Karibu tujifunze biblia.
Matendo 3:22 “ Kwa maana Musa kweli alisema ya kwamba, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye katika mambo yote atakayonena nanyi.
23 Na itakuwa ya kwamba kila mtu asiyemsikiliza nabii huyo ataangamizwa na kutengwa na watu wake”
Unabii huo unamhusu Bwana Yesu Kristo, lakini swali la Msingi hapa, je! Ni wakati gani ambao “watu wataangamizwa na kutengwa” kwa kutomsikiliza huyu Masihi…Kwasababu ni wengi leo hawamsikilizi wala kumtii lakini hawaangamizwi wala kutengwa na watu wao.
Hapo kuna mambo mawili ambayo yatatimia kwa pamoja.. 1) KUANGAMIZWA, na 2) KUTENGWA.
Haya ni mambo mawili ambayo yatatimia kwa wakati mmoja kwa wote ambao hawatamsikiliza Masihi.
Sasa swali, ni hili unabii huo utatimia lini wa watu kuangamizwa na kutengwa?
Tusome,
2Wathesalonike 1:7 “na kuwalipa ninyi mteswao raha pamoja na sisi; WAKATI WA KUFUNULIWA KWAKE BWANA YESU kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake
8 katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu;
9 watakaoadhibiwa kwa MAANGAMIZI ya milele, KUTENGWA na uso wa Bwana na UTUKUFU WA NGUVU ZAKE;”
Umeona hapo?. Kumbe wote wasioitii injili, leo siku ya mwisho (ya kufunuliwa Bwana Yesu) wataangamizwa!, na sio tu kuangamizwa, bali pia “watatengwa na uso wa Mungu” na “kutengwa na utukufu wa nguvu zake”…Maana yake wataanza kwa kutengwa kutoka kwa ndugu zao (wakati wa kutenganishwa kondoo na mbuzi Mathayo 25:31-35) na pia watatengwa na vitu vyote Mungu alivyoviumba ikiwemo dunia na kila kitu…sawasawa na Mithali 2:21-22.
Mithali 2:21 “Maana wanyofu watakaa katika nchi, Na wakamilifu watadumu ndani yake.
22 Bali waovu watatengwa na nchi, Nao wafanyao hila watang’olewa”
Ni jambo baya sana kutengwa na uso wa Mungu na kuangamizwa!..
Wengi leo wanamkataa Yesu na kuikataa Injili wakidhani ipo njia nyingine ya kufika mbinguni.. Bwana Yesu yeye mwenyewe alisema kwa kinywa chake kuwa..
Yohana 14:6 “..Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”.
Hakuna njia nyingine ya kumfikisha mtu mbinguni isipokuwa njia ya Msalaba!.. Usidanganyike kwa vyovyote vile.
Mwisho wa dunia unakuja, Mpokee Yesu leo, Itii injili yake inayosema… usizini, usiibe, usivae mavazi ya nusu tupu, usivae mavazi yapasayo jinsia nyingine, usijichore mwili, usitukane n.k
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa >> WHATSAPP-GROUP
Mada Nyinginezo:
Je mwanamke anaruhusiwa kupanda madhabahuni akiwa katika siku zake?
Ni kwa namna gani Kristo analitakasa kanisa kwa Maji katika Neno? (Waefeso 5:26)
Je Mungu ana njia ngapi za kuzungumza?
Wana wa Manabii walikuwa ni watu gani?
Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo lihimidiwe daima, karibu tujifunze Biblia Neno la Mungu wetu lililo taa ya miguu yetu na Mwanga wa njia yetu (Zab.119:105).
Maandiko yanatuonyesha kuwa si lazima watu wote wanene kwa lugha (1Wakorintho 12:30 na 14:23), kana kwamba ndio uthibitisho pekee wa mtu kuwa wa kiroho…lakini pia kuna faida kubwa ya kunena kwa lugha ikiwa mtu atajaliwa hilo.
Na pia kunena kwa lugha si jambo ambalo mtu anaweza kuamua, kwamba sasa naanza kunena, la! Kunena kwa lugha ni msukumo ambao Roho Mtakatifu anaushusha ndani ya mtu pasipo mtu kutaka au kupanga!.. Ni kama mtu anavyopokea unabii, au anavyopokea ndoto au maono.. hakuna mtu anayeweza kupanga unabii au maono au ndoto (labda awe nabii wa uongo)!.. kwani mambo hayo yanakuja tu yenyewe kutoka kwa Mungu, kwajinsi apendavyo Mungu… Na kunena kwa lugha ni hivyo hivyo, si lazima iwe kila siku au kila saa, bali ni wakati maalumu tu ambao Roho atalishusha jambo hilo ndani ya mtu.
Sasa zipo lugha za wanadamu, na vile vile za Malaika (Soma 1Wakorintho 13:1), Zozote kati ya hizo mtu aliyejazwa Roho anaweza kuzinena. Na zote zina faida katika kuzinena… Katika kunena lugha za wanadamu ni pale ambapo mtu haijui lugha Fulani ya jamii fulani ya watu, lakini ghafla anajikuta anaanza kuizungumza ile lugha vizuri sana.. Vile vile katika kunena lugha za malaika, ni pale ambapo anajikuta anazungumza lugha ambayo ni mpya kabisa isiyotumiwa na wanadamu mahali popote.
Na maneno anayoyazungumza yanakuwa aidha ni maneno ya unabii, au maonyo au ya kumsifu Mungu.. kwahiyo kama ni ujumbe kwa kanisa ni lazima awepo mfasiri..
