Title July 2023

Wivu ni nini na kuna aina ngapi za Wivu?

Wivu ni nini kibiblia na kuna aina ngapi za Wivu unaowapata watu? Na je ni dhambi kuwa na Wivu?

Katika kitabu cha Wagalatia biblia imetaja “Wivu” kuwa ni mojawapo ya tunda la mwili. Sasa swali ninapopata wivu wa kimaendeleo nafanya dhambi? Au ninapopata wivu wa mwanandoa mwenzangu kukosa uaminifu je nayo ni dhambi?


Jibu: Tusome,

Wagalatia 5:19-21
19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi..

20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira……….. ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu”

Ni kweli Wivu ni mojawapo wa matendo ya mwili ambayo ni dhambi mtu kuwa nayo, lakini kama ya kuingia ndani zaidi katika andiko hili..ni vizuri kuzijua kwanza aina za wivu..

Upo “Wivu wa kiMungu” na vile vile upo “wivu wa kidunia”, ni kama tu “hasira” au “hofu”. Ipo hasira ya kiMungu na vile vile ipo hasira ya kidunia au ya kiulimwengu.

Hasira ya kidunia ni ile inayoyoishia au inayompelekea mtu kutenda dhambi, kama kutukana, kuua, kuonea, kuiba n.k.. kwaufupi matunda yake ni mabaya daima… Lakini hasira ya kiMungu ni ile inaiyoishia katika kumjenga mtu na kumtengeneza zaidi, na kumrudisha kwa Mungu au katika njia sahihi kwa upendo.

Mfano wa hasira ya kiMungu ni ile Bwana Yesu aliyokuwa nayo juu ya Mafarisayo na Masadukayo.
Utaona Mafarisayo na Masadukayo walikuwa wanamwudhi sana Bwana lakini hasira ya Bwana haikuishia katika kuwatukana, au kuwashushia moto na kuwaangamiza ingawa alikuwa na uwezo huo, au kuwaharibu kwa njia yoyote ile… bali katika kuwahurumia..

Marko 3:1-5 “Akaingia tena katika sinagogi; na palikuwako huko mtu mwenye mkono uliopooza;

2 wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato; wapate kumshitaki.

3 Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, Simama katikati.

4 Akawauliza, Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya roho au kuiua? Wakanyamaza.

5 AKAWAKAZIA MACHO PANDE ZOTE KWA HASIRA, AKIONA HUZUNI kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena”.

Hasira ya namna hii biblia imesema tuwe nayo ila tusitende dhambi, jua lisizame tukiwa nayo bado mioyoni..(Waefeso 4:26).

Sasa tukirudi katika Mantiki ya hofu na wivu ni hivyo hivyo, ipo hofu ya kiMungu na ya ipo hofu ya kidunia, vile vile upo wivu wa kiMungu na upo wivu wa kidunia.
Wivu wa kidunia ni ule unaoishia kutenda dhambi.. Mfano mtu atamwonea mwingine wivu kwasababu kapata kitu fulani ambacho yeye hajakipata, hivyo atatamani au atatafuta njia yule mtu akipoteze kile kitu ndipo atulie.

Mfano wa wivu huu ni ule aliokuwa nao Kaini, alipoona sadaka ya ndugu yake imekubaliwa na kwake imekataliwa. Badala atafute njia ya kuboresha sadaka yake ikubalike mbele za Mungu kama ya ndugu yake, yeye akatafuta kumwua ndugu yake, (wivu unaoish kuleta chuki, masengenyo, vinyongo, visasi ni wa kishetani)..ambao ni dhambi mtu kuwa nao sawasawa na hiyo Wagalatia 5:20.

Wivu wa kiMungu ni ule unaomfanya mtu atamani kuwa mwema kama mwingine alivyo mwema, unaomfanya mtu atamani kufanya vizuri kama mwingine anavyofanya vizuri pasipo kumtakia madhara yule mwingine, (kwa ufupi haufurahii kuanguka wala kupunguka kwa mwingine)..zaidi sana mafanikio ya mwingine yanakuwa siku zote ni darasa kwake….

