Kuna gharama kubwa sana katika kuupata ufalme wa mbinguni kama Bwana Yesu alivyotangulia kusema kwenye Mathayo 11:12 “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka. ” Hii ikiwa na maana kuwa ufalme wa mbinguni ni kitu kinachogombaniwa kwa nguvu na watakaokipata ni wachache. Na kumbuka NGUVU zinazozungumziwa hapo sio nguvu za kimwilini, Tukisoma..
Mathayo 13:44-46 “44 Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda AKAUZA ALIVYO NAVYO VYOTE, akalinunua shamba lile.
45 Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri;
46 naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda AKAUZA ALIVYO NAVYO VYOTE, akainunua. “
Bwana Yesu alifananisha ufalme wa mbinguni na maisha yetu tunayoishi kila siku, kama tukisoma hiyo mifano hapo juu tunaona kuna mfanya biashara aliyekuwa anatafuta lulu nzuri ya thamani kubwa, na alipoiona akaipenda sana, pengine hakuwa na fedha za kutosha, kuinunua kutokana na gharama ya LULU hiyo ilivyokuwa na thamani kubwa, lakini kwasababu ni mfanya biashara, alitafakari sana, kwamba japo inauzwa kwa thamani nyingi, lakini akiipata ataweza kuiuza mahali pengine kwa gharama kubwa zaidi, Hivyo atarudisha fedha aliyoinunulia pamoja na faida nyingi juu yake.
Kwasababu hiyo basi ilimpasa aende kuuza kila kitu alichokuwa nacho pengine hata nyumba yake, na miradi yake yote, ilimradi tu afikie kiwango kile cha pesa akainunue lulu ile yenye thamani kubwa.
Labda pengine alivyodhamiria kufanya hivyo, alionekana mwendawazimu mbele za watu kuuza mali alizozitaabikia kwa muda mrefu, lakini kwasababu ni mfanya biashara alifahamu ni kitu gani anafanya.
Vivyo hivyo na yule mwingine aliyeona hazina iliyositirika katika shamba na kwenda kuuza vyote alivyonavyo hakuwa mwendawazimu, pengine aliiona ALMASI imejichimbia katika kiwanja cha jirani yake, hivyo ili aweze kuipata ni sharti kile kiwanja kiwe chake, ili awe na ruksa ya kuifukua,
Sasa kwa ujanja, akaenda kumshawishi mwenye kiwanja amuuzie hata kwa bei mara 10 ya bei halisi ya kiwanja kile ili aweze kukipata kwa haraka na bila ya usumbufu , kwa kuwa mtu huyo anajua ni kitu gani anachokifanya, akaamua akauze kila kitu alichokuwa nacho, pengine mifugo yake, au majumba yake, au magari yake, na kama fedha isingetosha angeweza hata kwenda kukopa ili atimize lengo lake la kupata kiwanja kile.
Lakini kwa namna ya kawaida watu wangemuona kama amelogwa, au amerukwa na akili, kugharimikia kitu kisichokuwa na faida, lakini yeye hakuona tu kiwanja, bali aliuona UTAJIRI mkubwa zaidi ya kile kiwanja.
Mifano hiyo hiyo inatufundisha sisi kama wanadamu, HATUTAWEZA KUUPATA UFALME WA MBINGUNI, KAMA BADO HATUJAJUA THAMANI YAKE. Kumbuka yule mfanyabiasha hakuona tu lulu bali aliona thamani kubwa iliyopo ndani ya lulu, ndiyo ikamgharimu kuuza kila kitu, vivyo hivyo na yule aliyenunua shamba, hakuona tu shamba, bali aliona thamani ya kitu kilichokuwa kimejificha ndani ya lile shamba na ndipo gharama za kukipata hicho kitu zinajitokeza.
Na katika ufalme wa mbinguni, usiuone tu ufalme wa mbinguni halafu basi, bali tazama thamani na utajiri ulioko ndani ya huo ufalme, ukishalifahamu hilo au kupata ufunuo huo utakuwa na nguvu za kuchukuliana na gharama zozote utakazokumbana nazo kwa furaha zote.
Tukirudi kwa kijana mmoja aliyeitwa Musa, tunaona alizaliwa katika makasri ya kifalme ya FARAO, aliyekuwa msomi, na mtawala mwenye cheo, pamoja na mali nyingi, lakini ilifika wakati neema za Mungu ilifunguliwa machoni pake,na kuuona uzuri ulio katika ufalme wa mbinguni, hivyo kwa furaha yote aliamua kuuza kila kitu alichokuwa nacho ili aupate ,alidharau elimu yake ya kipagani, alidharau cheo chake kama mfalme mrithi, alidharau anasa na fahari alizokuwa anazipata katika jumba la kifalme, ili tu aupate ufalme usioharibika wa mbinguni..
Mtume Paulo aliandika katika.Wabrania 11:24 Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;
25 akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;
26 AKIHESABU YA KUWA KUSHUTUMIWA KWAKE KRISTO NI UTAJIRI MKUU KULIKO HAZINA ZA MISRI; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.
27 Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana. “
Tunaona hapo Musa alihesabu kushutumiwa kwake Kristo ni Utajiri mkuu kuliko hazina zote za Misri, ilimpasa AUZE baadhi ya mambo, ili aweze KUUNUNUA ufalme wa mbinguni, aliuona utajiri mkubwa huko mbeleni kuliko hazina zote za Misri, Ilimpasa auze umaarufu wake, ilimpasa auze anasa zake, ilimpasa auze ujana wake, ilimpasa auze kiburi chake, ilimpasa auze fashion zake, ilimpasa auze majigambo yake na ujuzi wake, ilimpasa auze dhuluma yake, ili aweze kufikia viwango vya kuununua ule UFALME WA MBINGUNI.
Vivyo hivyo na mtume Paulo mwenyewe aliingia gharama hizo hizo..ukisoma Wafilipi 3:7-8 inasema..
” Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama “MAVI” ili nipate Kristo; “
Paulo ambaye alikuwa ni msomi mwenye cheo na kiburi alihesabu mambo yote kuwa kama mavi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni, kumbuka kilichomfanya achukue uamuzi huo sio tu kwasababu ni neno “ufalme wa mbinguni” , hapana bali ni UTAJIRI aliouna angeupata katika huo ufalme.Na kwa kufunuliwa na Roho Paulo alifika wakati na kusema
Warumi 8:18-19
18 Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama UTUKUFU ULE UTAKAOFUNULIWA KWETU.
19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu.
Hivyo ndugu fungua macho yako uone thamani na utajiri mkubwa ulio katika huo ufalme, ndipo utakapoona sababu ya kuacha kila kitu kisichompendeza Mungu kwa furaha zote na kumwandamia Mungu kwa hali zote,. Kumbuka thawabu za UFALME WA MBINGUNI, zitakazokuja huko ni mambo mazuri ambayo biblia inasema katika..1Wakoritho 2:9 “lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,)
Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. “, pia usisahau, kutakuwa na wafalme na wenye mamlaka kubwa, pamoja na makuhani wa Mungu hawa watakaa pamoja na Kristo na kuhudumu pamoja naye, na huko watakuwepo pia watu wa kawaida tu, thawabu zitatofautiana sana, na ni milele, ikiwa na maana kuwa kama wewe ni mdogo kule utabaki hivyo hivyo milele, na kama wewe ni mfalme kule utadumu mfalme milele, na Bwana wetu YESU KRISTO akiwa kama MFALME WA WAFALME.
Jina la BWANA YESU LIBARIKIWE.
Kuna wakati mitume walimuuliza Bwana..
Mathayo 19:27 “Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?
28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. “
Hivyo wale watakaoketi karibu na Bwana ni wale tu, walioona thamani na kuingia gharama za kuununua ufalme wa mbinguni, je! ufalme huu unathamani gani kwako? , wewe mwanamke hauwezi ukaacha fashion na kuvaa hivyo vimini na suruali, kwasababu hauoni faida yoyote ya kuacha kufanya hivyo, mwanamume hauwezi kuacha pombe na sigara kwasababu kwako ni sawasawa ni biashara isiyo na faida, hauwezi kuacha uasherati, wizi kwasababu faida ya ile LULU(UFALME WA MBINGUNI) haijafunuliwa machoni pako. Laiti ungeifahamu thamani ya LULU usingefanya hivyo.
Lakini kumbuka wana wa Mungu, sio wajinga kuwaona wanauza mambo ya ulimwengu huu sasa ivi ili wanunue mambo ya ulimwengu unaokuja, ni kwasababu wanaona mbele, na kujipenda na wanapenda maisha ndio maana wanatafuta maisha ya milele yanayodumu, na wanapenda furaha zaidi hata ya wewe unayejiona unajistarehesha katika anasa za ulimwengu huu.
Kanisa tunaloishi ndilo la mwisho linalojulikana kama LAODIKIA kulingana na Kalenda ya Mungu, na ujumbe wetu tuliopewa umeandikwa katika kitabu cha Ufunuo 3:14 unasomeka hivi..
“Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
18 Nakupa shauri, UNUNUE KWANGU DHAHABU ILIYOSAFISHWA KWA MOTO, UPATE KUWA TAJIRI, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.”
19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.