Vile vile kama ni lugha Mpya inayozungumzwa, maana yake ambayo haitumiki na jamii yoyote ya wanadamu, na ni ujumbe kwa kanisa, basi anahitajika pia mfasiri, lakini kama mtu yupo katika maombi yake binafsi na lugha hiyo ikamjia ndani yake, basi hapo hahitaji mfasiri bali anakuwa ananena maneno ya siri na Mungu wake.
Na leo tutaangalia faida moja kubwa ya kunena lugha mpya, uwapo wewe binafsi katika maombi yako ya faragha.
MAZUNGUMZA YAKO YANAKUWA NI YA SIRI.
Hii ndio faida kuu na ya kwanza. Kikawaida mazungumzo ya siri yanakuwa na upinzani mchache kuliko mazungumzo ya wazi!.. na njia mojawapo ya kuficha mazungumzo ni kutumia lugha nyingine!..
Kwamfano utaona Waarabu wawili, au Wachaga wawili, au wamasai wawili, au wasukuma wawili, wanapokutana mahali Fulani ili waongee kwa uhuru zaidi utaona wanatumia lugha zao za asili , lengo ni kuficha mazungumzo na pia kuzungumza mambo yao yale mambo ya ndani kwa uhuru zaidi.. watu walio kando kando inakuwa ngumu kuelewa na hivyo wazungumzaji wanakuwa wamefunga milango mingi.
Na sisi tunapozungumza na Mungu wetu, KUNA WAKATI TUNAHITAJI USIRI.. Maneno yetu tunayoyazungumza si lazima yaeleweke na watu wa kando yetu au na mapepo katika ulimwengu wa roho. Ili kuzuia vita visivyokuwa na msingi.
Shetani asipoelewa kile tunachoomba kwa Mungu, inamwia vigumu kwake kupanga mashambulizi, kwasababu hajui ni nini tunamwomba Mungu kwa wakati huo, hivyo anabaki tu hapo katikati, lakini akisikia unamwomba Mungu akupe Amani, au akupe riziki Fulani, tayari na yeye kashajua ni eneo gani aende kukupiga vita ili usipokee kile ulichomwomba Mungu. Ndio maana Mtume Paulo kwa ufunuo wa roho aliliona hilo na akawaandikia watakatifu..
1Wakorintho 14:2 “Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake”.
Hivyo usijizuie kunena kwa lugha kama umejaliwa hilo.. itakusaidia kuzuia vita vingi katika ulimwengu wa mwili na wa roho.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Je kunena kwa Lugha mpya kukoje?
JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?
MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)
Ikiwa unafanya matendo mazuri yanayompendeza Mungu, basi mshukuru Mungu kwa hayo lakini USIJISIFU wala kujigamba hata kidogo kwa hayo. Kwasababu wakati unadhani kuwa umefanya 100 yanayompendeza Mungu kwa siku moja, yapo mengine 200 uliyoyafanya yasiyompendeza Mungu, kwa kutokujua.
Laiti tukifunguliwa macho na kuona makosa yetu yote tunayoyafanya bila sisi wenyewe kujua, tusingeendelea kujitamani hata kidogo, tusingeendelea kujivuna, tusingeendelea kujisifia vimema vichache vichache tunavyovitenda kwa siku!!!…Kwaufupi maisha yetu yamejaa makosa mengi kuliko mema!, hata kama tutajiona kama tuna mema mengi kuliko kasoro.. Lakini uhalisia utabakia pale pale kwamba makosa yetu yamezidi mema yetu..
Kwahiyo kama Mungu ni wa haki, basi ni haki yake atulipe mabaya mengi kuliko mema.
Kama ukimlazimisha Mungu akuhesabie haki ya kukubariki kwa sadaka yako uliyotoa jumapili, vile vile anapaswa akuhesabie haki ya kuadhibiwa kwa mawazo yako ya kutamani na kwa hasira uliyomwonea ndugu yako siku hiyo hiyo ya jumapili. Na maandiko yanasema mtu amwoneaye ndugu yake hasira ni mwuaji, kwahiyo unapaswa uhukumiwe kama mwuaji..
Lakini kama hutaki Mungu atazame udhaifu wako huo na hutaki akuadhibu kwa makosa yako basi usilazimishe akulipe kwa matendo yako mazuri unayomfanyia. Bali kinyume chake nyenyekea!!!.. Fanya tu yakupasayo kufanya sawasawa na Luka 17:10.
Luka 17:10 “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya”.
Na kama tukiingia mkataba huo na Mungu wa kupokea haki yetu kwa matendo yetu, basi tunazo sababu nyingi za kulipwa mabaya kuliko mema. Kwasababu Mungu siku zote ni wa haki.
Lakini kama mara nyingi Mungu anatuvumilia kwa mabaya yetu tunayoyafanya sawasawa na Zaburi 130:3 “Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna msamaha, Ili Wewe uogopwe”…basi na sisi hatuna budi kutoyatumainia mema yetu tunayoyafanya!.
Ndio hapa sasa panazaliwa kitu kinachoitwa NEEMA!... Neema tafsiri yake ni upendeleo maalumu usiokuwa na sababu. Kwamba unapokea tu kitu kutoka kwa Mungu pasipo matendo yako.. Yaani Mungu anapenda tu kukupa si kwasababu wewe ni mtenda mema, au ni mwombaji sana, au ni mfungaji sana, au ni mhubiri mzuri… La!, bali anakutendea tu mema bila kwa upendo wake tu!, na huruma zake na kupenda kwake.
Ndio maana hatuna budi kila siku KUOMBA NEEMA YA MUNGU ije juu yetu. Kwasababu tukiipata hiyo tumepata kila kitu.
