Shalom
mpendwa wa Bwana, karibu katika kuyafakari maandiko matakatifu, Na leo
tutajifunza somo ambalo tunaweza kuliona nyuma wa wana wa Israeli kukaa
Babeli miaka 70, Ni kwanini Mungu aliamua kuweka bayana kuwa watakaa utumwani miaka ile 70 ,
na kuwaambia kuwa wakifika kule kama ni kuzaa waendelee kuzaa watoto,
wawaoze binti zao, wapende bustani, wajenge, n.k….yaani kwa ufupi
tunaona Mungu hakuwa na haja ya Dua zao za kuomba warudishwe katika nchi
ya Israeli kwa wakati ule, utaona hakuwashauri hata waishi kama
wapitaji kule Babeli watakapofika, badala yake aliwaambia waendelee na
shughuli zao za kawaida kama tu vile walivyokuwa wanaishi Israeli..
Ukisoma Yeremia 29 yote utaliona hilo.
Lakini
ukweli ni kwamba hata ingekuwa ni wewe leo hii yamekukuta mambo kama
hayo , mtu kaja kuiua familia yako yote, na ukoo wako wote halafu
anakuchukua mateka kukupeleka nchi ya mbali na kukwambia baada ya miaka
70 nitakurudisha nchini mwako, kwahiyo ukifika kule wewe jenga, panda ,
uishi maisha ya furaha, JE! Ni kweli utakuwa na Furaha hiyo nchi ya
ugenini unayoiendea ambayo huijui hata ikoje, wala hujui utakutana na
watu wa aina gani huko?, Ni wazi kuwa Mawazo yako kila siku yatakuwa
nyumbani,katika majozi ukitumaini siku yoyote utarudi lakini sio baada
ya miaka 70.
Hiyo
ndio hali iliyowakuta wana wa Israeli, Walipomkosea Mungu, kupita
kiasi, mpaka Mungu kukata tamaa juu yao, Mungu alimruhusu Nebukadneza
mfalme wa Babeli, aje kuwachukua utumwani, Hivyo lile kundi la kwanza
lililoenda utumwani, lilipokuwa kule lilitamani sana lirudi nyumbani
Israeli, mpaka kukatokea manabii wa uongo wakawa wanawadanganya kwa
kuwafariji kuwa watakaa kule miaka 2 tu kisha Mungu atawarudisha nchi
yao tena, lakini Mungu alizungumza nao kwa kinywa cha Nabii Yeremia na
kuwaambia kuwa watakaa utumwani kwa muda wa miaka 70 mizima haitapungua
wala haitaongezeka, na hivyo wasijitaabishe hata kidogo kufikiri hiyo
itakuwa ni habari ya hivi karibuni, kikubwa tu waendelee kuoa, wapande
na wajenge, wawatikie na mema hao maadui zao, siku zote watakazokuwa
huko. na ndiyo tunasoma iliyompelekea hata Nabii Yeremia kupitia
matatizo makubwa namna ile hata kufikia hatua ya kutaka kuuliwa na
wayahudi, kwa taarifa mbaya alizokuwa anazileta, kwasababu Iko wazi kuwa
hakuna mtu anayependa kufia utumwani,
Ni
habari za kukatisha tamaa sana kwa namna moja au nyingine,wakikumbuka
utumwa ule wa Misri jinsi walivyoteswa ndio wanaokwenda kukutana nao
tena, kufanyishwa kazi ngumu,kutumikishwa, kuchapwa.Lakini tunasoma
pamoja na hayo kuna maneno Mungu alizungumza nao kwa kinywa cha
Yeremia..Na maneno yenyewe ndio haya:
Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho”.
Wengi
wetu tunasoma huu mstari lakini hatujui ni kwanini Mungu alizungumza
maneno hayo…Maneno hayo Mungu aliwaambia wana wa Israeli wakati
wanachukuliwa utumwani, Babeli.
Kwa
kweli ni maneno ya faraja ambayo hata sisi mstari huu tunapenda
kuutumia tunapopitia matatizo. Lakini habari yao inatufundisha
nini?.Ndugu wana wa Israeli wanafananishwa na watoto wa Mungu sasa,
yaani wale waliomwamini Kristo na baadaye wakarudi nyuma, wale walioujua
ukweli wakaupinga..wale ambao Mungu amekuwa akiwaonya mara nyingi
waache njia zao mbaya kwa mahubiri wanayosikia kila siku, lakini
hawakusikia, mpaka imefikia hatua wamezama katika matatizo makubwa
ambayo hawajui watatokaje, wengine wamezama kwenye uzinzi na sasa
wamepata ukimwi, na leo hii kweli umetubu na kuacha uzinzi kabisa
unataka Mungu akuponye, nataka nikuambie, kila mtu atavuna alichopanda,
umemwomba Mungu akuponye lakini huoni mabadiliko yoyote, kesi yako wewe
ni sawa na hii ya wana wa Israeli.
Hivyo
nataka leo nikuambie kulingana na maandiko wala usihuzunike kujikuta
umekaa katika hiyo hali kwa muda mrefu sana.. kama yalivyowakuta wana wa
Israeli kwa makosa yao, ndivyo yalivyokukuta na wewe. Wao walikaa miaka
70 lakini siku moja walitoka….Na wewe usisahau Neno hili kuwa.. Mungu
anayajua mawazo anayokuwazia wewe, ni mawazo ya amani wala sio mabaya
kukupa tumaini siku zako za mwisho.
