Category Archive Vijana

NJIA SAHIHI YA KUMPATA MWENZA WA MAISHA KIBIBLIA.

Kuchagua mwenza wa Maisha si jambo la kulichukulia kiwepesi wepesi tu kama vile kuchagua Rafiki, ambaye hata mkigombana mnaweza mkaachana na kurudiana muda wowote.

Tena ikiwa wewe ni mtu uliyeokoka ndio unapaswa uwe makini mara dufu, kwasababu ukifanya maamuzi yasiyosahihi utajikuta sio tu kuupoteza wokovu wako bali pia kufanyika chombo cha kuwapoteza na wengine.

Ipo mifano mingi katika biblia ya watu ambao waliingia katika mikono ya wenza ambao sio sahihi. Kwamfano tunamwona mtu mmoja aliyeitwa Ahabu yeye alimwoa Yezebeli, hakuna asiyejua mke wake huyu jinsi alivyokuwa mwiba kwake na kwa Israeli nzima.. Na hiyo yote ni kwasababu alifanya uamuzi usiosahihi katika kuchagua mwenza wa maisha wa kuoa.

1Wafalme 21:25 “(Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. 

26 Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.)”

Tunamwona tena mtu mwingine aliyeitwa Samsoni, jinsi alivyoanguka katika mikono ya mwanamke Delila, binti wa kifilisti, Tunamwona tena Sulemani alivyoanguka kwa wanawake wa mataifa mengine jinsi walivyomgeuza moyo na kumfanya aabudu miungu mingine ikiwa kikwazo kwake kwa Mungu hadi ikafikia hatua ya Mungu kumuundokeshea maadui ….

Vilevile tunaomwona mwanamke Abigaili jinsi alivyoanguka mikononi kwa mume  mpumbavu  mlevi aliyeitwa Nabali..Ambaye ilikuwa ni nusura tu amsababishie mauti yeye pamoja na familia yake yote na wafanyakazi wake wote (soma 1Samweli 25).

Tunaomwona Herode naye, ambaye alijiingiza katika uuaji wa damu isiyokuwa na hatia ya Yohana Mbatizaji  kwa wivu tu wa mke wake, ambaye kiuhalisia hata hakuwa mke wake bali mke wa kaka yake alimuua Yohana kwa shinikizo la mke wake katili.

Matatizo kama hayo vilevile yanaweza kumpata mtu yeyote kama asipojua njia ipasayo ya kumpata mwenza wa maisha sahihi.

Leo hii tutajifunza kanuni chache za kibiblia ambazo ukizifuata utakuwa na uhakika wa kuwa huyu uliyempata asilimia mia ni mwenza Mungu aliyekupangia.

Sasa kabla hatujaenda mbali hapa natazamia kuwa naongea na mtu ambaye ameshaokoka. Kama hujaokoka basi mwisho wa somo hili fanya hivyo, ndio ujumbe huu utakuwa na manufaa kwako.

HATUA YA KWANZA:

Usiwe na haraka ya kuoa au kuolewa: Biblia inatuambia wazi kuwa mapenzi huwa yanachochewa na huwa yanaamshwa..na kama yanaamshwa inamaanisha kuwa kumbe huwa yanapoa  pia soma:

Wimbo uliobora 2:7 “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe”.

Hizi ni hekimu tunafundishwa.. mambo ya kuingia katika ndoa si ya kuyakurupukia. Kisa umemwona Fulani ameolewa au Fulani kaolewa, au umempenda binti yule au kijana yule hivyo na wewe ukaamua moja kwa moja ukaanze mahusiano naye ili mfunge ndoa..Biblia inatuasa tusiyachochee mapenzi kabla ya wakati wake..Mapenzi yana wakati wake..

Ikiwa wewe bado ni binti/kijana mdogo unatafuta mpenzi wa nini wakati unajua kabisa hamna mpango wa kuoana?. Hali kama hiyo ikikujia au vishawishi kama hivyo vikikujia vikatae, kwasababu wakati wake haujafika….Au wewe ni mwanafunzi hujamaliza masomo yako, unataka kuingia katika mahusiano ambayo lengo lake linapaswa liwe ni ndoa, Je utamwoa huyo au yule na huku ukiwa bado masomoni? Huoni kama huo sio wakati wake?..Hivyo ukijikuta unataka kufanya hivyo kataa hiyo hali, toa mawazo yako huko, fanya mambo yako kama vile mtoto mchanga, mpaka wakati wake huko mbeleni utakapofika..

Vilevile wewe bado upo chini ya wazazi wako, au unajijua bado hali yako kiuchumi bado haijaimarika vizuri, unakimbilia wapi kufikiria mambo kama hayo..Simaanishi kuwa mpaka uwe Tajiri ndio uoe, lakini unapaswa ujiandae kisaikolojia, je! Nikifanya hivi, huyo mke wangu nitaweza kumuhudumia hata kwa yale mahitaji ya msingi tu,?  Mambo kama hayo unatakiwa uyafikirie kabla hujaanza kutafuta mwenza wa maisha.

Wimbo uliobora 2:7 “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe”.

Usiogope labda umri umeenda au vipi, Isaka na Yakobo walipata wake zao wakiwa katika umri mkubwa tu, lakini tunaona wake waliowapata walikuwa ni bora Zaidi ya wake wa watu wengine..Vivyo hivyo usikimbilie tu kuoa au kuoelewa kwasababu Fulani Fulani bali uvumilivu pia ni muhimu katika kupata mwenza sahihi na ndoa iliyo bora.

