Yesu Kristo kwa kudhamiria kabisa kuacha maisha yake ya dhambi na kutaka kumwishia yeye basi siku hiyo hiyo Roho wa Mungu anaingia ndani yake kuyageuza maisha yake na kumfanya kuwa kiumbe kipya, hii haichukui nguvu, wala muda, ni jambo la kudhamiria na kuzingatia maagizo yote yanayoambatana na kuamini kwako. lakini hiyo haimaanishi kuwa Roho wa Mungu atatua juu ya mtu kama huyo siku hiyo hiyo aliyoamini.. Hilo ni jambo lingine.
Ukisoma biblia utaona Bwana wetu Yesu Kristo yeye alijazwa Roho Mtakatifu tangu alipokuwa tumboni mwa mama yake, lakini Roho Mtakatifu hakuwa juu yake tangu akiwa tumboni mwa mama yake, isipokuwa alipofikisha umri wa miaka 30, na ndivyo ilivyokuwa kwa Yohana Mbatizaji, yeye pia alijazwa Roho tangu akiwa tumboni mwa mama yake lakini Roho Alimfuata nyikani miaka mingi baadaye.. Vivyo hivyo na mitume wote wa Yesu Kristo, pale Bwana alipowachagua, siku ile wote walipochukua uamuzi wa kumfuata Bwana na kuacha mambo yao yote maovu na njia zao, na kazi zao, na familia zao kwa ajili ya Bwana, na kubatizwa walipokea Roho Mtakatifu ndani yao, ndiye aliyewapa uwezo wa kustahimili mambo yote kwa kipindi chote walichokuwa wanakipitia na Bwana. Lakini Roho Mtakatifu kuja juu yao haikuwa siku ile ile ni kitendo kilichowachukua muda wa miaka mitatu na nusu baadaye..
Kwasababu Kitendo cha Roho wa Mungu kutua juu ya mtu, ni lazima kwanza mtu ajue ni kwasababu gani Roho huyo aje juu yake, kwahiyo hakiji kiuwepesi kama kile cha kwanza cha kufanywa kuwa kiumbe kipya, bali hichi kinakuja kwa makusudi maalumu, hivyo yule atakaye kipokea ni sharti kwanza ayatambue makusudi hayo ni yapi na ndio hapo itamgharimu mtu apitie huyo hata madarasa Fulani fulani, ya kutosha pamoja na kuomba sana bila kukata tamaa kwa ajili ya Roho.
Na makusudi hayo tunayaona ndio kama yale Roho Mtakatifu alivyotua tena juu ya nchi tena, nayo si mengine zaidi ya kuifanya nchi IZAE na iwe mahali pa KUISHI wanadamu.
Na ndivyo itakavyokuwa pale Roho wa Mungu atakapotua juu ya mwamini baada ya kukamilishwa, atamfanya mtu huyo kuwa ni chombo cha kuzaa zaidi na cha kuhudumia kundi lake ziadi ya matakwa ya mtu binafsi. Tunaona mara baada ya Bwana kushukiwa na Roho juu yake ndio tunaona tangu huo wakati na kuendelea akaanza kuleta uamsho Israeli yote na dunia nzima, kadhalika ndivyo ilivyokuwa kwa Yohana mbatizaji na mitume wa Yesu Kristo siku ile ya Pentekoste. Kwasababu Roho ameshawatia mafuta na kuwafanya kuwa nchi izaayo kwa ajili ya kusudi lake.
Vivyo hivyo na sisi hatupaswi kuridhika na mahali tulipo, ni kweli tulipompa Bwana maisha yetu na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kimaandiko tulitiwa muhuri kwa Roho wake, tulizaliwa kwa Roho mtakatifu, tulifananishwa na nchi iliyoumbwa hapo mwanzo na Roho wa Mungu,lakini hiyo haitoshi kwasababu tukiendelea kubakia hivyo hivyo tutazidi kuwa katika hali ya UTUPU na UKIWA. Yatupasa sisi sasa tuongeze bidii katika kumwomba Mungu na kumtafuta Roho Mtakatifu kwa nguvu zetu zote, ili alete uhai katika kanisa lake kupitia sisi, alete uamsho tena katika kanisa lake kupitia sisi, auondoe ukiwa uliopo sasa duniani, inatupasa kila siku usiku na mchana tumwombe Mungu amlete Roho Mtakatifu aipindue tena dunia.
Kumbuka hatuzungumzii kumwomba atende miujiza na ishara hapana bali alete mageuzi katika kizazi chetu kama aliyoyaleta pale alipoitia mafuta nchi tena..kumbuka mitume walikuwa wanatenda miujiza hata kabla ya siku ya Pentekoste lakini biblia haitupi rekodi ya tunda lolote walilofanikiwa kulileta siku zote walizokuwa wanazunguka kufanya miujiza isipokuwa walipofikia kipindi cha Pentekoste, Roho wa Mungu aliposhuka juu ya kanisa na kuanza kuchoma mioyo ya watu,hapo ndipo badiliko kubwa lilionekana (yaani ndani ya siku moja waliokoka watu zaidi ya elfu 3), Nguvu hizo za uamsho ndizo tunazozihitaji siku za leo.
Embu fuatilia ushuhuda huu naamini na sisi utatupa jambo la kujifunza kwa kupitia hili.
EVAN ROBERTS.
Ni kijana aliyezaliwa katika nchi ya Wales huko bara la Ulaya mwaka 1878, Ni muhubiri mashuhuri sana anayejulikana katika vitabu vya historia za kidini, aliyesifika kwa kuletea uamsho mkubwa sana huko nchini Wales mwaka 1904-1905.
Inarekodiwa kuwa Evan tangu enzi za utoto wake alikuwa ni kijana aliyependa sana kuhudhuria kanisani , na aliyekuwa anakariri mistari mingi ya biblia. Ni kijana mdogo aliyejulikana kwa kutumia masaa yake mengi katika maombi binafsi hususani wakati wa usiku akimwomba Roho Mtakatifu ampe moyo usiogawanyika, na pia alijumuika katika vikundi vya maombi na watu wengine, Evan anasema alikuwa anamwomba Roho Mtakatifu kwa zaidi ya miaka 11 aitembelee tena Wales kwa nguvu ya uamsho wa kipekee watu wengi wamgeukie Mungu. Anasema tangu huo wakati alikuwa anaweza kukaa usiku kucha akitumia muda wake mwingi kusoma, na kuzungumzia tu habari za uamsho . Evans alikuwa akiungana na vijana wenzake wengine wakiomba juu ya uamsho wa Roho uje katika kijiji chao.
Mpaka ilipofikia wakati Mungu kusikia sauti yao, Mungu alileta Roho ya Mageuzi makubwa katika nchi ile ndogo ya Wales, watu ghafla wakawa wanachomwa na mafundisho ya Evan katika kanisa dogo alilokuwa anasali, watu wakaanza kumgeukia Mungu, hata wale ambao waliokuwa vuguvugu, kwa kuhudhuria tu mikutano ile katika kanisa lile dogo watu wote walikata shauri kwa moyo mmoja na kumgeukia Mungu kwa dhati kabisa, watu waliomtafuta Mungu waliongeza kwa haraka sana mikutano mingi ikaanza kupangwa katika miji mingine,na vijiji vingine na wote waliokuwa wanasikia walichomwa mioyo na kujihisi kumrudia Mungu wao kwa mioyo yao yote.
Magazeti na vyombo ya habari vikaanza kurekodi, badiliko kubwa la watu kumgeukia Mungu katika mji ule, watu walikuwa wanawahi kufunga maduka yao kabla hata ya wakati wao wa kawaida wa kufunga ili tu wawahi ibadani za kila siku jioni, makanisa yalijawa na watu mpaka yakawa hayana nafasi tena ya kuwahifadhi watu wanaofika makanisani, watu wanasimama nje, watu ambao walikuwa watukanaji, barabarani walikuwa wakitembea na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, Uhalifu ulishuka kwa asilimia kubwa sana katika mji wa Wales, hata mabaa mengi yaliyokuwa mashuhuri ya kuuza pombe yalifungwa kwa kukosa wateja, kwasababu mji mzima ni kama ulipigwa butwaa hata wakuu wa nchi walishangaa nchi ile imekumbwa na nini kwa uamsho mkubwa namna ile ulioletwa kijana mdogo tu Evan Roberts pamoja na vijana wenzake.
Kwa kipindi kisichozidi miezi 9, zaidi ya watu 150,000 katika nchi ile ndogo walitubu na kugeuka Mungu kabisa na kuwa wakristo waliosimama mbele za Mungu, uamsho ule ulizidi kuendelea mpaka nchi jirani za Wale.Jambo hilo lilimfanya Evan kuwa mtu maarufu sana duniani kwa wakati ule, Lakini Uamsho ule ulidumu kwa muda wa miezi 9 tu.(Mwaka 1904-1905).