22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. “
Bwana ametupa shauri tukanunue dhahabu kwake tupate kuwa matajiri, kumbuka ili KUNUNUA lazima TUUZE yote maovu tulionayo ili tuweze kukidhi viwango vya kuupata ufalme wa mbinguni. Maombi yangu ni Bwana akupe neema ya kuona THAMANI YA UFALME WA MBINGUNI kwasababu UFALME WA MBINGUNI unapatikana kwa nguvu, na wenye nguvu ndio wanaouteka.
Mungu akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Kwa maombezi/Ushauri/Ubatizo/ Whatsapp. Tupigie namba hizi: +255693036618
Mada Nyinginezo:
UFALME WA MUNGU HAUPATIKANI KIRAHISI.
AYUBU 28 : HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?
Kama tunavyofahamu wakati wa usiku kabla hatujalala, huwa ni lazima tufunge milango yetu yote, kwa makufuli na makomeo, na hii sio kwasababu tunapenda kujifungia tu hapana! bali ni kujiweka katika hali ya usalama dhidi ya WEZI usiku, Kwasababu hatujui ni wakati gani wataingia na kuleta madhara. Hii ni desturi kwa kila mtu,hakuna mtu asiyefahamu kuwa anapaswa kufunga milango yake wakati wa usiku.
Lakini pamoja na hayo kufunga mlango tu na kwenda kulala haitoshi, kwasababu mwizi anajua kabisa akienda atakutana na changamoto ya milango kufungwa hivyo atakuwa amekwisha jipanga kwa njia mbadala ili kuhakikisha kuwa zoezi lake la kuiba linafanikiwa kikamilifu, hivyo ni dhahiri kuwa atakuwa na vifaa husika vya kuvunjia nyumba.
Kwahiyo ili mwenye nyumba aweze kunusuru mali zake au roho yake sio tu KUBANA MILANGO yake bali anapaswa pia AKESHE, Kwasababu mwizi hawezi kuharibu kama mwenye nyumba yupo macho. Hivyo dawa pekee ya kudhibiti wizi usiku ni kubana milango pamoja na KUKESHA.
Ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Bwana Yesu Kristo,akifananisha kuja kwake na kama ujio wa mwizi wakati wa usiku alisema …
Mathayo 24:40-44″ Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;
41 wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.
42 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.
43 Lakini fahamuni neno hili; KAMA MWENYE NYUMBA ANGALIIJUA ILE ZAMU MWIVI ATAKAYOKUJA, ANGALIKESHA, wala asingaliiacha nyumba yake KUVUNJWA.
44 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa damu yuaja.
Tukisoma pia katika
Marko 13:32 Bwana Yesu alisema maneno haya: Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.
33 Angalieni, KESHENI, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.
34 Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe.
35 Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, KWAMBA NI JIONI, AU KWAMBA NI USIKU WA MANANE,au AWIKAPO JIMBI, au ASUBUHI;
36 asije akawasili ghafula akawakuta mmelala.
37 Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, KESHENI.”
Kumbuka hapo Bwana Yesu hakusema “fungeni milango” bali alisema “kesheni” kwasababu inajulikana ni wajibu wa kila mtu kufunga milango yake, na kufunga milango ina maana kujiona umeokoka lakini maisha yako hayaendani na ukristo,umebatizwa na unaenda kanisani lakini umelala katika roho(vuguvugu), nje milango imefungwa lakini ndani umelala kwasababu hiyo basi mwizi atakapokuja hautajua lolote.
Mkristo aliyeridhika na dhehebu lake au mapokeo yake lakini hazingatii mambo ya muhimu yanayohusiana na wokovu wake na maisha yake ya umilele ni sawa na mtu aliyejifungia na kulala usingizi.
Dunia sasa hivi ipo katika GIZA NENE SANA ikiashiria kwamba huu ni wakati wa USIKU na ndio wakati uliokaribia wa BWANA kurudi tena, kuongezeka kwa maovu ulimwenguni kama vile anasa,ulevi,uasherati uliokithiri hususani katika ulimwengu huu wa sasa wa utandawazi,mauaji,uchawi,rushwa,dhuluma, kupenda ulimwengu zaidi ya Mungu,n.k. vinawafanya watu wazidi KULALA usingizi wa mauti, na jinsi giza linavyozidi kuongezeka ndivyo wakristo nao wanavyozidi kushawishika kulala.
Sasa katikati ya kilele hichi cha maovu hapo ndipo Kristo atakaporudi, alisema kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu watu walikuwa wakila na kunywa(ikiashiria kufanya anasa),walikuwa wakipanda na kujenga, hata siku ile ikawajilia kama ghafla, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake mwana wa Adamu.
1Thesalonike 5:1 Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.
3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.
4 Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi.
5 Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.
6 Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.
7 Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku.
8 Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu. “
Bwana Yesu pia alisema..
Ufunuo 16:15 “(Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.) “.
Kukesha kunakozungumziwa ni KUKESHA KATIKA ROHO, kutokulala katika roho, kudumu katika utakatifu,huku matunda ya roho yakijidhihirisha upole,kiasi,upendo,uvumilivu,n.k pamoja na kuishi maisha ya kama mtu anayemngojea Bwana wake, kama msafiri duniani, asiyefanana na watu wa ulimwengu huu waliousingizini, huku macho yake yakitazama mambo ya mbinguni yanayokuja,
Utajisikiaje siku hiyo utakapoona wenzako wamekwenda kwenye unyakuo na wewe umebaki? ni uchungu usioneneka, mara nyingine Mungu anawaotesha watu ndoto kwamba unyakuo umepita na wenyewe wamebaki, hapo ni Mungu anajaribu kuwakumbusha watu kwamba maisha yao hayajakidhi vigezo vya kwenda mbinguni.Huu ni wakati wa kuamka usingizini biblia inasema..katika Waefeso 5:14 “Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.”
Amka ndugu utoke katika usingizi wa wafu wa ulimwengu huu, uasherati ni usingizi,kiburi cha uzima ni usingizi,ulevi,sigara,anasa,fashion,ushirikina,usengenyaji,rushwa,ulawiti,utoaji mimba,wizi,utukanaji vyote hivi ni usingizi wa kiroho, na kumbuka siku Kristo atakapokuja kulichukua kanisa lake hawa hawatajua lolote badala yake watabaki hapa wakingojea ile SIKU KUU YA BWANA inayowaka kama tanuru ndivyo biblia inavyosema,
2 Petro 3:10 “Lakini siku ya Bwana ITAKUJA KAMA MWIVI; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.
11 Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo,IMEWAPASA NINYI KUWA WATU WA TABIA GANI KATIKA MWENENDO WENU MTAKATIFU NA UTAUWA,
12 mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? “.
Kwa kuwa sisi sote hatujui ni saa gani Bwana atakayokuja , ni wajibu wa kila mtu aliye mkristo kukesha kwa kuishi maisha ya uangalifu katika giza hili nene lililopo dunian sasa.
Mungu akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Kwa maombezi/Ushauri/Ubatizo/ Whatsapp. Tupigie namba hizi: +255693036618
Mada Nyinginezo:
JINSI ITAKAVYOKUWA KATIKA SIKU ILE
LENGO LA SHETANI KWA WATOTO WA KIZAZI HIKI.
UKOMA NA UJANE ULIO NDANI YAKO, UMEUPATIA TIBA?
BWANA ALIPOSEMA KUWA YEYE NI “MUNGU WA MIUNGU” ALIKUWA NA MAANA GANI?..JE! YEYE NI MUNGU WA SANAMU?
Bwana alituweka duniani kila mmoja wetu tumzalie matunda, na kuna matunda ya aina mbili
1) Matunda ya Haki: (Wafilipi 1:11, wagalatia 5:22) nayo ni upendo, furaha, utu wema, kiasi, uvumilivu, upole, amani, fadhili, n.k. ambayo kwa ujumla tunaita ni UTAKATIFU.
2) Matunda ya kazi ya Mungu: Ambayo ni kuwavuta watu wa Kristo, kwa njia mbalimbali za kuhubiri, kufundisha, na kuhudumu, nk.
Biblia mahali pengine imefananisha matunda haya yote kama “TALANTA”. Tukisoma mfano Bwana Yesu aliowapa wanafunzi wake kwenye
Mathayo 25:14-30″
14 Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake.
15 Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.
16 Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano.
17 Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida.
18 Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake.
19 Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao.
20 Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida.
21 Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.
22 Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida.
23 Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.
24 Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya;
25 basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako.
26 Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya;
27 basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.
28 Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi.
29 KWA MAANA KILA MWENYE KITU ATAPEWA, NA KUONGEZEWA TELE; LAKINI ASIYE NA KITU, HATA KILE ALICHO NACHO ATANYANG’ANYWA.
30 Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.”
Mfano huu ni dhahiri unajulikana kuwa moja kwa moja unalenga katika kuifanya kazi ya Mungu kwa karama mtu aliyopewa, kama amepewa karama ya aulimu, au amepewa karama ya kichungaji, au karama ya kinabii au uinjilisti au nyingine yoyote ni jukumu lake kuitumia kuwavuta watu kwa Kristo ili siku ile Bwana atakapokuja na kumuuliza mtu huyo umemzalishia vingapi aweze kumpa vya kwake na vya ziada.
Lakini pia tafsiri kuu ya mfano huu, TALANTA haimaanishi karama peke yake, bali pia hata KILE MTU ANACHOSIKIA ni talanta. Unapohubiriwa NENO la Mungu hiyo ni talanta imepandwa moyoni mwako na Bwana ataihitaji ya kwake pamoja na ya ziada katika siku ile ya hukumu kwa yote uliyoyasikia.