Lakini sawa ikiwe umeyazingatia hayo vizuri na sasa upo tayari kuwa mwenza, basi zingatia mambo yafuatayo:

  1. NI LAZIMA AWE NI MKRISTO.

Nikisema ni lazima awe ni mkristo simaanishi awe amezaliwa katika dini ya ki-kristo, anaweza akawa amezaliwa lakini matendo yake yapo mbali na ukristo, bali namaanisha ni lazima awe ameokoka, na yupo katika mstari ulionyooka wa wokovu wake, Maisha yake yakimshuhudia kuwa ameokoka, kama wewe ulivyo.

Ukiangalia watu wote tulioona kwenye biblia kuanzia Ahabu mpaka Sulemani wote hao waliingia katika matatizo makubwa kwasababu waliyakaidi maagizo ya Mungu..Pale walipoambiwa wasioe wala wasioelewe na watu walio nje ya taifa la Israeli.

Soma

Kumbukumbu 7:3 “binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake. 

4 Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya Bwana juu yenu, naye atakuangamiza upesi”.

Mungu alikuwa na sababu kuwaambia vile, kwasababu alijua watawageuza moyo na kuandamana nao na miungu yao.

Nehemia 13:25 “Nikagombana nao, nikawalaani, nikawapiga baadhi yao, na kuwang’oa nywele zao; nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe. 

26 Je! Sulemani, mwana wa Daudi, hakufanya dhambi kwa kutenda hayo? Lakini katika mataifa mengi hapakuwa na mfalme mwingine mfano wake. Tena alipendwa na Mungu wake, naye Mungu akamfanya mfalme juu ya Israeli; walakini wanawake wageni walimkosesha hata yeye”.

Hivyo jambo la kwanza kabisa la kumtambua kuwa huyu ni mwenza wa maisha sahihi au sio sahihi usikimbilie kumtazama sura, au maumbile yake, au upendo wake kwako..Hilo jambo liondoe akilini kabisa..Usiangalie elimu yake au fedha zake, au ukarimu wake..wala usikimbilie kusema nimeoteshwa kwenye ndoto au nimeonyeshwa kwenye maono kuwa huyu ndio mpenzi wangu…Nataka nikumbie Neno la Mungu ni Zaidi ya ndoto au maono yoyote..Ndoto yoyote  au unabii unaokinzana  na Neno la Mungu unapaswa uukatae hata kama utaonekana unao uhalisia kiasi gani, Neno ndio linatuambia hivyo soma Kumbukumbu 13 utalithibitisha hilo.

Hivyo mwanamke yeyote au mvulana yeyote, anayekujia anataka kukuoa au unataka  kumuoa, mwangalie kwanza Je! yeye ni mkristo aliyesimama katika Imani?…Na kama sio mkristo Je! Yupo tayari kuamini na kumfuata YESU..Ikiwa yupo tayari aanze kwa  kugeuka kwanza ndipo hatua nyingine za kumtathimini sifuate.

2.USIWE NA HARAKA KUFUNGA NAYE NDOA:

Jambo lingine watu wasilolijua ni hili, pindi imetokea tu amemwona kuwa huyu ni mzuri, au anafaa, au ni mtakatifu, anaenda kanisani, bila kutuliza akili zao, moja kwa moja wanakimbilia kwenda kuoa au kuolewa naye..Na baadaye akishagundua kumbe yupo hivi au vile  hiki anaishia kujuta..

Sikuzote tendo la haraka haraka mara nyingi huwa halitokani na Mungu. Ukiona mtu Fulani anakushurutisha haraka haraka ufanye kitu Fulani, au mfanye biashara Fulani bila hata kuwa na nafasi ya kuitafakari vizuri basi ikatae moja kwa moja, ukiona mtu anakulazimisha ununue hiki au kile harakaraka bila hata ya kukiangalia vizuri basi usikinunue kwanza hata kama kwa macho kinaonekana ni kizuri.. Shetani naye huwa ndio anawashurutisha watu hivyo kuingia katika dhambi, atakuambia fanya hichi chapchap hakina shida, lakini baadaye ndio utakuja kujutia milele kwanini ulifanya vile.

Hivyo ukishamthibitisha kuwa huyu au yule ni mkristo, mtakatifu anampenda Mungu, chukua nafasi kumtathimini, pata muda wa kutosha hata miezi kadhaa, ikiwezekana hata mwaka kumwangalia Maisha yake, ..hiyo itakusaidia kuondoa kule kukurupuka ndani yako, na utapata nafasi ya kujua vile ambavyo mwanzoni alikuwa huvijui kuhusu yeye au vile ambavyo amevificha mbele yako. Yusufu hakuwa na haraka ya kumfanya Mariamu kuwa mke wake, bali alingoja kwa kipindi Fulani na ndio maana alipogundua kuwa ana mimba, kumbuka mpaka mimba ionekane labda ni kuanzia miezi 3 na kuendelea, hivyo wakati huo wote hakuwahi kumkaribia wala kumjua, isipokuwa alikuwa amemposa tu, na baadaye alipogundua kuwa ana mimba, akawa radhi kumuacha..Ndipo Mungu akasema usimuache.. Hivyo na wewe chukua nafasi ya kumtathimini huyo anayetaka kuwa mpenzi wako.

Kisha ukiwa katika hali hiyo ya kumtazama sasa ndipo umwombe Mungu..Hapo unajinyenyekeza mbele za Mungu unamwambia nimemwona dada huyu au kaka huyu, ikiwa ni sawasawa na mapenzi yako Ee Mungu naomba unifanikishe na ikiwa sio sawa na mapenzi yako uniepushe naye..