Usijivune, bali omba neema kwasababu Mungu huwapinga wenye kiburi na kuwapa wanyenyekevu Neema yake (1Petro 5:5).
Afya uliyonayo ni kwa neema tu, Uzima ulio nao ni kwa Neema tu, karama uliyo nayo ni kwa neema tu, zaidi sana hata Wokovu ulio nao ni kwa Neema tu na wala si kwa matendo yako.
Waefeso 2:8 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;
9 wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu”
Na zaidi ya yote pia Roho Mtakatifu tunampokea kwa Neema..
Wagalatia 3:2 “Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani”
Omba Neema!!.. omba Neema!, Omba Neema…usitumainie matendo yako..
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?
FUNDISHO KUU LA NEEMA YA MUNGU KWETU.
Kama tunaokolewa kwa neema kwanini wokovu tuupate kwa nguvu?
Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe.
Karibu tujifunze biblia, leo tujikumbushe historia fupi ya tafsiri ya biblia ya King James.
King James au kwa Kiswahili “Mfalme Yakobo” wa Uingereza, alikuwa ni mmoja wa wafalme ambao hawakuwa maarufu sana kwa wakati wao. Lakini alikuja kufanya jambo la kishujaa ambalo mpaka leo yupo katika rekodi ya watu maarufu na wakihistoria waliowahi kutokea Uingereza.
Mwaka 1604 baadhi ya wanazuoni wa Kiprotestanti (Wapuriti) walipendekeza kuchapishwa kwa tafsiri mpya ya biblia, kuchukua nafasi ya ile iliyokuwepo ambayo ilijulikana kama tafsiri ya “Geneva”. Tafsiri ya Geneva ndio ilikuwa tafsiri ya kwanza kwa lugha ya kiingereza kuchapichwa huko Ulaya, iliyotumiwa na Waprotestanti.
Upungufu wa tafsiri hiyo ya Geneva, ni kwamba ilikuwa ina “maoni ya ziada” yaliyoongezwa ili kutilia mkazo kile kilichoelezwa katika biblia, na maoni hayo ya mkazo, yalilenga sana kuwakosoa viongozi wa kisiasa na kidini.
Hivyo baadhi ya waprotestanti hao, jamii ya Wapuriti, walitoa mapendekezo yao kuchapiswa biblia nyingine ambayo itaondoa hayo maoni ya watu na kuiacha yenyewe kama yenyewe, pasipo maoni ya watu. Na pia chapisho hilo litalenga pia kuitafsiri biblia nzima katika kingereza kizuri zaidi.
Wapuri hao baada ya kutoa hilo pendekezo, walilifikisha kwa Mfalme ambaye alikuwa anaitwa YAKOBO (King James).
Kikawaida wafalme wengi huwa hawajihusishi na masuala ya kiimani, zaidi sana huwa wanayapinga, lakini ikawa ni kinyume chake kwa huyu King James, badala ya kulipinga au kulikosoa wazo lao, yeye alikubali biblia mpya hiyo ichapishwe na tena akatoa sehemu kubwa ya hazina ya utajiri wake kusaidia zoezi zima la utafsiri mpya.
Tafsiri hiyo mpya ya Biblia hiyo mpya iliandaliwa kwa kipindi cha Miaka 7, na wanazuoni zaidi ya 47 kutoka kila mahali, Uingereza. Walianza kuitafsiri biblia upya kutoka katika Lugha ya kigiriki kwa agano la kale, na kiaramu kwa agano jipya. Walipomaliza kuitafsiri biblia yote wakaiita biblia hiyo KING JAMES BIBLE, Yaani biblia ya Mfalme Yakobo.
Baada ya kumaliza kutafsiri, kazi ile ilionekana kama dhaifu sana, lakini muujiza ni kwamba ndani ya kipindi kifupi, tafsiri hiyo mpya ya King James, ilianza kupendwa na watu wengi, kwani haikuwa na mchanganyiko wa maoni ya watu, na ilikuwa na kiingereza kikamilifu na haikuongeza neno wala kupunguza Neno.
Kufikika Mwaka 1611, tafsiri ya King James ilikuwa imeshasambaa katika bara la Ulaya yote, na baadaye duniani kote. Na tangu mwaka huo wa 1611 mpaka leo karne ya 21 ndio kitabu kinachoongoza kwa kuuzwa kuliko vitabu vyote duniani, na kumfanya Mfalme James, kuendelea kushika nafasi za juu za watu maarufu waliowahi kutokea.
Ni nini tunajifunza katika Mfalme Yakobo (King James).
Ni Mfalme ambaye alikuwa na hofu ya Mungu, ingawa hakuwa mkamilifu sana, lakini alitii na kuheshimu pendekezo la watu wa Mungu, ambao walimshauri aridhie ombi la kukitakasa kitabu kitakatifu cha Bwana, kwa kuondoa maoni ya watu na kukiacha kisafi kama kilivyo.
King James, aliruhusu pendekezo hilo pasipo kujua kuwa litaenda kuubadilisha ulimwengu. Mpaka Leo hii tafisiri bora ya kiingereza inayosomwa na wengi ni tafsiri hiyo ya King James. Na kwa kufanya hivyo Bwana akampa King James kumbukumbu la daima.
Ni wafalme wengi na mamalkia wengi wamekuja na kupita, wameandika vitabu lakini vitabu vyao vimepita, lakini kazi ya James mpaka leo inadumu na itaendelea kudumu hivyo mpaka Kristo anarudi.
Na sisi tukitaka tupate kumbukumbu la kudumu hatuna budi kumfikiri Mungu kwanza katika maisha yetu, haijalishi ngazi tuliyopo tuwe maskini, matajiri, tuwe wafalme tuwe watu wa kawaida.. tukimjali Bwana kwa mioyo yetu yote, na akili zetu zote na nguvu zetu zote, bali tuna kumbukumbu kubwa mbele zake si tu katika maisha haya, bali hata yale yajayo.