Kama ukisoma kwa makini mstari wa 29 unasema “Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.”
Mstari huu huu umejieleza zaidi kwenye
Mathayo 13:2-13″ unasema…”Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani.
3 Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda.
4 Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila;
5 nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina;
6 na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka.
7 Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga;
8 nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini.
9 Mwenye masikio na asikie.
10 Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano?
11 Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa.
12 KWA MAANA YE YOTE MWENYE KITU ATAPEWA, NAYE ATAZIDISHIWA TELE; LAKINI YE YOTE ASIYE NA KITU, HATA KILE ALICHONACHO ATANYANG’ANYWA.
13 Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. “
Bwana Yesu mara nyingi alipokuwa akiwafundisha makutano, hakuzungumza nao moja kwa moja, kwa kufafanua mambo, bali kama kwa njia ya mafumbo, hivyo wengi walikuwa wakitoka na maswali mengi kichwani, au wengine hawakumuelewa kabisa, na wengine walimwona kama vile mtunga hadhithi tu zisizo na maana, lakini alifanya hivyo kwa makusudi ili ajue ni wangapi walio tayari kujifunza , na ndio maana tunaona baada ya kumaliza ile mifano ni kikundi cha watu wachache tu(wanafunzi wake) kati ya maelfu kilichoenda kumuuliza tafsiri ya ile mifano yote aliyokuwa anazungumza,
Na ndipo hapo anapowafunua macho yao na kuwaelewesha tafsiri ya mifano ile na kuponyeka roho zao, bali wale wengine waliosalia ambao hawakutaka kujifunza zaidi kwao ilikuwa ni kama hadhithi tu. Na mahali popote Bwana alipokuwa akifundisha kwenye makutano mengi hiyo ndiyo ilikuwa desturi yake. Na ndivyo anavyofanya hata sasa.
Jambo la kujifunza ni kwamba hawa wanafunzi walipopewa talanta za Neno la Mungu mikononi mwao kwa ile mifano, hawakuenda kuichimbia chini(yaani kuridhika na mifano ile), badala yake walikwenda kuifanyia biashara ili wanufaike, pale walipokwenda kumuuliza Bwana tafsiri ya mifano ile.
Na hao ndio pekee waliozidi kuimarika na kukua kiroho siku baada ya siku kwa kuzijua siri za Mungu, wakifananishwa na mbegu zile zilizotupwa katika udongo mzuri, zilizozaa moja 30, nyingine 60 na nyingine 100, lakini wale wengine walifananishwa na zile mbegu zilizoangukia njiani, na kwenye miamba na kwenye miiba ndege walipopita wakazila, jua lilipokuwa kali zikaungua, na mwamba ulipokuwa mgumu zikasinyaa kwa kukosa mizizi hawakuzalisha chochote.
Hawa ni mfano ya watu wasiotumia talanta zao vizuri (yaani kusikia NENO la Mungu), wale wa kwenye njia ndio wale wanaosikia Neno la Mungu kila siku likihubiriwa lakini wanalizembea kulitendea kazi au pengine hawajalielewa vizuri, kwao limekuja tu kama fumbo badala waendelee kutafuta kujua zaidi wao wanaliacha ,
Maana biblia inasema “kila atafutaye ataona” kama ulivyo mfano wa wale makutano ambao mwisho wa siku shetani anapata nafasi ya kulichukua mioyoni mwao na kulisahau, ni mara ngapi umesikia ukihubiriwa Neno la Mungu ubadilike lakini haubadiliki?, umefundishwa usivae vimini, hata kama haujalielewa au linakuchanganya je! ulishawahi kukaa na kumuuliza Mungu una maana gani kukataza mwanamke kuvaa suruali au kuweka make-up na kuvaa vimini??. Hiyo TALANTA uliyopewa na Mungu kwa kuhubiriwa umeitumiaje??..Ni dhahiri kuwa umeifukia chini na katika siku ile ya Hukumu utatoa hesabu yake.
Umehubiriwa mara nyingi uache uasherati, ulevi, usengenyaji, ushirikina, lakini huachi ulishawahi kukaa na kwenda kukufanyia kazi hicho ulichoambiwa? kumbuka hiyo ni talanta uliyopewa kwa kuhubiriwa Injili itatakwa na ya ziada siku ile ya hukumu.
Umefundishwa utukanaji, wizi, uvutaji sigara, utoaji mimba,usagaji, kutazama pornoghaphy, musterbation ni dhambi, talanta hizi zote zilipandwa ndani ya moyo wako kwa mafundisho mbalimbali uliyoyasikia ya Neno la Mungu, pengine mengi yalikuacha njia panda lakini je! ulishawahi kutenga muda na kwenda kumuuliza Mungu au kutaka kujua zaidi kama ni kweli au sio kweli, lakini umepuuzia kama yale makutano yalivyofanya. TALANTA hiyo itatakwa siku ile ya Hukumu.
Umesikia Neno la Mungu limepiga kelele masikioni mwako kwamba kuabudu sanamu, kusali rozari, mafundisho ya kwenda toharani na ibada za wafu ni mafundisho potofu yanayawapeleka mamilioni kuzimu, pengine uliposikia mara ya kwanza kwako ilikuwa kama ni kitendawili lakini je! ulishawahi kutenga Muda na kumuuliza Mungu je! mambo hayo ni kweli kuliko kupuuzia au kubisha, Kumbuka hiyo ni TALANTA ambayo Bwana alikupa moyoni mwako na usipoizalisha utaulizwa katika ile siku ya Hukumu.
Lakini kama ungependa kujifunza na kuyatendea kazi yale unayohubiriwa au kufundishwa..Bwana anasema: “KWA MAANA YE YOTE MWENYE KITU ATAPEWA, NAYE ATAZIDISHIWA TELE;”. Hivyo ungejikuta hata yale uliyokuwa huyajui Bwana anakuongezea na mengine mengi, Neno la Mungu linajifunua kwako , na kujikuta unaimarika kiroho siku baada ya siku.
Kwahiyo cha muhimu sana ni kuzingatia “kile unachokisikia” na kukifanyia kazi kwa bidii adui asije akakichukua hata hicho kidogo Mungu alichokupa neema ya kukisikia kikapotea moyoni mwako. Kwasababu alisema…
Marko 4:24 … ANGALIENI MSIKIALO; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa.25 Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. “
Maombi yangu ni uanze kukitendea kazi kile ulichokisikia tangu zamani, ili atakapokuja aone matunda ya kusikia kwako Neno lake.
Mungu akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Kwa maombezi/Ushauri/Ubatizo/ Whatsapp. Tupigie namba hizi: +255693036618
Mada Nyinginezo:
ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO
NINI MAANA YA HILI ANDIKO “USHUHUDA WA YESU NDIO ROHO YA UNABII” (UFUNUO 19:10)?
BWANA ALIPOSEMA “SIKUJA KUTANGUA TORATI BALI KUITIMILIZA” ALIKUWA ANAMAANISHA NINI?
Luka 23:32 “Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye.
33 Na walipofika mahali paitwapo FUVU LA KICHWA, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. “
Zamani zile tunafahamu utawala wa kikatili wa kirumi, uliua watu wengi kwa kuwatundika katika miti na misalaba, uliosambaa karibia ulimwenguni kote, na Israeli pia, Lakini tunaona wakati wa kumsulibisha Bwana wetu Yesu Kristo walimchukua na kumpeleka mahali panapoitwa FUVU LA KICHWA, Lakini swali la kujiuliza ni kwanini asipelekwe mahali pengine kama vile bethania, au Emau, badala yake walimpeleka mahali panapoitwa FUVU LA KICHWA.?
Vitu hivi vinafunua mambo ya rohoni, kuashiria kwamba kabla Kristo hajapandishwa msalabani tayari walishamsulibisha katika VICHWA vyao,Kupandishwa msalabani ni matokeo tu ya kitu kilichokuwa ndani , walishamkataa tangu siku nyingi na ndio maana biblia inasema Yohana 3:19 Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. “
Unaona hapo NURU ilikuja lakini waliipinga. Bwana alikataliwa tangu kuzaliwa kwake kama tunavyosoma katika maandiko habari hizo zilimfadhahisha Herode pamoja na Israeli yote. Alipingwa na viongozi wa dini pamoja na jamaa zake wakaribu, huko ndiko kumsulibisha Kristo katika vichwa vyao.
Isaya 53:3 Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.4 Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.
Ni rahisi kusema ningekuwepo kipindi kile cha Bwana Yesu kamwe nisingeshirikiana nao kumsulibisha Bwana, Lakini ukweli ni kwamba Kristo anasulibishwa mpaka leo, na jambo hili linaanzia katika VICHWA VYA WATU.
huwezi kusema moja kwa moja unamsulibisha Kristo lakini ulishamsulibisha Katika KICHWA CHAKO, kwa kulikataa Neno La Mungu lilipokuwa linalia ndani ya moyo wako, Kutoa maneno ya kijeli na mizaha juu ya jina la Bwana( maneno kama ” eti unakuja umekuwa Yesu?), ni kumsulibisha Kristo, unapoambiwa ukweli na moyoni unajua kabisa ni kweli lakini unapinga kama wale mafarisayo ni sawa na kumsulibisha Kristo huna tofauti na watu wa kipindi kile, n.k.