Ukishamaliza kuomba hivyo kwa muda wa kutosha, ikiwezekana kufunga kwa kipindi Fulani..Basi anza harakati za kwenda kutoa mahari kama wewe ni mume, na kama wewe ni mwanamke himiza tendo hilo kwa huyo mwanaume, kwasababu Mungu yupo pamoja na wewe katika kila hatua, kama huyo siye yeye Mungu mwenyewe atamwondoa kwako, au atakuepusha naye, hivyo uwe na amani kuanzia huo wakati kwasababu ulishazitanguliza kwanza kanuni zake, hivyo ni wajibu wa Mungu kukulinda baada ya hapo..

Hakikisha unakwenda kujitambulisha kwao, na yeye kwenu, unatoa mahari, mnafuata hatua zote za ndoa ya kikristo.Kisha baada ya hapo mnafungishwa ndoa kanisani…Hapo ndipo huyu anakuwa mwenza Mungu aliyemkusudia kwa ajili yako.

Ikiwa utazingatia kufuata hatua hizo zote, ondoa wasiwasi kuwa ndoa yako itakuwa na miiba ndani yake, kinyume chake ndio utaimarika hata katika Imani yako kwasababu mke atakuwa msaidizi kwa mume, na mume atakuwa ulinzi kwa mke..Wote wawili wakisimama katika imani mafanikio tele ya rohoni na mwilini yataambatana  nao, na Watoto wao pia watabarikiwa.

IKIWA HAUJAOKOKA:

Lakini kama wewe hujaokoka. Fahamu kuwa upo katika hatari kubwa sana, kwanza kwa kuukosa uzima wa milele, Na pili kwa kutokuwa na ndoa yenye baraka za Mungu..Kwasababu unataka kuoa au kuolewa lakini hujui kuwa anayeifungisha ndoa yenye heri na baraka ni Mungu..Sasa ikiwa umekosana na Mungu wako unatazamia vipi uwe heri katika ndoa yako unayoitazamia..Au upate wapi mwenza wa maisha aliye sahihi..Kwasababu wewe hapo ulipo tayari sio sahihi..utaishia kuoa asiyesahihi mwenzako na mwisho wake ni mlipuko.

Ni vizuri ukafanya uamuzi sahihi leo. Hizi ni siku za mwisho. Yesu yupo mlangoni kurudi..Dalili zote zinaonyesha kuwa unyakuo ni wakati wowote, Parapanda itakapolia wewe utakuwa wapi, wakati wenzako wapo mbinguni wewe utakuwa hapa chini katika dhiki kuu ya mpinga-kristo. Na baada ya hapo unaishia katika ziwa lile la moto. Kama ulikuwa hujui hili ndio kanisa la mwisho, lijulikanalo kama Laodikia, soma Ufunuo 3, Na kwanza hakutakuwa na kanisa lingine Zaidi ya hili,.Na kanisa hili ndio lililokemewa sana na Bwana Yesu kuliko makanisa mengine yaliyotangulia nyuma,.kwamba lipo vuguvugu,..Ni heri tungekuwa baridi au moto, kwasababu hiyo tumeambiwa tutatapikwa.Na tunajua matapishi huwa hayarudiwi tena. Hivyo ikifikia hatua ya wewe ndugu yangu kutapikwa, basi ujue hutakaa urudiwe tena, sehemu yako itakuwa ni katika lile ziwa la moto.

Unasubiri nini kwanini usimpe Yesu Kristo Maisha yako leo ayaokoe, Kesho inaweza ikawa isiwe yako. Nazungumza na wewe unayejiita mkristo, lakini huishi kama KRISTO, ndio maana Bwana anasema wewe ni vuguvugu…

Kama upo tayari kufanya hivyo kumpa Bwana Maisha yako…

Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Na Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Zingatia hayo na Bwana atakuwa pamoja nawe. Vilevile Usiacha kutembelea Website hii  https://wingulamashahidi.org mara kwa mara ili ujifunze maneno ya uzima..

Ubarikiwe sana.

Mada Nyinginezo:

NDOA NA HARUSI TAKATIFU.

Je! ni halali kutoa cheti kwa wakristo wanaooa?

Je! Ni halali kuoa/kuolewa na mtu ambaye tayari anao watoto?

Je! Ni sahihi kuoa/kuolewa na mtu uliyemzidi umri?

JE NI HALALI KUOA WAKE WENGI AU KUTOA TALAKA?

ANTIPA SHAHIDI WANGU, MWAMINIFU WANGU.

JE ADAMU ALIKUWA NA KITOVU?

Roho, Nafsi, na Mwili vina utofauti gani?

Rudi Nyumbani:

Print this post

JE! KUBET NI DHAMBI?

Ili kujua kama ku-BET ni dhambi au la! Ni vizuri kwanza kufahamu mapenzi ya Mungu ni yapi?…Huwezi kujua kipi kisichompendeza Mungu kama hujui kipi kinachompendeza…Sasa Mungu alivyotuumba watu wake na viumbe vyake vyote hata Wanyama, alituwekea kitu kinachoitwa dhamira ndani yetu…Hii dhamira kazi yake ni kutulinda sisi tusiende kinyume na mapenzi ya Mungu tunapoishi…Na ipo kwa viumbe vyote (wanadamu na wanyama)..Ndani ya hii dhamira kumefungiwa sheria za Mungu. Kwahiyo pasipo hata Mungu mwenyewe kuzungumza na mtu juu ya jambo Fulani tayari ile dhamira iliyopo ndani yake ina uwezo wa kukamata na kuhisi jambo ambalo sio sawa.