Wivu huu sio mbaya na si dhambi mtu kuwa nao, kwasababu matunda yake ni mazuri..
Mfano wa huu ni ule Mtume Paulo, aliojaribu kuutia kwa ndugu zake Waisraeli ili wamgeukie Mungu zaidi.

Warumi 11:14 “nipate kuwatia wivu walio damu moja na mimi na kuwaokoa baadhi yao”.

Lakini pia upo Wivu mwingine wa KiMungu ambao unaishia kuharibu vitu vya kishetani lakini si kimharibu mtu..

Mfano wa wivu huu ni alikuwa nao Bwana Yesu juu ya Hekalu la Mungu, alipoingia na kukuta watu wanafanya biashara ndani ya hekalu, maandiko yanasema Bwana alizipindua meza zao, na kuharibu biashara zao lakini si kuwaharibu wao.. Na wanafunzi wake wakakumbuka andiko la wivu wa nyumba ya Mungu utamla (Yohana 2:17).

Wivu huu pia na sisi tunapaswa tuwe nao tunapoona kazi ya Mungu inachafuka, ni lazima tusimame kuziharibu hizo kazi za shetani kwa maombi na kwa mafundisho sahihi, lakini si kwa kuwadhuru watu au kuwatukana, au kuwaletea madhara yoyote ya kimwili.

Wivu wa namna hii pia upo katikati ya wanandoa na wanafamilia, kama kuna kiashiria chochote cha mwanandoa au mwanafamilia kutoka kwenye mstari wa uaminifu, au nidhamu, au maadili au heshima…Wivu wa namna hii huwa unanyanyuka!, sasa vibaya yule aliyemwaminifu, au aliye imara katika ndoa au familia kusimama na kuharibu au kuziba upenyo wowote ambao shetani anataka kuchukua nafasi ndani ya hiyo familia au ndoa…lakini kwa hekima pasipo kumdhuru mtu.

Lakini wivu wa wanandoa au wanafamilia unaoishia kuua huo hautokani na Mungu!.

Je na wewe unasumbuliwa na dhambi ya Wivu wa kidunia ambao unaishia kusengenya, kuona hasira, kuua, kutukana n.k Na hujui utatokaje katika hilo shimo?.

Bwana Yesu amekuja kwaajili ya kututoa katika hayo mashimo, kwa nguvu zetu hatuwezi kutoka huko wala kujitoa.
Nguvu pekee ya kututoa huko ni kwa njia kwa ya Roho Mtakatifu, kwa somo kamili kuhusiana na Roho Mtakatifu, jinsi ya kumpomea na jinsi.atakavyokuwezesha kushinda yale usiyoweza kuyashinda basi tutumie ujumbe inbox ili uweze kupata somo hilo.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JIHADHARI NA DHAMBI YA WIVU/HUSUDA.

Kuhubiri injili kwa husuda na fitina ndio kupi?

MWE NA HASIRA, ILA MSITENDE DHAMBI.

USHUJAA WA ROHONI HAUANGALII UZOEFU WAKO.

USIWE NA HOFU, USHUKAPO CHINI.

Rudi nyumbani

Print this post

Kwanini samaki wasio na mapezi na magamba hawakuruhusiwa kuliwa?

Mambo ya Walawi 11:9-12

[9]Katika hao wote walio ndani ya maji mtakula hawa; kila aliye na mapezi na magamba, ndani ya hayo maji, na ndani ya bahari, na ndani ya mito, mtakula hao.

[10]Na hao wote wasio na mapezi na magamba, ndani ya bahari, na ndani ya mito, katika hao waendao majini, na katika wote wenye uhai, waliomo majini, hao ni machukizo kwenu,

[11]watakuwa machukizo kwenu; msiile nyama yao, na mizoga yao itakuwa machukizo kwenu.

[12]Kila asiye na mapezi wala magamba aliye ndani ya maji ni machukizo kwenu.

Mapezi ya samaki, ni vile vitu kama mbawa ngumu zenye mfano wa miiba  zinazokaa Kwa juu, au pembeni au nyuma mwa mwili wa samaki.Ukitazama samaki kama perege, sato au sangara utaona mapezi Yao.Na faida za mapezi hayo ni kuwa yanasaidia kuogelea, kuelea vema kwenye maji, kukunja Kona, kuongeza kasi na kusimama au kugeuka Kwa haraka.