Huu ni wakati wa kufungua moyo wako, Kristo ayafanye maisha yako kuwa mapya, badilisha fikra zilizo ndani ya fuvu la kichwa chako, kwa kulitii NENO la Mungu uokolewe uishie maisha ya yakumpendeza yeye, ili jambo lile lisikutokee kama lilivyowatokea wale watu wa wakati ule.
Ubarikiwe.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Kwa maombezi/Ushauri/Ubatizo/ Whatsapp. Tupigie namba hizi: +255693036618
Mada Nyinginezo:
NJIA YA BWANA INATENGENEZWA WAPI?
KWANINI BWANA YESU ALISEMA PALE MSALABANI NAONA KIU?
BIBLIA INAMAANA GANI KUSEMA “VILIVYOTAKASWA NA MUNGU, USIVIITE WEWE NAJISI”?
Kuna NJIA za kufikia kila jambo, ambayo Mungu tayari alishaziweka tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, kwa mfano ili mwanadamu amfikie Mungu, tayari njia ilishaandaliwa, nayo ni YESU KRISTO, (Yohana 14:6″ Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”. ), watu wengi wanapotea wakidhani au wakijifariji kuwa zipo njia nyingi mbalimbali za kumfikia Mungu na zote zinaishia sehemu moja, kwamba unaweza ukawa muhindu, au m-muhamedi au m-budha n.k. na bado ukafika kwa Mungu. Huo ni uongo NJIA ni moja tu (nayo ni YESU KRISTO) na Mungu alishaitengeneza na hakuna mikato. Hivyo kama unataka kumfikia Mungu ni sharti upitie hiyo, nyingine zote zinapotosha.
Vivyo hivyo pia katika kufikia BARAKA fulani za MAISHA, Kuna njia ambazo Mungu alishaziweka zifuatwe hapa duniani, kwamfano ili kupata afya, ili kupata maisha marefu, ili kupata mafanikio, ili kupata cheo, ili kupata amani,n.k. ni lazima uzingatie njia hizo ambazo Mungu alishaziweka vinginevyo utajikuta unakosa shabaha na kuona kama Mungu hana msaada wowote kwako kwasababu tu ulikosa kujua njia sahihi ya kupita ili kufikia malengo yako ni ipi?
Kwa mfano Njia ambayo Mungu aliiweka kwa mtu apate kuishi maisha marefu na ya kheri biblia inasema katika
Mithali 10:27″Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa. Na pia ukisoma..”
Waefeso 6:2-3 inasema ” Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia.”
Kwahiyo kama ungependa uwe na maisha marefu hapa duniani kwanza ni UMCHE BWANA, na lingine ni kuwaheshimu wazazi, lakini njia nyingine zinazoonekana kuwa ni sawa kama vile kuzingatia MLO KAMILI, kuzingatia MAZOEZI, au Kupata muda mrefu wa kupumzika, au kuzingatia vyakula vya asili, vyote hivyo ni sawa lakini Havikuongezei maisha marefu na ya Kheri duniani. Kumbuka kosa la kwanza lilofanya maisha ya wanadamu kupunguzwa kutoka miaka 1000 mpaka miaka 120 ilikuwa sio kutokuzingatia mlo kamili bali ni kwasababu ya kutokushika maagizo ya Mungu. Hivyo kama unalegalega na njia zako hazimpendezi Mungu badilika sasa ishi maisha ya kumpendeza Mungu kama Mkristo na zingatia pia kuwaheshimu wazazi Mungu aliokupa hapa duniani. Kwa kufanya hivyo Mungu atakuongezea maisha marefu na sio tu marefu bali pia na ya Kheri.
Vivyo hivyo ili kupata afya, ni vizuri ukafahamu njia ya Mungu ni ipi aliyoiweka yeye,
Mithali 3:7 Usiwe mwenye hekima machoni pako; MCHE Bwana, ukajiepushe na uovu. Itakuwa AFYA MWILINI PAKO, Na mafuta mifupani mwako. ”
Ukisoma pia.
Kutoka 15:26 “akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye. “.
Mara nyingi tunajiuliza kwanini kila kukicha magonjwa yanatuandama, nimezunguka kutoka kwa mtumishi huyu hadi mtumishi huyu, nimeombewa na kila mtu lakini hali inazidi kuwa mbaya unaona kama vile Mungu hayupo pamoja nawe, Lakini hujui kuwa wewe ndio umemwacha Mungu na shetani ndipo anapopata nafasi ya kukutesa kwasababu umeiacha njia ambayo Mungu aliiweka tangu mwanzo tuiendee na kuwa na afya zetu, huwezi ukawa mwasherati, mlevi, mvutaji sigara, msengenyaji, fisadi, mwizi, au mtukanaji n.k halafu hayo yote yasikupate. Kumbuka biblia inasema KUMCHA BWANA ni KUCHUKIA UOVU (Mithali 8:13).
Jifungue mwenyewe kwanza katika hivyo vifungo vya uovu kwa kuacha kutenda dhambi, kumpoke Yesu Kristo, ndipo Bwana akulinde na maradhi kwasababu yeye anasema “ndiye Bwana akuponyaye”, Kwahiyo hauhitaji nguvu nyingi kujinyima kula vyakula vya aina fulani, au kuzunguka kwenda kuombewa na watumishi wakati wewe mwenyewe unaweza kujifungua..KUMCHA BWANA ndio msingi wa kila kitu!!
Vivyo hivyo ili kupata mafanikio ya kimwili ipo njia ambayo Mungu alishaiweka ukiikosa hiyo utaona kama vile Mungu kakuacha kwasababu Mungu siku zote anatembea katika kanuni zake na si katika kanuni zetu sisi tunazotaka yeye azitembelee. Tumekuwa tukimkumbusha Mungu kila siku tukisema “Mungu umesema; Utatubariki mijini, utatubariki mashambani, utatubariki tuingiapo utatubariki tutokapo, utatubariki kapu letu, na vyombo vyetu vya kukandia unga, atatufanya kuwa vichwa wala si mikia, atatubariki mifugo yetu na uzao wa matumbo yetu n.k.”
Ni wimbo ambao tumekuwa tukiuimba pengine pasipo kuona matokeo yoyote, na kufanya watu waishie kuzunguka kutoka kwa nabii huyu hadi nabii huyu,.Nataka nikuambie tu ndugu yangu mtu anayekutamkia kwamba “pokea baraka mwaka huu”, ki-uhalisia ni kwamba huyo mtu hajakubariki bali “AMEKUTAKIA TU KHERI”..kama vile tu mtu anavyokutakia Kheri ya mwaka mpya, au kheri ya maisha marefu.
Tumesahau Neno moja katika hiyo mistari ambalo ni la muhimu sana nalo ni “IKIWA”..”IKIWA UTAKAPOSIKIA SAUTI YA BWANA MUNGU WAKO”
Kumbukumbu 28:1 inasema; ITAKUWA UTAKAPOSIKIA SAUTI YA BWANA, MUNGU WAKO, KWA BIDII, KUTUNZA KUYAFANYA MAAGIZO YAKE YOTE NIKUAGIZAYO LEO, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;
2 na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako.
3 Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani.
4 Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.
5 Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga.
6 Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo….”
Kwahiyo unaona hapo NJIA Mungu aliyoiweka ili kupokea hizo baraka, ni KWA KUYATUNZA NA KUYAFANYA MAAGIZO YOTE YA MUNGU, ambayo ki uhalisia ni wachache wanafanya hivyo, utakuta mtu ni fisadi au mla rushwa bado anakwenda mbele za Mungu na kumwomba baraka, utakuta mtu anaishi maisha ya anasa halafu anamfuata mtumishi amwombee abarikiwe, utakuta mtu hata hana mpango na Mungu na yeye pia anakimbilia kwenda kununua mafuta ya upako, hiyo ni sawa na uganga wa kienyeji tu, ni vyema ukaacha na kutubu.
Njia pekee Mungu aliyoiweka ni KUMCHA yeye na kuyashika aliyokuagiza, kwa kuzingatia hivyo hautahitaji kwenda kwa mtumishi yoyote akuombee, au kukesha kuomba, au kutumia mafuta au chumvi vinavyoitwa vya upako, ili kufanya mambo yabadilike, Mungu mwenyewe atakutengenezea njia, kwa wakati wake, kwasababu anasema yeye mwenyewe anajua kuwa tunahaja na hayo yote.
Na ndio maana biblia inasema..
Mathayo 6:32-33 “…kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”
Usihangaike huku na huko, hakutakusaidia chochote MCHE MUNGU.
Vivyo hivyo ukitaka CHEO (ukubwa mahali popote), njia ipo nayo ni “kuwa mdogo kuliko wote” jinyenyekeze kwa maana ajishushaye atakwezwa na ajikwezaye atashushwa,usitumie njia za kujipendekeza kwa watu ili upate kibali wewe jishushe kuwa mnyenyekevu hakuna mtu yeyote asiyependa mtu mnyenyekevu..hizo ndio NJIA zilizowekwa na Mungu, ukitaka kupokea vitu kutoka kwa watu, Bwana Yesu alisema.. katika
Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa. ”
Hata siku zote ili bomba litoe maji ya kujaza vyombo vingi ni sharti lifunguliwe, lakini likifungwa litabakia na maji yake ya ndani tu..vivyo hivyo ukitaka upokee “favour” inakupasa utoe kwa wengine na kwa Mungu.
Ukitaka furaha, amani na watu, mche Bwana kwa kuzishika amri zake,Mithali 16:7 ” Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye.”