Malaki 3:13 “Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani?
14 Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi?
15 Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.
16 Ndipo wale waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. Naye Bwana akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha Bwana, na kulitafakari jina lake.
17 Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye”.
Bwana atubariki.
Maran atha.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Dina akatoka kuwaona binti za nchi. (Mwanzo 34:1)
Biblia inamaana gani iliposema “Dhambi ilipozidi, Neema ilizidi kuwa nyingi Zaidi”.
WHAT DOES IT MEAN TO BE A CHRISTIAN?
Je ni viatu gani Musa aliambiwa avivue? Vya mwilini au vya rohoni? (Kutoka 3:5).
Biblia imetuonya imetutahadharisha vitu vitatu vilivyo na udanganyifu kuliko vitu vyote.
1.MOYO
Moyo wa mtu ndio kitu kilicho kidanganyifu kuliko vyote..
Yeremia 17:9 “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?”
Hakukuwa na shetani mwingine mbinguni aliyemdanganya shetani, bali kilichomdanganya shetani ni moyo wake mwenyewe… Moyo wake ulimtuma kuamini kuwa anaweza kuwa kama Mungu. Na hivyo akaufuata moyo wake na mwisho akaangukia upotevuni.
Na mioyo yetu sisi wanadamu ni midanganyifu sana, na mara nyingi inatuongoza pabaya…Mithali 16:2 “Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe…” Na maandiko yanatufundisha kulinda mioyo yetu kuliko vyote tulindavyo, kwasababu huko ndiko zinakotoka chemchemi za uzima (Mithali 4:23).
Na tunailinda kwa kuangalia yale tunayoyasikia au tunayojifunza, na biblia ndio kitabu pekee cha kutusaidia kupima mambo yote.
2. DHAMBI.
Dhambi ni adui wa pili wa kumwongopa kuliko “shetani”. Na dhambi siku zote inadanganya, (inavutia kwa nje lakini mwisho wake ni Mauti, Warumi 6:23). Ulevi unaonekana kama unavutia lakini mwisho wake ni Mauti, Anasa zinaonekana kama zinavutia, lakini mwisho wake ni Mauti, Vivyo hivyo na Zinaa, na usengenyaji, na wizi, na rushwa n.k Vyote hivyo vinavutia kwa nje lakini ndani yake ni Mauti.
Waebrania 3:13 “Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa UDANGANYIFU WA DHAMBI”.
3. SHETANI.
Maandiko yanasema wazi kuwa shetani ni baba wa Uongo.
Shetani atakuambia kuabudu sanamu si dhambi, kunywa pombe si dhambi, kuupenda ulimwengu si dhambi, kujiburudisha kwa anasa si dhambi n.k Na kumbe anasema Uongo, kwasababu yeye ni baba wa huo, ndivyo alivyomdanganya Hawa na ndivyo anavyoendelea kudanganya watu mpaka leo.
Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo”
4. MALI
Maandiko pia yanasema kuwa Mali zinadanganya!.. Mali zinasema ukizipata utaheshimika, ukizipata utapendwa, ukizipata utaishi vizuri.. jambo ambalo si kweli, Kristo pekee ndiye ukimpata mambo yote, yatakuwa sawa hata pasipo hizo mali… Kama alisema “mtu hataishi kwa mkate tu, bali Neno la Mungu”…si zaidi Mali???.
Lakini Mali zenyewe zinatuhubiria kinyume chake kuwa pasipo hizo, maisha yetu hayawezi kwenda au yatakuwa ya shida, maisha yetu yatakuwa ya tabu na mateso…
kwahiyo kama hatutaongeza umakini katika kumjua Mungu na uweza wake tutadanganyika na udanganyifu huo ambao Mali zinauhubiri.. tutajikuta tunatumia muda mwingi kuzisaka na kutumia muda mchache kumtafuta Mungu.. na hivyo kupotea..
Mathayo 13:22 “Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na UDANGANYIFU WA MALI hulisonga lile neno; likawa halizai”.
Mali zisikudanganye na kukupotezea muda wako mwingi, Mali zisikuambie kuwa usipoenda kuzisaka siku ya jumapili utakufa njaa!!, mali zisikudanganye kuwa usipotumia usipotumia muda mwingi kuzisaka basi zitakukimbia!!.. Jihadhari na udanganyifu huo.
Bwana atubariki na kutusaidia.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Kwanini Paulo aungane na wale watu wanne wenye nadhiri?
Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
KWA WALE WALIO NJE “YOTE” HUFANYWA KWA MIFANO.
Hesabu 14:22 “kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya WAMENIJARIBU MARA HIZI KUMI, wala hawakuisikiza sauti yangu;
23 hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona;
24 lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki”
Maandiko yanaonyesha kuwa wana wa Israeli walimjaribu Mungu MARA KUMI, je ni wapi katika maandiko panaonyesha hayo?
1. JARIBU LA KWANZA: (Mkabala na bahari ya Shamu)
Kutoka 14:9 “Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni.
10 Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia Bwana.
11 Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri?
12 Neno hili silo tulilokuambia huko Misri”
Hili ndio jaribu la Kwanza wana wa Israeli walilomjaribu nalo Mungu, ijapokuwa walishaona matendo yake makuu kwa Farao na Misri yote kwa ujumla jinsi alivyoipiga Misri na kuiharibu kwa ishara kubwa na maajabu mengi, lakini hapa wanamjaribu Mungu kuangalia kama atawapigania tena kinyume na Farao au la!.. jambo ambalo ni dhambi kwao kwani tayari wanaujua uweza wa Mungu na hivyo hakuna haja ya kumjaribu ili kuona atakachokifanya.