Kwamfano utaona, Simba anauwezo wa kula swala na kumrarua kikatili, lakini simba huyo huyo hamli mtoto wake…ni kwanini? Ni kwasababu dhamira iliyopo ndani yake inamshuhudia kuwa jambo hilo sio sawa…simba hajapewa sheria yoyote na Mungu, lakini ndani ya moyo wake kumefungiwa sheria, kwa kupitia dhamira aliyo nayo. Kadhalika huwezi kuona mbwa au mnyama yoyote analala na mnyama wa jinsia moja naye…

Ni kwanini? ni kwasababu ya dhamira iliyopo ndani yao..inayowashuhudia kuwa jambo Fulani sio sahihi, sio kwamba hawana hisia! Wanazo hisia lakini hawawezi wakavuka hiyo mipaka.

Na wanadamu ni hivyo hivyo, kuna kitu kinaitwa dhamira ambayo hiyo imebeba sheria za Mungu ndani yake, kiasi kwamba mtu anaweza asizijue kabisa amri za Mungu, lakini bado akazitimiza vile vile..

Haihitaji biblia kujua kuwa uuaji ni mbaya, au kuwatesa Watoto wako ni vibaya…Hiyo sheria tayari mtu anazaliwa nayo moyoni mwake…ndo maana hata wanyama pamoja na ukatili wao wote hawayafanyi hayo, hawasomi biblia lakini wanazitimiza sheria za Mungu….Haihitaji biblia kujua kuwa utoaji mimba ni vibaya, au kumdhulumu mtu ni vibaya, hiyo tayari mtu angejua hata kama hajawahi kusikia habari za Mungu. Haihitaji sheria kufahamu kumuoa dada yako/kaka yako wa damu ni makosa, hiyo tayari ipo ndani yako, hata hizo hisia zenyewe hazipo licha tu ya dhamira kukushuhudia.

Sheria ilipokuja, kazi yake ni kuitoa hiyo hiyo sheria kutoka katika roho na kuileta katika maandishi..Na hiyo ni kutokana na ugumu wa mioyo yetu, unajua hata watoto wanapotumwa dukani, na wanaonekana ni wazito kidogo kuelewa au wanasahausahu sahau, basi wazazi wanaamua kuwaandikia kikaratasi kidogo cha maelekezo ili wasisahau. Na sheria ilikuja kwa namna hiyo hiyo. Ililetwa kutufanya tuyakumbuke yale tuliyokuwa tumeyasahau katika roho zetu na dhamira zetu..

Sasa Watu waliokuwa wanaishi wakati wa Nuhu, walikuwa hawana sheria yoyote, Maana sheria ililetwa na Musa miaka mingi sana baada ya gharika?..Sasa unaweza kuuliza kama kulikuwa hakuna sheria, wale watu walikuhukumiwa kwanini?…Walihukumiwa kwa dhamira iliyokuwepo ndani yao…walikuwa wanafanya mambo ambayo ndani ya dhamira zao walikuwa wanajua kabisa sio sawa…lakini waliendelea kuyafanya! Hivyo ikawa dhambi kwao,(Warumi 1:17-30) Na Mungu akawaangamiza wote kwa gharika. Kwahiyo sheria hii ambayo tayari ipo ndani ya dhamira zetu ndio inayojulikana kama INJILI YA MILELE (Ufunuo 14:6). Kwa maelezo marefu juu ya injili hii ya milele  Bofya hapa >> INJILI YA MILELE

Sasa mpaka sasahivi hii INJILI YA MILELE ipo, Kuna vitu ambavyo havijazungumziwa hata kwenye Biblia takatifu lakini mtu akiona tu! Anajua hiyo sio sawa machoni pa Mungu..Mfano wa vitu hivyo ni Uvutaji wa sigara, utoaji mimba, mtu anayetoa mimba anajua kabisa ndani ya moyo wake anaua na anafanya jambo lisilo sahihi…ingawa ukitafuta mahali popote kwenye biblia palipoandikwa utoaji mimba ni dhambi huwezi kupata…Lakini mtu anayefanya hivyo anajua kabisa na anauhakika ndani ya moyo wake anamkosea Mungu, na ndivyo ilivyo…au mtu anayetumia madawa ya kulevya…anajua kabisa jambo afanyalo sio jema…

Jambo lingine ni mtu anayefanya masturbation, ukienda kumwuliza mtu anayefanya masturbation unajua ni kosa kufanya hivyo, wala hatakubishia Zaidi ataogopa na atakuuliza namna ya kuacha!…lakini ukienda kwenye maandiko ukitafuta mahali popote pamezungumzia suala la masturbation kuwa ni dhambi hutapaona!…lakini kwanini yule mtu ndani ya moyo wake anauhakika kuwa anachokifanya sio sahihi?..

Ni kwasababu ya dhamira iliyopo ndani yake! (Sheria ambayo Mungu alishaiweka ndani ya moyo wake) inayomshuhudia jambo sahihi na lisilo sahihi…Au leo hii ukimfuata mtu anayeangalia pornography, atakwambia kabisa mimi nafanya makosa, wala hatakubishia wala kukuuliza ni wapi pameandikwa hivyo kwenye biblia?…wala hatataka kujua, yeye anachojua kuwa anafanya dhambi, jambo lisilompendeza Mungu, hilo tu!…Au mtu anayecheza kamari, anajua kabisa jambo afanyalo sio sawa, na anajua kabisa huo mchezo ni wa kishetani, anajua kabisa ni mchezo wa dhuluma ambao wakati mwingine unaweza kuhatarisha, uchumi wake, na usalama wake, anajua kabisa Mungu hayupo katikati ya huo mchezo, Na dhambi nyingine nyingi zinazofanywa na wanadamu ndio hivyo hivyo, hazihitaji biblia kuzihakiki, tayari zimeshajihakiki zenyewe ndani yetu.

Sasa tukirudi kwenye suala la KU-BET na lenyewe ni hivyo hivyo, Kubet ni kamari, isipokuwa iliyohalalishwa na nchi.