Sulemani mtu aliyekuwa na mafanikio na mwenye utajiri mwingi kuliko watu wote waliomtangalia na waliokuja baada yake, japo katika ufahari wake wote alihitimisha na kusema..
Mhubiri 12:13-14″ Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; MCHE MUNGU, NAWE UZISHIKE AMRI ZAKE, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu. Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya. “
Sisi ni akina nani tusimche Bwana?.
Ubarikiwe sana na Bwana wetu YESU KRISTO.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Kwa maombezi/Ushauri/Ubatizo/ Whatsapp. Tupigie namba hizi: +255693036618
Mada Nyinginezo:
TUKAZE MWENDO KWA TULIYOANDALIWA.
Daudi aliyekuwa mfalme wa Israeli, mwenye sifa ya kuupendeza moyo wa Mungu na ushujaa mwingi, lakini chanzo cha kunyanyuka kwake kilikuwa cha kipekee sana, habari hii tunaisoma katika 1 Samweli 17, Tunaona pale ambapo Daudi alitoka kama mtu asiyejua wala kuwa na uzoefu wowote wa vita na kumuua mtu ambaye alikuwa jemedari wa vita wa jeshi la wafilisti(Goliathi).
Kumbuka Daudi alikuwa ni kijana mdogo tu na mchungaji aliyekuwa anakaa maporini akichunga kondoo wa baba yake, hii ni shughuli isiyokuwa na mahusiano yoyote na vita, tunasoma na ilipofika wakati vita kutokea wafilisti kupigana na waisraeli ndipo wafilisti wakamnyanyua Goliathi aliyekuwa hodari wa vita, kwa ukubwa wake na uzoefu wake wa vita, hakuna shujaa yoyote wa Israeli aliyeweza kumkaribia kupigana naye kwa hofu.
Tunasoma kijana mmoja mdogo Daudi asiyekuwa miongoni mwa wale mashujaa wa Israeli waliokuwa na ujuzi wa vita kwa miaka mingi, aliweza kunyanyuka na kumwangusha yule simba wa wafilisti.
Lakini siri ya Daudi kushinda na kuwa jemedari ni ipi?
Tukisoma …
1 Samweli 17:31 “Na maneno hayo aliyosema Daudi yaliposikiwa, watu wakamweleza Sauli; naye akatuma mtu kwenda kumwita.
32 Daudi akamwambia Sauli, Asizimie moyo mtu ye yote kwa ajili ya huyu; mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu.
33 Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake.
34 Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi,
35 mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua.
36 Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai.
37 Daudi akasema, BWANA ALIYENIOKOA NA MAKUCHA YA SIMBA,NA MAKUCHA YA DUBU, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe. “
Hapa katika habari hii tunaona Daudi akitoa ushuhuda wa matendo makuu ya Bwana aliyomtendea, katika nafasi yake ya udogo aliyokuwa nayo, jinsi alivyoweza kuwaua dubu na simba alipokuwa akichunga kondoo wa baba yake, AKAHESABU kuwa kama Mungu aliweza kumshindania katika makucha ya maadui wa mifugo yake, hatashindwa pia kumwokoa kutoka katika makucha ya maadui wa ndugu zake na Taifa lake Israeli.
Pengine Sauli alitegemea kusikia kutoka kwa Daudi ushuhuda wa madaraja mangapi ya uluteni amepitia, au mafunzo mangapi ya kijeshi amepitia, alitegemea kusikia aidha kama alishawahi kupitia mafunzo ya ukomandoo, lakini badala yake aliishia kusikia shuhuda za mbuzi na kondoo zaidi ya yote alionekana ni kijana laini hata mkuki hawezi kubeba vizuri, hivyo kwakuwa hawakuona jemedari mwingine kwa kujitokeza kupambana wakaona wamwache aende tu kama vile kwa shingo upande.
Lakini hawakujua kuwa Daudi anao UFUNUO wa Mungu ni nani kwake, ALIMUHESABIA MUNGU kuwa ni muweza wa yote. Hivyo hakutumia njia zao walizozizoea kumkabili adui yake, hakwenda na chepeo na dirii bali alikwenda na JINA LA BWANA WA MAJESHI (YESU KRISTO)
1 Samweli 17:45 Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.
46 Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya aWafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli.
47 Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu. “
Amina.
Kumbuka katika safari ya kuwa askari wa Mungu kwenye shamba lake, jua tu utakumbana na changamoto nyingi ikiwemo kukatishwa tamaa, na kibaya zaidi watakao kukatisha tamaa sio watu wengine bali ni hao askari wenzako waliokutangulia katika hilo shamba, kama vile tu Daudi alivyokatishwa tamaa na wale ndugu zake, walimwambia ana kiburi, na wakataka kumfukuza arudi kuchunga mbuzi za baba yake, lakini Daudi alipuuzia.
Vivyo hivyo inawezekana umesikia wito wa kumtumikia Mungu, watu wa kwanza utakaokutana nao na kukuvunja moyo hawatakuwa watu wasiomjua Mungu bali ujue tu watakuwa ni hao waliokutangulia katika kazi ya Bwana, sio kana kwamba ni watumishi wa shetani la! lakini ndivyo ilivyo, pale utakaposema tu nataka kumtumikia Mungu utasikia “ni chuo gani cha biblia umepitia wewe? “…utaulizwa “umepitia kwanza chini ya huduma ya nani mpaka wewe utake kumtumikia Mungu”..
Utasikia wenye ujuzi wameshindwa wewe ni kama nani, hata biblia huijui vizuri, kwanza ndio umeokoka juzi tu, mchanga wa kiroho, walau hata ungekuwa umepitia kwanza mafunzo fulani ndio uanze..na vitu vinavyofanana na hivyo vya kukatishwa tamaa vingi vitakuja, lakini fahamu kuwa huyo ni shetani akitaka kukatisha tamaa usisonge mbele, kama vile Daudi hakutumia uzoefu unaofanana na wao kumuua Goliathi bali alitumia uzoefu Mungu aliomshindania katika maisha yake aliyokuwa anapitia katika ufugaji wake..na kwa kufanya vile aliweza hata kuwa shujaa, kushinda hata wale askari waliokuwa wanajiona wenye uzoefu mwingi na kupitia mafunzo mengi ya vita kabla yake.
Inawezekana una wito fulani wa kumtumikia Mungu, lakini kulingana na mazingira ya watu waliokutangulia katika huduma yanakufanya ujione kama haustahili, kwasababu haujapitia chuo cha biblia, au hujaenda shule, au hujakaa chini ya mtumishi yeyote unajiona hauwezi, fahamu jambo moja kuwa “UNAWEZA katika yeye akutiye nguvu“..Kwamba unasikia wito wa Mungu ndani yako, kaza mwendo, uendee na Mungu atakuwa na wewe
Kumbuka kama Daudi alivyotumia ujuzi wa mambo yaliyopita ya maisha yake na kumhesabia Mungu kuwa anaweza kumpigania hata sasa na wewe vivyo hivyo kumbuka mambo yote ambayo uliona kabisa Mungu alikupigania kama sio yeye ungekwama, au kama sio yeye usingukuwepo leo, tumia huo huo uzoefu Mungu aliokuonekania katika maisha yako uulete katika kazi ya Mungu. Mungu yule yule aliyekupigania kule ndio huyo huyo atakayekupigania kwenye kazi yake.
Watakao mwangusha Goliathi(shetani) kwenye kanisa hili la mwisho hawatakuwa wanaodhaniwa kuwa wamekuwa katika huduma kwa muda mrefu, bali watakuwa ni vijana(wa kiroho) kama wakina Daudi wenye ufunuo, ambao watamwamini Mungu katika utimilifu wake wote. Hao wengine wataua wafilisti tu lakini Goliathi ni kwa Daudi.Kwa maana Bwana Yesu alisema,
Mathayo 11:25-26 ” Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako.
Na pia alisema..Mathayo 20:16 “Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho. “
Hivyo ndugu ni wajibu wetu kusonga mbele pasipo kukwazwa na jambo lolote, usitazame mpaka upate kitu fulani ndio ufanye kitu kwa ajili ya Mungu. 2Wakorintho 6:2 (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa)
Ni maombi yangu Bwana atupe neema hiyo ya kuwa mashujaa wake kama Daudi.
Mungu akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Kwa maombezi/Ushauri/Ubatizo/ Whatsapp. Tupigie namba hizi: +255693036618
Mada Nyinginezo:
WAKATI WA JIONI KUTAKUWAKO NA NURU
Kuna namna nyingi watu wanavyompokea YESU katika maisha yao, lakini sio namna zote zina manufaa kwa ajili ya uzima wa mtu. Ni muhimu sana kufahamu kusudi la msingi la Bwana Yesu lililomfanya aje duniani vinginevyo utadhani kwamba unatembea na Mungu kumbe Hayupo na wewe.
Tunaweza tukajifunza baadhi ya mifano katika biblia: Mahali fulani Petro alipokuwa anavua samaki, katika kuhangaika kwake usiku kucha bila kuwa na matumaini ya kupata chochote alimuona mtu anakuja asiyemfahamu na kuanza kufundisha watu kando kando ya Habari pembezoni mwa chombo chake, kisha alipomaliza akamwambia Petro tweka ukavue samaki vilindini, pengine Petro alimuona kuwa ni mtu wa Mungu hivyo akaona ayatii yale maagizo, lakini walipofika hata sio mbali, walipata samaki wengi sana kimiujiza kiasi cha nyavu kuweza kukatika, mpaka iliwabidi waombe msaada kwa wavuvi wenzao waliokuwa kando kando yao, nao pia wakajaza vyombo vyao kwa wingi wa samaki wale.