Sasa hiyo yote ilikuja kutokana na maombi yasiyokoma ya Evans Roberts kwa ajili ya nchi yake. Vivyo hivyo na sisi, tunapokuwa wakristo haitoshi tu kusema Roho Mtakatifu ni wa kwangu tu peke yangu, yatupasa tuingie katika kuliombea kanisa , na kuwaombea wengine Mungu mwenyewe alete Roho ya mageuzi alete UAMSHO mpya katika jamii zetu ili watu waokolewe. Mungu aachilie Roho ya kuwavuta wengi kwake..Na tukiwa watu wa tabia hiyo basi hata siku hiyo ikifika, Mungu atakapoleta UAMSHO huo atatupa sisi kipaumbele cha kwanza kuwa vyombo vyake vya kuokoa watu, kuliko tukikaa tu hivi hivi..
Na ndio maana Bwana Yesu alisema:
Na ndio maana Bwana YESU alitoa mfano huu na kusema:
Luka 11.5 “Akawaambia, Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu,
6 kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake;
7 na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe?
8 Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake.
9 Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.
10 Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.
11 Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?
12 Au akimwomba yai, atampa nge?
13 Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa ROHO MTAKATIFU HAO WAMWOMBAO?”.
Unaona hapo?. Mistari hiyo inatupa picha kuwa kumbe Roho mtakatifu sio ahadi tu kwa yeyote aaminiye bali pia anapaswa kuombwa, tena kwa kurudia rudia, bila kukata tamaa, Kama Bwana Yesu alivyokuwa, mtu wa dua sana na maombi kama biblia inavyosema katika Waebrania 5:7 Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu;
Unaona hapo? Aliendelea hivyo hivyo Mpaka siku ile Roho wa Mungu aliposhuka juu yake na kumtia mafuta zaidi ya watu wote duniani, siku hiyo ndiyo alipoachwa kuitwa YESU, na kuitwa YESU KRISTO. Nasi tunaona UAMSHO wake jinsi ulivyoleta madhara makubwa mpaka sasa katika vizazi vyetu.
Hivyo ni wajibu kwa kila mkristo anayeihurumia jamii yake na anayetaka jamii yake iokolewe, anayelipenda taifa lake liokolewe anayependa watu wengi waokolewe kuomba bila kukata tamaa Bwana ampe Roho Mtakatifu kwa lengo la kuzaa. Kwa lengo la kuleta Mageuzi, kwa Lengo la Uamsho,. Na kwakuwa yeye mwenyewe kashasema ikiwa sisi waovu tunaweza kuwapa watoto wetu vipawa vyema pale wanapotuomba je! si zaidi sana Baba yetu aliyembinguni?
Luka 18:7 “Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?8 Nawaambia, atawapatia haki upesi;” Hivyo sisi sote tuanze sasa, kuomba juu watu kuokolewa kwa bidii zote. Na Bwana atatusikia na kutujibu kwa wakati wake.
Bwana akubariki sana.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Tafadhali “Share” ujumbe huu kwa wengine. Na Mungu atakubariki.
Mada Zinazoendana:
WAISRAELI WENGI SANA WANARUDI KWAO SASA.
KWANINI SAMWELI ALIRUHUSUIWA KUHUDUMU HEKALUNI KAMA VILE WALAWI WAKATI YEYE NI MU-EFRAIMU?
Luka 19: 37 “Hata alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona,
38 wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu.
39 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. 40 Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, MAWE YATAPIGA KELELE”.
Zamani nilijua kuwa Mimi nisipofanya kazi ya Mungu, basi kazi ya Mungu itasimama katika eneo nililopo..Ndivyo nilivyokuwa nafikiri hivyo kwa muda mrefu sana..Nilijua tunapoihubiri Injili ni kama tunamsaidia Mungu, kwamba pasipo sisi kujitoa basi watu wengi hawataokolewa..Na ndivyo nilivyofundishwa hata mimi.
Lakini namshukuru Mungu, nilikuja kuelewa zaidi ya hapo…kwamba Mungu hasaidiwi kazi, wala hajalemewa na kazi, wala haitaji msaada wowote kutoka kwa Mwanadamu…Mungu alipoiumba dunia na watu ndani yake, hakuiweka pasipo mipango kama sisi wanadamu tunavyofanya kwamba tunafikia mahali tunabanwa na majukumu yanayotuumiza kichwa mpaka wakati mwingine tunakata tama ya kuendelea..
Mungu hayupo hivyo, alipoumba kila kiumbe chini ya jua alikwisha kiwekea sehemu yake katika dunia kwamba kitazaliwa wapi, kitahitaji kiasi gani cha chakula mpaka kife, kitahitaji hewa ya ujazo kiasi gani n.k …Hayo yote Mungu alishayaweka kabla hata ya hicho kiumbe kuzaliwa au kuwepo..
Kadhalilka na kila mwanadamu anayezaliwa chini ya Mbingu, Bwana alishampangia azaliwe wapi, aishi miaka mingapi, ale chakula kiasi gani, aokolewe wakati gani, afe wakati gani n.k Kwahiyo mwanadamu anapozaliwa ni kama anakuja tu kutimiza maandiko kwa yale aliyoandikiwa.
Kwahivyo basi hakuna mwanadamau yoyote anayeweza kumsaidia Mungu majukumu yake…Yeye mwenyewe anatenda kazi zake kama alivyopanga…Kama alipanga nchi ya Tanzania ifikie idadi ya watu milioni 60 mpaka mwishoni mwa mwaka 2019..penda tusipende hiyo idadi itafika tu!!..Hata kama mtu fulani akatae kuzaa watoto…hiyo haizuii idadi ile kufika..Bwana atatumia wengine kufidia nafasi yake.
Kadhalika tunapokuja katika suala la watu kuokolewa..Bwana Yesu alisema “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu asipovutwa na Baba aliyenipeleka”..Sentensi hii inaonyesha kwanza wokovu ni wa kuchaguliwa..Sio kila mtu tu anaweza kuupokea..Ni lazima uchaguliwe na kisha uitwe/uvutwe kwa Bwana ndipo umfuate..ikiwa na maana kuwa kama mtu hajasikia mvuto wowote au msukumo wowote ndani yake wa kwenda kumfuata au kumpokea Bwana Yesu huyo hawezi kamwe kumwamini ni sawa na kumlazimisha mtoto mdogo aliyezaliwa leo azungumze haitawezekana.
Kwahiyo kama Bwana amekusudia idadi fulani ya watu wamfuate yeye mwaka huu katika mji fulani labda wa Dar es salaam, hakuna yoyote atakayeweza kupunguza au kuongeza idadi hiyo..wala hakuna mtu yoyote atakayeweza kuisimamisha kazi yake.
Atanyanyua watu wake (watumishi wake) wanawake kwa wanaume, vijana kwa wazee labda tuchukue mfano watumishi 5,000 kwa mji wa Dar es salaam..atawatuma wakaihubiri injili katika huo mji na endapo hao aliowatuma walipaswa wavune idadi ya wale watu milioni 20 wale waliokusudiwa uzima wa milele, na ile idadi ikatimia basi kazi yao itakuwa imeisha watapelekwa mji mwingine..Lakini mfano endapo kati ya wale 5,000 waliotumwa 2,000 wakawa wavivu wasilete mazao..basi Bwana atawanyang’anya ile kazi na kuwapa watu wengine lakini mwisho wa siku ile idadi ya watu milioni 20 waliokusudiwa kuokolewa itatimia tu!..kwa vyovyote vile itatimia tu! Wataondolewa wale wavivu watapewa wale wachapa kazi.
Kwahiyo ndugu huu sio wakati wa kufikiri kazi ya Mungu itasimama endapo sisi (mimi na wewe) leo hii tukikataa kuitenda kazi..Hiyo haitakuwa hasara kwa Mungu bali itakuwa ni hasara kwetu.. kwasababu Nafasi zetu watapewa wengine walio na bidii kuliko sisi endapo tukizembea..Na sisi tutakosa thawabu mbele za Mungu siku ile.
Ukikataa leo kuwashuhudia wengine habari njema za wokovu usidhani umeathiri kazi ya Mungu kwa vyovyote vile..Kazi ya Mungu itafanyika tu na watu wale waliokusudiwa kuokolewa wataokolewa..Bwana alipotuambia tuenende ulimwenguni kote tukahubiri injili kwa kila kiumbe sio kwa faida yake yeye..Ni kwa faida yetu sisi, Hatutumi ili tukamsaidie kazi yake hapana! Yeye hasaidiwi..katutuma ili tukapate faida sisi sio yeye..
Wewe usipoihubiri injili mtaani kwako, mjini kwako au nchini kwako. Kazi ya Bwana haitasimama, Mungu atanyanyua mwingine na kumleta hapo mjini kwako, au nchini kwako kuitangaza habari yake na wale waliokusudiwa kuokolewa wataokolewa tu!..lakini utakuwa umejizuiliwa thawabu yako mwenyewe..
Wewe ukikataa kuichangia kazi ya Mungu mahali ulipo, usifikiri itasimama kwa vyovyote vile.. Hapana Mungu hasaidiwi kazi wala hategemei mfuko wa mtu hata kidogo..atanyanyua wengine kutoka mahali pengine watakaoipalilia ile kazi…Anapotushauri tumtolee yeye sio kwa faida yake yeye bali ni kwa faida yetu sisi..Yeye tayari ana kila kitu..sasa ana haja na nini tena? Dunia yote ni yake sasa ni nini tutamwongezea yeye??
Anapokuambia umtafute yeye, au umtegemee yeye..sio kwamba yeye ana uhaba wa watu au wa sifa, au anahitaji sana utukufu..hapana ndugu anao mabilioni ya malaika watakatifu huko mbinguni wanaomsifu usiku na mchana…anakuambia umsifu wewe kwa faida yako?? Sio kwa faida yake..
Ni sawa na mtu mwenye kampuni kubwa tajiri lililoendelea sana na lenye wafanyakazi wengi wanaojitosheleza, na akamwona mtu maskini na kwa huruma zake akaona ampatie nafasi ya kazi kwenye lile kampuni, sasa sio kwamba kampa ajira kwa sababu anaupungufu wa faida kwenye kampuni lake hapana bali kampa ajira kwasababu amemuhurumia yule maskini na anataka na yeye apate kitu..lakini endapo yule maskini akikataa ile nafasi basi hasara haitakuwa kwa yule mwajiri bali kwake yeye kwasababu yeye tayari anao wafanyakazi wengi wanaojitosheleza….Na kwetu sisi katika kumtumikia Baba yetu wa mbinguni ndio ivyo hivyo.
Ndio maana mahali fulani Bwana Yesu alipokuwa anaingia Yerusalemu aliwaambia mafarisayo maneno yale..
“ 39 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, MAWE YATAPIGA KELELE”.
Umeona! Hapo…Bwana alikuwa anataka kuwaonyesha kuwa sio kwamba Mungu ni maskini wa sifa..kwamba pasipo wao kumsifu yeye basi ndio hana sifa mahali pengine..hapana hata mawe yatapiga kelele endapo wao wakinyamaza.
Kama Mtume Paulo alivyosema pia kwa uwezo wa Roho…2 Timotheo 2: 13 “Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe”.
Kwahiyo tukiyafahamu hayo ni wakati wa kumtumikia Mungu kwa Nguvu zote..kwa talanta tulizopewa..tukijua kuwa ni kwa faida yetu, kwasababu siku ile inakuja katika Mbingu mpya na nchi mpya..ambapo Bwana hatakuwa na upendeleo kule..Kila mtu atakuwa na nafasi yake kule, kulingana na talanta alizozifanyia kazi hapa duniani.. Katika mbingu mpya na nchi mpya watakuwepo wafalme, na watu wakawaida, nafasi mtu atakayokuwa nayo kule ndio itakuwa yake hiyo milele..Kwahiyo tujitahidi tupige mbio tukiyatazamia mambo yale yanayokuja kama vile Mtume Paulo alivyokuwa anayatazamia..
Ufunuo 22: 10 “Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.
11 Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa.
12 TAZAMA, NAJA UPESI, NA UJIRA WANGU U PAMOJA NAMI, KUMLIPA KILA MTU KAMA KAZI YAKE ILIVYO.
13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho. 14 Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake”.
Tukaze mwendo, tumtumikie Bwana katika nafasi alizotuweka, naye atatuhifadhi kwa reema zake.
Bwana akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.
Mada Nyinginezo:
WALIO NA HEKIMA NDIO WATAKAOELEWA.
Jina la Bwana wetu Yesu Kristo lihimidiwe!
Karibu tujifunze pamoja Neno la Mungu ambapo leo tutajifunza juu ya KARAMA ILIYO KUU. Kama maandiko yanavyosema katika kitabu cha wakorintho..
1 Wakorintho 12: 28 “Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha.
29 Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza?
30 Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?
31 TAKENI SANA KARAMA ZILIZO KUU. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora”.
Tukisoma hapo juu tunaona maandiko yanasema kuna karama zilizo kuu, na kama kuna karama zilizo kuu ina maana kuwa kuna karama moja iliyo kuu zaidi ya nyingine zote. Na hiyo endapo mtu akiipata atakuwa mwenye huduma kubwa kuliko ya wote.
Tukirudi kwenye huo mstari hapo juu tunaona Mtume Paulo akitaja karama kadha wa kadha hapo, mfano Mitume, waalimu, miujiza, karama za uponyaji,karama za lugha, karama za kufasiri lugha,karama za masaidiano, karama za maongozi, karama za kinabii, karama za masaidiano n.k…Ametaja nyingi sana lakini tunaona hajataja karama iliyo kuu zaidi ya yote.
Sasa kwa akili zetu za kibinadamu tunaweza kufikiri kati ya hizo karama Mtume Paulo alizozitaja hapo juu kuna moja au mbili zilizo bora zaidi ya nyingine..au kuna moja kati ya hizo iliyo kuu kuliko zote..mwingine anaweza akafikiri karama ya uponyaji hapo ndio karama kuu Paulo aliyokuwa anaizungumzia…mwingine anaweza akafikiri karama ya kitume hapo ndio karama kuu Paulo aliyokuwa anaizungumzia kwamba tuitake.. Mwingine anaweza akasema karama ya kinabii ndio kuu kati ya hizo zote, mwingine karama ya lugha n.k Kila mtu anaweza kusema ya kwake kati ya hizo hapo juu.
Lakini je! Paulo aliposema takeni sana karama zilizo kuu alikuwa analenga moja wapo ya hizo alizozitaja hapo juu?.. Ili kuelewa ni karama ipi iliyo kuu kuliko zote ambayo Mtume Paulo alikuwa anailenga katika kifungu hicho cha mistari hebu tusome tena ule mstari wa 31..
“31 TAKENI SANA KARAMA ZILIZO KUU. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora”.
Umeona hapo? Anasema “hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora”…au kwa lugha rahisi na nyepesi Mtume Paulo alichokuwa anamaanisha ni kwamba “ hata hivyo nawaonyesha karama iliyo bora”
Sasa hiyo njia iliyo bora au karama hiyo iliyo bora ni ipi Mtume Paulo aliyokuwa anaizungumzia?
Tukiendelea kusoma mstari unaofuata baada ya huo wa 31,tunaona Mtume Paulo ameizungumzia hiyo njia iliyo bora au karama iliyo kuu, ambayo tunapaswa tuitafute sana..
1 Wakorintho 13:1 “ Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.
2 Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.
3 Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.
4 Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;
5 haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;
6 haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;
7 huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.
8 Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika”.
Umeona! Biblia inasema nijaposema kwa lugha za wanadamu na malaika; hii ikiwa na maana kuwa nijapokuwa na karama ya kuweza kunena lugha za malaika na za wanadamu wote kama sina karama hiyo kuu ya UPENDO mimi sio kitu. Anaendelea kusema nijapokuwa na karama ya KINABII kama sina UPENDO ni bure!..kwahiyo karama ya kinabii si kitu mbele ya karama ya upendo..Mtume Paulo anazidi kueleza nijapokuwa na karama ya Imani timilifu hata kuweza kuhamisha milima kama sijaipata hii karama iliyo kuu ya UPENDO mimi si kitu kabisa. Na karama nyingine zote nijapokuwa nazo lakini nikikosa karama moja iliyo kuu yaani ya UPENDO basi mimi sio kitu kabisa.
Kwahiyo karama iliyo kuu Mtume Paulo aliyokuwa anaizungumzia hapo ni UPENDO. Unaweza ukauliza kwanini UPENDO na si karama nyingine kama unabii, utume, lugha, imani, ualimu n.k kwanini upendo?
Karama ya UPENDO imekuwa ni karama KUU kuliko zote kwasababu NI KARAMA YA MUNGU MWENYEWE. Biblia inasema MUNGU NI UPENDO…(1 Yohana 4:8 “Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo”.)..Mungu sio MTUME, wala MWINJILISTI, wala MUHUBIRI, wala MNENAJI WA LUGHA wala kitu kingine chochote Mungu ni UPENDO..Hiyo ndio sababu UPENDO umekuwa ni karama kuu kuliko zote.
Mungu hakutuumba sisi kwasababu yeye ni nabii, hakutupatia pumzi kwa sababu yeye ni mponyaji, hatusamehi makosa yetu kwasababu yeye ni mwinjilisti, wala hatutimizii mahitaji yetu kwasababu yeye ni mtenda miujiza..Hapana Mungu ametuumba na kutupa pumzi na kutuokoa na kututimizia mahitaji yetu kwasababu yeye ni UPENDO wenyewe ni kama ni hivyo basi ni mwingi wa UPENDO.
Kwahiyo ndugu katika huu mwaka unaoanza pamoja na kwamba tumemwomba Mungu mambo mengi atutimizie, tumwombe pia tuwe kama yeye mwenye UPENDO alivyo, Ambao upendo huu unakuja kwa kujifunza Neno la Mungu, na pia kuchukua hatua ya kujifunza kupenda, kujifunza kusamehe kama yeye alivyotusamehe sisi, mwaka huu usianze na kinyongo na mtu, au na kisasi na mtu, mwaka huu uwe mwaka wako wa kupenda na kufadhili, wasamehe wote waliokuudhi huko nyuma, ili Mungu naye apate nafasi ya kukusamehe mambo yote maovu uliyomtendea mwaka wote wa jana ulioisha, bariki wengine kutoka moyoni kabisa ili na wewe uende kubarikiwa mwaka huu, Kwasababu biblia inasema kipimo kile kile upimacho ndicho na wewe utakachopimiwa..