Halikadhalika samaki waliokuwa na magamba ndio tu walioruhusiwa kuliwa. Na magamba yaliwasaidia kujilinda na maadui au wadudu wavamiaji kwenye mwili. Kwani ngozi ya samaki ni laini hivyo isipofunikwa na magamba magumu kama yale, meno makali ya maadui yanapopita ni rahisi kujeruhiwa, Yanakaa kama dirii kifuani mwa askari.

Lakini si samaki wote walikuwa na haya mapezi na magamba, Bali wengine hawakuwa nayo mfano wa Hawa ni kama kambale, papa, pomboo, pwezi.

Sasa Kwanini viumbe hivyo vikatazwe kuliwa na ufunuo wake ni upi Rohoni?

Kama tunavyofahamu agano la kale ni kivuli Cha agano jipya, sio kwamba viumbe hivyo vikiliwa vitamkosesha mtu mbingu, au vitamnajisi roho , hapana. Bali vilifanywa vile kwa makusudi ili kutupitishia sisi ujumbe wa Rohoni katika agano letu jipya. Kwamba na sisi kama tutafanana na mojawapo wa viumbe hivyo Rohoni basi tunakuwa najisi mbele za Mungu.

Samaki mwenye magamba ni mwenye ulinzi wa kutosha dhidi ya mashambulizi ya maadui. Na sisi tunapokosa ulinzi wa Rohoni mfano wa yule askari anayezungumziwa katika Waefeso 6, mwenye dirii ya haki kifuani, ngao ya Imani mkononi na chepeo ya wokovu kichwani. Tunakuwa ni wadhaifu, kiasi Cha kutoweza simama mbele ya adui yetu shetani. Hivyo ni kuhakikisha kuwa umesimama imara katika wokovu wako, lakini pia utambue haki uliyopewa katika  msalaba wa Yesu Kristo na Imani Yako timilifu ndani ya wokovu wako. Hapo utakuwa umejidhatiti vya kutosha mfano wa samaki mwenye gamba gumu, au mamba aliyefunikiwa na ngozi yenye gamba.

Ayubu 41:13 “Ni nani awezaye kumbambua magamba yake? Ni nani atakayepenya dirii yake maradufu?  14 Ni nani awezaye kuifungua milango ya uso wake? Meno yake yatisha kandokando yake.  15 Magamba yake yenye nguvu ndiyo fahari yake, Yamefungamana pamoja kama kwa kufungwa kwa muhuri.  16 Jinsi yalivyoshikamana Hata upepo hauwezi kupita kati.  17 Yamefungamana pamoja; Yameshikamana, hata hayawezekani kutengwa”

Vilevile samaki aliyekuwa na mapezi alikuwa ni mwepesi kukatiza katika maji. Ni sawa na mabawa Kwa ndege, au miguu na kwa mtu. Hivyo na sisi katika ulimwengu huu wa dhambi ili tusionekane kuwa najisi tuvae mapezi yetu ambayo maandiko yanasema .Ndio ule utayari wa kuihubiri injili.

Waefeso 6:15

[15]na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

Tusienende Kama watu wasio na kusudi maalumu la kufanya duniani, tuvae utayari, ndio mapezi yetu tutembee ulimwengu kote kiuhubiri/ kushuhudia habari njema.Kwasababu tukikosa haya, siku ile ya mwisho, tutatengwa samaki wema na waovu..Kisha wale waovu watatupwa nje.

Mathayo 13:47  ‘Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna;

48  hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. 49  Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki’

Tusiwe samaki najisi.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Injili iliyopo kwa Samaki aina ya Eeli.

Pomboo ni nini katika biblia?(Kutoka 25:5, Ezekieli 16:10)

Mjombakaka ni nani kwenye maandiko? (Walawi 11:29)

Lumbwi ni nini katika biblia?

Je! Ni kweli kuna samaki mtu (Nguva) Baharini.

Je! Ni dhambi kumpiga au kumuua mnyama bila sababu yoyote?

Manyoyota ni nini (Ayubu 37:6)

Rudi nyumbani

Print this post

Nini Maana ya Adamu?