Lakini je! jambo gani lilitokea baada ya hapo?
Tunasoma;
Luka 5:4″ Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.5 Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.
6 Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika;
7 wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama.
8 Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, ONDOKA KWANGU, KWA KUWA MIMI NI MTU MWENYE DHAMBI, BWANA.
9 Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata;
10 na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.
11 Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, WAKAACHA VYOTE WAKAMFUATA.
Hapo ni jambo gani tunajifunza? Petro baada ya kuona ule muujiza wa samaki saa hiyo hiyo alijisalimisha kwa Bwana na kumwambia, ondoka kwangu mimi ni mwenye dhambi!!..muujiza ule ulimfanya ajihukumu maisha yake akijua kuwa ni Mungu amesimama mbele yake na kusema naye, na zaidi ya yote aliacha hata ile kazi aliyokuwa anaifanya pamoja na wale samaki aliowapata na kumfuata YESU , Lakini kwa mtu mwingine asiyekuwa na ufahamu angechukulia lile tendo kuwa ndio FURSA ya kumtumia YESU kama chombo cha baraka katika kazi zake za uvuvi, kama wanavyofanya watu wengi leo.
Mtu angesema Mungu kaona mateso yangu ya kuteseka kwangu usiku kucha na leo hii kanikumbuka na kunibariki..Angesema leo hii Mungu kajifunua kwangu nimemuona biashara yangu inafanikiwa, Bwana kanipa utajiri jana tu nilikuwa maskini leo nimekuwa tajiri, Bwana kawaaibisha maadui zangu,
Nimeuona mkono wa Mungu katika maisha yangu mtaji wangu umeongezeka… Lakini kumbuka kwa PETRO haikuwa hivyo, hakuona hayo mambo kwa BWANA, alijua kuwa ile ishara sio kwa ajili ya tumbo lake bali ilikuwa kwake kama chachu ya yeye KUMTAZAMA KRISTO. Na ndio maana tunaona baada ya hapo alifikia mpaka hatua ya kuacha vyote na kumfuata YESU.
Lakini tunaweza tukajifunza pia katika kundi lingine la watu, na hili tunasoma habari zake katika kitabu cha Yohana 6:1-32. Watu hawa walitendewa muujiza unaofanana na ule wa Petro isipokuwa hawa Bwana aliwagawanyishia mikate 5 na samaki 2 kwa maelfu yao,
Lakini walipoona ile ishara walitaka kwenda kumshika wamfanye mfalme, sio kwasababu awe mfalme kwao ili waokolewe bali kwasababu waliona kama akiwa mfalme wao atawasaidia katika vipindi vya njaa na vigumu kwa kuwashushia chakula kimujiza kama vile Musa jangwani. Ni sawa tu na sasa hivi watu wanamtafuta Bwana Yesu ili awavushe tu katika vipindi vyao vigumu na si zaidi ..Tunasoma
Yohana 6:24-27″24 Basi mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu.
25 Hata walipomwona ng’ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa?
26 Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ISHARA, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.
27 Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu. “
Hiyo ndio sababu YESU aliwakimbia, hakuambatana nao, kwasababu walikuwa wanaangalia TUMBO na sio BWANA. Walimchukulia kama yeye ni fursa ya kuwafanikisha katika mambo yao lakini mambo mengine zaidi ya hapo hawakutaka,
Lakini tunaona wakati mwingine Bwana alimponya kipofu mmoja aliyekuwa vile tangu kuzaliwa kwake, na baada ya kuponywa alijua tu ni YESU amemponya ila hakumwona, lakini kwa kuzidi kutaka kumjua na kuushikilia ushuhuda wake mpaka walipomfukuza nje ya sinagogi kwasababu ya kiu yake kwa YESU, ndipo YESU akamjia na kujifunua kwake na kumjua, lakini hapo kabla alikuwa hamjui japo aliponywa na yeye(Yohana 9).
Vivyo hivyo katika maisha ya sasa, Bwana anawatendea miujiza watu wengi lakini hawatambui kwanini Mungu anawatendea hiyo miujiza, wanadhani kwa kuwatendea hivyo ni Mungu kajifunua kwao! Hapana, miujiza ni kitu(chambo) cha kuwafanya watu wamgeukie yeye, hivyo kusudi kubwa la yeye kufanya hivyo ni kuwafanya watu watubu, au wazidi kumsogelea karibu na sio kuwarahisishia mambo tu.
Mungu anapokuponya ugonjwa wako, hapo Bado haujamwona Mungu, Mungu kukufanikisha katika kazi za mikono yako, hapo bado haujamwona Mungu, ni sawa na wale waliovunjiwa mikate nyikani, wakala wakashiba na kuishia hapo hapo, Bwana kukufaulisha katika mambo yako hapo bado haujampata yeye, mpaka pale utapotambua maana ya yeye kukunyooshea mkono wake ni ipi?.
Siku utakapotambua UTATUBU na KUJINYENYEKEZA MBELE ZA BWANA..utafikia mahali na kusema kama Petro alivyosema..ONDOKA KWANGU MIMI NI MWENYE DHAMBI, kuonyesha kuwa haustahili mbele zake..Ukilijua hilo hautatamani hata vile vitu alivyokubariki navyo bali yeye tu wala hautamchukulia Bwana kwa jinsi unavyomchukulia leo.
Bwana aliyesema fedha na dhahabu ni mali yangu, ndiye huyo huyo alisema “ITAKUFAIDIA NINI UUPATE ULIMWENGU MZIMA NA KUPATA HASARA YA NAFSI YAKO?”. Kumbuka kusudi la msingi kabisa la Bwana Yesu kuja hapa duniani sio kutufanya sisi kuwa mabilionea, au kutuponya magonjwa yetu, au kutufanikisha katika mambo yetu, hapana bali ni KUTUOKOA sisi kutoka katika dhambi, kama tafsiri ya jina lake lilivyo {YESU= YEHOVA MWOKOZI}, ndipo mambo mengine yafuate.
Hivyo ndugu ishara na miujiza yote Mungu anayokutendea leo, ni kukufanya wewe utubu, akuponye roho yako, kumbuka Bwana ataanza tu KUJIFUNUA KWAKO pale utakapoamua kumruhusu afanye kazi katika maisha yako, lakini ukiangalia KIGANJA CHAKE tu atakupa nini! atakukimbia kama alivyowakimbia wale wasamaria hivyo ule wokovu hautafunuliwa kwako ambacho ndio kiini cha maisha ya kila mwanadamu…Siku ile atakuambia ulinifuata mimi si kwasababu ulitaka kuokolewa bali kwasababu ulitaka gari, ulitaka pesa, ulitaka mtoto, ulitaka kuolewa. Na kundi la namna hii ndilo kubwa kabisa katika kanisa hili tulilopo la siku za mwisho.
Maombi yangu ni utafakari mambo yote makuu Mungu aliyokutendea ujue kuwa hayo ni kukutaka utubu kabla wakati haujaisha, utubie uasherati wako, ulevi wako, wizi wako, ufisadi wako, usengenyaji wako, utukanaji wako, ibada zako za sanamu n.k.
hii ndio sababu ya Mungu “kuruhusu” miujiza na ishara nyingi kupita kiasi zitendeke KILA MAHALI katika kizazi chetu hichi tunachoishi, kila kitu unachomwomba Mungu hata kama ni mwenye dhambi anakupa, unaumwa anakuponya, sio kwasababu anafurahishwa na wewe, bali anataka utubu, lakini usipotubu alisema maneno haya:
Mathayo 11:20-24 “Ndipo akaanza kuikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu HAIKUTUBU.21 Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.
22 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi.
23 Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.
24 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe. “
Mungu akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Kwa maombezi/Ushauri/Ubatizo/ Whatsapp. Tupigie namba hizi: +255693036618
Mada Nyinginezo:
NINI MAANA YA KUTOKA KATIKA MADHEHEBU?
Tomaso akawaambia..
Yohana 20:25”…, Mimi nisipoziona mikononi mwake KOVU ZA MISUMARI, na kutia kidole changu katika mahali pa MISUMARI, na KUTIA MKONO WANGU KATIKA UBAVU WAKE, mimi sisadiki hata kidogo.”
Wengi tunadhani Tomaso alikuwa hatambui anachosema pale alipotoa matamshi kama hayo, lakini ukweli ni kwambaTomaso alitaka kupata uhakika ya kuwa je! Huyu ndiye Yule YESU aliyesulibiwa msalabani au la?. Na tunaona alipomthibitisha kuwa ndie mwenyewe kwa zile alama zilizokuwa mwilini mwake alimkiri na kusema.. “BWANA WANGU na MUNGU WANGU”.
Bwana Yesu alisema na sisi katika
Luka 9:23” Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.”
Maneno haya yanatufundisha kwamba USHAHIDI wa kwanza kama kweli tumeamua kumfuata YESU,ni lazima tutakuwa na misalaba migongoni mwetu, hii ikiwa na maana kuwa kama hatujaibeba misalaba yetu ni dhahiri kuwa bado hatujaanza safari ya kumfuata hata kama tutadai kiasi gani kuwa tunampenda YESU, au tunamwamini YESU, au vyovyote vile hapo bado hatujamfuata YESU mpaka siku ile tutakapochukua uamuzi wa kujitwika misalaba yetu na kuambatana naye.