Umekuwa
mwizi au mbakaji na sasa umefungwa, ni kweli umeshatubu kabisa kwa
kudhamiria kuacha, umekuwa mtoto mzuri wa Mungu, huibi tena wala huna
nia za Yule adui tena moyoni mwako…lakini unajiuliza ni kwanini mpaka
sasa bado upo kifungoni Mungu hakutoi huko?, nataka nikuambie,
kusamehewa ni kitu kingine, na kufutiwa adhabu ni jambo lingine, cha
msingi ukijikuta katika hali kama hiyo, wewe kuwa tu mtulivu kuwa mtu
mwema huko gerezani, mtumikie Mungu wako kwa uaminifu wote, ifanye kazi
ya Mungu huko huko uliko, fanya shuhuli zote zinazokuja mbele yako, kana
kwamba vile hutoki leo wala kesho, kwa kuwa Mungu anayajua mawazo
anayokuwazia wewe ni kukupa tumaini katika siku zako za mwisho.
Sasa
kumbuka wana wa Israeli walipofika Babeli japo walitubu na kulikuwa na
watu wa Mungu wengi tu mfano wa Ezekieli, na akina Danieli, lakini
hakuwaacha wateseke kama kwa utumwa ule wa Misri, aliwanyanyulia watu
hodari na wenye hekima kama Danieli, Meshaki, Shedraki na Abednego, na
kuwaweka katika jumba la kifalme mbele ya Nebukadreza, na kwa kupitia
hao Mfalme aliwapa heshima wayahudi wote waliokuwa Babeli pamoja na
Mungu wao , wamwabudu kwa uhuru na amani, waliishi kweli utumwani lakini
hawakuwa kama watumwa muda wote waliokuwepo kule, ni kama vile Yusufu
na ndugu zake, japo wote walikuwa utumwani lakini waliishi vizuri zaidi
hata wa Wamisri waliokuwa kule ndivyo ilivyokuwa kwa wale waliokwenda
Babeli.
Na baada ya ile miaka 70
ya adhabu kupita Mungu aliwafungulia mlango mkubwa wa kurudi katika
nchi yao, lakini hawakurudi mikono mitupu walirudi pamoja na zawadi
nyingi walizopewa kule Babeli, na hata wale waliosalia huko Babeli na
kwenye nchi za mataifa kwa hiyari yao na wale ambao walikuwa wamesambaa
duniani kote tunaona Mungu aliwanyanyulia tena watu kama Mordekai na
Esta, kwenye viti vya enzi vya Uajemi, hawa nao waliwafanya wayahudi
wapate heshima mara dufu duniani kote, waliogopeka na kuheshimiwa sana,
japo walikuwa katika nchi za ugenini. Unaona jinsi mawazo ya Mungu
yalivyokuwa mema juu yao mwisho wa siku, licha ya kutumikia adhabu
lakini pia alipenyeza kusudi lake katika adhabu zao.
Hivyo
na wewe ambaye ulimkosea Mungu na sasa umekutana na mabaya, mpaka sasa
upo shimoni, na kwa bahati nzuri ulitubu dhambi zako, na uliziacha
kabisa, ni wazi kuwa Mungu alikusamehe siku ile ile ulipogeuza Nia yako
na njia zako.., lakini bado unaona hujatoka katika hilo shimo ulilozama,
iadha la magonjwa, au vifungo, au shida, au taabu, nataka nikuambie
usivunjike moyo, endelea kumtumikia Mungu katika hali uliyopo,
haijalishi itakuchukua wiki, au mwezi au miaka mpaka kufunguliwa kabisa,
lakini wewe endelea kumtumikia katika hali uliyopo na yeye atakubariki
atakuongeza atakufundisha , atakuzidisha huko ulipo, na wakati wake
ukifika atakufungua moja kwa moja..shetani asikudanganye kuwa Mungu
amekuacha, au anakuchukia. Kutumikia adhabu haimaanishi kuwa Mungu
hakupendi..
Isaya 44: 21 “Kumbuka haya, Ee Yakobo; nawe Israeli, maana wewe u mtumishi wangu; nimekuumba; u mtumishi wangu; Ee Israeli, hutasahauliwa na mimi”.
Mithali 3:11 “Mwanangu, usidharau kuadhibiwa na Bwana, Wala usione ni taabu kurudiwa naye”.
Na
pia kama hujatubu dhambi zako ukihofia kwamba Mungu hatakusamehe…Hiyo
ni sauti ya Ibilisi inazungumza na wewe..inayotaka kukupeleka
ukajinyonge kama Yuda! Mungu anataka utubu akusamehe dhambi zako zote
bure kwasababu yeye ni mwenye rehema…Anataka utubu ukiwa kwenye hayo
hayo madeni ya kupindukia, anataka utubu katika hali hiyo hiyo ya
magonjwa na vifungo, katika hali hiyo hiyo ya ushirikina na uchawi
uliyopo, katika hali hiyo hiyo ya uuaji na utapeli uliyopo, katika hali
hiyo hiyo ya ukahaba na usagaji.Tubu leo naye atakusamehe! Na
kukubadilisha kwa maana anakuwazia mawazo mema sana huko mbeleni, kukupa
wewe tumaini.
Mwisho kabisa nataka umalizie kwa kuyatafakari maneno haya:
Zaburi 103: 11 “Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
12 Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.
13 Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao.
14 Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.
15 Mwanadamu siku zake zi kama majani; Kama ua la kondeni ndivyo asitawivyo.
16 Maana upepo hupita juu yake, kumbe haliko! Na mahali pake hapatalijua tena.
17 Bali fadhili za Bwana zina wamchao Tangu milele hata milele, Na haki yake ina wana wa wana;
18 Maana, wale walishikao agano lake, Na kuyakumbuka maagizo yake ili wayafanye”.
Ubarikiwe.
Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na utakuwa umefanya kazi ya kuipelekea injili mbele.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Print this post