Umefungua ukurasa mpya, basi uwe mpya kweli kweli katika roho yako pia,hapo utakuwa umemjua Mungu, naye Mungu mwenyewe atakupenda na kukutunza na kukuhifadhi kwasababu yeye mwenyewe ni UPENDO..
Ni maombi yangu kuwa Bwana atatujalia mambo hayo yote na zaidi ya hayo katika mwaka huu, Nakutakia Kheri ya Mwaka mpya 2019, Bwana akakutunze na kukuhifadhi dhidi ya yule mwovu wewe na watu wako na nyumba yako,na familia yako, akakulinde na kukupa afya njema, tangu mwanzo wa mwaka huu hadi mwisho wa mwaka, Bwana akakufanikishe katika mambo yote unayoyafanya yanayompendeza yeye katika JINA LA YESU KRISTO.
Amen!.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
MUNGU NDIYE ANAYEISHAWISHI MIOYO.
NI RAHISI KWA NGAMIA KUPENYA KATIKA TUNDU LA SINDANO, JE! NI SINDANO IPI HIYO INAYOZUNGUMZIWA?
SHETANI ANATOLEA WAPI FEDHA, ANGALI TUNAJUA FEDHA NA DHAHABU NI MALI YA BWANA?
2Nyakati 16: 9 “Kwa maana macho ya Bwana hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake”.
Tukisoma habari za wafalme katika biblia tunakuja kukutana na mfalme mmoja aliyeitwa ASA. Huyu biblia inasema aliiendea njia ya ukamilifu, alifanikiwa kuwaondoa watu wote waliokuwa mahanithi (Mashoga) katika nchi ya Yuda, akaondoa maashera yote pamoja na sanamu zote zilizokuwa zimewekwa na baba zake kabla yake. Kwa ujumbla ni mfalme aliyemtumainia sana Mungu kwa kila jambo na hivyo Mungu akamfanikisha sana(1Wafalme 15:9-15). Ilifikia hatua ambayo baada ya kugundua mama yake mzazi amesimamisha sanamu na kuziabudu, alimwondoa katika kiti chake cha umalkia bila kujali kuwa ni mama yake mzazi yupo hapo. Kwani kipindi kile cha wafalme, ilikuwa ni desturi mahali mfalme anapoketi ni lazima na mama yake awekewe kiti cha enzi kidogo pembeni yake.
Lakini Mfalme Asa mara baada ya kugundua kuwa mama yake Mzazi anaabudu miungu mingine, bila kujali hisia yoyote ya mtu alimwondoa asionekane tena katika jumba la kifalme daima. Jambo ambalo halikuwahi kufanywa na mfalme yeyote wa Israeli kabla yake… eti! Kumtoa mama yake aliyekuzaa katika cheo cha umalkia kisa tu kaisujudia miungu mingine?, Hakuna mfalme yeyote aliyedhubutu kufanya kitendo hicho cha kishujaa cha kumvunjia mamaye heshima na kumfanya kuwa kama mtu wa kawaida ili tu ailinde heshima ya Mungu wake japo wengi wao walikuwa wanawaona mama zao wakiwakosesha lakini walikaa kimya kulinda heshma za wazazi wao. Lakini kwa mfalme Asa ilikuwa tofauti, leo hii je! na sisi tunaweza kuyaweka mashauri ya wazazi wetu chini yale yanayopingana na Mungu na kuyaruhusu yale tu ya Mungu yasimame?. Mungu atusaidie katika hilo na sisi.
Mfalme Asa alisimamia kweli hakubakisha sanamu yoyote katika Yuda na Benjamini, aliingia maagano na Mungu kuwa yeye na watu wote wa Yuda watamtafuta Mungu kwa mioyo yao yote, kwa akili zao zote na kwa nguvu zao zote, akapiga mbiu katika nchi yote ya Yuda kwamba watu wote wamtufute Mungu muumba wa mbingu na nchi. Na wakakubaliana wote kuwa mtu yeyote ambaye hatamtafuta Mungu wa Mbinguni atauawa bila huruma, si mdogo, si mkubwa, si mwanamke, si mwanaume yeyote yule atauawa..
Hivyo Mungu akapendezwa sana na Mfalme Asa na hivyo akampa Amani na maadui zake wote waliokuwa wanamzunguka kwa muda mrefu tofauti na wafalme wengine waliosalia, na pindi maadui zake walipokuja kupigana naye Mungu aliwapa ushindi mnono, na nyara nyingi hivyo akaongezeka utajiri, na hofu kubwa ikawaangukia maadui zake wote waliokuwa wanamzunguka. Mungu akamjalia kuijenga Yuda kwa maboma, na minara na malango na makomeo makubwa, Na Hivyo mji ukathibitika na kuimarika kwa miaka mingi katika ufalme wake.
Lakini Bwana alimwambia Asa kwa kinywa cha Nabii Odedi ajitie nguvu wala mikono yake isilegee kwasababu kazi yake itakuwa ina malipo baadaye, haitakuwa bure aendelee hivyo hivyo kuulekeza moyo wake kwa Mungu, aondoe machukizo yote katika nyumba yake na katika Israeli aendelee hivyo hivyo kumtumaini Bwana wala asiwayategemee mataifa. Tunakuja kusoma ni kweli Mfalme ASA aliendelea kumsimamia Mungu kwa muda mrefu lakini ilifika wakati akapoa kidogo pindi maadui zake walipokuja kutaka kumzuia asitoke ndani ya mji wake, ndipo badala akimbilie kwa Mungu ambaye amekuwa akimtumainia na kumshindania kwa muda mrefu, Mungu ambaye amekuwa akimpigania vita vikubwa kwa muda mrefu, na kumfanikisha katika mambo yote siku zote za utawala wake, Mungu ambaye amekuwa akimpa amani pande zote, lakini badala yake akakimbilia kwa mfalme wa Shamu ili amsaidie kufanya vita na maadui zake, hivyo akampelekea na zawadi nyingi kutoka katika hazina ya nyumba ya Mungu, na kweli mfalme wa Shamu alimsaidia kupigana na maadui zake, na wale maadui zake wakaacha kuujengwa uzio wa kuwazuia, Hivyo nchi ikastarehe tena kwa muda mfupi.
Lakini jambo hilo halikumpendeza sana Mungu, kwasababu Mungu alimwona ASA kama ni mtu ambaye moyo wake ulimwelekea sana zaidi ya wengi waliotangulia, ni mtu ambaye Mungu angeweza kuonyesha uweza na nguvu zake zote kwa mataifa mengine kupitia yeye kama vile alivyoonyesha kwa Daudi na Sulemani, lakini sasa amefanya kitendo cha aibu, moyo wake kuwaelekea wanadamu na sio Mungu wake tena, kwenda kuwaomba wafalme wengine wa kipagani wamsaidie kupigana vita. Na ndio hapo tunakuja kusoma Mungu akimtumia nabii wake na kumwambia maneno haya.
2Nyakati 16: 7 “Wakati ule Hanani mwonaji akamwendea Asa mfalme wa Yuda, akamwambia, Kwa kuwa umemtegemea mfalme wa Shamu, wala hukumtegemea Bwana, Mungu wako, kwa hiyo limeokoka jeshi la mfalme wa Shamu mkononi mwako.
8 Je! Hao Wakushi na Walubi hawakuwa jeshi kubwa mno, wenye magari na wapanda farasi wengi sana? LAKINI, KWA KUWA ULIMTEGEMEA BWANA, ALIWATIA MKONONI MWAKO.
9 KWA MAANA MACHO YA BWANA HUKIMBIA-KIMBIA DUNIANI MWOTE, ILI AJIONYESHE MWENYE NGUVU KWA AJILI YA HAO, WALIOKAMILIKA MOYO KUELEKEA KWAKE. Kwa hayo umetenda upumbavu; kwani tangu sasa utakuwa na vita”.
Angalia hapo maneno hayo yalimjia mfalme Asa, hakujua kuwa macho ya Mungu yalishazunguka duniani kote kutafuta mtu aliyekamilika moyo ulioelekea kwake, ili Mungu ajionyeshe kuwa mwenye nguvu kwake, na akamwona ASA peke yake, lakini yeye hakulijua hilo, alidhani Mungu hakuwa anauthamini uthabiti wa moyo wake, alidhani Mungu hakumaanisha kumwambia yale maneno kuwa taabu yake kwake itakuwa na malipo (2Nyakati 15:7), yeye alichukulia juu juu tu, mpaka hapo alipoutoa moyo wake kwa Bwana na kuulekeza kwa wanadamu. Ndipo Mungu alipokasirika na kumwambia umefanya upumbavu…Mungu hapendi upumbavu kwa watu wanaomtumainia. Lakini pamoja na hayo yote Mfalme Asa alifanya mema machoni pa Mungu mpaka siku ya kufa kwake, na Bwana hakumwacha kabisa.