Ni Kiashiria cha dhiki au mateso utakayopitia kwa ajili ya Imani yako. Hivyo mtoto wa Mungu yeyote anapomwani Kristo, na kuchukua hatua ya kumfuata YESU kweli kweli ni lazima apitie mahali hapo kujaribiwa kwa imani yake kama kweli alimaanisha kuchukua uamuzi huo au alijaribu tu?.
Hichi ni kipindi cha dhiki za kitambo, ambacho hakikwepeki kama kweli utakuwa ni mtoto wa Mungu, ndio hapo utaona mtu akiamua kuchukua uamuzi wa kumfuata Kristo, ghafla vikwazo vinaanza kuibuka, pengine ndugu wanaanza kukupiga vita, au kujitenga na wewe, pengine hali yako ya kiuchumi inaanza kuyumba, wengine inafikia hatua hata ya kukosa chakula, wengine pindi tu wanapoamini wanakumbana na misiba kufiwa na wazazi au watoto, wengine magonjwa ya ajabu yanazuka, wengine wanafukuzwa kazi kutokana na imani yao, wengine wanaingizwa magerezani, wengine wanaishia kupigwa, wengine jamii inayowazunguka inakuwa kama mwiba katika maisha yao.
Wengine wanadharauliwa, heshima yao inashuka hata watoto wadogo wanawadharau kisa tu kaamua kuuweka msimamo wake kwa YESU. kiasi cha kwamba mtu anaweza akafikiria yeye ni mtu wa bahati mbaya au ana mikosi, Lakini si kweli, hapo ujue unajaribiwa kama utaiacha ile imani au la.
Kumbuka hapa namzungumzia mtoto wa Mungu aliyeamua kumfuata BWANA YESU kwa moyo wake wote, na sio mtu yeyote tu ambaye hana habari na Kristo anapitia matatizo akidhani kuwa anajaribiwa, hapo ni shetani anafanya kazi juu ya maisha ya huyo mtu.
Hivyo dhumuni la kukuambia haya yote sio kukuogopesha au kukukatisha tamaa, hapana bali ni kukutia moyo pale utakapokutana na mambo kama hayo katika safari yako ya kumfuata Kristo, usikate tamaa wewe upo katika njia sahihi, haujalaaniwa wala huna mikosi, japo wengi watakukatisha tamaa lakini wewe songa mbele, usirudi nyuma wala usimuacha Kristo. Habari njema ni kwamba dhiki hizo ni za muda tu utafika wakati hutaziona tena, zitaondolewa mbele yako biblia inasema…
1Petro 5:9 “Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani.10 Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, MKIISHA KUTESWA KWA MUDA KIDOGO, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na KUWATIA NGUVU.”
Unaona hapo dhiki hizo ni kwa muda tu, tena ni kwa ajili ya kututengeneza na kututhibitha, kwasababu yeye siku zote anatuwazia mawazo yaliyo mema kutupa sisi tumaini katika siku zetu za mwisho.(Yeremia 29:11).
Pia alisema katika 1Petro 4: 12 -16
”12 Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama MOTO ili KUWAJARIBU, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.
13 Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo,FURAHINI; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.
14 Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; KWA KUWA ROHO WA UTUKUFU NA WA MUNGU ANAWAKALIA.
15 Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine.
16 Lakini ikiwa kwa sababu ni “MKRISTO” asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo.”
Kama tu vile wana wa Israeli walipotoka Misri, hawakuingia moja kwa moja katika nchi ya AHADI iliwapasa wapitie kwanza jangwani katika nchi kame isiyokuwa na maji, walikula chakula cha shida, na kukumbana na hatari nyingi huko nyikani,(Kumb.8) lakini Mungu hakuwaacha aliwapitisha kule makusudi sio kwa kuwatesa hapana bali kwa kuwafundisha, na kuwapa hukumu zake, ili watakapoingia nchi yenye asali na maziwa waweze kuenenda nayo pasipo kumsahau Mungu wao.
Kwahiyo ndugu yangu MKRISTO wewe uliyeamua leo hii kuchukua msalaba wako na kumfuata yeye ambaye alikufa kwa ajili ya Roho yako, umeingia gharama ya kuacha anasa na marafiki wamekutenga, umeamua kuacha ibada za sanamu na ndugu zako wamekutenga au kukuchukia na kanisa limekutenga,
Binti umeamua kuacha suruali & vimini,lipsticks,bangili & hereni kwa ajili ya Kristo na umeonekana mshamba, pengine kwa kufanya hivyo imehatarisha kazi yako, umeamua kuacha pombe na sigara na uasherati unaonekana mwanaume ambaye hujakamilika, n.k. hayo mateso yote na hizo dhiki ambazo hukuziona hapo kabla ni uthibitisho kamili kwamba upo katika njia iliyosahihi…Umekidhi vile vigezo kuwa UMEBEBA MSALABA WAKO na kumfuata YESU na hakika utaiingia kaanani yako kwa muda Mungu aliouamuru.
Lakini wewe ambaye anajiita mkristo, halafu hauna ALAMA zozote kuonyesha kuwa umemfuata KRISTO, swali kwako litakuwa kama lile la Tomaso alilouliza, NIONYESHA MAKOVU YA MISUMARI katika mikono yako, onyesha ubavu wako ndipo tusaidiki kuwa uliuchua msalaba wako na kumfuata Kristo.
Onyesha ni wapi ulipitia changamoto kwasababu ya imani yako? Ni wapi ulidharauliwa, au ulichekwa,au ulitengwa,au uliabishwa, au ulipigwa,au ulitukanwa,au uliteseka, au ulishushwa chini, n.k. kwa ajili ya kuchukua uamuzi wa kumfuata Kristo??,. Kama bado basi ujue bado hujaanza safari ya kumfuata yeye. Bado upo Misri haijalishi unaenda kanisani namna gani, unaimba kwaya kiasi gani, unapaswa uchukue uamuzi wa moja kwa moja kumfuata Kristo. Kuweka mawazo yako mbinguni, na kusema mimi duniani ni mpitaji bali makao yangu ni mbinguni. Mimi na dhambi basi!!!
Hivyo ndugu huu ni wakati wako wa kujitathimini kwa kina je! Ni kweli umemfuata Kristo au umeifuata dini au umefuata dhehebu?. Kama ni kweli umemfuata Kristo ni lazima utabeba msalaba wako na kama unao msalaba lazima alama za makovu ya mijeledi na misumari, pamoja na taji la miiba, vionekane katika safari yako ya kumfuata Kristo. Yahakiki maisha yako na uchukue uamuzi. Na Bwana atakusaidia.
Ubarikiwe.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Kwa maombezi/Ushauri/Ubatizo/ Whatsapp. Tupigie namba hizi: +255693036618
Mada Nyinginezo:
MTUME PAULO ALIKUWA NA MAANA GANI KUSEMA NIKAKUFA KILA SIKU??
MBONA MUNGU ANARUHUSU WATU WAPATE SHIDA, ILHALI ANA UWEZO WA KUTUEPUSHA?
Biblia inatufananisha sisi na kama miti izaayo matunda, hivyo kila mmoja wetu anapaswa azae matunda kwa Mungu, kadhalika biblia imetuonya pia mti usiozaa matunda utakatwa, kama tunavyosoma mfano Bwana wetu alioutoa katika
Luka 13:6
“Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate.
7 Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, MIAKA MITATU HII naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?
8 Akajibu akamwambia, Bwana, uuache MWAKA HUU NAO, hata niupalilie, niutilie samadi;
9 nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.”
Mtini huo ulipewa muda wa miaka 3, ili uzae matunda, lakini haukuzaa, hivyo mwenye shamba alitaka kuukata lakini akauongezea neema ya mwaka mmoja zaidi iwe 4 ili kwamba ukizaa katika huo muda itakuwa ni vema lakini usipozaa ndipo ukatwe. Mfano huu ukitufundisha kwamba kila mmoja wetu amepewa muda wa kumzalia Mungu matunda, hichi ni kipindi kilichoanza tangu wakati ule uliposikia kwa mara ya kwanza NENO LA KRISTO katika masikio yako mpaka wakati huu uliopo sasa..Ni dhahiri kuwa pengine imeshapita miaka zaidi ya mitatu, lakini je! Tangu huo wakati uliosikia ulilikubali kwa kulizalia matunda? Au ulilipuuzia na kusema bado bado kidogo?.
Na kama kilishapita kipindi kirefu namna hiyo na bado hujabadilika basi ujue upo katika muda wa nyongeza, na wakati wowote unaweza UKAKATWA. Leo hii umeongezewa neema fupi, Mungu analia kwa nguvu ndani ya moyo wako, uache dhambi, umgeukie yeye, na dhamiri yako inakushuhudia kabisa kuwa unamuhitaji Mungu katika maisha yako, unaona kabisa upo katika vifungo vya uovu na dhambi na bado umesikia injili mara nyingi lakini hutaki kugeuka unaufanya moyo mwako kuwa mgumu, upo katika hatari ya kukatwa.