Hakuna mahali popote katika biblia imezungumzia habari za kubet…Lakini ipo INJILI YA MILELE ndani ya kila mtu…Inayokushuhudia kuwa hichi kitu sio sahihi.

Kama ukichunguza kwa makini mtu anayebet kabla hajaanza kufanya hicho kitu kina kitu ndani yake kinamshtua kwanza, anaanza kukosa amani na anakuwa na mashaka mashaka na huo mchezo, ndio hapo ataanza kujiuliza, hivi kweli huu mchezo ni wa KiMungu? Hayo ndio maswali ya kwanza mtu anayoanza kujiuliza kabla ya kuingia…Na anapoikataa hiyo sauti na kuingia huko, baadaye haisikii tena ndio anaanza kuona ni mchezo wa kawaida tu usio na madhara yoyote, lakini siku za kwanza kwanza atakwenda mpaka kuuliza watu kama ni sawa kuucheza au la?..Ukishaona hali kama hiyo jua kabisa kuna kitu cha hatari unakiendea..

Na ni kwanini unaanza kusikia hivyo viashiria kabla hata hujajiingiza kwenye huo mchezo? Ni kwasababu mchezo huo ni wa kishetani, na unamwingiza mtu kwenye roho moja kwa moja..Mashirika yote ya betting ulimwenguni yanafanya kazi ya shetani kama ulikuwa hulijui hilo ndugu yangu.., yanafanya mambo mengi ya siri ambayo shetani hawezi kuruhusu watu wayajue, ndio mashirika yanayokusanya utajiri mkubwa kwa shetani..Na hayo ndiyo yatakuja kushirikiana na mpinga-Kristo katika kumpa nguvu.

Mashirika hayo mengi yanamilikiwa na vikundi vya kichawi vikubwa duniani kama freemason, brotherhood, yana kivuli cha kulipa kodi, lakini yana agenda nyingine za siri nyuma ya pazia, yanapokea maagizo kutoka kwa lusifa mwenyewe kufadhili mikutano ya hadhara ya ushoga ili kuipalilia roho ya ushoga duniani,..kufadhili haki za mashoga na wasagaji, kufadhili agenda za utoaji mimba n.k kwa nje yanaonekana ni mazuri, lakini wamiliki wa mashirika hayo ni mawakala wa shetani mwenyewe waliowekwa na shetani kwa kazi hiyo.

Na baadhi ya mashirika hayo pia yanafadhili ugaidi kwa siri, ili kuihimiza dunia ilete ustaarabu mpya wa ulimwengu, na pia yanatumia fedha nyingi kuyanyanyua mashirika mengine madogo madogo yanayofanya kazi kama hizo za kuiharibu dunia.…Shetani anafanya kazi kubwa kuachilia mapepo ambayo yatahakikisha watu wengi wanakwenda kubet na kuhakikisha wanakosa, ili aongeze fedha nyingi katika ufalme wake kwaajili ya kumwekea njia mpinga-Kristo. Biblia inasema shetani anampa aliyewake jinsi apendavyo, yeye ndiye anayechagua ni nani apate na ni nani akose, na kumbuka anawapa walio wake, hawezi kumpa ambaye anajua hamsujudii wala haongezi chochote katika ufalme wake..

Mtu anayekwenda kubet kuna pepo Fulani linamvaa, ambalo litamfanya Kesho arudi tena kufanya hivyo hata kama atakosa mara ngapi lakini hatachoka kubet…Mwisho wa siku unakuwa fukara, na bado taabu yako umempa shetani aitumie.

Kwahiyo Biblia inatuambia tutoke huko? (2 Wakoritho 6:15-18)..tutatokaje! kwa kutubu na kudhamiria kuacha hivyo vitu…Biblia inasema shina moja la mabaya yote ni kupenda fedha, unapotamani kupata fedha za ghafla, tambua ni kama mtu aliyewasha WIFI kwenye simu yake, mtu aliyekaribu na yeye anaweza kuupata mtandao wake, na kadhalika mtu anayependa au kutaka kupata fedha za ghafla, anakuwa ni rahisi sana kuonekana kwenye mitandao ya mashetani na kuvaliwa na maroho…

1 Timotheo 6:9 “Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu.

10 Maana SHINA MOJA LA MABAYA YA KILA NAMNA NI KUPENDA FEDHA; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.

11 Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole”.

Hivyo tunaonywa tusipende fedha za ghafla! huo ni mtego mkubwa sana shetani anaoutumia…Tembea huko barabarani kwenye nguzo za umeme uone vibao vya waganga,..wote kitu cha kwanza watakwambia…njoo upate utajiri!..Mpango wa Mungu ni kuchuma kidogo kidogo…Sio kwamba hapendi tupate kingi hapana! Ndio mpango wake tuwe na vingi Lakini tukusanye kidogo kidogo…….Tukusanye shilingi mia, mia, kuanzia asubuhi hadi jioni na kupata milioni kumi hiyo ni sawa!….lakini kupata milioni kumi ndani ya dakika moja ogopa sana hizo njia!..Vingi vya hivyo ni mitego ya shetani, Na ndio betting inachofanya.

Mithali 13: 11 “Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa”.

Jiunge na group letu la Whatsapp la masomo ya kila siku kwa kubofya hapa >> Group-Whatsapp

Bwana akubariki sana.


Mada Zinazoendana:

INJILI YA MILELE.

JE! UKRISTO UNAMPA MTU DHAMANA YA KUWA TAJIRI?

KUCHEZA KARATA NI SAHIHI KWA MTU ALIYE MKRITO?

NJIA YA ‘UTAJIRI MKUU’ KWA KIJANA.


Rudi Nyumbani

Print this post

FANYA MAAMUZI KABLA HAZIJAKARIBIA SIKU ZA HATARI.