2. JARIBU LA PILI: (Maji ya Mara)
Kutoka 15:22 “Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji.
23 Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara.
24 Ndipo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, Tunywe nini?
25 Naye akamlilia Bwana; Bwana akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko”
Hili ni jaribu la pili, baada ya kuona uweza wa Mungu wa kupasua bahari, lakini bado wakamjaribu Mungu kuangalia kama atawafanyia muujiza wa Maji au la.. Na Bwana akawapa maji kama walivyotaka lakini bado hawakuridhika…
3. JARIBU LA TATU: (Katika bara ya Sini, kutaka Nyama)
Kutoka 16:1 “Kisha wakasafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikilia bara ya Sini, iliyoko kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri
2 Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung’unikia Musa na Haruni, huko barani;
3 wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote.”
Hili ni jaribu la tatu baada ya kumjaribu Bwana kwa maji ya Mara na sasa wanataka kumwangalia Bwana kama anaweza kuwafanyia muujiza wa Nyama katikati ya jangwa, na Bwana akawapa nyama, kama walivyotaka lakini bado hawakuchoka kumjaribu..
4. JARIBU LA NNE: (Kusaza kwa Mana).
Kutoka 16:19 “Musa akawaambia, Mtu awaye yote asikisaze hata asubuhi.
20 Lakini hawakumsikiza Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana”
Walipewa maagizo wasikisaze (yaani wasibakishe chochote mpaka asubuhi) lakini wao wakafanya kinyume chake kwa kusudi la kuchunguza ni nini kitatokea.
5. JARIBU LA TANO: (Ukusanyaji wa Mana siku ya Sabato)
Kutoka 16:26 “Siku sita mtaokota; lakini siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana.
27 Ikawa siku ya saba wengine wakatoka kwenda kukiokota, wasikione.
28 Bwana akamwambia Musa, Mtakataa kuyashika maagizo yangu na sheria zangu hata lini? “
Mungu aliwaambia wasitoke kwenda kuokota Mana siku ya Sabato, bali wapumzike, kwasababu hiyo mana haitapatikana siku hiyo, lakini wenyewe wakatoka kwenda kuhakiki kama kweli haitapatikana?.. hivyo ikawa ni dhambi kwao.
6. JARIBU LA SITA: (Maji ya Refidimu).
Kutoka 17:1 “Mkutano wote wa wana wa Israeli ukasafiri, kutoka bara ya Sini kwa safari zao, kama Bwana alivyowaagiza, wakatua Refidimu; napo hapakuwa na maji, watu wanywe.
2 Kwa hiyo hao watu wakateta na Musa, wakasema, Tupe maji tunywe. Musa akawaambia, Kwani kuteta na mimi? Mbona mnamjaribu Bwana?
3 Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung’unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?”
Baada ya kumjaribu Bwana kule Mara, kwa kutaka maji, sasa wanarudia tena yale yale makosa.. ya kutaka watokezewe maji ya kimiujiza..Kulikuwa hakuna haja ya kumjaribu Mungu mara ya pili, kwani tayari walishaona uweza wake mara ya kwanza, lakini wao walitaka kuona tena na tena..
7. JARIBU LA SABA: (Sanamu ya Ndama).
Kutoka 32:7 “Bwana akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao,
8 wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri”
Wametoka kunywa maji kimiujiza katika Mwamba, na kuhakiki kwamba Bwana yupo katikati yao, lakini hapa wanafanya makusudi kutengeneza sanamu ya Ndama, kama ishara ya kumsusia Mungu, ambaye wanajua kabisa yupo..
8. JARIBU LA NANE: (Moto wa Tabera)
Hesabu 11:1 “Kisha hao watu walikuwa kama wanung’unikao, wakinena maovu masikioni mwa Bwana; Bwana aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa Bwana ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago.
2 Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba Bwana, na ule moto ukakoma.
3 Jina la mahali hapo likaitwa Tabera; kwa sababu huo moto wa Bwana ukawaka kati yao’
Manung’uniko haya ni yale ya kutafuta kuona kitu cha kimwujiza kutoka kwa Mungu, kwasababu walikuwa wameshajua kuwa Mungu anaweza kufanya lolote..
9. JARIBU LA TISA: (Tamaa ya Nyama)
Hesabu 11:4 “Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule?
5 Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu;
6 lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu”
Wana wa Israeli wanataka nyama, si kwasababu walikuwa na njaa sana, bali kwasababu walikuwa wanataka kuona jambo jipya kutoka kwa Bwana..
10. JARIBU LA KUMI: (Wapelelezi wa Kaanani)
Hesabu 14:1 “Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule.
2 Kisha wana wa Israeli wote wakamnung’unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili.
3 Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?
4 Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri”.
Hili ndilo jaribu la mwisho, wana wa Israeli walilomjaribu nalo Mungu, nalo ndilo likawa Muhuri wa wao kuipoteza ahadi ya kuiona ile nchi, isipokuwa watu wa wawili tu, ambao ni Yoshua na Kalebu.
Nasi pia tunachoweza kujifunza katika habari hiyo kuwa “KUMJARIBU MUNGU NI DHAMBI KUBWA SANA”.