Kumbuka ni neema za Mungu tu unaishi katika muda huu wa nyongeza, hiyo sauti ya Mungu inayolia ndani yako inayokushuhudia hiyo njia yako sio sawa, haitadumu milele ipo siku itanyamaza,. Usitamani ufikie hiyo hatua kwa maana utakuwa ni wakati mgumu sana ambao hata uhubiriweje Injili hautashawishika tena kugeuka kwasababu umeshakatwa. Hali itakuwa mbaya hicho kipindi kiasi ambacho hata ukifanya uzinzi hautasikia kushitakiwa ndani yako, hata ukiwa mlevi utaona ni sawa tu, ukielezwa mambo yahusuyo wokovu utaona ni hadithi za kutunga, Utaishia kukosoa biblia na watakatifu kila siku kwasababu kifo cha kiroho kimeshakuvaa, mwisho wa siku utakufa na utaenda kuzimu kwenye majuto ya milele.
Utafananishwa na mti uliokatwa na kuangukia shimoni..
Muhubiri 11: 3 “……Na mti ukianguka kuelekea kusini, au kaskazini, Paangukapo ule mti, papo hapo utalala.”
> Ukishakatwa kama umeangukia kwenye ulevi utaishi huko huko mpaka kuzimu.
> Ukikatwa kama umeangukia kwenye uasherati utalala huko huko mpaka ile siku ya hukumu.
> Ukikatwa na kama umeangukia kwenye anasa utalala huko huko mpaka kuzimu.
Hivyo ni vema ukaitendea kazi neema ya Mungu, kwa kuizalia matunda unaposikia NENO lake kwa kumruhusu ayabadili maisha yako mapema angali wakati bado upo.
Mithali 28:13 inasema..” Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”
Tubu mgeukie Mungu,
Neema ya Bwana wetu YESU iwe pamoja nawe.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
USIMFANYIE JEURI ROHO WA NEEMA.
WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU
NI HALALI KUBATIZA WATOTO WADOGO?
Kama tunavyofahamu kuna hatua tatu za maisha ya mwanadamu; Kuna Utoto, Ujana, na Uzee. Na hatua ambayo mtu analazimika kufanya maamuzi juu ya hatma ya maisha yake ni Ujana. Biblia inasema katika Yeremia 21:8b”….Tazama naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti.” Njia hizi zinatokea mbele ya mtu anapofikia UJANANI. Hivyo inahitajika busara nyingi na hekima ya Mungu katika kuchagua njia ya kuiendea.
Katika biblia tunaweza kujifunza mifano ya vijana wawili ambao walifanya maamuzi ya kuchagua njia za kuendea na hatma zao zilivyokuwa mwishoni.
KIJANA WA KWANZA:
Mathayo 19:16-22
“16 Na tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?17 Akamwambia Kwani kuniuliza habari ya wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri.
18 Akamwambia, Zipi? Yesu akasema, Ni hizi, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo,
19 Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende jirani yako kama nafsi yako.
20 Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena?
21 Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.
22 Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi”.
Tunamwona kijana huyu alijaribu kumfuata Yesu lakini kuna vikwazo vilikuwa mbele yake vinamkwamisha, ni mtu wa kipekee ambaye Bwana Yesu alimpenda hata kufikia hatua ya kumpa nafasi ya kipekee ya kufanyika moja wanafunzi wake, pengine angefanikiwa mtihani ule angekuwa mwanafunzi wa 13, na pengine leo hii tungekuwa tunasoma nyaraka zake, au angekuwa miongoni mwa watakao keti pamoja na Kristo katika ufalme wake kuwahukumu kabila 12 za Israeli, Lakini kikwazo kimoja tu nacho ni cha MALI kilimfanya akunje uso wake na kuondoka kwa huzuni, na kuipoteza nafasi ile ya kipekee. Pengine alisema moyoni mwake, ;kwa taabu nilizojitesa kupata utajiri wote huu, halafu leo hii mtu huyu mmoja anataka kunigeuza kuwa maskini ndani ya siku moja, hilo haliwezekani?. Kwakweli jambo hilo lisingeweza kumuingia akilini kama lisivyoweza kuwaingia akilini watu wengi leo.
Kumbuka pia kijana huyu sio kana kwamba alikuwa ni mtenda dhambi la! Alikuwa anaenenda katika haki tangu utoto wake, lakini kuna kitu aliona bado kimepunguka ndani ya moyo wake, kwamba hana uzima wa milele. Na alipomwendea Yesu na kumuuliza! Akaambiwa maneno yale. Lakini hakufahamu kwamba Yesu kumwambia vile sio kana kwamba anataka kumwekea kitanzi cha kuwa maskini la! Bali ni kumtengeneza awe kama wanafunzi wake wengine..na ndio maana kama ukiendelea kusoma mbele kidogo utaona aliwaambia wale wanafunzi wake wale walioacha kila kitu na kumfuata kuwa watapata mara mia na kuurithi uzima wa milele, soma;
Mathayo 19:27-29 “27 Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.
29 Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele”.
Hivyo kama kijana yule angekuwa mvumilivu tu, baada ya muda mchache haya maneno ya faraja yangekuwa sehemu yake, na huo uzima wa milele alioukuwa anautafuta angeupata pamoja na mali zake mara mia. Lakini kwa kuwa alipenda kuweka MALI kwanza basi alimkosa Mungu. Alishindwa kufahamu yale maneno yanayosema
“Mathayo 16:25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.
26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?”.
Tunaona habari ya YULE KIJANA ikaishia pale pale, mali alibakiwa nazo lakini Kristo alimkosa.
KIJANA WA PILI:
Lakini tumwangalie kijana mwingine aliyechukua maamuzi sahihi katika maisha yake kwa kuamua kumfuata KRISTO kwa moyo wake wote, na huyu si mwingine zaidi ya kijana MUSA. Kijana huyu alizaliwa katika jumba la kifalme la Farao, hakujua shida, wala njaa ni nini!! Biblia inasema ni mtu aliyekuwa na Elimu kubwa ya kidunia kwasasa tunaweza tukasema ni msomi mwenye PH.D, Alikuwa ni mwenye ujuzi wa maneno, alikuwa ni tajiri sana katika ngome ya Farao ambayo kwa wakati huo ilikuwa inatawala dunia nzima, ni kijana ambaye angetaka chochote angepata, angetaka wanawake wazuri kuliko wote angepata, kama ni viwanja, na mashamba alikuwa navyo, na zaidi ya yote umaarufu alikuwa nao tayari.
Lakini ilifika wakati akakutana na KRISTO moyoni mwake, pengine maneno kama yale yale yalimjia moyoni mwake, “nina kila kitu lakini nimepungukiwa na nini, ili niupate uzima wa milele??”. Tunasoma kwenye biblia Musa akaacha vyote kwa ajili ya Kristo akakimbilia nyikani, kwenye taabu kwa ajili ya Mungu wake.
Waebrania 11: 24-27
“Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;
25 akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;
26 AKIHESABU YA KUWA KUSHUTUMIWA KWAKE KRISTO NI UTAJIRI MKUU KULIKO HAZINA ZA MISRI; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.
27 Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana.”
Hivyo Baada ya miaka 40 tunamwona Musa tena, akirudi Misri akiwa kama mungu kwa Farao, biblia inasema hivyo, zaidi ya yote japo aliacha ndugu zake, mashamba n.k. alikuja kuvipata vyote na zaidi, Wana wa Israeli wote walikuwa kama watoto wa Musa, na zaidi ya yote hakukuwahi nyanyuka nabii kama Musa aliyezungumza na Mungu uso kwa uso, mpaka leo hii tunaisoma habari yake, Mungu alimpa kumbukumbuku lisilofutika milele, tunamwona miaka mingi baada ya kufa,akitokea na kuongea na Bwana YESU kule mlimani.(Mathayo 17). Kwasababu alihesabu kushutumiwa kwake Kristo ni UTAJIRI MKUU kuliko hazina zote za Misri.
Vivyo hivyo na sisi je! Tumehesabu hivyo??. Je! Umehesabu kushutumiwa kwa kuacha dhambi, anasa, ulevi, uasherati, biashara haramu, rushwa, fashion, ufisadi, ibada za sanamu n.k. kwa ajili ya Kristo kuwa ni utajiri mkuu kuliko mambo yote ya ulimwengu?.
Wewe ni kijana sasa ni wakati wa kuchukua uamuzi sahihi kwa kumfuata BWANA YESU KRISTO kwa gharama zozote utakazoambiwa ukijua ya kwamba Mungu hafanyi hivyo kwa kukutesa bali kukupa tumaini zuri katika siku zako za mwisho. Kama ni utafutaji mali ndio unaokusonga jaribu kuweka kwanza kando uutafute ufalme wake na haki yake. Kama ni cheo au ukubwa vinakusonga, viweke kwanza kando, umtafute Mungu, na hayo mengine yatafuata huko baadaye.
Hivyo chukua uamuzi kama wa kijana Musa, na sio Yule kijana mwingine. Wakati ndio huu biblia inasema
Mhubiri 12: 1 Mkumbuke Muumba wako SIKU ZA UJANA WAKO, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.”
Na Pia inasema.
Maombolezo 3:26 “Ni vema mtu autarajie wokovu wa Bwana Na kumngojea kwa utulivu. Ni vema mwanadamu aichukue nira WAKATI WA UJANA WAKE.”
Ni maombi yangu kuwa ujana wako utaishia katika njia njema ya uzima.
Ubarikiwe na Bwana Yesu aliye mwokozi wetu sote.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP