Title April 2025

YESU NI ALFA NA OMEGA .

Jina kuu la BWANA WETU YESU KRISTO Libarikiwe, karibu tuyatafakari maandiko.

Endapo akitokea mtu faulani mkuu sana  na kujigeuza na kujifanya mtumwa, na kuvaa nguo za chini ya hadhi yake, mtu huyo ni rahisi kupitia dharau kama watu wengine wa hadhi za chini, na kejeli, na hata kupitia mateso na kukataliwa….lakini laiti watu wanaomdharau wangemjua  kwa undani ni mtu wa namna gani, hakuna hata mmoja angeonyesha kejeli au dharau!.. wote wangemheshimu na kumwogopa!.

Ni hivyo hivyo kwa Bwana YESU, walimsulibisha lakini hawakujua yeye ni nani,  walidhani ni mwalifu tu, au mfano tu wa manabii wengine waliopita, kumbe! Hawakujua kuwa ni ALFA na OMEGA mwenyewe!. Naam hata mimi pengine ningekuwepo kipindi hiko, ningefanya hapo hayo! Kwasababu wanadamu sisi ni wale wale hatuna jipya!.

1Wakorintho 2:7 “bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu;

8 ambayo wenye kuitawala dunia hii hawaijui hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu”.

Baada ya kuyatafakari hayo..hebu shika biblia yako ufuatilia maandiko yafuatayo maana leo utajua ya kwamba YESU KRISTO ni MUNGU mwenyewe katika MWILI wa kibinadamu!!?..na si mtu wa kawaida!.

Sasa si kwamba ukiishia kuamini tu ni Mwana wa MUNGU utakuwa umepotea!..la ni sahihi na ndio msingi!, lakini zaidi ya hapo, YESU ni zaidi ya tunavyomfikiria, ni jambo gumu kulielewa lakini unapolielewa linakuwa ni tamu na zuri..

Hebu tuyapeleleze maandiko kidogo kumhusu yeye katika kitabu cha Ufunuo..

Ufunuo 1:8 “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi”.

Hapa MUNGU aliyeumba Mbingu na Nchi anajitambulisha kama Alfa na Omega!.. hapana shaka juu ya hilo, lakini hebu tuendelee mbele kidogo kumsoma huyu Alfa na Omega anaendelea kusemaje…

Ufunuo 21:5 “Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.

6 Akaniambia, Imekwisha kuwa. MIMI NI ALFA NA OMEGA, MWANZO NA MWISHO. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.

7 Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu”.

Hapa tena huyu MUNGU wa mbingu na nchi ambaye ndiye ALFA na OMEGA, (yaani mwanzo na mwisho) anasema atayafanya yote kuwa mapya na atampa kila mwenye kiu ya maji ya uzima bure!.. Bila shaka hiyo ni karama ya MUNGU na njema sana… Lakini hebu tusogee tena mbele tumwone huyu ALFA na OMEGA anasema nini tena na anajizungumziaje..hapa ndipo tutashangaa!!.

Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.

13 MIMI NI ALFA NA OMEGA, MWANZO NA MWISHO, WA KWANZA NA WA MWISHO.

14 Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake.

15 Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya.

16 MIMI YESU NIMEMTUMA MALAIKA WANGU kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi”.

Mstari wa 12 unaosema “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami,” na ule wa 16 unaosema “MIMI YESU NIMEMTUMA MALAIKA WANGU kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa.”… Mistari hii inatupa uzito kuendelea kumfikri YESU kama mtu wa kawaida, lakini inatulazimisha kumfikiri kama ALFA na OMEGA, kwamaana ndivyo alivyojitambulisha hapo.

Oo kumbe! YESU ni Alfa na Omega, na ndiye Mungu mwenyezi katika umbile la kibinadamu, sasa tunaelewa kwanini Mtume Paulo alisema siri ya UTAUWA (yaani Uungu) ni KUU, kwamba MUNGU alidhihirishwa katika mwili..

1Timotheo 3:16 “Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu”.

Hayo maneno kwamba “Mungu alidhihirishwa katika mwili, na akachukuliwa juu katika utukufu” yanatufanya tufikiri mara mbili mbili kuwa YESU ni nani?.. Naam hata Bwana YESU mwenyewe kuna wakati aliwalazimisha watu kumfikiri yeye mara mbili mbili kuwa ni nani… Labda utauliza ni wapi hapo katika maandiko, twenda pamoja..

Mathayo 22:42 “Ni mwana wa nani? Wakamwambia, Ni wa Daudi.

43 Akawauliza, Imekuwaje basi Daudi katika Roho kumwita Bwana, akisema,

44 Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako?

45 Basi, Daudi akimwita Bwana, amekuwaje ni mwanawe?

46 Wala hakuweza mtu kumjibu neno; wala hakuthubutu mtu ye yote tangu siku ile kumwuliza neno tena”

Hawa walikuwa wanamjua Masihi (YESU) kama mwana wa Daudi, na ni kweli maandiko yamesema hivyo, lakini sasa inakuwaje Daudi amwite Masihi kama Bwana wake na wakati huo huo awe mtoto wake??.. hata mimi ningeulizwa hilo swali, ningekwama!..

Maana yake kuna siri nyingine katika YESU tusizozijua, ambazo ukisoma maandiko kwa makini na kwa msaada wa Roho Mtakatifu utaziona!..

Sasa si dhambi kujua kama YESU ni mwana wa Daudi peke yake, wala si kosa kutambua kuwa ni Mwana wa MUNGU peke yake, na hiyo haiwezi kumtolea mtu tiketi ya kuingia mbinguni, lakini maandiko yanathibitisha kuwa YESU KRISTO ni zaidi ya tunavyomjua au kumfikiri, kama YEYE ni MUNGU MWENYEWE KATIKA MWILI..NUKTA KUBWA!!!.

Huenda Lugha zetu za duniani na udhaifu wetu wa kufikiri unakuwa ni mgumu kupokea hilo!, lakini huo ndio ukweli na ni lazima tuupokee, kama tu ilivyo ngumu kufikiri na kupokea kwamba inakuwaje MUNGU hana mwanzo!.. hapo ukifikiri sana unakwama!, lakini unaamini hivyo hivyo kwasababu yeye ni MUNGU, vile vile kuhusu UUNGU wa YESU usiumize kichwa kutafuta kulifanya lieleweke kichwani mwako sasa, labda tutaelewa vizuri baada ya maisha haya, lakini hatuna budi kuamini hilo!.

Na kumwelewa YESU namna hii inatufanya tusiuchezee Wokovu wetu, maana hatujakombolewa na damu ya mtu, wala myahudi bali ya MUNGU mwenyewe!.

Kwa maarifa ya ziada Kuhusu Uungu wa YESU zaidi pitia Tito 2:13, na Isaya 9:6

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je Yesu ni Mungu au Nabii?

MJUE SANA YESU KRISTO.

Je Mariamu alikuwa na umri gani alipochukua mimba ya Bwana YESU?

MKUU WA UZIMA AKUWEKE HURU.

KAMA SI YESU, HABARI YETU INGEKUWA IMEISHA ZAMANI SANA.

Print this post