Kama tumeshaujua uweza wake kwanini tumjaribu?.. kama tumeshajua kuwa Mungu anaweza kutuokoa na hatari kwanini tujiweke katika hatari??.. Kama tumeshajua kuwa Mungu anaweza kutuokoa na yule mwovu kwanini basi tujisogeze karibu na yule Mwovu??.. Kama tumeshajua kuwa “tutakapokula vitu vya kufisha, havitatudhuru, kwanini basi tuvile makusudi”, kama umeshajua kuwa Mungu ni mponyaji kwanini basi tunywe sumu makusudi?..
Kama umeshajua kuwa Bwana anakupenda kwanini ujiuze kwenye dhambi ili uujaribu upendo wake???.. unadhani utabaki salama?
Ndicho wana wa Israeli walichokuwa wanakifanya, pasipo kujua kuwa wanafanya dhambi kubwa sana, ambayo itawagharimu kukosa kuingia Kaanani.
Kumbuka Hili ndilo jaribu ambalo shetani anawaangusha nalo watu wengi hata siku hizi za mwisho, na ndilo hata alilolichagua kama moja kati ya majaribu yake matatu yenye nguvu kubwa, ili aweze kumwangusha Bwana Yesu lakini alishindwa!,
Mathayo 4:5 “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu,
6 akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe
7 Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.”
Na wewe usimjaribu Bwana, usiujaribu Msalaba.
Bwana akubariki.
Maran atha.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Mada Nyinginezo:
KWA MIOYO YAO WAKAREJEA MISRI.
JIHADHARI NA MKUTANO WA WATU WALIOCHANGANYIKANA.
MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.
Je Ni kweli haturuhusiwi kula nyama kulingana na Isaya 66:3?
Jibu: Tusome,
Waamuzi 1:19 “Bwana alikuwa pamoja na Yuda; naye akawafukuza watu waliokaa katika nchi ya milimani; ASIWEZE KUWAFUKUZA HAO WALIOKAA KATIKA HILO BONDE, kwa kuwa wao walikuwa na magari ya chuma”.
Ni kweli Bwana hakuweza kuwafukuza hao watu waliokaa mabondeni… Lakini si kwamba alikuwa hana uwezo wa kuwafukuza, bali kulikuwa na kusudi kwanini hakuweza kuwafukuza..
Ili tuelewe vizuri tuanzie kuisoma habari hiyo kuanzia mstari wa 17..(zingatia maneno yaliyoanishwa kwa herufu kubwa).
Waamuzi 1:17 “Kisha Yuda akaenda pamoja na nduguye Simeoni, na WAKAWAPIGA WAKANAANI waliokaa katika Sefathi, na kuuharibu mji kabisa. Na jina la mji huo ulikuwa ukiitwa Horma.
18 Pamoja na haya Yuda aliutwaa Gaza pamoja na mipaka yake, na Ashkeloni na mipaka yake, na Ekroni na mipaka yake.
19 BWANA ALIKUWA PAMOJA NA YUDA; naye akawafukuza watu waliokaa katika nchi ya milimani; asiweze kuwafukuza hao waliokaa katika hilo bonde, kwa kuwa wao walikuwa na magari ya chuma”.
Mstari wa 19, unaanza kwa kusema “Bwana alikuwa pamoja na Yuda” maana yake ni kwamba, katika vita Yuda alivyokwenda kupigana, Bwana alikuwa pamoja naye..(kumbuka Yuda anayezungumziwa hapa sio Yule mwana wa Yakobo, wala sio Yule Yuda aliyemsaliti Bwana Yesu), bali ni kabila la Yuda kwa ujumla, ambalo wakati wa kuingia katika nchi ya Ahadi lilipaswa liupiganie urithi wake kwa kuwatoa wenyeji wa Kanaani ili kusudi wapate ardhi ya kukaa wao, kama urithi wa kabila zima.
Hivyo katika harakati za kupambania urithi wao huo walikutana na makabila mengi mbalimbali, ambayo mengine yalikuwa na nguvu sana na mengine manyonge, yale yaliyokuwa manyonge Yuda walikwenda kwa ujasiri na kuyapiga na kuyapokonya ardhi, kwasababu hayakuwa na silaha zenye nguvu za kuwazidi,
Lakini yale yaliyokuwa na Nguvu nyingi za kivita, Yuda waliyaogopa, hivyo hawakudhubutu kwenda kupigana nayo, na kwasababu hiyo Mungu asingeweza kuyaondoa kwasababu Mungu kamwe hatembei na watu wasio na Imani, hivyo akawaacha,
Lakini kama wangechukua hatua ya kwenda kupambana na hao maadui zao, pasipo kutazama ni silaha za aina gani wanazomiliki, ni wazi kuwa Mungu angewasaidia katika vita hiyo, na hatimaye wangewaondoa hao watu na kuutwaa urithi wao.
Sasa baadhi ya makabila ambayo Yuda waliyaogopa ndio hao waliokuwa wanakaa mabondeni, na sababu ya kuyaogopa biblia imeitaja pale kuwa “makabila hayo yalikuwa na magari ya chuma kwaajili ya vita”..Yuda wakaogopa wasiende kupigana nayo, jambo ambalo Yoshua mtumishi wa Mungu alishawaonya kuwa wasiyaogope makabila hayo..
Yoshua 17:17 “Kisha Yoshua alinena na nyumba ya Yusufu, maana, ni Efraimu na Manase, akawaambia, Wewe u taifa kubwa la watu, nawe una uwezo mwingi; hutapata kura moja tu;
18 lakini hiyo nchi ya vilima itakuwa ni yako; maana, ijapokuwa ni mwitu, wewe utaukata, na matokeo yake yatakuwa ni yako; kwa kuwa wewe utawafukuza hao Wakanaani, WAJAPOKUWA WANA MAGARI YA CHUMA, WAJAPOKUWA NI WENYE UWEZO”
Utaona pia hiyo sio mara ya kwanza wana wa Israeli kuyaogopa mataifa yenye nguvu kupita wao, soma pia Hesabu 13:33 na Waamuzi 4:3
Hiyo inatufundisha nini?
Tunachojifunza ni kuwa “Mungu hawezi kufanya jambo lolote kwetu pale tunapomkosea Imani” Hilo ndilo jambo ambalo Mungu hawezi kufanya!!! Na lingine ambalo hawezi kufanya ni DHAMBI!
Yakobo 1:6 “Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku.
7 Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.
8 Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote”.
Ukiamini kuwa Mungu hawezi kukuponya, basi fahamu kuwa KWELI HATAWEZA KUKUPONYA!, Ukiamini kuwa Mungu hawezi kukutendea jambo Fulani au kukupigania, basi fahamu kuwa ni KWELI MUNGU HATAWEZA KUKUTENDEA HILO JAMBO, wala KUKUPIGANIA katika hiyo vita iliyo mbele zako.
Siku zote fahamu kuwa PASIPO IMANI HAIWEZEKANI KUMPENDEZA MUNGU (Waebrania 11:6).
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Mtu akija kwangu naye HAMCHUKII baba yake hawezi kuwa mwanafunzi wangu?
Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia neno la Mungu wetu lililo taa ya miguu yetu na mwanga wa njia yetu (Zab.119:105).
Neno la Mungu linasema..
Warumi 5:1 “Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo”.
Je! ni haki gani hiyo tunayohesabiwa, ambayo tukiisha ipata basi tutapata amani?
Jibu ni kwamba si haki moja!, bali ni haki ZOTE Njema!… Mfano wa hizo ni kama zifuatazo…
1.HAKI YA KUISHI MILELE.
Tunapomwamini Bwana Yesu tunapata haki ya kupata UZIMA WA MILELE.. ambayo tuliupoteza pale Wazazi wetu wa kwanza walipoasi.
Yohana 11:25 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;
26 naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?”
Pia Yohana 3:36, Bwana Yesu anasema maneno kama hayo hayo…
2. HAKI YA KUWA NA UZIMA, NA AFYA.
Isaya 53:5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona”
Hivyo magonjwa hayatatutawala, bali uzima na afya, kama tukiwa ndani ya Yesu, maana yake AFYA ni haki yetu!.. tunapopitia maradhi ya muda mrefu maana yake hapo ni shetani katudhulumu haki yetu, hivyo hatuna budi kuishindania haki yetu mpaka tuipate katika mahakama ya kimbinguni, huku tukitumia katiba yetu biblia. Na tunapong’ang’ania kwa bidii bila kuchoka, wala kukata tamaa basi tunaipata haki yetu ya kuwa wazima siku zote.
3. HAKI YA KUMWONA MUNGU.
Unapomwamini Yesu ni haki yako kumwona Mungu katika maisha haya na katika yale yajayo.. Kumwona Mungu si lazima tumwone kwa macho, bali utamwona katika maisha.. Maana yake utapitia vipindi vingi vya maisha ambavyo vitakujulisha kuwa Mungu yupo nawe, pia utaona miujiza mingi ya kiMungu ambayo itakujulisha kuwa Mungu yupo nawe, na zaidi sana kila utakapomwita Mungu utamwona..
Mathayo 28:20 “……….na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari”.
4. HAKI YA KUPOKEA ROHO MTAKATIFU.
Zamani Roho Mtakatifu alikuwa anashuka juu ya baadhi ya watu tu (ambao ni manabii) tena kwa kitambo kidogo, lengo ni kuwapa ujumbe kutoka kwa Mungu, na baada ya hapo anaondoka.. Kwasababu ROHO TAKATIFU ya Mungu haiwezi kukaa ndani ya Mwanadamu aliye mchafu.
Lakini baada ya Bwana YESU kuja, kaja kutuletea Haki ya sisi kuwa na Roho Mtakatifu ndani yetu, jambo ambalo si la kawaida..
Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”
Hivyo yale matunda ya Roho tunayoyasoma katika Wagalatia 5:22, ambayo ni upendo, amani, furaha n.k Hayo yote ni haki yetu sisi kuyapata.. Kuwa amani ni haki yako wewe uliye ndani ya Kristo, kuwa na furaha ni haki yako.
5. HAKI YA KUFANIKIWA KIMWILI NA KIROHO.
Tunapomwamini Bwana Yesu na kukaa ndani yake, hatupati tu haki ya vitu vya kiroho, bali pia tunapata haki ya vitu vingine vya kimwili ikiwemo mafanikio.
3 Yohana 1:2 “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo”
Pia Neno la Mungu linasema..
2Wakorintho 8:9 “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake”.
Na haki nyingine zote zilizosalia, ni Ahadi yetu. Ndio maana kuna umuhimu mkubwa sana kuingia ndani ya Kristo.. Ukiwa nje ya Kristo, shetani atakudhulumu haki zako zote hizo na hakuna popote utakapokwenda kushitaki.
Bwana akubariki.
Maran atha.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?
Biblia inaposema “Wote tumetenda dhambi” si inamaanisha hakuna mtakatifu duniani?
JIBU: Wapo wanaofikiri kwamba shetani amefungwa, atakuja kufunguliwa kipindi Fulani huko mbele, lakini pia wapo wanaodhani, shetani anaishi mahali Fulani kuzimu( aidha chini ya bahari, au kwenye sayari fulani), ambapo huko kuna amesimika utawala wake unaofanana na huu wa duniani.
Lakini ukweli ni kwamba shetani hajafungwa, wala hayupo katika eneo Fulani rasmi la mwilini, ambalo unaweza kwenda ukakutana naye.
Ikumbukwe kuwa ibilisi anafanya kazi katika ulimwengu wa roho, alipoasi mbinguni, alitupwa chini duniani, akaanza kazi yake ya kuudanganya ulimwengu mpaka akafanikiwa kuuteka ukawa chini ya milki yake, Tunalithibitisha hilo katika maneno aliyomwambia Bwana Yesu.
Luka 4:5 Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja.
6 Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo.
7 Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako. 8 Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke
Hivyo shetani yupo anazunguka zunguka duniani hana makao rasmi, Alimwambia hivyo Mungu.
Ayubu 1:6 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. 7 Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo”.
Atakuja kufungwa kipindi ambacho utawala wa miaka 1000 wa amani wa Yesu Kristo kuanza, na baadaye atafunguliwa kidogo, lakini kwasasa hajafungwa yupo duniani ndio chanzo cha maovu yote, wala hana eneo Fulani rasmi kwamba amejijengea anaishi huko na mapepo yake, hapana bali wanafanya kazi katika ulimwengu wa roho, wakijigawanya tu katika vitengo mbalimbali, wengine katika anga, wengine, katika mataifa, wengine katika familia moja moja, na wengine katika kila huduma/au kanisa la Kristo lilipo, wengine katika uchawi n.k.
Hivyo, sisi tutamshinda na kumpinga tu kwa kulishika Neno la Mungu, na kudumu katika maombi daima.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
ZIFAHAMU HUDUMA KUU (10) ZA SHETANI DUNIANI.
ZIFAHAMU KAZI TATU ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA ULIMWENGU.
Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze biblia, Neno La Mungu wetu.
Mwanzo 8:6 “Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya;
7 akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi.
8 Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi;
9 bali YULE NJIWA HAKUONA MAHALI PA KUTUA KWA WAYO WA MGUU WAKE, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani”
Tunaona wakati wa Nuhu kutoka safinani… Aliwaachia ndege wawili ili kupima hali ya mazingira ya nje. Na ndege wa kwanza ambaye ni “KUNGURU” aliondoka lakini hakumrudia Nuhu.. lakini ndege wa pili ambaye ni “NJIWA” Alipoondoka na kukuta nje maji yamejaa kila mahali, alirudi safinani..
Sasa ni kwanini Njiwa arudi na kunguru asirudi?.
Siri ipo katika ile sura ya Saba, kuhusiana na wanyama Najisi na wasio Najisi.
Mwanzo 7:1 “Bwana akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki.
2 Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke.
3 Tena katika ndege wa angani saba saba, mume na mke; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote”
Sasa Kunguru yupo katika kundi la Ndege Najisi,
Walawi 11:13 “Kisha katika ndege hawa watakuwa ni machukizo kwenu; hawataliwa, ndio machukizo; tai, na furukombe, na kipungu;
14 na mwewe, na kozi kwa aina zake,
15 na kila kunguru kwa aina zake”
Na njiwa yupo katika kundi la ndege Safi (yaani wasio najisi) ndio maana alikuwa anatumika katika matoleo.
Sasa tabia ya ndege/wanyama najisi ni za tofauti na zile za wasio najisi. Wanyama najisi wanakula chochote na wanaweza kuishi popote.. lakini Wanyama/ndege wasio najisi wanachagua vitu vya kula, vile vile wanachagua mazingira ya kuishi, si kila mahali wanaweza kuishi.
Ndio maana tunaona huyu kunguru alipoachiwa, alienda kuzunguka zunguka huko nje, lakini njiwa aliona mazingira ya nje si salama, bado wakati wake, na hatimaye akarudi safinani.
Sasa wanyama najisi kiroho wanafananishwa na watu wa ulimwengu huu, walio mbali na MUNGU, na wanyama Safi (yaani wasio najisi) wanafananishwa na watu wa Mungu, waliookolewa kwa damu ya thamani ya YESU KRISTO, ambao hawajitii unajisi na mambo ya dunia.
Kama vile njiwa alivyozunguka huko na huko na kuona safinani ni mahali salama katika dunia iliyoharibika.. vile vile watu wa Mungu, kamwe hawawezi kuona hii dunia ipo salama, au ni mahali pa kustarehe kuliko safinani. Na safina ni BWANA YESU!.
Ukiona unaifurahia dunia iliyochafuka, dunia iliyojaa anasa, dunia iliyojaa mabaya basi katika roho wewe ni najisi.. Ukiona unaufurahia uasherati, ulevi, wizi unaoendelea duniani, na hata wewe mwenyewe kuwa mshirika wa hayo, basi fahamu kuwa unafanana na Yule kunguru! Na hivyo ni najisi mbele za Mungu kulingana na biblia.
Mathayo 15:18 “….vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi.
19 Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano;
20 hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi…”
Je! wewe ni miongoni mwa walio najisi au safi? Kama bado dhambi inatawala maisha yako basi upo hatarini hivyo suluhisho ni kumgeukia Yesu kwa kutubu na kumaanisha kuacha dhambi, na Yesu atakupokea na kukupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu, ambaye kupitia huyo atakutakasa kwa kukupa uwezo wa kufanya yale mema ambayo ulikuwa unashindwa kuyafanya kwa nguvu zako.
Kataa ukunguru!
Bwana akubariki
maran atha!
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Kwanini Mungu aliwaita Adamu na Hawa jina moja?
JIHADHARI NA ROHO ZIDANGANYAZO.
Je mwanamke anaruhusiwa kupanda madhabahuni akiwa katika siku zake?
Mahali pa juu palikuwa ni wapi kama tunavyosoma katika biblia?