Nini tafsiri ya jina Adamu,

Adamu ni neno la kiebrania lenye maana ya “wa udongo” yaani aliyetokana na udongo/ardhi. Mtu wa kwanza kuumbwa alipewa jina hilo Adamu na Mungu mwenyewe kufuatia asili yake alipotolewa.

Mwanzo 2:7 “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai”.

Na jina “Adamu” hakupewa mtu mmoja tu bali wote wawili (yaani mwanamume na mwanamke)

Mwanzo 5:1” Hiki ndicho kitabu cha vizazi vya Adamu. Siku ile Mungu alipoumba mtu, kwa sura ya Mungu alimfanya;

 2 mwanamume na mwanamke aliwaumba, akawabariki AKAWAITA JINA LAO ADAMU, siku ile walipoumbwa”.

Kwa urefu na kina Zaidi, kwanini Mungu awape wote wawili jina moja fungua hapa >>> Kwanini Mungu aliwaita Adamu na Hawa jina moja?

Watoto wote waliozaliwa baada ya Adamu, wakaitwa Wana-damu. (wana wa aliyekuwa wa udongo). Hivyo na sisi wote asili ya miili yetu ni ardhini, ndio maana tunakufa na miili yetu inaoza ardhini.

Lakini baada ya maisha haya, kama tukishinda vita vya kiimani vya ulimwenguni,  maandiko yanasema tutavikwa miili mipya ya kimbinguni, hivyo hatutaitwa tena wanadamu, wala hatutaishi kwa kula na kunywa kama wanyama, wala tamaa za mwili hazitakuwepo tena bali tutakuwa kama Malaika kwasababu tutapewa miili mingine isiyo ya udongo.

Marko 12:25 “Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni”.

Je una tumaini la kuvikwa mwili mpya wa kimbinguni?..

Kumbuka tumaini hilo na uhakika huo tunaupata tu endapo tupo ndani ya Kristo, na tunaishi maisha yanayompendeza yeye.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Mungu anatufundisha kusamehe mara saba sabini, ila Kwanini yeye hakumsamehe Adamu alipoasi?.

Tofauti kati ya mtu na mwanadamu ni ipi?

KWANINI YESU NI ADAMU WA PILI?

Kwanini Kristo aitwe Mwana-kondoo. (Yohana 1:29)

JE! Kaini alimpatia mke wake wapi?

Rudi nyumbani

Print this post

ALIPOKUWA ANGALI MBALI, BABA YAKE ALIMWONA.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo Bwana Yesu. Karibu katika kujifunza maneno ya uzima ya mwokozi wetu.

Leo tutaona jinsi “moyo wa toba ya kweli” unavyopokelewa kitofauti sana na Mungu. Kama tunavyoifahamu ile habari ya mwana mpotevu, jinsi alivyoingiwa na tamaa, ya kwenda kuanzisha maisha yake ya anasa mbali na baba yake. Na siku zilipozidi kwenda, mali zilipoisha, njaa kali ikamkuta Akaanza kula vyakula vya majalalani ambavyo viliwastahili tu nguruwe.  Lakini Biblia inasema, hakung’ang’ania tu  kuendelea kutaabika katika hali ile ile milele mpaka kufa kwake. Bali alijinyenyekeza akazingatia kurudi kwa baba yake akiwa na moyo wa toba, ili baba yake amfanye tu mtumwa. Na alipofanya vile, akiwa njiani anarudi, biblia inatumbia kuna tukio lilitokea.

Na tukio lenyewe ni “kuonekana kwake tokea mbali” . Tusome;

Luka 15:17  “Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. 18  Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; 19  sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. 20  Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. 21  Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. 22  Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; 23  mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; 24  kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia”

Embu tafakari, iweje, Baba yake ndio awe wa kwanza kumwona tokea mbali na sio watumwa ambao sikuzote wao ndio wanaosimama mlangoni mwa nyumba au kuzunguka zunguka huku na huko, au kwanini isiwe hata ndugu zake wengine, badala yake baba yake ndio anayekuwa wa kwanza kumwona?

Sio kana kwamba hao wengine walikuwa hawali mboga za majani, hawaoni mbali mambo yao kuwa hafifu, hapana, bali Baba yake alikuwa na jicho lingine la rohoni kama DARUBINI. Hilo lilikuwa linaona mahangaiko, na manyanyaso ya mwanaye tokea mbali, kiasi kwamba alipofanya geuko moyoni mwake, tayari baba yake alishahisi, na akiwa njiani anakuja tayari baba yake alishajua kuwa mwanawe yupo njiani. Hivyo kabla hata mtoto hajamwona Baba, kabla hata hajaifikia nyumba yao akiwa kilomita kadhaa mbali, tayari baba alikwenda kukutana naye na kukumbatia na kumbusu sana.

Ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu. Pale mtu anapokuwa na moyo wa toba ya kweli rohoni, haihitaji wewe kwenda kusema maneno mengi sana mbele za Mungu, kana kwamba ndio utasikiwa. Yeye anayo darubini yake, Lakini kule kuzingatia tu kurudi kwa Baba yako wa mbinguni, ukaanza kuchukua hatua. Hiyo ni toba kubwa sana ambayo itamfanya Mungu, kabla ya wewe kumfikia tayari ameshakufikia, haraka sana na kukupa tiba ya moyo wako, na raha nafsini mwako.

Hii ni kuonyesha kuwa toba ya kweli, ni ule moyo uliogeuka. Sio tu kuongozwa sala maalumu. Ndio tunajua sala ikiambatana na geuko ni vema sana, lakini ikiwa utasalishwa sala hizo elfu 10 halafu ndani yako, ni vilevile tu, hapo unapoteza muda wako ndugu.

Alikuwepo Yule mwanamke mwenye dhambi nyingi sana, alipokwenda kwa Bwana Yesu saa ile ile akaanza kulia akitubia dhambi zake, akidondosha machozi yake miguu pa Yesu, huku akiyapangusa kwa nywele zake. Lakini Yesu alipomwona akasema ‘Umesamehewa dhambi zako nyingi’, mwanamke Yule hakusalishwa sala yoyote.(Luka 7:36-50).

Ili Mungu afike kwako upesi, kuwa na toba ya kweli, ili upate kibali cha haraka kwa Mungu, sio wingi wa maombi yako, bali geuko la dhati. Na Bwana mwenyewe atakufikia kabla hujamfikia yeye.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

WALA HAKUACHA MTU ACHUKUE CHOMBO KATI YA HEKALU.

Kwanini Nuhu alimlaani Kaanani badala ya mtoto wake Hamu,

UMUHIMU WA KUISHI MAISHA YAMPENDEZAYO MUNGU SASA.

MUME / MKE BORA KUTOKA KWA BWANA UTAMWONA UKIWA KATIKA MAZINGIRA GANI?

JE! UKRISTO UNAMPA MTU DHAMANA YA KUWA TAJIRI?

Forodhani ni mahali gani?

Rudi nyumbani

Print this post

TAFUTA HEKIMA, MAARIFA, UFAHAMU NA BUSARA.

Jina la Mwokozi Mkuu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia.

Mithali 2:10 “Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;

 11 Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi. 

Haya ni mambo manne ambayo ni muhimu sana kuwa ndani yetu.

  1. Hekima – Ni uwezo wa kupanga na kupambanua mambo
  2. Maarifa- Ni elimu au taarifa kuhusiana na jambo fulani
  3. Ufahamu- Ni hali  ya kuweza kufahamu jambo Fulani kwa kina
  4. Busara- Ni hali ya kuona mbele (yaani mambo yajayo) na kuamua lililo sahihi. Mithali 27:12

Mambo haya manne ni Bwana pekee anayeweza kuyatoa.. Mithali 2:6 “Kwa kuwa Bwana huwapa watu hekima; Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu” .

Zifuatazo ni faida kuu tatu (3) za kupata Hekima, Maarifa, ufahamu na busara.

  1. KUOKOKA NA NJIA YA UOVU.

Hii ni faida ya kwanza ya kupata Hekima, Ufahamu, busara na Maarifa; “Kumwokoa mtu na njia ya uovu”

Mithali 2:10 “Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;

11 Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi. 