Mhubiri 12: 1 “MKUMBUKE MUUMBA WAKO SIKU ZA UJANA WAKO, KABLA HAZIJAJA SIKU ZILIZO MBAYA, Wala HAIJAKARIBIA MIAKA utakaposema, MIMI SINA FURAHA KATIKA HIYO”.

Biblia inasema “Mkumbuke” ikiwa na maana kuwa ni wakati ambao kuna “kusahau” wakati wa kupumbazwa na mambo mengi, …Na huo wakati si mwingine zaidi ya wakati wa UJANA. Na biblia inasema pia zitakuja nyakati au siku zilizo mbaya, ambazo zitakuwa sio za furaha, nyakati zisizofaa tena kumgeukia yeye,..

Tafakari kwa makini hiyo sentesi “Mkumbuke muumba wako kabla hazijaja siku !!” Ina maana sio kila wakati unafaa katika kumgeukia Mungu..Ni rahisi kusema nitakapokuwa MZEE nitamgeukia Mungu, au nitakapofikia kipindi Fulani au nitakapokuwa nimezidiwa sana, au nitakapokuwa nimefilisika sana, au nitakapokuwa katika ugonjwa wa kufisha, au siku nitakayokaribia kufa ndiyo nitakuwa karibu na Mungu. Ndugu hiyo ni hatari sana neema ya Mungu haiotewi. yeye anasema “mkumbuke Muumba wako kabla hazijaja siku zilizo mbaya”..zingatia hilo neno kabla!! Kabla!!,.Kumbuka Wengi wanaopata Neema ya kuokolewa katika hizo nyakati zilizo mbaya ni wale tu ambao hawajawahi kabisa kuisikia injili hapo nyuma, mfano wa Yule muhalifu aliyesulibiwa na Kristo pale Msalabani. Hivyo usiliweke hilo akilini kwa sisi wa kizazi hiki ambacho injili ya Kristo inahubiriwa kila siku barabarani lakini hatutaki kusikia au tunapuuzia tukitumaini itafika siku tu tumtafuta Mungu..Hilo tuliondoe akilini.

SASA HIZO SIKU ZILIZO MBAYA(au siku za matatizo) NI ZIPI? AMBAZO TUMEONYWA TUMKUMBUKE MUUMBA WETU KABLA HAZIJAFIKA??

Ukizidi kusoma mistari inayofuata utaona hizo siku siku mbaya zinazozungumziwa hapo ni zipi. Ukiwa na nafasi binafsi utasoma, sura yote ya 12,lakini kwasasa tutaangalia vipengele hivyo vikuu.

1)KABLA JUA, NA NURU, NA MWEZI, NA NYOTA, HAVIJATIWA GIZA; (Mhubiri 12:1-14)

Hapo anazungumzia siku ya Bwana inayotisha, ambayo ipo mbioni kuijilia dunia nzima,.Biblia inasema tumkumbuke Bwana kabla hiyo siku haijafika, siku ambayo Jua litatiwa giza, na mwenzi hautatoa nuru yake, na nyota za mbinguni zitakapoanguka…Siku ya kutisha ya hasira ya Mungu mwenyezi.

Amosi 5: 18 “Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya Bwana; kwani kuitamani siku ya Bwana? NI GIZA, WALA SI NURU.

19 Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma.

20 Je! SIKU YA BWANA HAITAKUWA GIZA, WALA SI NURU? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga” 

Amosi 8: 9 “Tena itakuwa siku hiyo, asema Bwana MUNGU, nitalifanya JUA LITUE WAKATI WA ADHUHURI, NAMI NITAITIA NCHI GIZA WAKATI WA NURU YA MCHANA.

10 Nami nitazigeuza sikukuu zenu kuwa maombolezo, na nyimbo zenu zote kuwa vilio; nami nitatia nguo za magunia katika viuno vyote, na upaa katika kila kichwa; nami nitayafanya haya kuwa kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu.”

Unaona sisi watu wa kizazi hichi, tunaishi karibu na siku hizo, mambo yote yanathibitisha hilo, siku yoyote mwisho unafika, kwani katika kalenda ya kibiblia tunaishi katika kanisa la mwisho linalojulikana kama Laodikia (Ufunuo 3).Na ndio kanisa hilo litakaloshuhudia mambo yote. Unyakuo pamoja na dhiki kuu.

2) KABLA YA KURUDI MAWINGU BAADA YA MVUA; (Mhubiri 12:2)

Kabla ya kurudi mawingu baada ya Mvua, inafunua “kipindi cha njaa kuanza” Kama vile Farao alivyoambiwa na Bwana itakuja miaka 7 ya neema, ya mvua tele na kisha baada ya hiyo itaanza miaka mingine 7 ya njaa, isiyokuwa na Mvua, kupanda wala kuvuna. Ndio kitu kile kile Biblia inachokizungumzia hapa, kwamba baada ya mvua mawingu yatarudi na kuanza vipindi vya njaa, Biblia inatabiri pia siku za mwisho Bwana ataleta njaa juu ya nchi, si njaa ya chakula bali njaa ya KUKOSA KUYASIKIA MANENO YA MUNGU.

Amosi 8: 11 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana.

12 Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione.

13 Siku hiyo wanawali wazuri na wavulana watazimia kwa kiu”.

Neno la Mungu linatuonya TUMKUMBUKE MUUMBA WETU KABLA HIZO SIKU HAZIJAFIKA, Na hizo siku zimeshaanza kujitokeza duniani…Tunaona sasa Njaa ya Neno la Mungu imeanza kuongezeka..

3) KABLA HAIJAKATIKA KAMBA YA FEDHA; (Mhubiri 12:6)

Kabla ya uchumi wako binafsi kuanguka, Unaona hapo?? usiseme siku nitakapoishiwa fedha au nitakapokuwa naumwa sana ndipo nitakapomgeukia Mungu, au siku nitakapokaribia kufa..Bwana hadhihakiwi, yeye anasema TUMKUMBUKE KABLA HIZO SIKU HAZIJAFIKA, ikiwa na maana kuwa kama tutamkataa leo kwa makusudi tukiwa katika hali nzuri, hatakuwa na sisi wakati wa matatizo. Tukimkana leo yeye wakati wa ujana wetu, na yeye atatukana sisi wakati wa matatizo yetu, kumbuka Watakaompata katika hali za matatizo ni wale tu ambao hawakuwahi kuisikia injili hapo kabla, lakini kama ulishawahi kuisikia na unaipuuzia hakutakuwa na nafasi ya pili wakati matatizo yatakapokukumba.

4) KABLA MAVUMBI KUIRUDIA NCHI KAMA YALIVYOKUWA, NAYO ROHO KUMRUDIA MUNGU ALIYEITOA. (Mhubiri 12:7)

Biblia inasema katika Waebrania 9:27 “MTU AMEANDIKIWA KUFA MARA MOJA NA BAADA YA KIFO HUKUMU”..Ndugu, hakuna maombi yoyote yanayoweza kumsaidia mtu baada ya kufa, Mafundisho ya Toharani hayapo katika biblia takatifu, ni mafundisho ya Yule mwovu, ili kuwafariji watu kuwa baada ya kufa unaweza ukaombewa na ukatolewa katika maumivu ya moto, hakuna kitu kama hicho, baada ya kifo ni hukumu ndivyo Neno linavyosema, ndio maana hapa Bwana anatuonya

“mkumbuke Muumba wako kabla roho yako haijamrudia yeye” ikiwa na maana kuwa baada ya kufa hakuna nafasi yoyote ya kumgeukia Mungu, au kuokoka na lile ziwa la Moto, kama ulimkataa yeye katika enzi za uhai wako.

Ujana wako unaweza usiwe tu ujana wa mwili wako, bali hata ujana wa akili yako, Na ujana wa akili yako ndio huu, ambao unaweza ukapata nafasi ya kusikiliza Neno la Mungu, Siku ile hutasema hukusikia, Leo hii mkumbuke Muumba wako, kabla ya siku za matatizo kufika, kabla ya vipindi vya njaa, shida, mauti, kabla ya kurudi kwa pili kwa Kristo, kabla ya Mpinga-Kristo kunyanyuka, kabla ya siku ya ghadhabu ya Mungu kumiminwa, uukumbuke msalaba, usiwe miongoni mwa hao wanaodhihaki ambao biblia inasema “Mungu amewaletea nguvu ya upotevu” wauamini uongo ili wapotee. Ujana wako unautumiaje?, nguvu zako unampa nani?.

Biblia inasema nimewaandikia ninyi vijana kwasababu mna nguvu ya kumshinda shetani, hii ikiwa na maana kuwa utafika wakati hizo nguvu hutakuwa nazo za kumpinga shetani maisha mwako kama hutakuwa ndani ya Kristo. Embu jaribu kifikiria unapata faida gani leo unavyoishi katika hayo maisha ya dhambi?. Huoni kama upo katika hatari kubwa sana. Tubu angali bado upo katika siku njema, siku za neema, siku ambazo bado hazijawa mbaya, tuipishe ghadhabu ya Mungu ambayo hivi karibuni inakwenda kumiminwa katika dunia nzima.

Ni maombi yangu kuwa Bwana atakujali kufanyika kiumbe kipya.

Tafadhali “share” kwa wengine, 

Print this post

NJIA YA ‘UTAJIRI MKUU’ KWA KIJANA.

Kama tunavyofahamu kuna hatua tatu za maisha ya mwanadamu; Kuna Utoto, Ujana, na Uzee. Na hatua ambayo mtu analazimika kufanya maamuzi juu ya hatma ya maisha yake ni Ujana. Biblia inasema katika Yeremia 21:8b”….Tazama naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti.” Njia hizi zinatokea mbele ya mtu anapofikia UJANANI. Hivyo inahitajika busara nyingi na hekima ya Mungu katika kuchagua njia ya kuiendea.

Katika biblia tunaweza kujifunza mifano ya vijana wawili ambao walifanya maamuzi ya kuchagua njia za kuendea na hatma zao zilivyokuwa mwishoni.

KIJANA WA KWANZA:

Mathayo 19:16-22

“16 Na tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?

17 Akamwambia Kwani kuniuliza habari ya wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri.

18 Akamwambia, Zipi? Yesu akasema, Ni hizi, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo,

19 Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende jirani yako kama nafsi yako.

20 Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena?

21 Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.

22 Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi”.

Tunamwona kijana huyu alijaribu kumfuata Yesu lakini kuna vikwazo vilikuwa mbele yake vinamkwamisha, ni mtu wa kipekee ambaye Bwana Yesu alimpenda hata kufikia hatua ya kumpa nafasi ya kipekee ya kufanyika moja wanafunzi wake, pengine angefanikiwa mtihani ule angekuwa mwanafunzi wa 13, na pengine leo hii tungekuwa tunasoma nyaraka zake, au angekuwa miongoni mwa watakao keti pamoja na Kristo katika ufalme wake kuwahukumu kabila 12 za Israeli, Lakini kikwazo kimoja tu nacho ni cha MALI kilimfanya akunje uso wake na kuondoka kwa huzuni, na kuipoteza nafasi ile ya kipekee. Pengine alisema moyoni mwake, ;kwa taabu nilizojitesa kupata utajiri wote huu, halafu leo hii mtu huyu mmoja anataka kunigeuza kuwa maskini ndani ya siku moja, hilo haliwezekani?. Kwakweli jambo hilo lisingeweza kumuingia akilini kama lisivyoweza kuwaingia akilini watu wengi leo.