Leo hii ndugu yangu biblia inatufundisha na sisi tuwe ni mioyo iliyomwelekea Mungu. Kwasababu macho ya Mungu yanakimbia-kimbia duniani kote, ikiwa na maana Mungu anaangalia anarudi tena anaangalia, anarudi tena anaangalia aone mtu atakayekuwa na moyo mkamilifu utakaomwelekea yeye kwa kila kitu ili azionyeshe nguvu zake. Kama ilivyokuwa kwa mfalme Asa. Tuweke tegemeo letu lote kwa Mungu, tumtwike yeye fadhaa zetu zote, tusiwe wepesi kuwakimbilia wanadamu, bali mioyo yetu siku zote tuielekeze kwa Mungu muumba wa mbingu na nchi, kwasababu yeye anawaangalia watu kama hao waliokamilika mioyo aonyeshe nguvu zake zote. Tuvumilie na kumtegemea Mungu hatari inapojitokeza mbele yetu..Tusiwapendelee wanadamu hata kama ni ndugu zetu, bali sisi tuangalie tu kile Mungu anachosema basi, tusifanye ibada za sanamu, ambazo biblia inazitaja kama uasherati, na tama mbaya, bali tuvivunje vunje vikae mbali nasi, ndipo hapo Mungu atakapotuona na kazi yetu ikawa na faida kubwa. Na Mungu atatuimarisha.
Ikiwa haujampa Bwana maisha yako, mlango wa neema bado upo kwa ajili yako, damu ya thamani ya Yesu Kristo bado inafanya kazi hata sasa hivi, imebaki kipindi kifupi sana isimame kufanya kazi yake. Usisubiri kipindi Fulani kifike , hicho hakitafika ndugu yangu, hiyo ni injili ya shetani anayokuhubiria moyoni mwako.. muda wa wokovu ni sasa biblia inasema hivyo. Chukua uamuzi sasa wa kuyakabidhi maisha yako kwa Bwana Yesu kikamilifu, na utakapofanya hivyo kwa kudhamiria kabisa kutoka ndani ya moyo wako, kutubu kwa kuacha dhambi na maisha yako ya kale, basi yeye mwenye atakupa uwezo wa kuzishinda dhambi. Na haraka mara baada ya kuamini kwako unapaswa ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwa jina la YESU KRISTO, upate ondoleo la dhambi zako. Kisha Roho wa Mungu ataachiliwa juu yako kukulinda na kukuongoza katika kweli yote. Na baada ya hapo utakavyozidi kuuelekeza moyo wako kwa Mungu na kumtegemea yeye siku zote ndivyo utakavyouona mkono wake katika maisha yako, Na Mungu atakutumia wewe kuonyesha nguvu zake kwa wengine.
Ni matumaini yangu utafanya hivyo. Na Bwana akubariki sana.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
MUNGU NDIYE ANAYEISHAWISHI MIOYO.
BWANA ALIMAANISHA NINI KUSEMA “HERI WALIOTASA, NA MATUMBO YASIYOZAA, NA MAZIWA YASIYONYONYESHA”?
Umeshawahi kujiuliza pale biblia inaposema ROHO MBAYA KUTOKA KWA BWANA ikamjia Sauli ni roho ya namna gani hiyo? Na ni kwanini Bwana atume roho mbaya kwa mtu, nasi tunajua siku zote Mungu huwa anaachilia roho nzuri, njema na ya amani kwa watu, anasema hapa roho mbaya kutoka kwa Bwana, inakuaje tena anaiachilia roho yake mbaya iende kwa mtiwa mafuta wake, tena inafanya kazi ya kumsumbua kiasi ambacho inataka kufanya uharibifu hata ya kuwadhuru watu wasio na hatia..Tukisoma kitabu cha Samweli inasema:
1Samweli 16:14-23
“14 Basi, roho ya Bwana ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa Bwana ikamsumbua.
15 Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua.
16 Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi
wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujilia, yeye atapiga kinubi kwa
mkono wake, nawe utapona.
17 Basi Sauli akawaambia, Vema, nitafutieni mtu aliye stadi wa kupiga kinubi, mkaniletee.
18 Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese,
Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu
mzuri, ambaye Bwana yu pamoja naye.
19 Basi Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee Daudi mwanao, aliye pamoja na kondoo.
20 Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli
kwa mkono wa Daudi mwanawe.
21 Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akapata kuwa
mtu wa kumchukulia silaha zake.
22 Kisha Sauli akapeleka watu kwa Yese, akasema, Tafadhali, mwache Daudi asimame mbele yangu;
maana ameona kibali machoni pangu.
23 Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa
mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha”.
Ili kufahamu vizuri ni kwanini hayo yote yalimpata Sauli, turudi nyuma kidogo tuitazame historia ya Mfalme Sauli jinsi ilivyokuwa. Kama tunavyosoma katika maandiko tunaambiwa kuwa Sauli alikuwa ni kijana mzuri sana, mrefu, mwenye haya ya uso, mlaini, hakuwa hata mtu aliyezaliwa katika mbari za kikuhani au za waamuzi walioamua Israeli wakati ule, hakuwahi hata kupigana vita yeyote, wala hakuwa na dalili ya kuonyesha kama ni mtu aliyeweza kusimama vitani, na ndio maana tunakuja kuona pindi tu siku ile alipokuja kutiwa mafuta na Nabii Samweli na kutangazwa kwa Israeli wote kama mfalme wao, baadhi ya watu walimkebehi kwa kumtazama tu mwonekano wake wa nje na uzoefu wake hafifu, alionekana kama ni mtoto tu, mtu mwenye tabia kama za kitoto, pengine walipomwona sura yake laini na uzuri aliokua nao au mazungumzo yake yasiyo na uzoefu wowote wa uongozi, watu wakamdharau na kumwona kama si kitu hawezi kuongoza taifa kubwa la kishujaa kama Israeli. Na ni kweli ndivyo alivyokuwa, alikuwa hana uwezo wowote ule Sauli.
Lakini siku Mungu alipomtia mafuta biblia inasema Roho ya Mungu ikamjilia kwa nguvu juu yake naye akageuzwa na kuwa mtu mwingine. (1Samweli 10:6). Sasa kumbuku kwasababu mtu kama Sauli alitiwa mafuta ya kuwa mfalme kuongoza taifa kubwa na hodari kama Israeli, ni sharti roho ambayo itaachiliwa juu yake itakuwa ni roho ya uongozi, roho ya ujasiri, roho ya maamuzi magumu, na roho ya udhubutu na roho ya ushujaa. Hivyo jambo ambalo lingemtokea mfalme Sauli hapo ni lazima liwe la namna hiyo.
Lakini Mfalme Sauli hakulitambua hilo vizuri mpaka siku ambayo maadui wa ndugu zao walipotokea na kutaka kuwatawala, tena kwa mapatano ya kila myahudi kung’olewa jicho lake la kuume, vinginevyo watawauawa. Hivyo habari hizo zikafika katika miji mingine yote ya Israeli, watu wote wakalia sana, wakizingatia kuwa huyo adui wa ndugu zao huko Yabesh-gileadi ni mkuu sana, hakuna mtu anayeweza kusimama mbele yake kuwatetea na kushindana naye ili kuwaokoa ndugu zao..Hivyo wakalia sana lakini habari zilimfikia Sauli mwezi mmoja tu baada ya kutiwa mafuta ya kuwa mfalme, Sauli ambaye alidharauliwa na watu, Sauli ambaye hakuwa na uzoefu wowote wa vita ghafla akanyanyuka kwa ushujaa mwingi na HASIRA nyingi, na kusema maneno haya.
1Samweli 11:4 “Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote wakainua sauti zao wakalia.
5 Na tazama, Sauli akaja akifuata ng’ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini,
hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi.
6 NA ROHO YA MUNGU IKAMJILIA SAULI KWA NGUVU, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka
sana.
7 Naye akatwaa jozi ya ng’ombe, akawakata-kata vipande, kisha akavipeleka vile vipande mipakani mwote
mwa Israeli kwa mikono ya wajumbe, kusema, Ye yote asiyetoka nyuma ya Sauli na Samweli, ng’ombe
zake watatendwa vivi hivi. Basi utisho wa Bwana ukawaangukia wale watu, wakatoka kama mtu mmoja.
8 Naye akawahesabu huko Bezeki; Waisraeli walikuwa mia tatu elfu, na Wayuda thelathini elfu.
9 Nao wakawaambia hao wajumbe waliokuja, Waambieni watu wa Yabesh-gileadi, Kesho, wakati wa jua
kali, mtapata wokovu. Basi wale wajumbe wakaenda, wakawaarifu watu wa Yabeshi; nao walifurahiwa.
10 Kwa hiyo watu wa Yabeshi walisema, Kesho tutawatokea, nanyi mtatufanyia yote myaonayo kuwa ni
mema.
11 Ikawa, kesho yake, Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu; nao wakaingia katikati ya marago
kwenye zamu ya asubuhi, wakawapiga Waamoni hata wakati wa jua kali; kisha ikawa wale waliosalia
wakatawanyika, hata wasiachwe wawili wao pamoja.
12 Ndipo watu walipomwambia Samweli, Ni nani yule aliyesema, Je! Huyo Sauli atatutawala? Walete watu
hao, ili tuwaue.
13 Lakini Sauli akasema, Hakuna mtu atakayeuawa leo, maana leo Bwana amefanya wokovu katika Israeli”.
Sasa tunaweza kuona hapo Roho ya Bwana pindi tu ilipomshukia Sauli alipatwa na Hasira kali. Na Tunafahamu hasira siku zote ikimwaka hata mtu yeyote huwa hajali ni madhara gani atakutana nayo, atapambana nayo kwa hali yoyote ilimradi tu atimize lengo lake, Sasa hii hasira iliyokuwa inamjia Sauli. Inayomfanya ashindwe kujitawala mwenyewe pindi imjiapo ambayo si kila wakati ilikuwa inamjia bali pale tu inapopaswa itimize kusudi fulani, ilitoka kwa Mungu mwenyewe. Hiyo ndio iliyowaokoa wana wa Israeli katika mikono ya maadui zao sikuzote, katika vita vigumu na vizito vilivyokuwa vinawajia waisraeli. Mungu alikuwa anaituma Roho yake kwa hasira nyingi juu ya Sauli, na bila kuogopa wala kujali lolote Sauli alishuka vitani kama simba na kusambaratisha maadui zao wote. Hapo ndipo hata mashujaa hodari wa vita wa Israeli ndipo walipokuwa wanamwogopea Sauli kwa Roho hiyo iliyokuwa juu yake.
Waamuzi 14:19 “Roho ya Bwana ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye akatelemkia Ashkeloni, akapiga watu waume
thelathini katika watu hao, na kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavao hayo.
Hasira zake zikamwaka, naye akakwea kwenda nyumbani kwa baba yake”.
Na ndivyo ilivyokuwa kwa mfalme Sauli, kwasababu alikuwa ametiwa mafuta na Mungu mwenyewe, Mungu alizielekeza HASIRA zile kwa kusudi maalumu la kuilinda Israeli dhidi ya madui zao, lakini wakati mfalme Sauli alipoacha kufuata njia za Mungu na kufanya vitu ambavyo Mungu hakuwa anamwagiza, ndipo Bwana akaghahiri kumtumia tena, hivyo akauamishia utawala wake kwa jirani yake Daudi. Lakini kumbuka Mungu hakumtoa Roho wake juu ya Sauli, isipokuwa roho ya utawala iliondolewa juu yake.
Hapo tunajifunza nini?. Mungu akishakutia mafuta, amekutia mafuta, hawezi kuyaondoa tena juu yako milele. Isipokuwa yataachwa tu yajiongoze kwa hisia zako na akili zako na sio tena kwa uvuvio au uongozi wa Roho Mtakatifu na hiyo ndiyo mbaya zaidi kwasababu ndio hapo mtu atatumia vipawa Mungu alivyompa kutimiza matakwa yake mwenyewe binafsi. Hilo ndio jambo lililomkuta mfalme Sauli baada ya Mungu kumrarulia ufalme na kumpa Daudi, kuanzia huo wakati mfalme Sauli akapoteza dira kabisa na mwelekeo wa kuitawala Israeli, akaanza kuzitumia nguvu zile za Hasira kuulinda ufalme wake na enzi yake badala ya kuilinda Israeli na ndio hapo akawa anamwinda Daudi siku zote, na hata wakati mwingine akiwa amestarehe tu nyumbani kwake kukiwa na amani, ile Roho pindi imjiapo, anajikuta anarusha rusha tu pasipo kujizuia ili tu amuue Daudi mtu asiyekuwa na hatia. Wakati hasira hizo zingepaswa zielekezwe kwa maadui wa Israeli.
Ni jambo hilo hilo lilimpata na shetani, baada ya shetani kushindwa kuilinda enzi yake Mungu aliyompa. Ambaye alikuwa ni kerubi aliyetiwa mafuta kuliko makerubi wote, yeye hakutaka kuenenda katika utaratibu Mungu aliomuwekea, Hivyo Mungu akaamua kuurarua utawala wake na kuwapa wengine. Lakini kumbuka kama tulivyoona Mungu akishakutia mafuta, hawezi kuyaondoa juu yako. Utaendelea nayo hivyo hivyo lakini yatakuwa hayaongozwi na Roho Mtakatifu bali kwa hisia zako na akili zako kujiundia ufalme wako.
Na ndio maana shetani mpaka sasa hajaondolewa nguvu zake alizopewa na Mungu, lakini sasa anazitumia kujiundia ufalme wake wa giza, ili kutimiza matakwa yake mwenyewe. Na hiyo ndiyo inayoitwa Roho mbaya kutoka kwa Mungu.
Vivyo hivyo na manabii wa uongo,na walimu wa uongo, na wachungaji wa uongo, na waimbaji wa uongo… waliopo leo, jambo ni lile lile, utakuta mwanzoni walitiwa kweli mafuta ya kundi la Mungu, walifundishe, walilishe, waliongoze katika njia njema..Lakini kwa jinsi siku zilivyozidi kwenda wakaanza kuyahalifu maagizo ya Mungu kidogo kidogo kama ilivyokuwa kwa mfalme Sauli. Na mwisho wa siku Mungu akaghahiri kuwaita Watumishi wake, hivyo ile Roho njema ya uongozi kutoka kwa Mungu iliyoachiwa juu yao kulilinda kundi la Mungu inawaacha, wanabakiwa tu na mafuta Mungu aliyowapa ili wajiongoze kwa tamaa zao wenyewe na sio kwa tamaa za Roho Mtakatifu.
Na ndio hapo utamwona mtu anajiita nabii anaona maono sahihi kabisa anatabiria watu mambo yajayo,na kweli yanatokea, lakini bado ni mwasherati, bado anaishi kidunia hawi tena kielelezo cha kuwapeleka watu mbinguni, utakuta badala awaelekeze watu kwa Mungu wao, anawaelekeza kwake, muda wote anajisifia yeye tu, utukufu wote wa Mungu anauchukua yeye, anasahau kuwa mafuta yale aliyopewa hayakuja kwa juhudu zake bali yalitoka kwa Mungu kwa kutimiza kusudi la kundi la Bwana, lakini yeye hajali hilo kwasababu Roho wa Mungu kashamwacha siku nyngi bali ile roho mbaya itokayo kwa Mungu ndiyo inayomwendesha mwisho wa siku anaishia kuleta madhara makubwa kwenye kanisa na kuhusika kuwapeleka watu wengi kuzimu, na kuwapoteza yamkini hata na wale walio wateule wa Mungu. Na siku zinavyozidi kuendelea utakuta yeye ndiye anayekuwa adui wa kwanza wa watumishi wa kweli Mungu kama Sauli alivyokuwa anafanya kwa Daudi.
Ndugu unayesoma, vipawa vya Mungu si vya kuvichezea. Kabisa, Mungu hadhihakiwi, usidhani kunena kwako kwa lugha ni ishara kuwa unaye Roho Mtakatifu, usidhani kuona kwako maono ni dalili kuwa unampendeza Mungu, usidhani kutoa kwako unabii ni ishara madhubuti kuwa upo katika mstari sahihi. Hayo yote hayakusaidii kitu kama hutasimama katika mstari wa Neno la Mungu. Biblia inatuambia
Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu ATAKAYEMWONA BWANA ASIPOKUWA NAO;”
Unaona, utafanya yote lakini kama utakatifu haupo ndani yako, ni mambo machafu tu yamejaa ndani yako, uzinzi,ulevi, anasa, pornography,miziki ya kidunia, mastubation,uchawi,ibada za sanamu, utukanaji n.k hayo yote, hata kama utakuwa unazungumza na malaika kila siku kiasi gani, mbingu hutaiona ndugu.
Embu tusiwe mojawapo ya hao walionza vizuri na kumaliza vibaya, embu tuiruhusu ile Roho njema tu ya Mungu ituongoze na sio fikra zetu ili mwisho wetu upate kuwa mzuri katika safari yetu hapa duniani.Kumbuka Bwana hampi mtu roho mbaya, isipokuwa sisi ndio tunayoitumia roho njema ya Mungu katika ubaya.
Bwana Yesu akubariki sana.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
JE! MTU ANAYETUNGISHA MIMBA KWENYE CHUPA MAHABARA, ANAHATIA MBELE ZA MUNGU?
JE! MABALASI BWANA YESU ALIYOYATUMIA KUGEUZIA MAJI KUWA DIVAI, YALITUMIKA TU KWA KAZI HIYO?
VITA VYA KIFIKRA BAADA YA KUZALIWA MARA YA PILI
Wakati tunakaribia kumaliza Mwaka ni kipindi maalumu sana cha kukaa na kutafakari na kuchukua hatua ya kumshukuru Mungu kwa Mengi aliyotutendea…Jambo kubwa la kuweza kumshukuru Mungu, ni juu ya pumzi aliyotupatia mwaka mzima, Katika safari ya mwaka mzima, kuna vipindi vingi tumepita lakini bado tunaishi..jua linachomoza na kuzama kila siku, hatujapitia matetemeko ya ardhi mwaka mzima, hatujapigana vita mwaka mzima, Mungu katuepusha na majanga mengi, katuepusha na magonjwa mengi, na hata tulipopata ugonjwa Bwana alituponya n.k Unafikiri ni kwasababu ya nani? Mpaka Mungu atuepushe na hayo yote?
si kwasababu tuna unafuu mbele zake, au kwasababu tunazingatia mlo kamili, wala si kwasababu tunajitunza sana na kujipenda, wala si kwasababu tunaustaarabu mzuri wa maisha, wala si kwaajili ya haki yetu sisi, wala si kwasababu sisi ni watakatifu, wala sio kwasababu tunabidii ya kumtafuta yeye, wala si kwasababu tunatenda mema sana, wala si kwasababu tunafunga sana, wala si kwasababu tunaomba sana, wala si kwasababu ni washirika wazuri wa kanisani au watoaji sadaka wazuri au wenye upendo sana.. Hakuna hata jambo moja kati ya haya ambayo Baba yetu wa mbinguni anayaangalia ili kutunyeshea sisi mvua yake, au kutupa pumzi, au kutupatia mema, au kutupatia uzima au kutuangazia jua lake, Hakuna hata moja!!
Sasa swali linakuja kama sio kwa ajili ya hayo yote, tunaumaliza mwaka salama..basi ni kwasababu gani? Kama si kwaajili ya utakatifu wetu, au bidii zetu, au juhudi zetu, au matendo yetu, au utakatifu wetu ni kwasababu gani basi tunapokea neema hii?.
Jibu ni rahisi, ni kwasababu ya haki ya mtu mmoja, ni kwasababu ya utakatifu wa mtu mmoja, ni kwasababu ya bidii ya mtu mmoja, ni kwasababu ya juhudi ya mtu mmoja, ni kwasababu ya matendo ya mtu mmoja, ni kwasababu ya maombi ya mtu mmoja, na huyo mtu ni BWANA YESU KRISTO, kwa huyo Baba wa mbinguni ndiye aliyependezwa naye.
Baba wa mbinguni hakupendezwa na maelfu waliopo duniani, hakuona mwenye haki hata mmoja duniani, wote tulikuwa tumetenda dhambi, tunakasoro nyingi, zisizokuwa na hesabu.
Zaburi 14: 2 “Toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja”.
Unaona! Sasa kama hakuna hata mmoja aliyemwona duniani mwenye haki??..unadhani vipi kama kuna ambaye angestahili kupokea baraka yoyote kutoka kwake?..hakuna hata mmoja..angestahili kupata pumzi kwa haki yake,wote tumestahili hukumu ya milele, Ndio maana inapasa atoke mtu mwingine kutoka mbinguni mwenye haki ambaye angestahili kupokea baraka kutoka kwa Mungu, kwasababu duniani hakuna hata mmoja mwenye akili, wote tumepungukiwa na utukufu wa Mungu..Hakuna hata mmoja mwenye unafuu.
Kwasababu hiyo basi kwa kuwa Yesu Kristo pekee ndiye aliyekuwa mkamilifu, ambaye hakutenda dhambi tangu kuzaliwa kwake mpaka ameondoka, yeye peke yake ndiye aliyehesabiwa haki kwa matendo yake binafsi, yeye peke yake ndiye Baba wa mbinguni aliyemwona mwenye AKILI anayemtafuta Mungu, alimchungulia toka juu akamwona akamtangaza “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” …hakusema hawa ndio wanangu wapendwa wangu..hapana bali “huyu ndiye”..maana yake yupo mmoja tu!! kwa haki yake amestahili kubarikiwa kwa kila namna. Ndugu mtu asikudanganye kwamba kuna wabarikiwa wengi..Mbarikiwa ni mmoja tu! Yesu Kristo.. Maandiko yanasema hivyo..
Mathayo 21:5 “Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda,
Na mwana-punda, mtoto wa punda.
6 Wale wanafunzi wakaenda zao, wakafanya kama Yesu alivyowaamuru,
7 wakamleta yule punda na mwana-punda, wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake.
8 Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani; na wengine wakakata matawi ya
miti, wakayatandaza njiani.
9 Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti, wakisema, HOSANA , MWANA WA DAUDI; NDIYE MBARIKIWA , yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni”.
Sasa basi kwasababu ni mmoja tu! Ndiye aliyestahili baraka, Yesu Kristo pekee asiyestahili kufa wala kuangamizwa milele…Yeye Yesu Kristo Bwana wetu alitununua sisi tusiokuwa wakamilifu kwa Baba wa mbinguni, akatushirikisha baraka zake alizobarikiwa na Baba wa mbinguni, akatuhusisha katika fadhili zake alizofadhiliwa na Baba, japokuwa sisi hatukustahili kubarikiwa, wala kupewa uzima, wala kuangaziwa jua..lakini sasa tunayapata hayo yote kupitia Yesu Kristo.
Kwasababu hiyo basi hata kipindi hichi tunachomaliza mwaka, kama bado tunaishi…tusijisifu ni kwa matendo yetu, sio kwa matendo yetu hata kidogo, bali kwa ajili ya matendo ya Yesu Kristo aliyoyaishi hapa duniani yaliyompendeza Baba..si kwa ajili tuna bidii za kujitunza hapana…wapo waliokuwa na bidii ya kujitunza sana lakini wameondoka..ni kwaajili ya Huruma ya Yesu Kristo juu yetu.
Sio kwasababu ya juhudi zetu, ndio tumebarikiwa na kupata mema ya nchi hapana ni kwasababu ya Mbaraka Bwana Yesu aliobarikiwa na Baba yake kwa haki yake..na sisi ndio tunaoushiriki . Yesu Kristo pekee yake ndiye Mbarikiwa, sisi ni kama waalikwa tu! Tumealikwa kwenda kula baraka za Yesu Kristo..Ndio maana na sisi tunajumuishwa kama miongoni mwa waliobarikiwa, lakini Mbarikiwa ni mmoja tu!
Kwahiyo ndugu, tukimfahamu Yesu Kristo kwa namna hiyo, hatuna budi kumshukuru Mungu kwa ajili yake, hatuna budi kunyenyekea sana na kumwambia Bwana Ahsante…Ni wakati wa kumshukuru Mungu kwa jambo moja moja alilotutendea kuanzia mwanzo wa mwaka huu hata mwisho. Hata kama bado ni mgonjwa mshukuru sana! Hata kama bado hukupata mwaka huu ulichokitamani, mshukuru tu Maadamu bado unaishi…Kwa wakati wake ukifika, atakutimizia matakwa yako.
Mshukuru kwasababu bado upo kwenye Imani, hujaanguka, shetani alikutafuta mwaka mzima kama simba angurumaye..Mshukuru kwasababu amekuepusha na yule mwovu..mshukuru kwasababu kama sio yeye kukubaliwa na Baba wa mbinguni usingekuwa hapo ulipo..kama sio yeye kuishi maisha makamilifu tangu anazaliwa mpaka anakufa usingepata hata hiyo pumzi, kama sio yeye kuwa mwenye akili ya kumtafuta Mungu, kwa kufunga na kuomba, na dua na sala nyingi…leo hii dunia pengine isingekuwepo, wote tungekuwa ni wana wa Jehanum ya moto.
Mshukuru kwa kila nyanja ya maisha yako, na pia mwombe Neema zaidi kwa Mwaka unaokuja, ukazidi kumtafuta yeye na kumsogelea zaidi, na kumjua yeye zaidi na uwezo wake, Akakupe Neema zaidi ya kuushinda ulimwengu na mambo yake, maana mambo ya ulimwengu huu yanapita, na yeye yupo mlangoni kurudi, na maandiko yanasema atakuja kama mwivi usiku wa manane!..Siku moja inapopita ndivyo tunavyokaribia mwisho, mwaka mmoja unapopita ndivyo siku ile tunavyozidi kuikaribia. Tumwombe Bwana neema na yeye atatusaidia..
Bwana akubariki sana!
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
KWANINI USIICHAGUE TUZO ISIYOHARIBIKA?
Tukisoma biblia hatuoni mahali popote ikitoa msisitizo juu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa au siku ya kufa kwa Bwana wetu YESU KRISTO. Kwamba ni jambo la lazima watu wote walifanye, au walizingatie kama sheria ya kidini, sasa swali linaweza kuulizwa kama ni hivyo basi hatupaswi kujiundia siku au kujiwekea utaratibu wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa au siku ya kufa kwa mwokozi wetu duniani, kwasababu maandiko yahatuagizi kufanya hivyo?.
Hilo swali ni rahisi kulijibu kama tutakaa na kufikiria juu ya maisha yetu ya kila siku. Embu jaribu kufikiria katika maisha yako tangu ulipozaliwa hadi sasa unavyoishi umeshawahi kualikwa katika sherehe za kuzaliwa za watu [Birthday] mara ngapi? Au umeshawahi kufanya sherehe ya kuzaliwa kwako mara ngapi?, au umeshawahi kusikia sherehe za kuzaliwa za watu wengine zikisheherekewa mara ngapi?. Ni wazi utafahamu kuwa aidha kama wewe hujawahi kufanya, au hujawahi kuthamini siku ya kuzaliwa kwako na hivyo huna mpango wa kujisumbua na mambo hayo fahamu kuwa hiyo haimzuii mwingine kutokuithamini siku yake ya kuzaliwa na kufanya sherehe kubwa na kuwaalika rafiki zake na ndugu zake baada ya kuona umuhimu wa kumshukuru Mungu kumwongezea mwaka mwingine wa kuishi duniani.