12 ILI KUKUOKOA NA NJIA YA UOVU, Na watu wanenao yaliyopotoka; 

13 Watu waziachao njia za unyofu, Ili kuziendea njia za giza; 

14 Wafurahio kutenda mabaya; Wapendezwao na upotoe wa waovu; 

15 Waliopotoka katika njia zao; Walio wakaidi katika mapito yao”

Njia ya Uovu ni njia yoyote ile ambayo itampelekea mtu kufanya maovu, mfano wa hayo ni yale yanayotajwa katika Wagalatia 5:19-21 “uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo”.

2. KUKUOKOA NA MALAYA:

Mithali 2:16 “…Ili kuokoka na malaya, Naam, malaya mwenye kubembeleza kwa maneno yake..”

Mtu aliye Malaya ni yule anayefanya uasherati aidha kwa lengo la kutafuta pesa au kujifurahisha, na hili ni neno linalotumika kuwakilisha jinsia zote mbili za watu wenye tabia hizo. Na Malaya anaweza kuwa ni mtu aliye ndani ya ndoa au nje ya ndoa.

Mtu mwenye busara (Maana yake anayeona mbele), hawezi kunaswa na mtego wa Malaya.. Mfano wa mtu aliyekuwa na busara katika biblia ambaye aliokoka na mtego wa Malaya ni Yusufu, ambaye alitegewa mtego na mke wa Potifa, lakini aliushinda mtego ule wa ibilisi.

Lakini kama Yusufu hangekuwa na Busara akilini mwake, basi angenaswa katika mtego ule wa  uasherati alipobembelezwa na mke wa Potifa, na hivyo angekuwa amejiingiza katika matatizo makubwa sana, ambayo yangehatarisha hata maisha yake ya kimwili na kiroho.. kama biblia inavyosema hapa..

Mithali 2:16 “Ili kuokoka na malaya, Naam, malaya mwenye kubembeleza kwa maneno yake;

17 Amwachaye rafiki wa ujana wake, Na kulisahau agano la Mungu wake. 

18 Maana nyumba yake inaelekea mauti, Na mapito yake yanakwenda kwenye wafu. 

19 Katika hao wamwendeao harudi hata mmoja, Wala hawazifikilii njia za uzima”

Soma tena maandiko mengine yanayohusu tabia za Malaya, jinsi anavyobembeleza katika Mithali 7:7-23, Mithali 22:14 na Mithali 23:27.

Ukiona mtu kanaswa na mtego basi ni matokeo ya kupungukiwa Hekima, busara, maarifa na ufahamu.. kama biblia inavyosema katika Mithali 6:32 “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake” .Kwasababu mtu aliyejaa mambo hayo hawezi kunaswa na mitego hiyo.

3. KUKUPELEKA KATIKA NJIA YA WATU WEMA

Faida ya kwanza tuliona ni “kumwokoa mtu katika njia ya uovu” lakini Hii ya tatu na ya mwisho, ambayo ni “Kukupeleka mtu katika njia ya watu wema”.. Hekima, busara, Maarifa na ufahamu haviishii tu kumwokoa mtu na njia mbaya na kumwacha hapo katikati bali pia kumpeleka/kumwongoza katika njia nzuri.

Mithali 2:20 “Ili upate kwenda katika njia ya watu wema, Na kuyashika mapito ya wenye haki.

21 Maana wanyofu watakaa katika nchi, Na wakamilifu watadumu ndani yake. 

22 Bali waovu watatengwa na nchi, Nao wafanyao hila watang’olewa”.

Watu wema wana Njia yao, wapo katika mkondo wao, si kila mahali wanapita, na hao ndio wanaodumu katika nchi, … Sasa ili kuiona hiyo njia waliyopo basi Hekima, Busara, Maarifa na ufahamu vinahitajika. Na vyote hivyo vinatoka kwa Mungu.

Sasa swali? Mtu anapataje Hekima, Ufahamu, Busara na Maarifa ili kuepukana na hayo yote, na kupata faida hizo.

Tukitaka Hekima, Maarifa, Ufahamu na Busara biblia imetupa kanuni rahisi katika kitabu cha Ayubu.

Ayubu 28:20 “Basi hekima yatoka wapi? Na mahali pa ufahamu ni wapi? 

21 Kwa kuwa imefichwa mbali na macho ya wote walio hai, Na kusitirika na ndege wa angani. 

22 Uharibifu na Mauti husema, Tumesikia habari zake kwa masikio yetu. 

23 Mungu ndiye aijuaye njia yake, Naye anajua mahali pake. 

24 Maana anatazama hata miisho ya nchi, Na kuona chini ya mbingu nzima. 

25 Apate kuufanyia upepo uzito wake; Naam, anayapima maji kwa kipimo. 

26 Hapo alipoiwekea mvua amri, Na njia kwa umeme wa radi. 

27 Ndipo alipoiona na kuitangaza; Aliithibitisha, naam, na kuichunguza. 

28 Kisha akamwambia mwanadamu, Tazama, KUMCHA BWANA NDIYO HEKIMA, NA KUJITENGA NA UOVU NDIO UFAHAMU”.

Kumcha Bwana na kuepukana na Uovu ndio chanzo cha Hekima, maarifa, busara na ufahamu.

Maana yake Jishughulishe sana na masuala ya kiMungu sana, Jifunze Neno la Mungu, kusanyika na wengine katika maombi, ibada na kufanya uinjilisti na mambo mengine yote yanayofanana na hayo, kwa kufanya hivyo ndivyo Hekima, na hayo mambo mengine yatakayoingia ndani yako na kujaa.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?

Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.

Mjombakaka ni nani kwenye maandiko? (Walawi 11:29)

Nini maana ya “Mwenye hekima huvuta roho za watu”

Mwandishi wa kitabu cha Zaburi ni nani?

Rudi nyumbani

Print this post

Neno vuruvuru linamaanisha nini katika biblia?

JIBU: Kibiblia ni neno linalomaanisha “mvurugano” au “mvurugiko”

Neno hilo utalisoma katika kifungu hiki;

Isaya 17:13 “Mataifa wananguruma kama ngurumo ya maji mengi; Lakini atawakemea, nao watakimbia mbali sana, Watafukuzwa kama makapi milimani mbele ya upepo, Na kama mavumbi vuruvuru mbele ya tufani.  14 Wakati wa jioni, tazama, kuna hofu; Na kabla ya mapambazuko hawako; Hilo ndilo fungu lao watutekao, Na ajali yao wanaotunyang’anya mali zetu”.

Hapo ni Bwana anawahakikishia watu wake ulinzi madhubuti dhidi ya adui zao. Anasema mambo matatu yatawakumba hao wanaojaribu kuwaangamiza watu wa Mungu.

La kwanza,watakemewa  na kukimbia mbali sana: Ni kama wakati wa washami kipindi cha nabii Elisha, Bwana alipowasikilizisha kelele za majeshi wakakimbia wakashindwa hata kuchukua na nyara zao nyuma(2Wafalme 7).

La pili ni “ watafanana na makapi mbele ya upepo: Kwa kawaida ngano inapopepetwa yale makapi huwa yanarushwa na upepo mbali sana, ndivyo watakavyofanywa waadui wa watoto wa Mungu wanapokaribiwa, watatoweka ghafla.

Na la tatu anasema  watakuwa kama mavumbi ‘vuruvuru’ mbele ya tufani: Kwa kawaida upepo  mkali wa kisulisuli au tufani  inapopita juu ya ardhi iliyokuwa kavu, ule upepo wake mkali unatabia ya kuvuruga mavumbi, na kuyafanya yaruke hewani yasambae tu ovyo vyo, na hiyo husababishia hali ya hewa kuchafuka sana. Hivyo, Bwana anasema, ndivyo itakavyokuwa kwa  watu hao, watavurugwa, kiasi cha kutokuelewana, kila mmoja atakuwa na lake, ni kuchanganyikiwa tu, Ndio maana ya hilo andiko.

Lakini ni nini Bwana anataka tujifunze?

Ni kwamba tuwapo ndani Kristo, hatuna haja ya kuwa  na hofu, kwasababu shetani na majeshi yake, yatakutana kwanza na jeshi la Bwana kabla ya kutufikia  sisi. Ndicho Elisha alichomwambia Gehazi, kwamba  jeshi letu ni kubwa kuliko la kwao.

Hivyo mtakatifu yoyote unayedumu katika wokovu (usio wa mdomo bali wa roho), ulinzi huu unao. Lakini kinyume chake ni  kweli ikiwa upo nje ya Kristo, huna ulinzi wowote kwa Bwana, na matokeo yake shetani anaweza kufanya lolote atakalo juu yako, hata kukuua.

Swali ni Je! Umeokoka?

Kama bado na upo tayari kufanya hivyo sasa basi fungua hapa kwa ajili ya mwongozo was ala hiyo. >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UPEPO WA KUSI HULETA MVUA;

Je! Sulemani alienda mbinguni?

Nini maana ya uvuvio?

MZUNGUKO WAKO NI UPI?

Uga ni nini? Na kazi yake ni ipi kibiblia?

Ila atapewa mara mia sasa,Ndugu wake(Marko 10:30)

Manyoyota ni nini (Ayubu 37:6)

Rudi nyumbani

Print this post

Kwanini Nuhu alimlaani Kaanani badala ya mtoto wake Hamu,

SWALI: Kwanini Nuhu alimlaani Kaanani badala ya mtoto wake Hamu, ambaye ndiye aliyekuwa na makosa?


JIBU: Ni kweli kama tunavyosoma katika maandiko, pindi ambapo Nuhu amelima shamba lake la mizazibu akaaanda divai nyingi akanywa akalewa mpaka akalala uchi hadharani, tunaona mtoto wake mmoja aliyeitwa Hamu alipomuona hakuchukua hatua stahiki kumsitiri Baba yake

Lakini wale watoto wake wawili (yaani Yafethi na Shemu) walipomwona baada ya kuambiwa na Hamu, hawakutaka kutazama bali walichukua mavazi yao mabegani Kisha wakaenda kinyume nyume wakamfunika Baba Yao. 

Nuhu alipopata taaarifa, aliyoyafanya mwanawe wa mwisho alimlaani, lakini laana yake haikuwa Kwa Hamu Moja Kwa Moja Bali Kwa mtoto wake aliyeitwa Kaanani..Sasa swali ni je Kwanini afanye hivyo Kwa Kaanani mjukuu wake, angali kitendo kimetendwa na Hamu.

Mwanzo 9:20-25

[20]Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu; [21]akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake. [22]Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. [23]Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao; na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao. [24]Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea. [25]Akasema, Na alaaniwe Kanaani; Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake.

Ipo mitazamo mingi katika jambo hilo, wapo wengine wanaomini kuwa Shemu alikuwepo na mwanaye huyo mkubwa Kaanani, na huwenda yeye naye alipuuzia kumsitiri Babu yake, au alifanya jambo baya kwake,  wengine wanasema Hamu tayari alikuwa amebarikiwa na Mungu hivyo Baba yake asingeweza Tena kumlaani mtu ambaye amebarikiwa (Mwanzo 9:1),ndio maana laana akaisogeza kwa mjukuu wake.

Wengine wanaaanimi aliposema alaaniwe Kaanani, ni lugha tu iliyomaanisha pia “Baba wa kaanani”

Lakini ni vema tukaona muktadha wa uandishi wote, ikumbukwe kuwa aliyekiandika kitabu hicho ni Musa, na tunafahamu hatma ya taifa la Israeli, ilikuwa si katika mataifa yote duniani, bali pale Kaanani. Hivyo, ulikuwa ni unabii, wa Nuhu, kuonyesha moja wa uzao Shemu uitwao kaanani utalaaniwa. Hivyo tunapokuja kusoma juu ya anguko la wenyewe wa taifa lile, walivyoangamizwa na kuteketezwa na taifa la Israeli, ni kutukumbusha kuwa tayari Kaanani ilikuwa imeshalaaniwa tangu zamani, kuangamizwa kwao na maovu yao ni matokeo ya laana iliyotajwa zamani.

Shalom

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Kaanani ni nchi gani kwasasa?

Nchi ya Nodi ambayo Kaini alikimbilia ndio nchi gani kwasasa?(Mwanzo 4:16).

Wakaanani walikuwa ni watu gani?

saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada

KWANINI NABII ISAYA ALIAGIZWA KUHUBIRI UCHI?

KWANINI NI NUHU, AYUBU NA DANIELI?

Rudi nyumbani

Print this post