Kumbuka pia kijana huyu sio kana kwamba alikuwa ni mtenda dhambi la! Alikuwa anaenenda katika haki tangu utoto wake, lakini kuna kitu aliona bado kimepunguka ndani ya moyo wake, kwamba hana uzima wa milele. Na alipomwendea Yesu na kumuuliza! Akaambiwa maneno yale. Lakini hakufahamu kwamba Yesu kumwambia vile sio kana kwamba anataka kumwekea kitanzi cha kuwa maskini la! Bali ni kumtengeneza awe kama wanafunzi wake wengine..na ndio maana kama ukiendelea kusoma mbele kidogo utaona aliwaambia wale wanafunzi wake wale walioacha kila kitu na kumfuata kuwa watapata mara mia na kuurithi uzima wa milele, soma;

Mathayo 19:27-29 “27 Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?

28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.

29 Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele”.

Hivyo kama kijana yule angekuwa mvumilivu tu, baada ya muda mchache haya maneno ya faraja yangekuwa sehemu yake, na huo uzima wa milele alioukuwa anautafuta angeupata pamoja na mali zake mara mia. Lakini kwa kuwa alipenda kuweka MALI kwanza basi alimkosa Mungu. Alishindwa kufahamu yale maneno yanayosema 

“Mathayo 16:25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.

26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?”.

Tunaona habari ya YULE KIJANA ikaishia pale pale, mali alibakiwa nazo lakini Kristo alimkosa.

KIJANA WA PILI:

Lakini tumwangalie kijana mwingine aliyechukua maamuzi sahihi katika maisha yake kwa kuamua kumfuata KRISTO kwa moyo wake wote, na huyu si mwingine zaidi ya kijana MUSA. Kijana huyu alizaliwa katika jumba la kifalme la Farao, hakujua shida, wala njaa ni nini!! Biblia inasema ni mtu aliyekuwa na Elimu kubwa ya kidunia kwasasa tunaweza tukasema ni msomi mwenye PH.D, Alikuwa ni mwenye ujuzi wa maneno, alikuwa ni tajiri sana katika ngome ya Farao ambayo kwa wakati huo ilikuwa inatawala dunia nzima, ni kijana ambaye angetaka chochote angepata, angetaka wanawake wazuri kuliko wote angepata, kama ni viwanja, na mashamba alikuwa navyo, na zaidi ya yote umaarufu alikuwa nao tayari.

Lakini ilifika wakati akakutana na KRISTO moyoni mwake, pengine maneno kama yale yale yalimjia moyoni mwake, “nina kila kitu lakini nimepungukiwa na nini, ili niupate uzima wa milele??”. Tunasoma kwenye biblia Musa akaacha vyote kwa ajili ya Kristo akakimbilia nyikani, kwenye taabu kwa ajili ya Mungu wake.

Waebrania 11: 24-27

“Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;

25 akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;

26 AKIHESABU YA KUWA KUSHUTUMIWA KWAKE KRISTO NI UTAJIRI MKUU KULIKO HAZINA ZA MISRI; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.

27 Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana.”

Hivyo Baada ya miaka 40 tunamwona Musa tena, akirudi Misri akiwa kama mungu kwa Farao, biblia inasema hivyo, zaidi ya yote japo aliacha ndugu zake, mashamba n.k. alikuja kuvipata vyote na zaidi, Wana wa Israeli wote walikuwa kama watoto wa Musa, na zaidi ya yote hakukuwahi nyanyuka nabii kama Musa aliyezungumza na Mungu uso kwa uso, mpaka leo hii tunaisoma habari yake, Mungu alimpa kumbukumbuku lisilofutika milele, tunamwona miaka mingi baada ya kufa,akitokea na kuongea na Bwana YESU kule mlimani.(Mathayo 17). Kwasababu alihesabu kushutumiwa kwake Kristo ni UTAJIRI MKUU kuliko hazina zote za Misri.

Vivyo hivyo na sisi je! Tumehesabu hivyo??. Je! Umehesabu kushutumiwa kwa kuacha dhambi, anasa, ulevi, uasherati, biashara haramu, rushwa, fashion, ufisadi, ibada za sanamu n.k. kwa ajili ya Kristo kuwa ni utajiri mkuu kuliko mambo yote ya ulimwengu?.

Wewe ni kijana sasa ni wakati wa kuchukua uamuzi sahihi kwa kumfuata BWANA YESU KRISTO kwa gharama zozote utakazoambiwa ukijua ya kwamba Mungu hafanyi hivyo kwa kukutesa bali kukupa tumaini zuri katika siku zako za mwisho. Kama ni utafutaji mali ndio unaokusonga jaribu kuweka kwanza kando uutafute ufalme wake na haki yake. Kama ni cheo au ukubwa vinakusonga, viweke kwanza kando, umtafute Mungu, na hayo mengine yatafuata huko baadaye.

Hivyo chukua uamuzi kama wa kijana Musa, na sio Yule kijana mwingine. Wakati ndio huu biblia inasema

Mhubiri 12: 1 Mkumbuke Muumba wako SIKU ZA UJANA WAKO, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.”

Na Pia inasema.

 Maombolezo 3:26 “Ni vema mtu autarajie wokovu wa Bwana Na kumngojea kwa utulivu. Ni vema mwanadamu aichukue nira WAKATI WA UJANA WAKE.”

Ni maombi yangu kuwa ujana wako utaishia katika njia njema ya uzima.

Print this post