Vivyo hivyo tukirudi katika ukristo, hakuna sharti lolote lililotolewa na Mungu juu ya kusheherekea sikukuu yoyote ile, iwe ni ya pasaka, iwe ni ya pentekoste, iwe ni ya kuzaliwa kwa Bwana YESU, iwe ni ya kubatizwa , iwe ni ya kitu chochote kile hakuna sharti lolote tulilopewa. Lakini wapo wanaothamini mambo kama hayo katika maisha yao. Wapo wanaoona umuhimu wa kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa mfalme duniani miaka 2000 iliyopita, hivyo wanaona si vema wauache mwaka upite hivi hivi bila kutafuta au kuchunguza ni siku ipi inayoweza kukaribiana na siku Bwana aliyozaliwa ili waisheherekee. Kadhalika wapo wanaodhimisha siku ya kufa kwa Bwana, wanaona umuhimu wa kifo cha Yesu msalaba kilichowaletea wokovu na hivyo hawawezi kujizuia kufurahia na kushangalia kwa sherehe siku hiyo, wapo pia wanaodhimisha siku za kubatizwa kwao, siku ambayo walizaliwa mara ya pili. Wapo pia wanaodhimisha siku za Bwana kuwajibu maombi yako .N.k.
Lakini jambo linalowakwamisha wengi ni pale wanaposhindwa kutambua ni siku ipi hasa ambayo Bwana YESU aliyozaliwa na hiyo inawapelekea wafikiri wanaabudu miungu mingine hususani wanapoona tarehe 25 Disemba, anahusishwa na sikukuu ya kuzaliwa kwa miungu ya kipagani ya kirumi, ndipo wanapoona kuwa ni dhambi mbele za Mungu hata siku hiyo kumfanyia Mungu ibada.
Ni kweli tukichunguka katika maandiko tunaona kuwa Bwana Yesu hakuzaliwa tarehe 25 Disemba, kulingana na baadhi vifungu vinavyodokeza majira ya kuzaliwa kwake, kwamfano kama tukisoma kitabu cha Luka tunaona kuwa malaika Gabrieli alimtokea Zakaria kuhani (babaye Yohana mbatizaji) siku za zamu za ukuhani wa ABIYA.
Luka 1: 5 “Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti.
6 Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama.
7 Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana.
8 Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu,
9 kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba”.
Kumbe katika siku za zamu za Abiya ambazo alikuwa anafanya kazi za kikuhani ndizo Zekaria alizotokewa na malaika Gabrieli. Na hivyo tukirudi katika agano la kale kuangalia zama ya Abiya ilikuwa ni ya ngapi na inadondokea mwezi gani ndipo tutakapopata majibu ya majira ya kipindi ambacho Zekaria alitokewa na Malaika Gabrieli. Na kama tunavyosoma katika 1Nyakati 24. Inasema:
1Nyakati 24: 7 “Kura ya kwanza ikamtokea Yehoiaribu, na ya pili Yedaya;
8 ya tatu Harimu, ya nne Seorimu;
9 ya tano Malkia, ya sita Miyamini;
10 YA SABA HAKOSI, YA NANE ABIA;
11 ya kenda Yeshua, ya kumi Shekania;
12 ya kumi na moja Eliashibu, ya kumi na mbili Yakimu;
13 ya kumi na tatu Hupa, ya kumi na nne Yeshebeabu;
14 ya kumi na tano Bilga, ya kumi na sita Imeri;
15 ya kumi na saba Heziri, ya kumi na nane Hapisesi;
16 ya kumi na kenda Pethahia, ya ishirini Ezekieli;
17 ya ishirini na moja Yakini, ya ishirini na mbili Gamuli;
18 ya ishirini na tatu Delaya, ya ishirini na nne Maazia”.
Kwahiyo hapo tunaona zamu ya Abiya ilikuwa ni ya NANE katika ufanyaji wa kazi za kikuhani. Na kazi hizo zilikuwa zinafanyia sabato mpaka sabato yaani wiki mpaka wiki, hivyo zama ya Abiya iliangukia wiki ya 8 katika utendaji kazi wa kikuhani. Na tunajua kuwa mwaka wa kiyahudi huwa unaanza mwanzoni mwa mwezi april, na hivyo ukihesabu hapo majuma mawili utaona zamu hiyo inadondokea katikati ya mwezi wa 6. Kwahiyo tunaona hapo Zekaria kumbe alitokewa majira ya mwezi wa 6 na muda mfupi baada ya hapo pengine mwezi wa 6 mwishoni au wa 7 mwanzoni mkewe Elizabethi alipata mimba, na biblia inatuambia pia miezi 6 baada ya kupata mimba kwake Elizabethi Malaika Gabrieli alimwendea Bikiria Mariamu na kumpasha habari za yeye kupata mimba ya Bwana Yesu (Luka 1:26).
Hivyo mpaka hapo tunaona ni mwezi wa 12 katikati au wa kwanza mwanzoni ndipo mimba ya Bwana YESU ilipotungishwa. Na tunajua kuwa baada ya miezi 9 mtoto huwa ndio anazaliwa, sasa ukipiga hesabu utaona kuwa uwezekano mkubwa wa kuzaliwa kwa Bwana wetu YESU KRISTO unaweza angukia katikati ya mwezi wa 9 au mwanzoni mwa mwezi wa 10, kwa kalenda yetu sisi. Na ndio maana utaona pia Bwana Yesu alianza kuhubiri akiwa na miaka 30 na akamaliza akiwa na miaka 33 na miezi 6, na siku aliposulibiwa ilikuwa ni Mwezi wa nne (April). Kwahiyo ukihesabu vizuri hapo utagundua alianza kuhubiri kati ya mwezi wa 9 hadi wa 10, ambao ndio mwezi aliozaliwa.
Zipo pia thibitisho nyingine zinaonyesha kuwa Kristo alizaliwa majira hayo lakini hatuwezi kuziandika zote hapa. Lakini je! wanaodhimisha siku hiyo tarehe 25 Disemba wanafanya makosa?. Jibu ni hapana kama tulivyotangulia kuona biblia haijatoa amri juu ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Yesu mahali popote, na hivyo yeyote anayefanya hivyo ikiwa ni kwa lengo lake binafsi kwamba anaona umuhimu wa kuunda siku yake inayoweza kukaribiana na siku ya kuzaliwa kwa Yesu ili amtukuze na kumfurahia Mungu, Iwe ni Aprili, iwe ni Agosti, iwe ni Septemba, Iwe ni Octoba, Iwe ni Disemba iwe ni siku yoyote ile hatendi dhambi maadamu kaiweka wakfu kwa Mungu wake, ili kumwabudu na kumshukuru.
Dhambi inakuja ni pale siku kama hiyo ambayo tayari umeshawakwa wakfu kuwa ibada kwa Mungu, halafu siku hiyo inageuzwa na kuwa siku ya kufanya sherehe za ulafi, ibada za sanamu,ulevi, pombe, anasa, uasherati n.k. hiyo ni sawa na kumkufuru Mungu moja kwa moja, na dhambi ya kumkufuru Mungu ni dhambi ya juu sana kuliko dhambi zote. Ni heri kama usingeichukulia kama ni sikukuu ya imani yako, kuliko kuiona hivyo halafu bado unainajisi. Hiyo ni sawa imeiweka nadhiri kwa Bwana halafu umeshindwa kuitoa.
Utakuta mtu ametoka kanisani siku hiyo, pengine hata kashiriki meza ya Bwana, na anajua kabisa siku kama hiyo inapaswa iwe takatifu, kama ni kusheherekea isheherekewa kwa upendo wa Kristo, isheherekewe kwa kuzingatia vigezo vya utakatifu na biblia, lakini badala yake mtu akitoka hapo na kwenda kunywa pombe, na kwenda kuzini, na kwenda kuzurura kwenye vikundi vya ngoma na disco, na kwenda kuabudu sanamu na kuzunguka kwa waganga, kuna hatari kubwa sana. Na Hivyo siku hiyo kwake inageuka kuwa ni laana badala ya Baraka.
Ndugu yangu upo sasa katika majira haya yanayoitwa ya sikukuu, embu kama umependa kuzifanya kuwa ni za Kristo, zifanye ziwe hivyo kweli kweli, uzilinde, na kuzifanya takatifu, vinginevyo itakuwa ni ibada ya kipagani kwako zaidi hata ya hao wapagani wenyewe. Ni maombi yangu wewe kama mkristo utapata akili katika hayo, kumbuka ni majira unayokwenda kuvuka mwaka, mambo mengi Mungu amekuepushia mabaya, tafakari miezi yote hiyo umevukishwa salama, hivyo usimalize mwaka wako vibaya kwa Bwana. Huu ni wakati wa kujinyenyezeka ili Mungu akupe rehema za Mwaka unaoanza.
Mungu akubariki sana.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Nikutakie sikukuu njema, na Heri ya Mwaka mpya katika jina la YESU KRISTO BWANA WETU.